Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Judith Salvio Kapinga (20 total)

MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:-

Je, lini TANESCO watalipa fidia kwa wananchi wa Rorya waliopisha eneo la kupitisha umeme mkubwa toka mwaka 2011?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge ahsanteni sana na kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa mbele, naomba nitumie dakika moja kwa ajili ya shukrani. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya rehema na baraka. Kipekee na kwa unyenyekevu mkubwa naomba kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa aliyoiweka juu yangu na kuniteua niweze kumsaidia kama Naibu Waziri wa Nishati nikimsaidia Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Dotto Mashaka Biteko ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu. Napenda nimwahidi Mheshimiwa Rais imani hiyo aliyonijalia nitaitumikia kwa weledi na ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, TANESCO tayari imekamilisha uthamini na uhakiki wa marudio ya mali zilizoathiriwa na mradi na kwa sasa ipo katika hatua za maandalizi ya malipo. Malipo hayo yanatarajiwa kuanza mwezi Novemba, 2023 na kukamilika mwezi Desemba, 2023.

Mheshimiwa Spika, tunawaomba wananchi wanaosubiri kulipwa fidia wawe na subira wakati maandalizi ya malipo yakiwa yanaendelea kufanyika.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza:-

Je, lini Vijiji vya Namikunda, Chipole, Machombe, Mtakateni, Machenje, Matawale, Mpekeso, Chakama na Kata ya Temeke vitapewa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Mwambe, Mbunge wa Masasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini inatekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ambapo vijiji vyote ambavyo havina umeme Tanzania Bara vitafikiwa na huduma ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Masasi, Mkandarasi NAMIS Corporate Limited alipewa jumla ya vijiji 17 ambavyo havikuwa na umeme. Hadi kufikia tarehe 15 Agosti, 2023, vijiji 11 vimeshawashwa umeme na vijiji sita vitakamilika kabla ya mkataba wa Mkandarasi kwisha tarehe 31 Desemba, 2023. Aidha, vijiji vya Namikunda, Mtakateni, Matawale, Mpekeso na Chakama vimeshawashwa umeme. Vilevile, hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2023, Vijiji vya Chipole na Machombe vitakuwa vimepatiwa umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa zoezi la kusimamisha nguzo katika Kata ya Temeke bado linaendelea na nguzo tayari zimesimamishwa katika Kijiji cha Machenje na zoezi la kuvuta waya linatarajiwa kufanyika mwezi Septemba, 2023. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:-

Je, nini mkakati wa Serikali wa kupeleka umeme wa uhakika katika Halmashauri za Ushetu, Msalala na Kahama?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme kwenye Halmashauri za Ushetu, Msalala na Kahama, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lina mpango wa muda mfupi wa kujenga kituo kidogo cha umeme (Switching Station) kwenye eneo la Nyamirangano lililopo kwenye Halmashauri ya Ushetu. Kupitia kituo hicho kidogo, TANESCO itaongeza njia nyingine za umeme kutokea kwenye kituo hicho kwenda Ushetu, Msalala na Kahama ambazo zitasaidia kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme. Mradi huu unategemewa kukamilika 2024 na unagharimu jumla ya shilingi bilioni 1.2, ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itamaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Manispaa ya Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO imechukua hatua mbalimbali katika kutatua changamoto ya kukatika kwa umeme katika Manispaa ya Morogoro, ikiwa ni pamoja na kufunga transformer yenye ukubwa na uwezo wa MVA 120 katika Kituo cha Msamvu. Kazi hiyo ambayo inagharimu jumla ya shilingi bilioni 10.5 inatarajiwa kukamilika mwezi huu wa Novemba, 2023. Aidha, sambamba na hilo, TANESCO inaendelea na ukarabati wa miundombinu ya usambazaji wa umeme katika Manispaa ya Morogoro ili kuondoa tatizo la kukatikakatika kwa umeme katika Manispaa ya Morogoro, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA K.n.y. MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, lini Mkoa wa Rukwa utaunganishwa na Gridi ya Taifa ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuunganisha Mkoa wa Rukwa na Gridi ya Taifa, Serikali inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme Msongo wa Kilovolt 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga kupitia Mbeya na Tunduma kwa Mradi wa TAZA, umbali wa kilomita 620. Mradi huu pia unahusisha ujenzi wa vituo vya kupooza umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa, Wakandarasi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wameshapatikana na Wakandarasi wa ujenzi wa vituo vya kupooza umeme wapo katika hatua za majadiliano. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi huu wa Novemba, 2023 na kukamilika mwezi Desemba, 2025, ahsante.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha kusambaza umeme kwenye Kata za Kikeo, Kinda na MaskatI – Mvomero?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mvomero ina jumla ya vijiji 129 ambapo kati ya hivyo, vijiji 92 tayari vimeshapatiwa umeme. Vijiji 37 vilivyosalia ambavyo baadhi vinapatikana katika Kata ya Kikeko, Kinda na Maskati vitapatiwa umeme na mkandarasi ambaye yupo maeneo ya mradi anaendelea na kazi za ujenzi wa miundombinu. Mkandarasi huyu anatarajia kukamilisha kazi ifikapo mwezi Juni, 2024, ahsante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: -

