Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Aloyce John Kamamba (32 total)

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kupeleka huduma kwa wananchi. Tatizo lililojitokeza hapa ni baadhi ya vitongoji hasa katika Mji wa Kakonko kurukwa. Mfano, vitongoji vya Itumbiko, Mbizi, Kizinda, Cheraburo zikiwemo taasisi kama shule za makanisa. Kwa nini taasisi na vitongoji hivi vinarukwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, lini sasa haya maeneo ambayo yamerukwa yatapewa huduma hiyo ya umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce Kamamba, Mbunge wa Kakonko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, vitongoji vya Jimbo la Kakonko havijarukwa isipokuwa Serikali inaendelea kupeleka umeme katika vijiji na vitongoji vyetu kwa awamu. Kwa hiyo, kadri ya upatikanaji wa fedha vitongoji vimekuwa vikipatiwa umeme kulingana na mazingira yalivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari umeme umepelekwa katika vijiji 40 vya Jimbo la Kakonko na wakati tunapeleka umeme katika vijiji hivyo baadhi ya vitongoji vilifikiwa katika awamu ya pili ya REA na awamu ya tatu mzunguko wa kwanza. Sasa awamu ya tatu mzunguko wa pili itapeleka umeme katika vijiji lakini na baadhi ya vitongoji pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kakonko lipo katika awamu ya pili (b) ya mraji jazilizi wa umeme katika vitongoji. Jumla ya vitongoji 49 vitapatiwa umeme katika Jimbo la Kakonko na mradi huu wa jazilizi unaanza kuanzia mwezi Aprili. Kwa hiyo, kadri ya upatikanaji wa fedha, vitongoji vya Jimbo la Kakonko lakini na vitongoji vingine vingi nchini vitaendelea kupelekewa umeme taratibu ikiwa ni pamoja na taasisi za umma. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza. Uhitaji wa viwanda kwa ajili ya kuchakata muhogo katika Jimbo la Vunjo unafanana sana na uhitaji wa huduma hiyo katika Jimbo la Buyungu. Jimbo la Buyungu na Wilaya ya Kakonko kwa ujumla ni wakulima wazuri sana wa zao la Muhogo. Tatizo letu ni upatikanaji wa mashine hizo za kuchakata na kuweza kupata unga na kuboresha thamani ya zao hilo, lakini pia ni bei…

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali, je, ni lini tutapata mashine hizo za kuchakata unga wa Muhogo katika Wilaya yetu ya Buyungu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aloyce Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba kupitia shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo SIDO tayari tuna teknolojia mbalimbali na hasa za kuchakata mazao mbalimbali ikiwemo kuchakata muhogo. SIDO tayari kupitia ofisi za mikoa na hasa katika Mkoa wa Kigoma tayari tuna mashine hizo za kuchakata muhogo katika ofisi za Kibondo DC, Kakonko, Kasulu na Uvinza. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge kupitia Ofisi zetu za SIDO, Mkoa wa Kigoma aweze kuwasiliana nao ili kuona kama atapata mashine kulingana na mahitaji yake ambayo yeye anaomba katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee kama katika mashine hizo ambazo zipo katika Mkoa wa Kigoma itakuwa kwamba hazitoshelezi mahitaji yake basi nimhakikishie SIDO tupo tayari kuwasiliana nae ili tuweze kutengeneza mashine zinazokidhi mahitaji ya Mheshimiwa Mbunge na wajasiriamali katika Jimbo lake la Buyungu. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ujenzi huu ni ahadi ya muda mrefu, ni miaka sita sasa lakini kama ambavyo ameweza kutoa majibu utekelezaji wake umeanza kwa kuweka kifusi katika Mji ule wa Kakonko. Ni miezi minne sasa shughuli za biashara katika Mji ule hazifanyiki, je, Serikali iko tayari angalau kifusi kiweze kusawazishwa katika maeneo yale ili wananchi waendelee na shughuli zao wakati taratibu hizo nyingine zikifanyika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya Kakonko – Kinonko – Nyakayenze - Muhange na Kasanda - Gwanumpu - Mgunzu ni barabara ambayo iko chini ya TARURA. Barabara hii imeharibika sana pamoja na kwamba ni maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa, wananchi hawawezi kusafirisha mazao yao. Je, nini jibu la Serikali kuhusiana na suala hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anaiuliza Serikali kwamba ni kwa nini sasa tusisambaze kile kifusi ili shughuli zingine ziendelee. Kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi ni kwamba barabara ile inajengwa kwa kiwango cha lami, kwa hiyo, kile kifusi ni sehemu tu ya process za kukamilisha barabara ile. Kama tulivyojibu kwenye jibu la msingi kwamba kufikia mwezi Mei, yaani mwezi ujao ile barabara itakuwa imekamilika kwa kiwango cha lami kwa sababu TARURA wako kazini. Hapa napozungumza wanasikia, nina hakika hilo zoezi litakuwa linaendelea na kazi inafanyika.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ameainisha barabara ambazo zimeharibika sana na kuiomba Serikali iweze kuzifanyia kazi. Nimwambie tu kwamba tutatuma wataalam wetu waende wakafanye tathmini na baada ya hapo nafikiri sisi na TARURA katika ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko tutakaa pamoja kuhakikisha barabara hiyo inajengwa ili kuondoa hiyo adha ambayo wananchi wanaipata. Ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na kuwepo kwa mgogoro huo kwa muda mrefu, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kwenda eneo lenyewe la mgogoro ili aweze kujionea hali halisi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, ikidhihirika kwamba katika utaratibu huo wa kugawa mipaka kuna makosa ambayo yatakuwa yamejitokeza wakati huo: Serikali iko tayari kuchukua hatua kwa wale ambao watakuwa wamekiuka taratibu za utoaji mipaka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Kamamba ni: Je, nipo tayari kwenda katika eneo hilo ili nikajionee mwenyewe huo mgogoro? Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ndani ya kipindi hiki cha Bunge la Bajeti nikipata nafasi ambayo itaniruhusu kuweza kwenda kwa sababu ni sehemu ya wajibu wangu kuyajua, kuyaona na kusikiliza changamoto za wananchi, nimhakikishie tu kwamba naenda kupanga ratiba na nitajitahidi nimjulishe tuweko pamoja ili kwa kushirikiana na maafisa kutoka hiyo Idara ya Wakimbizi, tuone namna ambavyo tunaenda kutatua hiyo changamoto ambayo kwa sasa wananchi inawakabili. Kwa hiyo, kwa ufupi ni kwamba, nipo tayari kufuatana naye kwenda katika eneo.

