Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Janejelly Ntate James (9 total)

MHE. JANEJELLY J. NTANTE Aliuliza:-

Serikali inawahimiza watumishi kujiendeleza kielimu, lakini baada ya kuhitimu wanapoomba kubadilisha kada huteremshwa vyeo na mishahara:-

Je, Serikali haioni ipo haja ya kuwaacha na mishahara yao ili kujiendeleza isiwe adhabu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntante, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imeendelea kutoa Miongozo mbalimbali kuhusu namna ya kuwabadilisha kada/kazi watumishi waliojiendeleza kitaaluma. Aidha, Serikali inatambua umuhimu wa watumishi kubadilishwa na kupangiwa kazi kulingana na taaluma zao. Hivyo, kupitia Waraka wa Barua Kumb. Na. C/AC.44/45/01/ A/83 ya tarehe 01 Desemba, 2009, Serikali iliweka utaratibu wa kufuata wakati wa kuwabadilisha kada watumishi waliojiendeleza kitaaluma ambapo kuna aina mbili za kubadilishwa kada bila kuathiri watumishi waliomo katika kada hizo.

(i) Kumbadilisha kazi mtumishi aliyejiendeleza na kupata sifa zinazompandisha hadhi kitaaluma, mfano Afisa Kilimo Msaidizi kuwa Afisa Kilimo. Watumishi wa aina hii hubadilishwa hadhi na kuingizwa katika kada mpya kwa kuzingatia cheo cha kuanzia cha kada mpya. Iwapo vyeo walivyokuwa navyo vilikuwa na mishahara mikubwa kuliko mishahara ya cheo walichopewa baada ya kubadilishwa, huombewa kibali cha kuendelea kulipwa mishahara waliyokuwa wakilipwa kama mishahara binafsi hadi watakapopandishwa vyeo vyenye mshahara mkubwa kuliko mishahara binafsi. Utaratibu huu pia unawahusu watumishi wa kada saidizi ambao taaluma walizo nazo hazina vyuo vinavyotoa Astashahada/Stashahada au Shahada katika fani wanazofanyia kazi mfano Walinzi na Wasaidizi wa Ofisi.

(ii) Aina ya pili ni kuwabadilisha kazi watumishi waliojiendeleza katika fani nyingine tofauti na zile walizoajiriwa nazo kwa lengo la kukidhi matilaba ya kazi (job satisfaction) bila kuzingatia mahitaji ya mwajiri. Hawa hulazimika kubadilishwa kazi na kuingizwa katika cheo na ngazi ya mshahara wa cheo kipya na hawastahili mishahara binafsi kutokana na kulinda ukuu kazini na kuwajengea uzoefu wa kazi mpya ambazo wamezichagua wenyewe.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huu, Serikali inasititiza watumishi wa umma kujiendeleza katika kada walizoajiriwa nazo ili kuimarisha ufanisi wa utendaji kazi na kuwa wabobezi katika fani zao. Aidha, watumishi wa umma wanaaswa kupata ushauri kwa waajiri wao wanapotaka kujiendeleza kwenye fani tofauti na wanazofanyia kazi. Waajiri wanao wajibu wa kutenga nafasi za kuwabadilisha kada wale waliojiendeleza katika fani zao ili kuhakikisha kuwa rasilimali hiyo muhimu inatumika ipasavyo. Aidha, waajiri wahakikishe kuwa wanawashauri vizuri watumishi wao kabla ya kubadilishiwa kada/kazi watumishi waliojiendeleza kwenye fani tofauti. Endapo kwa namna yoyote kuna suala ambalo lina mazingira tofauti na haya, mwajiri au mtumishi mwenyewe anaweza kuomba ufafanuzi kutoka katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati wowote.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. JANEJELLY J. NTATE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawalipa posho ya masaa ya ziada Watumishi wa afya waliofanya kazi kubwa sana katika kuokoa maisha ya Watanzania wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilitoa maelekezo kwa Mamlaka za Mikoa na Halmashauri kuandaa madai yote ya posho za masaa ya ziada wanazodai Watumishi wa Afya waliofanya kazi katika mapambano ya kukabiliana na janga la ugonjwa wa UVIKO-19. Serikali ilipokea na kuhakiki madai yaliyowasilishwa ambapo kiasi cha shilingi bilioni 3.44 ndicho kinachostahili kulipwa ikiwa ni stahili kwa watumishi na wazabuni. Kati ya madai hayo, kiasi cha shilingi bilioni tatu sawa na 87% tayari zimepelekwa kwa ajili ya kulipa madeni hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wowote taratibu za kifedha zitakapokamilika, madeni na stahili za watumishi na wazabuni zilizosalia zitalipwa. Aidha, nazielekeza Mamlaka za Mikoa na Halmashauri waliopelekewa fedha za madeni hayo wazisimamie na kuhakikisha kila mtumishi anapata stahiki yake. Ahsante.
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA K.n.y MHE. JANEJELLY J. NTATE aliuliza: -

