MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kusimamia majukumu au shughuli za Serikali. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwenye nchi nyingi duniani kumekuwa na sera lakini sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ambayo inatoa nafasi kwa wahitimu wa vyuo mbalimbali kujitolea kufanya kazi Serikalini na kupewa posho kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye nchi yetu tunayo Taasisi ya Wakala wa Ajira wa Serikali (TaESA) ambayo inapeleka wahitimu wachache kwenye maeneo mbalimbali ya kazi na kule wanapewa posho kidogo, lakini walio wengi wanajiombea wenyewe, kwa baadhi waajiri wanawalipa lakini wengine hawalipwi kabisa. Je, Serikali haioni ni muhimu wa kuwa na sera, sheria, kanuni na miongozo kama hii ili wale wote ambao wanajitolea (wahitimu) waweze kulipwa posho? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba Jijini Dar es salaam, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwenye michakato ya ajira ambayo pia inasimamiwa na Wizara ya Kazi iliyoko Ofisi ya Waziri Mkuu. Tunatambua kuwa tunayo makundi yanayopata ajira rasmi na wale ambao hawajapata ajira lakini wanatamani na wanapenda kujitolea. Kitendo cha kujitolea kinamsaidia sana mwajiriwa, kwanza kuimarisha uelewa wa sekta anayojiajiri, ambayo pia anakwenda kujitolea lakini pia anapata uzoefu mkubwa sana na waajiri wanatusaidia kubainisha watu wenye weledi, uaminifu, uadilifu katika utumishi wa ajira hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kazi na Ajira iliyoko Ofisi ya Waziri Mkuu nayo inafanya kazi kwa karibu na Baraza la Ajira (LESCO), LESCO iko kwenye Wizara yetu. Baraza hili lina ratibu pia ajira za kujitolea kupitia Sheria zetu za Kazi na Ajira. Tunafanya kazi pamoja na chombo ulichokitaja Mheshimiwa cha TaESA ambacho chenyewe ni chombo ambacho kinaratibu hawa wote wanaokwenda kwenye ajira za kujitolea na wakisubiri fursa za kuajiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nafasi hizo kama nilivyosema, wanapata nafasi ile ya kuwa wanapata uzoefu wa ajira zao, wawe wanatambuliwa kwenye chombo kile na kinasimamia maslahi yao. Kinahamasisha waajiri wale ambao wamewapokea wanaokwenda kujitolea kupata motisha wanapotekeleza majukumu yao, ile inasaidia sana kwa sababu hata mwajiri huyu iwe ni sekta ya umma au sekta binafsi anapohitaji waajiriwa, kuajiri watu ambao wanataka kufanya kazi kwenye taasisi yake anaanza na wale ambao wanajitolea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sheria zetu zinaruhusu watu kujitolea kupitia chombo chao cha TaESA akiamua kujiunga na chombo kile anasimamiwa kwa maslahi yake na motisha kwa kujenga mawasiliano kati ya TaESA pamoja na mwajiri. Kwa hiyo, kuwepo usimamizi natambua kwamba wako wengine hawaja kitambua hiki na wanajitolea.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kupitia swali hili ni vyema sasa wale wote ambao wanajitolea kwenye sekta mbalimbali wakajua kwamba tunacho chombo kinaitwa TaESA ambacho wao wakijitambulisha na kujisajili watasimamiwa wao wanaojitolea pamoja na kile chombo kinafanya mazungumzo, kinamtambua pia mwajiri na kumhamasisha mwajiri kuona kuwa hawa wanapofanya kazi wanahitaji huduma zao kama vile chakula, mavazi na huduma nyingine muhimu kama afya. Kwa hiyo, mwajiri lazima atenge kidogo motisha kwa ajili ya kuwafanya hawa waweze kufanya kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, chombo tunacho na baraza tunalo na Wizara ya Kazi na Ajira ipo, iko Ofisi ya Waziri Mkuu. Jukumu lake moja ni kusimamia na kuhamasisha pia hawa ambao wamesoma kwenye ngazi fulani au wana ujuzi wa aina fulani pale ambapo wanasubiri ajira wanaweza kujitolea kwenye eneo ambalo ajira yake anaweza kuitumia vizuri na vyombo hivi vinafanya kazi ya kuungana na hawa waajiri kwa kuona motisha zao wakati wote wanapokuwa kazini, ahsante. (Makofi)