Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Amandus Julius Chinguile (26 total)

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali yetu yenye kutia matumaini lakini bado kwa umuhimu wa barabara hii wananchi wa Jimbo la Nachingwea watapenda kusikia commitment ya Serikali. Kwa kweli, katika hili viongozi wengi wanahukumiwa kutokana na barabara hizi pamoja na mambo mengine. Je, nini commitment ya Serikali juu ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, viko vijiji vya Ikungu, Chiola kuelekea Ruangwa, hapa tayari walifanyiwa tathmini na wenzetu wa TANROADS. Watu wa TANROADS walikuja wakafanya tathmini wakiamini kwamba barabara itapita upande wa kulia baada ya muda wakarudi tena wakafanya tathmini upande wa kushoto. Kwa hiyo, hawa wananchi wamezuiliwa kwenye maeneo yale wasifanye maendelezo. Ni lini Serikali itakwenda kutoa ufafanuzi wa jambo hili, ili wananchi wa maeneo yale waweze kuendelea na shughuli zao? Ahsante sana.

SPIKA: Hiyo ni kwa barabara ya Nachingwea – Ruangwa?

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, ndiyo.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Chinguile, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, commitment ya Serikali ni kwamba tayari fedha ya awali za kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami zimeshatengwa. Pia barabara hii imeahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na pia ni kati ya barabara ambayo Mheshimiwa Rais ameahidi kuijenga kwa kiwango cha lami katika kipindi hiki cha miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ambalo ameuliza kwamba kuna wananchi ambao wameshindwa kuendeleza maeneo yao kwa sababu ya watu wa TANROADS waliokwenda kupima, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea kwamba suala hili linaendelea kufanyiwa kazi. Naomba kama kuna changamoto yoyote tofauti ambayo pengine mimi nitakuwa siifahamu basi tuwasiliane naye ili niweze kujua changamoto halisi ni ipi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kuna sintofahamu kwenye Jimbo langu la Nachingwea kuhusu pembejeo. Wizara ya Kilimo ilitoa tamko kwamba msimu huu wa korosho wakulima hawatakuwa na makato yoyote yatakayokatwa kuhusiana na pembejeo hizo. Hata hivyo, karatasi au fomu wanazosaini wakulima wetu kwenye zile AMCOS inaonekana kwamba kuna makato watakuja kukatwa kwa sababu ya kuchukua hizo pembejeo. Nini tamko la Serikali kuhusu suala hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nimekusoma na nimekuelewa.

Mheshimiwa Spika, labda nirudie tena na niseme kupitia Bunge lako Tukufu kuviambia Vyama vya Ushirika vya Mkoa wa Lindi, Mtwara na Pwani, Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia Suluhu Hassan, imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 61 kuwapa wakulima wa korosho wa maeneo hayo kwa ajili ya majaribio, asikatwe mkulima yeyote hata senti moja tutakapokwenda kwenye msimu.

Niwaombe Wakuu wa Wilaya wahakikishe kwamba hakuna mkulima yeyote anayesainishwa fomu yoyote ya kuonyesha kwamba anadaiwa hata senti moja. Pia nivitahadharishe Vyama vya Ushirika visijaribu kumkata mkulima shilingi 100, itawagarimu. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwanza nipende kuipongeza Serikali kwa kutuletea zaidi ya bilioni 1.9 kwa ajili ya ukarabati mkubwa kwenye Chuo hiki cha Nachingwea:-

