Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa (18 total)

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza:-

Je, ni lini mradi wa kujenga Sub-station ya Nyakanazi (KV 220) toka Rusumo na Geita utakamilika ili kuondoa tatizo la kukatikakatika kwa umeme Biharamulo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovolti 220 kutoka Geita hadi Nyakanazi. Mradi huu unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Geita - Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 144 ambapo Mkandarasi Kampuni ya M/S Kalpataru Power Transmission Ltd kutoka nchini India anaendelea na kazi za mradi. Hadi sasa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme pamoja na kituo cha kupoza umeme umefikia asilimia 60.

Mheshimiwa Spika, gharama ya mradi ni EURO milioni 45 sawa na takriban shilingi bilioni 117.79. Mradi huu unatarajiwa kukamilika Machi, 2021. Ni mategemeo ya Serikali kuwa mradi utakapokamilika utaimarisha na kuboresha hali ya upatikanaji umeme katika maeneo ya Wilaya ya Biharamuro na maeneo mengine ya jirani.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa mradi wa kutoa maji toka Ziwa Victoria kuyapeleka Biharamulo kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi hapo tarehe 16/09/2020 alipokuwa Biharamulo katika Kampeni za Uchaguzi Mkuu, 2020?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eng. Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto za upatikanaji huduma ya maji katika Wilaya ya Biharamulo. Hivyo, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali inatekeleza mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji wenye urefu wa km 10.9 katika maeneo ya Ng’ambo, Kalebezo, Nyakatuntu, Rubondo Chuoni na Rukaragata na kuchimba kisima katika eneo la Rukagarata. Thamani ya mradi huu ni shilingi milioni 178.9 na utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 70.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto ya uhaba wa maji katika Mji wa Biharamulo, Serikali iliamua chanzo cha uhakika cha maji kiwe Ziwa Victoria badala ya bwawa na chemichemi vinavyotumika kwa sasa. Hivyo mradi wa usambazaji maji katika Mji wa Biharamulo ambao utatoa maji katika Ziwa Victoria umefikia katika hatua ya kuandaa makabrasha ya zabuni (tender documents). Utekelezaji utaanza katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Aidha, kupitia Mradi wa Maziwa Makuu, Wilaya ya Biharamulo itanufaika kupitia chanzo cha Ziwa Victoria ambapo jumla ya vijiji 12 vya Rwekubo, Rusese, Kabindi, Runazi, Rukora, Kikomakoma, Kagoma, Songambele, Kasozibakaya, Nyamigogo, Chebitoke na Nyabusozi vitapata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza:-

Serikali ilitoa shilingi 500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo, lakini kiasi cha shilingi 204,000,000 kilirejeshwa baada ya kufunga mwaka Julai, 2020.

(a) Je, ni lini fedha hizo zitarejeshwa ili ujenzi uendelee?

(b) Gharama ya ujenzi ni shilingi 1,500,000,000; je, ni lini kiasi cha shilingi 1,000,000,000 kitatolewa ili kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ilipatiwa shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali mpya ya Halmashauri ambapo majengo yaliyojengwa ni Jengo la Wagonjwa wa Nje na Maabara na majengo yote mawili yamefikia asilimia 80 ya ukamilishaji. Aidha, kati ya fedha hizo zilizotolewa shilingi milioni 204 zilirejeshwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali baada ya kuvuka mwaka wa fedha 2019/2020 kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya fedha ya mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2016.

