Supplementary Questions from Hon. Khadija Shaaban Taya (11 total)
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwa kuwa Serikali ilikuwa na nia njema sana ya sisi kuhamia Dodoma, na Dodoma sasa imekuwa ni sehemu ambayo ina mrundikano wa watu na maji pia yamekuwa hayatoshelezi. Je, ni lini Serikali itatekeleza ile adhma yake ya kuleta mradi wa Ziwa Victoria mpaka hapa Dodoma ili tuweze kupata maji hapa Dodoma?
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru sana. Kubwa ni kwamba tulishafanya kikao mimi pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Dodoma na ukiwa kama mwenyekiti. Juzi Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo, na ameenda mbali zaidi ya kusema ukizingua, tutazinguana.
Mheshimiwa Spika, nikiwa kama Waziri wa Maji na timu yangu tumeshajipanga na tumeshafanya stadi tunahangaika kutafuta fedha…
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba niipongeze Serikali kwa majibu mazuri na wameonesha kabisa kwamba mmeongeza vitabu. Pamoja na hayo yote naomba niongeze swali la kuhusu watu wenye uoni hafifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wenye uoni hafifu shuleni wanapata taabu sana, kwa sababu Walimu wengi hawafahamu namna ya kuwafundisha hawa watu ili waweze kuelewa. Wanapata tabu ubaoni na kwenye karatasi kwa sababu maandishi yanakuwa ni madogo. Je, Serikali haioni haja ya kupeleka mwongozo kwenye shule zote na Walimu wote wafahamu namna gani ya kuwafundisha watoto wenye mahitaji maalum, hasa hao wenye uoni hafifu ambao wengi ni wenye ulemavu wa ngozi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tunafahamu kabisa, katika suala la afya na maradhi watu wenye ulemavu wanapata shida sana na wanapata maradhi kutokana na hali ya usafi na mazingira pale shuleni. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha miundombinu, kuongeza vyoo vya watu wenye ulemavu shuleni ili hawa watu waweze kusoma vizuri? Kwa sababu tunaamini kabisa kwamba elimu ndio ufunguo wa maisha na elimu ndiyo mkombozi wa watu wote wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khadija taya, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli anayoyazungumza Mheshimiwa, kwamba wenzetu wenye uoni hafifu, hasa wenzetu wenye ulemavu wa ngozi wanapata changamoto shuleni. Naomba nimhakikishie Mheshimwia Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali yetu hii ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan tumejipanga vyema katika kuhakikisha kwamba tunakwenda kuishughulikia changamoto hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Wizara iko mbioni kutekeleza au kukamilisha mwongozo ambao utakwenda kushughulikia eneo hili la wanafunzi wetu wenye changamoto ya uoni hafifu, tukishirikiana na wenzetu wa Shirika Binafsi la Under the Same Sun. Kwa hiyo nimwondoe kabisa wasiwasi, kwamba mwongozo huo uko mbioni kuja na mara utakapokamilika na kusainiwa tutausambaza kwenye maeneo hayo ili kuhakikisha kwamba tunaitatua changamoto hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie vile vile Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yetu tayari imeweza kusambaza vitabu vyenye maandishi makubwa kwa ajili ya wenzetu hawa ambao wana uoni hafifu. Kwa hiyo kule kwenye shule zetu zote za msingi pamoja na sekondari mambo yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anazungumzia suala la miundombinu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mgawanyo wa fedha za UVIKO-19, zile ambazo tulizipata kupitia Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI zaidi ya Shilingi bilioni 2.4 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo zaidi ya 2200 kwa ajili ya wanafunzi wetu wenye mahitaji maalum kupitia hizi za UVIKO-19 na zile za GPE lenses na mchakato huu unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kupitia mradi wetu wa EP4R umeweza kujenga jumla ya matundu 4,549 kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule zetu za msingi na sekondari. Tunaendelea kuboresha miundombinu hii kwa kuhakikisha na wao tunawatengenezea mazingira wezeshi ili isiwe changamoto kwao katika kupata elimu yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita, imeanzisha vyuo vya watu wenye ulemavu, kati ya mafunzo ambayo wanayotoa pale mojawapo ni kutengeneza viatu na hapo hapo katika Wizara hii hii wamefungua kiwanda cha kutengeneza viatu pale magereza Mkoa wa Kilimanjaro; je, katika hiki kiwanda walemavu wameajiriwa na kama wameajiriwa ni wangapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, kwa kuthibitisha spirit ile ile ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji mzuri wa sheria hii ya watu wenye ulemavu, katika kile kiwanda ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja zoezi bado kwanza kiko katika hatua ya awali ya kuanza kufanya mobilization na ukamilishaji wa ujenzi bado haujatimia.
