Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zahor Mohamed Haji (21 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na taadhima, naomba kwanza kukishukuru Kiti chako. Vilevile naomba nishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuweza kuwasilisha kwetu hapa bajeti hii ambayo ndani yake mna changamoto nyingi, lakini naamini Bunge hili ndiyo sehemu sahihi kwa ajili ya kupatia ufumbuzi baadhi ya matatizo yao mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunaapishwa hapa ulitukabidhi Katiba na Katiba hii kabla ya kuikabidhiwa tulikula kiapo. Maana yake kama sikosei ni wajibu wa Bunge hili, kwa sababu Katiba hii inako ilikotoka mpaka ikaja hapa pamoja na changamoto zote, lakini kubwa ni kwamba tuliapa kuilinda Katiba hii, nadhani mwenyewe umesema hivyo.

Kwa hiyo, mimi naomba kwa wenzetu wa Wizara ya Katiba na Sheria, mimi si mwanasheria by profession lakini najaribu kuisoma hii kwa sababu ushauri wako umesema someni, someni, someni, nilikuwa najaribu kuangalia hasa vitu vinavyoitwa changamoto na hapa nataka nijielekeze kwenye changamoto za mambo ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ikikupendeza ninukuu Katiba yako hii kwenye Sura ya Saba, Sehemu ya Kwanza na Sehemu ya Pili. Inasema: “Sehemu ya Kwanza, Mchango na Mgawanyo wa Mapato ya Jamhuri ya Muungano”.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Zahor, tusomee Ibara.

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara inasema…

NAIBU SPIKA: Ibara namba ngapi?

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 133.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ninukuu, inasema hivi: “133. Serikali ya Jamhuri ya Muungano itatunza akaunti maalum itakayoitwa “Akaunti ya Fedha ya Pamoja”…” Naomba kuishia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba twende kwenye Sehemu ya Pili, Ibara ya 135, inasema: “135.-(1)Fedha zote zitakazopatikana kwa njia mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, isipokuwa fedha za aina iliyotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya ibara hii, zitawekwa katika mfuko mmoja maalum ambao utaitwa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.” Naomba niishie hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yangu ni nini? Nimesema tulikubaliana kuilinda Katiba hii, ombi langu kwa wenzetu wa Wizara ya Katiba na Sheria; nimekuwa nikifuatilia na nikisikiliza maeneo mengi sana ibara hizi kila siku vinapigiwa kelele. Kwa hiyo, naomba Kiti chako na Bunge lako, endapo tutaona kwamba ibara hizi ni tatizo tokea Katiba hii imetengenezwa na ibara hizi kuwekwa kama sikosei ni mwaka 1984, maana yake tunalo tatizo sisi wenyewe kama Bunge kutokusimamia Katiba ambayo tumeapa kuilinda; ombi langu kwako, tulinde Katiba hii; hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, nimefuatilia mijadala mingi kuanzia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu mpaka hotuba ya leo ya kaka yangu, Mheshimiwa Prof. Kabudi, lakini nimefuatilia michango ya Waheshimiwa Wabunge, wengi wakizungumzia juu ya ukosefu wa fedha za vitendea kazi na ukosefu wa fedha za maendeleo kwenye maeneo mbalimbali.

Sasa ambalo nimeliona kwa haraka haraka, inawezekana nitakosea mtanisahihisha, kubwa ni kwa sababu sisi kama Bunge la Jamhuri ya Muungano tumeacha kufanya kazi yetu ya kuilinda Katiba hii ya kwamba ni kusimamia na kuishauri Serikali. Ndiyo maana tumeiacha Wizara ya Fedha kuchukua nafasi kubwa ya Serikali Kuu yenyewe kuamua nini ifanye nini isifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ambalo nimeliona kwa haraka haraka, inawezekana nakosea, mtanisahihisha; kubwa ni kwa sababu sisi kama Bunge la Jamhuri ya Muungano tumeacha kufanya kazi yetu ya kuilinda Katiba hii ya kwamba ni kusimamia na kuishauri Serikali. Ndiyo maana tumeiacha Wizara ya Fedha kuchukua nafasi kubwa ya Serikali Kuu yenyewe ya kuamua nini ifanye nini isifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapitisha bajeti hapa kama Wabunge, lengo letu na imani yetu ni kwamba tunakwenda kutekeleza kitu ambacho tumekipanga. Sasa ushauri wangu ni mdogo tu, kwamba kwa sababu Katiba hii imetupa nafasi ya kuunda Joint Financial Account na Joint Financial Committee. Ombi langu ni kwamba turudi kwenye basics hizi za sheria, kwamba Katiba hii tukiisimamia Wizara ya Fedha ifanye kazi zake mbili tu; moja, kutengeneza policy ambayo itatuwezesha kutafuta fedha na pili, ifanye kazi ya kukusanya fedha, period. Ili tuwaondolee wenzetu wa fedha makelele kwamba hamtupi, hampendi, hamtaki. Siyo kama hawapendi, lakini fedha haitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Bunge hili lifanye kazi yake ya kusimamia na kushauri ili liwe na nafasi ya kuweza kusema; kwa sababu nadhani tunayo Appropriation Committee hapa, sasa hii ifanye kazi ya kusema tumekusanya mbili; hizi zitakuwa za kazi hii na hizi zitakuwa na kazi hii. Wizara ya Fedha ifanye kazi zake mbili tu ya kutengeneza policy na kukusanya fedha ili Bunge hili liamue kwamba fedha hizi zitumike kwa aina eneo gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi. Pia naomba kuwashukuru wenzetu wa Kamati zote tatu kwa taarifa nzuri zilizo chambuliwa kutoka kwenye taarifa ya CAG ambayo imewafanya Wabunge waweze kuzisoma na kuzielewa taarifa hizi vizuri kabisa. Kwa sababu volume ni kubwa lakini wamefanya kazi kubwa sana wenzetu wa Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nataka kuishukuru Serikali, mwenzangu mmoja amezungumza hapa kwamba kwa kawaida taarifa hizi huwa hatuzipati mapema, halafu tukazipitia, kuzichambua na kuzichangia. Hii inaonesha ni jinsi gani Serikali yetu imeamua kwa makusudi kuheshimu misingi ya sheria.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika maeneo mawili; eneo la kwanza ni la PAC, lakini eneo la pili ni LAAC.

Mheshimiwa Spika, wamezungumza wenzetu wengi sana hapa juu ya upotevu wa fedha za Serikali. Wenzetu wamezungumza hapa kwamba TANROAD imetutia hasara ya Shilingi bilioni 68.7. Vile vile kwenye ujenzi wa vihenge, NFRA tumepoteza Dola milioni 33. Kwanza naomba hapa tuelewane. Unapozungumza Dola milioni
33 unaweza ukaona kama ni kitu kidogo hivi, lakini ukizigeuza Dola milioni 33, tunakaribia kwenye Shilingi bilioni 72 na kitu. Kwa hiyo, tusichukulie kama ni fedha ndogo, ni nyingi sana ambazo zingeweza kusaidia kwenye majimbo yetu.

Mheshimiwa Spika, kuna fedha nyingine hapa, amesema kaka yangu Mheshimiwa Maganga, kuhusu upotevu wa Dola milioni 153.4. Hizi ni fedha nyingi. Tunazungumzia karibu Shilingi bilioni 300 na kitu zimepotea na hazina maelezo. Vilevile wako wajanja hapa wengine, mwaka 2021 lilipoungua soko la Kariakoo, tumeambiwa kwamba shilingi bilioni 3.56 hazijulikani zilipo na hazina maelezo. Halafu, taarifa itoshe hivyo, haiwezekani.

Mheshimiwa Spika, pia tumeambiwa kwenye DART kuna malipo ya usumbufu. Haiwezekani kwenye Taifa hili lenye Wabunge walioteuliwa wakachaguliwa na wananchi halafu mambo yakaenda kawaida tu. Siyo Bunge hili. Bunge hili limekuja kwa asilimia kubwa na wengi hapa na wengi wetu tunasimamia Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. Moja katika ahadi zake CCM ni kupambana na mambo ya ubadhirifu wa fedha za Umma. Bunge hili ni lazima tuchukue hatua na lazima Chama chetu kilichotutuma kijue kwamba tumekuwa wakali kwenye hili. Kwa hiyo, asiondoke mtu kama ni business as usual. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiangalia kidogo kwenye LAAC, wenzetu wa Kamati wanasema wametuletea taarifa hii ili kutushawishi. Naomba ninukuu: “Lengo la taarifa hii ni kulishawishi Bunge liafiki ushauri wa Kamati wa kuitaka Serikali ichukue hatua.”

Mheshimiwa Spika, jana ulisema hapa, ulitupa moyo sana, kwamba kuna wakati wa kushauri na wakati wa kusimamia. Sasa hivi tunataka kusimamia kuhakikisha kwamba Serikali inatekeleza maelekezo na maamuzi ya Bunge hili. Kwa sababu hii ni mihimili mitatu; mhimili huu ndiyo unasimamia Serikali. Kwenye hili, wenzetu wa Kamati wala msipate taabu, siyo kazi yenu kutushawishi. Mmeweka facts kwenye meza, zimeonekana, na hizi mmezitoa kwenye taarifa ya CAG, tunawashukuru na tunakubaliana na ninyi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu wenzetu wamesema, naomba kidogo niipongeze Serikali kwamba angalau imefanya kazi kubwa; ukilinganisha miaka ya nyuma na ya sasa, wanasema kwamba, katika maeneo ya halmashauri zilizofanyiwa utafiti, zilizokaguliwa ni halmashauri 178 ambazo ni sawa na asilimia 96.2, hii ni hatua kubwa sana. Naomba niipongeze Serikali lakini tuendelee, kwa sababu tunahitaji mia kwa mia, kila aliyepewa pesa zetu ni lazima akaguliwe, kwa sababu hii siyo option, ni lazima. Kama kuna upungufu wa watenda kazi, tunaomba wenzetu Serikali ahakikishe kwamba wataalam wa ukaguzi wanafanya kazi yao, kwa sababu hao wenzetu wameona upungufu kwenye maeneo kumi.

Mheshimiwa Spika, nitataja machache tu, kwanza, anasema, ni upungufu kwenye mifumo. Mifumo inatengenezwa na kudhibitiwa na binadamu. Mifumo hii inakuwaje? Maana yake huu ni mkakati wa makusudi kuhakikisha kwamba fedha zinapita lakini katikati wako wajanja wanazichezea. Mifumo ni ya kwetu na wataalam tunao inakuwaje kuna kuchezewa kwenye mifumo?

Mheshimiwa Spika, vile vile wanasema kwamba kuna dosari kwenye matumizi na makusanyo. Tunaweza kufanya dosari ndogo kwenye makusanyo lakini kwenye matumizi hatuwezi kusema ni dosari bali ni makusudi. Kwa sababu tunapotumia tunazo Sheria za Fedha ambazo ndizo zinazotuongoza. Tuna Sheria za appropriation ndizo zinazotuongoza, tunakoseakoseaje? Wenzetu wamesema hapa kwamba ni mkakati wa makusudi kwa sababu sheria zimeonekana zina upungufu, wataalaam wanazijua, wanazichezea. Kwa hiyo, ningeomba hili kwa Wabunge wenzangu tukubaliane na mapendekezo ya Kamati kwa sababu Kamati ilifanya kazi kwa niaba yetu. Sasa sisi ni wajibu wetu kama Bunge kufanya maamuzi.

Mheshimiwa Spika, anasema kuna matumizi mabaya ya shilingi bilioni 9.74, amana za halmashauri. Sasa kwenye akaunti za amana bilioni 9.74 zinapoteapoteaje? Mbona hapa Kiswahili hakieleweki? Tokea tarehe Mosi Julai mpaka tarehe 30 Juni ya kila mwaka tunapoteza kwenye akaunti hii tu bilioni 9.74 kwenye akaunti nyingine ambazo hatuna taarifa nazo inakuwaje? Kwenye hili, pamoja na kwamba wenzetu tunawakubali wanafanya kazi, lakini waongeze kasi kwenye hili. Wenzetu wanafanya kazi kwa sababu wameona kuna upungufu kwenye sheria zetu.

Mheshimiwa Spika, naomba nielekee kwenye ruzuku za miradi ya maendeleo. Ukiangalia pale kwenye pesa za ruzuku zinazokuja kwenye halmashauri utagundua mambo yafuatayo na Kamati imetusaidia. Kuna halmashauri ambazo zimepewa zaidi ya asilimia 52 ya fedha ambazo zimeidhinishwa na Bunge. Ukiangalia kwenye mtiririko wa jedwali lile namba moja, utakuta kwamba kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka 2021 kuna halmashauri zimeongezewa 52% ziada.

Mheshimiwa Spika, suala langu liko hapa, Bunge hili tunakaa miezi mitatu kwa ajili ya kupanga bajeti, kuangalia maeneo gani tupeleke, maeneo gani tupunguze, tukimaliza tunaidhinisha ziende. Kama kuna dharura ni wajibu wa Serikali kutuita Bunge hili kwamba kuna fedha za ziada. Sasa naomba wenzetu watusaidie, unawezaje kuongeza mahali 52% ziada tena sio Sh.2000/=. Kwa mfano, kwenye jedwali namba moja, utakuta ziada ni Shilingi 41.787 bilioni, nani katoa kibali hiki? Mwingine amepewa ziada ya 30% Shilingi bilioni 20, nani katoa mamlaka ya hili? Kwa sababu mamlaka inayoidhinisha fedha ni Bunge hili. Sasa nadhani wenzetu waje watusaidie hapa, kwa sababu kwa kawaida kama kuna bajeti ya ziada ni Bunge hili ndilo linaloombwa.

Mheshimiwa Spika, naomba nirudi pale, nilisema kama Mabunge mawili yaliyopita hivi, kwamba tunalo tatizo kwenye sheria zetu na nilishauri na naomba niendelee kushauri kwamba, Bunge hili bado halijafanya kazi yake. Kuna kitu kinaitwa Appropriation Committee, Kamati hii ndio inatakiwa ifanye kazi mkono kwa mkono na Serikali ili kile kinachokusanywa kipelekwe kwa maelekezo ya Bunge hili si vinginevyo. Hatuwezi tunakutana hapa tunapanga, tunaamua, halafu mwingine kwa matashi yake tu anaamua wakati Bunge lipo na linaweza kuitwa wakati wote kama kuna dharura likafanya maaamuzi. Halafu mmoja anamua kwa sababu sheria zina nafasi, zinamruhusu au sisi kama Wabunge hatujaamua kufanya kazi kama wabunge?

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye ukurasa wa 11 kuna vitu vidogo sana, ukivisoma unaviona ni vyepesi sana. Anasema, ununuzi bila idhini ya bodi zinazohusika. Bodi za zabuni, watu wametumia shilingi bilioni 7.9, tuko wapi? Bunge liko wapi? Hao wenzetu wa Serikali wako wapi? Fedha hizi zinapotea mpaka tunakuja kuletewa taaarifa na CAG sisi kazi yetu nini?

