Supplementary Questions from Hon. Ali Juma Mohamed (7 total)
MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri nilikuwa na swali moja tu la nyongeza.
Serikali ina mpango gani wa kutafuta fursa mbalimbali za ajira ambazo ziko katika nchi mbalimbali duniani, kwa ajili ya Watanzania hususan nchi ya Qatar ambayo mwakani ni wenyeji wa Kombe la Dunia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Ali Juma Mohamed, Mbunge wa Shaurimoyo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuchangamkia fursa kwa ajili ya Watanzania kwenda kufanya kazi nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, pili, napenda kukufahamisha kuwa Serikali imeanza mazungumzo na nchi mbalimbali ambazo zina fursa ya ajira hizo, hasa zikiwemo nchi za Ghuba, ili kuwa na utaratibu maalum wa kutoa quarter maalum kwa ajili ya Tanzania. Ninapenda kutoa taarifa pia kwamba tayari Tanzania imesaini mkataba na nchi ya Qatar kwa ajili ya kuwa na quarter maalum ya watanzania kwenda kufanya kazi huko, hasa katika kipindi hiki ambako tunaelekea kwenye mashindano ya World Cup ambayo yanaanza Novemba mwakani 2022. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nilikuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza.
Je, Serikali ina mpango gani kwa kutumia ofisi zetu za kibalozi kuwasaidia wale vijana wetu wa Kitanzania ambao tayari wameshapata fursa ya kufanyakazi nje ya nchi, lakini mara kwa mara wamekuwa wakipata matatizo na shida ambazo wanakosa kusaidiwa?
Lakini la pili Serikali ina takwimu rasmi za vijana wote ambao wanafanyakazi nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mohamed kwa kuangalia sana haya maslahi ya ajira ya Watanzania nimpongeze sana kwa kazi hiyo nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi yetu, Ofisi ya Waziri Mkuu inashirikiana vizuri na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje kwa kuhakikisha kwamba masuala haya yanaratibiwa vizuri na hata hivi sasa tumekwisha kuanza utambuzi huo wa vijana wapo ambao walikuwa wanaenda wenyewe bila kutoa taarifa kwenye ubalozi au kwenye nchi na wamekuwa wakipata matatizo mbalimbali tumewaomba na tumetoa rai kwamba waendelee kujisajili kwenye Balozi zetu.
Lakini zaidi ya hapo pia katika mikataba ambayo tumeingia sasa maalum, kwa mfano Qatar tunakuwa na Kombe la Dunia hivi karibuni wafanyakazi wengi tunatarajia kuwapeleka kule na waweze kupata ajira.
Kwa hiyo, haya tunayaratibu vizuri kupitia Wizara ya Mambo ya Nje kwa kushirikiana na balozi zetu huko nchini na hivi karibuni mmeona Balozi wa Ubelgiji alitoa takwimu za maeneo ambayo Watanzania wangeweza kuchangamkia kuweza kupata ajira. Kwa hiyo uratibu upo kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu katika maeneo hayo.
MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza hivi sasa shirika letu la Ndege Tanzania limeanza safari zake za kubeba mizigo kwa ajili ya safari Guangzhou China, inaondoka China na kupitia Zanzibar na baadaye inarudi Zanzibar. Shirika hivi sasa wanatumia ndege yake ya Boeing 787 kwa ajili ya kubeba mizigo hiyo. Ndege hii imeundwa kwa ajili ya kubeba abiria na mizigo lakini eneo kubwa ya ndege hii ni kwa ajili ya kubeba abiria. Shirika letu sasa linabeba mizigo bila ya abiria kwa kwenda huko China.
Je, Shirika halioni hivi sasa kuendelea kufanya hivyo ni kuendelea kulitia hasara?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, hivi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la abiria kati ya Zanzibar, Pemba na Dar es Salaam. Je, ni lini Shirika la Ndege la Air Tanzania litaanza safari zake katika Kisiwa cha Pemba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ali Juma Mohamed Mbunge wa Shaurimoyo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna Ndege aina ya Dreamliner 787-8 ambayo inafanya biashara kati ya Tanzania na China na Ndege hii imekuwa ikibeba abiria lakini kipindi cha Covid 19 China kama tunavyofahamu kuingia abiria yeyote ndani ya nchi ya China. Kwa hiyo tukaona ni heri na bora Ndege hii aina ya 787-8 Dreamliner ambayo ina uwezo wa kubeba tani 40 ifanye biashara ya kubeba mizigo kuliko tungeiacha kuwa grounded na ingekuwa gharama zaidi kuliko hivi sasa ambavyo ipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge anatamani ama anapenda kwamba tuanzishe safari za kwenda Pemba. Nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote wa Zanzibar kwamba Shirika letu la ATCL litaanza safari zake za Pemba mwaka wa fedha 2023/2024 kwa maana ya kwamba mwaka ujao, ahsante. (Makofi)
MHE. ALI JUMA MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina masuala mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2025 iliielekeza Serikali kuhakikisha inaongeza Ofisi ndogo za ubalozi kule Zanzibar lakini pia mashirika pamoja na taasisi za kimataifa.
Mheshimiwa Spika, suala la mwanzo nililokuwa nataka kujua. Je, kuna ofisi ngapi na mashirika mangapi ya kimataifa ambayo yamefunguliwa kule Zanzibar?
