Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Issa Jumanne Mtemvu (67 total)

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa Mradi wa Maji Chunya unafanana na ule mradi wa 2F2B pale Tegeta A, ujazo wa lita milioni sita. Je, Wizara inaweza ikatuambia ni lini mradi ule utakamilika ili uweze kusaidia wananchi wote wa Goba?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ule mradi wa tanki Mshikamano kwa ajili ya wananchi wa Mpiji Magohe, Makabe yote na Msakuzi.

Je, ni lini pia mradi huo utakamilika ili wananchi wapate maji salama?

SPIKA: Swali sio lako, kwa hiyo unapaswa kuuliza swali moja tu, sasa chagua mojawapo katika hayo ya kwako.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Niweze kufahamu mradi unaotaka kujengwa mshikamano kwa ajili ya wananchi wa Mbezi, Makabe na Mpiji Magohe utakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Mtemvu kutoka Kibamba kama ifuatavyo:-.

Mheshimiwa Spika, Wizara sasa hivi inapitia miradi hii yote ambayo usanifu wake ulikamilika. Kwa hiyo nipende tu kumwambia Mheshimiwa Mbunge huo mradi upo katika miradi ambayo inakwenda kutekelezwa awamu hii kabla mwaka huu wa fedha haujaisha.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi huu wa Busanda unafanana sana na ule mradi uliopo Wilaya ya Ubungo, hasa mradi wa 2f2b, unaoanzia Changanyikeni, Chuo Kikuu mpaka Bagamoyo na hasa ujenzi wa tanki kubwa la lita milioni sita pale Tegeta A, Kata ya Goba. Je, mradi huu utakamilika lini ili wananchi wote wa Kata ya Goba wapate maji safi, salama na yenye kutosheleza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu kutoka Kibamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yote hii ambayo tayari utekelezaji wake unaendelea Wizara tunasimamia mikataba na namna ambavyo mkataba unamtaka yule mkandarasi kukamilisha mradi ule. Mheshimiwa Mbunge ninakupa uhakika kwamba tutasimamia kwa karibu na mradi ule utakamilika ndani ya muda ambao tumeupanga.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Jimbo la Kibamba ipo ahadi ambayo ndani ya Ilani ya miaka mitano mfululizo 2015/2020 na 2020/2025 ujenzi wa barabara ya Makabe – Msakuzi – Mpiji Majohe ikiungana na barabara ya Kibamba Njiapanda – Mpiji Majohe kwenda Bunju kupita Mabwepande. Lakini pia ikumbukwe barabara hii pia ni ahadi ya mwisho kabisa ya Mheshimiwa Hayati Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakiri kwamba ni kati ya ahadi za mwisho kabisa za Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Nadhani aliitoa wakati yuko kwenye ile stand na bahati nzuri nilikuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi ikishakuwa na Mheshimiwa Rais ni utekelezaji. Lakini atakubaliana nami kwamba ahadi aliyotoa isingekuwa rahisi kwamba tumeanza kuitekeleza, lakini ahadi ambayo tunaizingatia na tayari shughuli zimeshaanza kuona namna ya kuanza kutekeleza ile ahadi. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi kama zile zikishatolewa, kinachofuata ni utekelezaji na mimi nimhakikishie kwamba Serikali kupitia Wizara yangu hiyo ahadi tutaitekeleza. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali ya kuridhisha kwa kiasi, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamekuwa na watumishi wengi ambao wamekaa muda mrefu, zaidi ya miaka kumi hadi ishirini wakiwa wanalilia suala la muundo huu ambapo umetoka Waraka Na.3 wa Mwaka 2015 bila kutekelezwa kwa wakati. Serikali ina mpango gani wa kupandisha vyeo vyao kwa mserereko ili kuzingatia muda waliotumia kazini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, suala la hadhi ya Kitengo cha Uhasibu, ni kweli Serikali inajibu juu ya vigezo ambavyo vinafanyiwa tathmini mara kwa mara na Ofisi ya Rais, Utumishi. Natambua vigezo vyenyewe vinazingatia job analysis na job design. Kwa msingi huo, ni ukweli kada hii imeacha kutumia local standards kwa muda mrefu sana na sasa wanatumia international standards katika kutengeneza mizania mbalimbali ya taasisi. Vilevile hata ripoti za CAG tunaziona jinsi gani zinavyotoka tayari kila mmoja anahamaki juu ya kuiona hadhi ya taasisi inabebwa na sehemu au kitengo hiki. Tunao mfano, juzi tu taarifa ya CAG baada ya kuitoa tayari viongozi wa Serikali wametoa maelekezo magumu kwa section hii, yaani Wakuu wa Idara au Vitengo hivi.

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho hadhi hii inategemea kazi kubwa wanayoifanya. Tayari uchumi na mipango wana hadhi ya Kurugenzi…

SPIKA: Mimi nilifikiri swali huwa linakuwa ni swali.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ni swali, natengeneza hoja ya kuuliza swali la mwisho hili.

SPIKA: Hapana, unahutubia Mheshimiwa.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, basi kwa misingi hiyo miwili sasa Serikali haioni ni muda mwafaka wakifanya analysis yao wa kukipa hadhi Kitengo hiki cha Uhasibu na Idara ya Ukaguzi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza; kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mtemvu kwa kuwatetea watumishi hawa, lakini nimjulishe kwamba ni dhamira ya Serkali na Serikali imekuwa ikifanya hivyo kila mwaka kuhakikisha kwamba inapandisha vyeo na hadhi za wafanyakazi na watumishi wake ambao wanafanya kazi vizuri. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba hao Wakaguzi wa Hesabu, Wahasibu pamoja na Wasaidizi wao watapandishwa vyeo pale ambapo hali ya bajeti itaruhusu lakini kwa kuzingatia vigezo ambavyo vimewekwa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusiana na vigezo hivyo, kama ambavyo nimejibu katika swali lake la msingi ni kwamba utaratibu huu ambao umewekwa upo kwa mujibu wa Sheria ile ya Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi ambayo ndiyo imesababisha kutayarishwa Waraka huu Na.3. Kwa kuzingatia sheria hiyo na Waraka ule, ndiyo utaratibu huohuo ambao utaendelea kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa changamoto zilizopo ndani ya Jimbo la Kinondoni kuhusiana na Mto Msimbazi ni sawa kabisa na changamoto zilizopo katika Mto Mbezi na Mto Mpiji ndani ya Jimbo la Kibamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ni lini sasa itaanza kutengeneza kingo za mto Mbezi ili kuokoa taasisi za Serikali mashule lakini vile vile na nyumba za wananchi, kuondolewa na maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kwa juhudi yake ya kupitia na kufanya mambo yaliyomengi ndani ya Jimbo la Kibamba. Kwa hakika Serikali ipo tayari kufanya tathimini ama inafanya tathmini juu ya jambo hilo mara tu mwaka wa fedha tutakapopata idhini ya fedha za kutosha basi tutapita ndani ya Jimbo hilo na kutatua changamoto ambazo zinazikabili Jimbo la Kibamba.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa, ndani ya Jimbo la Kibamba ipo barabara ya Temboni – Msingwa kwenda Kinyerezi ina changamoto kubwa sana kwa muda mrefu. Je, mchakato unaoendelea kupata mkandarasi ni lini utakamilika na barabara hiyo kuanza kujengwa chini ya TARURA?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Issa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameainisha kwamba, barabara ya Temboni – Msimbwa kwenda Kinyerezi imeharibika na anataka kujua lini barabara hii itaanza kujengwa. Nimwambie tu kwamba, mchakato unaendelea na mchakato utakapokamilika kama ambavyo yeye ameainisha, tutakapomaliza huu mchakato hii barabara itaanza kujengwa mara moja kwa sababu, tumeshaitenga katika bajeti. Ahsante sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu yaliyotolewa na Serikali yanayoridhisha kwa wastani, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, majibu ya Serikali yanaeleza wazi juu ya utoaji wa hati 845 tu kati ya upimaji uliokamilika wa watu 100,041 asilimia 0.0056 katika kipindi chote cha miaka miwili. Je, Serikali haioni sasa ni muda sahihi wa kupunguza lile tatizo la premium ambalo linasababisha bei kubwa kwa wananchi ambao wanashindwa zaidi ya ile 180,000 ambayo wamelipa kwa wale wa kampuni? Sasa hapa ni kupunguza ile premium.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni kweli kwenye majibu ya msingi inasema wachangiaji ni 30,000, lakini kwa taarifa nilizonazo kama Mbunge ni zaidi ya wachangiaji 80,000. Kwa hiyo, jumla ya fedha ni bilioni nne wanazisema, mimi nasema bilioni 15. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kupeleka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ili akafanye ukaguzi maalum tuje na takwimu zilizo sahihi kwa ajili ya fedha za wananchi zilizopotea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali yake mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtemvu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimsahihishe, si kweli kwamba, hati 847 tu ndio zimeandaliwa. Kwenye jibu langu la msingi nimesema hati 1,754 kati ya waombaji 1,925 tayari zimeandaliwa na wamechukua, lakini tunaendelea kuandaa hati kwa sababu, viwanja vilivyokamilika ni 8,316 kwa hiyo sio 845 kama alivyosema.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia amezungumzia suala la kupunguza premium kwamba, pengine wananchi wanashindwa kuchangia. Naomba tukumbuke tu kwamba, premium hii awali ilikuwa ni 15% kwa viwanja vyote. Ikapungua ikawa 7.5%, lakini badaye Wizara ikapunguza zaidi kwenye zoezi la urasimishaji wanalipa 1% ya premium ambayo wanatakiwa kulipa tofauti na ule upangaji wa kawaida, ilitoka 7.5% wao wanalipa 2.5%. Kwa hiyo, kama ni suala la kupunguza ni kweli upunguzaji tumepunguza, lakini kwa sababu ni hoja inatolewa na Serikali ni sikivu basi tutaona namna kama kuna haja ya kupunguza tena au tuendelee na ileile 1%. Tukumbuke kodi hizi pia ndio zinarudi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili amezungumzia kwamba, pesa ambazo zimekusanywa tulizotoa takwimu hapa ni tofauti. Si kweli anachosema, kwa mitaa mitano haiwezi kukusanya bilioni 15 kwa zoezi la urasimishaji, ukizingatia kwanza walipaji wenyewe ni wachache na nimetaja kati ya waombaji 147,000 tunaoshughulika nao sasa hivi ni 1,925 tu ambao wamekamilisha malipo yote. Kwa hiyo, si kweli kwamba, kuna pesa nyingi ambazo zipo,

Mheshimiwa Naibu Spika, kama pengine Mheshimiwa Mbunge anajua kuna mahali ambapo kuna pesa zimekusanywa na pengine hazijulikani zilipo, ameomba ukaguzi ufanyike, tutalifanyia kazi ili tuweze kujua ukweli wa Mheshimiwa Mbunge aliouleta na takwimu tulizonazo Wizarani ili tuweze kuwa na uhakika na alichokisema. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; kwa kuwa Jimbo la Kibamba sasa changamoto yake kubwa ni usambazaji wa mabomba tu katika maeneo mbalimbali. Je, Serikali sasa iko tayari kutoa kauli au maelekezo ya utoaji wa mabomba yale ili wananchi wa maeneo mengi wapate maji safi na salama?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kidhati ya moyo nikupongeze sana kaka yangu Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu Mtemvu. Moja katika bajeti yako umeonesha masikitiko yako eneo ambalo halina maji na tumekwishakubaliana na commitment yangu mimi baada ya Bunge tunakwenda Kibamba tunakwenda kumaliza kabisa tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na tumeshatoa maelekezo mahususi kwa DAWASA, wamefanikiwa maeneo mengi sana, walipe kipaumbele Jimbo la Kibamba katika kuhakikisha kwamba, tunaenda kumaliza kabisa tatizo la maji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwa kuwa ipo barabara ambayo ilitolewa ahadi na hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, barabara ya Kibamba – Mpiji – Mabwepande na tayari bajeti ya Wizara hii imepita.

