Primary Questions from Hon. Aleksia Asia Kamguna (7 total)
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza: -
Je, Serikali imejipangaje kutoa elimu juu ya ugonjwa wa fistula?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aleksia Asia Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupambana na ugonjwa wa fistula Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa njia zifuatazo: -
a. Kuzuia mimba za utotoni kupitia elimu ya uzazi kwa vijana.
b. Kuwaelemisha akinamama kuhudhuria kliniki mapema ili wapate huduma muhimu na kupata ushauri wa mpango wa kujifungua.
c. Kutoa elimu kwa wajawazito kujifungulia katika vituo vya afya ili kuwahi kupatiwa msaada kama kutatokea tatizo la uchungu pingamizi au jingine.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuzuia wafugaji kuchunga mifugo katika Hifadhi ya Julius Nyerere?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aleksia Asia Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Sura Namba 283 iliyorejewa mwaka 2022, Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura 282 na Sheria ya Misitu ya mwaka 2002, zimeweka zuio la kuingiza mifugo ndani ya maeneo ya hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya uingizaji wa mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo Hifadhi ya Taifa Nyerere ni ya muda mrefu. Wizara inakabiliana na changamoto hii kwa kuimarisha doria katika maeneo ya hifadhi na kuwachukulia hatua wanaoingiza mifugo hifadhini kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo. Aidha, Wizara inaendelea kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukabiliana na changamoto hiyo.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA K.n.y. MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza: -
Je, Serikali imejipangaje kukomesha uvuvi haramu wa kuvua samaki kwa kutumia nyavu zenye matundu madogo?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aleksia Asia Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaboresha mfumo wa utoaji wa vibali vya kuingiza zana za uvuvi nchini ili kudhibiti uingizwaji wa zana haramu ikiwemo nyavu zenye matundu madogo na makokoro. Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha shughuli za ukaguzi wa zana za uvuvi zinazoingizwa nchini kupitia njia za mipakani na bandarini kwa kuongeza idadi ya watumishi na vitendea kazi. Hili litaongeza wigo wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya mipakani na bandarini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Rais - TAMISEMI imeandaa Mkakati wa muda mfupi na muda mrefu wa kudhiti vitendo vya uvuvi haramu nchini. Utekelezaji wa mkakati huo utashirikisha viongozi wa ngazi za Vijiji, Kata, Tarafa, Wilaya na Mikoa ili kudhibiti matumizi ya zana haramu ikiwemo nyavu zenye matundu madogo, kokoro na nyinginezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wavuvi, waingizaji na wasambazaji wa zana za uvuvi pamoja na jamii kwa ujumla kuhusu athari za matumizi ya zana haramu za uvuvi zikiwemo nyavu zenye matundu madogo, kokoro, timba, freemaya pamoja na matumizi ya vilipuzi katika uvuvi, ahsante.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha kilimo cha Mpunga katika Mkoa wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aleksia Asia Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imetekeleza mradi wa Kuongeza uzalishaji na tija ya zao la Mpunga katika Mkoa wa Morogoro. Matokeo hayo yamechagizwa na kuongezeka kwa upatikanaji wa mbegu bora za mpunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mpunga ulifanyika katika Halmashauri za Wilaya za Mlimba, Ifakara, Kilosa na Mvomero ambapo jumla ya maghala matano yamejengwa.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga uzio katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aleksia Asia Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi huu utaanza mwezi Januari, 2024 na kukamilika mwezi Septemba, 2024.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza: -
Je, Serikali imejipangaje kukomesha migogoro kati ya wakulima na wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendekeo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aleksia Asia Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwepo migogoro ya ardhi baina ya makundi mbalimbali ya watumiaji ardhi likiwemo kundi la wakulima na wafugaji. Katika kukabiliana na hali hii Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa vijiji vyote nchini vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ili kuepusha mwingiliano baina ya watumiaji hawa wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati hiyo ni pamoja na kuhamasisha halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika bajeti zao kila mwaka. Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi na kubuni programu na miradi mbalimbali ili kuongeza kasi ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi za vijiji. Hadi kufikia Januari, 2024 jumla ya vijiji 3,799 vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi kati ya vijiji 10,744 vilivyopimwa hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Wizara ni kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi 2,158 kupitia Mradi wa LTIP, Mradi wa Kupanga Matumizi ya Ardhi na bajeti za halmashauri ifikapo 2024. Hii itafanya idadi ya vijiji vilivyopimwa vitakavyokuwa vimepangwa kufikia 5,839 ambavyo ni zaidi ya nusu ya vijiji vilivyopimwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa halmashauri zote nchini kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika bajeti zao kila mwaka ili kuondoa migogoro ya baina ya makundi ya watumiaji wa ardhi ikiwemo wakulima na wafugaji nchini.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN K.n.y. MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupanda miti katika Mkoa wa Morogoro hususani Milima ya Uluguru na kandokando ya Mto Fulua, Mnyera na Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aleksia Kamguna, kama ifuatayo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha uhifadhi unaendelezwa katika Milima ya Uluguru, zoezi la kupanda miti limeendelea kufanyika katika Mkoa wa Morogoro hususani katika milima hiyo. Mathalani, kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi, 2024, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na halmashauri na wadau mbalimbali imepanda jumla ya miti 9,026,605 ikiwemo miti 1,000,000 ya mikarafuu kwa ajili ya viungo katika mpaka wa msitu wa Mazingira Asili Uluguru, pamoja na vijiji vinavyopakana na msitu huo na katika Mkoa wa Morogoro kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maeneo ya Mto Fulua, Mnyera na Kilombero, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali, wananchi na wadau imeendelea na jitihada za kutunza maeneo hayo kwa kupanda miti rafiki wa maji pamoja na kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa uhifadhi na kupanda miti stahiki katika maeneo ya kingo za mito.