Primary Questions from Hon. Ndaisaba George Ruhoro (19 total)
MHE. NDAISABA G. RUHORO Aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza mazingira wezeshi ya kuongeza bei ya zao la kahawa ili wakulima wa zao hili waweze kunufaika kama ambavyo wakulima wa nchi jirani ya Uganda wanavyonufaika?
(b) Utaratibu wa ununuzi wa zao la kahawa unapitia Vyama vya Ushirika, hali inayoonekana kutovutia ushindani. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi ili kuvutia ushindani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ndaisaba, kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua tunazochukua kwa ajili ya kuongeza bei bora ya kahawa kwa wakulima wa Mkoa wa Kagera na Tanzania nzima; moja tumeanza utaratibu wa kuwapatia vifaa kwa ajili ya kuweza kuchakata kahawa yao na badala ya kuuza kahawa ghafi wauze kahawa ambayo imeshaanza kuchakatwa. Aidha, Serikali inafufua na kujenga upya na kuimarisha ushirika wa wakulima kupitia umoja wao waweze kuamua na kupata bei nzuri ya kahawa. Pia, Serikali imeanza kuruhusu mifumo ya direct export ambapo Vyama vya Ushirika na wakulima moja kwa moja wamekuwa wakiuza moja kwa moja kwa wateja. Hatua nyingine ambayo Wizara inachukua sasa hivi tumeanza mchakato wa kutafuta identification logo ambapo kahawa ya Tanzania kokote kule itakaponywewa duniani iweze kutambulika kwamba ni Tanzania produce.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ununuzi wa kahawa hatua ambazo tunachukua kama Wizara ni kwamba Serikali sasa hivi tumeruhusu ushindani wa moja kwa moja wa makampuni binafsi, lakini vile vile yakishindana na Vyama vya Ushirika. Aidha, katika kuhakikisha kama nchi kufikia malengo ambayo tumejiwekea ya mwaka 2025 yaliyoainishwa katika Ilani kufikia tani 300,000 Serikali inatekeleza mkakati wa kuongeza uzalishaji wa miche bora ya kahawa ambapo jumla ya miche bora milioni 55 inazalishwa na kusambazwa kwa wakulima. Aidha, mkakati uliopo ni kuzalisha miche bora milioni 20 ambayo itakuwa ni specific kwa ajili ya organic coffee.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Wananchi wa Jimbo la Ngara wananufaika na uchimbaji wa Madini ya Nickel unaotarajia kuanza katika eneo la Kabanga?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Jimbo la Ngara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mbunge Mheshimiwa Ndaisaba kwa jinsi ambavyo anafanya ufuatiliaji kuhakikisha kwamba, wananchi wake wa Jimbo la Ngara wananufaika na mradi tarajiwa wa uchimbaji. Serikali imefanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Madini kupitia Marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 na kutungwa kwa sheria mpya za usimamizi wa rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Madini, Sura 123, imeweka bayana kuwa, makampuni yote ya uchimbaji madini ni lazima yawasilishe mpango wa ushirikishwaji wa Watanzania katika miradi ya uchimbaji kwa maana ya local content plan ambao ni lazima ubainishe manufaa yatakayopatikana kwa wananchi kutokana na uanzishwaji wa miradi ya madini. Hivyo, kwa kuzingatia matakwa hayo ya Sheria, Serikali itahakikisha kwamba inachambua kikamilifu mpango utakaowasilishwa na Kampuni ya Tembo Minerals Corporation Limited inayotarajia kuwekeza katika mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya nickel katika Jimbo la Ngara na kuusimamia kwa kushirikiana na Mamlaka zingine za Serikali kuhakikisha kuwa unatekelezwa na unaleta manufaa kwa wananchi wa Ngara na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, mbali na suala hili la local content, wananchi wa maeneo yanayozunguka mradi watanufaika kama ambavyo makampuni mengine yote yanafanya kupitia malipo ya ushuru wa Huduma kwa maana ya Service Levy lakini pia na miradi itakayotekelezwa kupitia mpango wa Corporate Social Responsibility kwa maana ya CSR.