Mheshimiwa Spika, swali langu, chuo hiki ni kikongwe, Je, Serikali sasa haioni haja ya kuanzisha kozi maalum ya masomo ya sayansi, ili tuzalishe wataalam wengi, na hasa kwenye masomo haya ya sayansi kwenye Chuo cha Nachingwe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kwa vile ametuletea wazo, basi tunaomba tulichukue twende tukalifanyie utafiti, tuangalie uhitaji wa kozi hiyo katika eneo hilo. Iwapo kama Serikali itabaini kwamba, upo huo uhitaji tutaweza kuingiza kwenye mipango yetu. Ahsante.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Katika Jimbo langu la Nachingwea kuna Chuo cha Ualimu lakini hakitoi kozi ya sayansi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kozi ya sayansi katika chuo hiki cha Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna Chuo cha Ualimu pale Nachingwea kwa vile Mheshimiwa Mbunge ametoa ushauri, naomba tuuchukue ushauri huu twende tukaufanyie tathmini ili tuweze kuangalia kama kuna uhitaji wa kuanzisha kozi hiyo ya sayansi katika chuo hicho.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa, kuna baadhi ya vitongoji katika vijiji hivyo havijawekwa kwenye orodha ya mpango wa kuwekewa vitu kwa ajili ya kuchotea maji. Je, Serikali inaweza kupokea maombi mapya sasa maalum kwa ajili ya kuongeza vituo vya kuchotea maji kwenye vijiji ambavyo vimepitiwa na mradi huu?

Swali la pili, miradi mingi kwenye Halmashauri zetu imekwama kwa sababu ya upatikanaji wa mabomba ambayo yananunuliwa kwa pamoja kupitia RUWASA Makao Makuu.

Je, Serikali sasa inatuhakikishiaje kwamba mabomba sasa yanakwenda kupatikana kwa wakati ili kutokukwamisha miradi mingi kwenye Halmashauri zetu?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya jukumu mahsusi na Wizara ya Maji ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama, tunao huu mradi mkubwa ambao unajengwa na kuna baadhi ya vitongoji ameviainisha ambavyo vinahitaji maji, nataka nimhakikishie kukamilika kwa mradi huu na hivyo vitongoji navyo vitapokea kuhakikisha nao wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji kupitia Wakala wa Maji Vijijini ni kuhakikisha tunatatua changamoto ya maji katika maeneo ya vijijini. Tulikuwa na changamoto ya manunuzi na tumepewa ombi na maelekezo ya Bunge ni kuhakikisha manunuzi haya yanafanyika katika maeneo ya Mikoa, tulishakaa na wenzetu wa manunuzi kwa maana ya RUWASA maelekezo ya Wizara ni kwamba manunuzi yote yanatakiwa kufanyika katika Mikoa husika ili kuharakisha utekelezaji wa miradi. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa nchi yetu imejaliwa wahitimu wengi wa vyuo vikuu kila kona wakiwemo kule Nachingwea. Je, Serikali inachukua vigezo gani kuwapeleka

hawa vijana wetu ambao wametapakaa nchi nzima huko Israel? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, cha kwanza hii programu inakuwa coordinated na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje kwa kushirikiana na taasisi ya Ministry Affairs ya Israel for International Development and Corporation. Mara nyingi Serikali huwa inatoa window na huwa kuna utaratibu maalum ambao unatumika namna ya kuwapata vijana wanao-apply na kuweza kwenda kushiriki katika windows za namna hii.

Mheshimiwa Spika, tumekutana na ubalozi wa Israel hivi karibuni na kujadiliana nao namna ya kuboresha huduma ya kuwapata vijana, kwa sababu wapo vijana ambao wana apply kwa ajili ya kwenda kufanya jambo A, wakifika kule wanajikuta wamekuwa committed kufanya jambo lingine tofauti na kile ambacho walitarajia. Tumeongea na Ubalozi wa Israel, tunaendelea nao na mazungumzo tukishirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje, badala ya kuwasafirisha hao vijana. Tunavyo vituo vingi katika nchi yetu. Ushirikiano ule wa utalaam tuweze kuutumia ndani ya nchi na waweze kuja kutusaidia ndani ya nchi yetu. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Jimbo la Nachingwea lina kata 36, kati ya hizo kata mbili hazina watendaji wa kata, lakini lina vijiji 127 na vijiji 37 havina watendaji wa vijiji. Na kwa kuwa tunajua watendaji hawa ndio wanaosukuma shughuli zote za maendeleo katika maeneo yetu;

