Contributions by Hon. Martha Nehemia Gwau (7 total)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii. Kwa vile ni mara yangu ya kwanza naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia mpaka kufikia siku ya leo. Pia naomba niishukuru familia yangu kwa support waliyonipa kipindi chote. Naomba nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kurudisha jina langu na kuniwezesha kuwa hapa lakini mwisho, naomba niwashukuru wapiga kura wangu akinamama wa Mkoa wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi kuchukua nafasi hii kuchangia Mpango huu wa Miaka Mitano tunayoiendea. Kwanza naomba nimpongeze Waziri kwa hotuba nzuri lakini maelezo mazuri yanayohusiana na Mpango huu ambao naamini yamejikita kwenye kusaidia wananchi na hasa wale wenye kipato kidogo. Mchango wangu kwa siku ya leo nitauelekeza kwenye kilimo ambapo najua wachangiaji wengi wameshachangia, lakini kwa sababu ni suala ambalo linagusa mtu wa chini, kwa hiyo tunaliongelea mara kwa mara na tunaamini kwamba yule mtu wa chini ndiyo mlengwa hasa ambaye anapata shida na ndiyo mwenye kipato cha chini. Kuna usemi wa three knows wanasema; no pharmacy, no food, no future.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa mimi ninayetoka Mkoa wa Singida naomba nijikite kwenye zao kubwa la alizeti. Hili zao, wewe mwenyewe ni shahidi kipindi cha nyuma kama miezi mitatu iliyopita tumepata uhaba wa mafuta. Pia tuna mashamba ya kulima, tuna watu wenye nguvu za kulima ili hii alizeti itosheleze sisi kwa mwaka mzima na hata kupata ziada ambayo itasababisha sisi tukasafirisha kwenda kuuza. Kwa hiyo naomba pamoja na Mpango mzuri wa Wizara ya Kilimo, hili zao la alizeti tulipandishe hadhi liwe kama zao la korosho na mazao mengine ya kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Tukipandisha hadhi hili zao tutakuwa na guaranteed market lakini pia tutakuwa na guaranteed price kama yalivyo mazao mengine kama korosho, lakini pia litatusaidia sisi Watanzania na watu walioko nje ya Tanzania. Kwa kulipandisha hadhi tuhakikishe kwamba mbegu bora zinapatikana ambazo tukikamua mafuta ya alizeti tutapata mengi ukilinganisha na sasa hivi mbegu zilizopo mafuta yanayotoka ni 40% tu. Tukipata mbegu bora tukapata bei bora ya mbegu ambayo mkulima wa chini anaweza ku-afford kununua, itasaidia hili zao listawi lakini pia tuuze kwa Mkoa wetu wa Singida lakini hata na mikoa mingine ya jirani waweze kulilima na kupata faida kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni utafiti ambao utasaidia, siyo tu kwa Mkoa wa Singida najua Mkoa wa Singida zao linastawi vizuri, lakini utafiti ukifanyika ina maana hata na mikoa mingine itaweza kulima hili zao la alizeti. Mwisho wa siku hatutapata hii aibu ya kuagiza mafuta nje ambapo tunatumia pesa nyingi sana kuagiza na wakati hizo resources tungeziweka kwa wakulima wetu, tungewa- empower wananchi wetu, wakalilima na wakapata masoko, huu uhaba wa mafuta hautakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni zao la vitunguu ambalo linapatikana Mkoa wa Singida. Nalo hilo tulipandishe hadhi, tukipandisha hadhi litatusaidia tutalima Singida na mikoa mingine watalima pia. Kwa hiyo kwa upande wa kilimo nilitaka nijikite kwa hilo. Tuna SIDO wanaweza wakatusaidia kutoa elimu kwa wakulima wetu kwa viwanda vyetu vidogo vidogo ambavyo vikitaka kusindika mafuta na vitataka kufanya shughuli nzima za uzalishaji Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine naomba niongelee suala la…
SPIKA: Samahani Martha lipandishwe hadhi kwa kufanyaje?
MHE. MARTHA N. GWAU: Kuwa zao la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine naomba niongelee suala la usafiri. Tunajua uwekezaji ndiyo kila kitu kwa sasa hivi na ndiyo unasaidia pato la Taifa na ajira kwa vijana wetu. Usafiri wa anga ni kitu muhimu sana ambacho mwekezaji anakiangalia, awe wa ndani awe wa nje. Kutoka Dar es Salaam mpaka Singida ni masaa 12 kwa gari, sasa tukifungua viwanja vya ndege, tukapata ndege, mwekezaji atatumia saa 1.30 kufika Singida kuona fursa zilizopo ambazo ataweza kuwekeza. Sio tu mwekezaji wa nje lakini hata mwekezaji wa ndani, mtu wa Mwanza atakuja Singida mara moja, ataona fursa, ataondoka, nami wa Singida nitaenda Mtwara, nitaona fursa naondoka, kwasababu ya usafiri ambao ni ndege itakuwa ni rahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipongeze kwa kweli Shirika la Ndege, mikoa mingi imepata ziara hizo na viwanja. Tunaiomba Serikali kwa mikoa ambayo ya kimkakati kama Singida itusaidie uwanja wa ndege ili tuweze kupata fursa watu wote waone mazao yetu, tuna uchimbaji wa madini, tuna zao la alizeti, tuna mambo mengi ambayo yanaendelea Singida, tukipata kiwanja cha ndege na ndege itatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho la kumalizia, ni suala la usafiri wa treni. Tuna treni yetu ya Singida ambayo ilikuwa inasaidia wakulima wetu kusafirisha mazao kwa bei rahisi kutoka sehemu moja mpaka nyingine. Kwa hiyo, hiyo ilikuwa inampa fursa mwananchi wa Singida kujua soko liko wapi. Kama liko Mwanza, atapeleka mazao yake akauze kule, kwa sababu ulikuwa ni usafiri affordable lakini pia na bei kidogo ni nzuri. Kwa hiyo naomba Serikali iangalie hili la kufufua treni ya Singida ili itusaidie kwenye suala zima la kusafirisha mazao yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nataka niwakaribishe wote Mkoa wa Singida, tuna uzinduzi wa kitabu cha uwekezaji kwa mkoa, tarehe 23 Januari mje mjionee fursa mbalimbali ambazo Waheshimiwa Wabunge mnaweza kupenda kuwekeza na niwakaribishe sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nikushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)
SPIKA: Martha umesema tarehe 23 Januari.