Je, ni lini serikali itamaliza ujenzi wa Kituo cha Polisi Mbande Kata ya Chamazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi cha Mbande ambacho ni cha Daraja B kilianza kujengwa kwa kutumia Shilingi 16,000,000 zilizochangwa na wananchi mwezi Agosti 2016. Kwa kutumia Shilingi 38,000,000 zilizochangwa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Mradi wa SONGAS na Kampuni ya Tatu Mzuka ujenzi uliendelea hadi upauaji mwaka 2020.

Mheshimwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi, ilitoa Shilingi 30,826,500 mwezi Juni, 2022 ili kuendeleza na kukamilisha ujenzi huo. Hadi sasa milango, grills za madirisha, mfumo wa majisafi na majitaka, umeme na blundering vimekamilishwa. Ni matarajio yetu kuwa Kituo hicho kitakamilika na kuanza kutumika kabla ya mwezi Novemba, 2022. Ninakushukuru.
MHE. JANEJELLY J. NTATE aliuliza: -

Je, lini Serikali itarekebisha Sheria za Utumishi zilizopitwa na wakati hasa kipindi hiki cha teknolojia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, naomba uniruhusu nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini kuendelea kudumu katika Wizara hii ya Utumishi na Utawala Bora. Sasa naomba kujibi swali la Janejelly James Ntate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa maendeleo makubwa ya kiteknolojia ambayo yamekuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha utendaji kazi katika utumishi wa Umma. Ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia, Serikali imeendelea kufanya mapitio ya Mfumo wa Kisheria unaosimamia Utumishi wa Umma ambapo mwaka 2019 Serikali ilitunga Sheria ya Mamlaka ya Serikali Mtandao Namba10 ya Mwaka 2019 ili kuweka mazingira wezeshi ya matumizi ya teknolojia katika utendaji kazi wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitishwa kwa Sheria hiyo kumeisaidia Serikali kuboresha utendaji kazi wake kupitia matumizi ya teknolojia. Pamoja na mambo mengine Sheria hiyo imewezesha kusanifiwa na kujengwa kwa jumla ya mifumo zaidi ya 860 ya TEHAMA Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na hatua za kupitia na kufanya marekebisho ya Sheria mbalimbali zinazosimamia Utumishi wa Umma na Kanuni zake ili kuhakikisha kwamba zinaendana na mabadiliko ya teknolojia.
MHE. JANEJELLY J. NTATE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka Askari Polisi katika Kituo cha Polisi Kata ya Kilungule - Mbagala ili wananchi wa kata hiyo wapate huduma?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dar es Salaam, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari ilishakipangia askari sita kituo kidogo cha Polisi cha Kata ya Kilungule - Mbagala na kinafanya kazi saa 24. (Makofi)
MHE. JANEJELLY J. NTATE aliuliza: -

