Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Alexander Pastory Mnyeti (27 total)

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga soko kubwa la Samaki Lindi Manispaa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa naomba nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kila kitu, pia ninaamshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Hassan Suluhu kwa imani yake kubwa kwa kunipa nafasi hii nimsaidie kumuwakilisha katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya uvuvi nchini, ikiwemo masoko ya samaki katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi, kwa kuzingatia upatikanaji wa maeneo na rasilimali fedha. Changamoto iliyopo ni upatikanaji wa maeneo katika Halmashauri zetu kwa ajili ya ujenzi wa masoko. Kwa sababu hii, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kwa nafasi yake, asaidie kupatikana kwa eneo la ujenzi wa soko hilo katika Manispaa ya Lindi na mara likipatikana, Wizara yangu itafanya tathmini za awali ikiwa ni pamoja na kuandaa michoro na gharama za ujenzi. Aidha, baada ya kukamilika kwa hatua hizo, Wizara itatafuta fedha za ujenzi wa soko hilo katika vyanzo vya ndani, yaani bajeti ya Wizara au miradi kwa ajili ya kuanza ujenzi.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuharakisha uwekaji samani kwenye maktaba na maabara Chuo cha FETA Mikindani?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024 Serikali kupitia Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) inaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia katika Kampasi zake ikiwemo ujenzi wa maabara na maktaba katika kampasi ya Mikindani. Pindi tuu ujenzi wa majengo hayo ya maktaba na maabara yatakapokamilika katika kampasi ya Mikindani, Serikali itaweka samani kwenye miundombinu hiyo muhimu. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza: -

Je, lini Serikali itatoa elimu kwa wafugaji kuhusu matumizi ya biogas ili kuhamasisha ufugaji wa kisasa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikitoa elimu ya ufugaji bora ikiwa ni pamoja na matumizi ya samadi kuzalisha biogas ambayo ni nishati mbadala ya kupikia na rafiki kwa mazingira.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya nishati mbadala ya biogas ambayo inatokana na kinyesi cha mifugo ikitumika vizuri, itapunguza matumizi ya kuni na mkaa hivyo kuboresha maisha ya wafugaji na kuhifadhi mazingira. Kutokana na umuhimu huo, Wizara kupitia Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA), inatoa mafunzo ya utengenezaji wa biogas kwa wanafunzi wanaosoma katika vyuo vyake katika ngazi ya cheti na diploma ili watakapohitimu masomo hayo, wawe na ujuzi wa teknolojia ya biogas na waweze kuwafundisha wafugaji matumizi sahihi ya teknolojia hiyo pia. LITA hutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wafugaji au vikundi vya wafugaji vinavyohitaji mafunzo hayo katika kampasi za Mpwapwa na Tengeru.
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR aliuliza: -

Je, ni kwa kiwango gani bahari zinachangia kukua kwa uchumi kupitia uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bakar Hamad Bakar, Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Uvuvi hutoa mchango katika uchumi wa nchi kupitia uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali zinazozalishwa ndani ya sekta. Aidha, baadhi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa hutumika kama mali ghafi katika uzalishaji ndani ya sekta nyingine kama vile viwanda na kuwa na mchango mkubwa zaidi katika sekta hizo. Katika mwaka 2022, sekta ya uvuvi ilichangia asilimia 1.8 ya Pato la Taifa huku ikikua kwa asilimia 1.9.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2022/2023, mazao ya uvuvi kutoka baharini yalichangia jumla ya tani 54,823 sawa na asilimia 10.6 ya mazao ya uvuvi ambayo ni tani 513,525. Vilevile, maduhuli ya Serikali ya shilingi bilioni 1.8 yalikusanywa kutoka katika shughuli za uvuvi baharini. Kiasi hicho cha mazao ya uvuvi kilichozalishwa kutoka baharini kilitokana na uvuvi mdogo na kilikuwa na thamani ya shilingi bilioni 356.3. Naomba kuwasilisha.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa mradi wa lambo Kata ya Nsimbo, Kijiji cha Mwenge, Halmashauri ya Nsimbo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo hapa nchini, Serikali ilianza ujenzi wa mabwawa manne ya maji kwa mifugo likiwemo bwawa la Isulamilomo lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo. Aidha, ujenzi wa Bwawa la Isulamilomo haukukamilika katika muda uliopangwa kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi, ikiwemo kukosekana kwa barabara ya kusafirisha mitambo kwenda eneo la mradi na kipindi kirefu cha mvua nyingi katika eneo la mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto hizo, Mkandarasi aliomba kuongezewa muda wa kukamilisha ujenzi wa bwawa hilo ambapo ujenzi unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2023. Kwa sasa, Mkandarasi yupo katika eneo la mradi akiendelea na kazi ya ujenzi wa tuta na njia ya utoro wa maji. Naomba kuwasilisha.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -

Je, lini mabwawa ya mifugo yatachimbwa Kata za Lagama, Masanga Mwamalasa, Ngofila, Bunambiyu, Mwasubi na Somagedi – Kishapu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo katika Jimbo la Kishapu. Kazi ya ujenzi wa mabwawa hufanyika kwa hatua kuu tatu ambazo ni; kutafuta chanzo cha maji (water source), kufanya usanifu na kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa kutambua changamoto ya upatikanaji wa maji katika jimbo la Kishapu hususani katika kata alizozitaja Mheshimiwa Mbunge, naomba kutoa wito kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kushirikiana na wataalam wa Wakala ya Huduma na Usafi wa Maji Vijijini (RUWASA), kuanza kazi ya kutafuta chanzo cha maji katika maeneo husika, kuandaa michoro (design) na mchanganuo wa gharama (BOQ) ili kuweza kupewa kipaumbele kwenye mpango na bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kutoa wito kwa wafugaji na wadau wengine, kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya maji ya mifugo ili kusaidia kupunguza changamoto ya maji kwa ajili ya mifugo hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -

Je, lini Serikali itafanya marekebisho ya sheria zisizo rafiki kwa wavuvi nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024 Serikali imepanga kuendelea kupitia na kufanya marekebisho ya Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 ili kukidhi mahitaji ya hali halisi ya sasa ya shughuli za uvuvi. Aidha, Serikali ina utaratibu wa kufanya maboresho ya kanuni mbalimbali za uvuvi mara kwa mara ili kuondoa kero na kuboresha mazingira ya biashara kwa wadau wa uvuvi. Kwa mfano, katika mwaka 2019 Serikali ilirekebisha kanuni kuruhusu leseni ya uvuvi iliyokatwa kwenye Wilaya moja kutumika katika Wilaya zote katika ziwa husika au ukanda wote wa bahari. Pia mwaka 2020 Serikali ilirejelea kanuni za uvuvi kuruhusu ongezeko la kina cha nyavu za makila katika Ziwa Victoria kutoka macho 26 mpaka macho 78 kwa uvuvi wa samaki aina ya sangara.

Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea na tathmini ya sheria, kanuni, na miongozo iliyopo katika sekta ya uvuvi ili kubaini sheria zisizo rafiki kwa wavuvi nchini na kuzifuta au kuzirekebisha. Aidha, Wizara yangu iko tayari kupokea maoni na ushauri wa wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge juu ya sheria zetu zinazohitaji kufanyiwa maboresho, naomba kuwasilisha.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Masoko ya Kuuzia Samaki katika Kata za Ninde, Wampembe na Kala Wilayani Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuboresha na kujenga miundombinu ya uvuvi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika. Katika mwaka 2023/2024, Serikali inajenga masoko ya samaki saba na mialo mitatu ambapo Wilaya ya Nkasi imepangiwa kujengewa mwalo wa Karungu. Aidha, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeingia Mkataba na Mkarandarasi Nice Construction and General Supplies Ltd. wenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kujenga mwalo wa Karungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalo huo wa Karungu utakaojengwa utakuwa na miundombinu ya soko ikiwemo chumba cha ubaridi, mtambo wa kuzalisha barafu na sehemu ya kuuzia samaki. Aidha, nimuombe Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Nkasi kutumia miundombinu hiyo kwa pindi itakapokamilika wakati Serikali inatafuta fedha za kujenga masoko ya samaki katika kata zingine zilizosalia. Vilevile, Serikali itaendelea kujenga miundombinu ya uvuvi katika maeneo mbalimbali nchini kuendana na upatikanaji wa fedha na mahitaji ya maeneo husika.
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa utambuzi wa mifugo baada ya kusitisha zoezi la utambuzi kwa kutumia hereni za mifugo?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Alexander Mnyeti majibu.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Novemba, 2022 Serikali ilisitisha kwa muda zoezi la utambuzi wa mifugo kwa njia ya hereni ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza ambazo ni pamoja na wafugaji kulalamika juu ya bei ya kuvisha hereni na baadhi ya wafugaji kukosa elimu sahihi ya utambuzi wa mifugo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekamilisha kufanya marekebisho ya kasoro la zoezi hilo la utambuzi zilizojitokeza ambapo bei ya kuvika hereni imeshuka kutoka 1,750 hadi shilingi 1,550 kwa ng’ombe na kutoka shilingi 1,000 kwa mbuzi na kondoo hadi shilingi 900. Pia, Wizara imekamilisha kuandaa mkakati wa utoaji elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa utambuzi wa mifugo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara kwa kushirikiana na wadau wa mifugo, inategemea kuanza awamu ya pili ya utambuzi wa mifugo kwa kuanza na mashamba makubwa ya mifugo ya Serikali, mashirika, watu binafsi, wawekezaji kwenye vitalu vya NARCO, vituo vya unenepeshaji ng’ombe wa maziwa, wafugaji wakubwa na wafugaji watakaokuwa tayari wakati wa zoezi hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. CHARLES M. KAJEGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Malambo ya kunyweshea mifugo katika Jimbo la Mwibara?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Charles Muguta Kajege, Mbunge wa Mwibara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa maji ya mifugo katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwa ni katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda; na aidha katika mwaka 2022/2023 Serikali ilianza ujenzi wa bwawa la maji ya mifugo katika Kijiji cha Kihumbo Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambapo ujenzi wa bwawa hilo umefikia asilimia 95. Kazi inayoendelea kwa sasa ni ujenzi wa mabirika ya kunyeshea maji ya mifugo kabla ya bwawa kuanza kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali za kujenga mabwawa na kuchimba visima virefu kwa ajili ya maji ya mifugo bado mahitaji ni makubwa. Hivyo nitoe wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya kuhamasisha wafugaji na wadau wengine kuwekeza kwenye miundombinu ya maji kwa ajili ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. ABEID R. IGHONDO K.n.y. MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, ni malambo/mabwawa mangapi yatajengwa katika Halmashauri ya Itigi kwa ajili ya kunyweshea Mifugo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, ikiwemo katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi. Aidha, mwaka 2021/2022 Serikali ilikamilisha ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo katika Kijiji cha Mhanga Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya mabwawa na visima kwa ajili ya maji ya mifugo nchini ni makubwa. Hivyo, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ujenzi wa mabwawa na kuchimba visima katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Itigi. Kulingana na upatikanaji wa fedha, vilevile, ili kukabiliana na upungufu uliopo, na nitoe wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kuhamasisha wafugaji na wadau wengine kuwekeza katika miundombinu ya maji ya mifugo.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: -