MHE. MARTHA N. GWAU: Samahani ni tarehe 23 Februari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii uliyonipa na mimi ya kuchangia Wizara hii ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; kwanza kabisa naomba niipongeze Serikali kwa kazi nzuri wanayofanya katika Wizara hii kwa ajili ya kusaidia vijana wetu, lakini na Taifa kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite kwenye sanaa, najua wenzangu wamechangia michezo naomba niongelee Sanaa na Sanaa inavitu vingi kuna mziki, kuna movie na vingine. Naomba nijikite kwenye upande wa movie peke yake. Sanaa ni kazi, sanaa inasaidia vijana wetu wanapata ajira, sanaa inasaidia kuitangaza nchi yetu nchi mbalimbali, lakini sanaa hii itasaidia utalii na vitu vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu zilizopo watoa huduma ambao ni wasanii wetu na walaji kidogo kunakuwa na kupishana au kidogo kunakuwa na walaji wanaona kwamba hawapati ile wanaohitaji kutoka kwa watoa huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kumekuwa na wimbi kubwa sana la watu hapa hapa Tanzania kuangalia movie za Kinaijeria, kuagalia movie kutoka kwenye channel tofauti tofauti netflix na zingine. Sasa huwa najiuliza kwa nini hatupendi vya kwetu? Kuna tatizo gani kwa nini tusiangalie movie za kwetu na tuangalie movie za watu wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikagundua tatizo lipo kwa upande wa Serikali pia, Serikali imejikita sana kwenye habari na michezo nadhani sanaa haiipi uzito mkubwa na ukiangalia ndiyo inayoajiri vijana wetu kwa asilimia kubwa, wanahangaika kutoka chini lakini mpaka watafika juu. Kwa hiyo, nilikuwa naomba nimepitia ripoti ya Waziri kwa kweli wamejitahidi sana pamoja na timu yake nzima kuainisha kwenye upande wa sanaa kwa mwaka wa fedha ujao watafanya nini, ameainisha ataanzisha tuzo za kitaifa, mikopo mbalimbali kwa wasanii, ameainisha mengi mazuri ambayo atawafanyia Sanaa ili iweze kukuwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata Kamati pia wamekiri kwamba kuna ukuwajuwaji wa asilimia kubwa kwenye sanaa kwenye nchi yetu toka mwaka 2015 wamesema ilikuwa asilimia 6.2, lakini sasa imekuwa mpaka asilimia 11, kwa hiyo tumeona kuna tija ya Serikali kuwekeza zaidi kwenye sanaa ili wavijana wetu waweze kujiajiri, lakini pia waweze kutengeneza vitu ambavyo vitakidhi matakwa ya malaji ambayo ni customer kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la sanaa yetu, tatizo la movie zetu za Tanzania zinakosa ubunifu, lakini zinakosa uhalisia kwa sababu ni kwanini watu wengi wanapenda kuangalia movie za nchi nyingine kama India, China, lazima tujiulize sababu ni nini, wale wana ubunifu na wana uhalisia; kwa hiyo na sisi tujikite kusaidia vijana wetu waje na ubunifu, lakini waje na uhalisia kwa sababu ni ukweli usiopingika sanaa ni another digital economic, mtu anaweza aka-act movie Tanzania ikaangaliwa Marekani na wakalipia netflix, tunalipia movie za kinaijeria kwanini vijana wetu wasiweze ku-act na nchi nyingine wakalipia wakapata kuangalia movie zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuna tatizo lazima tuangalie jinsi ya kulitatua, lakini lazima tuangalie jinsi ya kuli- facilitate. Mheshimiwa Waziri anaposema kwamba mashindano ya kitaifa, ya kimataifa, mikopo kabla ya kumpa mtu mkopo, kabla ya kumpa huyu mtu kufanya tuzo mbalimbali tuangalie ground, ground ya tatizo ni nini, kwa sababu uwezi ku-solve problem kama ujajua tatizo la problem nini tukitajiwa tatizo la problem tunaweza tuka solve problem. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema movie zetu hazina uhalisia na watu wengi hawapendi kuangalia kwa sababu ya vitu wanavyo act baadhi ya movie hizo hazivutii hata kutazama, lakini tukiongeza haya ya ubunifu na uhalisia kwa vijana wetu kwa kusaidiana na Serikali watafika mbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine kuna mataifa kama Korea, kuna mataifa kama Turkish wamefanya investment kwenye sanaa kwa sababu walitambua kwamba sanaa inaajiri vijana wengi sana wakawekeza kwenye taaluma mbalimbali, wakawekeza kwenye ubunifu mbalimbali na kwenye vitu mbalimbali ambavyo vitakuza hivi vipaji vya watu, lakini watoa huduma watoe huduma ambayo inakidhi matakwa ya mlaji ambayo ndiyo customer.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na ushauri mdogo tu kwa Serikali ambao nahisi kwamba itakuwa ni solution labda kwa soko letu la movie au wasanii wetu wa movie au wasanii wetu wa movie kwa ujumla. Unapotaka ku-solve problem kuna long term solution na kuna short term solution, mimi naona Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo waje na long term solution hata kama itatuchukua miaka mitano, hata kama kumi, lakini mwisho wa siku tuje na kitu ambacho mtu akiangalia wanasema kweli hii ni Tanzania imebadilika ya sanaa, long term plan ndiyo inatakiwa na wala siyo short term plan.