Sasa nataka kauli ya Serikali juu ya bajeti husika juu ya barabara hii; ni nini kimefanyika juu ya utengenzaji wa barabara hii katika mwaka huu ikitegemea Hayati alisema wapelekewe kwa udharura?
NAIBU WAZIRI, UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba bajeti yetu imepitishwa tarehe 27 na 28 Mei, 2021 hapa Bungeni tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kupitisha bajeti yetu. Tunaomba tuwahakikishie kwamba ahadi zote za viongozi wakuu, Mheshimiwa Rais Hayati Magufuli, Mama Samia aliyepo madarakani sasa, Mheshimiwa Waziri Mkuu na ambazo zimetajwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi zitatekelezwa. Tupeane muda tu. Mheshimiwa Mbunge, tutapitia kwa haraka haraka tuweze kujua ni barabara gani zimetajwa, zipo nyingi nchi nzima. Siwezi kukudanganya hapa lakini tukipitia kama ipo na fedha yake imetengwa tutaisimamia na kazi itafanyika na bahati nzuri tumepanga kwamba eneo hilo tutoe malalamiko mkoa wa Dar es Salaam, tumewekeza fedha za kutosha kuboresha barabara ili uchumi wa Tanzania uendelee kuku ana fedha hizo zifanye kazi za kujenga uchumi wa Watanzania kutoa huduma za kijamii. Ahsante sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Swali la kwanza; kwa kuwa majibu ya Serikali yanathibitisha kuwepo kwa watumishi 332 kukaimu wakiwa na sifa lakini zaidi ya watumishi 1,164 wanakaimu bila sifa yaani hawana kibali cha Katibu Mkuu Utumishi. Sasa na ni ukweli kuwepo kwa viongozi wengi wanaokaimu kunazorotesha utendaji kazi na hivyo kutofikia malengo tarajiwa. Je, ni ipi sasa commitment ya Serikali kuwathibitisha au kuwaondoa watumishi wenye kukaimu zaidi ya miezi sita? (Makofi)

Swali la pili; kwa kuwa mchakato wa uteuzi unachukua muda mrefu sana hata zaidi ya miaka kumi na mfano upo, Katibu Tawala Msaidizi upande wa uchumi na uzalishaji Mkoa wa Kilimanjaro Ofisi ya Mkuu wa Mkoa anakaimu mwaka wa tisa toka 2012. Je, Serikali ipo tayari kutengeneza kanzidata au database ya wale watumishi waliofanyiwa vetting wengi kwa ujumla wao ili waweze kusaidia kupunguza muda ule wa watumishi kukaimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Mtemvu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la kwanza tumekuta kuna changamoto kubwa sana ya waajiri kukaimisha watu wasiokuwa na sifa bila ya kupata kibali kutoka kwa Katibu Mkuu Utumishi kama mwongozo unavyotaka, matokeo yake mtu anakaa kwenye nafasi muda mrefu anakuwa hafanyiwi upekuzi na hivyo kufanya mtu kukaa kwenye nafasi hiyo kwa miaka mingi. Sasa tayari tulishawaagiza waajiri wote mapema mwaka huu kuleta majina yote ya watu wanaokamimu nafasi zao kwa zaidi ya miaka mitatu ili tuweze kupitia na kuangalia ni wapi wenye sifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba tayari tumegundua kuna watumishi 1,164 wasiokuwa na sifa na tunazidi kuwaomba waajiri waweze kuhakikisha wanakaimisha watu wenye sifa lakini vilevile kwa kibali cha Katibu Mkuu Utumishi. Waache kukaimisha kwa sababu anamtaka fulani au fulani mimi naweza nikafanya nae kazi na kumburuza, bali wakaimishe mtu kwa sababu ndie anayetakiwa kuwepo kwenye nafasi hiyo na hiyo itasaidia sana katika upekuzi na kuweza kuwathibitisha watumishi ndani ya miezi sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili la nyongeza Mheshimiwa ameuliza kama tuna kanzidata, sasa tayari tumeshaanza kukusanya taarifa na tumeshapeleka majina zaidi ya 2,300 kwa ajili ya upekuzi ili yawepo na wiki hii tunapeleka tena majina 2,400 kwa ajili ya upekuzi ili tuweze kuwa tuna watu katika kanzidata yetu wenye sifa. Tunapoona mwajiri amekuweka mtu asiye na sifa, Utumishi tutam-post moja kwa moja mwenye sifa ili akashike nafasi hiyo na aweze kuifanya kwa weledi na kuweza kufanya maamuzi. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Wabunge na watumishi wote wale wenye sifa muda si mrefu mtaanza kuwaona na tatizo hili la kukaimu litaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.

(a) Kwa kuwa majibu mazuri yametolewa na Serikali, kwa umuhimu barabara hizi pamoja na kuondoa msongamano sehemu ya pembezoni mwa Mkoa wa Dar es Salaam lakini pia zinasaidia kufungua uchumi wa wananchi wa pembezoni. Aidha, barabara hizi zilipata baraka za Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na kuzitamani zijengwe kwa haraka na udharura. (Makofi)

Je, Serikali sasa haioni inayo kila sababu kukamilisha barabara hizi katika mwaka wa fedha 2022/2023? (Makofi)

(b) Kwa kuwa kilomita zilizotajwa 33.7 ina sehemu ya kilometa 1 ya barabara ya njiapanda ya shule na wanahitaji fidia. Je, Serikali imejipanga vipi kulipa fidia wananchi hawa? (Makofi)
MHE. NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu Mbunge wa Kibamba kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika ni kweli kwamba Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyekuwa Rais aliahidi kwamba, barabara za Jimbo la Kibamba angetamani zijengwe zote kwa kiwango cha lami. Nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi za viongozi wa Kitaifa, zote tunazichukulia kwa umuhimu mkubwa sana na ndio maana hata akienda kwenye kitabu chetu cha bajeti, tumetenga tayari fedha, kwa ajili ya kuanza upembuzi kwa sababu, barabara zote zilizotajwa katika Jimbo lake ni za vumbi. Kwa hiyo, lazima hatuwezi tukaruka hatua ni lazima tutafanya upembuzi yakinifu na usanifu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awe na uhakika kwamba tunatambua pia tutafungua uchumi wa Jimbo lakini pia kurahisisha mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa kawaida barabara zote zinapojengwa tutahakikisha kwamba hiyo fidia aliyoitaja, tunailipa kabla ya ujenzi na kama kuna changamoto zaidi ya hii ambayo tunafahamu ya kuilipa kwa kawaida, basi nimuombe Mheshimiwa Mbunge tuweze kuonana naye kwa ajili ya kupata maelezo zaidi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Jiji la Dar es Salaam lina idadi kubwa ya watu zaidi ya milioni sita na tunategemea Chuo cha VETA kimoja tu maarufu cha Chang’ombe na Wilaya ya Ubungo sasa ipo pembezoni na idadi kubwa ya watu na eneo tunalo: -

Je, ni lini sasa Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Ubungo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kutoa jibu dogo kwa Mheshimiwa Mtemvu Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye maeneo mengine, nitoe rai na wito kwa Mheshimiwa Mtemvu, kwa sababu Ubungo ni Jiji na ni eneo kubwa na mapato yake ni makubwa, kwa hiyo, aone umuhimu nalo wa jambo hili. Basi angalau kwenye mapato ya ndani pale kama wanaweza wakatoa kasma kidogo wakaanza mchakato huu wa ujenzi, pindi pale Serikali itakapopata fedha kwa ajili ya vyuo hivi vya wilaya, basi tutakwenda kuongezea nguvu na kukamilisha chuo hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri naona Wabunge wengi wanauliza vyuo vya VETA huko kwenye maeneo yao, hebu tuambia kwa ujumla mpango wa Serikali kuhusu ujenzi wa vyuo vya VETA. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mpango uliokuwepo hivi sasa kwa mwaka huu wa fedha, bado tunaendelea na ukamilishaji wa vyuo vile 29 na vile vile kununua vifaa. Kwa sababu lengo letu ni kuhakikisha vyuo hivi siyo tunajenga tu majengo, bali vile vile kuhakikisha kwamba tunapeleka pamoja na vifaa ili viweze kufanya kazi na kutoa elimu kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika mwaka ujao wa fedha, jukumu la Serikali ni kuhakikisha kwamba sasa tunaweza kutenga bajeti kwa ajili ya awamu ya pili ya ujenzi wa vyuo vingine vya wilaya. Huo ndiyo mpango uliopo mpaka hivi sasa. Ahsante sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, wananchi wengi wa maeneo ya pembezoni katika Jimbo la Kibamba, hasa maeneo ya Mpijimagohe kule Mbezi, Tegeta A kule Goba na maeneo ya Ukombozi kule Saranga, wameanza kujenga maboma ya vituo vya polisi kwa ajili ya usalama wa maeneo yao. Je, Serikali ni lini sasa itakuwa tayari kukamilisha maboma yale ili wananchi wale wapate usalama katika maeneo wanayoishi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu tena swali la Mheshimiwa Mtemvu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mambo yote ambayo yanaelezwa au vitu vyote ambavyo vinahitajika kwa ajili ya kufanyiwa wananchi kutoka katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, hasa kwenye Jeshi la Polisi, ni mambo ambayo yanahitaji fedha. Tukizungumza vituo vya polisi, fedha, tukizungumza magari, fedha, tukizungumza nyumba za askari, tunahitaji fedha. Nimwambie tu mheshimkiwa Mbunge kwamba, kwa sasa tunakwenda kutafuta fedha na tumeshaanza hiyo michakato ya utafutaji wa hizo pesa. Lengo na madhumuni ya kufanya hivyo ni ili tuweze kumaliza maboma yote nchini ambayo yanahitaji kumalizwa kuwawezesha wananchi kupata huduma za ulinzi na usalama. Nakushukuru.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona ili niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa katika majibu yaliyotolewa ya swali la msingi imeonekana changamoto kubwa ni ufinyu wa bajeti kwa mwaka hadi mwaka, pamoja na ongezeko la bajeti tuliyoelezwa, lakini ni ukweli kwamba, wanafunzi wenye sifa wanakuwa wengi na wale wanaokosa nafasi katika mwaka husika wengine wamekuwa wana kiu ya kuendelea na wananchi wamekuwa wakiwasaidia au jamii wanayoishi, sasa wakienda mwaka wa pili na watatu wanaendelea kukosa. Je, Serikali haioni inayo kila sababu sasa katika miaka inayofuatia wale wanafunzi waliosaidiwa katika njia mbalimbali wawaingize katika mwaka wa pili kabla hawajaendelea kuwachukua wengine?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba, utaratibu huo upo. Sio kwamba, ukikosa mkopo katika mwaka wa kwanza basi unakuwa hu-qualify kwenye mwaka wa pili, provided ulikuwa umeomba katika ule mwaka wa kwanza. Unachofanya katika ule mwaka wa pili, unakuwa wewe sio mwombaji mpya, unakuwa uko katika dirisha la rufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaratibu huo upo Mheshimiwa Mbunge na tumekuwa tukiufanya na wanafunzi hao wamekuwa wakiwa-absorbed wakati wako mwaka wa pili ikiwa mwaka wa kwanza amekosa au mwaka wa tatu, hali ya mwaka wa kwanza na wa pili akiwa amekosa. Kwa hiyo, nikutoe wasiwasi na jambo hili tutaendelea nalo na ndivyo lilivyo.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Wizara hii tayari inaona ina changamoto sana ya kupata fedha kwa ajili ya kundi hili la wazee, lakini bado wazee hawa wana changamoto sana ya uwezo.

