Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon Ally Juma Makoa (16 total)

MHE. CECILIA D. PARESSO K.n.y. MHE. ALLY J. MAKOA Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakarabati au kujenga Hospitali mpya ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa kwa kuwa Hospitali iliyopo ni ya muda mrefu na miundombinu yake ni chakavu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa hospitali kongwe na chakavu katika baadhi ya Halmashauri nchini ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 102 ambazo zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Kwa kuwa, bado kuna Halmashauri 28 zisizo na Hospitali ya Halmashauri, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 14 ili kuanza ujenzi katika Halmashauri hizo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka kipaumbele kwa kuanza ujenzi katika Halmashauri hizo na baada ya hapo ukarabati wa Hospitali chakavu ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa utafanyika. Ahsante sana.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga Daraja la Mto Bubu ili wananchi wa upande wa pili wa mto waweze kuvuka na kupata huduma mbalimbali za kijamii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Daraja la Mto Bubu lijulikanalo kama Munguri B lipo katika barabara ya Kondoa – Nunguri – Mtiriangwi – Gisambalang – Nangwa yenye jumla ya urefu wa kilomita 81.4. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Manyara kupitia Wilaya za Kondoa na Hanang.

Mheshimiwa Spika, mvua kubwa zilizonyesha mwaka 2019/2020 zilisababisha Mto Bubu kutanuka na kufanya Daraja la Munguri B kutopitika wakati wa mvua. Kwa kutambua changamoto hii, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imetenga fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021 kwa ajili ya kufanya usanifu wa Daraja jipya katika Mto Bubu.

Mheshimiwa Spika, taratibu za ununuzi wa kumpata Mhandisi Mshauri zipo katika hatua za mwisho ambapo kazi hiyo inatarajiwa kuanza Juni, 2021. Aidha, katika mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022, daraja hili limetengewa shilingi bilioni sita kwa ajili ya kukamilisha kazi ya usanifu. Baada ya usanifu kukamilika, ujenzi wa daraja hili utaanza kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. ALLY J. MAKOA Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara muhimu ya Iboni – Bolisa – Gubalisa iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Iboni – Bolisa – Gubalisa iliyopo Halmashauri ya Mji wa Kondoa yenye urefu wa kilometa 14.7 inaunganisha maeneo muhimu ya kiuchumi na ni barabara mbadala ya kuingia na kutoka mjini kwa wananchi wanaoelekea Kondoa Vijijini pamoja na Wilaya ya Jirani ya Babati.

Mheshimiwa Spika, barabara hii ina mahitaji ya vivuko vitano na daraja moja ambapo tathmini na usanifu umebainisha kuwa ujenzi wake utagharimu jumla ya shilingi bilioni 2.15. Utekelezaji wa kazi hii umepangwa kufanyika katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwa kujenga vivuko na kuiwekea changarawe ili kuiwezesha kutoa huduma katika kipindi chote cha mwaka.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa mpango wa kuiwekea lami haujaandalliwa kutokana na ufinyu wa bajeti.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: -

Je, kuna mpango wowote kubadili mwelekeo wa ujenzi Barabara ya Tanga kupitia Handeni, Kiberashi, Mrijo, Mondo Bicha hadi Kwamtoro?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kulingana na taarifa ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, ujenzi wa barabara inayounganisha Mikoa ya Tanga, Manyara, Dodoma na Singida utaanzia Handeni - Kibirashi - Kijungu - Kibaya - Goima - Chemba - Donsee – Kwamtoro hadi Kititimo (Singida) ambayo itakuwa na urefu wa kilometa 463.5.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara hii umeanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa kujenga Kilometa 20 kwa sehemu ya Handeni – Mafuleta, ahsante.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: -

Je, ni Wananchi wangapi Kondoa Mjini walioharibiwa mazao yao na tembo wamehakikiwa na lini watalipwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya tarehe 25 na tarehe 28 Septemba, 2022, Wizara ilifanya uhakiki wa madai ya kifuta jasho ya wananchi 274 wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa walioharibiwa mazao yao na tembo. Baada ya uhakiki huo kukamilika, Wizara iliwalipa wananchi 198 wa Vijiji vya Chemchem, Tungufu, Tampori, Mulua na Iyoli mwezi Novemba, 2022. Jumla ya shilingi 40,013,750 ikiwa ni kifuta jasho kutokana na madhara yaliyosababishwa na wanyamapori.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imepokea madai mengine mapya ya wananchi 28 wa vijiji vya Unkuku, Kwapakacha, Serya, Damai, Chemchem na Mulua ambayo yamewasilishwa hivi karibuni. Madai hayo yanaendelea kufanyiwa kazi na malipo yatafanyika baada ya taratibu stahiki kukamilika.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: -

