Supplementary Questions from Hon. Ng'wasi Damas Kamani (22 total)
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, kwa kuwa ujenzi huu maazimio ya kikao hiki yaliuweka kusimamiwa na Serikali ya Tanzania na kwa kuwa ujenzi wa sanamu hii ya Baba yetu wa Taifa yatasaidia kutangaza utamaduni wa Tanzania na mchango mkubwa wa Baba yetu Taifa katika kupigania uhuru wa nchi mbalimbali za Afrika. Ningependa Serikali ituambie ni kwa nini tangu mwaka 2015 yalipopitishwa maazimio haya mpaka sasa ujenzi huu haujaanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, kwa kuwa maamuzi haya au maazimio haya ya kikao yalitoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa wa Tanzania kuwa wa kwanza kabisa kupewa tender hizi na kwa kuwa mwaka 2018 tender hizi zilipotangazwa ilionekana hakuna wasanii/ vijana Watanzania wenye vigezo vya kutosha kimataifa kujenga sanamu hii. Basi Serikali ningependa ituambie ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inakuza ujuzi na uwezo wa wasanii wa Tanzania ili pale tender kama hizi zinapojitokeza kimataifa.
MWENYEKITI: Swali.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo swali hili.
Ningependa Serikali itueleze ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wasanii wa Tanzania pale ambapo tender hizi za kimataifa zinatangazwa tena wanajengewa uwezo ili nao wapate kushiriki kama Nchi zingine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kamani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kamani kwanza amependa kufahamu kwa nini delays. Nipende kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba mchakato huu wa kujenga sanamu ya Baba wa Taifa Ethopia Addis, ilikuwa ni wazo zuri sana kwa wakuu wa nchi za SADC kuipa heshima Taifa letu lakini kumpa heshima Baba wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, delays hizi zinatokana na mchakato; kwanza Kamati lazima ziundwe za kitaifa lakini pia kupitia Kamati hizo lazima zikae na familia ya Baba wa Taifa ili kupata prototypes zile ambazo zinahitajika tatu kabla ya ujenzi wa sanamu hii. Lakini pia conditions ambazo SADC imetupa ni kwamba lazima picha ya Baba wa Taifa iwe ni enzi hizo miaka hiyo wakati anapigania uhuru wa Taifa hili.
Kwa hiyo michakato hii, pamoja na conditions mpaka sasa inaendelea vizuri lengo ikiwa ni kuhakikisha sanamu tutakayoijenga pale Ethiopia iwe ni samanu ambayo inaakisi picha halisi ya Baba wa Taifa. Kwa hiyo, michakato hii inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lako la pili la Mheshimiwa Ng’wasi, ni kwa kiasi gani wasanii wetu tunawashirikisha na tunawajengea uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeza Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge kwamba mlitupitishia bajeti katika Bunge hili ya zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya sanaa na utamaduni. Kupitia mfuko huu Mheshimiwa Mbunge tukuhakikishie tutaendelea kuwajengea uwezo wasanii wetu, lakini kwa kuwa Tanzania tumepewa nafasi ya kusimamia ujenzi huu wa sanamu ya Baba Taifa, meneja wetu huyu aliyeteuliwa pia amepewa nafasi mbili ya kwenda na wasanii wetu Ethiopia waweze kuona kwamba wasanii wetu waweze kujua teknolojia hii. Kwa hiyo, hii ni Wizara yetu tunalifanyia kazi kwa karibu kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, la kwanza; kwa kuwa, maelekezo haya yalikuwa ni maelekezo ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge hili la 12 ilifanyika tarehe 13 Novemba, 2020 ni mwaka mzima sasa umepita na zaidi. Na kwa kuwa, katika majibu yake Mheshimiwa Waziri amesema wako katika hatua ya mwisho, swali langu; ningependa sasa Serikali itoe commitment ni lini hasa taarifa hii itakuwa tayari na kuletwa hapa Bungeni kwa ajili ya kuanza utekelezaji?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; pamoja na haja ya kuunganisha mifuko hii, lakini changamoto kubwa zaidi ya mifuko hii ni ukosefu wa fedha za kutosha kwa mifuko hii kujiendesha. Sasa ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba, mifuko hii inapokuja kuundwa sasa inakabiliana na changamoto hii na inakuwa na fedha za kutosha kwa ajilinya kukidhi uwezeshaji wa wananchi kiuchumi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Ng’wasi kwa kuwa, ameendelea kuwasemea sana vijana katika maeneo mengi, ili kuwatetea na kuwawezesaha katika maendeleo ya nchi hii. Ni kweli kama anavyosema ni karibu zaidi ya mwaka sasa tangu maelekezo au jukumu hili tupewe kwa ajili ya kuunganisha mifuko hii.