Mheshimiwa Spika, ununuzi usiozingatia mpango wa manunuzi. Tumepoteza shilingi bilioni 3.84 kwenye halmashauri 24. Hii ni aibu kwetu. Narudia ni sisi kama Bunge hatujafanya wajibu wetu, ndio maana watu wanaona Bunge liko legelege, kwa hiyo wanaweza wakalichezea tu. Hili sio Bunge legelege. Hili ni Bunge ambalo likiamua kufanya maamuzi linafanya. Kwa hiyo ningeomba tufanye maamuzi ili kila mtu akae kwenye mstari wake.

Mheshimiwa Spika, naomba sana, kuna mtu mmoja anasema amelipa malipo ya ununuzi bila ya kuzingatia taarifa za mapokezi. Huyu amepoteza shilingi bilioni 2.02.

Mheshimiwa Spika, naona tabu hata kutaja hizi namba kwa sababu ni kama vile unajichoma kisu. Maana yake ni dhambi yetu sisi kama Wabunge. Sasa ningeomba niseme haya kwa sababu ni mengi sana. Kule kwetu Waswahili husema mchelea mwana kulia, hulia mwenyewe. Sisi hapa wengi wetu tumeletwa kwa heshima na kibali cha Chama Cha Mapinduzi lazima tukithibitishie Chama chetu kwa sababu Serikali ina wenyewe. Wenye Serikali hii naomba niseme kwa sasa ni Chama Cha Mapinduzi. Haitozidi mwezi mmoja tutakwenda kuulizwa pale mlitusaidiaje kama Chama cha Mapinduzi kuisimamia Serikali? Kwa sababu Serikali ni ya kwetu na chama kimetuingiza kwenye Bunge hili ili tuisimamie Serikali. Sasa ningeomba kushauri haya yafuatayo; pamoja na mengine waliyoshauri wenzangu nakubaliana nayo.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, kwenye PAC na LAAC; ningeomba tuhakikishe kwamba uchunguzi wa kina unafanyika ili kila aliyehusika abebe msalaba wake.

Mheshimiwa Spika, kwenye manunuzi, waliohusika sheria zitumike kwa sababu hawa ni watendaji wetu. Sheria zipo wanazijua, kanuni zipo wanazijua lakini kwa sababu wanajua loophole za sheria, wanafanya wanavyotaka. Kwenye hili naomba sheria, kanuni na taratibu kwa watumishi hawa zifanye kazi wala tusioneane huruma.

Mheshimiwa Spika, mwisho, ningeomba tupitie upya Sheria ya Manunuzi inayoonekana ni dudu lisilowezekana. Sheria ya Manunuzi inatuumiza sana. Kama mtakumbuka miaka michache nyuma, alikuwepo Rais wetu aliyetangulia, Mheshimiwa Jakaya Kikwete alisema Sheria za Manunuzi zina mapungufu mengi, mtu anaweza akafanya mazuri lakini sheria ikamkamata kwa sababu hakufuata taratibu na mtu anaweza akafanya madudu lakini kafuata sheria, huyo anaweza akawa free. Naomba tupitie sheria zetu za manunuzi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa heshima hii. Nitaomba nichangie kwa kifupi sana kwenye mada zote tatu, lakini kila mmoja atachukua la kwake halafu tutaelewana mbele ya safari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana ya Serikali ni chain of command na Serikali inatekeleza majukumu yake baada ya kuidhinishwa na Bunge kwa kufuata Sheria na Kanuni za Fedha na kiongozi anayestahili kulisimamia hili ni Bunge hili, kwamba Serikali tunairuhusu iende ikafanye matumizi baada ya kupitisha bajeti lakini baadaye tunakuja kuangalia nini kimefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huku nyuma niliwahi kusema kwamba huwa tunakutana muda mrefu hapa tunachagua, tunaamua halafu tuna wapa wenzetu wakatekeleze ila kwa bahati nzuri au kwa bahati mbaya sana inaonekana tunalo tatizo kwenye chain of command. Maana yake ni kwamba Serikali inatoa maelekezo, lakini watendaji nadhani hawaelewi au wanafanya kwa makusudi kutokusikiliza maelekezo ambayo yanatolewa na Serikali ili kuhakikisha kwamba sheria zinafanya kazi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe mfano hapa na nitaomba ninukuu ili nikae kwenye mstari. Liko tatizo la fedha ambazo hazitakiwi kubaki mwisho wa matumizi au mwisho wa mwaka. Sasa kwenye Waraka Namba moja wa Mwaka 2021/2022 tarehe 7 Juni, 2022 ulitolewa Waraka Namba Moja na Mhasibu Mkuu wa Serikali ambao unaandaa taarifa za mwaka ukiwakumbusha Maafisa Masuuli kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Serikali na kuhakikisha kuwa account ya masurufu haina bakaa mwishoni mwa mwaka wa fedha yaani tarehe 30 Juni, 2023. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni nini kilichobainika? Kilichobainika ni kwamba Taasisi saba zilikuwa na bakaa ya shilingi bilioni 2.45, nini maana yake? Maana yake Serikali inatoa maelekezo, lakini watekelezaji wanaopanga na kuruhusiwa kufanya wanafanya yaleyale kinyume kabisa na maelekezo, maana yake nini? Maana yake huu ni uvunjaji wa Sheria za Fedha na kanuni kwa makusudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taasisi nyingi hapa nitaomba nitaje chache, kwa mfano Wizara ya Mambo ya Ndani ilibakiza milioni 195, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya milioni 72, Hospitali ya Rufaa ya Sekou-Toure milioni 276 na nyingine. Ukifanya majumuisho unapata bilioni 2.45 zimekaa hazina maelekezo. Kwa maana hiyohiyo tunakwenda kwenye taasisi zilizofanya ununuzi nje ya mipango, lakini wakati huohuo ziko taasisi ambazo zimekusanya fedha, kwa mfano halmashauri zetu lakini zimekusanya fedha hazikuwasilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizifanyia hesabu kuna mambo matatu yanafanyika kwa wakati mmoja. Wako wanaokusanya fedha, lakini hawapeleki kwenye Mfuko Mkuu, lakini wako wanaokaa na fedha kwa muda mrefu, lakini wako wanaokaa na fedha ambazo zinatumika nje ya utaratibu. Sasa maana yake ni nini? Maana yake ukiangalia kwa haraka haraka ni mambo mawili au matatu: la kwanza, hawa wanaopewa maelekezo kwa mujibu wa sheria inawezekana sheria hizi kwa sababu wanazifahamu, lakini wanajua udhaifu wake wameamua kwa makusudi kukiuka maelekezo ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenye hili, lazima Serikali iwe na meno makali, Serikali iache kuchekacheka na kuwachekea hawa kwa sababu wanatuweka kwenye kipindi kigumu, bahati mbaya sana tunaelekea kwenye eneo ambalo tutakwenda kuulizwa. Niliwaambia wenzangu mwaka 2021 tutakwenda kuulizwa na wapigakura na Chama chetu tumefanya nini? Sasa kwa stahili hii maana yake lazima tujipange upya na lazima meno yetu yawe makali kuhakikisha kwamba kila maelekezo tunayoyatoa kwa watendaji wetu lazima wayafuate siyo kwa hiari. Kwa hiyo, mimi ombi langu Serikali iongeze meno, ing’ate na sisi tuone kwamba imeng’ata, isiwachekee hawa watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa ujumla fedha ambazo ziliachwa bila ya kutumika kwa harakaharaka tu ni shilingi milioni 409, lakini kule nyuma nimesema ni shilingi bilioni 1.8 zimeachwa tu bila ya kazi, lakini hizohizo zinakwenda kutumika huko bila kufuata utaratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda hautoshi, ninaomba nichangie kidogo tena kwenye hoja ya ongezeko la deni linalotokana na kupanda kwa viwango vya kubadilisha fedha. Ziko taasisi zetu kwa mfano, mimi natokea kwenye Kamati moja ya NUU (Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama) kwenye Kamati hii kuna chombo chetu sisi tunakiita Jeshi la Polisi. Kwa mwaka ule wa 2023 Jeshi letu lilikuwa linadaiwa shilingi bilioni 6.621, deni hili limekaa mpaka tunatakiwa kulipa shilingi bilioni 244.51.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake nini? Ni kwa sababu tu tumechelewa kulipa na ni kwa sababu ni fedha za kigeni, kwa hiyo kutoka 114 tunakiwa kulipa 244, nini maana yake? Maana yake ni kwamba tumeongeza zaidi ya mara mbili ya fedha hizi ambazo ni kwa sababu tu mmoja anafanya maamuzi mwingine anatekeleza, lakini hapa katikati hakuna kiungo, kwa hiyo mmoja anaamua lini alipe na nani amlipe. Jambo hili halijakaa sawa kwa sababu hii ni fedha nyingi ya wananchi ambayo tungeweza kuilipa kwa wakati deni hili lisingeweza kutoka 114 mpaka kufika 244 maana yake ni zaidi ya 50%. Sasa hili halikubaliki na halitujengei heshima kama Bunge kwa sababu sisi tunatakiwa tuongeze ukali kuishauri Serikali kwa kuwa mambo haya yanawaumiza sana wananchi na kwa kweli yanatuweka kwenye wakati mgumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa kifupi kabisa niongelee kwenye kutumia fedha nje ya mfumo wa electronic. Sisi tunapofanya bajeti na tukaiidhinisha Serikali ikatumie na Serikali inaweka mifumo maana yake lazima watendaji wetu watekeleze kwa mujibu wa utaratibu. Inakuwaje Serikali inaelekeza, lakini watalaam hawatekelezi na siku zinavyokwenda haya yanaongezeka, linatuweka kwenye kipindi kigumu kama Wabunge, lakini kama Wabunge kutoka kwenye Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona aibu hata kutaja hapa, lakini niruhusu nitaje kwa heshima kabisa ili wenzetu hawa wajifunze. Ukifanya hesabu ya harakaharaka hizi ni bilioni 149 nje ya mfumo wa electronic, hivi hii guts wanatoa wapi hawa? Ninaomba nirudie kusema bado huu ni mwaka wa nne ninasema bado Bunge letu halijafanya kazi ya kung’ata. Bunge letu lipo halijafanya kazi ya kung’ata ili kila mtu ajue kwamba Bunge lina jukumu la kusimamia na kuishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe mfano, Taasisi ya Wakala wa Barabara inazo 82, Shirika la Magereza 6,551, Wizara ya Elimu 51.24, halafu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Musoma 591. Ukiyataja haya unapata kichefuchefu hivi hawa watu hii nguvu wameitoa wapi? Hii Serikali ambayo tumeipa dhamana na sisi kama Bunge tunaisimamia na yenyewe ina sheria za kufanya kazi, hawa watu wamepata wapi guts hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwamba Bunge lako hili lazima lioneshe kwa nguvu zote kwamba hatukubaliani na mchezo huu. Kila siku tunaendelea kuilazimisha Serikali itafute hela, Serikali inatafuta, lakini wanaotekeleza kule wanafanya wanavyotaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ili tuweze kufanya kazi kama Bunge, ili tuweze kufanya kazi kama Wabunge, ili kila mmoja akae kwenye mstari wake, ninaona aibu kuyasoma haya maana yake hayanipi raha. Ninaomba sana nishauri haya na haya sikuyashauri leo niliyashauri mwaka 2021: la kwanza, tuhakikishe kwamba sisi kama Bunge na Kamati zetu zote zinazohusika na mambo ya fedha kwa ujumla zifanye kazi ya kuziita taasisi zote. Wenzetu hapa wamesema wamekagua kwa mfano kwenye halmashauri 30% au 31% ya halmashauri bado. Tulisema kila aliyepewa pesa ya Serikali lazima ziwe accounted for, hilo la kwanza; (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ninaomba nirudie wito wangu nilioutoa mwaka 2021 kwamba Bunge linatakiwa kufanya kazi sambamba na Serikali. Bunge hili kazi yake ni kuisimamia na kuishauri Serikali, sasa kama sisi tumefanya kazi ya kushauri lakini hatuisimamii Serikali maana yake sisi wenyewe hatufanyi kazi ya kutekeleza sheria ambazo tumezitunga wenyewe. Ombi langu, Bunge lichukue nafasi yake ya kuisimamia Serikali na kuishauri Serikali kwa sababu sisi tunaunda Mhimili mwingine ambao ndiyo Mhimili pekee unaoweza kuisimamia Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kwa kuwapongeza wataalam wetu wa Wizara ya Mambo ya Nje wakiongozwa na mama yetu, hakika ndani ya nafsi yangu nafarijika kwamba Wizara imepata mtaalam ambaye kwa kweli amelelewa na kukulia ndani ya chombo hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni muda mfupi nimewahi kufanya kazi naye lakini ndani ya nafsi yangu sina mashaka na uwezo wa Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake lakini Pamoja na hayo Wizara ikiongozwa na Waziri pamoja na wataalam wake ombi langu kwao warudishe heshima ya Taifa letu, warudishe umoja wa nchi yetu mbele ya jumuiya za kimataifa, tulitetereka kidogo hasa kwa sababu ya kutokuendana na wenzetu na mawazo ya wenzetu pamoja na kwamba sisi tunamini, lakini ni wajibu wetu kama walimwengu ambao tunaishi na wenzetu maana yake lazima tuishi na wenzetu ili tuweze kwenda nao pamoja na yale yote ambayo yanatupa changamoto kama walimwengu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mdogo ni suala la covid ambalo kwasasa nashukuru sana tumeanza kulivalia njuga na ninaamini sasa taaluma itatolewa na hatua za tahadhari zitaendelea ili tuendelee kuishi kama walimwengu, Tanzania siyo sehemu ya pekee Tanzania inaishi kama wanavyoishi wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Waziri Wizara ya Mambo ya Nje ni taaluma pekee, ni taaluma unique, siyo kila mmoja anaweza aka-practice mambo ya uhusiano wa kimataifa, ni taaluma iliyotukuka. Siyo kila mmoja anaweza kupangwa kwenda kufanyakazi Wizara ya Mambo ya Nje. Tumejifunza muda mfupi au miaka mchache iliyopita Pamoja na kwamba ni mamlaka ya Wizara yetu ya Utumishi kuweza kumtumia mfanyakazi yeyote kumpeleka popote ombi langu kwa Wizara yetu ya Utumishi lakini vilevile kwa wenzetu wa Wizara ya Foreign Affairs ikae ifanyekazi na wenzetu wakubaliane kwamba siyo kila mmoja anaweza akapangwa kwenda kufanyakazi hasa za kidiplomasia ndani ya Wizara hii. Tunaweza tukapeleka mwandishi wa habari, mhasibu, mpiga picha lakini kazi zinazohusu diplomasia tuwaache wanadiplomasia wafanyekazi za diplomasia ili nchi yetu iweze kufanyakazi zake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa maana hiyo hiyo ningeomba sana sasa tumezungumza wenzetu wengi hapa wamezungumza kuhusu economic diplomacy mana yake tunalazimika sasa kuondoka tulipokuwa tupo huko miaka ya nyuma, sasa hivi tunatakiwa kuangalia ni Nyanja gani na nani ambaye tunaweza kushirikiana naye hasa inapokuja maslahi ya Taifa letu. Marafiki wako wengi, lakini waswahili wanasema nionyeshe Rafiki yako nitakwambia wewe ni mtu wa aina gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani tulikuwa na mirengo ya siasa; kuna wenye siasa kali za kijamaa, kuna mabepari kuna na wasiofungamana, naamini kidogo tumeanza kutoka hapo sasa hivi tunaangalia economic diplomacy.