(b) Mheshimiwa Spika, mwezi Januari 2021 Serikali imetoa shilingi bilioni 1 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ili kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Majengo yatakayojengwa ni Jengo la Utawala na Jengo la Wazazi ambayo yamefikia asilimia 40 ya ukamilishaji, Jengo la kuhifadhia dawa na Jengo la kufulia ambayo yamefikia asilimia 60 ya ukamilishaji. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Hospitali hiyo imetengewa shilingi milioni 300.
MHE. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Nyamirembe – Chato mpaka Katoke Biharamulo ya kilomita 50 kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Nyamirembe Port – Katoke yenye urefu wa kilometa 50 ni barabara ya Mkoa inayounganisha Bandari ya Nyamirembe ambayo ipo Mkoa wa Geita na Mji Mdogo wa Katoke ambao upo Mkoa wa Kagera kupitia vijiji mbalimbali na Hifadhi ya Burigi Chato. Barabara hii inahudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza taratibu za kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa gharama ya Shilingi milioni 861.046 kwa kutumia fedha za ndani. Katika mwaka wa fedha ujao 2021/2022, fedha zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa Nyamirembe Port – Katoke, urefu wa kilomita 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii inaendelea kuiimarisha kwa kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali kila mwaka kabla ya ujenzi kwa kiwango cha lami kuanza ili barabara hiyo ipitike katika vipindi vyote vya mwaka. Katika mwaka huu wa fedha 2020/2021, jumla ya Shilingi milioni 447.771 zilitengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali na kwa sasa barabara hiyo ipo katika hali nzuri. Ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Soko la Kimkakati la Rusahunga Wilayani Biharamulo litakalogharimu shilingi bilioni 3.5 kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri Mkuu Bungeni?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na masoko nchini kwa ajili ya kukuza biashara na mauzo ndani na nje ya nchi kwa maendeleo na ustawi wa wananchi wake. Kutokana na umuhimu huo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha masoko yanaanzishwa, kuboreshwa na kuendelezwa ili kutoa fursa kwa wakulima wadogo pamoja na wafanyabishara kuuza mazao na bidhaa zao katika masoko hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kipindi cha mwaka 2017/2018, Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ilitenga eneo la uwekezaji katika Kata ya Lusahunga lenye ukubwa wa ekari 65 ambalo lina thamani ya shilingi bilioni 3.5. Eneo hili limetengwa kwa ajili ya kujenga viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, kujenga maghala ya kuhifadhia mazao, miundombinu ya majengo ya kibiashara kama mahoteli, ujenzi wa soko la kimkakati, kituo cha afya, viwanja vya makazi, na kituo cha mafunzo ya wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) imeendelea kusisitiza Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo kutenga fedha katika bajeti yake ili kufanikisha ujenzi wa soko hilo. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta wadau mbalimbali ikiwemo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili iweze kufanikisha ujenzi wa soko hilo.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka Hifadhi ya Burigi – Chato ili waache kuingiza Mifugo ndani ya Hifadhi na kumaliza mgogoro kati ya wananchi hao na Hifadhi hiyo?
NAIBU WAZIRI, MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TANAPA imeendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Burigi - Chato. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi 20,836,200 zilitumika kutoa elimu ya uhifadhi katika vijiji 37, ambapo katika Wilaya ya Biharamulo elimu hiyo ilitolewa kwa vijiji sita vya Kiruruma, Nyabugombe, Ngararambe, Kabukome, Katerela na vya Kitwechembogo.

Aidha, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga jumla ya Shilingi Milioni 96.7 kwa ajili ya utoaji wa elimu ya uhifadhi katika maeneo ya vijiji 38 vinavyopakana na hifadhi hiyo vikiwemo vijiji 10 vya Wilaya ya Biharamulo.

Mheshimiwa Spika, sambamba na utoaji wa elimu kwa vijiji, Serikali imejipanga kutumia makundi maalum wakiwemo viongozi wa dini, wanasiasa na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili waweze kusaidia katika kuelimisha faida za uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, ni lini kiasi cha shilingi milioni 204 zilizorejeshwa Hazina mwaka wa fedha 2019/2020 zitatolewa kwa ajili ya ujenzi wa majengo mawili ya Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante; kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, kiasi cha shilingi milioni 500 kilitengwa na kutolewa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo. Hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2020 kiasi cha shilingi milioni 204 kilikuwa hakijatumika, hivyo kilirejeshwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti kifungu namba 29(1).

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za afya karibu na maeneo yao. Hivyo kutokana na umuhimu wa mradi huu, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali ilitenga na kutoa shilingi bilioni moja kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa hospitali hii. Vilevile katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 676.6; shilingi milioni 300 kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi na shilingi milioni 376.6 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.

Mheshimiwa Spika, hivyo Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo inahimizwa kuomba fedha hizo mapema ili kuendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali hiyo ya Wilaya ikiwemo majengo mawili aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge. Ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, ni lini Vituo vya Afya vya Rukaragata na Nemba vitapewa vifaa vya upasuaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023, imetenga shilingi bilioni 69.65 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini. Kati ya fedha hizo Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo imetengewa shilingi milioni 250.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imepeleka vifaa vya upasuaji ikiwemo kitanda, taa ya upasuaji na X-ray machine kwa ajili ya Kituo cha Afya Nemba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Kituo cha Afya Rukaragata hakina jengo la upasuaji, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo katika mwaka wa fedha 2023/2024, itatenga shilingi milioni 50 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo hilo.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itarejesha fedha Shilingi milioni 204 iliyorudishwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 ili iweze kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eng. Ezra John Chiwelesa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya Mwaka 2015 na kanuni zake iliweka utaratibu kwa halmashauri zote nchi, kuomba kibali Wizara ya Fedha na Mipango kwa fedha za miradi zinazotarajiwa kuvuka mwaka wa fedha husika kurejeshwa mfuko mkuu wa Serikali. Maombi hayo yalipaswa kufanyika siku 15 kabla ya tarehe 30 Juni ya mwaka husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo haikufuata utaratibu huo. Hivyo, hali hiyo ilisababisha fedha hizo kurejeshwa katika mfuko mkuu wa Serikali. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilipeleka shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali hiyo, na katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga shilingi milioni 750 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo. Ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Vituo vya Afya vya Rugaragata, Kalenge na Nyabuozi – Biharamulo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vituo vya afya vya Rugaragata, Kalenge na Nyabuozi ni miongoni mwa vituo vya muda mrefu na miundombinu yake inahitaji maboresho kulingana na mahitaji ya sasa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali itatenga bajeti ya shilingi bilioni 8.75 kwa ajili ya ujenzi, upanuzi na ukamilishaji wa vituo vya afya 20 katika Halmashauri, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Biharamuro iliyotengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya upanuzi wa vituo vya afya viwili kati ya vitatu vyenye mahitaji.

