Supplementary Questions from Hon. Shabani Hamisi Taletale (22 total)
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza samahani, kwa kuwa leo ni siku yangu ya kwanza na mara yangu ya kwanza kuongea, napenda niwashukuru ndugu zangu wa Morogoro Kusini Mashariki. Pia nishukuru familia yangu, mama yangu mzazi na marehemu mke wangu popote alipo, Mungu amlaze mahali pema.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa majibu ya Serikali na kwa kutambua ufinyu wa bajeti na kuzingatia umuhimu wa barabara hii, je, Serikali iko tayari kushirikiana nami kutafuta mkandarasi wa building and finance? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamisi Shabani Taletale, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nimemuelewa vizuri kwamba Serikali itashirikiana naye kutafuta mkandarasi, utaratibu wa kutafuta wakandarasi ni utaratibu ambao uko kisheria na ni utaratibu ambao unatekelezwa na Serikali kupitia mamlaka husika.
Mheshimiwa Maibu Spika, kwa kuwa tumeahidi katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Rais katika hotuba yake barabara anayoizungumzia ameiahidi, hivyo, nimhakikishie tu kwamba itajengwa na kukamilika katika kipindi hiki cha miaka mitano ambayo Ilani hii itakuwa inatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli, alipopita kwenye Jimbo letu la Morogoro Kusini Mashariki alituahidi barabara ya Bigwa – Kisaki. Naomba kuiuliza Serikali barabara hii itaanza lini kujengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Babu Tale, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipotembelea Mkoa wa Morogoro, moja ya ahadi alizotoa na ilikuwa ni maagizo kwamba barabara hii ijengwe haraka kwa kiwango cha lami. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Babu Tale, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki na wananchi anaowaongoza wa Jimbo lake kwamba barabara hii kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri itajengwa kwa kiwango cha lami kuanzia kilometa 50. Kama navyoongea naye mara kwa mara, nimhakikishie kwamba barabara hii itakuwa ni kati ya barabara ambazo zitatangazwa muda si mrefu kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya swali dogo la nyongeza. Naomba kuuliza, Serikali iliahidi kutangaza tender ya ujenzi wa barabara ya Bigwa – Kisaki.
Je, ni lini Serikali itatangaza barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kwamba kwa sasa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ipo kwenye hatua mbalimbali za kutangaza baadhi ya barabara ili ziweze kujengwa kwa hatua mbalimbali, nyingine kwa kiwango cha lami na mengine ni madaraja ya kujengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira na maelezo mengine ya ziada yatatolewa kwenye bajeti yetu ambayo inatarajiwa kusomwa Jumatatu ijayo tarehe 17 na tarehe 18. Ahsante.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua barabara yetu ya Ubena Zomozi-Ngerengere ya kilometa 10?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Taletale Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Mbena Zomozi imeshapata kibali kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami hizo kilomita alizozisema. Ahsante.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nauliza Serikali, je, ni lini itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Bigwa – Kisaki ya kilometa 78?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamisi Taletale, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Bigwa – Kisaki (kilometa 78) ilishapata kibali na taratibu za kukamilisha zabuni hizo ilitangazwa, lakini itatangazwa tena kwa ajili ya kupata mkandarasi. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa kibali kilishatolewa, kwa hiyo ni taratibu tu za manunuzi ambazo zinaendelea ili ianze kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kuiuliza Serikali; je, ni lini barabara yetu ya Bigwa - Kisaki ya kilometa 78 itaanza matengenezo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Taletale, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara hii ilitangazwa, lakini kilometa zilikuwa chache na sasa barabara hii tunategemea kuitangaza muda wowote kuijenga kwa kiwango cha lami na tuko kwenye hatua za mwisho za manunuzi na barabara hii nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge itatangazwa mwaka huu wa fedha na itaanza kujengwa hizo kilometa 78, ahsante.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza Serikali ni lini itaanza kujenga barabara yetu ya Bigwa
– Kisaki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Taletale Mbunge wa Morogoro Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya Bigwa – Kisaki ni kati ya barabara 22 ambazo ziko kwenye taratibu mbalimbali za manunuzi ili ujenzi wa barabara hii muhimu ya kutoka Bigwa – Kisaki, kwenda Bwawa la Nyerere uanze. Kwa hiyo, muda wowote taratibu zikikamilika, barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba Serikali barabara yetu Bigwa na barabara yetu Ngerengere, Matuli, Matulazi:-
