Questions to the Prime Minister from Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe (3 total)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la kwanza. Tangu mwaka 2019, Serikali ilisitisha kutunga na kutoa mitihani kwa wanafunzi ambao walikuwa wanasoma masomo ya ufundi kwenye zile shule za msingi za ufundi na kusababisha miundombinu ya Serikali, vifaa vya kujifunzia, Walimu na samani nyingine ambazo zilikuwa zimeandaliwa kwa ajili ya kutoa mafunzo haya ambayo ni muhimu sana. Je, Serikali ina mpango gani sasa kufufua shule hizi za msingi za ufundi ambazo pia ni mahitaji sana kwa Tanzania. Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Hai kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali iliona umuhimu wa kutoa elimu ya ufundi kwa vijana wetu kuanzia umri mdogo na Serikali ikaanzisha mafunzo hayo kuanzia ngazi ya shule ya msingi. Hata hivyo, kwa kuwa tunazo shule nyingi za msingi, Serikali haikumudu kutoa vifaa vya ufundi kwa kada zote, kwa sababu ufundi upo maeneo mengi. Hapa ndipo Serikali ikaona ni muhimu kuanzisha mfumo wa kuwa na vyuo maalum vinavyoweza kuwapata vijana wale na kuwapeleka maalum kwenye chuo ambacho kimeandaliwa, kina vifaa na Walimu ili kuweza kuwapatia mafunzo na baadaye mafunzo hayo kuyaweka kwenye level ambayo pia inaweza kumsaidia kwenda kwenye level au ngazi nyingine. Kwa hiyo, Serikali iliamua kuimarisha VETA na ikaiondoa VETA kutoka Wizara ya Kazi na kuileta kuwa chini ya Wizara ya Elimu ambayo inasimamia sera ya elimu yote nchini.
Mheshimiwa Spika, VETA hiyo imeendelea kuchukua vijana wetu, mwanzo ilikuwa inachukua vijana waliomaliza kidato cha nne, lakini baadaye tukapanua wigo tukajenga vyuo kwenye ngazi ya mikoa yote nchini; ni zoezi ambalo limekamilika kwa sasa. Baadaye tukaona tupanue wigo huu tuweze kutoa fursa nyingi kwa vijana wetu na Serikali imeanza kutekeleza ujenzi wa VETA kila Wilaya, ni zoezi ambalo linaendelea sasa kwa lengo la kuwapatia vijana hawa fursa ya kwenda kusoma ufundi katika nyanja mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, wanaokwenda VETA ni wa kuanzia waliomaliza elimu ya msingi, kidato cha nne na kule sasa tumeweka level mbalimbali; hatua ya kwanza, ya pili, ya tatu na hatua zote wanafanya mitihani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali iliona ni busara kuanzisha vyuo maalum ambavyo tutaweza kuweka vifaa vya kutosha na Walimu wa kutosha ili kuweza kutoa elimu hiyo kwa urahisi na kwa uhakika zaidi, ndilo zoezi ambalo kwa sasa linaendelea nchini kote. Hata hivyo, tuliamua kutumia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) navyo pia vikahamishwa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii vikaletwa Wizara ya Elimu ili tuweze kusimamia sera ile ile ya kuwezesha vijana kuwa na ujuzi kuwa na utaalam kwenye sekta mbalimbali ili iweze pia kuchukua wanafunzi mbalimbali. FDCs pia inachukua hata wale ambao hawajamaliza darasa la saba wanajifunza uashi, useremala, sasa hivi TEHAMA, lakini pia ushonaji na karibu sekta zote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaendelea kuuimarisha utaratibu huu na kutoa fursa zaidi kwa watoto wetu nchini kupata ujuzi mbalimbali. Programu hizi zinaendelea Wizarani hata Ofisi ya Waziri Mkuu nayo pia imeanzisha programu inayowachukua wote waliomaliza darasa la saba hata chuo kikuu kuwapa uwezo wa kufanya ujuzi. Wakimaliza kozi yao kwa muda huo waliopangiwa wanaweza kufanya shughuli nyingine za kujiajiri, wanaweza pia kuajirika na kuanzisha kazi ambazo zinaweza kuwasaidia wao ikiwemo na kilimo pia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuliona kule chini uwezo wa kupeleka vifaa vyote katika kila shule ya msingi kwenye shule zetu 12,000 isingewezekana. Kwa hiyo, hivi vyuo sasa vinakuwa na nafasi nzuri na ndivyo hivyo ambavyo tunavijenga kwenye ngazi ya Wilaya. Hayo ndiyo malengo ya Serikali. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa nyakati mbalimbali wakati ugonjwa wa Covid 19 umeshamiri wananchi wengi waliokuwa wanaishi nje ya nchi walirejea nchini, ikiwemo wanafunzi waliokuwa wanaendelea na masomo kwenye kada mbalimbali.
