MHE. MUSTAFA MWINYIKONDO RAJAB aliuliza:-
Je, lini Serikali itarejesha huduma za afya zilizokuwa zikitolewa kwa wananchi na zahanati ya jeshi, Kambi ya Jeshi Kisakasaka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mustafa Mwinyikondo, Mbunge wa Dimani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Kisakasaka ni Kiteule cha 672 Rejimenti ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tazania ambayo ina kikundi kidogo cha Maafisa na Askari. Kiteule hiki hutoa huduma za matibabu za msingi zinazojumuisha madawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa Wanajeshi waliopo katika Kiteule hicho. Maafisa na Askari waliopo katika Kiteule hicho wanapozidiwa hupelekwa katika Zahanati ya Kikosi Mama iliyopo maeneo ya Welezo umbali wa kilometa 17.
Mheshimiwa Spika, hapo awali Kiteule hiki kilikuwa kinatoa huduma za afya kwa Wanajeshi na wananchi, Huduma kwa wananchi zilisitishwa mwaka 2010 kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za miundombinu kutokukidhi kutoa huduma kwa wananchi wengi na upungufu wa watalaam wa tiba.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika eneo la Kisakasaka kipo Kituo cha Afya cha Fuoni Kibondeni cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichoanzishwa mwaka 2004, ninapenda kuwaomba wananchi waendelee kupata huduma kupitia kituo hicho wakati Wizara inatekeleza mkakati wa kuimarisha huduma za afya Jeshini, kwa kufanya maboresho katika hospitali za kanda, vituo vya afya na zahanati zilizopo katika vikosi chini ya kamandi mbalimbali nchini, zikiwemo zahanati za Jeshi zilizopo Zanzibar, ahsante.
MHE. MUSTAFA MWINYIKONDO RAJAB aliuliza: -
Je, lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Maungani – Dimani kilichojengwa kwa nguvu za wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mustafa Mwinyikondo Rajab, Mbunge wa Dimani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Maungani kilichopo Dimani ulianza mwaka 1990 kwa kutumia nguvu za wananchi. Ujenzi huo ulisimama ukiwa umefikia hatua ya lenta kwa kukosa fedha na kiasi cha shilingi 30,000,000 zilikuwa zimetumika. Tathmini ya kumalizia ujenzi huo ili kuunga mkono nguvu na jitihada za wananchi imeshafanyika na kiasi cha fedha shilingi 108,000,000 kinahitajika. Fedha hizo zitatengwa kwenye mpango wa matumizi ya mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka 2024/2025, nashukuru. (Makofi)