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa vituo vya afya chakavu ni endelevu. Ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza na kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji toka Ziwa Victoria kwenda Biharamulo?

WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa Mji wa Biharamulo ni asilimia 86. Katika kupunguza kero ya maji kwa wakazi wa mji huo, Serikali ina mipango ya muda mfupi na mrefu. Katika mpango wa muda mfupi, Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa kuboresha miundombinu ya maji Biharamulo, na kazi zinazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa chujio, bomba kuu la urefu wa kilomita 2.8, tanki la ujazo wa lita milioni moja na ununuzi wa pampu yenye uwezo wa kusukuma maji lita laki 120 kwa saa. Utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 65 na unatarajia kukamilika mwezi Juni, 2023 na kuongeza huduma ya maji kufikia asilimia 90.

Mheshimiwa Spika, katika mpango wa muda mrefu, Serikali itajenga mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Biharamulo. Usanifu wa mradi huo umekamilika na ujenzi unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2023/24.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, lini Serikali itatoa kibali cha ajira za watendaji wa kata na vijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ilikuwa na upungufu wa watendaji wa vijiji 33. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 na 2022/2023 Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Biharamuro imeajiri watendaji wa vijiji 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ya Wilaya ya Biharamuro imeomba kibali cha kuajiri watendaji wa kata saba na watendaji wa vijiji 13.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendela kuajiri watendaji wa vijiji na kata katika halmashauri zote inchini iliwemo Halmashauri ya Wilaya ya Biharamuro kadri ya bajeti itakavyoruhusu.
MHE. NDAISABA G. RUHORO K.n.y. MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza:-

Je, nini mpango wa Serikali katika kunusuru uchumi wa nchi kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni, hususani Dola ya Kimarekani?
WAZIRI WA FEDHA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za muda mfupi, wa kati na za muda mrefu katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa fedha za kigeni, hususani dola ya Kimarekani hapa nchini. Changamoto hiyo imesababishwa na athari za mgogoro wa vita kati ya Ukraine na Urusi; kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii baada ya UVIKO-19; na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Spika, sababu nyingine ni utekelezaji wa sera za fedha ambayo inalenga kupunguza ukwasi katika uchumi wa nchi mbalimbali ikiwemo Marekani katika kukabiliana na masuala ya mfumuko wa bei. Kwa ujumla matukio hayo yameathiri mnyororo wa uzalishaji, usambazaji na uhitaji wa bidhaa na huduma katika soko la dunia.

Mheshimiwa Spika, hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kupunguza athari na changamoto za upatikanaji wa fedha za kigeni ni pamoja na:-

(a) Kuongeza kiwango cha kuuza fedha za kigeni katika soko la fedha za kigeni, ambapo kati ya Machi, 2022 na Agosti, 2023 Benki Kuu ya Tanzania imeuza katika soko la fedha za kigeni zaidi ya dola za Kimarekani milioni 500;

(b) Kuongeza vyanzo vya upatikanaji wa fedha za kigeni ikiwemo ununuzi wa dhahabu;

(c) Kutekeleza mikakati ya kuongeza mauzo ya nchi za nje na kuzalisha bidhaa mbadala wa zile zinazoagizwa kutoka nje ya nchi; na

(d) Kuendelea kushirikisha benki za biashara, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni, pamoja na wadau wengine katika kuimarisha sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya usimamizi wa fedha za kigeni hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto zilizojitokeza, hali ya upatikanaji wa fedha za kigeni nchini imeendelea kuwa himilivu ambapo akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani milioni 5,246.7 mwezi Julai 2023, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi 4.7 ikilinganishwa na malengo ya miezi minne.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza:-