Je, Wizara ya ina mkakati gani sasa wa kutumia ile sera ya asilimia 10 kuweza kuwaweka na wazee kupata kama asilimia mbili ili ziwasaidie?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Issa Mtemvu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Issa tunakuomba kwamba sheria bado zinafanya kazi na zitakapokamilika basi wazee hawa watapewa haki zao na watapewa msaada wa kuongezewa kiasi cha fedha kwa ajili ya mahitaji ya maisha yao. (Makofi)

MHE ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.

Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini ukweli mwenye dhamana ya kutafsiri sheria ni Mahakama na kumekuwepo na kesi ya ardhi chini ya Jaji Bongoyo ya mwaka 2005 ikahukumiwa mwaka 2013. Kesi ya Prochesta Lyimo na wenzake 72 dhidi ya AG na Wizara ya Ujenzi. Katika dhamana hiyo wadai walihalalishwa kwamba eneo ni la kwao na kama Serikali inalihitaji inatakiwa illipe fidia. Swali langu la kwanza, je, ni lini Serikali itatekeleza hukumu hii ya Mahakama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, Sheria ya Barabara ya mwaka 1932, Kanuni ya Mwaka 1955 na marekebisho Na. 13 mwaka 2009 inakinzana sana na Sheria nyingine za Mipangomiji na Sheria ya Vijiji ya mwaka 1999 ambayo ilifuta mikataba mingine na sheria nyingine zote zilizotangulia kwa kuweza kuwamilikisha watu ardhi ikiwa ilienda sambamba na zoezi la Operesheni Vijiji ya Mwaka 1974 na 1975 iliyoleta watu pembezoni mwa barabara kubwa na kuwapa miundombinu ya maji na elimu na kadhalika. Je, ni ipi kauli ya Serikali katika mchangamano huu au mchanganyiko wa sheria hizi ya barabara ya mwaka 1932 na hizi nyingine za ardhi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kiamba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge wa Kibamba, kwanza nimshukuru na kumpongeza kwa jinsi ambavyo amekuwa akilifuatilia suala hili kila wakati ili kuhakikisha tu wananchi wake hawa wanapata hicho ambacho anawapigania. Naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inaongozwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria iliyopo. Moja ya wajibu wa Serikali ni kulinda wananchi pamoja na mali zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi aliyoisema ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ipo kwa Wakili Mkuu wa Serikali ambae yupo chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Hatua waliyochukua wananchi hawa kupeleka suala hili kwenye vyombo vya kisheria, naomba nimhakikishie kwamba sheria itakapotamka mara ya mwisho nadhani haki itatolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusu sheria kukinzana naomba tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara tunatumia Sheria yetu ya Barabara, lakini suala la kukinzana kwa sheria nadhani Serikali imelichukua na itaenda kuangalia sheria mbalimbali zinavyokinzana ili ziweze kusomeka na kueleweka kwa pamoja. Ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, majibu yanatuonesha kwamba yapo malalamiko mengi sana ya fedha hizi takribani shilingi bilioni 60 ambazo zinarudi kila mwaka zinapatikana kutokea kwenye fungu hili la 10% na mifano imeoneshwa; Dar es Salaam kwenye Wilaya mojawapo tayari kuna ubadhirifu mkubwa sana wa fedha hizi: -

Je, Serikali haioni ni wakati sasa wa kupeleka ukaguzi maalum kwa nchi nzima ili tupate tathmini ya kweli? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya maeneo nchini kote kuhusiana na matumizi ya fedha za 10% na Serikali kama ambavyo Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Bashungwa ametoa maelezo mwanzoni, ni kwamba tunafanya tathmini ya kuona wapi kuna mafanikio, maeneo gani yana changamoto, na changamoto ni zipi; ili sasa baada ya tathmini hiyo, tuwe na direction ambayo itatuwezesha kuwa na fedha ambazo zinaleta tija kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kutakuwa na sababu ya kutazama uwezekano wa kufanya ukaguzi maalum tutalifanya kwa sababu kazi ya Serikali ni kudhibiti fedha hizo ili ziweze kuleta tija kwa watarajiwa. Kwa hiyo, tumelichukua wazo hilo na tutaendelea kulifanyia kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Imekuwepo Barabara ya Makondeko – Kwembe – Kisokwa ambayo imekuwa ndani ya bajeti katika kipindi cha miaka miwili mfululizo, 2021/2022 na 2022/2023. Je, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mtemvu na atakubaliana nami kwamba tumefika kwenye jimbo lake. Barabara hii ni kati ya zile barabara ambazo zinapunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam na ipo katika mpango wa kuanza kuijenga kwa awamu hiyo barabara kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa ni ukweli pamekuwa na migogoro mingi sana kwenye Jimbo la Kibamba kuhusiana na kutokamilika kwa urasimishaji, sasa je, Serikali ina mkakati gani kumaliza kabisa migogoro hii inayohusiana na urasilimishaji kwenye Jimbo la Kimbamba?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mtemvu kwamba kama ambavyo nimeeleza katika swali la msingi kutoka kwa Mbunge Kunambi, hatua hizo ambazo zimechukuliwa kule Mlimba ndiyo ambazo pia zinaendelea kuchukuliwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kama nilivyoeleza; kuendelea kutoa elimu na kuendelea kuhakikisha Halmashauri zetu zinaendelea kusimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi ikiwemo mipango iliyowekwa na kushirikisha wananchi katika kuweka taratibu za ardhi katika maeneo yao.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.

Kwa kuwa, ripoti ya sensa ya sasa ya mwaka 2022 imeonesha wazi kwamba ongezeko la watu ni zaidi ya Milioni 16 katika kipindi cha miaka Kumi, hii imeshabihiana sana na wananchi wengi wasio na ardhi kuvamia mapori yasiyo endelezwa kwa miaka mingi.

Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kufanya tathmini upya ili yale maeneo ambayo hayajaendelezwa na wananchi wako mle wamejenga waweze kurasimishwa rasmi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwangu mimi na upande wa Serikali ninaamini ushauri uliotolewa na Mheshimiwa Mtemvu Mbunge ni jambo nzuri na ni jambo la kufanyiakazi nasi ndani ya Wizara nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tumekwishapokea taarifa ile ya sensa na ndani yake yako mambo mengi sana ikiwemo kuangalia jinsi gani Serikali sasa inaenda kuondokana na maeneo ambayo hayajapangwa vizuri lakini pia kurasimisha maeneo ambayo yameiva kwa ajili ya urasimishaji.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu ya jumla ya Serikali kwenye changamoto hii kwamba imeandaa mwongozo wa usafishaji mchanga, kutoa tope na taka ngumu. Hili ni jukumu ambalo halmashauri yetu ya Manispaa ya Ubungo imeshafanya sana, lakini madhara ni makubwa sana kwenye mto ule, unazidi kupanuka na kuvunja shule na taasisi za Serikali pamoja na makazi ya watu.

Mheshimiwa Spika, inawezekana changamoto hii inahitaji Wizara ya kisekta ingejibu. Naomba niruhusu niulize maswali mawili ya nyongeza, swali la kwanza; je, Serikali itakuwa tayari kujenga kingo imara kwenye Mto wote huo wa Mbezi ili madhara haya yaweze kuondoka?

Mheshimiwa Spika, je, Mheshimiwa Waziri husika atakuwa tayari kwenda nami jimboni ili tuutembelee mto na aone madhara ambayo yametokea kwa wananchi na yatakayotokea kwenye siku zijazo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja ya miongoni mwa jukumu letu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ni kuhakikisha kwamba tunazingatia na tunashughulikia masuala ya vyanzo vya maji ili visiathiriwe na visiathiri wananchi. Niko tayari kufuatana na yeye kwenda kutembea katika Mto Mbezi kuona changamoto hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake lingine, Ofisi ya Makamu wa Rais, Serikali tuko tayari kuhakikisha kwamba tunajenga huo mradi wa ukuta ambao utatenganisha ili sasa maji yasiweze kuingia huko yakaleta mafuriko. Ila namwomba Mheshimiwa Mbunge yeye kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, kwanza wafanye tathmini ya ujenzi huo, lakini kingine waandike halafu watuletee Ofisi ya Makamu wa Rais ili tuone namna ambavyo tunaweza tukapata fedha kwa ajili ya kuandaa mradi huo. Nakushukuru.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nimesikia majibu ya Serikali ni mazuri na yanaleta moyo katika kupunguza changamoto ya upungufu wa Wahadhiri na hasa Wahadhiri Wabobezi katika Vyuo Vikuu vyetu. Pamekuwa na tafiti chini ya Chama cha Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (THTU) kwamba kuna upungufu mkubwa sana; utafiti wa 2017, lakini sababu kubwa waliyotoa ni Serikali kutumia sana wataalamu wao katika kujaza nafasi mbalimbali Serikalini: -