Mheshimiwa Spika, swali lingine ni: Je, ikidhihirika kama kuna makosa kuna watu wamefanya mambo mengine, mengine, Serikali ipo tayari kuchukua hatua? Serikali ipo kwa ajili ya kuwatetea, kuwasemea na kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi. Tumegundua kuna baadhi ya mambo yanafanywa na baadhi ya maafisa au baadhi ya watu ambayo yanavunja utaratibu na sheria katika maeneo haya. Kama Serikali tuko tayari kuchukua hatua ili kuhakikisha kwamba wengine wawe ni funzo na wasiendelee kufanya makosa hayo.

Mheshimiwa Spika, kikubwa nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wakimbizi hawa tuliamua kuwapokea kwa sababu ya Mkataba wa Kimataifa ambao tuliukubali sisi wenyewe, kwamba ikitokea machafuko katika nchi fulani, basi kama wakija na tuki-prove kwamba kweli kuna tatizo, sisi tunawapokea.

Mheshimiwa Spika, pia tulikubaliana kwamba migogoro ikimalizika katika maeneo yao, sisi tupo tayari kuwarejesha katika maeneo yao kwa kushirikiana na mashirika na kwa kushirikiana na nchi zao.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwambie tu kwamba eneo hili ikitokea wakimbizi hawa wameondoka na ikawa hakuna machafuko, maana yake ni kwamba eneo hili tutalirejesha kwa Serikali, halafu Serikali itaona namna ya kufanya. Unless ikitokea fujo nyingine huko kwenye nchi za wenzetu ikawafanya wakimbizi waje, tutawapokea na kuwahifadhi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika majibu ambayo ameyatoa ametaja mradi wa maji katika Kijiji cha Muhange ambao unapata maji kutoka Mto Mgendezi kwenda Muhange Centre na kwenda Muhange ya Juu. Hata hivyo mradi huu sasa maji yanayotoka hayafai kwa matumizi ya binadamu kwasababu ni machafu. Lakini vilevile mradi huu haukukamilika kama ilivyokusudiwa. Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na mradi huu?

Pili, kutokana na mradi wa maji na changamoto hizi ambazo nimezitaja, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana nami ili akazione hizo changamoto na hatimaye kutoa suluhu ya miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce Kamamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nipende kusema nimesikitika kuona kwamba Mheshimiwa Mbunge anasema maji ni machafu na mradi haujakamilika vizuri kwa sababu swali lake la pili ni ombi la kuambatana na mimi nipende kukuhakikishia Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili tutakwenda pamoja na nitakwenda kujihakikishia na wakati tunaendelea kukamilisha session hii ya Bunge ninatoa maagizo kwa Meneja wa eneo lile aweze kuwajibika haya maji yaweze kufanyiwa treatment kadri ya utaalamu wetu wa Wizara ili wananchi waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika majibu ambayo ameyatoa ametaja mradi wa maji katika Kijiji cha Muhange ambao unapata maji kutoka Mto Mgendezi kwenda Muhange Centre na kwenda Muhange ya Juu. Hata hivyo mradi huu sasa maji yanayotoka hayafai kwa matumizi ya binadamu kwasababu ni machafu. Lakini vilevile mradi huu haukukamilika kama ilivyokusudiwa. Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na mradi huu?

Pili, kutokana na mradi wa maji na changamoto hizi ambazo nimezitaja, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana nami ili akazione hizo changamoto na hatimaye kutoa suluhu ya miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce Kamamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nipende kusema nimesikitika kuona kwamba Mheshimiwa Mbunge anasema maji ni machafu na mradi haujakamilika vizuri kwa sababu swali lake la pili ni ombi la kuambatana na mimi nipende kukuhakikishia Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili tutakwenda pamoja na nitakwenda kujihakikishia na wakati tunaendelea kukamilisha session hii ya Bunge ninatoa maagizo kwa Meneja wa eneo lile aweze kuwajibika haya maji yaweze kufanyiwa treatment kadri ya utaalamu wetu wa Wizara ili wananchi waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, uhitaji wa Chuo cha Ufundi VETA ambao unawakabili wananchi wa Wilaya ya Igunga unafanana sana na uhitaji wa chuo hicho katika Wilaya ya Kakonko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lini Serikali itajenga chuo cha ufundi VETA katika Wilaya ya Kakonko? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kamamba Mbunge wa Buyungu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuwa na Chuo cha VETA katika kila Wilaya hapa nchini. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko makini, kwa hivi sasa tunakamilisha ujenzi wa vyuo hivi 29 katika Wilaya hizi 29 nchini.

