Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Maimuna Salum Mtanda (21 total)

MHE. MAIMUNA S. MTANDA Aliuliza:-

Halmashauri ya Wilaya ya Newala ina Kata 22 na Vijiji 107, lakini ina Vituo vya Afya vitatu tu, kati ya 22 vinavyohitajika.

Je, Serikali haioni haja ya kujenga Vituo vipya vya Afya katika Halmashauri ya Newala ili kuboresha huduma za Afya kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM) kwa kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Kuanzia mwaka 2015 hadi Septemba 2020, Serikali imejenga Zahanati 1,198; imejenga na kukarabati Vituo vya Afya 487 na imejenga Hospitali za Halmashauri102.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 na 2019/2020, Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Newala kiasi cha Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri na Shilingi milioni 400 kwa ajili kufanya ukarabati wa Kituo cha Afya Kitangari. Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni moja (1) kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri na Shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma matatu ya Zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa awamu kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itaongeza bajeti ya barabara za Newala Vijijini ambayo imetengewa fedha za kilometa 340 wakati zina mtandao wa barabara wa kilometa 960?

(b) Je, Serikali inatoa msaada gani wa dharula kwenye matengenezo ya barabara za vijijini vinavyozungukwa na milima au mito kama vile Mkongi – Nanganga, Mikumbi – Mpanyani, Namdimba – Chiwata, Mkoma – Chimenena na Miyuyu – Ndanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Newala ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 960.04. Serikali imekuwa ikiongeza fedha za bajeti ya matengenezo ya barabara katika Halmashauri ya Newala mwaka hadi mwaka. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, shilingi milioni 939.27 zilitengwa kwa ajili ya kuzifanyia matengenezo barabara zenye urefu wa kilometa 343.86, mwaka wa fedha 2020/2021, shilingi milioni 976.88 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 320.38.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.056 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 277.35 na ujenzi wa mifereji yenye urefu wa kilometa 1.37.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 barabara ya Mkwiti - Lochino - Nyangao yenye urefu wa kilometa 11.1 imefanyiwa matengenezo kwa gharama ya shilingi milioni 84.78. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 barabara hii imetengewa shilingi milioni 56.32. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi milioni 87 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Maputi – Mikumbi – Miyuyu – Ndanda Kibaoni yenye urefu wa kilometa 17.5 ikiwa sehemu ya kipande cha Mlima Miyuyu – Ndanda na shilingi milioni 56 kwa ajili ya matengenezo ya maeneo korofi yenye urefu wa kilometa 3.5 ili iweze kupitika hadi Kijiji cha Lochino.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itaimarisha na kuboresha miundombinu ya maji ya Mamlaka ya Maji Makonde ili Wananchi waweze kupata maji ya uhakika?

(b) Je, Serikali inachukua hatua gani za dharura kuboresha upatikanaji wa maji Newala Vijijini ambapo kwa sasa uzalishaji ni ujazo wa lita 6,700 tu kwa siku badala ya lita 23,741?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya maji ya Mamlaka ya Maji Makonde inayohudumiwa Wilaya za Newala, Tandahimba na Nanyamba.

Katika kutatua changamoto hiyo, Serikali imeendelea na ukarabati wa miundombinu ambapo katika mwaka huu wa fedha 2020/2021 kazi zinazofanyika ni kukarabati mitambo na mfumo wa umeme katika vituo vya kuzalishia na kusukuma maji. Utekelezaji wa kazi hizi unalenga kuongeza uzalishaji wa maji kutoka meta za ujazo 6,700 kwa siku hadi meta za ujazo 11,116 kwa siku, kazi inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupata suluhisho la kudumu la tatizo la maji katika maeneo hayo, Serikali kuanzia mwaka 2021/2022 imepanga kutekeleza kazi mbalimbali ikiwemo kuongeza idadi ya visima vya kuzalisha maji kutoka 6 hadi 12 kwenye Bonde la Mitema pamoja na kupanua miundombinu ya kusafirisha maji uchimbaji wa visima utaongeza uzalishaji wa maji kutoka meta za ujazo 11,116 hadi Meta za ujazo 23,741 kwa siku. Kukamilika kwa kazi hizo kutaboresha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 58 za sasa hadi asilimia 95.