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ukifanya long term plan utaanza kufanya kuanzia ground tatizo ni nini? Solution itakuwa ni nini? Na mimi kwa kufanya uchambuzi mdogo tu japokuwa na yapo mengi zaidi, lakini uchambuzi niliouona cha kwanza tufanye investment, Serikali lazima wawe willing kufanya investment, investment unaweza uka- invest leo return yake ikawa baada ya miaka 10, baada ya miaka mitano, but ikisha-turn around inakuja kuwa the best inakuja ku-solve tatizo lote kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tu-invest katika ku-empower watoto kuanzia wakiwa wadogo. Mataifa mengine wanakuwa kuwafundisha watoto kuongelea na miaka mitatu, anamfundisha mtoto kukimbia anamiaka mitatu huyu mtoto akifika hakija kuwa the best performer hakuna miujiza imetumika ni training aliyoipata kutoka chini, hawa ma- actor na ma-actress wakubwa wanaoingiza milioni za pesa kwenye nchi za wenzetu hawajatokea tu ukubwani kama mimi niende ku-act kesho wamepikwa kuanzia chini wakafundishwa, wakasaidiwa na Serikali yao kwa namna moja au nyingine kesho hakiwa anafanya vizuri ni matokeo ya investment ambayo imefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna shule za msingi, tuanzie kwenye shule za msingi tusiongelee kwamba tuna kuna chuo watoto wataenda kusoma, huyu mtoto wa maskini hatatokaje kule vijijini aende kwenye kile chuo, tukianza kufandisha masomo ya sanaa, lakini pia tukasaidia kuboresha hata kama yapo, wakaja mwisho wanamaliza la saba wanajua kuna kipaji cha huyu mtoto, wale watu wa sarakasi wanachukua, wa ku-act wanachukua, wa sehemu tofauti wanachukua, kunakuwa na designated sekondari moja kwenye kila kanda zitakuwa nne kwa mfano unasema Singida tunasema shule fulani tunaiweka inakuwa masomo ya kawaida, lakini na masomo ya sanaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mtoto akimaliza darasa la saba ataenda form one mpaka form six kwenye shule ambayo inatoa masomo ya kawaida, lakini inatoa na masomo ya sanaa pia. Kwa hiyo, akitoka hapo hata akichuliwa kwenda ku-act atakuwa the best kwa watakaishia pale, lakini watakaoendelea na chuo wataenda Bodi ya Mikopo na itawapa mikopo. Hizi programu za fine art and perfoming designing watakuwa the best, wanaenda kupewa mikopo watamaliza tukitoka hapo sasa tutazaa kizazi kipya cha bongo movie kwa sababu waliomaliza ndio watakwenda kuleta mapinduzi ya ubunifu, wataleta mapinduzi ya uhalisia, kwa sababu kaanzia kuanzia chini kujifunza na hata atakuja kuleta uhalisia na watu watapenda vya kwao kama ilivyo sasa tofauti watu wanapenda vya nje kuliko vya kwao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hayo kwa sababu Serikali isipoingilia kati kusaidia hili suala kwa long term solution tutaimba wimbo ule ule kila siku na tutaendelea kufaidika mataifa mengine tunaona Azam analipa pesa nyingi sisi tunaangalia movie zimekuwa translated Kiswahili, kwa nini tusiangalie za kwetu? Kwa nini ile pesa iende kule badala ya sisi tuipate hapa? Ni reform tu inayotakiwa kwenye suala la sanaa ambalo litasaidia vijana wetu waje na ubunifu mpya, waje na mbinu mpya tofauti na sasa hivi ukiangalia movie mtu anaweka sumu, anakoroga na anaonja; kweli utavutika kuangalia hiyo movie? Hapana, na movie hazina hisia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo soko hili ni kubwa lakini linaleta mamilionea na mabilionea wengi na tunawajua sitaki kuwataja, tuna tatizo gani tusitengeneze mabilionea hapa Tanzania au mamilionea ma-acter na maactress ambao watafanya kazi Tanzania zitauzika sehemu tofauti tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ulikuwa mchango wangu kwa leo, lakini naiomba Serikali ije na long term solution, tukifanya short term solution atakuja Waziri mwingine ataimba Wimbo wa Taifa huu, atakuja mwingine ataimba huu kwa sababu kwa mfano mzuri tu, hawa waliiomaliza bachelor of fine art and perfoming Mheshimiwa Waziri labda ni takwimu alizonazo ni wangapi wameajiriwa walipomaliza hizi shule? Unakuta hakuna, lakini hata bodi ya mikopo hii field ambayo ni muhimu kwa sasa hivi kwa digital economy je, hao wanafunzi wanapewa mikopo asilimia 100 inavyotakiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ndio hii tunasema tunasoma degree hazina faida lakini degree ya performing arts ina faida.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga hoja mkono, ahsante (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii uliyonipa nami niweze kuchangia Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwanza naomba niipongeze sana Serikali kwa kuja na Mpango huu wa Elimu bila Malipo. Naomba nipongeze sana kwa sababu Mpango huu umesaidia vijana wetu wengi, watoto wetu wengi kuweza kumaliza Kidato cha Nne tofauti na awali ilivyokuwa elimu yenye malipo. Kwa hiyo, kwa hili kwa kweli naomba niipongeze sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine naomba nijikite sana kwenye mitaala yetu au mtaala wetu uliopo kwa sasa hivi, naomba tuufanyie marekebisho au maboresho ili uendane na dunia inavyotaka au mahitaji ya dunia sasa hivi yanavyotaka, wanafunzi wawe na nini au wahitimu wawe na nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tujikite sana na kuwafundisha hawa watoto ubunifu na skills ili wakimaliza hapo wajiajiri na waweze kuajiriwa. NI tofauti na sasa hivi ambapo wakimaliza wengi wanajikita sana kusubiri ajira na hizo ajira hazipatikani kwa urahisi na siyo nyingi za kutosheleza. Katika hilo, nina ushauri wa vitu vitatu kwenye kuboresha mitaala yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza, tungeanzisha somo la technical subject katika elimu ya msingi mpaka sekondari. Kwa nini nasema hivyo? Hawa wanafunzi wanapomaliza Form Four kuna makundi matatu yanapatikana baada ya kuwa wamehitimu. Kuna kundi la kwanza watakwenda Form Five; kuna kundi la pili watakaokuwa wazazi wao wanaweza kuwalipia shule za VETA na ufundi na kadhalika; na kundi la tatu ambalo hilo halitaenda VETA, halitaenda Form Five; wanafanya nini na ndiyo kundi kubwa kuliko haya mawili niliyoyataja mwanzoni?