Je, lini elimu ya uvuvi na mikopo ya vifaa vya kisasa vitatolewa kwa wananchi wa Manda, Ruhuhu, Iwela, Lupingu, Lifuma, Makonde, Kilondo na Lumbila?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika awamu ya kwanza ya mradi wa kuwawezesha wavuvi boti za kisasa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa jumla ya boti nne za kisasa kwa wavuvi wa Ziwa Nyasa. Kati ya boti hizo, boti mbili zimetengwa kwa wanufaika wa Halmashauri ya Ludewa ambazo nitazikabidhi kwa wanufaika hao hivi karibuni. Aidha, katika hatua za awali za upatikanaji wa wanufaika wa mikopo hiyo, wavuvi wa Ludewa Kata za Manda, Ruhuhu, Lumbila, Lupingu na Ludewa walipatiwa elimu na mafunzo ya uvuvi endelevu na utaratibu, upatikanaji na urejeshaji wa mikopo yaliyofanyika Tarehe 16 - 25 Oktoba, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2023/2024, Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wavuvi boti za kisasa ambazo zitatolewa kwa wavuvi wa maeneo yenye shughuli za uvuvi hapa nchini ikiwemo Halmashauri ya Ludewa. Aidha, katika mwaka huu wa fedha, Wizara itaendelea kutoa elimu na mafunzo ya uvuvi endelevu, ujasiriamali katika uvuvi na namna ya kunufaika na fursa za mikopo kutoka taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo TADB kwa wananchi wa maeneo ya uvuvi ikiwemo Ludewa. Ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha muundo wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu¬: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agness Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, muundo (organization Structure) wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi yaani Fisheries Education and Training Agency - FETA uliokuwa ukitumika ulipitishwa tarehe 1 Oktoba, 2018. Muundo huo ulikuwa unaendana na matakwa ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi yaani National Council for Technical and Vocational Education and Training - NACTVET, ambalo ndio linaratibu vyuo vya ufundi stadi ikiwemo FETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto ya vyuo vinavyoratibiwa na NACTVET kuwa na miundo isiyofanana, NACTVET walihuisha miundo ya vyuo wanavyo viratibu ili kuongeza tija katika utoaji elimu na pia kupunguza gharama za uendeshaji. Hivyo, kufuatia uhuishaji huo wa NACTVET, muundo mpya wa FETA uliidhinishwa Novemba, 2022 na kwa sasa Serikali inaendelea na taratibu za kujaza nafasi za uongozi katika muundo huo mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Majosho kwenye Vijiji vya Gwandi na Takwa – Chemba?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa majosho nchini ili kudhibiti magonjwa yanayoenezwa na kupe na wadudu wengine. Kupitia mpango huo, jumla ya majosho mapya 747 yamejengwa kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2020/2021 hadi Juni, 2023 yakiwemo majosho matano yaliyojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba katika Vijiji vya Tumbakose, Mlogia, Mondo, Msaada na Masimba ambapo ujenzi umekamilika na yameshaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Sipika, kwa kutambua umuhimu wa majosho katika kudhibiti magonjwa ya mifugo nchini, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali itaendelea kutenga fedha za ujenzi wa majosho maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya Vijiji vya Gwandi na Takwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa msaada wa kitaalamu kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu ili kuongeza idadi ya samaki?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha samaki wanaendelea kuwepo na wanaongezeka katika maeneo yote ya maji, ikiwemo Bwawa la Nyumba ya Mungu. Mikakati hiyo ni pamoja na kufanya tafiti na kuimarisha ushirikishwaji wa jamii na taasisi zisizo za kiserikali katika kusimamia na kulinda rasilimali za uvuvi kupitia Halmashauri, Serikali za Vijiji na Vikundi vya kijamii vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU).

Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kufanya tafiti za kujua wingi na mtawanyiko wa samaki katika maziwa makuu na imejipanga kutanua wigo wa kufanya tafiti (frame survey) kwa maziwa madogo ili kutambua hali halisi ya uvuvi katika maziwa hayo. Aidha, tafiti hizo zinatoa taarifa sahihi ili kuiwezesha Wizara kutekeleza mikakati ya kuongeza wingi wa samaki ikiwemo uwezekano wa kupandikiza samaki.

Mheshimiwa Spika, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa, Wizara itaendelea na utoaji wa elimu ya Huduma za Ugani kuhusu athari za uvuvi haramu ili kulinda mazalia ya samaki na kuruhusu samaki kukua na kuongezeka kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, kwa nini Serikali isitoe elimu pamoja na chanjo bure kwa wafugaji wa ng’ombe nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imeendelea kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo kupitia vyombo vya habari, maonesho mbalimbali yakiwemo Maonesho ya Nanenane, Sabasaba, programu mbalimballi za utoaji elimu kwa umma na mafunzo rejea kwa wataalam wa mifugo. Aidha, Mamlaka ya Serikali za Mitaa kupitia wataalam wa mifugo zimeendelea kutoa elimu bure kwa wafugaji juu ya umuhimu wa chanjo na uchanjaji wa mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha wafugaji wanachanja mifugo yao, Wizara iliandaa Kanuni za Chanjo na Utoaji wa Chanjo (The Animal Diseases Vaccine and Vaccination Regulations of 2020) ambazo zinamtaka mfugaji kuchanja mifugo yake kuendana na kalenda ya uchanjaji wa magonjwa ya mifugo. Hata hivyo, hali ya uchanjaji kwa sasa ipo chini ya 50% ambayo ni chini ya malengo ya kuchanja mifugo, kwa angalau ya 70% kwa kila ugonjwa unaolengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha utoaji chanjo unafikia 70% iliyolengwa, Wizara imeandaa programu ya uchanjaji mifugo dhidi ya magonjwa ya kipaumbele ya miaka mitano ambayo itagharimu shilingi bilioni 216. Aidha, programu hiyo itaanza kutekelezwa katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 ambapo kiasi cha shilingi billioni 29 kimetengwa kwa ajili ya kuanza kampeni ya utoaji wa chanjo ya ruzuku, dhidi ya magonjwa ya mifugo ya kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza:-