Vilevile Wizara ya maji kupitia RUWASA katika mwaka wa fedha 2020/2021, imeendelea na utekelezaji wa miradi ya maji Mchemo na Chiule iliyotarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2021 na miradi ya maji Mtongwele, Miyuyu na Mnima inayotarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2021. Katika mwaka 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni
1.95 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali katika Wilaya Newala Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katika mpango wa muda mrefu, Serikali ilipata mkopo kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim India jumla ya dola za Marekani Milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa Miji 28 ukiwemo mradi wa Makonde; ambapo maeneo yatakayonufaika ni vijiji 155 vya Wilaya ya Newala. Ujenzi unatarajiwa kuanza wakati wowote katika mwaka wa fedha 2020/2021.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mkwiti – Amkeni inayounganisha Mkoa wa Lindi na Mtwara kupitia Mtama?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mkwiti – Amkeni yenye urefu wa kilometa 74.23 inayounganisha Wilaya ya Tandahimba na Newala katika Mkoa wa Mtwara na Wilaya ya Lindi Vijijini mkoa wa Lindi unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, jumla ya shilingi milioni 1,807.00 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa kilometa tatu ambapo jumla ya kilometa 2.8 zimekamilika kujengwa na kazi za ujenzi zinaendelea kwenye kipande chenye urefu wa mita 200. Wakati ujenzi kwa kiwango cha lami ukiendelea kutekelezwa kwa awamu, Wizara yangu itaendelea kuifanyia matengenezo barabara hiyo ili iweze kupitika majira yote ahsante.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya ujenzi wa mnara wa mawasiliano wa Halotel katika Kata ya Chilangala ambapo mkataba ulisainiwa mwaka 2020 lakini mpaka Septemba, 2021 mradi huo haujaanza?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARl alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) katika zabuni ya awamu ya nne ya kufikisha mawasiliano maeneo ya vijijini, iliingia mkataba wa kufikisha huduma ya mawasiliano ya simu katika Kata 114 ikiwemo Kata ya Chilangala na Kampuni ya Halotel (Viettel) mnamo tarehe 24 Januari 2020. Utekelezaji wa mkataba huo ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi tisa yaani tarehe 23 Oktoba 2020. Lakini kutokana na changamoto ya UVIKO-19 utekelezaji wa mradi huo ulichelewa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kutokana na ucheleweshaji wa utekelezaji wa mradi huo ulipelekea watoa huduma wengine kuboresha huduma za mawasiliano katika kata hiyo ambapo Kata ya Chilangala ina mawasiliano ya Mtandao wa Tigo ambao wana minara miwili katika Vijiji vya Chilangala na Namdimba. Hivyo basi, Serikali haitojenga mnara huo katika Kata ya Chilangala, na hivyo kuzielekeza fedha hizo katika maeneo mengine yenye changamoto zaidi za mawasiliano. Ahsante.
MHE. YAHYA A. MHATA K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ukarabati wa shule za msingi kongwe ambazo zimechakaa na majengo yake ni mafupi ulikinganisha na yanayojengwa kwa sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa shule kongwe za msingi zilizo katika hali ya uchakavu. Kazi ya kuzikarabati shule hizi ilishaanza kupitia miradi mbalimbali ya elimu.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu kwa kujenga na kukarabati miundombinu mbalimbali ya shule za msingi nchini. Katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali kupitia Programu ya EP4R (Lipa Kulingana na Matokeo) imeendelea na ujenzi wa vyumba vya madarasa ya shule za msingi 1,970, matundu ya vyoo 5,303, nyumba za walimu wa msingi 17. Ujenzi huu ni kwa ajili ya kuboresha mazingira ya miundombinu ya shule za msingi zikiwemo shule kongwe ambazo zina miundombinu chakavu. Vilevile kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 (TCRP), Serikali imejenga vyumba 3,000 vya madarasa katika vituo shikizi 970.