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwajengea uwezo kutoka primary wakamaliza Form Four na skills za kutosha, wakitoka hapo wataweza kwenda kwenye Halmashauri zetu, wakapata mikopo wakaweza kujiajiri, wakaunda vikundi, wakakopesheka, wakajiajiri na tukasaidia kutatua tatizo la ajira. Tofauti na sasa akimaliza Form Four anabaki nyumbani. Sasa atafanya nini na wakati tumempa elimu bure? Kwa hiyo, akimaliza na ujuzi itamsababisha yeye kujiajiri mwenyewe na kukopesheka kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, program ya pili tungeanzisha sports and games katika shule zetu ambapo awali zilikuwepo na tukapata wachezaji na watu wazuri tu, lakini naona zimefifia kwa muda uliopita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, michezo inaibua vipaji shuleni, inaibua wachezaji bora, wanamichezo bora kutoka utotoni na kutoka umri mdogo. Hatuwezi kusema mtu akienda kwenye degree ndiyo anaweza akawa mchezaji mzuri, hapana. Kuanzia level ya primary mpaka hapo Form Four atakuwa mchezaji mzuri, ndiyo tutakuwa na wachezaji wazuri. Kwa mfano, wachezaji wa nje kama akina Morisson, Chama, nasi tutapata wa kwetu hapa Tanzania. Nadhani wana-Simba wenzangu watakuwa wamenielewa. Kwa hiyo, tuanzishe hizo sports ambazo zitawasaidia watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, tuanzishe environmental subjects. Nina maana gani hapa? Tuna bahati ya kuwa na kanda tofauti tofauti na katika kila kanda kuna kitu wanajivunia. Kuna kanda wanafanya uvuvi, kuna kanda wanafanya kilimo, kuna kanda madini, kuna kanda wanafanya uvuvi na ufugaji na kadhalika. Tutakapowapa wanafunzi wetu mafunzo ya environmental studies, ataamua, mimi nataka kuwa mkulima. Atakuwa na mwalimu mkulima anamfundisha. Kuanzia level ya primary mpaka hiyo ya sekondari. Akitoka hapo anaweza akajiajiri mwenyewe kwa kufuga, kulima au kuchunga. Hayo tunamfundisha kutokana na mazingira alipo. Watu wa kanda ya kati tunajua tunafanya nini, watu wa kanda ya kaskazini na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya tukiyaongeza yatatusababishia vijana wetu wanaomaliza form four kwa kuwapa hii elimu bila malipo, lile kundi la tatu lililobakia, litapata kitu cha kufanya mtaani, badala ya sasa hivi wakimaliza wanakuwa wamekaa bila kazi yoyote, lakini hili lote itatusaidia sisi kama Serikali kupunguza suala la ajira kwa sababu, tutawakopesha kwenye halmashauri zetu na watajiajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la mwisho, naomba Serikali iongeze bajeti kwenye Wizara ya Elimu kwa sababu, Wizara ya Elimu inapaswa kuwapa Walimu mafunzo. Nimeongelea upande wa wanafunzi, lakini watoa huduma je, ambao ni Walimu. Naomba wapatiwe semina mbalimbali hata mara mbili kwa mwaka kwa sababu, unapompa Mwalimu semina ni kama motisha. Semina yenyewe hata iwe ya malipo, akipata semina yake anapata malipo yake inamsaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine motisha, kwamba, wanapopata zile semina basi kunakuwa na shule iliyofanya vizuri inapewa zawadi, kuna Mwalimu bora aliyefanya vizuri anapewa zawadi. Hii una-motivate Walimu wengine waliobakia au shule nyingine zilizobakia na wao kufanya vizuri zaidi, ili wapate hizo zawadi na recognition. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na uzuri zawadi sio lazima pesa. Mtu atakapopata certificate kutoka kwa Mkuu wa Mkoa au kwa Mkurugenzi wa Halmashauri anajisikia yuko well valuable, yaani anajisikia kwamba, ameheshimika na mchango wake umechukuliwa. Hii itasaidia Walimu wetu kuwa motivated na wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine pia ni reviews. Unapokaa na Walimu wa halmashauri moja wakasema kwa nini mimi nafaulisha zaidi kuliko wewe? Wata-exchange ideas, watapeana mbinu na mikakati mbadala ambayo itasababisha na yeye akirudi afanye vizuri kwenye shule yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndio ulikuwa mchango wangu kwa siku ya leo. Nashukuru sana kwa nafasi hii na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuwa mmoja wa wachangiaji katika Wizara hii muhimu kabisa ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa moyo wa dhati kabisa na kipekee nipongeze Wizara hii kuanzia Waziri mwenye dhamana, Naibu Waziri na wataalam wote waliopo katika Wizara hii, kwa jitihada madhubuti wanazozichukua kuhakikisha kwamba suala la