Je, ni lini Serikali itatoa vibali kwa ajili ya kupata hawa watendaji ambao watatusaidia kwenye maendeleo kwenye maeneo yetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kata mbili ambazo hazina watendaji na vijiji 37 ambavyo havina watendaji kule Nachingwea ni adhma ya Serikali kuhakikisha kwamba kila kata, kila kijiji kina watendaji. Kadri ya bajeti itakavuoruhusu basi viabali hivi vitaendelea kutolewa. Na nikutaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko mbioni kuajiri watendaji wa kata katika kata zote ambazo ziko wazi nchini. Kwa hiyo ni kuvuta Subira, nikuhakikishie kwamba hilo linafanyiwa kazi.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa nchi yetu kwa sasa ina wahitimu kila kona, na kwa sasa kwa sababu mfumo ulioko wa kuomba ajira una changamoto na una manung’uniko mengi.

Je, Serikali iko tayari sasa kupitia mfumo huu wa sasa ili kupeleka kwenye kila Jimbo idadi sawa ambayo itakwenda kutibu sasa tatizo hili la manung’uniko ambalo kwa kweli kila kona lipo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA N AUTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili halitofautiani nalile lililoulizwa na Mheshimiwa Mtemvu, tofauti ni kwamba Mheshimiwa Mtemvu kasema Wilaya lakini Mheshimiwa Mbunge kasema Jimbo. Kama nilivyosema tunaendelea kufanya utafiti kwa kutumia mifumo lakini na uhalisia wa jambo lenyewe kama tunaweza tukalitekeleza katika usahihi sana kinyume na utaratibu wa sasa wa kushindanisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna upungufu kwenye kushindanisha au kama hakuna uwazi wa kutosha kwenye kushindanisha inaweza ikawa kazi nyepesi zaidi kushughulikia kuliko kutafuta mfumo utakaoweza kuja na majawabu haya. Hata hivyo, katika jibu langu la msingi nimesema kwamba tutajitahidi kuandaa, tumeunda timu ambayo inaendelea kufanya utafiti hata sasa wako kazini watatuletea majawabu ya namna gani tunaweza kufanya yote mawili mfumo na uhalisia ili tuweze kuona manung’uniko haya yanakwisha kabisa. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Tarafa ya Ruponda katika Wilaya ya Nachingwea haina Jengo la Mahakama ya Mwanzo; je, ni lini Serikali itajenga Jengo la Mahakama ya Mwanzo kwenye Tarafa hii ya Ruponda iliyoko Makao Makuu ambayo yako kwenye Kata ya Ruponda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijibu swali Mheshimiwa Amandus Chinguile, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Tarafa hii ya Ruponda ambako Mheshimiwa Mbunge ametamka, iko kwenye mpango wetu wa bajeti. Kwenye zile Mahakama 60 tunakwenda kujenga Mheshimiwa Mbunge, na tunafahamu ina umbali wa zaidi ya kilometa 14 kufuata huduma eneo lingine. Kwa hiyo, liko kwenye mpango tumeweka. Ahsante. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mfumo wa ajira ulioko sasa una manung’uniko mengi; Serikali haioni iko haja sasa ya kupitia mfumo wenyewe kwa ujumla ili uwe rafiki kwa vijana wetu walioko? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amandus kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wakati tunawasilisha bajeti ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, hoja anayoeleza Mheshimiwa Mbunge ilitolewa pia katika kikao kile na yalikuwa ni makubaliano ya Bunge lako kwamba tutayachukua mawazo mazuri yale na kwenda kuyafanyia kazi, na haya yote yatakapokuwa yamekamilika basi yatakuja kuonekana katika sera na sheria ambazo baadae nafikiri zinaweza zikabadilika kutokana na mawazo mazuri ya Bunge lako.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maagizo ya Bunge yanaendelea kufanyiwa kazi, na tutakapokuwa tayari tutakuja kuleta taarifa katika utaratibu wa vile vikao vyetu.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Masasi – Nachingwea yenye kilometa 45 upembuzi yakinifu na wa kina umefanyika zaidi ya miaka tisa iliyopita. Ni lini Serikali itaanza ujenzi sasa barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chinguile, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii ambayo inaunganisha Wilaya ya Masasi na Wilaya ya Nachingwea, kwa maana ya Mikoa wa Mtwara na Lindi, ni muhimu sana. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii kama bajeti ambayo tunategemea kuiwasilisha wiki ijayo itapita, ipo kwenye mpango kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Nachingwea ni chakavu na limejengwa tangu enzi za wakoloni. Je, nini mpango wa Serikali wa kujenga jengo jipya litakaloendana na hadhi ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwamba ni kweli kama nilivyoeleza kwenye swali ambalo nimetoka kulijibu muda siyo mrafu, tunayo majengo ambayo yamechakaa lakini tunayo majengo ambayo yamekosa hadhi, kwa maana ya uhalisia wa miradi tuliyonayo kwa mwaka huu ambao unakwenda kumalizika tulikuwa tulikuwa na miradi 22, mwaka ujao tutakuwa na miradi 13 na inawezekana kabisa katika mwaka ujao ukawa umeingia kwenye mpango wa kuangalia uwezekano wa kujengewa Mahakama nyingine. Kwa hiyo, naomba tu Mbunge awe na utulivu katika kipindi hiki kwa sababu miradi yote mpaka kufikia 2025 tutakuwa tumekamilisha majengo yote ya ngazi ya Wilaya asante.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwenye Jimbo langu la Nachingwea kuna viwanda viwili ambavyo kwa muda mrefu havifanyikazi; Kiwanda cha Lindi Pharmacy lakini pia Kiwanda cha Mafuta Ilulu.