Baada ya awamu hii kukamilika Serikali tutajipanga vema kulingana na upatikanaji wa fedha tutahakikisha kwamba tunakwenda kujenga chuo katika kila Wilaya hapa nchini. Ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, katika majibu ya Serikali ambayo yametolewa na Mheshimiwa Waziri amesema kwamba, zimetengwa milioni 150 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati tatu.

Je, Serikali lini itapeleka hizo fedha milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha zahanati hizo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ukamilishaji wa zahanati hizo tatu utasababisha uhitaji mkubwa wa wataalam katika kada ya afya ambapo bado mpaka muda huu tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi katika kada hiyo ya afya.

Je, lini sasa Serikali itapeleka watumishi wa kutosheleza mahitaji ya watumishi wa kada ya afya katika wilaya ya Kakonko? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, fedha hizi ambazo zimetengwa kwenye mwaka huu wa fedha 2021/2022 zitaendelea kupelekwa kwenye majimbo yetu, kwenye kata zetu kadiri zinavyopatikana. Kwa hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mwaka huu wa fedha fedha hizi zitapelekwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hizi tatu katika Jimbo hili la Kakonko.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la watumishi; ujenzi wa zahanati na vituo vya afya unaenda sambamba na mipango ya ajira kwa ajili ya watumishi wetu kuhakikisha wanakwenda kutoa huduma katika vituo hivyo. Kwa hivyo, pamoja na ujenzi, lakini pia mipango ya ajira inaendelea kufanywa na vibali katika mwaka huu wa fedha vinaandaliwa kwa ajili ya kuajiri watumishi kwenda kutoa huduma za afya katika vituo hivyo. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba, suala hilo pia litakwenda sambamba na ujenzi wa vituo katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Aidha, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa madini hayo katika Wilaya yetu ya Kakonko ni uthibitisho wa utajiri na hazina kubwa ya madini katika Wilaya yetu.

Je, ni lini sasa Serikali itaanza uchimbaji mkubwa ili wananchi na Serikali iweze kufaidi kwa kiwango kikubwa zaidi? (Makofi)

Swali la pili, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwawezesha wananchi na wachimbaji wadogo wadogo mtaji ili uchimbaji uweze kufanyika kwa tija? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce John Kamamba Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa lini uchimbaji mkubwa utafanyika katika maeneo yenye madini Wilayani kwake, napenda kumjulisha kwamba Taasisi yetu ya Utafiti wa Kijiolojia na Madini (GST) wanaendelea na utafiti katika maeneo mbalimbali nchini na pale wanapobaini kiwango cha madini yanayopatikana katika eneo husika wanaendelea kutangaza fursa za uwekezaji kwa wawekezaji wakubwa wenye mitaji mikubwa, ambao kimsingi wakija wanaingia katika ubia na wachimbaji wadogo walioko katika maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili Wizara ya Madini tumeshaingia makubaliano na taasisi za kifedha za ndani ikiwepo Benki ya KCB, NMB, NBC, CRDB ya kuwapa wachimbaji wadogo mitaji waliokidhi vigezo ili waweze kuchimba madini hayo kwa tija. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu ambayo yametolewa na Serikali na mpango mzuri wa Serikali katika kupeleka watumishi katika maeneo mbalimbali hasa Wilaya ya Kakonko, bado watumishi hawa wamekuwa wakihama kutokana na upungufu wa miundombinu hasa nyumba za watumishi katika maeneo hayo.

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba watumishi hawa wa kada ya afya wanabaki katika maeneo hayo hasa kwa kujenga nyumba za watumishi hao?
(Makofi)

(b) Kutokana na changamoto hiyo: Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kufuatana nami kwenda Wilaya ya Kakonko ili hiki ambacho nakieleza kama changamoto aweze kuona na hatimaye aweze kutafuta njia sahihi za kuweza kumaliza changamoto hiyo? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza Mheshimiwa Mbunge ameainisha kwamba tunapeleka watumishi katika maeneo kama Buyungu, Halmashauri ya Kakonko, lakini asilimia kubwa ya hawa watumishi wamekuwa wakihama.

Kwa hiyo, alichokuwa anaainisha Mheshimiwa Mbunge ni kutaka Serikali moja, tujenge nyumba za watumishi ili watu wabaki; nafikiri kuongeza zile incentives kwa ajili ya watumishi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mkakati wa Serikali sasa hivi ni kuhakikisha watumishi wote wapya tunaowaajiri hawaruhusiwi kuhama katika maeneo yao, walau siyo chini ya miaka mitatu. Hiyo ni moja ya sehemu ya mikataba ambayo tumeiweka. Kwa hiyo, tutaendelea kuboresha mazingira kwa kutenga fedha ili kujenga nyumba za watumishi na kuongeza mahitaji mengine ambayo wanayahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili la kwenda Kakonko, niko tayari, hiyo nguvu ninayo na uwezo ninao na tuko tayari kwa ajili ya kuwatumikia. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Lengo la barabara hii ni kufungua mawasiliano kati ya Burundi na Tanzania. Kufuatia hili, katika kikao cha ushauri cha Bodi ya Barabara iliamuliwa barabara hii ihamishwe, kipande hiki cha Gwarama – Muhange, kitoke TARURA kwenda TANROADS . Nini kauli ya Serikali kuhusiana na suala hili?

Mheshimiwa Spika, la pili, kwa kuwa barabara hii ni muhimu, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana nami, aweze kuiona hii barabara? Nina hakika akishaiona atakuwa tayari kuchukua hatua za muhimu kujenga barabara hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Kigoma imeipendekeza kupandishwa hadhi; na kwa kuwa Serikali tunafanya kazi kwa pamoja, basi jambo hili tumelipokea na ninaamini wenzetu wa TANROADS na wenyewe wanalo. Kwa hiyo, endapo hii barabara itakuwa inakidhi vigezo vyote, basi Serikali italifanyia kazi na itekeleze kama ambavyo Bodi ya Barabara ya Mkoa imependekeza.