Ombi langu kwa Wizara tuchague marafiki zetu na tusione haya kuchagua ili mradi Taifa letu litafaidika pamoja na wananchi wake kuhakikisha kwamba tunatengeneza ajira, lakini na biashara zinafanyika ndani na nje ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imejaaliwa kuwa na bidhaa nyingi sana hasa zinazotokana na kilimo. Ombi langu sana kwa Wizara hii ifanye kazi ya makusudi wala isiogope kufungua balozi kwenye maeneo mengine eti kwa sababu tunaogopea gharama. Gharama ni pesa, lakini pesa zinatafutwa, lakini hakuna kazi kubwa duniani kama kutunza marafiki, ni kazi ya gharama, ni kazi ngumu, lakini lazima sisi kama Tanzania tuhakikishe kwamba tunaishi kama wanavyoishi wenzetu tuweze kuwatunza marafiki zetu. (Makofi)

Ombi langu sana tutafute mataifa ambayo balozi zetu zitafunguliwa, lakini kubwa liwe ni kuhakikisha kwamba Taifa letu linafaidika ili tuweze kufanyabiashara za ndani na nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati huo huo naomba nizungumzie hoja moja kuhusu wataalam wetu, ni kweli kwamba tunafundisha, ni kweli kwamba watoto wetu vijana wetu wanasoma kwenye maeneo mbalimbali, ombi langu kwa Serikali wenzetu hawa kama mtakumbuka hotuba aliyoisoma Mheshimiwa Waziri ukiipitia kwa ndani utagundua kwamba mambo mengi waliyoyapanga walishindwa kuyatekeleza kwa sababu tumeshindwa kuwapatia uwezo. Sasa tutaendelea kuwalaumu, tutawashambulia, lakini ukweli ni kwamba sisi kama Bunge tumepitisha bajeti, tumeidhinisha walichokitaka, bahati mbaya sana tulishindwa au Serikali haikuwapatia fedha kama ambazo walizoomba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali ili wenzetu waweze kufanya kazi zao na ili kesho na kesho kutwa tuje tufanye tathmini walichokiomba na walichokifanya, naiomba sana Serikali tuwapatie uwezo wenzetu ili waende wakafanye majukumu waliyojipangia ili Taifa letu lifaidike. Kama unajipangia kazi za Serikali halafu Serikali yenyewe haikuwezeshi maana yake ni kama vile tunatwanga maji kwenye kitu. Ombi langu kwa Serikali tuhakikishe kwamba tunawapatia wenzetu hawa ili waweze kufanyakazi zao kama walivyojipangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo linaweza likaungana na hili niliwahi kusema kule nyumba kwamba tutawalaumu Wizara zote tutazilaumu tutalaumu Mambo ya Nje, Polisi, Jeshi tutawalaumu Wizara ya Maji, Miundombinu tatizo siyo Mawizara, tatizo ni sisi wenyewe kama Wabunge tumeshindwa kuchukua nafasi yetu ya kuisimamia Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wajibu wetu basi kuisimamia na kuishauri ili waweze kupatiwa fedha wenzetu hawa wahakikishe wanatekeleza majukumu yao, then ndiyo tuje tuwahukumu hapa kwamba kuna kitu hawakutekeleza tuanze kulalamika. Vinginevyo kila mwaka tutapitisha bajeti haiendi, kila mwaka tutapitisha bajeti kwa sababu tumeiachia Wizara ya Fedha kwa mujibu wa makubaliano yetu kwamba ndiyo iamue nani impe, nani isimpe, impe lini, impe kiasi gani, hili halijakaa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nawaomba sana naiomba sana Serikali naliomba sana Bunge hili tuone namna gani tunaweza kusimamia au kufanyakazi yetu kama Wabunge kusimamia Serikali lakini kuhakikisha yale tunayoamua humu ndani basi yanatekelezwa kwa mujibu ambavyo tumeamua, vinginevyo sisi hatufanyi wajibu wetu na Serikali hatuisaidii ili iweze kuwahudumia wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nishukuru kiti chako kwa ufupi. Pili, naomba niseme kwamba ninashikiri au niko kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama. Nimekuwa nikijaribu kuwasikiliza Waheshimiwa Wabunge hapa kwa muda mrefu toka tumeanza Bunge kuna jambo linaendelea kujitokeza sana. Sasa naomba hasa wenzetu wa Serikali hili walitafakari tena kwa kina na hatua za dharura zichukuliwe.

Mheshimiwa Spika, mara nyingi tunapata mafunzo au tunachukua hatua tunapoona matokeo yanazidi kukithiri. Siku chache zilizopita tulisikia tatizo dogo kutoka kutoka TRA kwamba mifumo kila siku iko chini lakini baadaye tukasikia tatizo la TANESCO kwamba watu hawawezi kununua LUKU lakini hapa kiongozi amerudia tena kuongelea suala hili inaonekana limerudiarudia. Ombi langu kwa TANESCO, tuko kwenye cyber war, kuna kitu tunaita cyber war na kitu tunaita cyber-crime, umeme ndiyo unaotumika kupeleka athari zote kwenye mifumo yetu. Naomba sana na hili TANESCO mliangalie sana, vinavyotokea havitokei kwa bahati mbaya, ni mambo yanayopangwa na yanapangwa yatokee ili siku moja tu-collapse. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie wenzetu kwamba TANESCO tumewapa kuongoza Serikali kwa sababu leo maji tunalipia kwa internet, umeme tunalipia kwa internet maana yake ni kwamba hata benki zetu zinatumia internet kufanya mambo yake maana yake ndiko kelele ziliko. Hata hivyo, internet leo inawezeshwa kupitia kwenye umeme, ombi langu kwa TANESCO haya mambo hayaji kwa bahati mbaya iko siku sote tuta-faint kwa sababu tunaelekea kwenye cashless economy ni kwamba ni mitandao ndiyo inayotuwezesha kufanya mambo yote maana yake tumewapa kuendesha Serikali kwa kutumia umeme. Tunawaomba sana muwe makini na suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkiangalia attempt zinazofanywa BoT, iko siku tutawaomba hapa waje watuambie attempt za mara ngapi zinafanywa kwenye benki zetu kwa kutumia internet ambazo zinapitia kwenye umeme. Tunawaomba sana tumewapa shirika hili au taasisi hii muweze kutulindia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu alitukumbusha kwenye backup maana yake tuweze kujilinda lazima tuwe na plan B na plan C kwenye kujilinda ili tusifikie siku tukawa hatuwezi au kila kitu kime-paralyze kwa sababu ya internet kumbe siyo internet ni kwa sababu ya umeme. Kwa hiyo, nawaomba sana mlitilie maanani suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili naomba uendelee kutusaidia wataalam wetu walikumbuke kwamba umeme ndiyo unaotumika kupitisha kila kitu. Juzi Marekani nadhani mmeona wataalam, Serikali ya Marekani ililazimika kuwalipa wataalam wa IT ambao huku tunawaita hackers, si kwa sababu walipenda kwa sababu system zao za mafuta ziliingiliwa na hackers, waliwalipa! Pamoja na policy zao kwamba hatuzungumzi na watu ambao hawahusiki na system zetu lakini waliwalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba shirika letu au Wizara yetu ilisimamie suala hili ili kuhakikisha kwamba hatufiki mahali tukashindwa kufanya mambo yetu kwa sababu tumeshindwa huko. Lazima tuwe na wataalam wetu wa ndani ambao watalinda mifumo yetu ili tusishindwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kuongea kwa ufupi; la kwanza tupo kwenye kitu tunaita crisis management. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Mbunge, tatizo letu tunataka wananchi wa-feel kwamba Bunge linafanya kazi yake na Serikali inatusikiliza kwenda kulifanyia hili. Naomba tufanye yafuatayo, kwa sababu tunajua chanzo cha tatizo na tunajua tutokee wapi; kuna tozo, kuna kila kitu; watu wanasubiri majibu, ningeomba Serikali kwa haraka iwezekanavyo; tutazungumza mpaka asubuhi hapa hatutafikia mahali isipokuwa Serikali waje na jawabu tunatokaje hapa ili kupunguza maumivu ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamezungumza huko vita, kitu gani, hatuna tatizo, lakini vita ni opportunity, kwa hiyo huko mbele ya safari tutajua nini cha kufanya, lakini leo tunawaomba sana Serikali njooni na majibu, sasa hivi nini kinafanyika, tupunguze tension ya wananchi ili maisha yarudi kama kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani na kupewa Tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nikushukuru kwa kunipa heshima, hii ni heshima kubwa ambayo kwa kweli sikuidhania wala sikuiamkia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kusema kwa niaba yangu lakini kwa niaba ya Wabunge wenzangu, kwamba Mama sisi kama Wabunge tunakupongeza sana sana sana. Kwa kawaida upo msemo wa Kiswahili unasema hakuna Nabii aliyewahi kupendwa kwao lakini mama sisi wenzako, Wabunge wenzako tunakupenda, tunakuthamini sana sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kwenye hili nadhani ipo nafasi ya sisi kama Wabunge lakini sisi kama taifa kuanza kujitathimini upya kwasababu si lazima tusifiwe na wengine tunayo nafasi ya kujisifu na kusifu vya kwetu. Mheshimiwa Rais amefanyakazi kubwa, Mheshimiwa Rais anafanyakazi kubwa tunaiona, tunaithamini. Kwa hiyo, tunaomba tukupe moyo ili uendelee kufanya mema zaidi ili watanzania waendelee kufaidika kwa kuhakikisha kwamba unawaondoa walipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa maana yangu ni nini, zawadi au chombo hiki kilichotolewa ni kuashiria kazi kubwa aliyoifanya na anayoifanya mama kwaajili ya maslahi ya taifa lake. Mimi ningeomba mama yetu asirudi nyuma na sisi wabunge kwa kushirikiana na wananchi tuendelee kumpa moyo ili aone kwamba bado anahitajika kufanya mambo mazuri zaidi. Asiogope mama yetu kwasababu atakapofanya jema na sisi Wabunge tukaliona, tukamuunga mkono maana yake hili ndilo ambalo Watanzania wanalolitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba niseme kwa ufupi hivi, kwamba kwasababu dunia imeona, kwasababu Afrika imeona, kwasababu Wabunge wenzangu mmeona maana yake ni nini, ni kuonesha kwamba mama yetu tokea ameteuliwa kuwa Makamu lakini pia kuteuliwa kushika nafasi ya chombo hiki kama taifa maana yake amekubali kuendeleza yale yote waliyoyapanga na yanakwenda mbio na hayasimami. Kwa hiyo, ningeomba sana sisi tumpongeze kwa kauli moja kama tulivyofanya lakini tumpe nguvu tukimuambia kwamba tupo pamoja na yeye, tutafanya naye kazi na hakika hatutamuangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa nafasi, lakini ningeomba niseme ni yeye pamoja na mawaziri wake lakini kwa kusaidiwa zaidi na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Rais wa Zanzibar naye, kwasababu haya wanayafanya kwa umoja wao. Kwa hiyo, zawadi hii imetolewa kwa viongozi wetu wote ambao wanasaidia kuliongoza taifa hili. Nawapongeza, nawashukuru sana sana, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nichangie kidogo kwenye hoja hii, lakini naomba nianze kwenye kitabu chetu kitukufu, kinaitwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba nianze kwenye Kifungu cha 62(1) Sura ya 3 ya Katiba hii. Kuna chombo kimoja kinaitwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba ninukuu: (Makofi)

Kifungu cha 62(1) kinasema: “Kutakuwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano, ambalo litakuwa na sehemu mbili; yaani Rais na Wabunge.” Naomba niendelee kwenye Kifungu 63 (1): “Rais kama sehemu moja ya Bunge atatekeleza madaraka yote aliyokabidhiwa na Katiba hii kwa ajili hiyo,” lakini 63 (2) inasema: “sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.” Hili ndiyo Bunge la Jamhuri ya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee 63 (3) (d) kinasema hivi: “Kwa madhununi ya utekelezaji wa madaraka ya Bunge, laweza (b) kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa Bajeti.”

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nichangie. Nimekuwa nikifuatilia bajeti zetu za miaka mingi, Bunge linakaa kama chombo chenye mamlaka iliyopewa na wananchi, lengo ni kuziandalia Wizara hizi na kuzipitishia bajeti zake kwa mujibu wa zilivyoomba. Marekebisho yanafanyika, lakini hatimaye Bunge linapeleka fedha kwenye Wizara husika. Matokeo yake ni nini? Matokeo yake ni kwamba mara nyingi tunarudi kwenye kuangalia Bunge au Serikali imetekelezaje bajeti kwa mwaka uliopita? Pia kuangalia kwa mwaka ujao.