Mheshimiwa Spika, lakini katika uthibitisho wa hilo kwamba tunazingatia hili kama Serikali, Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu katika nafasi za walimu 8,000 zilizotoka mwaka 2020 watu wenye ulemavu 242 waliajiriwa ambao ni asilimia 3.2. Sambamba na hiyo katika nafasi za mwaka 2021 za ualimu zilizotolewa zilikuwa nafasi 6,949 watu wenye ulemavu 145 waliajiriwa ambao ni sawa na asilimia mbili.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo pia mwaka 2022 katika usimamizi na utekelezaji mzuri wa Serikali ya Awamu ya Sita, ajira zilizotolewa 9,800 za nafasi ya ualimu watu wenye ulemavu 261 walipata sawa na asilimia
2.66. Katika sekta ya afya na maeneo mengi sababu ya muda nafasi 7,612 ambazo zilitolewa watu wenye ulemavu waliopata nafasi hiyo ni 0.63 kulingana na sifa na vigezo ambavyo viliwekwa.
Mheshimiwa Spika, katika Serikali hii tumeweka minimum standard, kwamba hata vile viwango vya ufaulu tunaviangalia katika hali ambayo yule anakuwa sifa kwa sababu watu wenye ulemavu wanakuwa wachache katika uombaji wa nafasi hii.
Kwa hiyo, tutaendelea kuzingatia sheria na kuhakikisha kwenye private sector na Serikali tunazingatia takwa hili la kisheria la kuajiri watu wenye ulemavu, kwa sababu kufanya hivyo pia ni ibada kwa nchi.
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na kuonyesha namna gani Serikali imejipanga kwa kutumia hizi takwimu.
Mheshimiwa Spika, kwa kutumia takwimu zilizopita, za 2010 na sasa hivi tuko 2022/2023 kwenye maandalizi ya bajeti ya Mpango wa mwaka 2022/2023.
Je, Serikali imejipangaje kupitia Wizara yake hii ya Fedha na Mipango kuondoa matatizo ya watu wenye ulemavu; kwa sababu hii Wizara ndiyo ambayo ina bajeti Kuu ya Serikali? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha Sensa yetu tukapata takwimu sahihi na kuweza kujua idadi ya watu wenye ulamavu na aina ya ulemavu ambayo ipo nchini, tutaandaa mipango rasmi na kutoa vipaumbele ambavyo vinaweza kuingizwa hadi katika bajeti yetu kwa maslahi ya wananchi wote.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan haiko tayari kuacha kundi lolote nyuma, makundi yote yataainishwa katika vipaumbele vya nchi hii na kwa maslahi ya umma. Ahsante. (Makofi)
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu zuri: -
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza; kwa kuwa, Serikali inafahamu fika michezo sanaa na tamaduni ni moja ya suluhu ya kuongeza ajira katika nchi yetu. Sasa Serikali haioni sababu ya kuipa kipaumbele michezo, sanaa, ili waweze kutatua tatizo la ajira kwa watu wenye ulemavu?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khadija, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa naibu Spika, ahsante. Swali lake la kwanza alipenda kufahamu ni kwa kiasi gani Wizara tunahakikisha kwamba, tunaendelea ku- promote michezo hii ya wtu wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yetu inahakikisha na tunashirikiana na vyama mbalimbali, katika miundombinu tunahakikisha watu wenye ulemavu wanapewa kipaumbele, hata katika ujenzi wetu wa shule 56, miongoni mwa shule ambazo tumezitenga zipo za watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, tunaendelea kuwashirikisha na kuwajengea miundombinu.