Mheshimiwa Spika, lakini mtakumbuka kwamba, mifuko hii imegawanyika katika maeneo tofauti, ipo mifuko ile ambayo inatoa mikopo moja kwa moja, lakini ipo mifuko ambayo ni ya dhamana, mingine ni ya kutoa ruzuku na mingine ni ya uwezeshaji, lakini zaidi yah apo mifuko mingine ni ya sekta binafsi. Kwa hiyo, Serikali inafanya tathmini ya kutosha kujiridhisha ili tunapokuja kuona mifuko ipi iunganishwe iwe na tija kweli.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Serikali inaliangalia kwa umuhimu sana na tukikamilisha taarifa hiyo, kama nilivyosema tutaileta hapa Bungeni ili tuweze kuendelea kuboresha mifuko hii.
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili la ukosefu wa fedha za kutosha; ni kweli baadhi ya mifuko imekuwa na changamoto ya kuwa na bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuhudumia wahitaji au kuwawezesha wanaokopa.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema na sisi tulikubaliana ndiyo maana tumesema tunataka kuunganisha mifuko hii ili iweze kuwa kwanza na fedha za kutosha ile ambayo inatoa huduma zinazofanana. Lakini pili mkakati wa Serikali ni kuona kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kwa mfano ile kwenye halmashauri ambako tunatoa 10% maana yake mapato yakiimarika yakiongezeka maana yake hata ile 10% itakuwa ni fedha za kutosha zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hiyo ni mikakati ya Serikali kuhakikisha fedha pia zitaendelea kutengwa kwenye mifuko mingine ambayo itakuwa imeunganishwa hapo baadaye ili waweze kuwa na bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuhudumia wananchi.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Hivi karibuni nchi jirani ya wenzetu imeingia makubaliano na nchi za uingereza za kupeleka wataalam wa afya vijana kwa ajili ya kufanya kazi kule. Majibu ya Serikali ni mazuri, lakini matokeo yake hayaridhishi. Ni lini hasa Serikali itaona haja ya kuja na mikakati mbadala ya kuhakikisha inatumia Balozi zetu tulizonazo katika nchi zaidi ya 25 na Balozi Ndogo kwenye nchi zaidi ya 15 kuhakikisha inaongeza mawanda ya vijana kupata ajira? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mheshimiwa Rais wa nchi yetu, Mama Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya juhudi kubwa sana za kuhakikisha anapanua mawanda ya mahusiano ya Kimataifa kwa nchi yetu katika nchi za Kimataifa, lakini takwimu zinaonesha kwamba, vijana wachache sana wanapata nafasi za ajira kwenye nchi jirani. Serikali je, inalitambua hili? Na kama inalitambua ni lini hasa itaanza kuchukua hatua ili kuhakikisha juhudi za Mheshimiwa Rais zinapata tija ya ajira kwa vijana? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna haja ya Serikali yetu kuongeza juhudi katika kuhakikisha kwamba, vijana wetu wanapata fursa za ajira nje ya nchi. Miongoni mwa mbinu hizo ni kuhakikisha kwamba, tunaingia mikataba na nchi mbalimbali ili kuhakikisha kwamba, fursa zilizopo huko zinapatikana.
Mheshimiwa Spika, mfano hivi sasa tayari tumeshaingia mkataba na nchi ya Qatar mwezi uliopita tu ujumbe mkubwa wa Tanzania ulikwenda Doha mahsusi kwa ajili ya kufuatilia mkataba huo. Katika makubaliano yao tayari nchi ya Qatar imekubali kufungua Visa Centre hapa Tanzania maalum kwa ajili ya vijana wa Tanzania kwenda kufanya kazi Qatar. Pia tumeanza mazungumzo na nchi za Falme za Kiarabu na Oman na Saudi Arabia kwa ajili ya kuingia nao mkataba. Hii mikataba ni muhimu sana kwa sababu ndiyo inayotupa uhakika wa kupata hizo ajira.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kwamba, Serikali imeona kuna umuhimu mkubwa sana wa vijana wetu kupata ujuzi kabla ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi. Hivyo basi, kupitia TAESA ambao ni wakala maalum wa taasisi ya ajira hapa Tanzania, imeanzisha kanzi data na ina portal maalum ili vijana waweze kujiandikisha mara zinapotokea fursa za ajira waweze kuajiriwa.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa tayari portal hiyo ina vijana wanaofika 40,000 na umuhimu wake ni kwamba, hao vijana kabla ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi huwa wanapewa mafunzo maalum ili kuhakikisha kwamba, wanapokwenda huko nje hawaharibu katika kazi ambazo wamepelekewa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini bado jukumu la msingi la kulinda maslahi na vipato vya Watanzania linabaki kuwa la Serikali, basi swali langu la kwanza; je, Serikali inatambua uwepo wa makampuni haya ambayo Watanzania wamewekeza kwa kununua hisa yanafanya biashara, yanatengeneza faida na bado hayalipi magawio kwa Watanaznia hawa waliowekeza?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali inasemaje au ina mkakati gani wa kuja na mpango madhubuti na wa wazi wa kuhakikisha kwamba inalinda maslahi ya Watanzania hawa waliowekeza dhidi ya wizi huu wa kuaminiwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kamani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza tumepokea shauri hilo na tunafuatilia mara moja. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge tuwe na mashirikiano ya pamoja katika kuzitambua kampuni hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nielekeze DSE na CMA kufanya uchunguzi juu ya tuhuma hii ya wizi na mara tu zitakapobainika hatua za kisheria zitachukuliwa.