Pia hivi karibuni wakati vita ya Ukraine na Urusi inaendelea hali kadhalika wananchi wakiwemo wanafunzi wamerejea nchini. Wanafunzi ambao walikuwa wanaendelea na masomo kwenye kada mbalimbali na kwenye vyuo mbalimbali nchini sasa hivi wako hapa nchini wengine wamesitisha masomo kabisa, wengine wanasoma kwa njia ya mtandao kwa mazingira magumu sana. Ni nini kauli ya Serikali kwa wanafunzi hawa ambao wamekosa masomo? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Mbunge Hai Mkoani Kilimanjaro kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna vijana wa kitanzania wanasoma kwenye vyuo mbalimbali nje ya nchi na ugonjwa huu wa Covid 19 ulipoingia nchi kadhaa ziliamua kuwarudisha vijana kwenye nchi zao wakiwemo vijana wetu wa kitanzania ambao walikuwa wanasoma huko na wamerudi. Na si tu Covid 19 hata hii vita inayoendelea nchini Urusi na Ukraine tunaona vijana wetu wengi wamerudi hapa nchini. Nini kinafanyika hapa ndani ya nchi kuokoa miaka waliyoipoteza kwenye masomo?
Mheshimiwa Spika, tulitoa tangazo kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Elimu kwamba vijana wote wa kitanzania waliorudi kutoka nje waliokuwa wanasoma nje kuja nchini waripoti Wizara ya Elimu ambako pia Taasisi ya TCU inayoshughulikia vyuo vya elimu ya juu kwa sababu wengi wanasoma vyuo vya elimu ya juu waende wakieleza elimu yao walikuwa wanasoma course gani, wamefikia kipindi gani halafu tuone ufaulu wake huo kutoka hapo alipo mpaka alipoishia ili sasa Taasisi yetu ya TCU iweze kuchukua zile alama. Wanavyo vigezo vyao ambavyo vinatumika katika kurasimisha taaluma waliokuwa wanasoma nje na taaluma iliyoko ndani ili waweze kuendelea na vyuo vya ndani, utaratibu huo ndio tumeutumia.
Mheshimiwa Spika, sasa kama wako vijana ambao wamerudi utaratibu huu haujawapitia kuna mambo mawili. Moja atakuwa hajaenda kuripoti ili apate huduma hiyo; lakini mbili course anayoisoma kama inafanana na course ya Tanzania, course zetu zina vigezo vya kimataifa. Anaweza kuwa alikuwa anasoma chou ambacho hakifikii viwango vya vyuo tulivyonavyo nchini hawa watakuwa bado hawajapata nafasi hiyo mpaka pale ambapo watapewa ushauri wa course gani sasa anaweza kuianza hapa nchini ili aweze kuisoma.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuna hayo mambo mawili ambayo Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua ya kwa nini vijana wengine ambao hawajarasimishwa kuingia kwenye vyuo mpaka leo wako nje ya vyuo.