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana Serikali kwa majibu mazuri na mipango mizuri na mikakati mizuri kwa ajili ya Bima ya Afya kwa watu wote. Naomba niulize swali langu la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwamba watu wenye ulemavu ni watu ambao hawajiwezi wengine. Je, Serikali haioni haja sasa ya kuweka dirisha maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu kama vile kwa Wazee?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Kwa kuwa Bima ya Afya mara nyingine vipimo vingine havifanyiki. Je, Serikali haioni haja sasa kwamba vipimo vya Kansa ya Saratani ya Ngozi viweze kufanyika bure katika hizo Bima ambazo mnaziandaa kuja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, moja amesema kuwa na dirisha maalum kwa ajili ya watu wenye Ulemavu. Hili ni wazo zuri sana tunalichukua, vilevile pamoja na kuwa na dirisha lakini ni katika kila infrastructure ya hospitali kwenye wodi na kila mahali kuwepo na sehemu ambazo ni maalum zinazowezesha watu wenye ulemavu kuweza kupata huduma kirahisi kama wanavyopata watu wengine.
Meshimiwa Spika, nimeona vilevile amezungumzia na watu wenye ulemavu wa ngozi. Sasa hivi kwa mfano kwenye Hospitali ya Kanda ya KCMC wamepelekwa watu kutoka Hospitali mbalimbali za Mikoa. Moja kujifunza kwa ajili ya kuzalisha dawa maalum kwa ajili ya wale watu wenye ulemavu wa ngozi hasa ile screening ile ya kujipaka kwa ajili ya kuzia miale ya jua. Kwa hiyo, hayo yanaboreshwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni suala la kwamba kuna baadhi ya mahitaji ambayo ya kitiba ambayo wanahitaji baadhi ya Walemavu ambayo hayapo kwenye Mfuko wa Bima ya Afya. Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tunaenda kuboresha kuja na Muswada wa Bima ya Afya kwa watu wote, ni wakati wa muafaka wa sisi kuhakikisha kwamba vitu vyote hivyo vimeingia kwenye utaratibu. Lakini wakati kabla hatujafikia hilo la Sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya, naomba mimi na wewe tukae unianishie hayo mambo maalum ili Mheshimiwa Waziri wa Afya aweze kuyafanyia kazi mapema, ahsante. (Makofi)
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika nashukuru sana, ningeomba kujua kwenye hii Wizara ilitolewa milioni 60 kwa ajili mafuta ya watu wenye uarubino. Nataka nifahamu ni lini sasa yale mafuta yataanza kusambaa Tanzania nzima, kwa sababu nina amini kuna Wabunge hapa wananiuliza kila siku wanahitaji haya mafuta? (Makofi)
NAIBU WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE.PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa
Spika, hili ni la kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu aliona umuhimu huo. Tulikuwa tunapata mafuta kutoka nje ya nchi sasa yanatengenezwa pale KCMC, na gharama zinalipwa na Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Awamu ya sita. Suala la usambazaji na ufikaji wa mafuta ni suala la uratibu tu ambalo nitaomba Mheshimiwa Mbunge niwasiliane naye kama kuna changamoto sehemu za wao kuweza kuyapata; lakini pia tutaweka utaratibu wazi wa kuweza kuona ni namna gani kila eneo wataweza kuyapata mafuta haya muhimu kwa ajili ya watu wetu wenye ulemavu, ahsante sana.