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilitenga eneo la ekari 50 kuipa Wizara ya Elimu bure kabisa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA: Sasa ni lini chuo hiki kitaanza kujengwa rasmi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ng’wasi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Ilemela ni miongoni mwa Wilaya 63 ambazo tunaanza ujenzi katika mwaka huu wa fedha.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, ni lini ujenzi wa barabara ya kutoka Mwanza Airport kwenda Nyanguge kilometa 46 itaanza rasmi kujengwa kwa kiwango cha lami kama ilivyoahidiwa katika ilani mbili za uchaguzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara tajwa ni sehemu ya barabara ya bypass, imeshafanyiwa usanifu wa kina na Serikali inaendelea kutafuta fedha ili iweze kujengwa yote kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, la kwanza: Pamoja na Bunge lako hili Tukufu kupitisha Sheria hii ya Fedha mwaka 2019 inayotoa nafuu ya mjasiriamali kwa mtu anayeanza biashara kulipa kodi baada ya miezi sita, lakini bado wananchi wakienda kutafuta leseni kwenye Halmashauri zetu wanatakiwa kupeleka Tax Clearance kutoka TRA. Ili aipate hii Tax Clearance anatakiwa afanyiwe makadirio ya kodi na alipe kodi ya mwanzo. Sasa nini Kauli ya Serikali juu ya mkanganyiko huu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Sheria ya Uwekezaji Tanzania ikisomwa pamoja na Sheria mbalimbali za Kodi nchini, inatoa ruhusa kwa mamlaka mbalimbali za mapato kutoa msamaha wa kodi kwa wawekezaji wa nje mpaka mitano; na hii ni nzuri kwa ajili kukuza uwekezaji nchini. Sasa ni lini Serikali itaona haja ya kufanya mapitio ya Sheria hii ya Fedha ya mwaka 2019 ili kuongeza muda wa msamaha wa kodi kwa wazawa angalau kwa miezi 12 mpaka 18 ili: moja, kuendelea kutoa motisha kwa wawekezaji hawa wa ndani: na pili, kuwapa mazingira bora ya ushindani wawekezaji hawa wa ndani sambamba na wawekezaji hawa wa nje katika biashara? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kamani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa idhini yako, naomba nielekeze Kamishna wa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria. Sheria hii imepitishwa, hakuna Mjasiriamali yeyote mpya anayetakiwa kulipia chochote kabla ya biashara yake. Kwa hiyo, naomba nimwelekeze kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba nipokee maoni ya Mheshimiwa Mbunge tuyachukue kwenda kuyafanyia kazi.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika,nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali; nina maswali mawili ya nyongeza.
i. Serikali inatumia mfumo gani kutathmini tija na matokeo ya programu hizo hasa ukizingatia kasi kubwa ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia iliyopo sasa?
ii. Serikali ina makakati gani wa kuhakikisha kwamba Vijana wengi wananufaika na programu hizo ukizingatia uhitaji ni mkubwa kuliko nafasi zinazopatikana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI, MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ameuliza maswali mawili ya nyongeza; la kwanza ni kuhusu mfumo wa namna gani tunafanya tathmini kwa vijana hawa. Chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ipo Idara ya Maendeleo ya Vijana. Chini ya mkurugenzi huyo kuna timu maalum ambayo inafanya tathmini ikiwa ni pamoja na kuweka mifumo na utaratibu wa kuweka kanzidata katika vyuo husika ambavyo tunawapitisha vijana hao kupata mafunzo. Kwa hiyo tunabaki na takwimu kwa ajili ya kuwawezesha pia baada ya mafunzo waweze kupata fursa za ajira lakini zaidi tunawapa pia hadi vifaa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika,kuhusu swali la pili nalo ameuliza kuhusu vijana, sikuweza kulipata vizuri nikuombe kwa ridhaa yako, niweze kulisikia vizuri.
MHE.NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha vijana wengi zaidi wananufaika na programme hizo ukizingatia uhitaji ni mkubwa kuliko nafasi zinazopatikana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mikakati ambayo Wizara imeweka ni pamoja na huo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya kuhakikisha vijana wengi wanaingia kwenye blue economy, kwa maana ya ufugaji wa samaki. Mkakati mwingine ni huu wa ukuzaji ujuzi ambapo tayari tumefundisha vijana zaidi ya 74,598, lakini pili upo mkakati mwingine huu ambao uko chini ya Wizara ya Kilimo unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu wa BBT ambapo tayari vijana 821, na Mheshimiwa Rais alizindua programme hiyo.