utalii Tanzania linatangazwa vilivyo na pia tunapata watalii wa kutosha. Naomba nitoe pongezi hizo za dhati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, naomba nijikite kwenye utalii; utalii ni sekta muhimu sana kwa nchi yetu ambayo inatuingizia pato, lakini pia vijana wetu wanapata ajira, lakini pia pesa za kigeni, kwa hiyo unaweza kuona umuhimu wa sekta hii ya utalii nchini kwetu ilivyokuwa kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite kuelezea watalii wanaotoka nje kuja Tanzania. Mikakati ya Serikali kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri ni kujitahidi kuhakikisha namba ya watalii wanaotoka nje kuja Tanzania inaongezeka kwa miaka mitano ijayo. Mikakati hii ni mizuri na naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati hii itafanikiwa tukifanya mambo matatu; cha kwanza lazima tukubali kuwa creative na innovative. Lingine, tukubali kuwa competitive, lazima tukubali kushindina na wenzetu na la tatu lazima tukubali ku-learn from others, waliofaulu walifanyaje na sisi tunafanyaje, kwa nini tunakwama hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukizingatia Tanzania ni ya pili kuwa na vivutio vingi duniani, lakini kwa nini Tanzania siyo ya kwanza au ya pili au tatu, au ya tano kwa namba ya watalii wanaoingia Tanzania, ina maana hapa kuna shida ambayo hatujaitatua vizuri na ndiyo maana tunashindwa kufikia ile idadi ya watalii kuwa wengi kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza tukajifunza kutoka kwa wenzetu wa Comoro, Egypt na South Africa, wamefanya nini, kwa nini wenyewe wanapata namba kubwa ya watalii wanaokuja nchini mwao na sisi Tanzania hatupati namba hiyo, lazima kuna shida ambayo inabidi tujifunze na tukubali kubadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, napenda kuongelea sana quality of service inayotolewa baada ya wageni kuja Tanzania. Mheshimiwa Waziri na timu yake wanaweza wakatangaza matangazo yote ya promotion za utalii watu waje Tanzania. Wanaweza wakatumia wacheza mpira, ma-celebrity tofauti tofauti, lakini, je, wameshawahi kujiuliza swali mtalii akifika hapa anapata huduma inayostahili? The quality of service is it equal to value of money? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kama anakuja kuangalia tembo Tanzania na hapati huduma nzuri na tembo huyo huyo yupo Kenya ina maana ata-opt kwenda kwenye service nzuri ya Kenya na asije Tanzania. Kwa hiyo tukitoa quality service tutamvutia huyu mtu aseme Kenya kuna tembo mfano, Uganda kuna tembo na Tanzania kuna tembo na opt kwenda Tanzania because I will get a quality service na nitapata huduma nzuri inayotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nime-highlight mambo machache ambayo naona kama ni tatizo na of course tumesafiri sana unakutana na watu kwenye ndege popote huko duniani, wanakwambia Tanzania mnavivutio vizuri, lakini kuna shida kwenye huduma zenu. Kwa hiyo naomba Wizara wavi-note; cha kwanza, service provider wetu waiter, waitress, guide, chefs na receptionist hawa ni face ya watalii wote wanavyoingia nchini. Hawa watu ni lazima wapewe mafunzo mbalimbali, training mbalimbali ya kuhakikisha kwamba mtalii anapofika hapa yeye ndiyo kioo cha kumpokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Waziri na Naibu na Waziri na timu yake kumtangazia kuna Ngorongoro Tanzania, akishafika anakutana na nani, anakutana na service provider atahitaji kulala, anahitaji kula, anahitaji kutembezwa hawa watu Wizara inawaangaliaje, ili wao watoe huduma nzuri, huyu mtalii aridhike, aseme badala ya kwenda Kenya nataka niende Tanzania kwa sababu nitapata huduma nzuri. Hilo ni tatizo (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la pili ni lugha, watoa huduma wengi Tanzania wanaongea Kiswahili na Kiingereza, lakini wangeongeza lugha ya tatu kwa mfano, Wachina wengi wanapenda kwenda kutembea Thailand kwa nini? Ina maana kule wanaongea Kichina, kuna mtu anaye-guide anaongea kachina, anavutika kwenda kule, lakini barabara zetu ni mbovu za kwenda na ndani ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine network, communication network, siku hizi kuna kitu wanaita live, mtu akiwa kule kwenye mbuga za wanyama ataonyesha live nipo na simba kwa hiyo network communication iboreshwe…(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Haya ahsante sana.