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume ya Madini itaandaa mpango mahsusi wa uendeshaji wa semina elekezi kwa wananchi wa Halmashauri ya Ngara na halmashauri yenyewe na maeneo jirani ili kuwawezesha kubaini fursa zilizopo ikiwa ni pamoja na bidhaa na huduma mbalimbali ambazo wataweza kuzitoa katika mradi huo ili waweze kujiongezea kipato. Ahsante.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka Kivuko katika Mto Ruvuvu ili kuunganisha Vijiji vya Mayenzi na Kanyinya vilivyopo Wilayani Ngara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kuendelea kuboresha huduma za usafiri kwa njia ya maji ikiwa ni pamoja na kuunganisha maeneo yenye mahitaji ya vivuko ikiwemo Mayenzi na Kanyinya kila inapopata fedha. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Sekta ya Ujenzi, ilitenga fedha kwa ajili ya kujenga maegesho ya Mayenzi na Kanyinya, ili iweze kupeleka kivuko ambacho kitaunganisha wananchi wa maeneo hayo. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maegesho hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) uko kwenye hatua za ununuzi wa kumpata mkandarasi wa kufanya ujenzi wa maegesho ya kivuko hicho na mkandarasi wa kufanya ukarabati huo chenye uwezo wa kubeba abiria 60 na magari mawili ambacho hapo awali kilikuwa kinafanya kazi eneo la Rusumo
– Nyakiziba, yaani MV Ruvuvu ya zamani, ambacho kwa sasa kimeegeshwa katika Mto Ruvuvu. Baada ya ukarabati huo kukamilika, kitatoa huduma kwenye eneo la kati ya Mayenzi hadi Kanyinya. Ahsante.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo la maji safi katika maeneo ya Ngara Mjini pamoja na maeneo ya jirani ya Murukulazo, Nyamiaga, Muruguanza na Buhororo yanayohudumiwa na Mamlaka ya Maji Safi Ngara?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Jimbo la Ngara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Mji wa Ngara ni wastani wa asimilia 63. Uzalishaji wa maji ni mita za ujazo 1,500 kwa siku ambapo mahitaji ni mita za ujazo 2,500.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Ngara, kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali itachimba kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha maji lita 80,000 kwa saa, kukarabati mtandao wa bomba umbali wa kilomita 1.73 na kuongeza mtandao wa mabomba ya kusambaza maji umbali wa kilomita 1.5. Kazi hizo zitaanza kutekelezwa mwezi Desemba, 2021 na kukamilika mwezi Aprili, 2022. Kukamilika kwa kazi hizo kutaboresha huduma ya maji katika Mji wa Ngara kufikia asilimia 78.9.
Mheshimiwa Spika, mpango wa muda mrefu ni kujenga mradi mkubwa wa maji utakaotumia chanzo cha Mto Ruvuvu. Mradi huo utanufaisha Mji wa Ngara na maeneo/Vijiji vya jirani vya Nterungwe, Nyakiziba, Kumutana, Mayenzi, Mukirehe, Murukulazo, Nyamiaga, Muruguanza na Buhororo. Kazi ya usanifu imepangwa kukamilika katika robo ya pili ya Mwaka wa Fedha 2021/2022. Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa mradi anatarajiwa kupatikana kabla ya mwezi Julai, 2022.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA K.n.y. MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -
Je, ni lini mifuko ya kuwezesha wananchi kiuchumi itaunganishwa ili kuleta tija na manufaa kwa Watanzania hasa waishio vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Jimbo la Ngara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inaratibu utekelezaji wa mifuko na programu 62 za uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha tathmini ya mifuko na programu za uwezeshaji ishirini. Napenda kutumia fursa hii kukujulisha kuwa, Serikali inafanyia uchambuzi wa kina taarifa ya tathmini hiyo na kuja na hatua za kuchukua ili kuboresha utoaji wa huduma wa mifuko husika. Nakushukuru sana.