Meshimiwa Naibu Spika, tunao mkakati mwingine kupitia NACTVET pamoja na mafunzo ya TEHAMA ambayo tunaendelea nayo. Vilevile tuna Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa ambao unatutaka tuweze kuwafikia vijana zaidi ya 681,000 kwa kipindi hiki katika mpango huo wa miaka mitano. Tayari Serikali imeanza engagement na wadau wa maendeleo wakiwemo GIZ, International Labour Organisation pamoja na wadau wengine ni pamoja na Serikali yenyewe katika kuweka fedha kuhakikisha mafunzo haya tunayatoa kwa vijana walio wengi zaidi na kuwatafutia ajira ndani na nje ya nchi, ahsante.
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, moja, kwa vile wakati tunapitisha bajeti ya Wizara hii, Wabunge wengi ambao ni wawakilishi wa wananchi walionesha haja ya kuiomba Serikali kuwaangalia vijana mbalimbali wanaojitolea kwa jicho la tatu, hasa katika maombi ya kazi, na kwa vile Serikali yenyewe ndiyo imesema kwamba ilitengeneza mazingira haya ili kuwapa competitive advantage vijana hawa wanapotoa nafasi za kazi, swali la kwanza: -
Je, Serikali haioni haja ya kuja na mabadiliko ya hizi sera, kanuni au sheria ili kuweka hii competitive advantage kwa hawa vijana pindi maombi ya kazi yanapopelekwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nini sasa kauli au commitment ya Serikali kwa vijana mbalimbali waliopo katika vituo mbalimbali vya kazi sasa wakiwa wanajitolea kutoa huduma mbalimbali kwa Watanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA
UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ng'wasi Damas Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza kabla sijajibu maswali yake ya nyongeza, nataka nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo hajawasahau vijana wake, na kwa kweli anafanya kazi nzuri, na Mwenyezi Mungu atakujalia dada yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maelezo ya ziada aliyoyatoa Mheshimiwa Ng’wasi Kamani ninaunaga naye moja kwa moja, ni kweli Bunge lako wakati linajadili Hotuba ya Bajeti hii ya Wizara yetu ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Wabunge wengi walizungumza sana juu ya jambo la vijana wanaojitolea. Na nataka nirudie tena kueleza kwa kifupi juu ya commitment ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilikiri kupokea maoni ya Wabunge wote na kwamba tutakwenda kuyafanyia kazi. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ninapozungumza leo saa nane kikao cha kwanza kwa ajili ya kujadili jinsi gani Serikali inakabiliana na tatizo la ajira tunakwenda kuanza chini ya uongozi wangu, kwa sababu Mheshimiwa Waziri amenikasimia mamlaka hayo niweze kulisukuma mbele jambo hili la ajira kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwenye swali lake la pili juu ya commitment ya Serikali; kwa maelezo niliyotangulia kutoa hapa, ni wazi kwamba Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejizatiti kuhakikisha kwamba inakabiliana na jambo hili, na tuko bega kwa bega naye Mheshimiwa Rais sisi kama watendaji wake, kuhakikisha kwamba tunakwenda kuli-address jambo hili na kulitafutia mwarobaini wake.
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Tunatambua kwamba lengo la Serikali kuweka utaratibu huu ni pamoja na kutambua uwezo wa kiakili wa watoto wetu pamoja na uwezo wao wa kusoma kwa muda fulani. Tunavyozungumza, kuna shule za primary hasa za watu binafsi ambazo mwanafunzi wa kutwa anaenda shuleni kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa kumi na moja na wa bweni anasoma tena kuanzia saa moja mpaka saa tatu au saa nne usiku, zaidi ya muda ambao umepangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Je, Serikali inatambua kwamba kuna shule ambazo zinafanya utaratibu huu ambao ni kinyume kabisa na utaratibu na inahatarisha afya za akili za watoto wetu? Kama inatambua, inachukua hatua gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa ajili ya umuhimu wa afya za akili za watoto wetu: Je, Serikali haioni haja kwenye marekebisho haya yanayofanyika ya utaratibu wa elimu na mfumo wake kuliingiza suala hili katika mfumo? Ahsante.