Mheshimiwa Spika, suala la pili, nilikuwa nataka kufahamu ni sababu zipi ambazo zimesababisha kufungwa kwa Ofisi ndogo ya Ubalozi wa Egypt kule Zanzibar? Ukizingatia, Egypt ni nchi ya mwanzo baada ya mapinduzi ya mwaka 1964 kutambua Mapinduzi ya Zanzibar. Pia, kipindi chote imekuwa ikiisaidia sana Zanzibar katika sekta ya elimu na kilimo. Je, ni sababu zipi zimesababisha Ofisi hii kufungwa ambayo iko takribani miaka 40 sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE (MHE. BALOZI MBAROUK NASSOR MBAROUK): Mheshimiwa Spika, mbali na Konseli kuu ambazo ziko Zanzibar lakini pia kuna ofisi za mashirika ya kimataifa hususani ya UN kama vile UNDP, UNESCO, UN AIDS, UN WOMEN, FAO, ILO na nyinginezo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu nchi ya Misri kufunga ubalozi wake mdogo Zanzibar. Katika ulimwengu wa kidplomasia, kufungua na kufunga ubalozi ni suala la kawaida. Mara nyingi sababu zinazopelekea nchi kufunga ubalozi au ubalozi mdogo inakuwa kwanza ni kutetereka au kuharibika kwa mahusiano baina ya nchi na nchi. Pia, kubadilika kwa muelekeo wa nchi kistratejia na kimaslahi, pia kuna suala la usalama na mwisho kuna suala la uchumi katika kubana matumizi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Misri hawakueleza bayana sababu zilizosababisha kufunga ubalozi wao mdogo Zanzibar mwaka 2012. Vilevile naomba kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba, mbali na Nchi ya Misri kufunga ubalozi wake hapo Zanzibar lakini uhusiano kati ya Misri na Zanzibar umeendelea kuimarika siku hadi siku. Pia, wanashirikiana katika katika masuala mbalimbali ya kimkakati kama vile kilimo na elimu. Ahsante sana.
MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa vile sasa hivi ajali za bodaboda zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku, kwa nini Serikali isiboreshe sasa mfumo wa usafirishaji katika miji yetu ili kupunguza matumizi ya mfumo wa usafirishaji usio rasmi? (Makofi)
Swali la pili, ninataka nifahamu Serikali inatumia utaratibu gani sasa kuwapa leseni madereva wa bodaboda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, Ali Mohamed, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya utaratibu na mapendekezo ya kuboresha mfumo wa usafiri ili kuwa na mfumo rasmi, tunachukua pendekezo lako na tutawasiliana na mamlaka ya utoaji wa leseni kwa maana ya LATRA wa usafirishaji abiria waweze kulizingatia katika uboreshaji wa mfumo huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utoaji wa leseni, matakwa ya sheria yanataka Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na TRA waweze kutoa leseni kwa mtu ambaye amefuzu mafunzo ya udereva kwenye vyuo na taasisi zinazotambuliwa na Serikali, huo ndiyo mfumo. Kwa hiyo, yeyote aliyepata leseni nje ya utaratibu huo ikibainika leseni hiyo hufutwa na hatua za kisheria huchukuliwa dhidi yake, nashukuru.
MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina ushauri mdogo tu kwa Serikali. Kwa vile haya makosa ya uhalifu mitandaoni yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku, ninaishauri Serikali ijaribu kukiwezesha Kitengo hiki cha Cyber, ili kiwe na mfumo mzuri wa kufanya kazi zake kwa wepesi pamoja na kujaribu kurekebisha baadhi ya sheria ambazo zimekuwa kikwazo katika utendaji wao wa kazi za kila siku.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, tumepokea ushauri na tutaufanyia kazi, ahsante.
MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza. Kwa vile bado kuna wimbi kubwa la watumishi ambao wamestaafu lakini hawajapata malipo yao ya kimsingi kwa maana ya kiinua mgongo. Je, Serikali haioni sasa kubadilisha sheria ili watumishi wa Serikali waendelee kubaki katika utumishi wao hadi pale taratibu za malipo zitakapokuwa zimekamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ali Juma Mohamed, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba kwa sasa kwa sababu tayari tumekwishatungia sheria na inataka ndani ya siku 60 mafao yawe yamekwishalipwa. Kwa mfano, kama ana kesi mahususi yeye ya wastaafu ambao hawajaweza kupata, niipate kwa sababu, mpaka sasa hivi kwa Mfuko wa PSSSF kwa mwaka wa fedha 2023/2024, wastaafu walioomba wote kwa ujumla walikuwa 8,957, kati ya hao 5,016 wamekwishalipwa ndani ya siku 60, ambao ni sawa na 54% kwa PSSSF.
Mheshimiwa Spika, lakini pia tumeendelea kuhakikisha kwa wale 3,941 ambao wana changamoto pengine labda kutokana na waajiri wao kutokupeleka michango au mapungufu ya kinyaraka na mazingira mengine ambayo yanasababisha pengine kuna changamoto za kumbukumbu yameendelea kushughulikiwa na yanapofikishwa mwisho ndani ya wiki mbili anakuwa amelipwa mafao yake. Kwa upande wa Mfuko wa NSSF kwa private sector, nakumbuka tulikuwa na maombi zaidi ya 3,344 ya wastaafu ambao walikuwa wanahitaji kulipwa. Kati ya hao zaidi ya 3,325 tayari wamekwishalipwa na hii ni sawa na zaidi ya 90% ya ulipaji ndani ya siku 60.
Mheshimiwa Spika, kuna wale 16 tu ambao bado kwa NSSF nao pia ni kwa sababu waajiri hawajapeleka michango na kuna kesi zipo mahakamani na tumeendelea kuchukua hatua. Kwa hiyo, sasa hivi hakuna mstaafu ambaye anachelewa kupata mafao yake au kulipwa pensheni yake ndani ya siku 60 kwa mujibu wa sheria, tunalitekeleza hilo na kama kuna hizo kesi muda wote tumeendelea kuomba waweze kutufikishia ofisini kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki, ahsante.