Mheshimiwa Spika, suala la mimi kuongozana naye, nipo tayari mara baada ya Bunge lako Tukufu tutakapomaliza. Ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi cha Tarafa ya Nyalonga kilichopo katika Kijiji cha Nyadibuye majengo yake yamechoka sana, na hivi wakati wa mvua yanavuja tena sana.

Swali; lini Serikali itafanya ukarabati wa kituo hicho cha polisi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tulishazungumza na Mbunge na moja ya ziara yangu ilikuwa nifike, lakini sikuweza kufika kwamba kuna changamoto kwenye kituo hiki na ukanda ule ni ukanda wa mvua kubwa, ni kweli changamoto tunaiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe ahadi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutawasiliana na OCD na RPC wa Mkoa wa Kigoma ili katika vipaumbele vyake vya ukarabati wa majengo chakavu ya polisi hiki kipewe kipaumbele, ili hatimaye fedha zitakapotoka kiweze kukarabatiwa, nashukuru.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kakonko au Jimbo la Buyungu lina Kata 13. Kata zenye uhakika wa mawasiliano ni tano tu. Kutokana na hali hii, ndiyo imepelekea kuleta swali hapa Bungeni.

Je, Serikali inatoa kauli gani kwa kata nane ambazo ni Nyamutukuza, Nyabibuye, Gwarama, Kasoga, Rugenge, Gwanombo, Katanga na Mgunzu ambazo bado zina matatizo ya mawasiliano ya simu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kufuatana nami Buyungu ili aweze kuliona na kubaini tatizo hili ambalo nalitaja sasa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Aloyce kwa kazi kubwa anayoifanya, na kwa kweli ameendelea kushirikiana na Wizara kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto za mawasiliano ndani ya jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Jimbo ambalo lina Kata 13, Kata tano zina uhakika lakini vile vile kuna Kata karibia tano nyingine ambazo mawasiliano yapo lakini bado kuna changamoto mbalimbali ambazo naamini baada ya kuzifanyia kazi tatizo lake litaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nitumie fursa hii, kwa sababu kwa uwepo wa TCRA kwa mujibu wa Sheria Na. 12 ya mwaka 2003, inaipa TCRA mamlaka ya kuhakikisha huduma ya mawasiliano inatolewa kwa ubora unaotakiwa. Sasa niwatake waende katika Jimbo la Buyungu wahakikishe kwamba wanaenda kufuatilia na kuangalia quality of service kama inaridhisha katika jimbo hili ili wananchi wa Buyungu waweze kupata huduma ya mawasiliano ya uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile jambo lingine, Kata ya Katanga, Kasuga pamoja na Kata ya Gorama ambapo Mheshimwa Mbunge ndipo anapotoka; Gwarama ni kweli kabisa hakuna kabisa mawasiliano, lakini hii Kata imeingizwa katika mradi wa Special Zone and Boarders ambapo utaanza kutekelezwa muda siyo mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine Kata ya Katanga, Kasuga pamoja na Kata ya Gwarama ambapo Mheshimwa Mbunge ndiyo anapotoka. Gwarama ni kweli kabisa hakuna kabisa mawasiliano lakini hii Kata imeingizwa katika mradi wa Special Zone and Boarders ambapo utaanza muda si mrefu katika kutekelezwa. Mkandarasi katika eneo hilo amepatikana (Vodacom) na kwa hiyo tunaamini ndani ya miezi miwili, mitatu, ujenzi wa minara katika maeneo haya utakuwa umeshaanza na kwa hakika vijiji ambavyo viko katika Kata ya Katanga ambavyo ni vijiji viwili, Kata ya Kasuga vijiji vinne na Gwarama vijiji vitatu, tunaamini kwamba, wananchi wa maeneo haya watanufaika na huduma ya mawasiliano. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.

Katika Wilaya ya Kakonko ambako Jimbo la Buyungu lipo zipo skimu za Katengera, Gwanumpu, Ruhwiti na Muhwazi ambazo miundombinu yake imeharibika na haifanyi kazi vizuri.

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu hiyo ili waweze kuendelea na kazi kama ilivyokusudiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aloyce kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika miradi aliyoisema Mheshimiwa Mbunge ukiacha mradi wa Ruiche hii miradi mingine miwili tutaiingiza katika mipango yetu kuhakikisha kwamba inafanya kazi katika utaratibu ambao nimeuanisha awali wa kuipitia nakuona changamoto ulizonazo.

Mheshimiwa Spika, mradi wa Ruiche tumeshapata no objection na hivi sasa tutaelekeza kazi ya usanifu ifanyike ili baadae tuanze kazi ya ujenzi.
MHE. ALYOCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Wilaya ya Kakonko, zipo Kata za Nyamtukuza, Nyabiboye, Gwarama, Kasuga, Lugenge, Gwanubu, Katanga Namguzu, zina tatizo kubwa sana la mawasiliano ya simu. Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano katika kata hizo. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kamamba, Mbunge wa Kakonko, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Kakonko, ni jimbo ambalo liko mpakani na tayari tumeshaliingiza katika utaratibu wa miradi ya mipakani. Tayari tumeshawasiliana na Mheshimiwa Mbunge na kata hizo ambazo amezitaja, zimeshaingizwa katika mpango huo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge asubiri utekelezaji kulingana na taratibu za kimanunuzi ukamilike na baada ya hapo changamoto ya mawasiliano katika Jimbo la Kakonko itakuwa imepungua kama sio kwisha kabisa.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, tatizo lililopo ni kwamba, hata wale ambao wameshapata vitambulisho hawapewi huduma inayostahili kadiri ya utaratibu uliopo. Nini kauli ya Serikali kwa hawa ambao wamepata vitambulisho, lakini hawapati huduma ambayo wanastahili?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; lini sasa hawa waliobaki 3,440 nao watapata vitambulisho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika,
naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaelekeza kuhakikisha kila halmashauri kwanza inaandikisha na kuwapa vitambulisho wazee
wote wenye umri wa miaka 60 na kuendelea, wasio na uwezo, lakini inatenga dirisha kwa ajili ya huduma kwa wazee na kuhakikisha kwamba, dawa zote muhimu zinapatikana kwa ajili ya wazee. Kwa hiyo, naomba nitoe Kauli ya Serikali kwamba, wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wahakikishe maelekezo ya Serikali yanatekelezwa na wazee wetu wapate huduma kama inavyostahiki.