Je, lini Serikali itatuangalia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamisi Taletale, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya Ngerengere kwenda Matulazi ni moja ya barabara muhimu na ya kipaumbele. Moja ya kazi kubwa ambayo tunaifanya sasa hivi, ni kufanya usanifu ili sasa tuiweke katika mipango yetu ya kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo. Ahsante sana.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Moja ya changamoto kubwa ya wananchi wa Morogoro Kusini Mashariki na Morogoro Vijijini kwa ujumla ni ukosefu wa mitaji. Je, Serikali ina uratatibu gani wa kutuletea mitaji wana Morogoro Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Hamisi Shabani Taletale, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mitaji kwa wakulima ni suala ambalo tunalipa kipaumbele Serikali, tupo tayari kukaa na Mheshimiwa Mbunge pamoja na ushirika wa wakulima hawa ili tuangalie fursa ambayo wanaweza kuipata kuimarisha mitaji yao.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kuiuliza Serikali; je, ni lini italeta mradi wa maji kwenye Tarafa ya Ngerengere?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Taletale kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Ngerengere ipo kwenye mpango wa Wizara, Mheshimiwa Waziri alishapita maeneo hayo. Mheshimiwa Mbunge tuko mbioni kuleta mradi huu wa maji tutatumia Mradi wa Chalinze ama Morong’anya kuhakikisha maji yanafika Ngerengere.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, ni lini Serikali itaenda kujenga barabara ya Bigwa – Kisaki ya kilometa 78 kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Taletale, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba barabara ilishatangazwa kwa ajili ya kuijenga na kwa hiyo sasa hivi ipo kwenye hatua ya manunuzi kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini Serikali italeta mawasiliano katika Kata ya Gwata, Tununguo na Tomondo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamisi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kata ya Gwata ipo katika utekelezaji na tusubiri Mheshimiwa Mbunge mradi huu ambapo ukiwa unaendelea kutekelezwa ndani ya kipindi cha mkataba, tunaamini Kata ya Gwata itakuwa imefikishiwa huduma ya mawasiliano, ahsante sana.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza Serikali Bunge lililopita iliahidi kujenga na kusaini barabara ya Bigwa – Kisaki hadi sasa ipo kimya; je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Bigwa – Kisaki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, barabara hiyo imeshapata mkandarasi na sasa hivi kinachoandaliwa tu ni taratibu za kuisaini hiyo barabara. Kwa hiyo tuna barabara kama 16 ambazo zinaandaliwa utaratibu mzuri wa kuzisaini ili Wakandarasi waanze kazi, ikiwepo na hiyo barabara ya Bigwa – Kisaki.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza, je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya maji katika Tarafa ya Ngerengere?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamisi Taletale, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Tarafa ya Ngerengere tayari tuna miradi ambayo ipo kwenye utekelezaji, lakini tuna mipango thabiti ya kuona kwamba eneo hili nalo linaenda kupata huduma ya maji safi na salama mwaka ujao wa fedha Mheshimiwa Mbunge atashuhudia shughuli nyingi sana zikifanyika katika Tarafa hii.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kituo cha afya cha Kata ya Mkuyuni kinachangamoto ya gari la wagonjwa; je, na sisi lini tutaletewa gari la wagonjwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamisi Taletale, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, magari haya yatakayo kuja yatapelekwa kwenye vituo vyetu vikiwemo vya Morogoro ambavyo vitakidhi vigezo. Kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutawasiliana tuone namna ya kufanya tathimini kwenye kituo hiki kama kinakidhi vigezo hivyo, ahsante.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, kutokana na ahadi ya Serikali barabara yetu ya Ubena Zomozi – Ngerengere je, lini itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Taletale Mbunge wa Morogoro Kaskazini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara iliyotajwa imetengewa fedha katika bajeti hii kuianza kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama yote hayo wanayafahamu, sasa ni zaidi ya mwaka wa tatu tumesimama hapa kuomba Kituo cha Afya cha Ngerengere, hakina jengo la Huduma ya Mama na Mtoto, Mortuary hakuna. Wakazi wa Kata ya Ngerengere ni 15,000, Kata ya jirani ya Kidugalo ni 8,000, leo hii Mheshimiwa Waziri anajibu majibu ambayo anafahamu tatizo liko wapi, mpaka nashindwa kuelewa. Naomba kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri; je, ni lini mtakwenda kutatua hili tatizo? Siyo kwamba majibu mnayo na utatuzi hakuna, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamisi Shabani Taletale, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa upanuzi wa Kituo cha Afya cha Ngerengere. Nasi kama Serikali, taarifa hii tunaifahamu na ndiyo maana tulitoa maelekezo kwa Mkurugenzi, kuongeza eneo la ujenzi wa Kituo cha Afya, ekari 4 na nusu hazitoshi kujenga Kituo cha Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya hiki kilikuwa ni cha Mission, kwa hiyo, kilichukuliwa na Serikali kikiwa tayari kinatoka Mission. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba mara hili eneo la ekari mbili la Posta ambalo halijaendelezwa, ambalo liko mkabala kabisa na Kituo hiki, likishachukuliwa na kuwa na ekari sita na nusu, basi mapema iwezekanavyo tutatafuta fedha kwa ajili ya kuongeza majengo haya ambayo yanapungua katika Kituo cha Afya cha Ngerengere, ahsante. (Makofi)