Je, Wavuvi wangapi Ziwa Tanganyika wamewezeshwa na shilingi ngapi zimetumika kuwawezesha?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatekeleza mradi wa kukopesha vyombo vya uvuvi kwa wananchi wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi katika maeneo yote yenye uvuvi nchini ikiwa ni pamoja na Ziwa Tanganyika. Mradi huu unalenga kuwawezesha wavuvi boti za kisasa na vifaa vyake ili waweze kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi, kipato chao na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika awamu ya kwanza ya mradi huo, kwa upande wa Ziwa Tanganyika, makundi yaliyowezeshwa boti za kisasa ni vyama vya ushirika viwili vyenye idadi ya wanachama 169, vikundi viwili vyenye idadi ya wanachama 17 na wavuvi binafsi watano ambapo wamekabidhiwa jumla ya boti tisa zenye thamani ya shilingi 596,762,192.72.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ROBERT C. MABOTO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza changamoto ya uvuvi haramu katika Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imedhamiria kumaliza kabisa changamoto za uvuvi haramu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza mchakato wa kuanzisha chombo maalumu kitakachokuwa na jukumu la kulinda rasilimali za uvuvi katika maeneo yote ya uvuvi ikiwemo Ziwa Victoria. Chombo hicho kitakuwa na jukumu la kudhibiti uvuvi haramu na kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinakuwa endelevu kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Benki ya Kilimo (TADB) imeanzisha mpango maalum wa mikopo isiyo na riba ya boti za kisasa za uvuvi na vifaa vyake vikiwemo nyavu halali nchi nzima ili kuwawezesha wavuvi kutumia vifaa vinavyokubalika kisheria, kufanya uvuvi wenye tija na kuachana na uvuvi haramu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huo, Wizara imeanza kutoa boti hizo ambapo boti za kisasa 55 pamoja na vifaa vyake zimetolewa kwa Kanda ya Ziwa Victoria. Aidha, Serikali imekuja na mpango mahsusi wa kuhamasisha ufugaji samaki kwenye vizimba ambapo kwa kuanzia jumla ya vizimba 222 vimetolewa kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa Victoria ili kupunguza nguvu ya uvuvi kwenye maji asilia (fishing effort).

