Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Agnesta Lambert Kaiza (12 total)

MHE. AGNESTA L. KAIZA Aliuliza:-

Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu ucheleweshaji wa kupandisha vyeo kwa Askari wa Jeshi la Polisi katika ngazi ya Wakaguzi Wasaidizi na kwa Wakaguzi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi ni Taasisi ya Serikali ambayo mfumo wake wa upandishwaji wa vyeo huzingatia sheria na kanuni za utumishi. Askari, Wakaguzi na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi hupandishwa vyeo pamoja na watendaji wengine wa Jeshi la Polisi kwa kuzingatia ikama na bajeti ya mwaka husika.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 mpaka 2018 jumla ya askari 2,354 walipandishwa vyeo kuwa Wakaguzi Wasaidizi na kwa kipindi cha kuanzia 2015 mpaka 2020 jumla ya Wakaguzi Wasaidizi 1,163 walipandishwa vyeo kuwa Wakaguzi wa Polisi. Serikali itaendelea kuwapandisha vyeo Askari Wakaguzi na Maofisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi kulingana na taratibu zilizoelezwa hapo awali. Ahsante.
MHE. AGNESTA L. KAIZA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka maji safi na salama Butiama ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa Baba wa Taifa katika Taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambart Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upatikanaji wa maji safi na salama katika Wilaya ya Butiama ni 61.18%. Katika kuhakikisha wananchi wa Butiama wanapata huduma ya maji safi Serikali kupitia RUWASA imekamilisha miradi ya maji katika Vijiji vya Nyabanje, Magunga, Kongoto, Bukwaba, Kamgendi na Masurura, vinavyohudumia wananchi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa lengo la kutatua tatizo la maji katika muda mrefu Butiama, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa Mugango – Kiabakari – Butiama mwezi Disemba, 2020 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2022. Kazi zilizoanza kutekelezwa ni upimaji wa maeneo ya ujenzi wa matenki, mtambo wa kusafisha maji, njia kuu ya bomba na uletaji wa vifaa katika eneo la mradi. Mradi huu unatarajiwa kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji kwa asilimia 100 katika eneo la mradi pamoja na vijiji vilivyoko ndani ya kilometa 12 kutoka bomba kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huo utatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa Maendeleo wa Saudia (Saudi Fund for Development – SFD) kwa gharama ya dola za Marekani milioni 30.69 sawa na takribani shilingi bilioni 70.
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji katika Mikoa ya Kigoma, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma na Morogoro ili kuongeza mazao ya kilimo yatakayosafirishwa kupitia SGR?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambart Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kutekeleza na kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji katika mikoa inayopitiwa na reli ya kisasa ya mwendokasi kuanzia Mkoa wa Pwani na kufanya kutathmini maeneo yote yenye sifa ya kufanya uzalishaji kwa kutumia njia ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 na 2020/2021 eneo linalomwagiliwa limeongezeka hadi kufikia hekta 695,045 na hivyo kufikia asilimia 58 ya lengo la kufikia hekta milioni 1.2 ifikapo 2025. Ongezeko hilo limetokana na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu za umwagiliaji za Kilangali Seed Farm (Kilosa) kupitia mradi wa ERPP na akimu 13 za SSIDP kupitia mradi wa SSIDP. Serikali inakamilisha ujenzi wa awali kwa skimu za umwagiliaji katika Mikoa ya Shinyanga, Tabora, Kigoma, Singida, Morogoro, Dodoma na Kagera. Aidha, Serikali itaendelea na ukamilishaji wa skimu hizo hili ziweze kutumiwa ipasavyo na wakulima.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inakamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa Mradi mkubwa wa Umwagiliaji katika Mkoa wa Kigoma wenye hekta 3,000 ambapo ujenzi wa mradi huo wa Luiche unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Aidha, miradi mingine ya umwagiliaji inayopitiwa na reli ya SGR itakayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2021 ni pamoja na Skimu za Ngomai (Kongwa), Idudumo (Tabora) na Msufini pamoja na Shamba la Mbegu la Msimba (Morogoro).
MHE. OMAR ALI OMAR K.n.y. MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:-

