Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Twaha Ally Mpembenwe (10 total)

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itahakikisha minada ya zao la Korosho na Ufuta inafanyika kwa wakati mmoja ili kuondoa mporomoko wa bei kwa baadhi ya maeneo yanayolingana kwa misimu sawa ya kuvuna mazao hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally, Mbunge wa Kibiti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatumia mifumo miwili katika minada. Mfumo wa kwanza ni mfumo wa TMX na wa pili ni mfumo wa kutumia sanduku ambao umekuwa ukitumika katika maeneo mengi kwa muda mrefu katika nchi yetu. Serikali itaendelea kutumia mifumo yote hiyo miwili ili kuhakikisha minada inafanyika kwa wakati mmoja kwenye maeneo yenye msimu wa mavuno unaofanana ikiwemo Mkoa wa Pwani ili kuongeza ushindani wa bei na uwazi katika mauzo ya Korosho, Ufuta na mazao mengine.

Mheshimiwa Spika, kuanzia msimu wa 2019/2020 Serikali kupitia Bodi ya Korosho, Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Soko la Bidhaa kwa kushirikiana na Vyama Vikuu vya Ushirika, imeanza kutekeleza mauzo ya Korosho na Ufuta katika minada ya kielektroniki sambamba na mfumo wa uwekaji zabuni kwa njia ya sanduku kwa zao la Korosho.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya mfumo wa kielektroniki yatasaidia kuendesha minada kwa wakati mmoja na kujenga mazingira bora ya ushindani na kuondoa changamoto iliyopo sasa ambapo baadhi ya wanunuzi hulazimika kwenda kwenye minada inayofanyika kwa nyakati tofauti. Ili kuhakikisha mkulima anapata bei nzuri, Serikali inasimamia suala la ubora na uzalishaji wa tija ili kuhakikisha mazao ya Korosho, Ufuta na mazao mengine yanafikia viwango vya ubora vinavyohitajika sokoni, pamoja na kuimarisha uwazi katika uendeshaji wa minada kwa lengo la kuimarisha ushindani wa bei.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza hatua hizo, Serikali kupitia Bodi ya Korosho ya Tanzania na Soko la Bidhaa, zimeweka utaratibu wa kusajili wanunuzi wa Korosho na Ufuta mapema kabla ya msimu wa mazao kuanza, na kuhakikisha mazao yaliyokusanywa na wakulima kupitia Vyama vya Ushirika yanatangazwa kwa wanunuzi mapema ili kuvutia wanunuzi wengi watakaoshindana kwa bei kulingana na ubora wa mazao yao ili mkulima aweze kuuza mazao yake kwa bei itakayompatia faida.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa uamuzi wa kuwaruhusu Wavuvi wa Kamba Koche kuvua kuanzia mwezi Desemba hadi Julai kila mwaka?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Meshimiwa Mweyekiti, kwa niaba wa Waziri ya Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe Mbunge wa Kibiti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mweyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003 pamoja na kanuni zake za Mwaka 2009 na Marekebisho yake ya mwaka 2020, Serikali haijawahi kuzuia uvuvi wa Kamba Koche au maarufu kama prawns. Hata hivyo, Serikali imeweka utaratibu kwa ajili ya uvuvi wa Kambamiti kwa wavuvi wadogo na wakubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi wa Kambamiti kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo unaruhusiwa kufanyika kuanzia mwezi Machi hadi Septemba kila mwaka kwa ukanda wa Kaskazini unaohusisha Wilaya za Bagamoyo, Pangani Chalinze na kuanzia mwezi Aprili hadi Agosti kila mwaka kwa ukanda wa Kusini unaohusisha Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Kilwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi kilichobaki kimeachwa ili Kambamiti kwa maana ya prawns waweze kuzaliana na kukua. Maamuzi haya yamefanyika baada ya taarifa za utafiti wa Kisayansi na kwa kuzingatia uendelevu wa Rasilimali hii.