Mheshimiwa Spika, lakini pili, kuhusu vitambulisho kwa wazee waliobaki, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi kwamba, mwaka ujao wa fedha Halmashauri watatenga fedha kwa ajili ya kuwapa vitambulisho wazee waliobaki 3440.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kakonko inayo shule moja tu ya kidato cha tano na sita, ambayo ni Shule ya Sekondari Kakonko, lakini tunazo Shule za Sekondari Nyamtukuza, Mhange, Shuhudia, Kasanda na Gwanum ambazo zina sifa, kwa maana ya kwamba zina madarasa lakini hatuna hosteli.

Je, ni lini Serikali itatuletea fedha kwa ajili ya kujenga hosteli ili wanafunzi waanze kupokelewa kidato cha tano na cha sita? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Aloyce Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Kakonko kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba mahitaji ya shule za sekondari kidato cha tano na sita yanapewa kipaumbele kwenye takriban majimbo mengi kwa sasa; na ndio maana katika jitihada zake Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutafuta fedha mliona, kwamba kwa kushirikiana na kampuni ya madini African Barrick walipewa dola milioni, takriban bilioni 70, ambazo ni kwa ajili ya ku-support elimu nchini. Fedha hizo zimeelekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya kidato cha tano na sita. Kwa hiyo lengo la Serikali ni kuhakikisha hii adha inaondolewa. Kwa hiyo Mheshimiwa Kamamba nikuondoe hofu kwa sababu iko katika mipango ya Serikali.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naitwa Aloyce John Kamamba.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tunaishukuru Serikali kwamba imekamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kakonko, lakini tuna upungufu mkubwa wa watumishi na vifaa tiba. Lini Serikali itapeleka watumishi na vifaa tiba katika hospitali yetu ya Wilaya ya Kakonko? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, Serikali inaajiri watumishi wa afya 8,070, na katika hawa ambao wataajiriwa, Hospitali ya Wilaya ya Kakonko nayo itapata watumishi hawa.

Mheshimiwa Spuika, kwenye vifaa tiba, vilevile Serikali imetenga zaidi ya Shlingi bilioni 34 ambazo zimeshakwenda kwa wenzetu wa MSD kwa ajili ya kupeleka vifaa tiba kwenye hospitali za Wilaya mbalimbali hapa nchini na tutaangalia kama Hospitali ya Wilaya ya Kakonko nayo ipo, kama haipo tutaiweka katika mwaka wa fedha unaofuata.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itafunga taa za barabarani katika Mji wa Kakonko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara za Kakonko anazozizungumzia Mheshimiwa Mbunge pale ni kama lilivyokuwa swali la kwanza la Tunduru Mjini ni barabara ya TANROADS na tayari ni mkakati wa TANROADS kuhakikisha kwamba wanafunga barabara katika barabara zote zinazopita makao makuu ya wilaya, na hivi karibuni zoezi hilo litaanza.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Kakonko na halmashauri yake ni mpya na hivi watumishi hawana nyumba za kuishi je lini Serikali sasa itajenga nyumba kwa ajili ya watumishi waliyoko katika Wilaya ya Kakonko? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kakonko na maeneo yote ambayo ni halmashauri mpya niwaombe kama nilivyosema kwenye swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Ushetu kwamba tutenge maeneo. Kwa sababu wakati mwingine mkienda kwenye maeneo hayo unakuta hakuna hata maeneo yaliyotengwa na halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za taasisi kama National Housing na Watumishi Housing.

Mheshimiwa Spika, hata hizi nyumba zilizopo bahati mbaya sana inatokea watumishi wengi hawaendi kukaa kwenye hizi nyumba na badala yake mashirika haya yamekuwa sasa yakipangishwa watu wa kawaida na hiyo ni mifano ipo hata hapa Dodoma tunazo nyumba nyingi pale Iyumbu lakini watumishi hawaendi pale kwa ajili ya kuzitumia. Ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kabla sijauliza maswali naomba niweke kumbukumbu sawa ni Shule ya Sekondari Gwanumpu na Shule ya Sekondari Shuhudia. Baada ya masahihisho hayo ninashukuru kwa majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kakonko inayo shule moja tu ya sekondari ambayo ni Shule ya Sekondari Kakonko, na katika majibu ya Serikali amebainisha kwamba Shule ya Sekondari Muhange inapungukiwa mabweni mawili tu.

Je, lini sasa Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kujenga hayo mabweni mawili ili masomo yaweze kuanza pale?