Je, wakandarasi wangapi kutoka Mkoa wa Kagera wamepata kazi katika mnyororo wa ujenzi wa Bomba la Mafuta la Hoima – Tanga?

NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakandarasi Wakuu wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani (Tanga) wameendelea kushirikiana na Wakandarasi wadogo wajenzi pamoja na watoa huduma mbalimbali katika maeneo yote inayopitiwa na mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mkoa wa Kagera hadi sasa, jumla ya wakandarasi na watoa huduma 42 wamepatiwa kazi mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa ujenzi wa mradi huu, zikiwemo uuzaji wa vifaa vya ujenzi, huduma za usafirishaji, ulinzi, usambazaji wa mafuta, huduma za umeme na hoteli, nashukuru.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka utaratibu ili bei ya mafuta ya dizeli na petroli iwe moja kwa nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia EWURA inafanya tathmini ya uwezekano wa kupanga bei moja ya bidhaa za petroli nchi nzima. Utaratibu huu uliokuwa ukitumika miaka ya nyuma, ulikwama kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo za kisera na kiusimamizi. Hivyo, wafanyabiashara wa mafuta waliruhusiwa kupanga bei za bidhaa za mafuta kuendana na ushindani wa soko. Tathmini hiyo itakapokamilika, Serikali itaweza kujiridhisha iwapo utaratibu huu una tija ikiwa ni pamoja na kujua namna bora ya kuusimamia ili kuhakikisha changamoto zilizojitokeza kipindi cha nyuma hazijirudii. Ahsante.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka ruzuku kwenye nishati ya gesi ili wananchi waweze kumudu kununua?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015 inaielekeza Serikali kuchukua hatua madhubuti za kufanikisha matumizi ya nishati safi na vifaa sahihi vya kupikia. Kwa sasa Serikali inakamilisha kuandaa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kuhakikisha asilimi 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo Mwaka 2033. Hivyo, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kutatua vikwazo vinavyokwamisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza gharama za upatikanaji wa nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia, ahsante.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-

Je, makubaliano ya mkataba ujao kati ya SONGAS na Serikali yamefikia hatua gani ikiwa mkataba wa awali upo katika mwaka wa mwisho?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mwaka 2001, TPDC iliingia mkataba wa kuuziana gesi asilia iliyotengwa na Songas. Kiasi cha futi za ujazo bilioni 320 za gesi asilia iliyotengwa zilitengwa kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa miaka ishirini (20) kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2024. Mwaka 2004, TANESCO iliingia mkataba wa kuuziana umeme ambapo kwa sasa kiwango kinachozalishwa ni Megawatt 189.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa TPDC na TANESCO wameanza majadiliano na Songas kuhusu mikataba hiyo. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kunakuwa makubaliano ambayo yanazingatia maslahi ya pande zote mbili. Ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-

Je, ni tafiti ngapi za mafuta zimefanyika nchini na yapi matokeo ya tafiti hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, Kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni za Kimataifa za Nishati imeendelea na tafiti za mafuta na gesi nchini kwa maeneo ya baharini na nchi kavu ambapo hadi kufikia mwezi Januari, 2024, jumla ya tafiti 84 zimefanyika.