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kwamba ziko shule ambazo wanafunzi wanakaa muda mrefu zaidi shuleni na vile vile wanatumia muda mrefu sana kwenda shuleni na kuna aina mbili ya changamoto katika jambo hili. Kwanza, sio wanafunzi wote wanatumia mitaala ile ile. Ziko shule ambazo zinatumia mitaala tofauti na ile ambayo imetolewa na Serikali. Kwa mfano, kuna wale wanaotumia mitaala ya Cambridge na muda wao wa kusoma siyo lazima uwe sawa na muda wetu. Pili, kwa kuchagua shule, hasa hizi binafsi na umbali wa shule na nyumbani, baadhi ya wanafunzi wanajikuta wanaondoka mapema sana nyumbani na wanarudi kwa kuchelewa sana, kwa sababu tu ya choice ya wazazi kwamba pengine wanaishi Mbezi Beach lakini mtoto wako anaenda kusoma Kimara tofauti na kusoma eneo lile lile la Mbezi Beach.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili suala ni changamoto kweli kwa sababu tungependa watoto wapate fursa vile vile ya kucheza na kuwa watoto na kuwa na makuzi mazuri na wasitumie muda wote tu kwa ajili ya shughuli za darasani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutajitahidi kuendelea kukaa na wadau wa shule binafsi kuangalia namna bora zaidi ya kutatua changamoto hii. Vile vile tunaendelea kuhimiza ujenzi wa shule mbalimbali za watu binafsi ziwe karibu zaidi na makazi ya watu na kuhimiza wazazi wachague shule ambazo ziko karibu zaidi na nyumbani ili watoto wasitumie muda mrefu sana barabarani wakati wanaenda shuleni.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, kwa kuwa lengo kuu la hizi programu ni kutatua changamoto kubwa za vijana ikiwemo kukuza elimu ya ujuzi na kutatua changamoto ya ajira, kumekuwa na changamoto ya vijana wengi ambao wananufaika na hizi programu kushindwa kuunganishwa moja kwa moja na masoko ya ajira na mitaji pale wanapohitimu. Sasa, ni upi utaratibu au mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kuwa vijana hawa wanapohitimu programu hizi wanaunganishwa moja kwa moja na masoko ya ajira au mitaji ili wasirudi mitaani na kuondoa tija ya hizi programu wanazopata?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, bado kuna changamoto ya taarifa hasa kwa vijana wengi waliopo vijijini ya namna gani programu hizi zinapatikana, vigezo na utaratibu wa kuweza kupata programu hizi. Sasa ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha inaboresha mifumo ya taarifa ili vijana wengi wa Tanzania waweze kufahamu fursa hizi na kunufaika nazo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, upo utaratibu ambao Serikali inaendelea nao na tumekuwa tukiendelea kuufuatilia na kufanyia tathimini kuhusu namna ya kuunganishwa na ajira lakini pia kupata fursa za mitaji. Wote tutakuwa mashahidi kuwa kupitia Halmashauri zetu wapo Maafisa Maendeleo ya Vijana lakini pia Maafisa Maendeleo ya jamii. Wote hawa wanaendelea kutoa mafunzo kwa utaratibu wa mwongozo. Mikopo ya asilimia kumi kwanza inatangazwa lakini pili ni takwa la Ilani ya Chama cha Mapinduzi na tatu inaendelea kutangazwa katika Halmashauri zetu zote. Viongozi wengi sana na hata Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakihamasisha uwepo wa ile mikopo ya asilimia kumi. Pia ipo mifuko mingine ya uwezeshaji vijana ukiwemo Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao upo Ofisi ya Waziri Mkuu na tumekuwa tunautangaza kupitia Mwenge wa Uhuru.
Mheshimiwa Spika, pia zipo programu nyingine katika wizara za kisekta. Ipo mipango ya kisekta ya kuwasaidia vijana kwa mfano kwenye masuala ya fursa za ajira, kuwaandaa kwenye ajira na mitaji. Pia tuna Wakala wa Ajira (TaESA) ambaye ana jukumu kubwa; kwanza la kuwatambua vijana wote wahitimu, pili kuwapeleka kwenye programu mbalimbali ikiwepo utarajali na kuwapeleka kwenye mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Wizara zote za Kisekta zimekuwa na programu za vijana zinazohusiana na uandaaji wao wa kupata ajira hata ukiangalia Wizara ya Kilimo tunayo Building a Better Tommorow (BBT) ambayo ni kwa ajili ya kilimo biashara. Wizara ya Mifugo na Uvuvi nayo ina programu ambayo ni BBT Life ambayo inahusiana na unenepeshaji mifugo.