Je, lini Serikali itaweka mkakati maalum wa kumaliza mashtaka katika Bodi na Mahakama za Rufaa za Kodi?
WAZIRI WA FEDHA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly Ntate, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Oktoba, 2023 Bodi ya Rufani za Kodi ilikuwa na mashauri 889 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha shilingi trilioni 6.46 na dola za Kimarekani milioni 4.66. Katika kipindi hicho, Bodi imesikiliza mashauri 167 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha shilingi trilioni 2.66 na dola za Kimarekani 200,001. Aidha, Baraza la Rufani za Kodi lilikuwa na mashauri 176 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha shilingi bilioni 266.94, ambapo mashauri 91 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha shilingi bilioni 166.32 yamesikilizwa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Bodi ya Rufani za Kodi na Baraza la Rufani za Kodi zinaendelea kutekeleza Mpango Maalum (Special Sessions) ambapo kuanzia mwezi Novemba, 2023 hadi Juni, 2024 wanasikiliza na kumaliza mashauri ya kodi yaliyofunguliwa. Kupitia mpango huo, mashauri mengi zaidi yatasikilizwa katika Mikoa mbalimbali nchini kwa kuzingatia wingi wa mashauri haya ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Morogoro, Ruvuma, Tabora, Mara, Manyara, Kilimanjaro, Iringa, Mbeya, Songwe pamoja na Njombe.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeanzisha Taasisi ya Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (Tax Ombudsman) ambayo jukumu lake kubwa itakuwa ni kupokea malalamiko na kutatua masuala ya kikodi yanayotokana na huduma, hatua za kikodi au utekelezaji wa sheria za kikodi kutoka kwa mlipakodi mbalimbali pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania.
MHE. JANEJELLY J. NTATE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaajiri wataalamu wa kuendesha mikopo ya halmashauri ya 10% badala ya kufanywa na Maafisa Maendeleo ya Jamii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiwatumia Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kusimamia na kuratibu utoaji wa mikopo ya halmashauri ya 10% kwa sababu ya utaalamu wao katika shughuli za maendeleo ya jamii. Aidha, wataalamu hawa wamekuwa wakihusika katika kuunda na kusimamia vikundi mbalimbali vya kijamii hususani wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali kwa sasa ni kuendelea kuwaajiri na kuwajengea uwezo zaidi Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na kuwawezesha kwa kuwapatia rasilimali mbalimbali ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi zaidi.
MHE. JANEJELLY J. NTATE aliuliza:-

Je, Serikali inawasaidiaje walioguswa na Mwongozo wa Waraka wa miaka minne baada ya Serikali kurejea Mwongozo wa Upandaji Madaraja kwa miaka mitatu? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Miundo ya Maendeleo ya Utumishi wa Kada Mbalimbali (Scheme of Services) na miongozo mingine, muda wa watumishi kutumikia cheo kimoja kabla ya kupandishwa cheo kwa watumishi walioajiriwa kwa mara ya kwanza katika Utumishi wa Umma ni angalau kipindi cha miaka mitatu. Hata hivyo, katika kipindi cha zoezi la uhakiki wa vyeti feki na watumishi hewa, baadhi ya watumishi walichelewa kupandishwa vyeo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imechukua jitihada mbalimbali za kuoanisha na kuwianisha upandaji vyeo wa watumishi ambapo katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imewapandisha vyeo watumishi 180,000 wakiwemo watumishi walioathirika na zoezi hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika utekelezaji wa Ikama na Bajeti ya Mwaka 2023/2024, Serikali imewapandisha vyeo watumishi zaidi ya 216,000 wakiwemo walioathirik
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. JANEJELLY J. NTATE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaajiri wataalamu wa maabara shule za sekondari, ili kupunguza mzigo kwa walimu wa sayansi kufanya kazi kama wataalamu wa maabara?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa wataalamu wa maabara shuleni. Wataalamu wa maabara ni wasaidizi muhimu wa walimu wa masomo ya sayansi hasa katika kufundisha kwa vitendo.

Mheshimiwa Spika, kati ya Mwaka 2020/2021 hadi 2022/2023 Serikali iliajiri wataalamu wa maabara 165 ambao walisambazwa katika shule mbalimbali za Serikali kadiri ya mahitaji. Serikali itaendelea kuajiri wataalamu wa maabara kila mara nafasi za kuajiri zinapotolewa kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, kwa sasa walimu wa masomo ya sayansi wamekuwa wakitumika kuandaa vifaa na kemikali kwa ajili ya mazoezi kwa vitendo na mitihani.

Mheshimiwa Spika, natumie fursa hii kuwapongeza walimu wetu wa masomo ya sayansi nchini kwa kazi nzuri wanayoifanya.