Swali la pili, amebainisha shule hizi za Sekondari Shuhudia, Kasanda, Nyamtukuza na Gwanumpu zinapungukiwa miundombinu mbalimbali, lakini kinachohitajika hapo ni fedha. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba miundombinu hii inayopungua inakamilika na masomo yaweze kuanza katika shule hizi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Spika, nikijibu swali lake la kwanza la lini fedha itakwenda kukamilisha mabweni haya ambayo tayari yameshaanza kujengwa. Serikali itapeleka fedha kadiri ya upatikanaji wake na tutaangalia katika bajeti hii iliyopitishwa ya mwaka wa fedha 2023/24 kuona kama hiyo shule imetengwa fedha, kama haijatengewa tutajitahidi tuitengee fedha 2024/2025.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili kuhusu Shule za Gwanumpu, Shuhudia na Nyamtukuza ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja, tutaangalia vilevile kuona uwezekano wa kuzitengea fedha katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Buyungu, wapo wafugaji wa samaki ambao wapo katika vikundi, lakini wapo wengine ambao ni mmoja mmoja, lakini wanapungukiwa maarifa na mtaji kwa ajili ya kuwawezesha kufuga kwa tija. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba tunawawezesha hawa wafugaji waweze kufuga kwa tija? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge. Mkakati wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni pamoja na kuwezesha vikundi mbalimbali vya wavuvi na wavuvi binafsi. Ndiyo maana ukiangalia katika mwaka huu wa fedha tumetoa fedha nyingi na tunaenda kutoa mikopo ya maboti. Kwa hiyo, waliwemo wavuvi wa Jimbo la Mheshimiwa Mbunge, Buyungu kule na wenyewe tutawafikia. Kwa hiyo, tuwaondoe shaka kwenye hilo.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Serikali ambayo hayajakidhi swali langu, kwa sababu Skimu za Katengera, Ruhwiti na Muhwazi ambazo nimezitaja, siyo skimu mpya, ni skimu ambazo zimekuwepo na zimekuwa zikifanya kazi. Tatizo miundombinu yake imeharibika na hivyo hazifanyi kazi sasa.

Mheshimiwa Spika, swali; Je, lini mtapeleka fedha kwenye skimu hizi kwa ajili ya ukarabati ili ziweze kufanya kazi inayostahili?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; wananchi wetu wakulima hawana taaluma juu ya utumiaji wa miundombinu ya umwagiliaji kwa maana ya kwamba hawana taaluma;

Je, ni nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba wanakuwa na maarifa na taaluma ya kutosheleza kutumia miundombinu ya umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika majibu yangu ya msingi nimeeleza vyema kabisa tunayo mabonde 22 ya kimkakati. Katika Mkoa wa Kigoma tunafanyia kazi Bonde la Mto Malagarasi na Bonde la Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Spika, katika maziwa na mito hii miwili ambayo nimeisema ndani yake skimu hizi zinapatikana. Kwa hiyo Serikali imeamua ifanye kazi kubwa kwanza ya upembuzi yakinifu kwenye mabonde haya ambayo pia ndani yake itajumuisha skimu ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitamka. Kwa hiyo nimwondoe hofu kwamba skimu ambazo amezitamka ni ndani ya mkakati wa Serikali katika utekelezaji wa haya mabonde ambapo kazi imekwisha kuanza na ujenzi utaanza mwaka wa fedha ujao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu elimu; tumeajiri wahandisi wa umwagiliaji wa kila wilaya. Hawa watakuwa na jukumu pia la kuhakikisha kwamba wanawapa elimu wakulima wetu juu ya matumizi sahihi ya maji katika kilimocha umwagiliaji. Hivyo wananchi pia wa Jimbo la Buyungu watanufaika na huduma hii kupitia wahandisi wetu walioko wilayani.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lipo tatizo la umeme kukatika-katika hali inayosababisha vifaa vya umeme vinavyotumiwa na wananchi kuharibika.

Nini mkakati wa jumla wa Serikali kuhakikisha kwamba tatizo hili linaisha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuja Wilayani Kakonko kwa ajili ya kueleza mazuri sana haya ya Serikali ambayo Serikali inaendelea kuyafanya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce Kamamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunakiri kwamba bado kuna maeneo yanayo tatizo la kukatika umeme na maeneo mengine kukatika ni kwingi, maeneo mengine ni kudogo, maeneo mengine tumepunguza kwa sehemu kubwa. Eneo analolisema linayo line ya siku nyingi ya kilometa zaidi ya 280 inayohudumia maeneo ya Kakonko, Buhigwe, Kasulu na Kibondo ambayo sasa imeunganishwa na line ya Gridi ya Taifa inayotokea Nyakanazi kwenda mpaka maeneo hayo yenye kilometa takribani 25.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti hii ambayo tunamaliza tumefunga kifaa kinachoitwa Auto Voltage Regulator ambacho kinaongeza nguvu ya umeme unaosafiri kwa muda mrefu ili angalau umeme uweze kufika mwingi kwa wadau mbalimbali. Katika bajeti inayokuja tumetenga pesa kwa ajili ya kwenda kuirekebisha na kuifanyia marekebisho makubwa hii line ikiwa ni pamoja na kubadilisha miti iliyochakaa, kubadilisha vikombe, lakini pia kubadilisha maeneo kidogo ya waya ambayo yamekuwa yakisababisha umeme kukatika kwenye maeneo haya.

Kwa hiyo, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika kipindi kinachokuja cha mwaka wa fedha unaokuja katika kipindi kifupi ataona mabadiliko ya kurekebisha hii line ili iache kuwa inaathirika sana na matatizo ambayo yamekuwa yakitokea.