Mheshimiwa Spika, hao wote wamekuwa wakikutanishwa na masoko ya ajira lakini pia masoko ya malighafi ambazo wanazitengeneza katika maeneo hayo. Nikiongelea la mwisho ambalo ameniuliza kuhusu changamoto za vigezo na taarifa, hili limeelezwa wazi kwenye mwongozo wa utoaji wa mikopo ya asilimia kumi yaani 4:4:2, almaarufu katika Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, hata sisi kwa upande wa Wizara tumeendelea kufanya hivyo siyo tu katika ufuatiliaji na tathimini lakini pia tumeendelea kutoa elimu kwa vijana na kuitangaza katika maeneo mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, ahsante.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuona potential iliyoko kwenye Ziwa Viktoria na haja ya kulitumia ziwa hili kuweza kutatua changamoto za kiuchumi na ajira kwa vijana walioko katika Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza fedha hizi zimetengwa takribani Shilingi bilioni 20 kwa mwaka wa fedha 2022/2023; na tunavyozungumza sasa utaratibu ulianza tangu mwaka 2022 na sasa tumebakiwa na kama siku saba tu kumaliza mwaka huu wa fedha 2022/2023; naomba commitment ya Serikali: Ni lini hasa utekelezaji wa mradi huu utaanza kwa sababu, taratibu zote za awali zimeshatimia?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa vile tayari kuna sintofahamu na changamoto fulani kwa vijana wa Mwanza na Mikoa yote ambayo inahusika na mradi huu ambazo baadhi yake nilizungumza jana: Je, Serikali au Waziri na wasaidizi wake wako tayari kuambatana nami baada ya Bunge hili la Bajeti kwenda kuwasikiliza vijana wanaonufaika na mradi huu juu ya changamoto na sintofahamu zao kuweza kuzitatua? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia jambo hili kwa ukaribu kabisa. Nimhakikishie tu kwamba tuko katika hatua za mwisho za maandalizi za ugawaji wa hivi vifaa, hususan maboti kwa wavuvi wa Kanda ya Ziwa Victoria. Uzinduzi huu tutafanyia huko huko ukanda wa Ziwa Viktoria. Kwa hiyo, tuko katika hatua za mwisho na ninaamini ndani ya muda mfupi Wizara ya Mifugo na Uvuvi itataja hiyo tarehe rasmi ya lini sasa tunatoa vifaa hivyo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuambatana na Mheshimiwa Mbunge, mimi pamoja na Mheshimiwa Waziri tuko tayari muda wowote mara baada ya Bunge lako kuahirishwa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali ya nyongeza;
(i) Je, nini kauli ya Serikali juu ya waajiri wa sekta binafsi ambao bado wanatumia kigezo hiki cha uzoefu kwenye kutangaza ajira?
(ii) Je, Serikali iko tayari kufufua ule utaratibu maalum uliokuwepo mwanzo na kuutengenezea sera ambao utawatambua na kuwapa kipaumbele wahitimu ambao wanajitolea kwenye ofisi mbalimbali za umma kwa ajili ya kupata uzoefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imekuwa inafanya jitihada kubwa hasa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuhakikisha kwamba wale waajiri wanazingatia vigezo ambavyo vinatakiwa katika ukuzaji au uenezaji au ule usimamizi wa soko la ajira. Mojawapo ni katika eneo la watu binafsi ambako nako mara kwa mara tunawaelekeza kwamba lazima vigezo vya kuingia viangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwenye sekta binafsi, pamoja na utaratibu ambao sisi kwenye soko la ajira tumeuzoea lakini ni kweli kwamba kwenye sekta binafsi kinachoangaliwa zaidi ni tija ili kuweza kusaidia mtu aweze kupata faida katika jambo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mawazo yaliyotolewa na Mheshimiwa Mbunge tunayachukua na tutaendelea kuyasimamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo la pili; kwa wale wahitimu ambao wanaomba kazi, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inawatambua; na sasa tuko katika hatua za mwisho, kama nilivyowahi kueleza mwanzo, ya kukamilisha ule muundo mzima au taratibu nzima za jinsi wao pia tunawaingiza katika soko la ajira kwa kuzingatia vigezo. Vigezo hivyo ni pamoja na kigezo cha kuwajengea uwezo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa maana ya lugha ya internship, lakini pia, kuweka vigezo vingine ambavyo vitawasaidia vijana waweze kuingia katika soko la ajira kirahisi, nashukuru.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali na pamoja na kwamba focus ya Serikali sasa hivi ni kufanya kazi na sekta binafsi kwa mfumo wa PPP. Je, ni lini sasa uhuishwaji huu wa hizi kanuni utakamilika ili kuweza kuwezesha sekta binafsi kuingia na kutoa elimu ya majanga haya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa madhumuni ya kuharakisha hili jambo ambalo amelipendekeza Mheshimiwa Kamani, ni jambo jepesi kwa sababu Kanuni zinaishia kwa Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wataandaa mapendekezo ya namna ya kuzingatia kwenye Kanuni zilizopo ili kuhuisha na kujumuisha hili suala kwenye utendaji wa Zimamoto na Uokozi, nashukuru.