Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Abeid Ighondo Ramadhani (20 total)

MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa maboma ya vituo vya afya yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi katika Kata za Makuro na Ngimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Singida shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, hospitali hiyo imetengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wa wodi tatu na shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma ya Zahanati Minyeye, Mnung’una na Msikii katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi milioni 250 kwa ajili ya kukamilisha maboma matano ya zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wananchi katika kujenga na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya huduma za afya katika Jimbo la Singida Kaskazini zikiwemo Kata za Makuro, Ngimu na nchini kote ili kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE K.n.y. MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza barabara za Singida Kaskazini zinazounganisha Vijiji ambazo hazipitiki kwa sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Singida Kaskazini ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 811.68 ambao umekuwa ukifanyiwa matengenezo pamoja na kujenga na kukarabati vivuko. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Singida ilifanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 78.55 na vivuko 22 kwa gharama ya shilingi milioni 739.39.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka fedha 2020/2021, barabara zenye urefu wa kilometa 67.8 na vivuko 20 vimetengenezwa kwa gharama ya shilingi millioni 711.08 ambapo hadi Machi, 2021 barabara zenye urefu wa kilomita 45 na vivuko 15 vimekamilika. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 barabara zenye urefu wa kilomita 62.5 na vivuko 24 vitajengwa kwa gharama ya shilingi millioni 711.08.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Halmashauri ya Wilaya ya Singida itafanya tathmini ya barabara zote za Singida Kaskazini ili kuandaa mpango wa namna bora ya kuweka vipaumbele vya ujenzi na matengenezo ya barabara.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itavipatia huduma ya maji safi na salama Vijiji vya Kinyamwenda, Igauri, Matumbo, Itamka na Msimihi katika Jimbo la Singida Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhan, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa mwaka wa fedha 2020/21 imekamilisha miradi ya maji katika vijiji 7 ambavyo ni Mughamo, Mgori, Ngimu, Sefunga, Ghalunyangu, Kijota na Malolo hivyo, huduma ya upatikanaji wa maji kufikia asilimia 66.4 katika Wilaya ya Singida Vijijini.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 utafanyika utafiti wa kina kwa ajili ya kuainisha maeneo yenye maji ya kutosha chini ya ardhi. Hivyo vijiji vya Kinyamwenda, Igauri, Itamka na Msimihi vitapata maji baada ya kukamilisha uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji.

Aidha, kijiji cha Matumbo kitapata huduma ya maji ya uhakika baada ya ukarabati wa mradi wa maji kukamilika mwezi Julai, 2021.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, ni lini Vijiji na Kata katika Jimbo la Singida Kaskazini ambavyo havijapata umeme vitapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vijiji 26 vya Jimbo la Singida Kaskazini ambavyo havijapata umeme kati ya vijiji 84 vitapelekewa umeme kupitia utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ulioanza mwezi Machi, 2021. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba, 2021 na gharama ya mradi ni shilingi bilioni 26.6.
MHE. ABEID I. RAMADHANI aliuliza: -

Barabara ya kutoka Singida kupitia Mji Mdogo wa Ilongero – Mtinko hadi Hydom ni muhimu kwa uchumi wa Mkoa wa Singida, Manyara na Simiyu.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Ilongero – Mtinko hadi Hydom kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Singida kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami Barabara ya Ilongero – Mtinko hadi Hydom yenye urefu wa kilometa 93.3. Mkataba wa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulisainiwa mwezi Oktoba, 2021 na kazi inatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2022. Mara baada ya kazi ya Usanifu kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Wananchi wa Kata za Mgori, Mughungu na Ngimu Jimbo la Singida Kaskazini wapo tayari kukabidhi Msitu wa Mgori kwa Serikali kuwa Hifadhi ya Taifa: -

Je, mchakato wa Serikali kukamilisha zoezi hilo umefikia wapi na faida gani wananchi watazipata kwa msitu huu kuwa hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kupongeza jitihada zote zilizochukuliwa na Serikali katika ngazi ya Vijiji, Wilaya na Mkoa pamoja na Mheshimiwa Mbunge katika kuhakikisha Msitu wa Mgori ambao ni makazi ya wanyamapori wadogo na wakubwa hususani tembo unahifadhiwa.

Mheshimiwa Spika, hatua iliyofikia mpaka sasa ni mchakato wa kupata Tangazo la Serikali ili kuutambua msitu huo kama hifadhi. Rasimu ya kwanza ya Tangazo la Serikali imetolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tarehe 4 Februari, 2022. Tangazo hilo litadumu kwa siku 90 kabla ya kutolewa tangazo la mwisho ambalo litatoa idhini kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kusimamia msitu huo.

