MHE. ABDI HIJA MKASHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni muda gani tangu Jeshi la Polisi lifanye tathmini ya ukarabati wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ilifanyika mwaka jana, 2023. Nami nimhakikishie Mheshimiwa Mkasha, kwa sababu, liko kwenye bajeti ya 2023/2024, mara fedha hizo ambazo tayari zimeombwa Hazina zitakapotoka, kituo hiki kitaanza kukarabatiwa. (Makofi)
MHE. ABDI HIJA MKASHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina swali moja la nyongeza ambalo lina sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -
(a) Naomba nitoe taarifa katika hili Bunge kama ndani ya Wilaya yetu ya Micheweni bahati nzuri Ofisi ya Uhamiaji tunayo lakini kubwa ni suala zima la makazi kwa wale askari wetu. Je, ni lini ujenzi huu utaanza?
(b) Je, Waziri yupo tayari kufuatana nami ili twende akajionee uhalisia wa hali ilivyo katika eneo lile? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, ujenzi wa majengo haya ya makazi ya Askari wa Uhamiaji katika Wilaya ya Micheweni itaanza katika mwaka wa fedha 2023/2024 na tayari tumetenga shilingi 1,250,000,000 ili kazi ianze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu kuongozana na Mheshimiwa Mbunge, nipo tayari kuongozana naye kwenda Micheweni baada ya Bunge la Bajeti, kwa hiyo, asiwe na wasiwasi. ahsante sana, (Makofi)