Mheshimiwa Spika, lakini katika eneo la pili, mimi niko tayari kwenda pamoja na yeye kuwaambia wananchi mipango mizuri kabisa ya Serikali, lakini pia na kusisistiza wao kushirikiana na Serikali katika kulinda miundombinu ambayo inapeleka umeme katika maeneo hayo, nakushukuru.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inayowakabili wananchi wa Uvinza, inakwenda sambamba na Wilaya ya Kakonko. Mkuu wa Polisi wa Wilaya hana ofisi, anatumia iliyokuwa Ofisi ya Polisi ya Kata. Kwa hiyo, Waziri anaweza akaona hali halisi:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha kwamba Wilaya ya Kakonko nayo inapata Kituo cha Polisi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye majibu ya msingi, wilaya zote mpya hazijawa na vituo vya Polisi vya ma-OCD. Ndiyo maana tumekuja na mkakati wa kujenga vituo hivyo kwenye maeneo ambayo hayana. Katika bajeti iliyopita tutaanza ujenzi wa vituo hivyo, lakini kipaumbele kitawekwa kwenye maeneo yaliyoko mpakani ikiwemo hii Wilaya ya Kakondo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, bado kwa takwimu Mkoa wa Kigoma una zaidi ya wananchi 2,000,000 lakini waliotambuliwa ni 975,844 na waliopata vitambulisho ni 123,962 sawa na asilimia 12 tu. Jibu lake anasema kwamba mwaka huu watapewa vitambulisho; sasa swali nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wote wanaostahili ambao wako katika Mkoa wa Kigoma wanapata vitambulisho vya NIDA?

Mheshimiwa Spika, la pili; wananchi wa Wilaya ya Kakonko muda mwingine wanaombwa vitambulisho ambavyo ni vya NIDA ambavyo hakika Serikali inajua kwamba haijavitoa kwa wananchi hao, mpango ukoje kuhakikisha kwamba wananchi wa Wilaya ya Kokonko sasa wanapata vitambulisho vya NIDA? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kamamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwa takwimu hizo idadi ya waliopata vitambulisho ni ndogo sana, lakini kama ilivyoelezwa wakati nawasilisha bajeti hapa kulikuwa na changamoto ya kimkataba kati ya Serikali na mzabuni, na hivyo karatasi za kutolea vitambulisho hivi hazikuwepo, lakini tatizo hilo limeondolewa, tumeshahuisha mkataba na ndio maana tunauhakika kwamba kwa mwaka ujao wa fedha tutatatua tatizo hilo kwa wale wote waliotambuliwa na kusajiliwa na wale wapya tutakaokuwa tunaweza kutawambua na kuwasajili, nashukuru kwa swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kuhusu kugawa vitambulisho kama nilivyosema kwenye jibu la msingi linahusiana moja kwa moja kwa mwaka ujao tunauhakika wananchi wale ambao wameshatambuliwa watapewa vitambulisho na wale wapya watakaokuwa wanaendelea kutambuliwa watapewa vitambulisho, nashukuru.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri, niliomba kujengewa chuo na sasa ujenzi umeanza, naishukuru sana Serikali. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza:

Mheshimiwa Naibu Spika, majengo ambayo yameanza kujengwa katika chuo kile ni majengo Tisa kati ya majengo mengi ambayo yatajengwa katika eneo hilo; Je, ni lini majengo hayo ambayo yapo katika mpango huo yataaanza kujengwa?

Swali la pili; ni lini ujenzi sasa utakamilika ili wananchi wa Wilaya ya Kakonko ambao wanasubiri chuo hiki kwa hamu sana utakamilika na mafunzo yaweze kuanza? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kamamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ujenzi wa vyuo hivi unagharimu zaidi ya shilingi bilioni tatu, kwa awamu ya kwanza tumetenga zaidi ya bilioni 1.5 kwa ajili ya majengo ya awamu ya kwanza ambayo ni majengo tisa na ujenzi huo umeanza mwezi wa Nane mwaka huu na ni ujenzi ambao tunatarajia utachukua kati ya miezi nane mpaka 12. Kwa hiyo, ni matarajio yetu ifikapo mwezi wa Sita au wa Saba mwakani majengo haya Tisa ya awamu ya kwanza yatakuwa yamekamilika na yatakapokamilika kwa sababu tumejenga kimkakati, tutahakikisha kwamba majengo haya yatakapokamilika chuo kiweze kuanza kutoa huduma hapohapo wakati tunaendelea na ujenzi wa awamu ya pili. kwa hiyo ujenzi wa awamu ya kwanza unatarajiwa kunako mwezi wa Sita, ama mwezi wa Saba mwakani utakuwa umekamilika then tutaanza ujenzi wa awamu ya pili kwa kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu. Nakushukuru
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, moja, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Katika majibu ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ametoa, ameunganisha skimu mpya zinazotarajiwa kuanzishwa na skimu ambazo zipo sasa.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu kubwa ni kwamba, Skimu ya Murwazi, Ruhwiti na Katengera zipo. Tatizo ni miundombinu yake imeharibika na hivyo hazifanyi kazi inavyostahili. Swali langu, ni lini Serikali itapeleka fedha hizo kwa haraka ili kuhakikisha skimu hizo zinakarabatiwa na ujenzi unafanyika ili wananchi waweze kufaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa baada kikao hiki twende pamoja ili kuhakikisha kwamba anaiona skimu hizi ili kutoa suluhisho haraka sana? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, moja ya maelekezo ambayo tumeyapata kutoka kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha kwanza tunakarabati skimu zote ambazo zilikuwepo na zimeharibika. Pili, tujenge maeneo mapya na kutambua maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Hayo ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, sasa katika maelekezo yake, sasa hivi tunapotaka kufanya maboresho ya hizi skimu zilizoharibika, ni lazima tufanye upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili tupate gharama halisi, tofauti na ule utaratibu uliokuwa unatumika zamani, mtu akiona tu dharura anapeleka shilingi milioni 500, lakini hajui kuna gharama kiasi gani zinahitajika. Ndiyo maana kulikuwa na mwendelezo wa matatizo mengi katika skimu zetu nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo kwa sasa hivi lipo katika utekelezaji na tukimaliza tu tutatenga fedha kwa ajili ya kuzikarabati na kuzijenga. Kuhusu kwenda, niko tayari mara tu baada ya Bunge lako Tukufu kumalizika.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wa Muhange katika Wilaya ya Kankonko unaunganisha nchi ya Tanzania na Burundi na uwepo wa forodha katika mpaka huo utapelekea Serikali kuweza kuongeza kipato, lakini bahati mbaya eneo hilo mpaka sasa halijajengewa Kituo cha Forodha. Ni lini Kituo cha Forodha kitajengwa katika mpaka wetu wa Muhange? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia sana eneo hilo na Mbunge amefuatilia si tu Kituo cha Forodha bali amekuwa akifuatilia pia barabara inayoelekea eneo hilo. Tulikaa na Waziri wa sekta tumepokea jambo hilo kwa sababu ni barabara na kituo ambacho kinaelekea kwenye makao makuu mapya ya nchi ya Burundi na mimi napanga kufika katika eneo hilo ili kuweza kujionea.