Mheshimiwa Spika Serikali kupitia Mradi wa BOOST utakaotekelezwa katika shule za msingi inatarajiwa kujenga madarasa 12,000 katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 na itaendelea kutumia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri kujenga na kukarabati shule za msingi kongwe nchini.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufikisha mbegu za Soya kwa Wakulima wa Jimbo la Newala Vijijini hasa katika Kata za Tarafa ya Chilangala?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijin,i kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2022/2023 Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Newala imetenga shilingi 6,000,000 za kuwezesha ununuzi wa kilo 3,000 za mbegu bora za soya. Mbegu hizo zitasambazwa kwa wakulima wa soya katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala ikiwemo Tarafa ya Chilangala.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeiwezesha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania kituo cha Utafiti (TARI) Naliendele kilo 2,260 za mbegu ya msingi ya soya itakayotumika kuzalisha tani 90 za mbegu iliyothibitishwa ubora ili kuimarisha upatikanaji wa mbegu katika Mikoa ya Kusini kwa msimu wa mwaka 2023/2024 na kulifanya zao hilo kuwa la tatu kwa wakulima wa kusini baada ya korosho, ufuta na sasa Soya.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje katika kuondoa changamoto ya ucheleweshwaji wa viuatilifu kwa wakulima wa zao la korosho?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa huko nyuma kumekuwa na ucheleweshwaji wa viuatilifu. Katika kuondoa changamoto ya ucheleweshwaji wa pembejeo unaosababishwa na mlolongo mrefu wa manunuzi kutoka kwa mzalishaji hadi kumfikia mkulima, Serikali inasimamia uagizaji wa pembejeo kwa kupitia Kamati ya Pamoja ya Pembejeo inayoundwa na Vyama vya Ushirika ambavyo kimsingi ni wakulima wenyewe. Kutokana na utaratibu huo, jukumu la Serikali ni kufuatilia mchakato huo ili manunuzi yafanyike kwa muda muafaka na pembejeo kuwafikia wakulima kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2022/2023 Vyama Vikuu vimeagiza sulphur ya unga tani 25,000, viuatilifu vya maji lita milioni 1.5 pamoja na mabomba ya kupuliza 35,000 kwa ajili ya msimu wa 2022/2023 na hadi kufikia Aprili moja jumla ya tani 1,600 na lita 730,724 tayari zimeshapokelewa na kiasi kilichobaki kinatarajiwa kupokelewa kufikia mwisho wa mwezi Mei.
MHE. YAHYA A. MHATA K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, hali ya upatikanaji wa vitabu vya kufundishia na kujifunza katika shule za msingi na sekondari ipoje?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge Wa Newala Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha uandishi, uchapaji na usambazaji wa vitabu vya kiada na viongozi vya mwalimu kwa masomo yote ya elimu ya awali na msingi darasa la I – VII. Vitabu hivyo ni pamoja na vitabu vya kiada vilivyotafsiriwa kwa ajili ya shule zinazotumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia. Vitabu vya kiada vya wanafunzi walio nje ya mfumo rasmi (Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Waliokosa – MEMKWA), vitabu vya kiada vya breli kwa wanafunzi wasioona na vitabu vilivyokuzwa maandishi kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu. Aidha, imekamilisha kuandika, kuchapa na kusambaza jumla ya vitabu vya kiada vya masomo 171 kati ya 183 ya sekondari ikiwemo vitabu vya masomo ya sayansi, hisabati, sanaa, lugha, biashara, kilimo, michezo, muziki na vitabu vya ufundi ambavyo vipo hatua ya uchapaji. Vitabu 12 vilivyobaki ni vya masomo chaguzi (optional subjects) ikiwemo Kichina ambavyo vinatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2023.

Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada hizo, hali ya upatikanaji wa vitabu, kwa shule za msingi na sekondari imefikia uwiano wa kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga meli katika Bandari ya Mtwara itakayorahisisha mawasiliano na nchi ya Comoro?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa mawasiliano baina yake na mataifa jirani, hasa Nchi ya Comoro. Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), imetenga fedha kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu (feasibility study) katika Bahari ya Hindi kwa lengo la kujiridhisha na kiwango cha mahitaji ya usafiri huo kwa wananchi wa mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi na nchi jirani ikiwa ni pamoja na Visiwa vya Comoro. Upembuzi huo utasaidia Serikali kuamua aina ya meli itakayojengwa kulingana na hitaji la wananchi na soko kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua hiyo ya kufanya upembuzi yakinifu, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari imefanikiwa kuishawishi Kampuni ya Meli ya CMA CGM kutumia Bandari ya Mtwara kama kitovu (hub) cha mizigo inayokwenda Visiwa vya Comoro. Hivyo, mizigo inayotoka Nchi za Ulaya na Asia kwenda Comoro na ile inayotoka Tanzania kwenda Comoro (transshipment) imeanza kuhudumiwa katika Bandari ya Mtwara.