Je, nini kauli ya Serikali kuhusu ucheleweshaji fedha zinazotumwa Nje ya Nchi kutokana na Mabenki kuwa na uhaba wa fedha za Kigeni?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imechukua hatua kadhaa katika kupunguza athari kwenye soko la ndani la fedha za kigeni ili kusaidia shughuli za biashara na miamala kuendelea kufanyika. Hatua hizo ni pamoja na:-

a) Kuanzia Machi 2023 Benki Kuu imeongeza kiasi cha fedha za kigeni kinachouzwa katika soko la jumla la fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani milioni moja hadi Dola za Marekani milioni mbili kila siku.

b) Kuongeza kiwango kinachoruhusiwa kuuzwa kwa muamala mmoja kwa njia ya rejareja kwenye soko la fedha za kigeni baina ya Mabenki kutoka Dola za Marekani 250,000 hadi Dola za Marekani 500,000.

c) Kuhakikisha ukwasi wa Shilingi ya Tanzania unabakia katika viwango vinavyoendana na mahitaji halisi ya kiuchumi kwa kutumia nyenzo mbalimbali za sera ya fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, benki za biashara nchini zimeendelea kutunza amana ya kutosha katika akaunti kwenye benki nje ya nchi ili kufanikisha miamala ya ulipaji wa bidhaa na huduma mbalimbali zinazoagizwa na kuuzwa nje ya nchi. Aidha, nazielekeza benki zote nchini, kuhakikisha kuwa zina akiba ya kutosha ya fedha za kigeni kabla ya kupokea fedha kutoka kwa mteja anayetarajia kuzituma nje ya nchi ili kuepuka ucheleweshaji.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA K.n.y. MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Jengo jipya la Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo, mwezi Februari, 2022 iliwasilisha maombi maalum ya shilingi bilioni 3.475 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri. Maombi hayo yaliwasilishwa nje ya muda ambapo ukomo wa bajeti kwa mwaka 2022/2023 ulikuwa umeshatolewa hivyo kushindwa kutengwa kwa bajeti hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 itatenga kiasi cha shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo kwa kuwa ni kiasi ambacho kimewekwa na Wizara kwa ujenzi wa majengo ya Halmashauri. Ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Madarasa katika Shule za Msingi Nemba na Nyakanazi ambazo zina Wanafunzi wengi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wa madarasa katika shule mbalimbali za msingi kufuatia ongezeko la wanafunzi. Katika kutatua changamoto ya upungufu wa madarasa kwenye maeneo hayo shule shikizi tatu za msingi (Nemba B, Chakirabu na Kikaimara) zilianzishwa na sasa zimesajiliwa kuwa shule kamili.

Mheshiwa Naibu Spika, mwaka 2023/2024, Serikali ilijenga shule mpya ya Ilagaza katika eneo la Nyakanazi iliyogharimu shilingi milioni 400. Aidha, Serikali ilijenga Shule ya Msingi Kizota kwa gharama ya shilingi milioni 250. Vilevile, kupitia Mradi wa BOOST Serikali imejenga vyumba vinne (04) vya madarasa katika Shule ya Msingi Nyakanazi ili kuiongezea nafasi shule hiyo kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Mji wa Biharamulo kwa kukamilisha sub-station ya Nyakanazi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Nyakanazi mwezi Desemba, 2023. Aidha, kukamilika kwa kituo hicho kumeenda sambamba na ufungaji wa circuit breakers kwenye laini ndefu iliyokuwa inapeleka umeme katika Wilaya za Bukombe, Mbogwe, Biharamulo na Chato hii imepelekea kutenganisha matumizi ya umeme kwenye wilaya hizo na kwa sasa kila wilaya inajitegemea hivyo kupunguza kukatika kwa umeme ndani ya Wilaya ya Biharamulo. TANESCO inaendelea na matengenezo ya kuimarisha miundombinu ya kusafirishia na kusambaza umeme wilayani humo ili kuwe na umeme wa uhakika, ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza:-

Je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha Wahitimu wa Mafunzo ya Jeshi USU wanapata haki ya ajira sawa na Watanzania wengine?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, taasisi zinazounda Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori na Misitu hufuata utaratibu wa ajira kwa kuzingatia miongozo iliyopo katika Utumishi wa Umma, ambapo taasisi huomba kibali cha ajira kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Baada ya kupata kibali, hutolewa tangazo la ajira kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma pamoja na kuainisha vigezo vya mwombaji kwa kuzingatia Miongozo ya Utumishi wa Umma, Kanuni na Amri za Jumla za Jeshi la Uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia utaratibu huo wa ajira, kila Mtanzania mwenye sifa ana haki sawa ya kuomba na kupata nafasi ya kazi katika Taasisi za Jeshi la Uhifadhi.