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii uliyonipa ya kuchangia Wizara hii muhimu sana ya Kilimo, ambayo kwa wananchi wetu tunaowawakilisha ndio shughuli kubwa wanazozifanya kwa kujipatia kipato, nimshukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kabla sijaendelea nisiwe mchoyo wa fadhila kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuishika Wizara hii, lakini pia kwa kuona umuhimu wa Wizara hii na kuiongezea bajeti mwaka hadi mwaka wa fedha. Kwa hiyo nimpongeze sana. Pili, niipongeze Wizara chini ya kaka yangu Mheshimiwa Bashe na Naibu Waziri Mheshimiwa Mavunde, lakini na watendaji wote wa Wizara kwa juhudi kubwa na mikakati mingi wanayokuja nayo kwa ajili ya kumkwamua mkulima wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu leo utakua kwenye mambo mawili; suala zima la kilimo cha alizeti na suala zima la mbolea. Tanzania tuna wakulima nadhani wa aina tatu. Kuna wale ambao ni small scale farmers ambao ni majority ya watu wetu, ndio hao wanajishughulisha na kilimo kidogo kidogo. Pia tuna wale middle ambaye Kaka yangu Bashe amekuja na hii program ya BBT, mimi naweza nikasema kama hao ndio middle farmers. Vile vile tuna wale large farmers ambao wao wanakuja na mitaji yao na teknolojia yao. Sasa leo nijikite kuwaelezea au kuwatetea hawa small scale farmers ambao ndio mama zetu, baba zetu, wajomba zetu na watu wetu wote waliopo mikoani mwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nielezee zao la alizeti. Zao la alizeti ni kati ya mazao ya kibiashara yanayolimwa katika Mkoa wangu wa Singida. Pamoja na mazao mengine ya kibiashara lakini zao la alizeti ni zao letu moja la kibiashara. Tulipata heshima ya Waziri Mkuu kuja kuzindua mikoa ya kimkakati ambayo Singida ilikuwa kati ya hiyo mikoa ya kimkakati itakayolima zao la alizeti. Nimshukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna uongozi wa mkoa chini ya Mkuu wetu wa Mkoa Mheshimiwa Peter Serukamba na Wakuu wa Wilaya zote tano wakihamasisha na wakisaidia wananchi kuhamasisha kulima zao hili la alizeti, kwa sababu Serikali imetusaidia mbolea, ruzuku pamoja na mbegu. Kwa hiyo wao wanafanya uhamasishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoka kwenye kulima hekari laki nne na sasa tumelima laki sita na projection ya mwakani tutalima mpaka hekari milioni moja na tutakuwa na uwezo wa kulisha zaidi ya asilimia 40 ya mafuta kwa Nchi hii ya Tanzania katika Mkoa wetu mmoja wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, pamoja na juhudi nyingi wanazofanya na mikakati mingi, zao hili la alizeti sasa wakulima wetu wa Singida wanakata tamaa kulima. Wanakata tamaa kwa sababu bei ya mafuta ya alizeti imeshuka na zao la alizeti limeshuka kwa sababu Serikali haijaweka kodi kwa mafuta yanayotoka nje. Sasa how can you compete na Mheshimiwa Waziri kaka yangu slogan yake ni kumkomboa mkulima wa Tanzania. Ukombozi wa mkulima wa Tanzania, moja lazima iwe kulinda bei ya zao lake analolilima kwa sababu, nimesikiliza hotuba yake mwanzo mwisho kaongelea masoko ya ndani, ya nje na mambo mengi mazuri. Bahati mbaya sijasikia Mheshimiwa Waziri kaka yangu akiongea jinsi gani atalinda bei za mkulima huyu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapowahamasisha watu, Serikali wanapoweka mikakati mizuri ya kupata mbolea za ruzuku wananunua, lakini mbegu bora, sasa zao kama halina soko hawa watu wanakata tamaa, wanavunjika moyo. Kwa hiyo kabla Waziri hajaruhusu kodi kutowekwa kwenye mafuta ya nje, kutoa au kutokutoa, je, hivi wanawaza implication kwa hawa wakulima itakuwaje? Kwa hiyo nadhani ni mikakati ambayo Wizara inabidi ifanye kabla haijaruhusu kwa wakulima hawa kuvunjika moyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, Mheshimiwa Waziri aje na mikakati, atueleze na hawezi kushindwa kwa sababu he is the one of the best Ministers, ataweza kuwalinda wakulima wetu na kulinda bei za wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine cha pili hapo hapo, ni ushauri kuwa, wakulima wetu wauze final product badala ya kuuza mbegu. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri amekuja na wazo la BBT, hawezi kushindwa kwa wakulima hawa kutengeneza au kujenga kiwanda labda kila halmashauri ili wakulima hawa wauze final product, badala ya sasa hivi wananuza magunia ya lumbesa ambayo wanalaliwa tu au wanalanguliwa na watu ambao wanaenda kufaidika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama kuna kiwanda wakakamua mafuta watauza mafuta, lakini watauza mashudu nao watapata kipato kizuri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nashauri tu katika hili zao la alizeti naomba aliangalie kwa sababu Mkoa wa Singida kiuchumi kwa kweli zao la alizeti ndio zao ambalo wanalitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa mwisho ni suala zima la mbolea. Tuna mbolea na Serikali waliweka ruzuku kwa mbolea, lakini nashauri kwa nini hii ruzuku isitolewe kwa mbolea ya viwanda vyetu vya ndani? Nasema hivi kwa sababu viwanda vya ndani vina economic benefit ya kupewa ruzuku. Mbolea zote zinazoagizwa sisi tunafanya kama tuna export job, kwa sababu ukitoa ruzuku kwa mbolea za nje ni kama una-export job badala ya kufanya job creation. Tukiweka ruzuku kwa mbolea za viwanda vyetu vya