Je ni kwa nini askari polisi wasiwekewe utaratibu wa kusamehewa kodi katika vifaa vya ujenzi na kupewa viwanja kwa bei elekezi ili wawe na moyo wa kulitumikia Taifa bila kujiingiza katika njia za udanganyifu kwa lengo la kujiandaa na maisha baada ya kustaafu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa utoaji wa msamaha wa kodi kwa bidhaa mbalimbali vikiwemo vifaa vya ujenzi kwa askari wa Jeshi la Polisi ulikuwa unatekelezwa kupitia Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), na kutokana na changamoto za kimuundo na mfumo uliosababisha uvujaji wa mapato na utozaji kodi usio na usawa, Serikali ilifanya marekebisho yaliyopelekea kufutwa kwa baadhi ya misamaha ya kodi ikiwemo ya vifaa vya ujenzi kwa vyombo vya ulinzi na usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua kazi kubwa na nzuri katika kulitumikia Taifa letu inayofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo Jeshi la Polisi, ilianzisha utaratibu mwingine wa kibajeti wa kutoa nyongeza ya posho maalum kwa kila Askari ili kufidia gharama za kodi pale wanapofanya manunuzi ya vifaa vya ujenzi pamoja na mahitaji yao mengine. Nakushukuru.
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kukutana na Wafanyabiashara na kutafuta namna bora ya kuwa na utaratibu wa ukadiriaji kodi wenye usawa na unaozingatia mabadiliko ya biashara ili kulinda mitaji ya wafanyabiashara wa ndani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa idhini yako naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Rahim, ambaye ametujalia afya na uzima. Jambo la pili, nimshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Tatu ninaomba niwashukuru sana Wabunge wenzangu kwa ushirikiano wao mkubwa kwangu, dua na sala zao kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukadiriaji wa kodi hufanyika kwa mlipakodi kuandaa taarifa za biashara yake na mwisho wa mwaka kufanya makadirio ya kodi kulingana na taarifa hizo. Kwa msingi huo, mlipakodi hufanya makadirio mwenyewe (Self-Assessment). Kazi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni kuhakiki usahihi wa makadirio aliyofanya mlipakodi endapo yamefuata matakwa ya sheria. Kwa hiyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania hukutana na walipakodi mara kwa mara kwenye michakato ya ukadiriaji wa kodi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa wafanyabiashara kujikadiria kodi wenyewe ni utaratibu unaotumika na kukubalika duniani kote. Utaratibu huu umewekwa kwa madhumuni ya kukuza mwamko wa ulipaji kodi kwa hiari (Voluntary Tax Compliance), kurahisisha ukusanyaji kodi na kupunguza gharama za ukadiriaji. Hata hivyo, biashara ambazo hazifuati misingi ya utunzaji kumbukumbu hulazimika kuingizwa kwenye utaratibu wa ukadiriaji kulingana na mauzo (Presumptive Tax System) ambapo TRA hutoa makadirio ya kodi kulingana na mauzo ya biashara husika katika kipindi cha mwaka. Ahsante. (Makofi)
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kukutana na Wafanyabiashara na kutafuta namna bora ya kuwa na utaratibu wa ukadiriaji kodi wenye usawa na unaozingatia mabadiliko ya biashara ili kulinda mitaji ya wafanyabiashara wa ndani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa idhini yako naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Rahim, ambaye ametujalia afya na uzima. Jambo la pili, nimshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Tatu ninaomba niwashukuru sana Wabunge wenzangu kwa ushirikiano wao mkubwa kwangu, dua na sala zao kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukadiriaji wa kodi hufanyika kwa mlipakodi kuandaa taarifa za biashara yake na mwisho wa mwaka kufanya makadirio ya kodi kulingana na taarifa hizo. Kwa msingi huo, mlipakodi hufanya makadirio mwenyewe (Self-Assessment). Kazi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni kuhakiki usahihi wa makadirio aliyofanya mlipakodi endapo yamefuata matakwa ya sheria. Kwa hiyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania hukutana na walipakodi mara kwa mara kwenye michakato ya ukadiriaji wa kodi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa wafanyabiashara kujikadiria kodi wenyewe ni utaratibu unaotumika na kukubalika duniani kote. Utaratibu huu umewekwa kwa madhumuni ya kukuza mwamko wa ulipaji kodi kwa hiari (Voluntary Tax Compliance), kurahisisha ukusanyaji kodi na kupunguza gharama za ukadiriaji. Hata hivyo, biashara ambazo hazifuati misingi ya utunzaji kumbukumbu hulazimika kuingizwa kwenye utaratibu wa ukadiriaji kulingana na mauzo (Presumptive Tax System) ambapo TRA hutoa makadirio ya kodi kulingana na mauzo ya biashara husika katika kipindi cha mwaka. Ahsante. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA K.n.y. MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kulipatia Jeshi la Polisi magari mapya kama moja ya vitendea kazi ili litekeleze majukumu yake ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kulipatia Jeshi la Polisi magari kama nyenzo ya kutendea kazi. Mkakati wa Serikali ni kutenga fedha kwenye Bajeti yake kila mwaka ili kununulia vitendea kazi muhimu yakiwemo magari na pikipiki. Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Jeshi la Polisi limetengewa kiasi cha Shilingi Bilioni 15 kwa ajili ya ununuzi wa magari 101 na pikipiki 336. Nashukuru.
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: -

Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa mradi wa kuzuia mafuriko katika Mto Msimbazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Lambert Kaizer, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mradi huu kwa sasa uko katika hatua za kufanya uhakiki wa taarifa na mali za wananchi wanaopaswa kupokea fidia na kusainiwa kwa mkataba baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia. Mradi huo unategemewa kuanza rasmi mwezi Julai, 2022.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira inaamini kuwa utekelezaji wa mradi huu utawezesha kuondoa kabisa tatizo la mafuriko katika Bonde la Mto Msimbazi.
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: -