Je, lini barabara ya kilometa 0.8 kutoka Benki ya NMB hadi National Milling Kondoa Mjini itajengwa kwa kiwango cha lami?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) katika mwaka wa fedha 2023/2024 imepanga kuanza ujenzi wa barabara za Mji wa Kondoa kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilomita 3, ikiwemo kipande cha barabara ya kutoka Benki ya NMB hadi National Milling chenye urefu wa km 0.8. Ahsante.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga shule ya Bweni ya Wasichana katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Kondoa tayari ina shule moja ya wasichana ya Serikali inayoitwa Kondoa Girls. Shule hii ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 660. Kwa sasa shule ina wanafunzi 572 wa kidato cha tano na sita na Halmashauri imeomba kuongezewa mchepuo wa HGE ili iweze kutumika kwa full capacity.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuongeza shule za bweni za wasichana kulingana na uhitaji na upatikanaji wa fedha.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji katika Kata ya Serya utaanza?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kata ya Serya iliyopo katika Tarafa ya Kondoa Mjini ipo takriban kilometa 20 kutoka Kondoa Mjini. Mwaka 2007, Vijiji vya Mongoroma na Serya vilitenga eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji lenye ukubwa wa hekta 3000. Pia Kijiji cha Mongoroma kilitenga eneo la ujenzi wa bwawa ambalo linapakana na eneo la pori la hifadhi ambalo lilikuwa tayari na aina mbalimbali za wanyama. Skimu inatarajiwa kutumia maji ya mvua pamoja na kuchepusha maji ya Mto Bubu na kuyahifadhi kupitia ujenzi wa Bwawa la Mongoroma. Eneo hili linastawisha mazao mbalimbali yakiwemo mahindi, mtama, mbaazi na mbogamboga zinazolimwa kwa kiwango kidogo pembezoni mwa Mto Bubu kwa njia ya Umwagiliaji wa kutumia pampu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/2011, Serikali kupita Mfuko wa Kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji ngazi ya Wilaya chini ya ASDP 1 ilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina wa bwawa na skimu, pamoja na maandalizi ya awali ya jamii husika katika kushiriki katika ujenzi wa Skimu na Bwawa la Mangoroma/Serya.

Mheshimiwa Spika, aidha, kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, ongezeko la watu na makazi kufuatia kasi ya kukua kwa Mji wa Kondoa eneo la bwawa kupakana na hifadhi Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, kwa kushirikiana na Halmashauri ina mpango wa kuhuisha tafiti za awali zilizofanyika mwaka 2010/2011 pamoja na kufanya utafiti mpya wa athari za mazingira na jamii, matokeo ya uhuishaji wa tafiti hizo, yataiwezesha Serikali katika mwaka wa fedha 2024/2025 kutega fedha za ujenzi wa Bwawa na Skimu ya Mongoroma/Serya.
MHE. MIRAJI J. MTATURU K.n.y. MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga majosho katika Kata za Kolo, Kingale na Bolisa?

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa majosho nchini ili kudhibiti magonjwa yanayoenezwa na kupe. Katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Sekta ya Mifugo, imetenga jumla ya shilingi bilioni 5.7 kwa ajili ya ujenzi wa majosho 246 katika Halmashauri 63 nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Kondoa Mjini jumla ya shilingi milioni 115,000,000 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa majosho matano katika kata za Kingale Mitaa ya Msui na Tampori, Serya Mtaa wa Chandimo, Suruke Mtaa wa Tungufu na Kondoa Mjini Mtaa wa Tumbelo chang’ombe. Hivyo basi, ninamshauri Mheshimiwa Mbunge kuwasiliana na kujadiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri ili kama kuna haja ya mabadiliko ya maeneo ya ujenzi wa majosho yaweze kufanywa kulingana na vipaumbele vya wananchi na Halmashauri. Ahsante.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara za mitaa ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa kwa kiwango cha lami kupitia Miradi ya TACTIC?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Jimbo la Kondoa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza Mpango wa Kuboresha Miundombinu ya Msingi katika Miji Nchini, Serikali kupitia Mradi wa Tanzania Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness Project (TACTIC) utakaotekelezwa katika miji 45. Mradi huo utatekelezwa katika Halmashauri za Majiji, Manispaa na Miji kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia wenye jumla ya Dola za Kimarekani milioni 500, baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa na Benki ya Dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Kondoa ni miongoni mwa miji 45 nchini ambayo imepewa kipaumbele cha kupata ufadhili wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu katika Miji. Aidha, Halmashauri hii ipo kwenye kundi la tatu lenye jumla ya miji 18 ambayo inatarajiwa kuanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi iliyopendekezwa na Halmashauri husika katika mwaka wa fedha 2022/2023.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka gari la wagonjwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa?