Je, Serikali haioni sasa ni wakati mzuri wa kushauri mamlaka za uteuzi kuacha kutumia wataalam hawa, hasa Wahadhiri Wabobezi katika nafasi mbalimbali Serikalini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Mbunge ametoa wazo na Mamlaka za Uteuzi zipo, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuichukue hoja yake hii ili tuweze kuifikisha kwenye vyombo hivi vya uteuzi ili waweze kufanya evaluation au tathmini toshelezi kabisa iwapo kama wanaona inafaa kufanya hivyo, basi liweze kufanyiwa kazi. Nakushukuru sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona niulize swali la nyongeza. Pamoja na nia njema ya Serikali kupeleka miradi ya barabara za lami kwenye Jimbo la Kibamba hata hivyo pamekuwa na sintofahamu ya miradi hiyo kutobeba components za fidia zaidi ya migogoro na wananchi. Je, Serikali inasema nini juu ya jambo hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE: Mheshimiwa Spika, naomba nimwombe Mheshimiwa Issa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, aweze kuwasilisha swali kama swali kwa maana ya masuala ya fidia. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona, niulize swali dogo moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Jimbo la Kibamba maeneo ya King’azi A, B na maeneo ya Manzese Malamba Mawili ni maeneo ambayo wananchi wanaendelea kukosa maji safi na salama kwa kutumia maji ya chumvi ya visima vifupi; na ahadi ya Serikali ni kujenga tenki kubwa la ujazo siyo chini ya lita milioni kumi pale Kilimahewa: Je, ni lini sasa Serikali itaanza kutekeleza mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tenki lipo kwenye hatua za mwisho kabisa kuja kuanza kutekelezwa, usanifu umekamilika. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa shughuli zote zilizotajwa ambazo zimeanza kufanyika ndani ya Pori la Akiba la Mabwepande, tayari wananchi wengi hawajui na hata wananchi wa Jimbo la Kibamba pia hawajui;

(a) Je, Serikali ipo tayari kufungua geti upande wa Jimbo la Kibamba ili wananchi wengi sana waweze kushiriki kwenye shughuli zilizotajwa kwenye jibu la msingi?

(b) Kwa kuwa katika kila uwekezaji tunategemea mapato na seerikali imejibu hapa imeshatumia shilingi 710,789,122. Je, ni yapi makadirio ya mapato katika mwaka 2022/2023?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Mtemvu Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, pori hili la Mabwepande ni pori ambalo limepekena na Mikoa jirani ikiwemo Pwani na pori hili lipo katikati ya Dar es salaam, kwa sasa tumeshaanza kufanya hamasa mbalimbali na kwa kuwa mwanzoni tulikuwa hatuna miundombinu tumeweza sasa kuwekeza na sasa hivi tuna miundombinu ya kutosha na hivyo watalii wameshaanza kuingia na matamasha mbalimbali yameshaanza kufanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaanza pia kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha wananchi, pia tunatumia televisioni matamasha mbalimbali kama ambavyo nimeyataja ikiwemo nyama choma festival hii yote ni kuwafanya wana Dar es salaam wawe na maeneo maalum ya kupumzika ikiwemo kulala ambapo tumeshaandaa maeneo ya camp site kwa ajili ya wananchi kulala.

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuhamasisha Watanzania wote unapofika Dar es Salaam basi tembelea Pori la Pande utapata huduma zote za kiutalii na utaweza kuwa umepumzika kama vile upo Serengeti National Park.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa mapato tangu tulipowekeza katika pori hili kwa sasa tumesha kusanya jumla ya shilingi milioni 4.9 na kwa kuwa uwekezaji ni endelevu tunaendelea kuwekeza ili kuhakikisha kwamba eneo hili linakuwa ni kivutio kikubwa katika mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri na ya kuridhisha ya Serikali ningeomba kuuliza haya maswali mawili. Moja, stendi yetu ya Magufuli inaruhusu kuingiza mabasi yote yanayotoka mikoani bila kwenda kokote na kushusha pale abiria, lakini pamekuwepo bado na mabasi mengi kwenda Urafiki na maeneo ya pale kwa Wachina na Maghorofani. Pamoja na maelekezo mengi yanayotolewa na viongozi wa mkoa na wilaya. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya kushindwa kwa muda mrefu kusimamia maelekezo yake?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni ukweli stendi ile pamoja inaenda kukamilika kwa wachache walioingia kupitia mnada wanalipa square mita au mita za mraba Sh.40,000 tofauti na maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam ikiwepo hata maeneo ya pale Mlimani City, kati ya shilingi 15,000 hadi shilingi 25,000, lakini hawa wanalipa shilingi 40,000.

Je, Serikali haioni sasa ni sababu ya kupunguza kufikia hiyo kati ya shilingi 15,000 hadi shilingi 25,000 ili matumizi yaende kama yalivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mtemvu kwa kazi kubwa anayoifanya kuwasemea wananchi wa Jimbo la Kibamba na nimwakikishie Serikali itaendelea kumpa ushirikiano ili aweze kutekeleza miradi mbalimbali ya wananchi wa Kibamba. Kuhusu mabasi ambayo hayaingii kwenye stendi ya Magufuli, ni kweli kumekuwa na baadhi ya makampuni ambayo hayatumii ipasavyo stendi kadri ya maelekezo na malengo ya ujenzi wa stendi ile. Kwa hivyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunalichukua hili tunalifanyia kazi na tutatoa maelekezo mahususi kuhusiana na utaratibu wa mabasi kutumia stendi ile ya Magufuli.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na gharama ya upangishaji kwa square mita kufika hadi Sh.40,000 mapendekezo yake ni Sh.15,000 hadi Sh.25,000 naomba niseme tunalichukua hilo kama Serikali tutalitazama na tuweze kuona mazingira kama yanaruhusu basi tuweze ku- review bei hizo ili wananchi wapate unafuu katika upangishaji.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa ndani ya Jimbo la Kibamba kuna Mto Mbezi na Mto Mpiji ambao kwa muda mrefu wananchi wamedhurika sana na mafuriko, nyumba zao lakini pia na taasisi kama shule zimekuwa zikiondoka.

Je, Serikali ina mkakati gani sasa kukabiliana na hali hiyo katika mito hiyo miwili Mto Mbezi na Mto Mpiji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunayo mikakati mingi kwa sababu tunafahamu athari za kimazingira zinazosababishwa na mito hii ni athari kubwa. Mwisho wa siku zinaharibu vipando, zinaharibu makazi lakini pia zinaweza kuleta hata maradhi kwa sababu maji yakija yanakuja na takataka, yakirudi yanarudi maji peke yake takataka zinabakia kwa hiyo tunajua hata maradhi yanatokea. Kwa hiyo iko mikakati mingi kama Serikali ambayo tumeamua kuifanya, ikiwemo kwanza kuhakikisha kwamba tunajenga hizo kingo lakini pia tunasaidia katika kuwaelimisha wananchi namna ambavyo wanaweza wakapunguza hizo athari na wakaepukana na hizo athari zinazosababishwa na mito hii. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwa kuwa ipo Barabara ya Makondeko – Kwembe – Kisopwa hadi Mloganzila ya kilometa 14.66 imekuwa kwenye mpango na bajeti kwa miaka mitatu mfululizo. Je, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga kipande cha Makondeko kuelekea Kwembe hadi Kisopwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Makondeko – Kwembe kwenda Kisopwa ni kati ya barabara ambazo zimejumuishwa kama barabara za kupunguza misongamano katika majiji. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mpango upo wa kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa wananchi wa Kibamba wanayo shukrani ya kukamilisha matenki ya Tegeta A – Goba na Mshikamano – Mbezi na mtaa Msumi hauna maji toka kupata uhuru.

Je, ni lini Serikali mtapeleka miundombinu ya kutosha, ili Mtaa huu wa Msumi, Kata ya Mbezi kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Wizara tumeagiza vifaa vya kuhakikisha mradi huu na miradi yote ya eneo lile la jimbo lake tunakwenda kuikamilisha. Tayari tumeshagharamia miundombinu ya matenki makubwa kwa hiyo sasa usambazaji ndio unaofuata.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ningeomba kuuliza maswali mawili madogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitoa misamaha ya kodi ya VAT kwa taulo za kike na vishikwambi lakini tija haikuwepo kabisa. Je, Serikali inachukua hatua gani kukabiliana na changamoto hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa misamaha hii ya VAT kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi imekuwa ikichelewa sana na inasababisha hata miradi ya maendeleo mingi kutokamilika kwa wakati. Je, Serikali inachukua hatua zipi kutatua kadhia hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Issa Mtemvu kwa ufuatiliaji wa misamaha hii ama harakati za ulipaji kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba misamaha ilitolewa kwa vishikwambi na taulo za kike lakini wako ambao walienda kinyume na taratibu lakini Serikali ilichukua hatua mbalimbali ikiwemo kufuta misamaha hiyo na kuhakikisha kwamba wafanyabiashara hao wamelipa kodi inayostahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili mikakati ambayo imechukuliwa na Serikali. Moja ni kubadilisha sheria, sheria iliyokuwepo zamani lazima Baraza la Mawaziri ndiyo litoe msamaha lakini kwa sasa iko juu ya Waziri wa Fedha na Mipango. Jingine Serikali imetengeneza mfumo ambao kwa sasa inaratibu misamaha yote hiyo na inatolewa kwa wakati.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi. Ipo barabara ya kutoka Mbezi kwenda Mpiji Magohe au barabara ya Victoria Road. Ni barabara ambayo iko ndani ya mpango kwa miaka mingi na bajeti lakini iko chini ya ahadi ya Mheshimiwa Rais lakini ndani ya ilani kwa miaka 10. Ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Mtemvu, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii iko kwenye Ilani lakini pia tumekwisha ifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na katika bajeti ijayo nikuombe Mheshimiwa Mbunge tutakayoisoma jumatatu na jumanne, tuipitishe bajeti hiyo ili barabara hii iweze kujengwa kwa kuwa ni miongoni mwa barabara hizo pia, ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, barabara ya njia nane kilometa 19.2 kutoka Kimara hadi Kibaha, imekosa kabisa vituo vya dala dala kwa abiria kupumzika; kwa hiyo, wanaumia na jua na mvua: Je, ni lini Serikali itatengeneza hivi vituo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Japo suala hili Mheshimiwa Mbunge amekuwa akilileta mara kwa mara, lakini nimhakikishie kwamba pia Kamati ya Miundombinu imeshatoa maelekezo kwa Wizara kuhakikisha kwamba suala hili inalifanyiwa kazi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili tumeshaliona na tayari Wizara imeshalipokea kwa ajili ya kutengeneza hivyo vituo kama alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge, ahsante sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ningeomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa waombaji wengi wanasifa za kitaaluma za jumla zinazofanana kwa sababu wamesoma katika vyuo au shule za pamoja hapa nchini, lakini bado malalamiko yapo mengi kwa sababu hamna nafasi wanazopata katika ajira katika Wilaya kadhaa.

Je, Serikali sasa iko tayari kutoa orodha za kiwilaya wakati inatoa hizo ajira ili waonekane wale katika kila Wilaya waliopata nafasi?