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Vituo vya Polisi vya Nyamagana, Keza na Djululigwa vilivyojengwa na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini jitihada na michango ya wananchi katika kujenga vituo vya Polisi nchini. Vituo vidogo vya Polisi vya Nyamagana, Keza na Djululigwa ambavyo viko Wilaya ya Ngara, ni vituo vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi. Tathmini imefanyika na kubaini kuwa kiasi cha shilingi 125,000,000 kitahitajika ili kugharamia uwekaji wa mfumo wa umeme na maji, kupiga plasta, kuweka sakafu, dari, milango, madirisha, samani na kupaka rangi. Serikali kupitia Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau inatafuta fedha ili kuweza kumalizia kazi ya ujenzi huo.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Ngara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Jimbo la Ngara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ni miongoni mwa Halmashauri 25 zilizoanza kutekeleza ujezi wa Hospitali kwa awamu ya tatu katika mwaka wa fedha 2021/2022, ambapo ilipokea fedha shilingi milioni 500 na kuanza ujenzi wa Jengo la Wagonjwa wa nje (OPD) na Jengo la Maabara.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Ngara katika mwaka wa fedha 2022/2023 imetengewa fedha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali. Halmashauri hiyo ilipokea fedha hizo mwezi Novemba 2022 kwa maelekezo ya kutumia fedha hiyo kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma ya mama na mtoto, pamoja na chumba cha upasuaji wa dharura. Kwa sasa Halmashauri ipo kwenye utaratibu wa kutangaza kazi ili kupata kandarasi ya kusimamia ujenzi, ahsante.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji Kabanga?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro Mbunge wa Ngara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Mradi wa Maji Kabanga unaendelea kwa gharama ya Shilingi 941,351,342.74. Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 75 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2023 na kuhudumia wananchi zaidi ya 15,000 wa Vijiji vya Kabanga, Murukukumbo na Kumwuzuza. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa dakio, nyumba ya mashine, tanki la kukusanyia maji lenye ujazo wa lita 120,000, tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 230,000 na ujenzi wa viosk vitatu. Kazi zinazoendelea ni pamoja na uchimbaji wa mitaro kwa ajili ya kulaza mabomba umbali wa kilometa 20.694 na ukamilishaji wa ofisi ya CBWSO.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -
Je, lini Mradi wa Bwawa la kufua umeme wa RUSUMO utazinduliwa ili kuondoa tatizo la kukatika kwa umeme Ngara?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swala la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa kufua umeme wa Rusumo wa Megawati 80 wa nchi tatu za Tanzania, Burundi na Rwanda ambazo zitagawanywa sawa, umefikia asilimia 99 na utaanza kufanya kazi mwezi Juni, 2023.
Mheshimiwa Naibu Spika, mashine tatu za kuzalisha umeme zitawashwa kwa mashine moja kila mwezi kuanzia mwezi wa Juni na hivyo tunatarajia kuuzindua baada ya mwezi wa saba baada ya kuwashwa kwa mashine zote tatu kukamilika, nashukuru.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa soko la mnada wa ng’ombe wa Murusagamba?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Jimbo la Ngara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa miundombinu ya mnada wa mpakani wa Murusagamba umekamilika na ulihusisha ujenzi wa uzio, mazizi na ukarabati wa ofisi. Baada ya ujenzi kukamilika Wizara inaandaa utaratibu wa kuanza kuhamasisha wafanyabiashara na wafugaji kuanza kutumia mnada huo ili kufanikisha mauzo ya mifugo nje ya nchi na kuongeza maduhuli kwa Serikali Kuu na Halmashauri.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa mradi mkubwa wa bilioni 41 wa kupeleka maji safi Ngara?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu,
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge Jimbo la Ngara Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maji inatarajia kutekeleza wa mradi mkubwa wa maji Ngara Mjini kwa gharama ya Shilingi bilioni 41. Usanifu wa mradi huu umekamilika na na unatarajiwa kuhudumia wananchi wapato 170,678 waishio katika Kata ya Ngara Mjini, Kanazi, Kibimba, Nyamiaga na Murukulazo. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha ili utekelezaji wa mradi huo uanze.