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 itanunua magari 195 ya kubebea wagonjwa ambayo yatapelekwa kwenye Halmashauri 184 nchini kote ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Kondoa. Ahsante.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaimarisha Mawasiliano ikiwemo Minara ya Simu na usikivu wa Radio ya Taifa (TBC) – Kondoa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) wakishirikiana na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) imekamilisha ujenzi wa majengo ya mitambo ya redio pamoja na miundombinu ukiwemo mnara wa redio wilayani Kondoa ambapo kwa sasa TBC wanasubiria vifaa ambavyo vipo katika hatua ya manunuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itafanya tathmini katika jimbo la Kondoa Mjini na kuona maeneo yaliyobaki yenye changamoto za mawasiliano na kuviingiza vijiji husika katika orodha ya miradi itakayotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha. (Makofi)
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:-

Je, ni lini TANROADS watalipa fidia kwa kujenga shule mbadala baada ya shule ya Msingi Unkuku kupitiwa na Barabara ya Dodoma – Arusha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Dodoma ilikwishalipa fidia kwa jengo la Shule ya Msingi Unkuku, miti pamoja na sehemu ya eneo la shule ambavyo viliathiriwa na ujenzi wa barabara ya Dodoma – Babati ambapo mnamo tarehe 10 Septemba, 2014 kiasi cha shilingi 8,370,221.00 kililipwa kwa Mkurugenzi wa Halmasauri ya Wilaya ya Kondoa, ahsante.
MH. ALLY J. MAKOA aliuliza:-

Je, lini umeme wa REA utapelekwa Mitaa ya Chemchem, Tampori, Kwamtwara, Guluma, Mongoroma, Chandimo, Chang’ombe na Tura?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini imeendelea kutekeleza kazi ya kusambaza umeme katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mitaa ambayo ipo katika mamlaka za miji na miji midogo yenye hadhi sawa na vijiji. Kwa kuwa Jimbo la Kondoa Mjini lipo katika mamlaka ya mji, kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, REA itapeleka umeme katika mitaa 15 ambayo imefikiwa na miundombinu ya msongo wa kati, ikiwemo Mitaa ya Chemchem, Tumbelo na Chang’ombe. Aidha Mitaa ya Tura na Tumbelo imepatiwa umeme kupitia Mradi wa Ujazilizi Mbili (A). Serikali kupitia REA itaendelea kuratibu kazi ya kusambaza umeme katika vitongoji na mitaa ambayo haina umeme kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka fedha za ujenzi wa uzio wa Shule ya Wasichana Kondoa ili kuimarisha ulinzi na usalama wa wanafunzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, mwaka 2021/2022 mpaka 2023/2024, Serikali Kuu imepeleka shilingi milioni 600.8 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo vyumba vya madarasa nane, mabweni mawili, matundu ya vyoo 14 na vitanda 660 katika Shule ya Wasichana Kondoa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa uzio kwa ajili ya ulinzi wa mali na wanafunzi wa bweni. Hata hivyo, kwa sasa kipaumbele cha Serikali Kuu ni ujenzi wa miundombinu ya msingi inayowezesha kuongeza nafasi za udahili wa wanafunzi.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka fedha za ujenzi wa uzio wa Shule ya Wasichana Kondoa ili kuimarisha ulinzi na usalama wa wanafunzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, mwaka 2021/2022 mpaka 2023/2024, Serikali Kuu imepeleka shilingi milioni 600.8 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo vyumba vya madarasa nane, mabweni mawili, matundu ya vyoo 14 na vitanda 660 katika Shule ya Wasichana Kondoa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa uzio kwa ajili ya ulinzi wa mali na wanafunzi wa bweni. Hata hivyo, kwa sasa kipaumbele cha Serikali Kuu ni ujenzi wa miundombinu ya msingi inayowezesha kuongeza nafasi za udahili wa wanafunzi.