Kwa hiyo, tumepokea tutalifanyia kazi na Mheshimiwa Mbunge tutakupa mrejesho ili uweze kuwaarifu na wananchi wako. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, lini Serikali itapeleka umeme katika Vitongoji vya Nyamwilonge, Lutenga, Kavungwe katika Kata ya Nyantukuza, Bwela Kata ya Muhange, Nyakavilu Kata ya Gwarama katika Wilaya ya Kakonko? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aloyce Kamamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, vitongoji ambavyo havina umeme vipo katika awamu mbalimbali za kupelekewa umeme kulingana na upatikaji wa fedha, lakini tunao Mradi wa REA III Round II ambao unaendelea kupeleka umeme katika vijiji vyetu inawezekana kabisa kuna baadhi ya vitongoji ambavyo vitaguswa na mradi huo. Kwa vile ambavyo havitapata, kama tulivyosema tunatafuta fedha nyingi zaidi kwa ajili ya kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote kwa wakati mmoja tulivyosema kwenye bajeti iliyopita Sh.6,500,000,000,000 kwa ajili ya kufanikisha mradi huu wote. Serikali ya Awamu ya Sita inayo azma ya kufanya kazi hii na tunaamini tutafanikiwa.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wa Muhange katika Wilaya ya Kankonko unaunganisha nchi ya Tanzania na Burundi na uwepo wa forodha katika mpaka huo utapelekea Serikali kuweza kuongeza kipato, lakini bahati mbaya eneo hilo mpaka sasa halijajengewa Kituo cha Forodha. Ni lini Kituo cha Forodha kitajengwa katika mpaka wetu wa Muhange? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia sana eneo hilo na Mbunge amefuatilia si tu Kituo cha Forodha bali amekuwa akifuatilia pia barabara inayoelekea eneo hilo. Tulikaa na Waziri wa sekta tumepokea jambo hilo kwa sababu ni barabara na kituo ambacho kinaelekea kwenye makao makuu mapya ya nchi ya Burundi na mimi napanga kufika katika eneo hilo ili kuweza kujionea.

Kwa hiyo, tumepokea tutalifanyia kazi na Mheshimiwa Mbunge tutakupa mrejesho ili uweze kuwaarifu na wananchi wako. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, tatizo lililopo kwa wananchi wa Wilaya ya Kakonko ambao ni wakulima wazuri wa Zao la Muhogo ni bei ya zao hilo. Hata wakulima wakipata mnunuzi bei inakuwa chini.

Je, Serikali ipo tayari sasa kuanzisha Chama cha Wasindikaji wa Zao la Muhogo Wilayani Kakonko ikiwa ni pamoja na kuwapa mikopo ili waweze kuboresha zao hilo? (Makofi)

Swali la pili, zao la Muhogo ni zao la chakula na baishara kwa Mkoa wa mzima kwa maana ya Wilaya zake zote.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri anayezungumza yupo nyuma yako. Mheshimiwa Naibu Waziri, urejee kwenye kiti ulichokuwa. Ahsante sana.

Mheshimiwa Aloyce Kamamba malizia swali lako la pili.

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante, swali la pili lilikuwa kwamba zao la Muhogo kwa Mkoa wetu wa Kigoma linalimwa katika Wilaya zake zote. Sasa, ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba, zao hilo linafanyiwa utafiti ili kupata mbegu bora ambayo inatoa mazao mazuri zaidi? Ahsante sana (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Serikali inatambua kuna changamoto ya bei ya zao la muhogo ndiyo maana katika moja ya jitihada kubwa tulizofanya ni kuanzisha Chama cha Wazalishaji na Wasindikaji wa Zao la Muhogo Tanzania (TACAPPA). Kwa hiyo, kwa sasa hivi wanatakiwa washuke katika Wilaya na kwa sababu Mbunge ameomba hilo tutalifanya hivyo kwa kuhakikisha tutakuwa na tawi katika Halmashauri ya Kakonko ili iweze kuwasaidia kupata bei ya uhakikka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuhusu tafiti nimthibitishie kwa asilimia 100 TARI wameshafanya tafiti ya zao la Muhogo na sasa hivi wana mbegu ambayo inaweza kuzalisha mpaka tani 50 kwa heka moja. Kwa hiyo, tutakachokifanya sasa hivi ni kuhakikisha TARI inapeleka mbegu katika maeneo ya Kigoma ili iweze kuleta tija zaidi kwa wananchi hawa, ahsante. (Makofi)