Mheshimiwa Spika, mara nyingi kwa masikitiko makubwa tunashindwa au Wabunge tunalalamika kwamba Serikali kupitia Wizara ya Fedha haipeleki fedha zinazotakiwa kama tulivyopitisha. Sasa maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba Bunge kama Bunge linafanya kazi yake ya kupitisha lakini Bunge linashindwa kusimamia bajeti iliyoipitisha ili kuhakikisha kwamba kila Wizara inafanya kazi kwa mujibu wa maelekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ombi langu, ukiangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Wizara ya Fedha ina majukumu 10 imejipangia pale. Moja katika hayo ni kuhakikisha kwamba Serikali inatekeleza bajeti kama ilivyoahidiwa au ilivyopitishwa na Bunge. Bahati mbaya sana kwamba kwa asilimia kubwa Wizara nyingi tunakuja kuzilaumu hapa kwamba hazikutekeleza; wenye maji wanalalamika, wenye barabara wanalalamika, wenye kilimo wanalalamika, uvuvi wanalalamika, kila Wizara kwa asilimia kubwa tunakuja kulalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu kwa Bunge lako, Bunge lichukue nafasi yake ya kupitisha lakini kusimamia ili miaka ijayo au mwaka mwingine wa fedha tusije kumlaumu mtu, kwa sababu kazi yetu kubwa hapa tumeambiwa sisi kama Bunge ni kuisimamia Serikali na kuishauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama hoja ni hiyo, ombi langu na ushauri wangu kwa mujibu wa kifungu hiki cha 63 (2) naomba basi kushauri kwamba Bunge hili sasa likubali kutunga au kuandaa Kamati ambayo itafanya kazi ili Wizara ya Fedha pamoja na mambo mengine, kazi zake kubwa ziwe mbili: kwanza, kutengeneza sera na ya pili iwe ni kukusanya, period. Hii ni ili Bunge hili lije lifanye kazi ya kusimamia fedha zilizokusanywa na kuzipeleka kunakohusika ili tuje tujiulize wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nilishauri Bunge lako lifanye kazi ya kuunda Kamati ambayo ndiyo itafanya kazi ya uhakika kuhakikisha kwamba kile ambacho tumekipitisha kama Bunge, basi kinapelekwa kwenye Wizara zote na taasisi zote ili baadaye tuje tujitathmini wenyewe na wala siyo Serikali kuja kutuambia hiki sikupeleka. Maana yake kwa taratibu hizi tumewaachia Wizara ya Fedha mamlaka ya kujiamulia nani wampe? wampe nini? Kwa wakati gani? Kwa kiasi gani? Hii siyo kazi ya Wizara ya Fedha, ni kazi ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maneno haya mafupi, naomba kuchangia hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru. Mimi napenda kuchangia kitu kimoja tu, lengo la Serikali yetu hii ni kuhakikisha kwamba tunaondoka tulipokuwepo tunapiga hatua za mwendokasi ili kuhakikisha wananchi wanayaona na wana-feel maendeleo ambayo Serikali yao imeamua kuyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewasikia Waheshimiwa Wabunge wengi hapa wakizungumza juu ya maendeleo au mikwamo ya maendeleo inayotokana na jitihada za wananchi, hasa wakulima wetu. Mapendekezo yalitoka hapa na moja ya eneo ambalo bado hatukui, kila siku tunaendelea kupiga mark time, ni eneo hili tunaloliita la road and fuel toll, maana yake ni nini? Ukiangalia statistics za matumizi yetu ya mafuta kwa miaka yote hatukui, leo tuna miaka saba, lakini magari yanaendelea, kampuni zinakuja, mafuta yanatumika, lakini hesabu zinaonekana tuko palepale hatukui. Maana yangu ni nini, tunalo tatizo kwenye hesabu zetu au kwenye statistics zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Serikali imeleta maboresho, kwanza mnisamehe mimi si mwanasheria by profession, naomba nisome hiki ili nitafsiri kwa lugha isiyo sahihi au isiyo official. Kifungu 47 kinasema:

“The principal Act is amended in section 4A by deleting paragraph (a) and substituting for it the following:

“(a) Tanzania shillings 363 per litre imposed on petrol or diesel shall be deposited into the account of the Fund:

Provided that, Tanzania shillings 100 per litre imposed on petrol or diesel out of the Tanzania shillings 363 per litre shall be allocated to Tanzania Rural Roads Agency and the remaining Tanzania shillings 263 per litre shall be distributed amongst the Fund and the Tanzania Rural Roads Agency in the manner prescribed in the regulations made by the Minister in consultation with the Minister responsible for local government.”

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini? Tumekusudia kuondoka tulipokuwa kwenye shilingi 263. Waheshimiwa Wabunge wameomba tuongeze shilingi 100 iwe shilingi 363. Kwanza shilingi 100 hii imewekwa makusudi iende TARURA peke yake, lakini katika shilingi 263 tunayo shilingi 78.90 ambayo na yenyewe inarudishwa kwenye hii ili tuwe na shilingi 178.90 ili tuweze kupiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwenye hili ningeomba sana kusiwe na mchanganyiko hapa kwamba Waziri kwa kushauriana na nini, hapana. Tuiseme categorically kwamba shilingi 178.90 inakwenda kutumiwa na TARURA full stop. Tusiwape watu nafasi ili tuweze kuja kujitathmini kwamba tulipata hela hii tukaiweka hapa ili ifanyiwe kazi na TARURA. Tusimpe mtu mwingine nafasi ya kuweza kuamua kuwapa au kutokuwapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mchango wangu mimi kwenye hili ni kuipongeza Serikali kwa kusikiliza Wabunge, lakini kuliomba Bunge lako hili tuzungushe wigo hapa tusimpe mtu nafasi ya kuamua yeye. Sisi tumeamua utekelezaji ukafanywe moja kwa moja. Nakushukuru. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niwe sehemu ya wachangiaji katika Muswada huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, naomba niseme kwamba amani tuliyonayo Watanzania ni mtaji, amani tuliyonayo ndiyo kivutio cha wawekezaji, na amani tuliyonayo ndiyo msalaba tulionao na tunatakiwa kuutunza kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani? Uhalifu na ugaidi ni vitu vinavyoendana. Tofauti yetu hapa ni maana ya neno ugaidi. Ila ugaidi ni uhalifu uliokithiri ambao unaweza kutoka nchi moja kwenda nyingine. Yuko mwenzetu amesema hapa kwamba vitendo vya kigaidi vinaweza vikapangwa katika nchi nyingine lakini vikatekelezwa katika nchi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni nini hapa? Ni kwamba amani tuliyonayo kama Watanzania haikuja kwa bahati mbaya. Amani tuliyonayo haikai hapa kwa bahati mbaya, ipo kwa sababu kama Taifa tumeamua; ipo kwa sababu Taifa linawekeza fedha nyingi kwa ajili ya kulinda amani ndani na nje ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tuweze kuendelea na ili tuweze ku- maintain amani tuliyonayo, sisi kama Watanzania, majirani zetu na dunia yetu, ugaidi ni jambo linalosomewa. Huwezi ukaibuka tu leo ukawa gaidi. Kuna vitendo vya ku-recruit, ku-train na ku-equip. Lazima uwezeshwe uwe gaidi, huwezi ukaamka leo ukasema mimi nataka kuwa gaidi, haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mambo haya hayaji kwa bahati mbaya. Sisi kama Watanzania tuna mtihani mkubwa kwa sababu amani tuliyonayo wenzetu inawapa matatizo na wako katika kutujaribu kila siku, kwamba kwa nini Tanzania iendelee kubaki kuwa na amani? Kwa nini wawekezaji waende Tanzania? Kwa nini tusiharibu image ya Watanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ombi langu kwa Waheshimiwa Wabunge, ni kwamba itifaki hii, pamoja na kuchelewa kwake, lakini sasa ni wakati mzuri kwa sababu tumeichakata kwa kipindi kirefu, tumeangalia pay turn ya matatizo. Maana yake, ugaidi, kama alivyosema mwenzangu, unaweza kupangwa eneo lingine lakini ukaja ukatekelezwa kwenye nchi nyingine. Sisi kama Watanzania kwa sababu Tanzania siyo kisiwa, na kwa sababu tunaweza kuondoa tatizo moja kulipeleka eneo lingine, Tanzania ni eneo ambalo kila mtu ametazama na angependa kutujaribu kuona kwamba kwa kweli tunataka tuvunje historia ya Tanzania kwamba ni eneo la amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenu; kwanza, turidhie itifaki hii kwa sababu Tanzania siyo kisiwa, Tanzania ni eneo ambalo tunaishi na wenzetu na walishafanya ratification, nasi kama sisi tunahitaji kuwa sehemu ya dunia. Kwa sababu matukio haya pamoja na kwamba yalitokea muda mrefu kwenye maeneo mengi, lakini bado yanaendelea kwenye nchi za wenzetu, nchi za jirani zinaendelea. Nasi tumekuwa tumo kwenye majaribio. Majaribio haya ni viashiria vya kwamba bado ugaidi unaendelea na sisi kama Taifa tunahitaji taaluma, nyenzo na kuendelea kuji-equip ili tuhakikishe kwamba tunaendelea kubaki kuwa salama. Kwa sababu wawekezaji kila siku wanatafuta wapi wataweka fedha zao ambapo pana amani? Bila ya hivyo tutaendelea kuwapoteza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo niwape mfano. Tanzania inasifika baada ya Royal Tour. Royal Tour hii haikuja kwa bahati mbaya, wala siyo bahati mbaya, ipo kwa sababu vyombo vyetu viko imara, havidharau taarifa na vinaendelea kutafuta taarifa kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwetu ni kwamba tusidhani kwamba tumechelewa, hatujachelewa, lakini ni wakati muafaka ili sasa tuweze kuingia kama Taifa kwenye mataifa mengine tuweze kupata kila ambacho kinastahili kupatikana ili tuweze kufanya zoezi hili lifanyike vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo hiyo, hatuingii eti kwa sababu tu tumeingia. Tumejiridhisha vya kutosha kama Kamati, tumejiridhisha kama Taifa kwamba sasa ni kipindi muafaka kwa sababu matukio yanayoonesha ni ishara na viashiria kwamba bado tunawindwa kama Tanzania, bado tunayo nafasi ya kuungana na wenzetu. Vile vile hatusubiri tatizo litokee. Ndiyo maana sheria zetu zinasema kwamba tuna-prevent kwanza halafu ndiyo runa-combat.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenu ni kwamba turidhie itifaki hii ili tuweze kuendana na tuweze kutumia facilities zote zilizoko dunia nzima kuweza kupata taarifa na kuzitumia kwa ajili ya kushughuika na hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo hiyo, wanaokuwa-recruited ni vijana wetu, watoto wetu wadogo ambao wanaghilibiwa ili kuweza kuingia wakioneshwa kwamba hapa kuja jambo haliko sawa, kwa hiyo tuingie. Kwa hiyo, naomba; mwenzangu amesema hapa, na Mheshimiwa Waziri amesema, kwamba mara nyingi hili linatakiwa lianze ulinzi kwenye nyumba zetu, familia zetu, mitaa yetu, ili kila mmoja aweze kufahamika tabia zake na nyendo zake, itusaidie kuendelea kulinda heshima yetu kama Taifa, itusaidie kutulinda sisi na kuhakikisha kwamba na wenzetu wanaendelea kuwa na amani na imani kwamba Tanzania bado ni nchi iliyo salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile na watoto wetu, kwa sababu hili siyo kwamba tumelizungumza kama Kamati kwamba hatuna ushahidi. Kama mtakumbuka miaka michache nyuma, watoto waliotoka Uingereza na Mataifa mengine, wamevutika tu na neno ugaidi, wamekuwa recruited wamekwenda kufunzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwamba ili tuweze kuwazuia watoto wetu wasiingie katika mkumbo huu wa kughilibiwa na wakadhani kwamba hiki ni kitendo cha fahari, siyo fahari. Ugaidi ni tendo la kudhalilisha utu wa mtu na sisi kama Bunge tunayo nafasi na wajibu wa kuhakikisha kwamba tunazuia vitendo hivi visifundishwe kwa watoto wetu kwa kuwa-recruit lakini kuwapeleka halafu wakaja wakatudhuru sisi au wakadhuru binadamu wengine wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, nawaomba sana kwamba hili tulichukue, turidhie ili tuendelee kuwa Taifa lenye salama na amani ili tuendelee kubaki kama Tanzania ambayo tumeirithi na sisi tuwarithishe vizazi vyetu ikiwa bado ni Taifa lililo salama. Ninawaomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kusema kwamba amani tuliyonayo ndiyo mtaji, amani tuliyonayo ndiyo fahari tuliyonayo ambayo dunia nzima inaihitaji na tungependa kama Kamati, kama Bunge, tuendelee kuwa Taifa lenye utulivu na kila mtu akiliheshimu akijua kwamba hapa ndipo eneo la kukimbilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kuliko hayo, nimezungumza hapa nyuma kidogo kwamba Royal Tour haikuja kwa bahati mbaya. Royal Tour imetufungulia mambo mengi sana lakini moja kubwa zaidi ni kuongeza imani ya watalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwape kisa kimoja. Watalii ni kama njiwa. Kama wapo wenzangu hapa waliowahi kufuga njiwa; njiwa kwa kawaida hata ukimwaga mchele anakuja mmoja mmoja, wa pili, wa tatu, wanakuwa wengi; lakini ukidondosha jiwe, wanaondoka wote kwa wakati mmoja. Kwa hiyo, ombi langu, tusidhani kwamba jambo hili linawafurahisha wote. Hili linatufurahisha sisi kama Watanzania lakini tumepeleka au linaonekana ni tatizo kwa competitors wetu kwenye mambo ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana litusaidie kuhakikisha kwamba tunalinda Royal Tour yetu ya kwanza na ya pili na ya tatu itakayokuja kwa kuhakikisha kwamba tunaendeleza amani, na dunia iendelee kuamini kwamba bado Tanzania ni eneo salama, utalii uendelee na sisi tuweze kupata yale ambayo Taifa limejipangia ili kufikia malengo yake kwenye suala la utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima sana, naomba niunge mkono hoja, lakini naomba turidhie kwa faida yetu kama Bunge, kama Taifa, kama East Africa, Afrika na jumuiya za Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii adhimu. Kwa sababu ya muda, naomba nijikite kwenye mambo manne kwa ufupi na ninaamini wenzangu watanielewa.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, tunayo hoja ya mambo ambayo Mheshimiwa Waziri ameyazungumza ambayo tumekubaliana. Ameyataja katika hotuba yake. Naomba kushauri kwamba haya ambayo tumekubaliana, basi sasa mchakato wa kisheria uendelee ili mambo haya yaeleweke kisheria kwamba sasa ni mambo tuliyokubaliana na yanatambulika kisheria. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, tunayo hoja ya mazingira. Mimi natoka Jimbo moja linaitwa Mwera. Kwa lugha ya kawaida, Mwera ni mbali sana, lakini kiuhalisia Mwera ipo mjini, imezungukwa na majimbo mengi sana. Mwera ni chimbuko la maji, ni chimbuko la chakula, ni chimbuko la matunda na ni chimbuko la Zanzibar. Kwa sababu Mwera hii ndiyo ambayo imeleta Mapinduzi ya Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana kwa sababu tumejaribu lakini bado tunayo changamoto. Mwera tunayo changamoto ya uharibifu wa mazingira, hasa kwa sababu maji yanatuathiri sana. Sasa kwa ufupi kabisa naomba Wizara yako na hili lichukuliwe kwa sababu tulishazungumza na hali halisi unaielewa, Mwera unaielewa na umeshakwenda siyo mara moja; siyo mara mbili na siyo mara tatu.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Mwera itazamwe kwa jicho maalum ili kujua inasaidiwaje kutatua tatizo letu la mazingira. Mwera inaumia, Mwera inaangamia, Mwera inazama kwa sababu kila mvua inapokuja Mwera tunaingia kwenye matatizo ya mafuriko. Naomba sana iwe ni mradi maalum wa kusaidia Mwera ili kuiondolea tatizo la kuzama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine dogo kabisa, tunazungumza issue ya nafasi za ajira za Muungano. Hizi nafasi kwa mujibu wa sheria, tumekubaliana Zanzibar watapata ngapi, wenzetu watapata ngapi? Sasa sipo kwenye hoja hiyo; hoja yangu ipo kwenye hili; mara nyingi tunaangalia vijana wetu ambao wamepata nafasi ya kwenda kwenye Jeshi la Kujenga Taifa au Jeshi la Kujenga Uchumi. Sasa hiki kimekuwa kigezo kikubwa, kwa hiyo, vijana wetu wengi wanakosa nafasi hii kwa sababu hawakupata nafasi ya kwenda kwenye majeshi haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama Serikali hatuna uwezo wa ku-absorb vijana wote hawa wakaenda kwenye majeshi yetu, hatuna nafasi hiyo, kwa hiyo, hawawezi kwenda wote kwenye Jeshi la kujenga Taifa wala hawawezi kwenda wote kwenye Jeshi la kujenga Uchumi, nawaomba sana, kigezo hiki cha kwamba mtu amepitia kwenye JKU au JKT kisiwe kigezo pekee. Hiki kiwe ni nyongeza, lakini muhimu iwe elimu na vitu vingine ndiyo viwe vinazingatiwa. Siyo kwamba eti kwa sababu hakwenda JKT au JKU, ndiyo kigezo cha kumfelisha, naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha mwisho, amezungumza pale kaka yangu issue ya kuheshimiana. Naomba nirudie hapa, kwamba ili mradi sisi ni binadamu, hakuna nafasi kwamba tutakuwa wakamilifu mpaka tunayoingia kaburini. Kwa hiyo, nawaomba sana wenzetu, taaluma ya Muungano mwendelee kuitoa kwa sababu bila ya hivyo tutaendelea kulumbana kila siku; na bila hivyo kila siku tutaendelea kuona tuna matatizo. Matatizo ni sehemu yetu na yataendelea kutatuliwa taratibu, lakini kubwa tuendelee kutoa elimu kwa sababu bila elimu, kila siku tutazungumza hayo hayo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya upendeleo, ili niwe ni miongoni mwa Wabunge ambao wamechukua nafasi hii kuunga mkono azimio hili la kumpongeza mama yetu. Sasa naomba nisema hivi, na nitazungumza kwa ufupi, ili na wengine wapate nafasi.

