Supplementary Questions from Hon Kassim Hassan Haji (6 total)
MHE. KASSIM HASSAN HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza, kituo hiki kina miaka 13 hakijamalizika, je, Waziri atakuwa tayari kuongozana nami kwenda kuzungumza na wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, kwa kuwa uhalifu umeongezeka katika Jimbo la Mwanakwerekwe, sasa hivi kuna vibaka na waporaji wengi lakini hata miundombinu ya Serikali nayo imekuwa ikiharibiwa kwa makusudi.
Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusiana na kadhia hii wanayoipata wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kassim Hassan Haji, Mbunge wa wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu rafiki yangu Mheshimiwa Kassim niko tayari kuambatana naye kwenda katika kituo kile na kukiona. Nimuambie kwamba kituo kile nakifahamu na kipo kwa muda mrefu ni kweli, lakini niko tayari kuambatana naye kwenda kukiangalia kituo kile na kuona namna ambavyo tunaweza tukawasaidia wananchi ili kuimarishiwa hizi huduma za ulinzi na usalaama katika eneo lao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lingine ni kuhusu vitendo hivi vya uhalifu ambapo vijana wanafanya vitendo vikiwemo vya uvunjifu wa miundombinu na uharibifu wa vitu vingine. Ndani ya jimbo lake kuna kituo kingine kikubwa cha Mwanakwerekwe na hicho kinafanya kazi muda wote, hasa kupitia kituo hiki tutajitahidi tuwe tunafanya doria za mara kwa mara ili kuweza kuwakamata na kuwashughulikia wale wote ambao wanavunja amani ama wanafanya vitendo vya uhalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine tuko tayari kuendeleza na kuimarisha ulinzi shirikishi ili wananchi na wao waweze kutoa mchango wao katika kulinda amani ya wengine. Kikubwa, tuko tayari kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu wale wote ambao watakuwa wanafanya vitendo hivi. Nakushukuru.
MHE. KASSIM HASSAN HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante; kwa kuwa kuna ucheleweshaji mkubwa wa malipo ya watu wanaomiliki maduka hayo na hospitali.
Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuweka njia nzuri ya kuwafanya wamiliki wa maduka yale waweze ku-invest au kuingia katika uwekezaji huu wa kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa mfumo uliokuwepo kabla wa kuandika karatasi na kujaza fomu za kawaida umekuwa ukichelewesha hayo malipo ambayo imekuwa ni sababu mojawapo ya wamiliki wengi wa vituo na maduka kusita kujiunga na Bima ya Afya, lakini sasa bima ya afya imeshatengeneza mfumo mtandao ambapo sasa malipo hayo yanaweza moja kwa moja yakaingizwa kwenye mtandao siku hiyo na akaweza kulipa mapema kila baada ya mwisho wa mwezi.
Kwa hiyo, tunaielekeza Bima ya Afya sasa waweze kufikisha hiyo huduma Zanzibar mara moja ili hilo tatizo liweze kuondolewa. (Makofi)
MHE. HASSAN HAJI KASSIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nashukuru kwa majibu ya Serikali. Hata hivyo, kwa kuwa utaratibu uliokuwepo sasa hivi, wa abiria ambao wanasafiri wanasubiria sana nje kabla ya kuingia ndani. Je, ni lini Serikali hii itatoa maelekezo ya wale abiria ambao tayari wana tiketi, wasisimame pale nje, waingie ndani moja kwa moja na kusubiria usafiri ndani?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hassan Haji Kassim, Mbunge wa Mwanakwerekwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba eneo ama jengo lilipo la kusubiria abiria pale Dar es Salaam Kwenda Zanzibar lina uwezo wa kubeba abiria 150 na jengo ambalo tutajenga litakuwa na uwezo wa kubeba abiria 400.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa hatua ambayo Serikali inachukua tunaweza ratiba maalum, mahususi kwa boti zote mbili ambapo boti ya kwanza kama ambavyo iko inaondoka saa moja asubuhi, boti ya pili itaondoka saa tatu na nusu, boti ya tatu itaondoka saa sita, nyingine saa nane mpaka saa kumi na mbili. Kwa abiria wote ambao wanakuwa nje na wana tiketi, hawa ndio wanatakiwa waingie kwenye jengo hili ili kuruhusu wasafiri kuliko mwingine yeyote kwa sababu eneo lile bado ni dogo. Kwa hiyo, ni maelekezo kwa Serikali kwa abiria wote, lakini pia wale wote wanaosimamia eneo hili.