Kwa hiyo, nitoe wito kwa watanzania wale ambao wameenda kusoma nje wamerudi nchini kwa matukio yote mawili covid 19 na vita ya Ukraine na Urusi waripoti TCU wapeleke taarifa za course aliyokuwa anazisoma chuo ili TCU ifanye ulinganisho wa course aliyokuwa anasoma na course zilizopo nchini kwenye vyuo vyetu, baada ya hapo atapata maelekezo ili kuondoa tatizo hilo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa swali ili niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu sote kwamba vijana ni kundi muhimu sana katika ukuzaji wa uchumi wa nchi yetu. Hivi karibuni kumeibuka wimbi kubwa la vijana kulewa sana wakati wa kazi wakati wa mchana na hii ni kutokana na uingizwaji wa vilevi vikali sana kutoka nje ya nchi, lakini vilevi ambavyo vinapatikana kila mahali kiasi kwamba kijana anaweza kwenda gengeni akamiminiwa kakinywaji kidogo baada ya hapo analewa kabisa na kushindwa kuendelea na kazi. Je, Serikali ina kauli gani juu ya udhibiti wa vileo hivi vikali ambavyo vinaathiri uchumi wa vijana na vinaathiri ujenzi wa uchumi wa nchi yetu? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu inao utaratibu unaowezesha kutambua uzalishaji, uuzaji lakini pia kudhibiti bidhaa ya vileo inayoingia hapa nchini. Vileo hivi vinaendelea kusambaa kwa wateja kwa utaratibu uliowekwa wa wanaopata vibali vya biashara na kuendesha biashara za vileo. Serikali yetu inaendelea kutoa elimu kwa jamii yetu, ile ya kuelekeza au kuonesha madhara ya ulevi uliopitiliza, ikiwemo na hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameeleza, kwamba vijana wengi wanalewa wanakosa uwezo wa kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, kwenye hili siachi kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amefanya kazi kubwa ya kuhamasisha vijana kujiunga pamoja na kutengeneza makundi yanayoweza kufanya shughuli za ujasiriamali. Vipo vikundi vya ujasiriamali vya mtu mmoja mmoja pamoja na vya pamoja wanaofanya biashara kwa siku zima na vinawapatia mapato. Utaratibu huu umesaidia sana vijana wetu kupata pato linaloendesha yeye na jamii yake.
Mheshimiwa Spika, tumeona hapa Dodoma Machinga Complex vijana wa kawaida wapo pale wanafanya biashara zao. Tumeona kila Wilaya waendesha bodaboda, bajaji, wafanyabiashara za kawaida na machinga. Hii yote ni jitihada za Mheshimiwa Rais katika kuhamasisha kwamba wanakaa pamoja na kutafuta shughuli ya ujasiriamali. Sasa hivi tunaendelea kuwahamasisha nchini kwa vijana wote kuingia kwenye shughuli ambazo zinawazalishia mali kuliko kuingia kwenye makundi ambayo hayana tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ni nini kinafanyika; ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii hii kuhakikisha kwamba wanaingia zaidi kwenye shughuli za uzalishaji mali huku pia tukiimarisha sheria kwa wazalishaji wanaoingiza bidhaa za vilevi ndani ya nchi, wauzaji na watumiaji, hasa kwenye maeneo yale ya wanaokiuka sheria maana tunazo sheria zetu. Kwa hiyo wale wanaokiuka sheria huwa tunawachukulia hatua. Hii inasaidia kupunguza kuingiza kwa pombe ambayo ni kali kupitiliza kiasi. Malengo yetu ni kwamba kila aina ya kileo kinachoingia nchini kinakidhi mahitaji ya afya ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jamii itusaidie kutambua uingizaji na utengenezaji wa bidhaa usiokuwa rasmi ambao haujapata vibali. Hawa ndio wanaotengeneza bidhaa hiyo ambayo ni kali kupita kiasi bila kutambuliwa na wale wote ambao wana leseni wanatengeneza bidhaa ambayo nayo imepimwa na inakidhi mahitaji ya afya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe wito kwa taasisi zote zinazofanya shughuli za vijana kuendelea kuwaelimisha vijana hawa maadili mema na pia kuendelea kutoa elimu stadi za maisha kwa vijana hawa. Muhimu zaidi kutoa elimu ya ujasiriamali kwa lengo la kuwaonesha kwamba njia nzuri sahihi ni hii ambayo utakuwa unajishughulisha, unapata pato kuliko njia hii ya kuendelea kula viroba ambavyo baadaye vitamlaza siku zima; hana mtaji hawezi kupata mafao, hawezi kupata kujikimu kwenye familia. Huu ndio mpango mkakati ambao Serikali tunao, wa kuhakikisha kwamba vijana wetu tunawapa fursa za kushiriki kwenye ujasiriamali ili waachane na shughuli nyingine waendelee kwenye ujasiriamali. Ahsante sana. (Makofi)