Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Amandus Julius Chinguile (4 total)

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE Aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea kwa kiwango cha lami utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amandus Julius Chinguile, Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kuzingatia umuhimu wa barabara ya Masasi – Nachingwea inayounganisha makao makuu ya wilaya ya Masasi na Nachingwea, imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina tangu mwaka 2015. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami, barabara yenye urefu wa kilometa 45. Katika mwaka wa fedha huu 2020/2021, jumla ya shilingi bilioni 1.43 zimetengwa kwa ajili ya maandalizi ya kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha za ujenzi pia imeendelea kutenga fedha za matengenezo mbalimbali kwa barabara hii ambapo katika mwaka wa fedha wa 2020/2021, jumla ya shilingi milioni 232.66 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ili barabara hii iendelee kupitika katika majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA K.n.y. MHE. AMANDUS J. CHINGUILE aliuliza:-

Je lini maji safi na salama yatapelekwa katika Kata za Kiegei, Kilimarondo, Matekwe na Namapwia – Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amandus Julius Chinguile, Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu spika, katika kuhakikisha Kata za Kiegei, Kilimarondo, Matekwe na Namapwia zinapata huduma ya majisafi na salama na yenye kutosheleza, Serikali katika mwaka wa fedha 2023/2024 itafanya utafiti wa maji chini ya ardhi (Hydrogeological Survey) pamoja na kuchimba visima virefu vinne katika kata hizo. Kazi hiyo inatarajiwa kufanyika na kukamilika mwezi Disemba, 2023. Uendelezaji wa visima hivyo utafanyika mara baada ya uchimbaji kukamilika na maji kupatikana.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE aliuliza: -

Je, lini Serikali itatoa leseni kwa wachimbaji wadogo wa madini Kata za Nditi na Kiegi – Nachingwea na maeneo mengine ya Mkoa wa Lindi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amandus Julius Chinguile, Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini hadi Oktoba 2023, imetoa jumla ya leseni 2731 za uchimbaji mdogo wa madini katika Mkoa wa Lindi. Aidha, leseni zaidi ya 200 za Uchimbaji Mdogo wa Madini zimetolewa katika Vijiji vya Kiegei na Nditi Wilayani Nachingwea.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini itaendelea kutoa leseni za madini katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Wilaya ya Nachingwea na maeneo mengine ya Mkoa wa Lindi kadri itakavyokuwa ikipokea maombi ya leseni kutoka kwa wananchi ili kuwezesha ushiriki wao katika uchumi wa madini, ahsante sana.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE aliuliza: -

Je, lini Serikali itafufua viwanda vya Mafuta Ilulu na kubangua korosho – Nachingwea?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, Serikali ilifanya zoezi la tathmini na ufuatiliaji kwa viwanda vyote vilivyobinafsishwa nchi nzima ikiwa ni pamoja na viwanda vya Mafuta Ilulu na kubangua korosho - Nachingwea. Tathimini hiyo imeisaidia Serikali kuweka mikakati ya kufufua viwanda hivyo, ikiwemo kuvirejesha Serikalini na kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia wawekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Korosho cha Nachingwea kimepata mwekezaji ambaye ni kampuni ya ANH & RAKA Ltd. ambaye amesaini Mkataba wa Pango kwa maana ya Lease Agreement na mamlaka ya EPZ tarehe 11 Desemba, 2023 kwa ajili ya kuchakata mazao ya kilimo ikiwemo korosho, ufuta na karanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Kiwanda cha Mafuta Ilulu kimepata mwekezaji kampuni ya MCL Agro Co. Ltd. ambaye amesaini Mkataba wa Pango yaani Lease Agreement na Mamlaka ya EPZ tarehe 28/3/2023 kwa ajili ya kuchakata mazao ya kilimo ya korosho, ufuta na karanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa, wawekezaji hao wapo katika hatua mbalimbali za maandalizi ya kuanza uendelezaji. Aidha, kwa mujibu wa mikataba wawekezaji hao wanapaswa kuwa wameanza uzalishaji ndani ya miezi 24 kutoka tarehe ya kusaini mkataba, nakushukuru.