Mheshimiwa Spika, naomba kwanza kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu. Tumshukuru kwa sababu, kwanza ameamua kutekeleza kwa vitendo kulinda na kuheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwenye hili, waswahili wanasema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni; kwa kitendo chake cha kushirikisha vyama na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha kwamba, nchi yetu inaendelea kuwa na amani na yenye maendeleo, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa maana hiyo kwenye mfumo huu wa demokrasia kuna msemo wa Kiswahili unasema, wengi wape lakini wachache wasikilizwe. Kwenye hili, mama yetu ameonesha mfano kwa vitendo na sisi kama Wabunge, kama Bunge, tunao wajibu wa kuendelea kumuunga mkono kwa sababu ni jambo alilolifanya kwa vitendo kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naomba niendelee kusema hivi kwamba, kwenye hoja ya mambo ya uchumi mama yetu amefanya mambo mengi. Wenzangu wamezungumza mambo mengi sana, ametoka nje, ametafuta wawekezaji, Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza pale wawekezaji wengi wako njiani wanataka kuja, sisi naomba Waheshimiwa Wabunge tumuunge mkono mama yetu. Tumuunge mkono kwa sababu, jitihada hizi zinahitaji amani, jitihada hizi zinahitaji imani, bila ya imani wawekezaji hawawezi kuja, lakini bila ya amani wawekezaji pia hawawezi kuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule nyuma niliwahi kusema kwamba, amani tuliyonayo Tanzania ni tunda adimu ambalo duniani halipo, tuendeleze. Na sisi Wabunge tukishikamana tunaweza kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ningeomba basi kwa sababu, jitihada zote zinazofanyika ni kuweka nchi pamoja, ni kuweka wananchi pamoja, ili tuweze kujenga Taifa letu, ningewaomba sana basi tumuunge mkono katika jitihada zake za kuhakikisha kwamba, uchumi unaendelea kukua. Mama yetu naomba tukuthibitishie uchumi huu utakua, lakini na wewe mama yetu endelea kutupa nguvu, ili tukupe nguvu, ili kazi ziende vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hili kwa sababu hii, Mheshimiwa Ole-Sendeka amezungumza hapa kwamba, kwa kweli mama yetu anafanya jitihada za kuleta wawekezaji, lakini tuko baadhi yetu ambao tunamshika mashati, ili kumrudisha nyuma. Kule nyuma mama aliwahi kusema, rangi zake ni nyingi tusizitafute, lakini juzi tumeiona moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba niombe hivi, na ninaomba niombe kwa heshima kubwa sana, mama amezungumza lugha nyepesi ya kistaarabu wale wenyewe wajitathmini na watupishe. Sikuelewa hiyo lugha yake, lakini naomba niiseme hivi, wale waliopewa nafasi na wanazijua nafasi zao kwamba, mama amechukia kwa sababu tunamrudisha nyuma, naomba sana tumpishe ili afanye kazi zake, tusimrudishe nyuma. Na mama yetu tunakuomba sana, umewapa nafasi na waswahili wanasema mwenye kuvuliwa nguo huchutama, naombeni sana wale wote wenye kujijua hili wasisubiri kuvuliwa nguo halafu tukawazomea maana kwa kweli, tutawazomea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa heshima na taadhima Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono jitihada hizi, mama amefanya kazi kubwa, anaendelea kufanya, lengo na dhamira yake ni kuhakikisha kwamba, Taifa letu linasonga mbele, naomba sana. Kwenye hili naomba nitoe angalizo au nitoe pendekezo; mnaposafiri baharini wako wengine wanayo kawaida ya kutoa boti, sasa ili boti hili lisizame naomba tukubaliane hivi, wale ambao tunawaona wanaendelea na wana jitihada za kutoa boti, ili tusifike safari yetu, tunaomba tuwatose kabla hatujazama sote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi, lakini naomba pia ikikupendeza au ikupendeze, endapo nitakukwaza kwa muda wako basi univumilie kidogo ili tuweze kusaidia mchango kwenye otuba hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja, na pia nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu ndiye nguzo anayehakikisha kwamba Muungano wetu huu unaendelea kubaki kuwa Muungano; lakini ni kiongozi anayeongoza kwa upenzi, kwa masilizano, kwa mashirikiano wala haongozi kwa bakora. Kwa hiyo mimi naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini vile vile naomba nimpongeze na Rais wa Zanzibar kwa sababu watu wawili hawa ndio wanaotengeneza kitu kinachoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bila ya hawa na bila ya kufuata misingi ya Katiba, Sheria na Kanuni zetu maana yake hakuna kitu kinachoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake wote, bila ya kuwasahu wenzetu waliopewa dhamana ya kusimamia Wizara inayohusu mambo ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa leo niende kwenye namba lakini sitaingia kwenye namba, leo nitaingia kwenye foundation ya Muungano. Wenzetu hawa wamepewa chombo kikubwa sana, wamepewa chombo ambacho ndicho kinachoshikamanisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bila Dira kukihenga henga chombo hiki sisi sote hapa hatuna sababu ya kuwepo. Kwa sababu tunakuwekwa hapa kwa kuwaenzi wazee wetu walipoamua, na wazee wetu waliamua kuunda kitu kinachoitwa Tanzania si kwa sababu ya Sheria, si kwa sababu ya Kanuni ila ni kwa sababu ya mapenzi waliyokuwa nayo kwa kitu kinaitwa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba ninukuu kidogo na ikupendeze. Kwenye katiba yetu hii kwenye eneo la kwanza kabisa la utangulizi, halafu mengine yatafuata; naomba ninukuu kwa heshima. Anasema hivi, Misingi ya Katiba; Na kwa kuwa sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa haikuzungumzwa katiba wala sheria, naomba nirudie, imesema misingi ya uhuru, haki, udugu na amani. Wasomi wamekuja baadaye wakatutengenezea mambo yote haya lakini kubwa ni uhuru na imani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maana yake ni nini? Naomba niwaombe ndugu zetu hasa waliopewa dhamana ya kuunda au kusimamia Wizara inayohusu mambo ya Muungano, kwamba wako wazee wetu waliounganisha pamoja na mama yangu amesema pale kwamba tumeunganisha mchanga sasa tunaunganisha damu. Sasa naomba niseme hivi iko misingi ya kuunganisha zaidi imetajwa katika Katiba yetu, lakini kuna Vyombo viwili ambavyo vimetajwa katika Katiba hii ambavyo wasomi wetu wametuletea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye ukurasa wa 88 wa Katiba hii au kwenye Kifungu cha 102 kwenye Sura ya Nne inazungumza kitu kinachoitwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Maana yake Sura yote ya Nne inazungumza uwepo wa Zanzibar na Serikali yake. Vile vile, kwa maana hiyo hiyo kuna kitu kinaitwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, kuna kitu kinaitwa Makamu wa Rais, kuna kitu Kinaitwa Waziri Mkuu, lakini kuna hiki kitu kinaitwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hivi ndivyo vifaa vilivyoundwa kwa mujibu wa Katiba hii ili kuifanya Katiba yetu na nchi yetu iwe moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ombi langu ni hili, sababu ya kunukuu hii inaonekana au wengine wasomi wanaamini kwamba Katiba ndio Tanzania. Naomba tu niwambie Tanzania ni mapenzi ya damu. Tuliwahi kusema huko nyuma kwamba tumeungana kwa sababu ya mapenzi, ningewaomba wenzetu hasa wanaosimamia hili, waelewe kwamba wapo walioamua kwa makusudi ili kuifanya Tanzania ibaki kuwa Tanzania. Kwa hiyo ombi langu sana kwao, waendelee kuheshimu makubaliano tuliyokubaliana, wameyataja wenzetu wengi hapa. Kuna mambo ya ajira, kuna mambo ya mazingira, kuna mambo mengi tu. Naomba waendelee kuheshimu kwa sababu dhamana hii waliyopewa waelewe kwamba ina kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwakumbushe wenzangu kwamba tumetoka mbali. Mara baada ya Muungano wa mwaka 1964 kulikuwa na kitu kinaitwa mutiny, sijui kama mliwahi kukumbuka vijana wenzangu, hii kwa Kiswahili ni uasi lakini kwa sababu kuna kitu kinaitwa Jamhuri, naomba niwakumbushe wenzangu kwamba uwepo wa Zanzibar ndio ulisababisha Muungano ukawepo kwa sababu jeshi lililoko upande wa Zanzibar lilikuja kuchukua nafasi huku ili kuhakikisha kwamba Tanzania inaendelea kuwa salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuelewe kwamba, kwanza kila upande wa Muungano kwa maana ya Zanzibar na Bara wote ni maeneo yaliyo sawa kwa mujibu wa Katiba hii. Hata hivyo, kwa maana hiyo hiyo ningeomba kwamba hata Wabunge walioko humu nashukuru hata katiba imesema, Wabunge wote waliotoka kwenye majimbo, waliotoka kwenye maeneo mbalimbali wote ni Wabunge walio sawa, hakuna aliye bora wala hakuna aliye na daraja la pili. Kwa hiyo, ningeomba sana wenzetu wa Muungano waendelee kutekeleza dhima yao ya kuhakikisha kwamba Muungano unaendelea kudumu kwa sababu sasa si matashi tena, sasa ni damu. Hatuna nafasi ya kurudi nyuma tunayo nafasi ya kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba kuendelea. Kuna hoja wameizungumza wenzangu hapa, kwamba hoja ya jambo la mazingira. Amesema Profesa pale na amesema dada yangu pale kwamba tumeweka bajeti asilimia ndogo kwa ajili ya kupambana na mazingira. Wanasema kutenda kosa sio kosa, lakini kosa ni kurudia kosa. Ningeomba sana na hili namwomba Mheshimiwa Waziri alitafakari sana kwa sababu kuishi ni haki yetu kwa mujibu wa Katiba, lakini kutengeneza matatizo ambayo yatatufanya sote tuondoke ni kinyume cha Katiba, kwa sababu Katiba inatutaka tuishi, imetupa mamlaka ya haki ya kuishi. Kwa hiyo, ningeomba wenzetu wa Wizara kwamba bajeti inayokuja wahakikishe kwamba kwa asilimia kubwa lazima tutengeneze mazingira ya ku-survive sisi kama Tanzania. Tunapoendelea kutegemea wafadhili hata kama kwa sababu wamefanya commitment. Commitment ni jambo lingine, lakini commitment inatakiwa ianze na sisi kama watanzania. Kwa sababu hatuwezi kusubiri mwenzetu ajengewe ukuta kwa sababu athari inamuathiri Nungwi kule eti mpaka mfadhili aje, lazima tuanze sisi wenyewe, tusisubiri wafadhili waje eti ndio tuanze kujenga ukuta wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Tanga pale kunaliwa na Bahari, eti tumsubiri mfadhili aje atufanye kazi ya kutujengea ukuta kwa sababu sisi hatuna nafasi hiyo. Naomba sana kwamba tuzingatie bajeti yetu kwa maana lazima iwe na priority ya mambo yetu ya athari za mazingira kwa sababu ni wajibu wetu na ni haki yetu kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, pamoja na kwamba muda umeisha ningeomba sana kwamba suala la mazingira ni suala la kufa na kupona…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Dakika moja.

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.

NAIBU SPIKA: Endelea dakika moja.