Mheshimiwa Spika, kwa mpango wa muda mfupi wa kupunguza kero ya maji katika Mji wa Ngara na viunga vyake, Serikali katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 imetenga kiasi cha fedha shilingi milioni 600. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na uchimbaji wa visima viwili ambapo kisima kimoja kimekamilika, ujenzi wa tanki la ujazo wa lita 250,000 na ulazaji wa mtandao umbali wa kilometa 12 na ufungaji wa pampu mbili za kusukuma maji.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka umeme kwa wananchi wanaoishi kwenye mitaa 17 ya Mamlaka ya Mji Mdogo Rulenge – Ngara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza miradi mbalimbali ya kupeleka umeme kwenye vijiji na vitongoji ambapo kupitia mradi wa REA awamu ya Tatu mzunguko wa pili, vijiji 32 vya Wilaya ya Ngara vitapata umeme. Aidha, Wakala wa Nishati Vijijini yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za ununuzi wa kuwapata wakandarasi wa kutekeleza mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji (Hamlet Electrification Project - HEP), ambapo vitongoji 15 katika Jimbo la Ngara vitapatiwa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mitaa 17 katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Rulenge, Serikali kupitia TANESCO na REA itatenga bajeti katika mwaka ujao wa fedha ili kuwapatia umeme wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Ngara wananufaika na uchimbaji wa madini ya Nickel?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Jimbo la Ngara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchimbaji wa madini ya Nickel katika eneo la Kabanga unafanywa na Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited iliyopewa leseni mnamo tarehe 25 Oktoba, 2021. Mradi huo unatarajiwa kuchangia ushuru wa huduma kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kiasi cha dola za Marekani milioni 65, sawa na takribani shilingi bilioni 151 kwa kipindi cha uhai wa mgodi huo. Aidha, mradi huo unatarajia kutoa ajira za moja kwa moja 978 kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Aprili, 2022 mradi ulikuwa umetumia jumla ya dola za Marekani milioni 1.5 katika ununuzi wa bidhaa na huduma ndani ya nchi. Kati ya hizo, Dola 125,673 zilitumika kufanya ununuzi katika Wilaya ya Ngara. Hivyo, nitoe rai kwa wananchi wa Wilaya ya Ngara na Taifa kwa ujumla kuchangamkia fursa zilizopo katika mradi huo. Aidha, kupitia Sheria ya Wajibu wa Makampuni kwa Jamii (Cooperate Social Responsibility - CSR), mradi huo ulichangia takribani Shilingi milioni 39 kwa mwaka 2021 na unatarajiwa kuchangia jumla kiasi cha shilingi milioni 207.8 mwaka huu 2022, ahsante sana.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza:-
Je, kuna mpango gani wa kupandisha madaraja kwa mserereko Walimu wenye changamoto ya kupandishwa madaraja wakiwemo wa Ngara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 6(a) na (3) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298 kikisomwa pamoja na Kanuni ya 17(5) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022; upandishaji vyeo watumishi wa umma pamoja na vigezo vingine huzingatia sifa za kielimu na kitaaluma zilizoainishwa katika miundo ya maendeleo ya utumishi, utendaji mzuri wa kazi, uwepo wa bajeti na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na ofisi yangu kuhusu utekelezaji wa ikama na bajeti kwa mwaka husika.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia miongozo hiyo, ofisi yangu imeendelea kuhakiki taarifa na kuwapandisha vyeo watumishi wa kada ya ualimu waliobainishwa na waajiri kuwa na changamoto katika upandishwaji vyeo wakiwemo Walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara.
Mheshimiwa Spika, naliahidi Bunge lako kuwa, zoezi hili litakapokamilika, watumishi wa kada ya ualimu waliobainishwa na waajiri wao, wakiwemo Walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara waliothibitishwa kuwa wametimiza sifa za kupanda madaraja watapandishwa.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza:-
Je, kuna mpango gani wa kupandisha madaraja kwa mserereko Walimu wenye changamoto ya kupandishwa madaraja wakiwemo wa Ngara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 6(a) na (3) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298 kikisomwa pamoja na Kanuni ya 17(5) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022; upandishaji vyeo watumishi wa umma pamoja na vigezo vingine huzingatia sifa za kielimu na kitaaluma zilizoainishwa katika miundo ya maendeleo ya utumishi, utendaji mzuri wa kazi, uwepo wa bajeti na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na ofisi yangu kuhusu utekelezaji wa ikama na bajeti kwa mwaka husika.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia miongozo hiyo, ofisi yangu imeendelea kuhakiki taarifa na kuwapandisha vyeo watumishi wa kada ya ualimu waliobainishwa na waajiri kuwa na changamoto katika upandishwaji vyeo wakiwemo Walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara.