ndani, ina maana tunaruhusu hivi viwanda viajiri watu wengi, lakini tunaruhusu uchumi u-circulate kwa sisi kwa sisi hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna faida ya kuweka ruzuku kwa viwanda vyetu vya ndani, mojawapo ni accountability. Mheshimiwa Waziri amekuja na ule mfumo wa zile namba za kugawa mbolea. Sasa kama viwanda vyetu vya ndani vitapelekwa ruzuku moja kwa moja kiwandani, ina maana tutakuwa na uwezo wa kusema Mkoa wa Singida peleka tani kadhaa na tutafanya accountability, kwamba hizo tani zimepelekwa na kweli zimewafikia wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine tutaweza kufikisha mbolea kwa wakati. Mbolea nyingi wananchi wanalalamika hazifiki kwa wakati. Ule msimu wanataka kulima, mbolea inakuwa haijafika, lakini tukitoa ruzuku kwa viwanda vyetu vya ndani kuanzia mwezi Julai wanaanza kusambaza hizo mbolea kwa wakulima wetu wa vijijini. Kwa hiyo itafika mahali mwezi Desemba mbolea zishawafikia wakulima. Tofauti na sasa, wakulima hawapati mbolea kwa muda muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine tutapata kodi kwa Serikali kwa sababu uzalishaji wa viwanda vyetu vya ndani utakuwa mkubwa na wakulima watakuwa na choices. Wataambiwa bei hii ya mbolea ya nje, lakini bei hii ni mbolea ya ndani ambayo tayari ina ruzuku. Kwa hiyo, nashauri hayo kwa Waziri ayachukulie kama chachu, lakini ayachukue kama atatengeneza ajira na atakuza uchumi. Kiwanda cha Dodoma mfano, wakiajiri watu 3,000 na uchumi wa Dodoma utabadilika na wananchi maisha yao yatabadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ukatili kwa wadada wa majumbani ambao wamekuwa wakisaidia familia nyingi majumbani maarufu kama house girl; ni muhimu kuweka mkazo na kutoa elimu kwa jamii hususani kwa familia ambazo zinawachukulia wadada wa kazi kama watumwa na kuwatumikisha kinyume na utaratibu na maelewano. Mambo kadhaa ambayo wanapitia na kuwa yanahitaji kuangaliwa kwa ukaribu ni kama ifuatavyo; kwanza ni mishahara yao ilipwe kwa wakati na kiwango kiwe elekezi ili kusaidia wadada wa majumbani wapate haki zao; pili muda wa ufanyaji kazi na kupata hata siku moja ya mapumziko tofauti na sasa kuna baadhi ya familia wanawafanyisha kazi siku saba za wiki na bila mapumziko.
Mheshimiwa Spika, ni vyema Maafisa Maendeleo ya Jamii wakawaelemisha wadada wa majumbani kuhusu haki zao za msingi na ni wapi wakaripoti endapo watapata kunyanyaswa na waajiri wao na hasa suala la ukatili kwa kutaka kulazimishwa na baba tendo la ndoa kwa madai asipokubali atafukuzwa kazi.
Mheshimiwa Spika, nashukuru na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana kwa nafasi hii uliyonipa na mimi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu sana ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee naomba nipongeze Wizara, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri lakini na wataalam wote katika Wizara hii kwa ajili ya jitahada zao wanazochukua kuhakikisha kwamba suala zima la utalii nchini kwetu linapewa kipaumbele, lakini pia kwa namna moja au nyingine wanajitahidi kutangaza na kuvutia watalii kuja wengi Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna vivutio vingi sana Tanzania ambavyo tumebarikiwa na Mungu, tuna Serengeti, Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na vingine vingi ambavyo siwezi kuvitaja kwa sababu ya muda, lakini tunavyo vivutio vingi ambavyo tumepewa na Mungu ila ni swali la kujiuliza ni kwa nini hatuna watalii wengi kama nchi nyingine pamoja na kuwa tuna vivutio vingi tulivyonavyo. Kwa hiyo, mimi nikaja na mambo mawili/matatu ambayo najua au nahisi yanasababisha tusipate watalii wengi, lakini pia yanasababisha hatujajitangaza vya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kipekee naomba nichukue nafasi hii kwa unyenyekevu mkubwa nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa video yake ile ya Royal Tour ambayo kwa kweli imeenda kuwa ni suluhisho katika Wizara hii ya utalii, lakini pia katika uchumi wa nchi yetu. Najua Mheshimiwa Rais alivua Urais akavaa uzalendo, uzalendo ndiyo uliotawala hatimaye akaamua kuwa kipaumbele na kutangaza utalii wa nchi yetu. Kwa hiyo, kwa unyenyekevu mkubwa naomba nimpongeze sana na naomba nimwambie kwamba hii mifano ni ya kuigwa kwa sisi wengine na kwa watumishi wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi inaeleza ifikapo mwaka 2025 tuwe na watalii milioni tano lakini mpaka sasa tuna takribani watalii 1,500,000 na tuna miaka mitatu kufikia Ilani yetu ya uchaguzi. Kwa hiyo, mimi naamini kwamba tukiweka njia Madhubuti na tukiwa na mikakati maalum tutafikia hii idadi ya watu milioni tano kama ilivyoandikwa kwenye ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Royal Tour ya mama imeleta mafanikio makubwa sana nchini kwetu na itaendelea kuleta, mojawapo ni kutangaza vivutio vilivyopo, lakini pia kuwasadia wawekezaji, kusaidia pato la Serikali, lakini kusaidia jamii kwa ujumla kama vile ajira nakadhalika. Kwa hiyo, jukumu langu kumpongeza mama lakini pia ni jukumu letu kumuunga mkono na sisi kuja vitu mbadala ambavyo vitasaidia kuunga juhudi zake mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fursa za uwekezaji pia zimefunguliwa kutokana na Royal Tour, ni kweli usiopingika wawekezaji watakuwa wameona fursa zilizopo Tanzania na angle gani waje wawekeze kwa kutumia Royal Tour ya Mama. Kwa hiyo kwa hayo tu machache mama aliyotufungulia sasa ni jukumu letu la kubeba ule uzalendo wa mama na sisi kama Wabunge kuishauri Serikali, lakini pia na Wizara kuchukua yale maono ya mama na kuyaweka kwenye uhalisia ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitajikita kwenye ushauri kwa Serikali kwa mambo mawili; ushauri wa kwanza ni njia za kisasa za utangazaji wa utalii, lakini wa pili utakuwa ni chombo cha ku-regulate standards na watoa huduma kwa ujumla. (Makofi)