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Naomba sana kwa sababu ya muda ningeomba sana wenzetu wa Wizara inayohusu mambo ya Mazingira, mazingira ni suala la kufa na kupona sio la kumsubiri mfadhili eti atuonee huruma au aji-commit leo, atoe mwaka 2025, huo ni wajibu wetu sisi kama Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuanza naomba nimshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, kubwa kwa kuendelea kuiunga mkono Wizara hii pamoja na vyombo vyetu vyote kwa sababu yeye ndiye kiongozi wa majeshi haya na ndio mkuu wa ulinzi wa Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, lakini pia naomba kumshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake yote kwa sababu mara zote wamekuwa wakishirikiana vizuri na Kamati yetu ili kuhakikisha kwamba Kamati zinafanya majukumu yake kwa mujibu wa Kanuni zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi naomba kuchangia mambo machache sana, nikiamini kwamba Serikali itaweza kutusikia, kutusikiliza na kutekeleza. Kwanza naomba niwashukuru kwa sababu Serikali imeamua kuongeza asilimia kama moja nukta kitu hivi kwa ajili ya shughuli za Wizara yetu hii. Lakini ninaomba kuomba zaidi, tena kwa heshima kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, huko nyuma niliwahi kusema kwamba Jeshi ni chombo cha utafiti, Jeshi ni chombo cha ulinzi. Chombo hiki kinatulinda angani, kinatulinda ardhini, kinatulinda baharini na mipakani. Sasa pamoja na kwamba Serikali yetu inafanya jitihada kubwa za kuwaongezea uwezo, bado naiomba Serikali iendelee kutafakari kwa kina sana, kwa sababu kazi kubwa ya Jeshi letu ni kulinda mipaka yetu, period. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninaomba sana, pamoja na kwamba Serikali imefanya kazi ya kuongeza lakini bado kwa sababu Jeshi hili halina pa kulia, Jeshi hili sehemu ambayo itaomba ipatiwe nyenzo za kufanyia kazi ikiwemo utafiti ni Bunge lako hili. Kwa hiyo ninaomba sana, kwa niaba ya Kamati yangu, lakini kwa niaba ya Bunge hili, tuombe sana Serikali itusikie na ituelewe kwamba tunahitaji Jeshi la kisasa, ambalo tutaliwezesha ili kazi yake iwe moja tu, ya kulinda mipaka yetu ili kuhakikisha kwamba Tanzania inaendelea kubaki kuwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, wakati tunasoma taarifa yetu pale, tulizungumzia hoja ya kuliwezesha Bunge. Moja miongoni mwa kuliwezesha Bunge Jeshi letu hili ni kuhakikisha kwamba linapata vitendea kazi lakini vilevile na sisi tunaendelea kusaidia kuhakikisha kwamba halitumii fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jeshi letu linapata gharama kubwa kwenye kulipa kodi. Sasa mimi naomba niliombe Bunge lako, na naomba niiombe Wizara, kwamba sasa wakati umefika wa kuhakikisha kwamba Jeshi letu linapatiwa msamaha wa asilimia 100 kwa vifaa vyake vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu kama sikosei tunatafsiri vifaa vya Jeshi kwamba ni silaha, kwa maana ya risasi na mizinga; hapana, tunakosea. Huko nyuma Jeshi letu lilikuwa na msamaha fully kwa vifaa vyake vyote inavyotumia. Inawezekana yalitokea mapungufu kwa watu wachache, lakini tumeliadhibu Jeshi kwa kutokuona kwamba hata uzi wa askari ni silaha. Sasa ombi langu, naiomba Serikali, hasa Wizara ya Fedha, ituletee mabadiliko ya sheria ili kuhakikisha kwamba Jeshi tunalipa msamaha kwa vifaa vyake vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu kuitoza kodi Wizara ya Ulinzi ni sawasawa na kutoa pesa mfuko wa kushoto ukaweka kulia ukitegemea tija; haipo. Lakini pili, Jeshi hili ndilo linalotulinda, mimi sioni sababu ya kuwa na wasiwasi na chombo chetu halafu ukawapa nafasi baadhi ya watu pale bandarini wanakwenda kuchungulia Jeshi wameleta nini. Siyo kazi yetu vifaa vyetu kuchunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kama vifaa vyetu vimeletwa kama Jeshi, ombi langu, kwa sababu ndio wanaotulinda, tumewaruhusu na tumewapa fedha ya kununua vifaa hivyo, hatuna sababu ya kuendelea kuwatoza kodi Jeshi. Ombi langu, watuletee sheria tuibadilishe, tena iletwe kwa hati ya dharura ili tuipitishe hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuendelea kwenye pointi yangu nyingine, kwamba pamoja na Serikali kuendelea kujitahidi bado naomba tuendelee kwa sababu sisi ndio tunaosimamia Wizara hii pamoja na nyingine mbili; bado tunahitajika kuhakikisha kwamba Jeshi letu hili, hasa kwenye suala la kuewezesha makazi yao na vifaa vyao, bado. Kwa sababu wenzetu hawa wanafanya kazi kubwa, ninaomba sana Serikali iendelee kuona namna gani tutaliongezea Bunge Jeshi letu hili ili makazi yao na vifaa vyao viendelee kuwa vya kisasa kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, sisi sote hapa ni wastaafu watarajiwa. Sote hapa kwa njia moja au nyingine ama tutastaafu kwa muda ukifika au tutastaafishwa na Mungu kwa sababu hatma ya kufa pia ipo. Sasa ninaomba basi, wale wenzetu wote ambao wamestaafu au wale ambao wametangulia mbele ya haki lakini wao wenyewe au wale warithi wao bado hawajapatiwa yale mafao yao, ninaomba sana, kwa sababu umepoteza mzazi au mlezi halafu yale mafao unapata usumbufu. Si kwa sababu Jeshi hawapati, hapana, ni kwa sababu bado Wizara ya Fedha haijatekeleza hoja ya kuwapa fedha ili waweze kuwalipa waliostaafu na waliofiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba wenzetu hawa, hasa Wizara ya Fedha, wajue kwamba Jeshi ni chombo cha kujitolea. Sisi kama Serikali, kama Taifa, hatuna cha kuwalipa Jeshi ambao wametoa roho zao na nafasi zao kwa ajili yetu. Ninaomba sana tuwathamini, tuwalinde, kuwalinda wao ni pamoja na kulinda haki zao na waliowaacha ili waweze kujenga Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya upendeleo. Mimi ningeomba kuchangia mambo machache ili kuwa miongoni mwa wachangiaji kwenye hotuba hii ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi yake kubwa ya kuendelea kulitumikia Taifa, na kwa kazi yake kubwa ya kuendelea kutafuta vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Watanzania. Ni kazi kubwa, ngumu, inahitaji ujasiri, uimara na umakini wa ku-focus wapi Tanzania iende. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza wasaidizi wake wawili ambao kwa kweli ili nchi yetu iendelee inahitaji vijana makini ambao kwa kweli watatusaidia na watalisaidia Taifa kwa kufanya kazi chini ya mama ili kuhakikisha kwamba nchi inaendelea. Nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wako wote. Hakika mnafanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niwatie moyo, kwa sababu, kama Taifa linahitaji kusonga mbele; na ili Taifa lisonge mbele lazima tuwe na vyanzo vya mapato kutoka maeneo mbalimbali ambavyo vitalisaidia Taifa, ili kuweza kutimiza mahitaji ya Watanzania. Moja kati ya hayo, mlituletea hapa Muswada na tukaupitisha kwa ajili ya kuiunga mkono Serikali ili iendelee kutafuta wawekezaji. Naomba sana kwenye hili msirudi nyuma kwa sababu tunafanya uwekezaji mkubwa ikiwemo kujenga SGR, na kufufua reli zetu zote pamoja na reli ya TAZARA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, SGR kama hesabu zangu zinaniambia sawasawa, wametuambia inahitaji mzigo wa tani milioni 25 kwa mwaka, leo tuna uwezo wa chini ya tani milioni 20. Kwa hiyo, tuna SGR, tuna Reli ya Kati, tuna TAZARA, tuna reli nyingine na Barabara. Zote hizi zinahitaji mizigo. Sasa kama tunahitaji kuendelea, lazima tuwaunge mkono wenzetu ili waweze kutafuta mizigo zaidi ili Serikali iweze kuwahudumia wananchi. Naomba hapa msivunjike moyo, kwa sababu ili tuweze kuwahudumia wananchi ni lazima tutekeleze au tutimize ahadi zetu kama Serikali ambayo inasimamiwa na Chama cha Mapinduzi, msirudi nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema kelele za mlango huwa hazimzuii mwenye nyumba kulala. Tuendelee kuchapa kazi kwa sababu ndio wajibu wetu. Tumeaminiwa na wananchi, tuhakikishe kwamba lazima tunawahudumia. Ndiyo Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, tuendelee ku-stick on the game. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba univumilie, mimi nina kawaida ya kusoma hiki kitabu, maana ndiyo nilichokikuta. Naomba ninukuu Katiba yako hii ya mwaka 1977 ya Jamhuri ya Muungano, kwenye Sura ya Kwanza ile inasema: “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano,” lakini kifungu cha pili inasema: “Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo la Tanzania Bara na eneo la Tanzania Zanzibar na ni pamoja na sehemu yake ya Bahari ambayo Tanzania inapakananayo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa naomba kutoa angalizo, hasa kwa wenzetu wote, wale ambao wanadhani kwamba chama chetu na Serikali yetu haishughuliki na matatizo ya Watanzania. Ni kweli Katiba hii imetoa nafasi ya kutoa maoni, nafasi ya vyama vingi, lakini haikutoa nafasi ya kuvunjiana heshima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kuwakumbusha wenzetu, sisi wa umri wetu, kwa mujibu wa data zilizopo, zaidi ya asilimia 70 ni vijana ambao wako chini ya miaka 50. Maana yake tunachokijua ni Katiba hii ni ya Tanzania, ndicho tunachokifahamu. Kwa hiyo, wenzetu msitengeneze maneno ya kuligawa Taifa hili. Taifa hili limepiganiwa na Taifa hili linaitwa Taifa la Tanzania. Hakuna Mtanzania nusu, wala hakuna Mtanzania kipande, msituvuruge. Nawaombeni sana, wala msimvunje moyo mama kwa sababu analihudumia Taifa. Analihudumia kama Mtanzania mwenye haki kamili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama kuna mmoja anadhani yeye ni Mtanzania zaidi kuliko mwingine, ajitathmini. Kwa sababu haiwezekani, Katiba hii imetupa haki sawa sote kama Watanzania. Kwa hiyo, asijitokeze mmoja kwa sababu ya ulevi, kwa sababu ya kulewa madaraka, akadhani yeye ana haki zaidi kuliko mtu mwingine yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo haki zote kama Watanzania. Kwa hiyo, nawaomba sana, tuheshimu matakwa ya Katiba hii, na pia tuheshimu haki ya kila Mtanzania. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba, jitihada zinazofanyika zinafanyika ili kutuondoa Tanzania tulipo ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana mama yetu ambaye ni Rais wetu, mama usivunjike moyo. Tulikuahidi hapa, tunakuunga mkono, tutaendelea kukuunga mkono kwa sababu dhamira yako tunaielewa sisi watoto wako kwamba ni kuiongoza Tanzania ili iweze kupiga hatua. Shika kamba, endelea, tunakuunga mkono. Sisi vijana wako, Wabunge wenzako, tuko pamoja na wewe kuendelea kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kuliko yote naomba sana hili tulizingatie kwa sababu sisi kama Watanzania hatuna Taifa lingine. Sisi kama Watanzania tunao wajibu wa kulilinda Taifa hili ili vizazi vyetu vije kurithi Tanzania iliyo bora kuliko iliyo leo. Kwa hiyo, tusiwavunje moyo. Wale wanasiasa wenzetu ambao wanajifunza kufanya siasa, kwa sababu, wako vijana wanajifunza kufanya siasa, siasa siyo kuwadanganya watu, siasa ni kutekeleza matumaini ya watu kwa kutumia vyanzo vilivyopo ili kuboresha maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tujiheshimu, tuheshimu Katiba, tuheshimu viongozi wetu, na pia tuwape nguvu ili waweze kufanya kazi ya kulihudumia Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naiunga mkono sana bajeti hii. Asanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Pamoja na uchache wa muda, naomba nizungumze mambo machache yafuatayo; kwanza naomba kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu, lakini naomba nimshukuru pia kwa kututeulia kiongozi mzuri wa Wizara hii ambaye sisi kama Kamati ya Ulinzi tunafanya naye kazi kwa karibu na kwa kweli, amekuwa mtendaji wa karibu sana kwetu sisi kama Wanakamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia naomba nilishukuru jeshi letu likiongozwa na afande CDF, lakini pia likisaidiwa na wenzetu wa Jeshi la Kujenga Taifa, niwashukuru sana. Naomba nitoe shukrani kwa sababu kwanza nchi yetu imetulia, nchi yetu inafanya kazi kwa amani, imejenga mahusiano mazuri pamoja na majirani zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu ya muda naomba kuzungumza mambo matatu yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza; wenzangu wamezungumza maneno mengi sana ambayo ni muhimu na kwa kweli inasaidia kulijenga jeshi letu hili, lakini na kuweka usalama wa nchi yetu pamoja na mipaka yake. Ningeomba la kwanza, tusaidie kwanza kuipitisha bajeti hii, lakini kama itawezekana tuone namna ambavyo tunaweza kuiongezea bajeti kwa sababu jeshi ni utafiti, jeshi ni vifaa na jeshi ni nyenzo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuwa na jeshi ambalo tunaliminya minya tunataka lifanye kazi yetu ya kutulinda halafu bajeti yake tumeifinya. Tunamshukuru mama yetu kwa kuongeza bajeti, lakini bado jeshi letu linahitajika liwe na bajeti ya kutosha ili liweze kufanya kazi zetu kwa sababu jeshi kazi yake ni moja tu, ni kulinda mipaka ya Taifa letu kuhakikisha kwamba, sisi tunaishi vizuri, lakini tunalinda Taifa letu bila migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili; wakati wa amani jeshi letu linatumika kuzalisha mali. Nawaombeni sana Waheshimiwa Wabunge, Jeshi hili limeonesha uimara na weledi mkubwa katika kutekeleza mambo yake. Amesema dada yangu pale, tumekwenda kutembelea Makao Makuu ya Ulinzi, chombo hiki kimetengeneza au kinajenga Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa letu ambayo kwa kweli haijapata kutokea, lakini inatengeneza kwa gharama ndogo kabisa. (Makofi)

Kwa hiyo, maana yake jeshi letu kwa kutumia wenzetu pia wa Jeshi la Kujenga Taifa wanatumia gharama ndogo. Nawaombeni sana tutawawezeshe na iwe ndio priority yetu sisi kama Bunge kuhakikisha kwamba tunatumia gharama ndogo lakini kwa utaalamu wetu wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mfano hapa, juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu alitangaza kuondoa wenzetu wanaoishi kwenye mbuga zetu kule. Mimi nilitegemea kwamba priority tungewapa wenzetu wa Jeshi la Kujenga Taifa kwa sababu gharama ni ndogo, lakini utaalamu ni mkubwa. Sina hakika, lakini nina wasiwasi tumewatumia wenzetu wale wa JKT kama ndio ni substitution, hatukuwapa priority. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana tuwaamini wenzetu wa Jeshi la Kujenga Taifa, lakini tuamine kwamba, uwezo wao ni mkubwa. Tusiwafanye kwamba hawa ni second class wajenzi, hapana, tuwatumie, tuwape kipaumbele. Ninaamini watafanya kazi kubwa, ninaamini watafanya kazi kwa kuzingatia uzalendo wa hali ya juu kwa hiyo, ningeomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho kuliko yote nilizungumza juzi hapa kwamba, namna tunavyowaajiri vijana wetu kwenye jeshi vigezo vinatumika vingi. (Makofi)

Naomba nirudie tena leo kwamba kigezo pamoja na elimu, kigezo cha kwamba, vijana wetu wanaopitia Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Kujenga Uchumi kwamba ndio kigezo kikubwa naomba sana hii iwe ni addition kwa sababu sisi kama jeshi hatuna uwezo wa kuwachukua vijana wote waliomaliza kidato cha pili, cha nne na cha sita kuingia ili wakapate mafunzo haya ya msingi. (Makofi)

Kwa hiyo, naomba sana tusiwanyime vijana wetu wengine ambao wanao uwezo wa kuingia katika vyombo vyetu hivi, simply kwa sababu, hawakupata nafasi ya kupita kwenye majeshi haya, naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa nafasi na naomba nianze kwanza kwa kuipongeza Serikali lakini hasa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake wa hotuba yake kwa umahiri mkubwa sana hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nimpongeze kwa kazi kubwa anayoifanya yeye pamoja na wasaidizi wake, hakika nchi imetulia, nchi imeongeza marafiki, lakini diplomasia yetu inaendelea kukua kwa kuongeza marafiki. Kwa sababu Wizara yako ndio Wizara ya marafiki, ni kazi ngumu sana kutunza marafiki, lakini kwa kweli umewatunza, endelea kuwatunza kwa niaba yetu sisi kama Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba kidogo nikupe pole na nikupe pole kwa sababu unafanya kazi kubwa ya kuleta taswira yetu nzuri nje au duniani huko, lakini bahati mbaya sana kazi yako ni ngumu kwa sababu sisi kama Wabunge hatujafanya kazi yetu ya kukusimamia kuhakikisha unapatiwa uwezo wa kufanya kazi zako kama Wizara. Hakika huu ni wajibu wetu na hakika ni sisi ndio wa kujilaumu kwa sababu tunapoanguka huko kwenye mataifa kwamba hatuiwezeshi Wizara ni kosa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana tulisema hapa kwamba sisi kama Bunge tunakutana, tunapitisha bajeti nani apewe nini, lakini tunaiacha kwenye eneo fulani ili mmoja aamue kwa discretion yake, hii haijakaa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima Bunge linapofanya maamuzi lichukue nafasi yake ya kuisimamia na kuishauri Serikali tunapopitisha bajeti, maana yake hatuchezi mchezo wa kitoto hapa, tunafanya kazi serious kwa ajii ya Taifa. (Makofi)