Mheshimiwa Spika, kupitia tafiti ambazo zimeshafanyika, tumeweza kugundua uwepo wa gesi asilia tu. Hata hivyo, TPDC inaendelea na utafutaji wa mafuta katika maeneo ambayo yana viashiria vya uwepo wa mafuta. Maeneo hayo yanajumuisha bonde la Eyasi Wembere, Ziwa Tanganyika na bonde la Kilosa-Kilombero, ahsante.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka utaratibu ili bei ya mafuta ya dizeli na petroli iwe moja kwa nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia EWURA inafanya tathmini ya uwezekano wa kupanga bei moja ya bidhaa za petroli nchi nzima. Utaratibu huu uliokuwa ukitumika miaka ya nyuma, ulikwama kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo za kisera na kiusimamizi. Hivyo, wafanyabiashara wa mafuta waliruhusiwa kupanga bei za bidhaa za mafuta kuendana na ushindani wa soko. Tathmini hiyo itakapokamilika, Serikali itaweza kujiridhisha iwapo utaratibu huu una tija ikiwa ni pamoja na kujua namna bora ya kuusimamia ili kuhakikisha changamoto zilizojitokeza kipindi cha nyuma hazijirudii. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaweka pipes za gesi Jijini Dar es Salaam kila nyumba ili wananchi wapikie nishati nafuu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imeshasambaza miundombinu ya gesi asilia katika nyumba 880 katika Jiji la Dar es Salaam. Pia imejenga bomba la gesi (pipe) lenye urefu wa kilomita 12.4 kutoka Mwenge hadi Mbezi Beach kupitia barabara ya Bagamoyo na tayari viwanda viwili na hoteli sita zimeshaunganishwa na bomba hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha wananchi wengi Jijini Dar es Salaam wanatumia gesi asilia, TPDC kwa kushirikiana na Kampuni ya TAQA Dalbit inafanya utafiti za mahitaji ya gesi asilia kwa njia za kusambazia utakaokamilika Julai, 2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti huu utaonesha namna bora ya kufikisha mabomba kwenye maeneo yenye changamoto na utabainisha maeneo gani yanayoweza kupelekewa mabomba na maeneo gani hayawezi kupelekewa mabomba ambapo njia nyingine zitatumika kuhakikisha gesi inawafikia wananchi. Ahsante
MHE. YAHYA A. MHATA K.n.y. MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaajiri Madereva na Mafundi ambao wamekuwa vibarua wa muda mrefu TANESCO?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limekuwa likiajiri watumishi wa kada mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya kiuendeshaji na uwezo wa kibajeti kwa mwaka husika. Katika ikama na bajeti ya mishahara ya mwaka 2024/2025 pamoja na mambo mengine, shirika limetenga fedha kwa ajili ya nafasi 430 za ajira mpya kwa mchanganuo ufuatao:-

Mheshimiwa Naibu Spika, wahandisi 67, fundi sanifu 135, fundi mchundo 205 na madereva 23. Aidha, ujazaji wa nafasi hizi utazingatia sheria na taratibu katika utumishi wa umma. Ahsante. (Makofi)
MH. ALLY J. MAKOA aliuliza:-