Mheshimiwa Spika, faida za kuhifadhi msitu huu wenye ukubwa wa hekta 49,000 ni pamoja na: -

(i) Kuweka hali ya hewa nzuri kwa Mkoa wa Singida wenye misitu michache sana ya hifadhi na kuwezesha upatikanaji wa mvua hivyo kusaidia kwenye ukuaji wa sekta nyingine kama kilimo, ufugaji na maji;

(ii) Lakini vilevile utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji;


(iii) Lakini pia uwepo wa baioanuai nyingi za mimea ya asili na makazi ya wanyamapori kama tembo na wengine hivyo, kuchochea shughuli za utalii;

(iv) Sambamba na hilo kuwepo kwa fursa za ufugaji nyuki kwa wenyeji ili kuwaongezea kipato.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, ni lini mradi wa kufua umeme wa upepo na jua wa MW 100 utaanza rasmi katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhan, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwekezaji aitwaye Upepo Energy alifanikiwa kushinda zabuni ya kuendeleza miradi miwili ambapo Megawatt 100 za umeme zitazalishwa kwa nguvu ya upepo na Megawatt 45.08 zitazalishwa kwa nguvu ya jua.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa majadiliano baina ya TANESCO na Mwekezaji kuhusu bei ya kuuziana umeme (PPA) yamekamilika. Majadiliano kuhusu mkataba wa utekelezaji (Implementation Agreement-IA) yanaendelea. Ipo changamoto ya mwekezaji kuhitaji “Government Guarantee” kinyume na Sera ya Serikali na masharti ya zabuni kama ilivyotangazwa. Iwapo mwekezaji atakubali kutekeleza mradi huu bila masharti mapya aliyoweka, mradi huu utaanza kutekelezwa mwezi Januari, 2023.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya katika Jimbo la Singida Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kujenga vituo vya polisi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhudumia wananchi katika kudhibiti uhalifu. Katika tarafa ya Ilongero eneo la Kinyagigi Jimbo la Singida Kaskazini kunajengwa kituo cha Polisi cha Daraja C na kimefikia hatua ya umaliziaji. Kazi iliyobaki ni kuweka miundombinu ya umeme, maji safi na taka, milango na madirisha, dari, sakafu na kupaka rangi. Kiasi cha fedha shilingi 46,000,000 kinahitajika kumalizia ujenzi, na fedha hizo zinatarajia kutengwa kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka Vifaa Tiba katika Hospitali ya Ilongero pamoja na Vituo vya Afya vya Msange na Mgori Wilayani Singida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali ilipeleka Bohari Kuu ya Dawa Shilingi Bilioni 34 kwa ajili ya ununuzi wa Vifaa Tiba. Tayari Vifaa Tiba vimeanza kusambazwa kwenye Hospitali 67 za Halmashauri ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida ambayo imekwishapokea vifaa vya aina 17 vikijumuisha vifaa vya upasuaji na maabara.

Mheshishimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/ 2023 Serikali imetenga Shilingi bilioni 69.95 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vitakavyopelekwa kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizokamilika.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, lini Miradi ya Umwagiliaji katika Vijiji vya Msange na Mnghamo – Singida Kaskazini itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Ighondo Ramadhani Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi wa Mughamo na kuanza ujenzi wa bwawa na miundombinu mingine ya umwagiliaji katika Skimu ya Msange.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Singida – Ilongero hadi Haydom?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANROADS tayari imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Singida – Ilongero – Haydom yenye urefu wa kilometa 93. Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza kazi ya ujenzi, ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga soko na stendi ya kisasa eneo la Njiapanda Merya Halmashauri ya Wilaya ya Singida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida imeanza utekelezaji wa hatua za awali za ujenzi wa Stendi ya Njiapanda ya Merya. Katika mwaka wa fedha 2019/2020 halmashauri ilitenga kiasi cha shilingi milioni 10 na kufanya upimaji wa eneo la stendi, kufanya usafi na kusawazisha eneo.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inakamilisha tathmini ya gharama za ujenzi wa stendi hiyo na kuanza kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi. Halmashauri inaendelea na maandalizi ya andiko la mradi wa soko na litakapokamilika litawasilishwa Serikalini kwa ajili ya uchambuzi na endapo litakidhi vigezo litatengewa bajeti na kuanza ujenzi, ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kufanya mageuzi ya kilimo nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali wa kuleta mageuzi ya kilimo. Mikakati hiyo inatekelezwa kwa lengo la kubadili kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kuwa kilimo biashara, chenye tija, himilivu kinachoratibiwa na kusimamiwa na Serikali na kushirikisha sekta binafsi ili kuwa na mifumo endelevu ya chakula na kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia misingi hiyo ya kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo, Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024 inatekeleza vipaumbele mikakati yenye lengo la kuongeza tija na uzalishaji; kuongeza ajira zenye staha na ushiriki wa vijana na wanawake kwenye kilimo; kuimarisha usalama wa chakula na lishe; kuimarisha upatikanaji wa masoko, mitaji na mauzo ya nje ya nchi na kuimarisha maendeleo ya ushirika.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaboresha miundombinu ya vituo vya polisi vya Ilongero, Ngamu, Ngimu, Msange na Mtinko katika Jimbo la Singida Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Abeid Ramadhan Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uchakavu wa vituo vya polisi vya Ilongero, Mtinko na Ngamu. Tathmini iliyofanyika imebaini kuwa kiasi cha fedha shilingi 46,480,000 zinahitajika ili kugharamia ukarabati wa vituo hivyo. Katika maeneo ya Ngimu na Msange hakuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya vituo vya polisi. Napenda kutumia fursa hii kuishauri Halmashauri ya Wilaya ya Singida itenge maeneo yenye ukubwa stahiki pamoja na kutoa hatimiliki ili kuwezesha Serikali kupanga na kutelekeza kazi ya ujenzi wa vituo vya polisi kwenye maeneo hayo kwa kushirikiana na wadau. Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Kisangi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwamba maeneo yote ambayo kuna miradi ya makampuni sheria ifuatwe ili waweze kupata ile huduma ya jamii kwa maana CSR. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba sheria zipo kanuni zipo. Tutahakikisha kwamba Halmashauri ya Ilala pia inapata haki yake kutokana na ujenzi wa bomba hili la gesi, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hufanyika kwa kuzingatia mwongozo wa mwaka 2014 ambapo kusudio hujadiliwa katika vikao vya Ngazi ya Halmashauri, Wilaya na Mkoa kisha kuwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa, Serikali imetoa kipaumbele katika kuboresha na kukamilisha miundombinu kwenye maeneo ya kiutawala yaliyopo ili yaweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na baadaye kuendelea na maeneo mengine kwa kufuata taratibu na vigezo vilivyoainishwa. Hivyo, maombi ya kugawa Kata za Mtinko, Makuro, Ughandi na Ngimu pamoja na kijiji cha Mikulu yatafanyiwa kazi na Serikali itakapoanza kuanziasha maeneo mapya ya utawala, ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, kuna mpango gani kuvipatia mawasiliano ya simu vijiji 13 na Kata za Mughunga, Ngimu, Makuro, Mudida, Ughandi, Msisi, Msange na Mgori?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa Kata za Ngimu, Kijiji cha Lamba, Kata ya Msisi Vijiji vya Mnung’una na Mkwae, Kata ya Msange, Vijiji vya Muriga na Endeshi UCSAF imeingia makubaliano na TTCL kupeleka huduma za mawasiliano katika kata tajwa. Aidha, UCSAF pia imeingia makubaliano na Vodacom kwa ajili ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata ya Ughandi, Kijiji cha Misinko na kwa upande wa Kata ya Mudida, Kijiji cha Migugu UCSAF imeingia makubaliano na Kampuni ya Simu ya Halotel.

Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa miradi hii, Serikali kupitia UCSAF itafanya tathmini ya hali ya mawasiliano katika kata hizo na kuchukua hatua stahiki kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukomesha mapenzi ya jinsia moja nchini pamoja na ukatili dhidi ya watoto?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara za kisekta inaratibu utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na tatizo la mmomonyoko wa maadili na ukatili dhidi ya watoto. Mikakati hiyo ni pamoja na:-

(i) Kusimamia utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto pamoja na kuanzisha na kuimarisha madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto katika shule za msingi, sekondari na vyuo; na

(ii) Kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) pamoja na Mpango wa Taifa wa Kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe (NAIHA). Aidha, Wizara itaendelea kutoa elimu kwa umma na kuongeza afua za malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto pamoja na kuimarisha taasisi za familia kwa lengo la kupunguza au kumaliza kabisa changamoto ya mmomonyoko wa maadili nchini, ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kununua Jenereta katika Hospitali ya Ilongero na Vituo vya Afya Mgori, Makuro na Msange - Jimbo la Singida Kaskazini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida Ilongero pamoja na Kituo cha Afya Msange vimeshapokea jenereta kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na taratibu za ufungaji zinaendelea. Kituo cha Afya Mgori kitapokea mgao wa jenereta katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Singida itatenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa jenereta la Kituo cha Afya Makuro.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwajengea masoko wajasiriamali wanaouza mafuta ya alizeti pembezoni mwa barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa wajasiriamali ambao wamekuwa wakiuza mafuta ya alizeti katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Singida. Biashara hii imekuwa ikifanyika pembezoni mwa barabara hali inayosababisha kupungua kwa ubora wa mafuta na kupoteza mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Serikali itafanya tathmini ili kuona njia bora zaidi ya kuwawezesha wafanyabiashara hao kufanya biashara katika maeneo bora na salama zaidi. Ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kuwakamata na kuwachukulia hatua watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM aljibu:-

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 154 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura Na. 16 ya Sheria za Tanzania kinatamka bayana kuwa, vitendo vya mapenzi ya jinsia moja au mahusiano kinyume na maumbile, iwe faragha au kwa makubaliano ni kosa la jinai. Aidha, Kifungu cha 155 cha sheria hiyo, kinaweka adhabu kwa kosa la kujaribu kufanya vitendo vinavyokatazwa chini ya Kifungu cha 154. Hivyo, tutaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi na Mahakama katika kusimamia utekelezaji wa Kifungu cha 154 na 55 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16. Ahsante.