Swali la pili, kwa kuwa hapa Bungeni Serikali ilisema mwezi wa pili kwamba wale wote sasa ambao wapo kwenye database waliofika katika hatua ya mahojiano au oral watapelekwa kwenye vituo au watapangiwa moja kwa moja katika vituo, lakini practice kwa sasa inaonesha si hivyo, kuna watu wanachomekwa chomekwa.

Je, Serikali iko tayari kutoa orodha ile ambayo iko kwenye database ili wananchi waweze kuona wanaopangiwa kwamba ni wale ambao wako kwenye orodha? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA N AUTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba waombaji wengi wana sifa zinazofanana na kwa kweli wamesoma kwenye vyuo vyetu lakini changamoto tunayoipata hapa ni kwamba pamoja na sifa hizo lakini nafasi ni chache, kwa hivyo namna pekee ya kuweza kuwapata hawa wanaotakiwa, mathalani nafasi zinaweza zikatangazwa labda 200, waombaji wakawa 1,000, namna pekee ya kuwapata hawa 200 ni lazima tu uwashindanishe. Sasa huo ushindani haumaanishi kwamba pengine wengine walisoma ni bora zaidi, ni kama mbio tu za marathon, lakini kimsingi tungetamani wote wanaoomba wapate lakini nafasi ni chache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo kutoa orodha au kuweka utaratibu wa mfumo wa kiwilaya na wenyewe bado tunaendelea kuutafakari kama nilivyosema kwenye majibu yangu wakati tunahitimisha bajeti yetu kwamba tutajitahidi ku – design mfumo ambao utawabaini waombaji na maeneo wanayotoka ili tuweze kutafuta hicho ambacho kilisemwa sana kwa sauti kubwa na Waheshimiwa Wabunge juu ya hisia za upendeleo wa kimaeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili tunaendelea kulifanyia kazi na mpaka sasa tumeunda timu inajaribu kuchakata tuone namna gani bora siyo jambo jepesi, ukilisema hivi kama jepesi lakini kiuhalisia ni ngumu kutengeneza mfumo utakaobaini maana yake hatufuati kabila. Kwa sababu mwingine anatokea mahala kulingana na asili alikokulia au anaomba akiwa yuko Dar es Salaam hatokei Kibakwe lakini anaomba yuko sehemu nyingine, je unamuwekaje? sasa hilo nalo tunaendelea kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kwamba wale waliokwishafanya usaili na mfumo wetu wa usaili ni wa aina mbili, kwanza ni wa kuandika na mwingine ni usaili wa kuulizwa maswali ya papo kwa papo. Sasa wanapotokea watu wamefika kwenye hatua ya pili maana yake wamejitahidi kufanya vizuri na pale napo utampata wa kwanza mpaka wa mwisho lakini uhitaji pengine ni wachache wanaobaki ndiyo Mheshimiwa Mbunge anasema kuwepo na uwazi ili wajulikane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie kwamba tutajitahidi sana kuweka uwazi huo ili wajulikane, ili wanapochukuliwa wao wenyewe wadhihirishe kwamba kweli alikuwa wa kadhaa na waliochukuliwa na yeye ameweza kupata fursa ili tuondoe haya manung’uniko.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kumekuwa kuna utaratibu wa uuzwaji wa maji kupitia ma – bowser ya magari kwa gharama kubwa kwa wananchi na ilihali ya Serikali imeweka mtandao mzuri sasa hivi wa maji Kibamba;

Je, Serikali mko tayari kutoa kauli ya usitishaji wa uuzaji wa maji kupitia magari?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, usitishaji wa kuuza maji kwenye magari, huu sio utaratibu rasmi. Tutalifanyia kazi pamoja na Wizara husika.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwanza nipongeze sana majibu ya Serikali na nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Mawaziri wa Fedha, TAMISEMI na Ujenzi kwa kuendelea kuchakata jambo hili liende vizuri katika mchakato huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja tu la nyongeza; kwa sababu Serikali ipo katika hatua za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina maana yake tayari imeshafanya utambuzi wa barabara zote zitakazoingia kwenye mradi wa DMDP Awamu ya Pili.

Je, ni barabara zipi ndani ya Jimbo la Kibamba ambazo na zenyewe zitakuwa sehemu ya mradi huu DMDP Awamu ya Pili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kwa niaba ya Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, namna mradi huu ulivyokuwa design kwamba kila Halmashauri katika Mkoa wa Dar es Salaam imewasilisha mapendekezo ya barabara ambazo zitatakiwa kufanyiwa ukarabati kupitia mradi huu wa DMDP II.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumjulisha Mheshimiwa Mtemvu na Wabunge wote wa Dar es Salaam kwamba kwa maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mheshimiwa Anjela Kairuki wiki ijayo mtaitwa wote Waheshimiwa Wabunge wa Jiji la Dar es Salaam ili kushuhudia utiaji saini wa mradi huu wa consultancy ambazo anaenda ku-design barabara zetu hizi. Kwa hiyo, nimtoe hofu ni barabara zote kama walivyoziwalisha wao katika halmashauri zao ambazo zitawekwa katika mradi huu.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa fedha za Mfuko wa Jimbo zinategemea sana idadi ya watu kwenye majimbo yetu, na ni ukweli sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 imekamilika na hivyo tunazo takwimu mpya kwenye majimbo yetu.

Je, katika mwaka wa fedha 2023/2024 fedha zitakazotolewa zitazingatia idadi ya watu kwenye majimbo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba fedha za Mfuko wa Jimbo zinategemea idadi ya wananchi katika jimbo husika, ukubwa wa kijiografia lakini pia na kasi ya umaskini katika eneo husika.

Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kipindi cha mwaka wa fedha uliopita iliongeza fedha za Mfuko wa Jimbo. Waheshimiwa Wabunge wote ni mashahidi; iliongezeka na imeendelea kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi hiyo. Suala la kuzingatia matokeo ya sensa ya mwaka jana ni muhimu na Serikali itaendelea kufanya kazi kwa sababu moja ya kigezo ni idadi ya watu katika maeneo hayo. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nitumie nafasi hii kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kutekeleza miradi yetu kwa haraka sana, lakini pamoja na hilo naomba niulize maswali au maombi mawili kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, moja, hapo ambapo tumewekewa kivuko cha pundamilia na taa sasa hivi tunavuka salama, lakini inatubidi tutembee mita sabini pembezoni mwa barabara ili tuingie kwa Musuguri ambapo jioni tunagongwa sana na magari. Ni ombi kwa Serikali, haioni sababu au haja ya kutengeneza Barabara ya wapita kwa miguu katikati ya road reserve ili tuweze kuingia kwa Musuguri kwa usalama?

Mheshimiwa Spika, pili, kwa chini hapa kwenye makutano ya Magari Saba na Mbezi kuna kivuko kingine ambacho Serikali imeanza kukijenga kwa kuweka taa, lakini imekiacha kwa muda mrefu. Je, ni lini Serikali itakamilisha taa zile ili nah apo wananchi wavuke kwa usalama?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mawili ya nyongeza na pongezi.

Mheshimiwa Spika, hili suala ni la utekelezaji. Naomba nichukue nafasi hii kumuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na TANROADS Makao Makuu waende wakaone uwezekano wa haya mawazo ya Mheshimiwa Mbunge kuona namna watakavyofanya ili wananchi waweze kutumia haya maeneo ya road reserve ili waweze kupita kwa usalama katika eneo hili. Hili ni suala la utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, na suala la pili pia ni utekelezaji kwa sababu, mkandarasi yuko site, waweze kumsimamia na kuhakikisha kwamba, anakamilisha kazi ambayo anaendelea nayo ya kukamilisha mataa, ili kuweza kuleta usalama hapa katika hii barabara ya njia nane. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni kweli kabisa Dar es Salaam, hasa Dar es Salaam Vijijini, Kibamba kule, mawasiliano ni shida. Maeneo ya Mabwepande eneo la Kibesa na maeneo ya Kata ya Saranga, maeneo ya mpakani na Ilala hakuna kabisa mawasiliano: -

Je, Serikali mko tayari kwa minara 600 hii kupeleka na maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge wiki jana alinifikishia changamoto hii, na tayari Serikali tumeshaipokea na tunaifanyia kazi. Tutamjulisha Mheshimiwa Mbunge hatua ambayo tutakuwa tumefikia kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na sintofahamu sana kwa wananchi wengi wakiwepo wa Jimbo la Kibamba kubambikiwa madeni makubwa ya ununuzi wa umeme au LUKU bila kuelewa kutokana na kukosewa kwa makadirio ya awali na TRA. Je, Serikali mko tayari kuwaelekeza TRA waweke mpango mzuri ambao wananchi hawa wataweza kupunguza madeni yale kila mwezi wakiwa wanalipa LUKU zao kila mwezi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Mtemvu, kwa swali lake. Juzi wakati tunapitisha bajeti jambo hili lilijitokeza na ulitolewa Mwongozo na Mheshimiwa Spika kwamba, Wizara ya Nishati pamoja na wenzetu TRA ambao hasa ndiyo wenye hizo pesa tukae na kuweka utaratibu mzuri. Sisi tumeshawafikishia wenzetu, tumewapelekea concern hiyo wanatengeza utaratibu mzuri wa kuonesha deni na mwananchi aweze kulipa taratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili Wizara ya Nishati kupitia TANESCO ni kama bomba la kupitisha mapato hayo ambayo yanatoka kwa mwananchi kupitia TRA. Hata hivyo, tunashirikiana na wenzetu kuweka mifumo mizuri ili wananchi wanaopata huduma ya umeme sasa wasipate adha ya kulipa kodi hii ya majengo ambayo inapitia kwetu. Kwa hiyo, tutalifanyia kazi kwa pamoja Serikalini.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuahidi kupeleka mradi mkubwa wa Shilingi bilioni 42 kwa ajili ya wananchi wa Kinazi A na B na maeneo ya Msingo ambao hawana kabisa majisafi na salama. Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issa Mtemvu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumshukuru Mheshimiwa Rais. Shilingi bilioni 42 ni mradi mkubwa. Mheshimiwa Mbunge hongera pia kwa kuendelea kufuatilia miradi hii mikubwa ya kimkakati na mradi huu tunaanza kuutekeleza mwaka ujao wa fedha. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ni dhahiri nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa utekelezaji wa miradi hii iliyotajwa na Serikali, tunawashukuru sana Serikali. Pamoja na changamoto sasa iliyopo tayari miradi ya Tegeta A na Mshikamano tunayo mizuri usambazaji wa mabomba umekuwa ni changamoto sana kwa sababu ya yale maboza, magari yanayouza maji kwa wananchi…

SPIKA: Swali lako Mheshimiwa.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali kwa sababu tayari wanatakiwa wasambaze watoe kauli hapa ya kusitisha uuzaji wa maji kwa magari. Hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa kuna mradi huo wa usambazaji maji…

SPIKA: Mheshimiwa Issa Mtemvu, hebu ngoja kwanza, Naibu Waziri kwa sasa hivi hasikilizi mchango, anataka swali ili akujibu kwa sababu hiki ni kipindi cha maswali na majibu. Muulize swali Naibu Waziri akujibu.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza Serikali mpo tayari kutoa kauli ya usitishaji wa uuzaji wa maji kwa magari Jimbo la Kibamba kwa sababu mlishatekekeleza miradi miwili kule?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu King’azi hakuna maji kabisa wanatumia maji ya chumvi, ni lini mradi wa usambazaji Dar es Salaam Kusini utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtemvu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na uuzaji wa maji kwenye magari hili suala tulishalipigia marufuku kwa maeneo mengi na hususani eneo la Kibamba, lakini tutaendelea kuhakikisha kwanza tunahakikisha miradi ile imekamilika na uhakika wa maji ya uhakika wa kila siku kwa wananchi, suala hili naamini litatekelezeka.