Je, lini umeme wa REA utapelekwa Mitaa ya Chemchem, Tampori, Kwamtwara, Guluma, Mongoroma, Chandimo, Chang’ombe na Tura?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini imeendelea kutekeleza kazi ya kusambaza umeme katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mitaa ambayo ipo katika mamlaka za miji na miji midogo yenye hadhi sawa na vijiji. Kwa kuwa Jimbo la Kondoa Mjini lipo katika mamlaka ya mji, kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, REA itapeleka umeme katika mitaa 15 ambayo imefikiwa na miundombinu ya msongo wa kati, ikiwemo Mitaa ya Chemchem, Tumbelo na Chang’ombe. Aidha Mitaa ya Tura na Tumbelo imepatiwa umeme kupitia Mradi wa Ujazilizi Mbili (A). Serikali kupitia REA itaendelea kuratibu kazi ya kusambaza umeme katika vitongoji na mitaa ambayo haina umeme kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa njia ya umeme ya msongo mkuu Tabora – Mpanda utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TANESCO inatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 yenye urefu wa kilometa 383 kutoka Tabora hadi Mpanda, Katavi lengo likiwa ni kuunganisha Mkoa wa Katavi katika Gridi ya Taifa. Gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 116. Aidha, utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Septemba, 2022 na umefikia 58%, ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya upya tathimini ya maeneo kwenye Jimbo la Mbulu Mjini ambayo yalirukwa na Mradi wa REA I na II?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mbulu Mjini lina jumla ya vijiji 34, kati ya hivyo, vijiji 31 vimepatiwa umeme na vijiji vitatu vilivyosalia yaani Kwam, Aicho na Tsawa vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA III Mzunguko wa II ambapo kazi imeshaanza na inatarajia kukamilika tarehe 30 Juni, 2024. Aidha, Jimbo la Mbulu Mjini lina mitaa 58 ambapo mitaa 46 imepatiwa umeme na mitaa 12 haina umeme. Kutokana na tathmini iliyofanywa na REA, mitaa 12 iliyosalia itapatiwa umeme kupitia mradi mkubwa wa kupeleka umeme vitongojini ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2024/2025 kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante. (Makofi)
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha kusambaza umeme wa REA kwenye vijiji 20 vilivyobaki – Mkalama?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mkalama lina vijiji 70 na vyote vimepatiwa umeme, vikiwemo vijiji 25 vilivyokuwa katika Mradi wa Kusambaza Umeme, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili, uliotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Aidha, Jimbo hilo lina vitongoji 388 ambapo vitongoji 192 vimepatiwa umeme na vitongoji 196 bado havijapatiwa umeme. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia REA imetenga fedha za kutekeleza mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 15 vya kila jimbo ikiwemo Jimbo la Mkalama. Kwa sasa, REA inakamilisha taratibu za kuwapata Wakandarasi watakaotekeleza mradi huu. Vitongoji vitakavyobakia vitapatiwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha zoezi la kupeleka umeme katika Shule zote na Taasisi za Dini katika Mkoa wa Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma una vijiji 307 ambapo vijiji 257 vimepatiwa umeme na kazi ya kupeleka umeme katika vijiji 50 vilivyosalia inaendelea kupitia Mkandarasi aitwaye State Grid Electrical and Technical Works Limited anayetekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili. Wakati wa uunganishaji wa wateja katika miradi, wakala hutoa kipaumbele kwa taasisi za umma zikiwemo shule na taasisi za dini. Serikali kupitia Wakala, inaendelea kuratibu upatikanaji wa umeme katika taasisi za umma vijijini, hususan Shule na Taasisi za Dini kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itakuja na mkakati wa kutumia gesi asilia kuendesha magari nchini ili kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikwishaanza programu mbalimbali za matumizi ya gesi iliyogandamizwa (CNG) kwenye magari. Mpaka sasa Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imefanikiwa kufungua vituo vitano na inatarajia kufungua vituo vingine vitatu ifikapo mwezi Desemba, 2024. Aidha, jumla ya vituo 16 (vituo mama viwili na vituo vidogo 14) vikijumuisha vituo vinavyohamishika vinatarajiwa kufunguliwa ifikapo mwezi Desemba, 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza upatikanaji wa gesi asilia, mwaka 2022 Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) lilifunga seti tatu za compressor zilizoweza kuongeza pressure ya futi za ujazo milioni 20. Kwa sasa TPDC imeanza utaratibu wa kumpata mzabuni kwa ajili ya kufunga mitambo ya kuongeza mgandamizo wa gesi yenye futi za ujazo milioni 20 kwenye kitalu cha uzalishaji Songosongo. Kazi hiyo inatarajia kukamilika mwezi Machi, 2026.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine ili kuhamasisha matumizi ya magari yanayotumia gesi asilia, Serikali inaendelea kutoa msamaha wa kodi kwenye mitungi ya kuhifadhi gesi iliyoshindiliwa kwenye magari na kupunguza ushuru wa magari yanayotumia gesi asilia. Tunaamini mikakati yote hii itachangia kuongeza idadi ya magari yanayotumia gesi nchini itakayopelekea kupunguza uagizaji wa mafuta nje ya nchi na mwisho kuokoa fedha za kigeni, ahsante.