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama yote hayo wanayafahamu, sasa ni zaidi ya mwaka wa tatu tumesimama hapa kuomba Kituo cha Afya cha Ngerengere, hakina jengo la Huduma ya Mama na Mtoto, Mortuary hakuna. Wakazi wa Kata ya Ngerengere ni 15,000, Kata ya jirani ya Kidugalo ni 8,000, leo hii Mheshimiwa Waziri anajibu majibu ambayo anafahamu tatizo liko wapi, mpaka nashindwa kuelewa. Naomba kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri; je, ni lini mtakwenda kutatua hili tatizo? Siyo kwamba majibu mnayo na utatuzi hakuna, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamisi Shabani Taletale, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa upanuzi wa Kituo cha Afya cha Ngerengere. Nasi kama Serikali, taarifa hii tunaifahamu na ndiyo maana tulitoa maelekezo kwa Mkurugenzi, kuongeza eneo la ujenzi wa Kituo cha Afya, ekari 4 na nusu hazitoshi kujenga Kituo cha Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya hiki kilikuwa ni cha Mission, kwa hiyo, kilichukuliwa na Serikali kikiwa tayari kinatoka Mission. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba mara hili eneo la ekari mbili la Posta ambalo halijaendelezwa, ambalo liko mkabala kabisa na Kituo hiki, likishachukuliwa na kuwa na ekari sita na nusu, basi mapema iwezekanavyo tutatafuta fedha kwa ajili ya kuongeza majengo haya ambayo yanapungua katika Kituo cha Afya cha Ngerengere, ahsante. (Makofi)
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kuuliza Serikali ni lini itakuja kukamilisha mawasiliano katika Kata ya Gwata, ukizingatia ipo barabarani karibu Morogoro, kwaheri Morogoro na bado watu hawapatikani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamisi Taletale, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika minara 758 bahati mbaya Kata hii hatukuiingiza, na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutafuta fedha na kuna minara takribani 636 ambapo katika hiyo, minara 15 inaenda kwenye upande wa TBC.
Mheshimiwa Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Kata yake tutaiingiza kwenye minara hiyo 636, ahsante sana.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali italeta huduma ya X-ray katika Kituo cha Afya cha Mkuyuni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba Kituo cha Afya cha Mkuyuni bado hakina jengo la X-ray na majengo haya ni maalum kwa sababu mashine zile ni mashine za mionzi. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Morogoro kutenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo maalum kwa ajili ya mashine ya X-ray na baada ya kukamilisha tutapeleka mashine ya X-ray kwa ajili ya huduma hizo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba kuuliza kwamba, Mheshimiwa Waziri wanasema uhondo wa ngoma uingie ucheze. Naomba, kama itawezekana, Wizara ije kwenye Tarafa ya Ngerengere. Kiukweli kabisa, sisi wakazi wa Kata ya Tununguo tuna changamoto kubwa sana ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kusikia kwamba kwamba tutapata visima sita, lakini hayo maji hayanyweki kabisa. Je, Serikali ni lini itaweza kutoka kwenda kwenye Tarafa nzima ya Ngerengere ili kuona hatima ya sisi Wanangerengere kupata maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua changamoto iliyopo katika Tarafa hii ya Ngerengere. Vilevile nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwa kushirikiana na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kubainisha maeneo yenye changamoto ya maji ili Serikali ikachukue hatua na wananchi waweze kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Sekta ya Maji iko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kujionea hali ya upatikanaji wa huduma ya maji ili nasi tuingize katika mipango yetu ya muda mfupi na kati ili kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Afya cha Ngerengere maana hatuna jengo la mama na mtoto wala sehemu ya kuhifadhia maiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli Kituo cha Afya cha Ngerengere hakina jengo la mama na mtoto, lakini pia hakina jengo la kuhifadhia maiti. Tulishawasiliana na Mheshimiwa Taletale na tumekubaliana kuanza kutenga fedha kwa awamu kupitia mapato ya ndani, lakini pia kupitia Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi huo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kutafuta fedha na itaenda kujenga majengo hayo kwa awamu.