Mheshimiwa Spika, suala la Dar es Salaam kusini maeneo ya King’azi usambazaji wa mabomba, tunatarajia mapema mwaka wa fedha ujao kuanzia mwezi Julai au Agosti, suala la usambazaji wa mabomba katika maeneo haya yote aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge tunakuja kuyafanyia kazi.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ilikuwa niseme kwa niaba yake kwa sababu aliwasiliana na mimi pia. Nakushukuru.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba hili tulichukue tukalifanyie kazi. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kata ya Goba, Mtaa wa Tegeta A wameweka nguvu zao nyingi sana kujenga Kituo Polisi chenye hadhi ya ghorofa moja kuungana na nguvu za Mbunge Mfuko wa Jimbo. Je, Mheshimiwa Waziri utakuwa tayari kuja Kibamba kuona ile kazi kubwa iliyofanywa na wananchi wale wa Tegeta A juu ya ukamilishaji wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari. Kwa juhudi zinazofanywa na Mheshimiwa Mtemvu na wananchi wake na wadau wengine katika jimbo lake niko tayari kwenda kushuhudia jitihada hizo na kuelekeza kuwaunga mkono kutoka Jeshi la Polisi ili kukamilisha vituo ambavyo tayari wameshavianzisha kwenye Jimbo lake, nashukuru.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, kwanza niishukuru Serikali kuwa na mkakati mzuri wa kuboresha kilimo cha nazi nchini. Nitaomba niwe na swali moja tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Dar es Salaam pembezoni kwa maeneo ya Kibamba, Segerea na Ukonga pamekuwa na vikundi vingi vinafanya kilimo cha mbogamboga; je, ni upi mkakati wa Serikali kuwawezesha hawa ili wafanye kilimo bora cha mboga mboga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali hivi sasa imeweka mkazo mkubwa kwenye kuhamasisha kilimo cha mboga mboga na matunda ili kuongeza uzalishaji ambao kwa mwaka uliopita kupitia mazao haya yametuletea fedha za kigeni zaidi ya dola milioni 750 na lengo letu kufikia dola bilioni 1.2 kwa mwaka 2030. Hivyo kwa hivi sasa tunaendelea kuwawezesha wakulima wadogo wadogo kwanza kabisa katika upatikanaji wa green houses ambao utasaidia katika uzalishaji mkubwa au vilevile mbegu bora ambayo pia itasaidia katika kuzalisha kwa wingi na sambamba na hilo pia tunatafutia masoko kupitia mwamvuli wa TAHA ambao hivi sasa tumeshafungua masoko mengi na wakulima wengi wameanza kuuza mboga mboga na matunda nje ya nchi kupitia mwamvuli huu wa TAHA.

Kwa hiyo, kama Serikali pia tutahakikisha masoko ya uhakika yanapatikana ili tuendelee kuhamasisha vijana wengi zaidi kushiriki katika kilimo hiki cha mboga mboga.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, naomba niulize swali moja tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wananchi wale wa Kibesa sehemu ya Mpiji Magohe, wanatembea kilometa 8.2 kufuata sekodari pale Mpiji Center.

Je, Mheshimiwa Waziri utakuwa tayari kuja ili uone ushuhudie ile adha ya wananchi wale wanayopata ili mimi na wewe tushirikiane kufuata taratibu, sheria na miongozo ili waweze kupewa hilo eneo katika sehemu ya hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, eneo nalifahamu na nilishafanya ziara mara nyingi. Na ukiangalia jibu la msingi, nimejibu kiufasaha, kwamba maeneo ni machache na Jiji la Dar es Salaam linaendelea kukua, tukikosa maeneo ya kupumulia watu wanazidi kuongezeka lakini tukaendelea kunyima maeneo ambayo angalau watu wanapopumua…

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba haya maeneo tunayatenga, si kwa sababu tu ya msuala ya utalii. Serikali inatambua kwamba kuna umuhimu wa ku-balance ikolojia. Kuna maeneo kama Pugu tumetenga ile Kazimzumbwi na upande wa Kibamba na huku kaskazini tumetenga hili Pori la Mambwepande. Lakini lengo ni kuifanya Dar es Salaam ipate maeneo ya kupumulia kwa sababu watu wanazidi kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu, kilometa za mradba katika eneo hili ni 15 tu, ni chace sana. tulitamani hata ziwe nyingi. Sasa tukiendelea kuzimega tena, kwanza tunawafanya wana-Dar es Salaam wakose pa kupumlia; cha pili, ni kufanya sasa maeneo mengi ambayo tunajitahidi kuyatunza kwa ajili ya ku-balance ikolojia yatakuwa yanazidi kupungua zaidi.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Moja ya eneo ambalo Serikali inatekeleza chini ya asilimia 50 kwenye bajeti na mpango ni ahadi za Viongozi wa Kitaifa.

Je, ni upi mkakati wa Serikali kumaliza ahadi zote za Viongozi wa Kitaifa za miaka ya nyuma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha mawasiliano lakini inaendelea kuimarisha makusanyo ya fedha, na hivi nimuombe Mheshimiwa Mbunge naye awe ni Balozi wa kushawishi na kuwashauri wafanyabiashara pamoja na yeye na mimi kuendelea kukusanya kodi ili tuweze kutekeleza ahadi za viongozi wetu kwa wakati.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Umekuwepo mradi wa Kwembe-King’azi wa muda mrefu ambao uliahidiwa kukamilika mwezi wa Kumi na Mbili mwaka 2021 mbele ya Mheshimiwa Waziri na mpaka sasa haujaanza:-

Je, ni lini mradi wa Kwembe-King’azi A utaanza ili wananchi wa pale waweze kupata maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu tunaendelea katika hatua zake za mwisho kabisa na unaelekea kwenye utekelezaji.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri sana na yenye matumaini kwa wananchi wa Wilaya ya Ubungo;:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa vikao vya mashauriano baina ya Wizara na Mkoa wa Dar es Salaam vinaendelea kuona uwezekano wa kujenga hiyo Sport Arena katika eneo la Luguruni la ekari 10.5 lililotolewa na Mheshimiwa Rais:-

(a) Je, Serikali au wizara mpo tayari sasa kumshirikisha Mheshimiwa Mbunge katika vikao hivyo kama mdau?

(b) Pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kujenga Arena hiyo, ikiwa sasa tayari imeshakamilisha ile michoro yote ya Arena: Je, Serikali imeweza kuzingatia au kuweka miundombinu ya kuingia na kutoka katika Arena hizo?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtemvu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wizara hatuna tatizo kushirikisha Wabunge. Hivyo niagize BMT na Mkurugenzi wetu wa Michezo, watakapokutana na Uongozi wa Dar es Salaam, wawashirikishe Wabunge wote wa Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili alitaka kufahamu kama hiyo michoro imezingatia miundombinu mbalimbali ya kuingilia na kutokea katika viwanja hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumezingatia hili. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa barabara nyingi za ndani za TARURA ndani ya Jimbo la Kibamba zimeharibika sana na wananchi wanashindwa kufanya shughuli zao za maendeleo; je, ni upi mkakati wa Serikali kwenye kujenga barabara ya King’ong’o – Temboni - Saranga – Ukombozi - Goba – Majengo - Kwandogo – Kwashija na Luguluni – Mbokomu? Upi mkakati wa Serikali wa kukamilisha barabara hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Jimbo la Kibamba kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara nyingi za Jimbo la Kibamba zina hali mbaya na sisi kwenye bajeti ya TARURA ya mwaka ujao wa fedha tumeweka kipaumbele na bajeti imeongezeka sana ya Jimbo la Kibamba na namuelekeza pia Meneja wa Manispaa ya Ubungo kuhakikisha anazipa kipaumbele barabara za Jimbo la Kibamba ili ziweze kujengwa na kuhakikisha wananchi wanapata ahueni ya kupita katika barabara ambazo ziko bora, ahsante sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa barabara nyingi za ndani za TARURA ndani ya Jimbo la Kibamba zimeharibika sana na wananchi wanashindwa kufanya shughuli zao za maendeleo; je, ni upi mkakati wa Serikali kwenye kujenga barabara ya King’ong’o – Temboni - Saranga – Ukombozi - Goba – Majengo - Kwandogo – Kwashija na Luguluni – Mbokomu? Upi mkakati wa Serikali wa kukamilisha barabara hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Jimbo la Kibamba kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara nyingi za Jimbo la Kibamba zina hali mbaya na sisi kwenye bajeti ya TARURA ya mwaka ujao wa fedha tumeweka kipaumbele na bajeti imeongezeka sana ya Jimbo la Kibamba na namuelekeza pia Meneja wa Manispaa ya Ubungo kuhakikisha anazipa kipaumbele barabara za Jimbo la Kibamba ili ziweze kujengwa na kuhakikisha wananchi wanapata ahueni ya kupita katika barabara ambazo ziko bora, ahsante sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Kwa kuwa ujenzi wa madaraja haya ya juu (flyovers) yamekuwa yana lengo la kupunguza foleni, lakini baada ya ujenzi wenyewe tu kunakuwa na kuwekwa matuta sasa kwenye barabara ambayo inakwenda ku-distort au kuharibu ile dhima ya kujenga zile flyover.

Je, ni ipi kauli ya Serikali juu ya mkanganyiko huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli lengo la flyover ni kupunguza foleni na hili alilolisema wakati fulani inakuwa ni kwa ajili ya usalama kwamba tuweke matuta ili kupunguza ajali. Kwa hiyo, tutazingatia kuona kama hakuna ulazima wa kuweka hayo matuta tutayaondoa, lakini tukizingatia sana kwamba usalama wa wale watumiaji wa hizo barabara, ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya mwisho ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nilitaka kumuuliza tu swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa tunazungumzia sana asilimia kumi kama kuwafikia vijana, na tunatambua vijana wanaozungumzwa kwenye asilimia 10 zile asilimia nne zao ni vijana wanaoishia miaka 35 na machinga wengi wanazidi miaka 35.