Meshimiwa Mweyekiti, Serikali imekuwa ikisisitiza kwa wadau wote wa Uvuvi hususani Uvuvi wa Kambamiti yaana Prawns kufanya shughuli zao kwa mujibu wa Sheria na taratibu zilizopo kwa lengo la kuwa na uvuvi endelevu kwa maslahi mapana ya vizazi vilivyopo na vile vijavyo.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha mpango wa uvunaji wa mikoko kwa wananchi wanaoishi maeneo ya Delta wanaotegemea zao hilo kuendesha shughuli zao za kimaisha?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba ama napenda kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, misitu ya mikoko ina umuhimu mkubwa katika nyanja za kiuchumi na kimazingira, kutokana na kuvamiwa kwa misitu hii kwa kufanya shughuli zisizokubalika kiuhifadhi kama vile kilimo, ufugaji utayarishaji wa chumvi, Serikali ilisimamisha uvunaji wa mikoko yote kote nchini ili kutoa fursa ya kuweka mipango na mikakati ya matumizi endelevu. Hivyo, Wizara inaandaa mpango na mwongozo wa usimamizi wa matumizi endelevu ya misitu ya mikoko utakaotoa utaratibu wa uvunaji. Mipango na miongozo hiyo ipo katika hatua za mwisho za maandalizi na inatarajiwa kukamilika robo ya kwanza ya mwaka 2021/2022 na baada ya kukamilika utaanza kutumika.
MHE. SUBIRA K. MGALU K.n.y. MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza Ujenzi wa barabara ya Nyamisati hadi Bungu katika Jimbo la Kibiti?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Bungu – Nyamisati yenye urefu wa kilometa 40.2 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) iliyopo katika Wilaya ya Kibiti, Mkoa wa Pwani.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2021/ 2022, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania, imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii. Taratibu za kumpata mshauri elekezi wa kufanya kazi hiyo, ziko katika hatua za mwisho za kusaini mkataba. Baada ya usanifu kukamilika na gharama kujulikana Serikali itatafuta fedha za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea na maandalizi ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania, inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii. Ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka na katika mwaka huu wa fedha wa 2021/2022 jumla ya Shilingi milioni 732.67 zimetengwa. Ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO K.n.y. MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibiti?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana na kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu nikiwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria nimshukuru Mwenyezi Mungu lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kuendelea kuniamini naahidi kwamba nitaendelea kufanya kazi kwa unyenyekevu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria sasa naomba kujibu swali Mheshimiwa Twaha Ally kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mahakama inaendelea kutekeleza mpango wake wa ujenzi na ukarabati wa majengo katika ngazi zote. Katika mpango huo, Mahakama ya Wilaya ya Kibiti imepangwa kujengwa katika mwaka wa fedha 2023/2024. Aidha, maandalizi ya awali yameshaanza kufanyiwa kazi na kukamilika, ikiwemo usanifu wa mradi, pamoja na maandalizi ya kabrasha za zabuni. Hivyo, mara baada ya bajeti kuanza, utekelezaji wa mradi huu utaanza mara moja. Ahsante.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza kugawa maeneo ya kilimo kwa njia ya mnada katika Bonde la Mto Rufiji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Bonde la Mto Rufiji ni miongoni mwa mabonde 22 ya kimkakati na linakadiriwa kuwa na eneo lenye ukubwa wa hekta 64,896 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bonde hilo ili kujua ukubwa wa eneo na gharama halisi za kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji katika bonde hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, baada ya upembuzi yakinifu kukamilika, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Mkoa wa Pwani, zitaandaa Mpango shirikishi wa namna bora ya ugawaji wa maeneo ya kilimo katika bonde hilo ili kuongeza uzalishaji na tija.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE K.n.y. MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Ofisi ya Wilaya ya TANESCO – Kibiti?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa umahususi na umuhimu wa Wilaya ya TANESCO Kibiti, TANESCO inafanya tathmini ya gharama kuangalia namna ya kujenga jengo lake la ofisi ili kuepuka kuendelea na ofisi iliyopo sasa ambayo ni ya kupanga.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia, kwa sasa huduma nyingi zinatolewa kwa njia ya mtandao. Aidha, programu kama vile NIKONEKT, NIHUDUMIE, kununua umeme (LUKU) na nyinginezo zimeanzishwa ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wateja bila kulazimika kwenda ofisi za TANESCO. Aidha, pamoja na faida nyingine programu hizi zimesaidia kuondoa vishoka waliokuwa wanawalaghai wateja katika ofisi za TANESCO.

Mheshimiwa Spika, shirika limeelekeza fedha nyingi katika kuanzisha na kuboresha huduma zinazotolewa kwa njia ya mtandao. Sambamba na hili, shirika linaendelea kuanzisha viunga/ofisi ndogo zitakazokuwa karibu zaidi na wananchi ili kuwahudumia kwa haraka kwa huduma chache ambazo hazipatikani kwa mtandao kwa sasa. Katika Wilaya ya Kibiti, TANESCO imeanzisha viunga viwili katika maeneo ya Hanga na Bungu ili kusogeza huduma kwa wateja. Ahsante.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE K.n.y. MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Bungu hadi Nyamisati Wilaya Kibiti?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Bungu hadi Nyamisati yenye urefu wa kilometa 40.03. Kazi ya usanifu inatarajiwa kukamilika tarehe 30 Juni, 2023. Baada ya kukamilika kwa usanifu, Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ukarabati wa shule chakavu za msingi Jimbo la Kibiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Jimbo la Kibiti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza ukarabati wa shule chakavu ambapo katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali ilipeleka shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukarabati wa Shule ya Msingi Kiasi. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2023/24, Serikali imepeleka shilingi milioni 180 kwa ajili ya kukarabati shule chakavu za msingi katika Jimbo la Kibiti ambapo jumla ya shule nne zitakarabatiwa ambazo ni Pongwe (maradasa matatu yalikarabatiwa), Mchinga (madarasa mawili), Saninga (madarasa mawili) na Misimbo (madarasa mawili).
MHE. SUBIRA K. MGALU K.n.y. MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza:-

Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuweka huduma za Wakala wa Forodha katika Bandari ya Nyamisati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembene, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, maandalizi ya kutoa Huduma za Wakala wa Forodha katika Bandari ya Nyamisati yanaendelea ambapo Novemba, 2023, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilifanya tathmini kujiridhisha na mawanda ya shughuli zinazofanyika katika eneo hilo. Matokeo ya tathmini hiyo yanaonesha kuwa, eneo hilo lina uhitaji wa huduma za forodha. Hivyo, Serikali inatarajia kufungua ofisi za forodha katika Bandari ya Nyamisati mwaka 2024/2025. Ahsante.