Je, Serikali ipo tayari kuruhusu uraia pacha kwa Watanzania wenye uraia wa nchi nyingine?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, uraia wa Tanzania unaongozwa na Sheria ya Uraia ya Tanzania Sura ya 357 Rejeo la mwaka 2002. Sheria hii inabainisha aina tatu za uraia wa Tanzania ambazo ni uraia wa kuzaliwa, uraia wa kurithi na uraia wa tajnisi.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Uraia tajwa hapo juu, Serikali hairuhusu uraia pacha kwa watu wazima isipokuwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka kumi na nane ambao wanakuwa na uraia wa Tanzania na uraia wa nchi nyingine.
MHE. AIDA J. KHENANI K.n.y MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:-

Je, kwa nini Serikali isisamehe kodi na kuondoa baadhi ya tozo katika Sekta ya Elimu na Afya ili kuvutia taasisi binafsi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa misamaha ya kodi katika Sekta ya Elimu na Afya kwa kuzingatia sheria na miongozo mbalimbali kama ifuatavyo: -

(a) Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332:-

(i) Wafanyabiashara wanaojihusisha na utoaji wa huduma za afya na elimu wanasamehewa kulipa kodi ya makampuni yanayotangaza kupata hasara kwa mfululizo wa miaka zaidi ya mitatu;

(ii) Mchango wowote anaofanya mfanyabiashara kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa Elimu anajirejeshea kama gharama wakati wa kutengeneza faida;

(iii) Taasisi yoyote iliyoanzishwa kwa ajili ya kujishughulisha na uendelezaji wa elimu na afya au kutoa huduma za umma kwenye Sekta za Afya na Elimu imepewa hadhi ya charitable organization na kupata unafuu wa kodi.

(b)Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148:-

(i) Msamaha wa kodi umetolewa katika ujenzi wa majengo kwa ajili ya kutoa huduma za afya na elimu kwa jamii;

(ii) Bidhaa na huduma zinazoingizwa nchini na Serikali au kununuliwa katika soko la ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi katika Sekta ya Afya na Elimu zimesamehewa Kodi ya VAT; na

(iii) Madawa na vifaa vya utabibu na huduma za afya zilizoorodheshwa katika para 7 la jedwali la kwanza la misamaha zimesamehewa Kodi ya VAT.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha miongozo na taratibu za usimamizi wa kodi ili kuimarisha biashara na kuvutia wawekezaji, ahsante.
MHE. NUSRAT S. HANJE K.n.y. MHE. AGNESTA L. KAIZA auliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Magereza ili kulinda haki za wafungwa na mahabusu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Magereza limejipanga kukarabati Magereza kwa kutumia fedha za vyanzo vya ndani na fedha inayotengwa kwenye bajeti kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika mwaka 2021/2022 Serikali ilitenga Shilingi 840,000,000/= kwa ajili ya ukarabati wa Magereza matano ambayo ni Gereza Maweni, Isanga, Kondoa, Lindi na Mkuza na limetumia vyanzo vya ndani kukarabati Magereza yafuatayo: Gereza Rombo, Ukonga, Mkono wa Mara, Kwitanga, Idete, Mbigili, Shinyanga, King’ang’a, Butimba, Luanda, Liwale na Babati.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa fedha 2022/2023 Jeshi la Magereza limetenga Shilingi 4,569,000,000/= ili kujenga Magereza sita ya Wilaya za Kilosa, Kaliua, Karatu, Kakonko, Gairo na Msalato.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. (Makofi)
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:-

Je, kwa kiwango gani Sheria zilizopo za kupambana na matukio ya ubakaji zinajitosheleza?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwanza niweke sawa. Ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, najibu kwa niaba ya Waziri wa Katiba.

Mheshimiwa Spika, Mwaka 19...

SPIKA: Sasa hebu ngoja kwanza. Haya endelea Mheshimiwa.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Mwaka 1998 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga sheria mahususi inayosimamia makosa ya kujamiiana na makosa yanayoendana nayo, yaani “The Sexual Offence Special Provision Act, No. 4 of 1998”. Sheria hii ilifanya marekebisho ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16; Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20; Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6; Sheria ya Ukomo wa Adhabu, Sura ya 90 na Iliyokuwa Sheria ya Mtoto na Mtu mwenye Umri Mdogo, Sura ya 13.

Mheshimiwa Spika, lengo la kutungwa kwa sheria hiyo lilikuwa ni kumlinda mwanamke na mtoto dhidi ya makosa ya kujamiiana na makosa yote yanayoshabihiana. Sheria hii iliongeza adhabu ya makosa hayo kuwa ni kifungo cha maisha au kifungo kisichopungua miaka 30. Hivyo, kwa kiasi kikubwa, sheria zilizopo zinajitosheleza kupambana na matukio ya ubakaji.