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, imekuwa takribani miezi kumi tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, atoe maelekezo ya kusitisha mikopo iliyokuwa inatolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa kupisha utaratibu mpya ambao utakuwa na manufaa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua ni lini hasa Serikali itarejesha utaratibu huu, ili vijana waendelee kunufaika na mikopo hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Vijana, Mheshimiwa Ng’wasi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili kwa kuwa lilifuata utaratbu na wenzetu wa TAMISEMI, wameendelea kulizungumzia, tuendelee kuwaachia wenzetu wa upande wa TAMISEMI watatupa taarifa rasmi ya wapi wamefikia na lini wataanza kutoa mikopo hiyo, lakini niwahakikishie kwamba, mikopo ile ipo, fedha ipo. Utaratibu utakapoanza makundi haya yajiandae kwa ajili ya kunufaika na programu hiyo.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali kwa majibu yake mazuri. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kwa kuwa Mkoa wa Mwanza umethibitika kuwa ndiyo mkoa ambao ni wa pili kwa idadi kubwa ya watu katika nchi yetu kwa sasa, na kwa kuwa tayari barabara hizi zimeshakuwa na jam kubwa inayozuia shughuli za maendeleo kufanyika kwa wakati: Je, Serikali haioni kwamba sasa ni wakati wa kutenga fedha katika bajeti hii ya mwaka unafuata ili kutengeneza barabara hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni nini mpango wa Serikali wa kujenga barabara nne katika Barabara ya Usagara – Buhongwa - Mkolani kuja katika Jiji la Mwanza na katika zile barabara za makutano ya pale Kenyatta ili pia kupunguza msongamano katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyojibu katika jibu la msingi, ni kweli Mji wa Mwanza sasa hivi una msongamano mkubwa wa magari na ndiyo maana Serikali tayari tumeshakamilisha usanifu kwa ajili ya kuweka flyover katika eneo la Buzuruga. Kwa hiyo, Serikali inatafuta fedha kuhakikisha kwamba inajenga flyover.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kupunguza msongamano katika Jiji la Mwanza, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pia tumeshakamilisha usanifu kutoka katikati ya Jiji la Mwanza kwenda Usagara na vile vile kutoka katikati ya Jiji kwenda Nyanguge ili ziwe njia nne ikiwa ni lengo la kupunguza foleni katika Jiji la Mwanza, na tayari tumeshakamilisha usanifu, ahsante.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa takwimu zinaonesha kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la ndoa nyingi zinazovunjika baada tu ya miaka miwili ya kufungwa kwake. Kufuatia takwa la Sheria za Ndoa la mwaka 1971, Serikali haioni haja ya kuondoa au kupunguza takwa hili au kigezo hiki cha miaka mitatu kwa waajiriwa wanaotafuta uhamisho kwa kigezo cha kufuata wenza wao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa ni ukweli usiopingika kwamba malezi mazuri ya watoto na kuwepo kwa familia imara na bora kunategemea malezi ya wazazi wote wawili na sasa hivi nchini tumekuwa na changamoto kubwa sana ya mmomonyoko wa maadili kwa watoto. Hatuoni haja au Serikali haioni haja ya kuondoa kabisa kigezo hiki cha miaka mitatu kwa watu wanaotafuta uhamisho? Au kuwaweka moja kwa moja waajiriwa ambao ni wanandoa sehemu moja ya ajira? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Kamani kwa namna ambavyo anafuatilia masuala ya haki za watumishi ikiwemo uhamisho.
Mheshimiwa Spika, katika kujibu swali lake anasema kwamba kigezo cha miaka mitatu kuondolewa, Serikali iliweka kigezo hiki cha miaka mitatu kwanza ili kuweka stability ya taasisi, kwa maana ya kwamba ukiruhusu watumishi wakakaa kwa muda mfupi namna ya ku-retain na performance ya taasisi inaweza kushuka. Hii imeoneshwa katika Mikoa ya Pembezoni baada ya kuweka muda mfupi watumishi wengi wanachukua check number na kuondoka na baadaye kupelekea uhaba wa watumishi.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali imeendelea kutoa vibali vya uhamisho kwa wale watumishi hasa wanaotaka kuungana na wenzao. Kwa mwaka wa fedha 2023/2024, maombi yalikuwa takribani 3,374 na Serikali imetoa vibali 1,136. Kwa hiyo, Serikali itaendelea na jitihada hiyo bila kuathiri haki na maombi ya hawa watumishi wanaoomba kufuata wenza wao. (Makofi)
MHE. NGW’ASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wa majimbo matatu, Jimbo la Kwimba, Jimbo la Sumve na Jimbo la Magu na ni barabara ambayo inapitisha shughuli nyingi sana za kiuchumi kwa wananchi hawa. Hizi kilomita 10 za barabara hii zilitengewa fedha katika bajeti iliyokwisha, mwaka 2023/2024, lakini mpaka sasa mkandarasi hajaweka hata vifaa site. Je, ni lini mkandarasi ataanza kazi rasmi katika barabara hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuhusiana na zile kilomita 61 zilizobaki. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kilomita hizi kwa kiwango cha lami ukizingatia zimekuwa zikiahidiwa katika ilani mbalimbali za uchaguzi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba barabara hii inaunganisha majimbo matatu, Sumve, Magu na Kwimba, tunatambua umuhimu wake na pia barabara hii iko kwenye ilani na ndiyo maana tumeanza kuijenga kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, tumeshajenga roundabout na sasa tumeshasaini mkataba na mkandarasi ili tuanze kujenga kwa awamu hizo kilomita 10. Mkandarasi sasa hivi yuko kwenye maandalizi ya awali kwa ajili ya kuanza hizo kilomita 10.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, kwa sababu mpango ni kuijenga barabara hii yote, Serikali inaendelea kutafuta fedha na tukipata fedha, basi tutaijenga yote kwa pamoja, lakini kama fedha itakuwa inapatikana kwa awamu tutaendelea kuijenga kwa awamu ili kuikamilisha hiyo barabara. Ahsante.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa takwimu zinaonesha kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la ndoa nyingi zinazovunjika baada tu ya miaka miwili ya kufungwa kwake. Kufuatia takwa la Sheria za Ndoa la mwaka 1971, Serikali haioni haja ya kuondoa au kupunguza takwa hili au kigezo hiki cha miaka mitatu kwa waajiriwa wanaotafuta uhamisho kwa kigezo cha kufuata wenza wao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa ni ukweli usiopingika kwamba malezi mazuri ya watoto na kuwepo kwa familia imara na bora kunategemea malezi ya wazazi wote wawili na sasa hivi nchini tumekuwa na changamoto kubwa sana ya mmomonyoko wa maadili kwa watoto. Hatuoni haja au Serikali haioni haja ya kuondoa kabisa kigezo hiki cha miaka mitatu kwa watu wanaotafuta uhamisho? Au kuwaweka moja kwa moja waajiriwa ambao ni wanandoa sehemu moja ya ajira? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Kamani kwa namna ambavyo anafuatilia masuala ya haki za watumishi ikiwemo uhamisho.
Mheshimiwa Spika, katika kujibu swali lake anasema kwamba kigezo cha miaka mitatu kuondolewa, Serikali iliweka kigezo hiki cha miaka mitatu kwanza ili kuweka stability ya taasisi, kwa maana ya kwamba ukiruhusu watumishi wakakaa kwa muda mfupi namna ya ku-retain na performance ya taasisi inaweza kushuka. Hii imeoneshwa katika Mikoa ya Pembezoni baada ya kuweka muda mfupi watumishi wengi wanachukua check number na kuondoka na baadaye kupelekea uhaba wa watumishi.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali imeendelea kutoa vibali vya uhamisho kwa wale watumishi hasa wanaotaka kuungana na wenzao. Kwa mwaka wa fedha 2023/2024, maombi yalikuwa takribani 3,374 na Serikali imetoa vibali 1,136. Kwa hiyo, Serikali itaendelea na jitihada hiyo bila kuathiri haki na maombi ya hawa watumishi wanaoomba kufuata wenza wao. (Makofi)
MHE. NGW’ASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wa majimbo matatu, Jimbo la Kwimba, Jimbo la Sumve na Jimbo la Magu na ni barabara ambayo inapitisha shughuli nyingi sana za kiuchumi kwa wananchi hawa. Hizi kilomita 10 za barabara hii zilitengewa fedha katika bajeti iliyokwisha, mwaka 2023/2024, lakini mpaka sasa mkandarasi hajaweka hata vifaa site. Je, ni lini mkandarasi ataanza kazi rasmi katika barabara hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuhusiana na zile kilomita 61 zilizobaki. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kilomita hizi kwa kiwango cha lami ukizingatia zimekuwa zikiahidiwa katika ilani mbalimbali za uchaguzi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba barabara hii inaunganisha majimbo matatu, Sumve, Magu na Kwimba, tunatambua umuhimu wake na pia barabara hii iko kwenye ilani na ndiyo maana tumeanza kuijenga kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, tumeshajenga roundabout na sasa tumeshasaini mkataba na mkandarasi ili tuanze kujenga kwa awamu hizo kilomita 10. Mkandarasi sasa hivi yuko kwenye maandalizi ya awali kwa ajili ya kuanza hizo kilomita 10.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, kwa sababu mpango ni kuijenga barabara hii yote, Serikali inaendelea kutafuta fedha na tukipata fedha, basi tutaijenga yote kwa pamoja, lakini kama fedha itakuwa inapatikana kwa awamu tutaendelea kuijenga kwa awamu ili kuikamilisha hiyo barabara. Ahsante.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwanza nianze kwa kuishukuru na kuipongeza sana Serikali kwa majibu mazuri. Pia, nitumie fursa hii kuipongeza sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na hii ndiyo maana nzima ya kuahidi na kutenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 - 2025 ukurasa wa 43 iliahidi kutoa vifaa hivi na kuwawezesha vijana 400, lakini jibu la Mheshimiwa Waziri linaonesha kwamba wamewawezesha vijana 420. Maana yake ni zaidi ya utekelezaji wa 100%. Sina swali la nyongeza, naipongeza Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, naomba sasa kuwepo na series ya ufuatiliaji wa vijana hawa ili vifaa hivi walivyopewa viweze kweli kuwaletea yale manufaa ambayo yalitegemewa tangu mwanzo na manufaa kwa wakulima katika utunzaji wa chakula baada ya mavuno. Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: ahsante sana.