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba nikupe pole kwa sababu ni kazi ngumu lakini fanya kwa sababu wanasema kazi ngumu mpe Mnyamwezi, I am not sure kama wewe ni Mnyamwezi au laa, lakini nikupe hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa maana hiyo hiyo naomba sana liko jambo la utekelezaji wa miradi ya maendeleo nimekusikia Waziri, lakini tumesoma hapa hotuba ya Kamati, kwa miaka miwili mfululizo Wizara hii haijapewa hata senti tano ya maendeleo. Sasa hili pia ni tatizo letu sisi kama Bunge kwa sababu wanasema duniani nothing is constant, maana yake ni kwamba changes ni kila kitu kinabadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ningeomba basi na niishauri sana Serikali kwamba tunapopanga kama Bunge na wenyewe waione kwamba Wizara hii ni muhimu ndani na nje kwa sababu ndio inayotuletea marafiki, ndio inatuongezea uchumi, inaongeza imani kwa wawekezaji tuwape nafasi na nyenzo za kuweza kutekeleza mipango yao ya maendeleo. Kama hatutaki waendelee tuwaambie kaeni msituletee mipango ya maendeleo, lakini haiwezekani tunakaa, tunapanga, tunapitisha, tunaamua halafu nothing is going on. Haiwezekani hii, ningeomba sana wenzetu hasa wenzetu wa Wizara ya Fedha mtusikilize Wizara ya Mambo ya Nje ndio kioo chetu duniani. Hakikisheni mnaiwezesha, msiiache kwa sababu ni wataalam hawapendi kupiga kelele mkaona hapana tutaiacha tu kama ilivyo, hakikisheni mnaiwezesha Wizara ili iweze kufanya mambo yake ya mipango ya maendeleo, ni lazima sio choice. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nichukue nafasi hii kuwaomba wenzetu wa Wizara kwamba tuendeleze diplomasia ya uchumi kwa sababu tunayo maeneo yetu mengi duniani. Mimi nilijaaliwa kuishi India kuanzia mwaka 1992 mpaka mwaka 2000 pale Delhi tulikuwa na kiwanja chetu tumepewa miaka ya 1960, lakini mpaka tunaondoka mwaka 2000 kiwanja kile hakijaguswa na bahati mbaya sana kilichukuliwa wakapewa Ubalozi mwingine, sisi tukaishia patupu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumetafutiwa eneo lingine dogo, tumejenga, simply kwa sababu hatukuona umuhimu wa kujiendeleza au hatukupata nafasi, Wizara haikutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza viwanja hivi. Ningeomba sana kwa viwanja vya aina hii au kwa nafasi za aina hizi tusidharau kwa sababu juzi tumekwenda Addis Ababa pale viwanja vyetu viwili tumenyang’anywa, sio kwa sababu Wizara haitaki, hapana, lakini kwa sababu utaratibu uliotumika lakini na sisi tumepewa hatukuweza kuviendeleza, hatukuona umuhimu huo. Leo tumerudishiwa lakini ninaamini tukizembea watachukua wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ningeomba sana hii ni nafasi yetu ya kukuza mahusiano, lakini na kukuza uchumi kama Taifa. Ningeomba sana tukubaliane, tuwawezeshe wenzetu, lakini maana yake wenzangu wamesema hapa kwamba tuhakikishe basi tunawashirikisha na wenzetu wa ndani, yako mashirika kwa mfano mwenzetu amezungumza National Housing Corporation wanaweza wakafanya, lakini ziko benki zinaweza zikafanya, lengo letu asset hizi zinajengwa na sisi zinatusaidia sisi, lakini zinajenga Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ningeomba niipongeze Serikali pamoja na jitihada kubwa, lakini bado iendelee kufanya jitihada kwa sababu hatuwezi tukaishi, hatuwezi tukakuza Wizara ya Mambo ya Nje bila ya kuwaendeleza vijana wetu. Lazima tuwaendeleze kwenye mafunzo kwa maana tuanze kwenye recruitment, tuwafunze, lakini tuwa-place ili kuwe na kitu kinaitwa continuity, bila hivyo Wizara hii itaumia, inazungumza inajipanga, inatumia nguvu nyingi, lakini haipati nyenzo za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja kwa Kamati zote mbili. Pili; naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini kuzipongeza Wizara na taasisi zote ambazo kwa kweli zinajitahidi kufanya kazi pamoja na mazingira kuwa magumu sana; lakini niwapongeze kwa sababu kutenda ni wajibu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wenzangu wamezungumza mambo mengi sana. Sasa mimi naomba niya-summarize kidogo kwa kuleta maombi au ushauri kwa Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningeomba Serikali, pamoja na jitihada zake za kupeleka fedha kwenye maeneo mbalimbali tukifanya ulinganisho kati ya miaka mitano, sita iliyopita na sasa tumepiga hatua kubwa sana kwenye kupeleka fedha za mendeleo. Kwa sababu mchakato wa maendeleo ni endelevu, maana yake ni kwamba kila siku lazima tutoke hatua moja kwenda hatua nyingine ya kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti; maana yangu ni nini? Maana yangu ni kwamba ni lazima tuhakikishe kwamba mipango yetu tunayoipanga kwa kupitia bajeti yetu lazima tuiheshimu kwa sababu ndicho tulichokipangia tukiwa tunaamini kwamba makusanyo yetu yanalingana na mipango yetu. Ndiyo maana Serikali inatoa ceilings ili kuona kwamba hatuzidi kwa kulinganisha na makusanyo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Mbunge amesema hapa, na wenzangu wamesema kwamba kwa mfano wenzetu wa Zimamoto kwa kipindi chote hichi karibuni tunamalizia nusu ya mwaka hawajapewa hata senti tano ya maendeleo. Hiki ni chombo kikubwa sana, chombo kina kazi kubwa sana lakini bahati mbaya sana ni chombo kipya ambacho ni mwaka uliopita tulikitengeneza kuwa jeshi. Maana yake ili chombo kiwe jeshi lazima kiwezeshwe kifedha na mafunzo na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba sana kwa Serikali kwamba tuhakikishe kwamba tunawawezesha wenzetu hawa ili waweze kutulinda; kama ambavyo tunawawezesha Polisi angalau wameweza kufikia asilimia fulani. Ninawaomba sana, ninaiomba Serikali ihakikishe kwamba tunaliwezesha Jeshi hili la Zimamoto kwa sababu kwa kweli bado linahitajika kuundwa. Chombo hichi ni kipya kinahitajika kiundwe ili kiweze kufanya kazi kama ambavyo tunategemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningeomba hapo hapo ambalo linafanana na hilo. Miaka miwli iliyopita tumekuwa tukizungumza sana hapa juu ya Serikali, hasa Wizara ya Fedha kufanya mgawanyo wa mafungu ya fedha kama Bunge lilivyopitisha. Sasa inasikitisha sana kila mwaka tunakuja hapa tunalalamika kwamba, kwa kweli hatujafika mahali tukaweza angalau kupeleka mafungu haya kwa mlingano. Tunaamua nani tumpelekee, nani tusimpelekee. Hivi vigezo nadhani Bunge lilishapitia, tumekubali huyu apewe fedha kwa kazi hii. Sasa mimi ningeomba sana, na niliomba huko nyuma tujitathmini tuone; je, tunachokipanga kama Bunge ndicho kinachotekelezwa kwenye mganwanyo? Jawabu lake inaonekana yako maeneo wanapata hela nyingi, yako maeneo bado hayapati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tumeunda vyombo vingi hapa. Tunayo Wizara ya Mambo ya Nje, tunayo Wizara ya Ulinzi, tunayo Wizara ya Mambo ya Ndani; Hivi vyombo vinatulinda masaa 24; vinalinda mali zetu, vinalinda mipaka yetu. Sasa bahati nzuri au bahati mbaya sana ninadhani bado hatujavipa umuhimu ili kuhakikisha kwamba vyombo hivi ndivyo vinavyomulika mipaka yetu kwa nje, kwa angani na ardhini. Ninaomba sana Wizara ya Fedha wakati inafanya mgawanyo wa fedha hizi isivione vyombo hivi kwamba havina kazi, vina kazi kubwa sana, na ndivyo vinavyolinda uhuru wa kwetu sisi kama Watanzania, naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba kusema hivi, kwamba miaka miwili pia iliyopita tulizungumza juu ya maendeleo ya viwanja vyetu ambavyo tumepewa kama Taifa kwenye nchi mbalimbali. Taarifa yetu imezungumza hapa kwamba bado viwanja vile vingi hatujaviendeleza na viwanja vile vingi maana yake uwezo kwa kunyang’anywa ni mkubwa. Sasa siyo kwamba Wizara hizi hazitaki kutekeleza lakini hatujazipa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tuliwahi kutoa mfano; India pale kuna eneo moja kubwa sana tumepewa, lakini kwa sababu ya tamaduni zetu kuamini kwamba wenzetu wameganda kama tulivyoganda ilituchukua mida ya miaka mingi sana mpaka tukajenga. Tulinyang’anywa kiwanja kile tukapewa kingine kidogo ambacho angalau kimejengwa sasa hivi ndiyo tunafanyia shughuli zetu za kibalozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana; tukivipoteza hivi kwa mazingira yetu hatuwezi kupewa tena maeneo yale yale. Wamezungumza wenzangu hapa Adis tumepewa viwanja viwili vizuri sana, pale DRC tumepewa viwanja vizuri sana, Msumbiji tuna viwanja viwili wengine tumekwenda kuangalia lakini jengo moja lile kama vile tuligaiwa lakini eneo moja liko empty na ni miaka na miaka hatujafanya lolote. Si kwamba Wizara hawataki lakini kwa sababu hatujawawezesha. Mimi naliomba Bunge; sasa Bunge lichukue dhamana yake, lichukue nafasi yake ili kulinda heshima ya Taifa letu mbele ya mataifa mengine, naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ningeomba sana kwamba Jeshi au vyombo vyetu hivi tumevitaka sana kushiriki kwenye mfumo wa kushiriki kwenye mambo ya uchumi. Ningeomba tukajifunze; wenzetu wa Jeshi la Egypt wanashiriki na wanasaidia Pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 50, ni chombo cha jeshi hicho. Si kwa sababu wanaakili zaidi ya sisi lakini ni kwa sababu Serikali inawawezesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningeomba sana tuwezeshe vyombo vyetu hivi vikiwemo vyombo vya ulinzi kwanza kwenye kufanya utafiti lakini pili kuviwezesha ili viweze kushiriki kwenye uchumi wa Taifa. Kwa sababu bila ya kuviwezesha tutaendelea kuvilaumu lakini sisi hatuviwezeshi kuhakikisha kwamba vinafanya wajibu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningeomba sana sana kwamba tuhakikishe kwamba sisi kama Serikali yale tunayoyapanga kama Bunge kuielekeza Serikali itekeleze naombeni sana tusimamie mipango yetu kuielekeza Serikali ili Serikali itekeleze matakwa ya Bunge kwa sababu ndiyo matakwa ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba tena kuunga mkono hoja; nashukuru sana. (Makofi)
The Fire and Rescue Force (Amendment) Bill, 2021
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kwanza kuishukuru Serikali na pia kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa aliyoifanya na kubwa kuliko yote kuweza kufanya kazi kwa karibu sana na Kamati yetu, jambo ambalo limetufanya kuwa kitu kimoja kwa lengo na maslahi ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye Muswada na nitazungumzia mambo matatu. La kwanza, tumekubaliana kwamba kwa mujibu wa Muswada huu, Jeshi la Zimamoto sasa linakuwa jeshi kamili, kwa maana ya kwamba litaingia katika mlolongo wa kijeshi; litafuata kanuni na taratibu zote za kijeshi, wala siyo jeshi kwa maana ya jina. Kwa hiyo, wenzetu wataalamu wafanye kazi zao, wali-train jeshi hili liwe kama jeshi kamili na siyo kwa maana ya kuzima moto tu, lakini kwa maana ya kuwa Jeshi la Akiba wakati wote likihitajika litaendelea kuwa jeshi. Nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo hiyo, kwa sababu, tumeliita “jeshi,” maana yake ni kwamba, litatakiwa kufuata taratibu zote zikiwemo za mafunzo pamoja na kumiliki silaha. Kumiliki silaha ni kwa sababu, hatuwezi tukawa na jeshi ambalo linamiliki maji, lakini halimiliki silaha. Wenzetu hawa wanafanya kazi kubwa katika maeneo mbalimbali na mara nyingi changamoto zinatokea kwa sababu kwenye moto wako wanaoathirika, lakini wako wanaopenda athari itokee ili wao waweze kufanya uhalifu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Bunge lako kwenye hili lione kwamba tumekubaliana kama Kamati na Serikali kwamba tuliwezeshe jeshi hili ili pamoja na kufanya kazi yao ya msingi ya kuhakikisha wanazuia moto, wanahakikisha wanatoa taaluma ya moto na pia waweze kufanya kazi ya kulinda mali wakati ambapo pia wanazima moto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo kulinda mali tu, kuhakikisha kwamba wanazuia uhalifu, lakini nao wenyewe wanajilinda, kwa sababu mara nyingi askari wetu hawa wanashambuliwa na wanaposhambuliwa wanakuwa hawana uwezo wa kujikinga wao wenyewe kama askari. Kwa hiyo, nashauri Bunge lako lisaidie hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo hiyo, naomba sana; na hili naomba wenzetu wa Jeshi la Polisi, tumekubaliana sasa vyombo vyote hivi vinafanya kazi kwa pamoja kwa maana ya Polisi, kwa maana ya Uhamiaji, kwa maana ya wenzetu hawa wa Jeshi la Zimamoto, wote wanakuwa kwenye umbrella moja. Ombi langu, waendelee kufanya kazi kwa pamoja kwa sababu moja ya msingi, mara nyingi linapotokea tukio la moto wanaowahi kwenye tukio hili ni wenzetu wa Jeshi la Zimamoto, lakini mara nyingi inatokea kwamba, wenzetu wa Jeshi la Polisi wanachelewa ama kupata taarifa ama kufika kwenye eneo la tukio. Kwa hiyo, madhara yake yanakuwa makubwa kwa sababu watu wanavamia; wako watu wabaya na wako watu wema. Kwa hiyo, tatizo letu ni watu wabaya.

