Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe (1 total)

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza. Kwa kuwa mwezi huu ndiyo mwezi wa Pili sasa, na majibu yake yanaonesha kwamba ujenzi unaanza mwezi huu wa Pili, nataka kujua, je, wameshampata mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi huu?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Changamoto iliyopo Wilaya ya Momba ndiyo changamoto kubwa iliyopo Wilaya ya Ileje. Nataka kujua, Serikali mna mpango gani wa kujenga Mahakama nzuri na ya kisasa yenye hadhi ya wilaya ndani ya Wilaya ya Ileje?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kuhusu kumhakikishia kama mkandarasi amepatikana, katika jibu la msingi nilisema wako katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi. Baada ya mkandarasi kupatikana, atakabidhiwa site na kwa mujibu wa Mahakama, mwezi huu ndiyo anatarajiwa kukabidhiwa site. Kwa hiyo, dada yangu Mheshimiwa Mbunge awe na uhakika kwamba litatekelezwa na vinginevyo mimi na yeye tutafuatilia ili kuona kwamba lengo hilo linafikiwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu uwepo wa ujenzi wa Mahakama ya aina hiyo Ileje, kama nilivyowahi kusema katika nyakati tofauti, Mahakama ina mpango mkakati wa miaka mitano mitano. Katika mpango mkakati huu wa awali, Ileje haikuwemo, lakini katika mkakati unaofuata tunatarajia Wilaya ya Ileje itaingia, ahsante.