Mheshimiwa Spika, naliahidi Bunge lako kuwa, zoezi hili litakapokamilika, watumishi wa kada ya ualimu waliobainishwa na waajiri wao, wakiwemo Walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara waliothibitishwa kuwa wametimiza sifa za kupanda madaraja watapandishwa.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Mugoma?
WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya eneo au kituo kuteuliwa kuwa eneo la forodha na kuweza kufunguliwa kama Kituo cha Forodha mahali popote nchini kuna taratibu za kisheria ambazo inabidi zifuatwe. Taratibu hizo ni pamoja na kutangazwa na kuchapishwa kwenye Gazeti la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya mwaka 2004, kifungu namba 11.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tathmini na fidia kwa ajili ya kutoa eneo hilo lilishafanyika na sasa taratibu nyingine za kisheria zinaendelea na baada ya taratibu hizo kukamilika ujenzi utaanza.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa vibali vya misimu katika Ofisi za Uhamiaji ngazi za wilaya?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 Rejeo la 2016 ilifanya marekebisho ya Kanuni za Uhamiaji za mwaka 1997 kwa ajili ya kuzingatia haki ya kundi la wageni hasa kutoka nchi jirani wanaoingia nchini kufanya vibarua hususani katika sekta ya kilimo na nyinginezo za msimu. Kupitia marekebisho hayo, Serikali ilianzisha aina maalumu ya kibali cha msimu yaani Seasonal Migrant Pass kupitia GN Na. 518 ya mwaka 2018 ambacho hutolewa kwa wageni hao kwa kipindi cha kuanzia miezi mitatu hadi sita ili kuendana na msimu wa kilimo. Kwa sasa Serikali imekamilisha ufungaji wa mfumo kwa ajili ya utoaji wa vibali hivyo katika ngazi ya mikoa na kwamba Serikali inaendelea na maandalizi ya kupeleka huduma hiyo katika ngazi ya wilaya kwa kuanzia na wilaya za mpakani.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -
Je, lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi kati ya Gereza la Rusumo na Wananchi wa Kijiji cha Rusumo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa spika, Gereza kilimo Rusumo lipo Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera lenye ukubwa wa ekari 9,442.9. Gereza hilo limepimwa na kupata Hati Na.5548 katika mwaka 2023.
Mheshiwa spika, Serikali kupitia Jeshi la Magereza inatambua changamoto ya uhitaji wa ardhi kwa wananchi wa Kijiji cha Rusumo na kilichopo ni wananchi kudai majira ya nukta za upimaji ya Gereza Rusumo uliofanywa na Halmashauri ya Wilaya Ngara uliopitiliza hadi kwenye barabara na maeneo ya Hifadhi ya Mto Kagera. Aidha, Serikali kupitia Jeshi la Magereza imeendelea kuchukua hatua mbalimbali vikiwemo vikao vya ujirani mwema na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kwa ajili ya kushughulikia changamoto hiyo, ahsante.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Mugoma?
WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya eneo au kituo kuteuliwa kuwa eneo la forodha na kuweza kufunguliwa kama Kituo cha Forodha mahali popote nchini kuna taratibu za kisheria ambazo inabidi zifuatwe. Taratibu hizo ni pamoja na kutangazwa na kuchapishwa kwenye Gazeti la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya mwaka 2004, kifungu namba 11.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tathmini na fidia kwa ajili ya kutoa eneo hilo lilishafanyika na sasa taratibu nyingine za kisheria zinaendelea na baada ya taratibu hizo kukamilika ujenzi utaanza.