Mheshimiwa Spika, meli ya Kampuni ya CMA CGM ilianza safari za kupitia Bandari ya Mtwara tarehe 20 Aprili, 2023 na itaendelea kutoa huduma hiyo kila baada ya wiki moja. Aidha, meli ya kwanza kutoka Mtwara kwenda Comoro iliondoka tarehe 02 Mei, 2023 na itaendelea kutoa huduma hiyo kila baada ya wiki mbili, ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka maji katika Vijiji 62 Jimbo la Newala Vijijini ambavyo havina huduma ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Newala ina jumla ya vijiji 155 na kati yake vijiji 77 vinapata huduma ya maji. Serikali inaendelea na jitihada za kupeleka huduma ya maji kwenye vijiji visivyo na huduma na katika mwaka wa fedha 2022/2023 miradi 12 inaendelea kutekelezwa ukiwemo mradi mkubwa wa Makonde. Kukamilika kwa miradi hiyo kutanufaisha vijiji 61. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itafanya usanifu wa miradi ya maji katika vijiji 17 vilivyobaki ikifuatiwa na utekelezaji.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara za vijijini zinazopita katika vilima vikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali ilitenga fedha shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa barabara kilometa mbili kwa kiwango cha lami katika Kilima Kikali wa Miyuyu - Ndanda na kazi imekamilika. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, shilingi milioni 825 zimetengwa kwa ajili ya kujenga kilomita mbili za lami, kilometa mbili kwa kiwango cha changarawe na kujenga daraja dogo (box culvert) moja katika kilima hicho ambapo kazi hizo zinaendelea kutekelezwa na zimefikia asilimia 52.2 ya utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 jumla ya shilingi bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara kilometa moja kwa kiwango cha lami katika kilima kikali cha Miyuyu-Ndanda na kiasi cha shilingi milioni 300 kimetengwa kujenga kilometa 0.5 kwa kiwango cha zege kwenye eneo la kilima katika Barabara ya Malatu Juu – Mnauke – Mitahu -Mkululu yenye urefu wa kilometa 16.4.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TARURA imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kufanya usanifu na kujenga barabara zenye changamoto ya vilima vikali kwa kiwango cha lami kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha kwa kila mwaka.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaboresha miundombinu ya Chuo cha VETA Kitangari?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuongeza baadhi ya majengo yanayokosekana katika Chuo cha VETA cha Kitangari ili kuimarisha uwezo na ufanisi katika kutoa mafunzo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetenga fedha kiasi cha shilingi 666,904,745.01 kwa ajili ya kukiimarisha Chuo cha VETA Kitangari ikiwemo ujenzi wa mabweni, jiko, bwalo la chakula, madarasa na nyumba za watumishi. Ujenzi wa majengo hayo umeanza mwezi Mei, 2023, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga mabweni pamoja na miundombinu mingine katika Chuo cha VETA Kitangali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimwa Naibu Spika, Serikali inatambua mahitaji ya miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ikiwemo mabweni katika Chuo cha VETA Kitangali ambapo mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali ilitoa Sh.299,267,002.00 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, jengo la utawala na vyoo na ukarabati wa karakana ya ushonaji, umeme pamoja na uwekaji wa samani na vifaa.

Mheshimwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya miundombinu ikiwemo mabweni, bwalo, nyumba za Walimu na uzio katika Chuo cha VETA Kitangali.

Mheshimwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha wazee zaidi ya miaka 60 wanaostahili kupata huduma za afya bila malipo wanapata huduma hizo?
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge Newala Vijijini, kuhusu za afya bila malipo kwa wazee wa miaka 60 na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha Julai, 2022 mpaka Juni, 2023, jumla ya watu milioni 2.2 wakiwemo wanaume milioni 1.3 na wanawake 735,169 wametambuliwa kuwa ni wazee wa miaka 60 na kuendelea katika Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara. Kati ya hao, Wazee 585,672 sawa na asilimia 27.65 walithibitishwa kutokuwa na uwezo wa kugharamia huduma za matibabu hivyo Serikali imewapatiwa vitambulisho vya bima ya afya iliyoboreshwa (ICHF).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kufanya utambuzi wa Wazee wasio na uwezo katika Halmashauri zote nchini ili kuhakikisha wanapata huduma za matibabu zilizolipiwa gharama na Serikali.
MHE. TECLA M. UNGELE K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, kwa nini baadhi ya miradi inayoibuliwa na jamii kupitia TASAF hukataliwa na kutekelezwa miradi ambayo haikuibuliwa na jamii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi yote inayotekelezwa kupitia TASAF huibuliwa na jamii kwa kutumia utaratibu shirikishi unaokutanisha jamii yote katika Kijiji/Mtaa au Shehia katika mkutano wa kuchagua miradi inayoondoa kero za wananchi, inayokubaliwa na jamii na inayokidhi vigezo vya kisekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo jamii itaibua mradi ambao haukidhi vigezo vya sekta na kuangalia manufaa ya miradi ya kipaumbele cha kwanza kwa jamii, mradi wa pili katika orodha ya vipaumbele vya jamii hutekelezwa.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kupeleka walimu katika Chuo cha VETA Kitangari ili kuleta ufanisi wa elimu inayotolewa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Mtanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kupeleka Walimu katika Chuo cha VETA cha Kitangari kwa ajili ya kuleta ufanisi na tija katika elimu na mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa kwa wananchi wa Newala ili waweze kushiriki vema katika kutekeleza shughuli zao za kiuchumi na kuchangia pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeshapeleka jumla ya walimu sita katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Newala kilichopo Kitangari ili kuwezesha utoaji wa mafunzo katika fani tatu zilizopo pamoja na masomo mtambuka. Aidha, katika ikama na bajeti ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imekasimia walimu watatu wa masomo mtambuka ambayo utekelezaji wake utafanyika baada ya kuidhinishwa utekelezaji wa ikama hiyo. Nakushukuru.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga upya Uwanja wa Ndege wa Newala ambao umeharibika kwa kiasi kikubwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Uchukuzi kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Newala ipo katika hatua za kufanya tathmini ya uchaguzi wa eneo jipya kufuatia eneo la sasa kutofaa kwa ujenzi wa kiwanja cha ndege. Baada ya kukamilika kwa tathmini ya eneo hilo ambalo tayari limeshajumuishwa kwenye Ramani ya Mipango Miji Na.03/NEW/31/04/2021, taratibu za utwaaji na umilikishwaji wa ardhi zitafanyika. Taratibu za utwaaji na ukamilishaji zitakapokamilika, fedha za ujenzi wa kiwanja cha ndege zitatengwa kwa ajili ya bajeti husika.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga karakana na mabweni katika Chuo cha VETA Kitangari?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, majengo ya Chuo cha VETA Kitangari yalitolewa na Mfuko wa Elimu wa Newala na yalikuwa yanatumika kama majengo ya shule ya Sekondari. Majengo hayo wakati yanachukuliwa na VETA yalikuwa chakavu. Serikali ilifanya ukarabati na kujenga upya baadhi ya majengo ili yaweze kukidhi mahitaji ya kuwa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya chuo hiki mwaka hadi mwaka ambapo jengo jipya la utawala lilijengwa na kukarabati baadhi ya majengo ili kupata karakana mbili za ushonaji na umeme na darasa pamoja na bweni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya chuo kwa kujenga bweni la wasichana pamoja na nyumba ya Mkuu wa Chuo. Aidha, katika mwaka wa fedha 2024/2025 kiasi cha shilingi milioni 100 kimetengwa kwa ajili ya umaliziaji wa miundombinu hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuongeza miundombinu mingine ya majengo ikiwemo mabweni na karakana katika chuo hicho, ninakushukuru.
MHE. CECIL D. MWAMBE K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa nguzo za kilometa 2 katika Vijiji ambavyo REA III Mzunguko wa Pili unatekelezwa - Newala Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia REA, inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa R3R2 ambapo kwa upande wa Newala Vijijini inatekeleza katika vijiji 76 na imefanikiwa kuwasha umeme katika vijiji vyote 76 kwa umbali wa kilomita moja. Aidha, kwa nyongeza ya umbali wa kilometa mbili, REA kupitia mkandarasi aitwaye Central Electrical International Limited, anaendelea na kazi na amefanikiwa kufikisha umeme kwenye vijiji 32 kati ya vijiji 76. Vijiji vilivyosalia vinatarajiwa kukamilika hivi karibuni, ahsante.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya cha Mkwedu – Newala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Mkwedu ni miongoni mwa vituo vya afya 202 kongwe ambavyo vinahitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa. Kituo hiki kina upungufu wa miundombinu muhimu ikiwemo wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, jengo la maabara na jengo la kufulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itavifanyia ukarabati vituo hivyo kwa awamu kikiwemo Kituo cha Afya Mkwedu katika Halmashauri ya Newala, ahsante.