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa watu wengi hawafahamu uwepo wa Sheria ya Manunuzi ya asilimia 30 kwa makundi maalum. Sasa je, Serikali ina mkakati gani kueneza uelewa juu ya uwepo wa sheria hii ya asilimia 30 ya manunuzi kwa makundi maalum ambayo ni wanawake, vijana na watu wenye ulemavu? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, labda kwa kuwa linakwenda kwenye sekta zote ninaomba tu niseme kwamba kwa sababu Serikali inafahamu umuhimu wa makundi hayo tutajipanga ndani ya Serikali ili sekta zote zihakikishe zinasimamia jambo hili na makundi hayo maalum ambayo yamekwisha kutamkwa kwenye sheria hiyo waweze kunufaika. Hiyo ni fursa muhimu sana kwa maendeleo na ustawi wa Taifa. (Makofi)
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kutokana na tatizo la maji katika Wilaya hizi za Mkoa huu wa Dodoma, naomba niulize swali kwamba ni lini Bwawa la Farkwa litaanza ujenzi kama ilivyo katika mkakati wa Serikali? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Khadija Taya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kusema nina furaha kubwa sana kwa sababu, sasa ujenzi wa Bwawa la Farkwa upo tayari kwenye pipe. Ni wiki iliyopita tu wameweza kusaini mkataba wa kazi hii kuanza na tutarajie kazi itakwenda vizuri kwa sababu ni mradi ambao tunautarajia sana katika kupunguza changamoto ya maji kwenye Jiji la Dodoma. (Makofi)
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini kwa kuwa kumekuwepo na minong’ono ya kutokukaa kwa Baraza hili, sasa naomba Serikali iuambie umma wa Tanzania ni lini mara ya mwisho hili Baraza limekaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante. Baraza hili mbali na minong’ono ambayo inasikika lakini uhalisia wa Serikali ni kwamba, Baraza hili tayari lilikwishaundwa na Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa kifungu cha 11 ambaye ndiye anakuwa na wajibu wa kumteua Mwenyekiti na Mwenyekiti wake ni Dkt. Kija Luhende na Katibu wake anakuwa ni Mkurugenzi wa masuala ya watu wenye ulemavu. Mara ya mwisho wamekaa katika kikao chao mwezi wa Disemba mwaka 2023.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo majukumu yanaendelea kutekelezwa na wajumbe wanakuwa 15 ambao wanateuliwa na Mheshimiwa Waziri na tayari wajumbe hao wapo na kazi zinaendelea kufanyika. Hivyo, kazi mojawapo ambayo waliifanya ni pamoja na kushauri kuhusiana na marekebisho ya sera ya watu wenye ulemeavu ambayo kwa sasa imedumu kwa kipindi cha muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, pia jukumu la pili, ni pamoja na kwenda kufanya maandalizi ya kuboresha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010. Ahsante.
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, pamoja na majibu hayo nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa tatizo hilo bado lipo na linajitokeza. Je, ni kwa kiasi gani watendaji wanaufahamu wa sera hii ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri umeisema?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je, sasa Serikali haioni haja ya kutoa mwongozo tena mara nyingine kwa watendaji wanaohusika na masuala ya sherehe za Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Keysha, kama nilivyojibu jibu la msingi tuna sera na sheria. Nitoe rai kwa wale wanaoandaa shughuli za Serikali na sisi Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Waziri wetu Mheshimiwa Jenista, tumekuwa tukifanya jambo hili kwa pamoja. Maadhimisho mbalimbali ya sherehe tuna kitengo cha sherehe waendelee kuweka nafasi hizi za watu wenye Ualbino na watu wengine kwa sababu tunaweka masuala ya tenti kuweka vizuri ili waweze kukaa. Tuna mkakati gani? Tunaendelea kushirikiana na Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS) pamoja na wadau wengine wanaofanya kazi kwenye eneo la watu wenye ulemavu kujengea elewa jamii ili kufahamu haki za watu wenye ulemavu na sera.
Mheshimiwa Spika, pia tuko kwenye marekebisho ya Sera ya Taifa ya Watu Wenye Ulemavu ambayo pia nayo inagusa kundi la watu wenye Ualbino. Kwa hiyo nimtoe mashaka Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya maarufu kama Keysha kwamba mambo yanaenda vizuri Serikali ya Awamu ya Sita, Mheshimiwa Rais, Daktari Samia tunaendelea kuwajali watu wenye ulemavu na watu wenye Ualbino. Ahsante. (Makofi)