Suala la kwanza, sasa hivi dunia iko kiganjani watu wanaita hivyo, kwa hiyo ni jukumu la Wizara au ni jukumu letu sisi sote ni kuhakikisha ni njia gani tunatangaza utalii na njia gani zinawafikia walengwa hasa tunaotaka kuwatangazia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imekuwa ikijitahidi kwa namna mbalimbali kwenda labda kwenye makongamano mbalimbali, lakini labda kutoa brochures tofauti tofauti, ila kwa dunia ya sasa hivi lazima tujiulize je, ni kweli hizi njia zinafanya kazi? Kwa sababu ni wangapi wanaosoma hizo brochures na hata kama Wizara wakienda kwenye maonesho wana banda la Tanzania labda vivutio vya Tanzania; je, ni kweli hilo banda linatembelewa na watu wengi? Kwa hiyo, utakuta hawapati idadi ya watu wa kutosha, lakini tukienda digital marketing inawafikia watu kwa haraka na kwa muda mfupi pasipo kutumia gharama kubwa sana kama sasa kusafiri sehemu mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefanya utafiti mdogo sana kwenye nchi jirani za Afrika, lakini na nchi za wenzetu zilizoendelea. Nimeona juzi juzi tu hapa siyo muda mrefu Kenya imeingia Mkataba na mtandao wa TikTok, TikTok ni mtandao wa vijana siyo vijana na watu wengi wanatumia kwa ajili ya ku-post vitu mbalimbali. Wametengeneza short videos ambazo zinaonesha utalii wao na hii yote ni njia ya ku-recover kutoka kwenye COVID-19 ambapo sekta yetu ya utalii iliyumba sana. Kwa hiyo, kama sekta iliyumba lazima tujifikirie ni namna gani mbadala za haraka haraka ambazo zitasababisha sisi tujitangaze kwa urahisi lakini tupate matokeo kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, digital marketing is the way forward kwa sababu hiyo ndiyo inakupa majibu ya haraka haraka. Hata kuna document moja ya World Bank wameandika digital platform na demand kwenye business ya utalii, hivi ni muhimu kwa sababu siku hizi watu wakiamka asubuhi anashika simu ya mkononi kwanza tofauti na zamani ilivyokuwa. Kwa hiyo, tukitumia digital platform ya kuwatangazia vivutio, tuwatangazie tunatoa vitu gani Tanzania wataweza kuja kuona kwa kutumia simu ya mikononi bila ya kuwa tumeenda kutangaza, tumeenda nchi hii na nchi hii. Kwa hiyo, mimi nashauri tujikite sana kwenye digital economy. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kuna nchi jirani ambazo huwa wanafanya vizuri kwenye utalii kama Morocco, wao walikuja na mkakati maalum baada ya COVID wakaja na mkakati maalum wa utangazaji wa utalii unaitwa Aji and We Are Open. Huo mkakati ulikuwa unalenga kuleta watalii tena baada ya COVID kuwapa awareness kwamba sasa tumefungua utalii wetu karibuni. Kwa hiyo, na sisi Tanzania tuje na different programu mbalimbali japo tunayo hii moja ya mama yetu mpendwa ya Royal Tour, lakini tuongeze na zingine kuonyesha kwamba sasa tumeshafungua utalii na sasa tuko tayari kupokea wageni waje kwa wingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine cha pili katika hiyo hiyo digital marketing tuna watu mbalimbali mashuhuri ambao wanafuatwa na watu mbalimbali na kwa wingi mkubwa wa mamilioni na wengine wana ma-followers wengi. Tukiainisha target market yetu kama tunataka nchi ya Urusi, tunataka wa Marekani, tunataka wa London, tunataka watu wapi, ni kiasi cha kutafuta mtu mashuhuri wa hiyo sehemu akaja kutangaza utalii. Aki-post kwenye platform zake sisi tunapata watalii, nakuhakikisha msanii aki-post au mtu mashuhuri hata ukiwa na viewers watu milioni tano, milioni 10 huwezi ukakosa watu milioni moja wa kuja kutembelea Tanzania. Kwa hiyo, ni wazo langu na rai yangu kwamba Serikali mtachukua hilo suala kwa ukubwa wake kama nchi za wenzetu walivyofanya na mpaka sasa namba yao ya utalii imeanza kuwa kubwa na kurejesha kutoka kwenye ile hali ilivyokuwa ya COVID-19.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la pili lilikuwa ni chombo cha ku-regulate standards za watoa huduma wetu na niungane na mchangiaji aliyepita, shida nyingi Tanzania kwanza zile punctuality, standards za watoa huduma wetu bado haziridhishi. Tunakuwa tunawatoa huduma ambao moja whether hawana mafunzo ya kutosha, mbili hawana uzoefu wa kutosha au walimu wao wanaowafundisha hawana enough skills za kuwapa hawa wanafunzi waka-compete au wakawa competent kwenye maeneo yao ya kazi.
Sasa mimi nikiangalia mfano wanasheria wana chombo chao kile Law School lakini wa leseni zao, watu wa NBAA wanatoa CPA; je, kama sisi tumeamua kujikita kwenye utalii na kama utalii huu ni muhimu kwa nini utisije na chombo chetu cha ku-regulate hawa watoa huduma, simaanishi hoteli hiyo tayari ipo. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Martha kwa mchango wako.
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)