Je, ni upi sasa mkakati wa Serikali katika kuwafikia machinga walio wengi zaidi ya hawa wa miaka 35? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Issa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli, asilimia 10 zile zimelenga zaidi akinamama, vijana na wale wenye ulemavu, lakini kwenye kundi hili la vijana ni kweli wakishavuka ule muda wao maana yake wanakuwa hawawezi kukopesheka.

Mheshimiwa Spika, lakini kama nilivyosema Serikali inaendelea na juhudi mbalimbali ikiwemo kupitia taasisi za kifedha ili kuhakikisha wamachinga hawa, hawa wajasiriamali ambao watakosa fursa kwenye ile asilimia 10 ambayo inatengwa katika Halmashauri, basi wapate fedha kupitia taasisi nyingine kama nilivyosema SIDO na taasisi za kifedha nyingine ambazo zinatoa mikopo kwa wajasiriamali. Nakushukuru sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa kwenye Mkoa wa Dar es Salaam eneo lililobakia kuwa na Mahakama ya Wilaya ni Jimbo la Kibamba ndani ya Wilaya ya Ubungo na eneo tayari tunalo: Je, Serikali mko tayari kujenga Mahakama pale ya Wilaya katika mwaka huu 2022/2023?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kumjibu Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, swali lake kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari mpango wa kuanza ujenzi katika eneo alilolitaja umeshakamilika. Nami naomba baada ya hapa tuweze kuwasiliana ili tuone ni lini tunaanza mpango huu? Ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwa muda mrefu Jimbo la Kibamba halijapata fedha hizi za mambo na ninayo maboma ya zahanati ya Saranga King’azi na Msakuzi. Je, ni lini Serikali inaweza kuweka commitment hasa kwa mwaka huu 2023/2024 ili waweze kuleta fedha tumalizie maboma haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Maboma ya zahanati katika Jimbo la Kibamba Halmashauri ya Ubungo yatatafutiwa fedha kwa ajili ya ukamilishaji. Hata hivyo, nitumie fursa hii kuwakumbusha wakurugenzi wa Manispaa zenye mapato makubwa kama Ubungo na Manispaa nyingine, kuweka kipaumbele cha fedha za miradi ile asilimia 40,60 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma hayo wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma hayo. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya jumla ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; ipo barabara ya Makabe – Msakuzi kuelekea Mpiji Magoe ambayo ina sifa hizo ambazo amezizungumza na sasa barabara hii imeanza kutengenezwa, wananchi bado wako kwenye sintofahamu kama watalipwa fidia au lah! Je, ni ipi kauli ya Serikali kwenye barabara hii. (Makofi)

Swali la pili, ipo barabara ya Victoria au inaitwa Mbezi Shule – Mpiji Magohe, kilometa 9.5; ni barabara ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais lakini ipo ndani ya bajeti kwa kipindi cha miaka miwili, lakini ina watu takribani 50,000 ambao ni wengi zaidi hata ya majimbo mengine.

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Makabe – Msakuzi, ni barabara ambayo tangu kuwepo kwake iko chini ya TANROADS na wakati ule ilikuwa chini ya ujenzi Mkoa wa Dar es Salaam, TANROADS ilipoanzishwa ikawa imehamia moja kwa moja TANROADS. Kwa hiyo, kwa wananchi ambao watakuwa ndani ya mita 22.5 kutoka katikati hawatastahili kulipwa, ila pale ambapo tutakwenda 7.5 wananchi ambao wako katika barabara hii watalipwa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara ya Victoria, pale kuna barabara mbili, kuna barabara ya Kibamba Shule – Magoe Mpiji na Victoria kwenda Magoe Mpiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kibamba Shule tayari imeshaanza kujengwa kwa awamu, pia, ndiyo tunayoitegemea itakuwa outer ring road ya Mkoa wa Dar es Salaam na usanifu unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Victoria imekuwa ni barabara ambayo inahitajika sana hasa baada ya kuanzisha stendi ya Magufuli, tunavyoongea sasa hivi Mhandisi Mshauri yuko field kufanya usanifu na tunategemea baada ya kukamilisha kwa bajeti ambayo tunaiandaa iweze kuingia ili ijengwe kwa kiwango cha lami, ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza natumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kupitia Serikali anayoiongoza ya Awamu ya Sita kwa kuwa msikivu sana kwa kilio cha wajasiriamali, Wilaya ya Ubungo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maswali mawili ya nyongeza, swali la kwanza; kwa kuwa ni kawaida sana vinavyotengenezwa vibanda hivi vya wajasiriamali, wananchi mbalimbali kutokea kwenye maeneo mbalimbali ya nchi wanavamia na kusababisha walengwa kutofikiwa.

Je, Serikali au Wizara ya Ujenzi mko tayari kuiachia Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo kupanga wajasiriamali hao ili kufikia malengo tuliyotarajia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa mpaka sasa wajasiriamali wanateswa sana kupitia Wizara ya Ujenzi katika eneo lao la TANROADS katika maeneo haya waliyopo.

Je, Serikali ipo tayari kuchukua ombi la kuwaacha kipindi hiki wajasiriamali mpaka mradi utakapokamilika katika maeneo haya ya pembezoni mwa barabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Serikali nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua kazi nzuri anayofanya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nasema tu kwamba, kwa kuwa tunaowalenga ni wajasiriamali wa eneo husika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatafuta mpango mzuri ambao utahakikisha kwamba wale walengwa ndiyo wanaopata vibanda hivi. Ofisi ya Mheshimiwa Mbunge mhusika tutahakikisha kwamba inashiriki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kikubwa ambacho hapa tunaangalia ni kulinda usalama wa hawa wanaofanya biashara. Tunaweza tukawaacha wakaendelea kufanya biashara, lakini kukatokea madhara. Hata hivyo, nasema tu tumelipokea, tutatafuta namna nzuri ya kuona namna gani wanaweza wakafanya biashara bila madhara. Ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ziada kwanza niseme pongezi sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kunijengea matanki mawili Mshikamano na Tegeta A kwa kuwasaidia wananchi lakini sasa bado kilio cha miaka miwili kuhusu usambazaji wa mabomba kwa wananchi, mahitaji ni bilioni tano, uwezo wa ndani bilioni mbili tayari.

Je, Wizara mko tayari kutoa kauli kuisaidia DAWASA bilioni tatu, ili wakamilishe usambazaji wa mabomba kwa wananchi wale?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa kweli kazi ambayo ameifanya Kibamba Mheshimiwa Mbunge ni kubwa na DAWASA kazi wanayoifanya katika jimbo lake ni kubwa, kazi iliyobaki ni usambazaji. Sisi kama Wizara ya maji tupo tayari kushirikiana na DAWASA katika kuhakikisha tunamaliza tatizo la maji hasa katika eneo la Kibamba. Ahsante sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri na tuendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kututekelezea miradi hiyo mitatu katika kipindi chake cha miaka mitatu. Pamoja na majibu hayo, naomba niulize maswali ya mawili (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, ukamilishaji wa miradi iliyotamkwa kwenye majibu ya msingi ni ukamilishaji wa matanki au vihifadhia maji, lakini ili mradi ukamilike ni lazima usambazaji wa mabomba kwenda kwa wananchi ukamilike ili thamani ya fedha itimie. Sasa yapo maeneo kama CCM ya zamani Mpijimagohe, Torino kwa Mvungi, kwa Mzee Kadope na maeneo ya kwa Yusuph Michungwani.

Ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya muda mrefu kupeleka mabomba hapa katika maeneo hayo?

(b) Mheshimiwa Spika, Mtaa wa Msumi hasa Msumi Center na Darajani ni muda mrefu hawajawahi kuyaona maji safi na salama, lakini tayari Serikali imefanya utafiti wake na kutekeleza mradi au ina nia ya kutekeleza mradi wa shilingi bilioni 13.9. Je, ni lini sasa Serikali inatoa commitment kwa wananchi wa Kibamba ya kuanza kutekeleza mradi huo ambao mmeshaufanyia tathmini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia miradi hii kwa niaba ya wananchi wake wa Jimbo la Kibamba na kwa kweli anaendelea kufanya kazi nzuri. Sasa kupitia mradi wa kuboresha huduma za maji katika Mkoa wa Dar es Salaam, Serikali imepenga kiasi cha shilingi bilioni 33 ambapo ndani ya fedha hizo kuna shilingi bilioni 13.9 kwa ajili ya kutekeleza mradi katika maeneo ya Msakuzi, Makobe, Msumi A, B, C, Tegeta, Mpindi na Magohe. Maeneo yote hayo yatakuwa ndani ya mradi huo wa kuboresha huduma ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, mradi huu utakapokamilika pamoja na maeneo ya Tegeta, utaweza kunufaisha wakazi takribani 166,548. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvuta subira katika bajeti hii itakapopitishwa, basi mradi huo utaanza mara moja. Katika maeneo ya usambazaji wa mabomba, yote hayo yapo ndani ya mradi huu wa kuboresha huduma ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam. Nakushukuru sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mkwamo wa kuendelea kuijenga barabara ya Makondeko – Kwembe – Kisokwa hadi Mloganzila na Serikali imejenga kilometa nne tu kutoka Kibamba hadi Mloganzila; je, Serikali mko tayari kuanza kujenga kipande cha Makondeko hadi Kwembe kwa kilometa nne tu angalau ili wananchi waweze kuishi salama kwenye barabara ile?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja ni kati ya barabara ambazo tunasema katika Mkoa wa Dar es Salaam ni barabara ambazo zinapunguza msongamano na bado tutaendelea kuijenga. Sina uhakika kama ni kilometa nne, lakini zipo kwenye mpango wa kuhakikisha kwamba zile barabara zote tunazikamilisha ikiwa hatua madhubuti ya Serikali kupunguza misongamano ya magari katika Jiji la Dar es Salaam, ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili yenye kifungu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilishawahi kutengwa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili la kivuko hiki, lakini haijatekelezwa. Leo majibu ya msingi yanaonesha kwamba wanaendelea au wamekamilisha tathmini na gharama wamezipata upya, sasa wanatafuta fedha. Nini commitment ya Serikali kujenga daraja hili ili kuokoa vifo vya watoto ambapo hata jana tu mtoto mmoja amekufa kwenye kivuko hiki?