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani kwa watumishi wanaokaimu nafasi kwa muda mrefu katika Vyuo vya FETA ikiwemo Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu¬: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto za kimuundo (organization structure) ya Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (Fisheries Education and Training Agency - FETA) watumishi wengi waliokuwa wanakaimu kwa muda mrefu walishindwa kuthibitishwa katika nafasi zao. Changamoto hiyo ya kimuundo imeisha baada ya Muundo mpya wa FETA kuidhinishwa mwezi Oktoba, 2022.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa Serikali inaendelea na taratibu za kujaza nafasi za uongozi katika Muundo huo mpya ikiwemo kuwafanyia upekuzi wote wanaokaimu ili wakikidhi vigezo wathibitishwe katika nafasi hizo au kama hawakidhi vigezo wateuliwe watumishi wengine kujaza nafasi hizo.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, lini Serikali itaajiri Maafisa Mifugo katika kila Kata ili kuwasaidia wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwongozo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa utoaji huduma za ugani wa mwaka 2011 unaelekeza katika kila Kata na kila Kijiji kuwa na Afisa Ugani. Hata hivyo, idadi ya Maafisa Ugani wa Mifugo waliopo kwa sasa ni 4,406 ikilinganishwa na mahitaji ya Wagani 20,537 nchini, sawa na upungufu wa Maafisa Ugani 16,131.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na upungufu uliopo na kuongeza wigo wa utoaji huduma za ugani, Serikali imeendelea kuajiri Maafisa Ugani kila mwaka, ambapo kati ya mwaka 2021 hadi 2023 jumla ya Maafisa Ugani 1,205 waliajiriwa na kupangiwa vituo katika Kata na Vijiji mbalimbali hapa nchini. Aidha, Wizara inaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI kuomba vibali zaidi vya ajira za Maafisa Ugani na kuendelea kuajiri Maafisa Ugani kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanzisha Kituo cha Madume Bora ya Ng’ombe Wilayani Bahi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea na utekelezaji wa Mpango wa Mabadiliko ya Sekta ya Mifugo wa Miaka Mitano Kuanzia Mwaka 2022/2023 hadi Mwaka 2026/2027. Aidha, kupitia mpango huo, uboreshaji wa mbari za ng’ombe unafanyika kupitia matumizi ya madume bora na uhimilishaji ambapo kwa upande wa madume, Wizara imesambaza bure madume bora ya ng’ombe wa nyama 366 kwenye vikundi vya wafugaji katika halmashauri nane ili kuzalisha mifugo yenye tija zaidi ile ya asili.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Wizara kwa sasa ni kusambaza madume bora ya ng’ombe kwa vikundi vya wafugaji ili kuboresha mifugo yao badala ya kuanzisha vituo vya madume. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Wizara imepanga kununua madume bora 200 yatakayosambazwa kwa vikundi vya wafugaji, wakiwemo wafugaji wa Halmashauri ya Bahi ambao watapewa madume 20. Naomba kuwasilisha.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Malambo ya kunyweshea mifugo katika Jimbo la Meatu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa bwawa/lambo hufanyika kwa hatua tatu ambazo ni kutafuta chanzo cha maji (water source), kufanya usanifu (design) na kutekeleza kazi ya ujenzi. Wizara itawasiliana na Halmashauri ya Wilaya Meatu kwa ajili ya kupata mapendekezo ya eneo linalofaa kujenga lambo ambalo halina mgogoro wa umiliki, ili hatua za usanifu ziweze kufanyika na kuingiza gharama zake kwenye Mpango wa Bajeti ya Wizara kadiri ya upatikanaji wa fedha za miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kutoa wito kwa wafugaji na wadau wengine hapa nchini kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya maji ili kusaidia kupunguza changamoto ya maji kwa ajili ya mifugo. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa Chuo cha Uvuvi na Mifugo utaanza katika Kata ya Igamba, Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, mafunzo ya mifugo katika ngazi ya Astashahada na Stashahada hutolewa na Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA) kupitia kampasi zake nane na vyuo binafsi 12 vinavyotambuliwa na Serikali. Aidha, kwa upande wa Sekta ya Uvuvi, mafunzo ya uvuvi hutolewa na Wakala wa Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kupitia kampasi zake tatu na vituo vya mafunzo viwili.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA) imepanga kujenga kampasi ya kutoa mafunzo ya mifugo katika Kata ya Igamba, Wilaya ya Mbozi, Mkoani Songwe. Ujenzi wa Kampasi ya Igamba, Mbozi, utagharimu takribani kiasi cha shilingi bilioni 15 ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024, Wizara kupitia LITA imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi. Aidha, ujenzi kwa awamu ya kwanza utahusisha ujenzi wa jengo la utawala, hosteli ya wanafunzi na ukumbi wa mihadhara.

Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuongeza majengo ya chuo hicho kadiri itakavyopata fedha za maendeleo ili kuhakikisha ujenzi na usimikaji wa miundombinu yote ya mafunzo inayohitajika unakamilika na kampasi hiyo kuanza kutoa mafunzo. Ahsante.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka fedha na wataalam katika eneo la Mbongo, Kata ya Manda ambalo linafaa kwa ufugaji wa samaki kwenye vizimba?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika ziwa ni lazima kuzingatia vigezo vya kisheria na kitaalam, ikiwemo kufanya tathmini ya kimkakati ya mazingira (Strategic Environmental Assessment). Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024, kupitia Progaramu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II), Serikali imetenga kiasi cha shilingi 233,500,000 kwa ajili ya kuiwezesha Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) kufanya tathmini ya kimkakati ya mazingira, ambayo ni takwa la kisheria katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa yakiwemo maeneo ya Manda ili kutambua maeneo yanayofaa kwa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.