MHE. KASSIM HASSAN HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa huduma hizi za Bima ya Afya upatikanaji wa dawa kwa upande wa Zanzibar zimekuwa za chini sana.
Je, ni lini Serikali itaenda kuboresha huduma hizo ili watu wapate dawa katika hali ambayo itakuwa ni ya kawaida?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe tu Mbunge, wakati wa sisi kupitisha Muswada wetu wa Bima ya Afya kwa watu wote, wote kwa pamoja tushirikiane kuweka input nzuri ambayo mwisho wa siku italeta suluhu ya kuduma bila tena kuona wazee wanarudi kule kule ambako hatukupenda warudi. (Makofi)
MHE. KASSIM HASSAN HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kuwa watu wengi ambao wameiona historia ya Tanzania na Zanzibar wameandika vitabu katika historia hii.
Je, ni lini vitabu vile vitatafsiriwa, Serikali itachukua maamuzi ya kutengeneza filamu ya vitabu vile ili kizazi kinachokuja kiweze kujivunia na kuona uhalisia wa historia ya Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kassim Hassan Haji, Mbunge wa Mwanakwerekwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa lengo la Serikali siyo tu kuhifadhi historia ya nchi na mashujaa wetu kwenye filamu, lakini ni kuhifadhi katika kiwango na hadhi inayotazamika kwenye majukwaa ya Kitaifa na ya kimataifa. Kwa hivyo Serikali kwa sasa inafanya juhudi kubwa kuhakikisha uwekezaji mkubwa unaongezwa kwenye tasnia ya filamu nchini kuhakikisha hilo linatokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kudhibitisha hilo, ni juma lililopita tu Mheshimiwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, mama yangu, Mheshimiwa Balozi Pindi Hazara Chana, alihudhuria utiaji saini mkataba wa makubaliano kati ya Bodi ya Filamu Tanzania na Taasisi ya Mashirikiano ya Kimataifa ya Korea Kusini (BFIC), makubaliano ambayo pamoja na mambo mengine yanakwenda kuona uwekezaji mkubwa ukiongezeka kwenye tasnia ya filamu nchini ambapo filamu ambazo unazizungumzia Mheshimiwa zitakwenda kufanywa kwenye kiwango na hadhi inayotazamika kwenye majukwaa ya Kitaifa na ya kimataifa, nashukuru.
MHE. KASSIM HASSAN HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kodi inayokatwa katika matumizi ya mfuko huu ni kubwa sana, ni lini Serikali itaenda kuondoa kodi hiyo katika matumizi ya Mfuko wa Jimbo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Wakurugenzi wetu wengi ni wapya ambao wamechaguliwa katika kuendesha halmashauri zetu. Je, ni lini Serikali itakwenda kupeleka mafunzo kuwawezesha Wakurugenzi hawa kujua thamani ya Mfuko wa Jimbo kwa Waheshimiwa Wabunge? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kassim Hassan Haji, Mbunge wa Mwanakwerekwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba tulipokee suala la kodi inayokatwa katika fedha za Mfuko wa Jimbo na hususan kwa upande wa Zanzibar. Suala hili ni la kiutaratibu, tutafanya utaratibu kuhusiana na Wizara ya Fedha lakini pia Wizara ya Muungano, Ofisi ya Rais TAMISEMI, kwa pamoja tuweze kuona njia nzuri zaidi ya kurekebisha changamoto hii ili tuweze kwenda vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la pili kuhusiana na Wakurugenzi wengi kuwa wapya. Ni kweli na tunahitaji kuona Wakurugenzi wetu wanaelewa vizuri wajibu wao wa kutekeleza Mfuko wa Jimbo. Nitumie fursa hii kwanza, kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya mafunzo kwa Wakurugenzi wote ili wajue wajibu wao katika kusimamia Mfuko wa Jimbo.
Mheshimiwa Spika, natoa msisitizo kwa Wakurugenzi wote kote nchini, kumekuwa na changamoto, Waheshimiwa Wabunge wanakaa na Kamati za Mfuko wa Jimbo, wanapitisha miradi lakini Wakurugenzi wanazuia fedha zisiende kutekeleza miradi ile.
Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, kuelekeza kwamba Mkurugenzi yeyote atakayekiuka utaratibu baada ya Mwenyekiti wa mfuko huo kuidhinisha matumizi, tutachukua hatua kali za kinidhamu dhidi yake. Miradi hii itekelezwe kwa wakati baada ya Waheshimiwa Wabunge kupitisha miradi hiyo. Ahsante. (Makofi)