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Jimbo la Kibamba kuna Mto Mpiji wenyewe na Mto Mbezi ambapo kuna vivuko vingi sana hatarishi kwa watoto wetu na watu wanaotumia. Je, ni ipi ahadi ya Serikali kuleta fedha maalum kujenga vivuko hivi ili tuokoe maisha ya watu wetu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu yangu ya msingi, tayari Serikali imefanya tathmini na imebaini kwamba zinahitajika shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo kazini na ndiyo maana kuna ongezeko kubwa la bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka muda huu Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia imeridhia kuongeza bajeti maalum ya shilingi bilioni 350 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hii. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepokea na itaweka kipaumbele kikubwa sana kuhakikisha kwamba inaanza ujenzi wa miundombinu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, vivyo hivyo nirejee maelezo yangu ya awali kwamba Serikali inaona umuhimu mkubwa sana wa miundombinu hii muhimu kwa maslahi ya wananchi, na tayari bajeti ya dharura ya TARURA imeongezeka. Vile vile kuna bajeti maalum kwa ajili ya ukarabati na marekebisho na ujenzi wa miundombinu hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalichukulia suala hili la ujenzi wa miundombinu hii kwa umakini mkubwa na itakuja kujenga miundombinu hii.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ningeomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Serikali inasimamiwa na Mwongozo wa Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2009 zinazotaka madeni ya watumishi wa umma yanapotokea tu yalipwe ndani ya miezi 12. Je, ni lini Serikali itasimamia mwongozo huu wa kikanuni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa madai mengine ya wazabuni na wakandarasi yanapochelewa kulipwa hulipwa na riba. Je, Serikali haioni haja sasa ije na sera na sheria hapa Bungeni ili iweze kuweka hiyo nafasi ya kuchelewa kulipa itawalipa na riba watumishi wa umma ili hiyo haja ya kuwalipa iende kwa kasi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo unaozungumzwa na Mheshimiwa Mbunge wa mwaka 2009 ni mwongozo unaohusu udhibiti wa ongezeko la madeni ya Serikali kwa watumishi wa umma. Ni kweli maneno kama anayosema Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ilieleza kwamba pamoja na mazingatio mengi ambayo yameelezwa ndani ya mwongozo huu, lakini moja ya jambo la msingi kabisa ni kuhakikisha kwamba Serikali inakuwa na mpango mzuri kwa ajili ya kurithisha madaraka na mara nyingi huo mwongozo unafanywa kwa kupitia bajeti zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika swali lake la kwanza kwamba Serikali inaendelea kusimamia mwongozo huu na pale ambapo panatokea mapungufu Serikali kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu - Utumishi imekuwa inapeleka maelekezo na kuendelea kukumbusha juu ya wale maafisa uajiri kuendelea kusimamia mwongozo huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, madeni haya yanalipwa lini? Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imejipanga vizuri. Nataka nikutoe wasiwasi wewe, lakini pia kulitoa wasiwasi Bunge lako kwamba Serikali inaendelea kusimamia mwongozo huu na kuhakikisha kwamba madeni yote yale ambayo yamehakikiwa na taarifa zake zimeletwa katika mamlaka husika kwa ajili ya malipo, tunafanya hivyo.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Ndani ya Jimbo la Kibamba wapo wananchi wengi sana ambao walilipia Sh.27,000 waunganishiwe umeme, lakini mpaka sasa wamekuwa wakisumbuliwa na bado hawajaunganishiwa. Je, Serikali ipo tayari kutoa maelekezo katika Ofisi za TANESCO Mkoa wa Kimara na Kibamba ili wananchi hao waunganishiwe umeme haraka?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunakiri kwamba kuna watu ambao walishalipia huduma ya umeme lakini walikuwa hawajaunganishiwa. Nitoe maelezo katika maeneo mawili, agizo la kwanza kwa wenzetu wa TANESCO ambao tayari walishalipata; ni kwamba hakutakuwa kuna mabadiliko ya bei, yule ambaye alishalipia gharama ataunganishiwa kwa gharama hiyo hiyo. Nasisitiza kwamba yeyote atakayeambiwa ulilipa Sh.27,000 lakini sasa unatakiwa ulipe zaidi tupatiane taarifa ili tuweze kufanya ufuatiliaji na kuwajibishana katika eneo hilo. Yeyote aliyelipa shilingi 27,000 ataunganishiwa kwa gharama hiyo hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande huo huo, ni kweli kwamba tunayo load kubwa ya wateja ambao wamelipia na tunaendelea kuhangaika nayo na tuna mkakati wetu wa kuhakikisha kwamba hatuwi na backlog ya zaidi ya mwezi mmoja; kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita sasa imetuwezesha kupata fedha za kutosha kwenda kupeleka umeme, namhakikishia Mheshimiwa Mtemvu kwamba tutafanya kazi hiyo na uunganishaji utakamilika kwa wakati.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sheria hii ya mwaka 1932 ndiyo iliyotumika kuvunja makazi kwa ajili ya upanuzi wa barabara njia nane kuanzia Kimara mpaka Kibaha, na wananchi bado wanaendelea na sintofahamu juu ya uhalali huo wa kuvunjiwa: Je, Serikali iko tayari kutoa maelekezo kwa Mamlaka za Wilaya na Mkoa kutoa majibu rasmi kwa wananchi ili wasiendelee kufuatilia kwenye Ofisi za Mbunge? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi kwamba hii Sheria ya Mwaka 1932 na hasa kwa barabara ya kuanzia Dar es Salaam hadi Ruvu kulikuwa na maeneo ambayo ni mita 22.5 lakini kuna maeneo ambayo ilikuwa ni mpaka mita 121. Kwa hiyo, niseme tu ni sheria iliyotumika na wananchi wa maeneo husika hasa katika Kijimbo la Kibamba wanatakiwa waelewe kwamba Serikali ilitumia sheria hiyo ya mwaka 1932.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Mkakati wa Serikali wa mwaka 2020 mpaka 2034 una jukumu muhimu la kupunguza gharama pamoja na kuongeza usambazaji kufikia 80% kwa Watanzania. Je, mpaka sasa mmefikia wapi kwenye eneo la kupunguza gharama na usambazaji kwa Watanzania kuelekea hiyo 80%?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa mkakati huu ni wa miaka kumi na kwa sasa kumekuwa na utumiaji wa nguvu kutafuta Watanzania mmoja mmoja ambao wanatumia mkaa kwenye makazi yetu. Sasa je, kuna kauli ipi ya Serikali juu ya jambo hili, kwa sababu muda bado ni mwingi sana mpaka mwaka 2034? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kwa kuwa ni rafiki wa mazingira na amekuwa akifuatilia sana mambo yanayohusu mazingira, lakini kwa kuangalia usalama wa watu wetu pamoja na wapiga kura wake wa Kibamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo; swali la kwanza, kinachofanyika kwa sasa ni kuendelea kuita wawekezaji waje wawekeze katika eneo hili la nishati safi ya kupikia wakati Serikali inaendelea na jukumu na taratibu za kuangalia ni jinsi gani ya kupunguza gharama lakini na kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana katika maeneo yote ndani ya Taifa letu kwa bei nafuu na inaweza kununulika kulingana na uwezo wa wananchi wetu. Kwa hiyo, hilo ndilo ambalo linafanyika ndani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili kuhusu kauli ya Serikali, kwanza siyo sahihi kumfata Mtanzania mmoja mmoja kwenye nyumba yake kuangalia ana mkaa au hana mkaa, kwa sababu kinachofanyika ni kurudi kule kwenye misitu yetu ambapo tunazo taasisi zetu zinazosimamia misitu yetu ili isiweze kukatwa kwa sababu ukimfata Mtanzania mmoja mmoja ndani ya nyumba yake huwezi kujua mkaa alionao kama una kibali au hauna kibali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba wenzangu ndani ya Serikali ili tuweze kurejea kwenye masharti na kanuni zetu zinavyotuelekeza ili tuweze kulinda mazingira yetu na tuendelee kuelimisha wananchi wetu juu ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na kwa hili nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa ni kiongozi na kinara kwenye eneo hili na tayari tunaraji kwenye tarehe 8 Septemba tutamuona mama mwenyewe akipika jikoni. Hiyo ndiyo njia ya kuhamasisha Watanzania tunayoisema ili wajue kwa nini tunawaelekeza wananchi wetu waelekee kwenye nishati safi ya kupikia kwani ni salama na haina madhara yoyote na gharama yake ni nafuu, nakushukuru. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Mtaa wa King’azi na Mtaa wa Saranga, wananchi hawana kabisa huduma ya afya na wanahudumiwa chini ya miti katika Ofisi za Serikali za Mitaa. Pamekuwa na ahadi ya Serikali za miaka miwili kukamilisha maboma katika mitaa hii miwili. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha tukamilishe maboma yale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge, amefuatilia lakini nilishamshauri pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa sababu ya uwezo wa mapato yao ya ndani, wana uwezo wa kukarabati na kuwezesha zahanati ile ianze kutoa huduma.

Mheshimiwa Spika, fedha za mapato ya ndani ni fedha za Serikali, kwa sababu kumekuwa na kasumba ya baadhi ya watendaji kuamini kwamba fedha ya Serikali ni fedha inayotoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI au Serikali Kuu. Fedha ya mapato ya ndani ni fedha ya Serikali kama ambavyo fedha nyingine zinafanya kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii nimwelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo kwamba tunampa kipindi cha miezi sita waanze ukarabati na ukamilishaji wa majengo hayo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaambatana mimi na yeye kwenda kukagua pale na kazi ile itakuwa imeanza kupitia mapato ya ndani ya Manispaa ya Ubungo.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya mpango wa kurithishana madaraka Serikalini au wanaita succession plan. Hii inasababishwa na kutokustaafu kwa watu wengi, lakini kutokuajiri kada nyingi kwa muda mrefu. Je, ni upi mpango wa Serikali kusimamia hii succession plan au mpango huu kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba Serikali inao mpango wa succession plan katika kada zote. Kwa sababu katika utaratibu wa kupitisha muundo ili muundo wako uweze kukubalika katika Ofisi ya Katibu Mkuu Utumishi, moja ya kitu kikubwa ambacho lazima ukiweke ndani ni succession plan na hili Mheshimiwa Mbunge na Bunge linaweza likathibitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na maombi mengi sana yanayoletwa kwa Katibu Mkuu tukiombwa kuongezea baadhi ya kada fulani au watu fulani muda wa nyongeza kabla hawajastaafu na Katibu Mkuu amekuwa anasisitiza sana. Hili jambo liende kwa Wizara na Taasisi zote ikiwemo wenzetu wa Serikali za Mitaa kwamba, kabla haujaleta muundo kwa Katibu Mkuu Utumishi, ni vyema uhakikishe kwamba ndani yake upo mpango wa kurithishana madaraka kama ambavyo inaelekezwa katika taratibu. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mkwamo wa kuendelea kuijenga barabara ya Makondeko – Kwembe – Kisokwa hadi Mloganzila na Serikali imejenga kilometa nne tu kutoka Kibamba hadi Mloganzila; je, Serikali mko tayari kuanza kujenga kipande cha Makondeko hadi Kwembe kwa kilometa nne tu angalau ili wananchi waweze kuishi salama kwenye barabara ile?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja ni kati ya barabara ambazo tunasema katika Mkoa wa Dar es Salaam ni barabara ambazo zinapunguza msongamano na bado tutaendelea kuijenga. Sina uhakika kama ni kilometa nne, lakini zipo kwenye mpango wa kuhakikisha kwamba zile barabara zote tunazikamilisha ikiwa hatua madhubuti ya Serikali kupunguza misongamano ya magari katika Jiji la Dar es Salaam, ahsante. (Makofi)