Mheshimiwa Spika, baada ya tathmini kukamilika, maeneo yatakayobainika kuwa yanafaa kwa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba yataingizwa kwenye Bajeti na Mpango wa Wizara wa mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuwezesha upatikanaji wa fedha na wataalam katika eneo hilo, ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, kuna utafiti wa kisayansi unaoonyesha kufunga shughuli za uvuvi Ziwa Tanganyika kuruhusu kuzaliana kwa Samaki kutakuwa na tija?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha uvunaji wa rasilimali za uvuvi katika Ziwa Tanganyika unafanyika kwa njia endelevu, Wizara kwa kushirikiana na nchi zinazounda Mamlaka ya Ziwa Tanganyika inatekeleza Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika unaoweka hatua za usimamizi wa uvuvi endelevu katika Ziwa Tanganyika na Bonde lake. Aidha, miongoni mwa hatua za usimamizi ni kuanzishwa kwa utaratibu wa kupumzisha shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika kila ifikapo tarehe 15 Mei hadi 15 Agosti ya kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upumzishaji wa Ziwa Tanganyika katika kipindi cha miezi mitatu, unatarajiwa kuwa na tija ya muda mrefu kwa kuwa tafiti katika nchi zinazozunguka ziwa zinaonesha kuwa kipindi hicho kunakuwepo na samaki wengi wachanga aina ya migebuka na dagaa. Samaki hawa wanahitaji kipindi cha miezi mitatu mpaka minne kufikia kiwango cha kuvuliwa. Aidha, kupumzisha ziwa katika kipindi hicho kutaruhusu samaki kukua na mavuno kuongeza.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:-

Je, Serikali imefanya utafiti kubaini sababu zilizopelekea wakulima kupata hasara katika mavuno ya mwaka 2022/2023?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI imekuwa ikiratibu na kufanya tathmini ya uzalishaji na upatikanaji wa chakula nchini. Lengo la tathmini ni kuiwezesha Serikali kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha utengamano wa hali ya usalama wa chakula nchini unaimarika.

Mheshimiwa Spika, kupitia tathmini hiyo, uzalishaji wa mazao ya chakula nchini kwa msimu wa mwaka 2022/2023 ulikuwa tani 20,402,014 ambapo mahitaji ya chakula ni tani 16,390,404 sawa na utoshelevu wa asilimia 124. Pamoja na mafanikio hayo, changamoto mbalimbali zilijitokeza na kusababisha hasara kwa baadhi ya wakulima nchini. Miongoni mwa changamoto hizo ni mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha unyeshaji mvua kwa mtawanyiko usioridhisha, matumizi madogo ya teknolojia na milipuko ya visumbufu vya mazao shambani hususan viwavi jeshi na kwelea kwelea kwenye baadhi ya mashamba ya wakulima nchini.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -

Je, nini mkakati wa Serikali kujenga Kiwanda cha Kuchakata Samaki katika Ukanda wa Bahari ya Hindi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) chini ya mfuko wa IFAD inaendelea kuliwezesha Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata samaki katika eneo la Kilwa Masoko. Ambapo, eneo la ujenzi wa kiwanda hicho lina ukubwa wa ekari 8.5. Aidha, mpaka sasa taarifa ya awali ya upembuzi yakinifu imewasilishwa TAFICO kwa ajili ya kufanyiwa mapitio na inategemewa kukamilika mwisho wa mwezi Mei, 2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Januari, 2022 Kampuni ya Albacora Group kutoka nchini Hispania inayomiliki Meli ya FV Pacific Star inayopeperusha Bendera ya Tanzania iliingia makubaliano na Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) ya kujenga kiwanda cha kuchakata samaki katika eneo la Kijiji cha Mwambani kilichopo Halmashauri ya jiji la Tanga. Aidha, hatua inayofuata kwa sasa katika eneo hilo ni kufanya tathimini ya athari za kimazingira itakayowezesha kuanza kwa ujenzi wa kiwanda hicho. Vilevile, Serikali inaendelea kuwekeza, kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuboresha miundombinu ya uvuvi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Ukanda wa Bahari ya Hindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)