Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Juliana Didas Masaburi (5 total)

MHE. JULIANA D. MASABURI Aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Kiwanda cha MUTEX kilichopo Wilaya ya Musoma Mjini kinafunguliwa na kurudisha ajira kwa vijana wa Mkoa wa Mara?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Didas Masaburi, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina jumla ya viwanda 12 vya nguo na mavazi na viwanda vitatu kati ya viwanda hivyo havifanyi kazi ikiwemo Kiwanda cha Musoma Textiles.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha MUTEX ni moja kati ya viwanda vilivyobinafsishwa na Serikali kwa wawekezaji kwa lengo la kuviendeleleza ili viweze kukuza sekta ndogo ya nguo na mavazi, kutoa ajira kwa wananchi, kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuleta ustawi kwa jamii. Kiwanda hiki kimekuwa kinafanya kazi kwa kusuasua na mara kadhaa kimesimamisha uzalishaji. Kiwanda cha MUTEX ni moja kati ya viwanda 20 ambavyo vimerejeshwa Serikalini baada ya wawekezaji wa awali kushindwa kuviendeleza na kukiuka masharti ya mkataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, dhamira ya dhati ya Serikali ni kuona viwanda hivyo vinafanya kazi kwa tija na ufanisi mkubwa ili kuongeza ajira kwa ajili ya maendeleo ya watu, kuchochea shughuli za kiuchumi, na kuongeza mapato ya ndani ya nchi. Serikali imeshatoa Tamko la kuvitafutia wawekezaji wapya wa kuviendeleza kwa tija viwanda vyote vilivyorejeshwa Serikalini ili vilete manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla. Ni matumaini ya Serikali, kuona kuwa wawekezaji makini watajitokeza kwa lengo la kutumia fursa hii adhimu kuwekeza katika viwanda hivi. Serikali inaandaa utaratibu maalum utakaowezesha kupatikana wawekezaji wapya kwa njia ya zabuni ya kiushindani na wazi kwa kuzingatia vigezo vitakavyowekwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha wawekezaji wenye nia na uwezo wa kuwekeza katika Kiwanda cha MUTEX na viwanda vingine vilivyorejeshwa Serikalini kuwasilisha maombi yao mara baada ya utaratibu utakapotangazwa rasmi. Nashukuru.
MHE. JULIANA D. MASABURI aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje katika kudhibiti uchafuzi unaofanyika pembezoni mwa Ziwa Victoria ambao unapunguza samaki kuzaliana?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Didas Masaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, uchafuzi wa mazingira unaofanyika pembeni mwa Ziwa Victoria unatokana na shughuli za kibinadamu zisizozingatia hifadhi ya mazingira. Shughuli hizo ni pamoja na utiririshaji wa majitaka kutoka katika maeneo ya makazi, utupaji taka ngumu kutoka majumbani na viwandani, kilimo kisicho endelevu kinachosababisha uchafuzi wa maji kutokana na kuongezeka kwa tabaki, matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu na mbolea za viwandani na uchimbaji wa madini usio endelevu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa Kanuni, miongozo na mikakati ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya maziwa. Aidha, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa tathmini ya athari za kimazingira (TAM) inafanyika kwa miradi ya maendeleo iliyopo inayotarajiwa kufanyika pembezoni mwa Ziwa Victoria ili kuhakikisha udhibiti wa vyanzo vya uchafuzi wa maji ya Ziwa Victoria inayotokana na shughuli za kibinadamu zisizohusisha miradi hiyo unazingatiwa.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa tathmini ya athari za kimazingira (TAM) inafanyika kwa miradi ya maendeleo iliyopo, inayotarajiwa kufanyika pembezoni mwa Ziwa Victoria ili kuhakikisha udhibiti wa vyanzo vya uchafuzi wa maji ya Ziwa Victoria inayotokana na shughuli za kibinadamu zisizohusisha miradi hiyo, inazingatiwa.

Mheshimiwa Spika, vile vile Serikali imepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastic kwa ajili ya kubebea bidhaa ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ikichangia uchafuzi pembeni mwa Ziwa Victoria.
MHE. JULIANA D. MASABURI aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kufanya ukaguzi wa kudhibiti uingizaji na utengenezaji wa vipodozi fake nchini?
NAIBU WAZIRI UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Didas Masaburi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Shirika la Viwango Tanzania yaani TBS imeendelea kudhibiti uingizaji na utengenezaji wa vipodozi visivyokidhi viwango vya ubora kwa mujibu wa Sheria ya Viwango Na. 2 ya Mwaka 2009 na Sheria ya Fedha Na. 8 ya Mwaka 2019. Pia Serikali imeendelea kudhibiti bidhaa fake kupitia Tume ya Ushindani (FCC) kwa mujibu wa Sheria ya Ushindani Na. 8 ya Mwaka 2003.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA K.n.y. MHE. JULIANA D. MASABURI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapa Vichanja vya kuanikia dagaa Wanawake Wajasiriamali wa Mkoa wa Mara?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Didas Masaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kukuza na kuendeleza zao la dagaa na kuliongeza thamani ili liwe moja ya zao kuu la kimkakati litakalochangia katika kuongeza fursa za ajira, usalama wa chakula na lishe na kukuza uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutimiza azma hiyo, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Wizara inatekeleza programu maalum kwa kutumia fedha za mkopo uliotolewa kupitia dirisha la Extended Credit Facility kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa; ambapo shilingi bilioni 1.25 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya ubaridi na mitambo ya kuzalisha barafu kwenye masoko saba ya mazao ya uvuvi na ujenzi wa vichanja vya kukaushia dagaa katika mialo mitatu ya kupokelea samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaangalia uwezekano wa kuwajengea vichanja vya kuanikia dagaa wanawake wajasiriamali wa Mkoa wa Mara katika awamu ya pili ya utekelezaji wa programu hiyo.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO K.n.y MHE. JULIANA D. MASABURI aliuliza:-

Je, Serikali haioni haja ya kusimamia sheria kikamilifu na kukomesha utaratibu wa wapangishaji nyumba kutoza pango kwa fedha za kigeni?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hakuna sheria mahsusi inayoelekeza aina ya fedha inayotakiwa kutumika katika kutoza pango kwa wapangishaji wa nyumba. Hata hivyo, Benki Kuu imekuwa ikitoa miongozo kuhusu matumizi ya fedha za kigeni nchini ambayo pamoja na mambo mengine inakataza matumizi ya fedha za kigeni kwa wakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kulipia bidhaa na huduma nchini. Mwongozo unaotumika sasa ulitolewa mwezi Desemba, 2017.

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha utendaji wa soko la nyumba nchini, Wizara ipo katika mchakato wa kutunga Sheria ya Milki ambayo pamoja na masuala mengine itaweka utaratibu wa utozaji wa pango hususan kwa raia wa Tanzania. Ahsante.