Mheshimiwa Spika, ombi langu sasa, mtandao wa mawasiliano kati ya Jeshi la Zimamoto na Jeshi la Polisi kwa sababu, wako chini ya umbrella moja, wawe kitu kimoja ili wapeane taarifa kwa pamoja. Anapotokea fire kama ni advance na mwenzetu wa polisi awe pale ili kusaidia kazi hii ya kulinda watu na mali zao. Tusiwaachie wenzetu wa Jeshi la Zimamoto tu kazi ile kwa sababu kazi yao kubwa na ya msingi ni kuhakikisha kwamba, wanazuia moto usitokee au wanazima moto pale maeneo ambayo janga limetokea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ombi langu na ushauri wangu kwa wenzetu wa Jeshi la Polisi, wawe faster au wawe na haraka kwenye kutafuta taarifa au kuzipokea, kuzichakata na kuhakikisha kwamba wanafika kwenye eneo la tukio kama ambavyo wenzetu wa Jeshi la Kuzima Moto wamefika. Naomba sana hilo.

Mheshimiwa Spika, mwisho kuliko yote, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, kama alivyosema Mwenyekiti wetu, kwamba tuliwezeshe jeshi letu hili liweze kufanya kazi zake kama inavyotakiwa ili tuweze kufanya kazi kubwa ya Serikali, kulinda raia wake, kulinda na mali zao na kuhakikisha kwamba wanaendelea kuishi kwa usalama na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania wa Mwaka 2022
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa nafasi. Naomba kuelekea kwenye Muswada wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi, lakini nataka kujikita kwenye maeneo matatu.

Mheshimiwa Spika, kwanza malengo ya kudhibiti, kwa sababu inawezekana hapa wengi tusielewe, lakini kwa nini umeletwa Muswada huu; ndiyo ambapo nataka kwenda.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye ukurasa wa nane, naomba ninukuu kwanza ila kwa interest ya muda nitasoma tu haraka haraka halafu nitajaribu kueleza. Yako malengo (a) mpaka (e), kwa maana haya ni malengo Matano: -

(a) Kudhibiti uchakataji;
(b) Kuhakikisha kwamba uchakataji wa tarifa binafsi za muhusika unaongozwa na misingi;
(c) Kulinda faragha;
(d) Kuweka utaratibu wa kisheria; na
(e) Kuwapa wahusika wa taarifa haki na nafuu ya kulinda taarifa.

Mheshimiwa Spika, kwenye hili, nini maana yake? Maana yake hapa duniani tulipo, whether tunapenda au hatupendi, lazima tulinde faragha za taarifa za watu binafsi. Kwa sababu dunia hii ni ya mitandao na taarifa unaweza ukazitafuta kwa njia ya mitandao. Kwa hiyo, lengo au madhumuni ya hii ni kulinda. Tumejiwekea hapa malengo lakini kubwa zaidi ni kulinda faragha ya mtu mmoja mmoja lakini ikiwa inalindwa kwa mujibu wa sheria. Sasa utakapokiuka sheria hii maana yake nini? Maana yake kutakuwa na sheria ya kuweza kumdhibiti kila mtu ambaye anachakata au anakusanya taarifa nje ya utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo hiyo, kwa sababu kuna malengo, tumejiwekea na misingi. Wenzetu hapa wameweka misingi nane. Kwa interest ya time, naomba ninukuu tu haraka haraka. Kwanza, zitakuwa zinachakatwa kihalali kwa maana ya mujibu wa sheria. Hapa tunajifanyia tu lakini sasa tunaweka sheria ili kuhakikisha kwamba taarifa zinachakatwa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, zinakusanywa kwa madhumuni maalum. Ili taarifa zifanyiwe kazi, ili zichakatwe, zitafutwe maana yake zinatafutwa kwa sababu maalum, siyo kwamba unamtafuta mtu tu kwa sababu unamtafuta. Zinatafutwa ili zifanyiwe kazi maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, zinatosheleza na ni muhimu kwa madhumuni ya uchakataji. Tunatafuta taarifa kamilifu, siyo kipande kipande. Lengo letu ni kwamba tunapohitaji taarifa, lazima ziwe na mwanzo na ziwe na mwisho na ziwe za kujitosheleza na sahihi. Tunatafuta taarifa sahihi, siyo za ku-cook. Hata hivyo zitahifadhiwa kwa namna inayoruhusu utambuzi wa mhusika, na zitachakatwa kwa kuzingatia haki. Hatuwezi kutafuta taarifa hizi halafu zikawa zinachezewa bila kujali kwamba kuna mwingine zinavyochakatwa taarifa zake ni kwa kumwonea.

Mheshimiwa Spika, mwisho zinachakatwa kwa namna ambayo itahakikisha usalama wa taarifa binafsi ikijumuisha ulinzi dhidi ya uchakataji usioruhusiwa au ulio kinyume cha sheria. Maana yake ni nini? Ni kwamba kila kitakachofanyika katika kutafuta taarifa hii, kitafanywa ndani ya misingi ya sheria wala haifanywi kwa ajili ya kumkomoa mtu, tunahitaji taarifa kwa kazi maalum, kwa shughuli maalum, lakini kitu kizuri zaidi, mtu mwenyewe atakuwa anapewa taarifa kwamba tunazitafuta hizi kwa ajili hii, lakini hata yeye mwenyewe atapewa fursa ya kuweza kuhakikisha kwamba anashiriki na kama anazo zitatumika na ataombwa zitumike akijua kwamba zinatumika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba twende kwenye ukurasa wa 13 pale, kuna chanzo cha utoaji wa taarifa. Naomba pia kwa interest ya muda, ninukuu hapa kwenye ukurasa wa 13 ambayo inazungumzia chanzo. Wanasema chanzo, imeandikwa hapa, kwa mujbu wa kifungu cha 23(1). Kwa kuzingatia kifungu hicho, kinasema hivi: “Kabla ya kukusanya taarifa binafsi, mkusanyaji atahakikisha kuwa muhusika; moja, anatambua madhumuni ya ukusanyaji; pili, anafahamu kuwa ukusanyaji wa taarifa binafsi na madhumuni yake; na tatu anawafahamu wapokeaji wa taarifa binafsi.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inawezekana tulio wengi hatuelewi na tulio wengi inawezekana tunaamini kwamba tunatafutana. Naomba sana Waheshimiwa Wabunge, nasi tuwe sehemu ya kuwapa taaluma wengine kwamba dunia ya leo hatuna pa kujificha. Dunia ya leo taarifa ziko kiganjani, lakini dunia ya leo ukitaka la kwako la dhahiri linajulikana, la siri litajulikana tu. Sasa ni bora tufanye utaratibu wa kisheria ili mwananchi yeyote ambaye taarifa zake zitatumika bila ya consent yake, maana yake huyu anayo nafasi ya kwenda Mahakamani. Leo tunafanya kwa sababu tu, lakini sheria hii itatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi, sisi kama Tanzania hatuishi kwenye kisiwa. Tunahitaji kupata taarifa kutoka kwa wenzetu pia kwenye Mataifa mengine kwa sababu sasa hivi taarifa zinasafiri mara moja. Ndani ya dakika moja au second moja unaweza kupata taarifa kutoka China au popote. Kwa hiyo, litakapokuwa limewekwa hili, nasi kama Bunge tukawa tumeridhia kupitisha sheria hii, maana yake tutalisaidia Taifa letu na tutajisaidia na sisi wenyewe kuhakikisha kwamba taarifa zetu hazichezewi.

Mheshimiwa Spika, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, walielewe hili, lakini nao wawe sehemu ya kuisaidia Serikali kwa sababu kinyume chake sisi tutapambana na vikwazo vingi vya uchumi ambavyo wenzetu kama hatukupitisha hii wataona kama sisi hatufanyi kazi na wao. Kwa sababu ni ulimwengu wa kubadilishana taarifa, lakini taarifa za ukweli, taarifa ambazo siyo za kutengeneza ili kuhakikisha kwamba taarifa iliyoko Tanzania ndiyo hiyo hiyo iliyoko kwenye eneo lingine ili tusiweze kufanya makosa kwenye utambuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, waikubali sheria hii, waipitishe ili tuweze kufanya kazi na dunia, ili tuweze kukusanya taarifa, tuzichakate, tuzi-share lakini ndani ya sheria na wenzetu waweze ku-share na sisi ili nasi tukitaka za kwao iwe ni rahisi sana kuweza kuzipata ili tusaidie maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi!)
Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa Mwaka 2022
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa nafasi. Naomba kuelekea kwenye Muswada wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi, lakini nataka kujikita kwenye maeneo matatu.

Mheshimiwa Spika, kwanza malengo ya kudhibiti, kwa sababu inawezekana hapa wengi tusielewe, lakini kwa nini umeletwa Muswada huu; ndiyo ambapo nataka kwenda.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye ukurasa wa nane, naomba ninukuu kwanza ila kwa interest ya muda nitasoma tu haraka haraka halafu nitajaribu kueleza. Yako malengo (a) mpaka (e), kwa maana haya ni malengo Matano: -

(a) Kudhibiti uchakataji;
(b) Kuhakikisha kwamba uchakataji wa tarifa binafsi za muhusika unaongozwa na misingi;
(c) Kulinda faragha;
(d) Kuweka utaratibu wa kisheria; na
(e) Kuwapa wahusika wa taarifa haki na nafuu ya kulinda taarifa.

Mheshimiwa Spika, kwenye hili, nini maana yake? Maana yake hapa duniani tulipo, whether tunapenda au hatupendi, lazima tulinde faragha za taarifa za watu binafsi. Kwa sababu dunia hii ni ya mitandao na taarifa unaweza ukazitafuta kwa njia ya mitandao. Kwa hiyo, lengo au madhumuni ya hii ni kulinda. Tumejiwekea hapa malengo lakini kubwa zaidi ni kulinda faragha ya mtu mmoja mmoja lakini ikiwa inalindwa kwa mujibu wa sheria. Sasa utakapokiuka sheria hii maana yake nini? Maana yake kutakuwa na sheria ya kuweza kumdhibiti kila mtu ambaye anachakata au anakusanya taarifa nje ya utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo hiyo, kwa sababu kuna malengo, tumejiwekea na misingi. Wenzetu hapa wameweka misingi nane. Kwa interest ya time, naomba ninukuu tu haraka haraka. Kwanza, zitakuwa zinachakatwa kihalali kwa maana ya mujibu wa sheria. Hapa tunajifanyia tu lakini sasa tunaweka sheria ili kuhakikisha kwamba taarifa zinachakatwa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, zinakusanywa kwa madhumuni maalum. Ili taarifa zifanyiwe kazi, ili zichakatwe, zitafutwe maana yake zinatafutwa kwa sababu maalum, siyo kwamba unamtafuta mtu tu kwa sababu unamtafuta. Zinatafutwa ili zifanyiwe kazi maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, zinatosheleza na ni muhimu kwa madhumuni ya uchakataji. Tunatafuta taarifa kamilifu, siyo kipande kipande. Lengo letu ni kwamba tunapohitaji taarifa, lazima ziwe na mwanzo na ziwe na mwisho na ziwe za kujitosheleza na sahihi. Tunatafuta taarifa sahihi, siyo za ku-cook. Hata hivyo zitahifadhiwa kwa namna inayoruhusu utambuzi wa mhusika, na zitachakatwa kwa kuzingatia haki. Hatuwezi kutafuta taarifa hizi halafu zikawa zinachezewa bila kujali kwamba kuna mwingine zinavyochakatwa taarifa zake ni kwa kumwonea.

Mheshimiwa Spika, mwisho zinachakatwa kwa namna ambayo itahakikisha usalama wa taarifa binafsi ikijumuisha ulinzi dhidi ya uchakataji usioruhusiwa au ulio kinyume cha sheria. Maana yake ni nini? Ni kwamba kila kitakachofanyika katika kutafuta taarifa hii, kitafanywa ndani ya misingi ya sheria wala haifanywi kwa ajili ya kumkomoa mtu, tunahitaji taarifa kwa kazi maalum, kwa shughuli maalum, lakini kitu kizuri zaidi, mtu mwenyewe atakuwa anapewa taarifa kwamba tunazitafuta hizi kwa ajili hii, lakini hata yeye mwenyewe atapewa fursa ya kuweza kuhakikisha kwamba anashiriki na kama anazo zitatumika na ataombwa zitumike akijua kwamba zinatumika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba twende kwenye ukurasa wa 13 pale, kuna chanzo cha utoaji wa taarifa. Naomba pia kwa interest ya muda, ninukuu hapa kwenye ukurasa wa 13 ambayo inazungumzia chanzo. Wanasema chanzo, imeandikwa hapa, kwa mujbu wa kifungu cha 23(1). Kwa kuzingatia kifungu hicho, kinasema hivi: “Kabla ya kukusanya taarifa binafsi, mkusanyaji atahakikisha kuwa muhusika; moja, anatambua madhumuni ya ukusanyaji; pili, anafahamu kuwa ukusanyaji wa taarifa binafsi na madhumuni yake; na tatu anawafahamu wapokeaji wa taarifa binafsi.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inawezekana tulio wengi hatuelewi na tulio wengi inawezekana tunaamini kwamba tunatafutana. Naomba sana Waheshimiwa Wabunge, nasi tuwe sehemu ya kuwapa taaluma wengine kwamba dunia ya leo hatuna pa kujificha. Dunia ya leo taarifa ziko kiganjani, lakini dunia ya leo ukitaka la kwako la dhahiri linajulikana, la siri litajulikana tu. Sasa ni bora tufanye utaratibu wa kisheria ili mwananchi yeyote ambaye taarifa zake zitatumika bila ya consent yake, maana yake huyu anayo nafasi ya kwenda Mahakamani. Leo tunafanya kwa sababu tu, lakini sheria hii itatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi, sisi kama Tanzania hatuishi kwenye kisiwa. Tunahitaji kupata taarifa kutoka kwa wenzetu pia kwenye Mataifa mengine kwa sababu sasa hivi taarifa zinasafiri mara moja. Ndani ya dakika moja au second moja unaweza kupata taarifa kutoka China au popote. Kwa hiyo, litakapokuwa limewekwa hili, nasi kama Bunge tukawa tumeridhia kupitisha sheria hii, maana yake tutalisaidia Taifa letu na tutajisaidia na sisi wenyewe kuhakikisha kwamba taarifa zetu hazichezewi.

Mheshimiwa Spika, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, walielewe hili, lakini nao wawe sehemu ya kuisaidia Serikali kwa sababu kinyume chake sisi tutapambana na vikwazo vingi vya uchumi ambavyo wenzetu kama hatukupitisha hii wataona kama sisi hatufanyi kazi na wao. Kwa sababu ni ulimwengu wa kubadilishana taarifa, lakini taarifa za ukweli, taarifa ambazo siyo za kutengeneza ili kuhakikisha kwamba taarifa iliyoko Tanzania ndiyo hiyo hiyo iliyoko kwenye eneo lingine ili tusiweze kufanya makosa kwenye utambuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, waikubali sheria hii, waipitishe ili tuweze kufanya kazi na dunia, ili tuweze kukusanya taarifa, tuzichakate, tuzi-share lakini ndani ya sheria na wenzetu waweze ku-share na sisi ili nasi tukitaka za kwao iwe ni rahisi sana kuweza kuzipata ili tusaidie maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi!)