Nini mpango wa Serikali kufufua viwanda hivi ili viweze kuzalisha ajira kwa vijana wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali kupitia ubinafsishaji tulibinafsisha viwanda 156 lakini katika viwanda hivyo viwanda 88 ndiyo vinafanyakazi vizuri, 68 vilikuwa havifanyikazi vizuri na moja ya maeneo ambayo tumekwishayafanyia kazi ni kuvirudisha baadhi ya viwanda ambavyo vipo 20, mojawapo vikiwa hivi viwanda viwili ambavyo alivitaja Mheshimiwa Mbunge, Kiwanda cha Mafuta Ilulu na kile kingine cha kubangua korosho cha Nachingwea.

Mheshimiwa Spika, lakini katika hatua za awali tumeshafanya tathmini viwanda hivi ni kati ya viwanda ambavyo tutaviweka katika maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya kuzalisha bidhaa kwa ajili ya mauzo nje (SEZ).

Kwa hiyo, tayari tumeshachukua hatua mbalimbali na sasa tunaendelea kutafuta wawekezaji ambao tutashirikiana nao, ili wazalishe bidhaa aidha za mafuta au kubangua korosho kama ilivyokuwa awali kwa ajili ya kuuza nje. Kwa hiyo, tayari tumeshachukua hatua kwamba hivi vitakuwa chini ya maeneo huru ya uwekezaji kwa ajili ya mauzo nje na hivi viwanda vitafufuliwa tutakapopata mwekezaji mapema iwezekanavyo. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Nachingwea ni chakavu na limejengwa tangu enzi za wakoloni. Je, nini mpango wa Serikali wa kujenga jengo jipya litakaloendana na hadhi ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwamba ni kweli kama nilivyoeleza kwenye swali ambalo nimetoka kulijibu muda siyo mrafu, tunayo majengo ambayo yamechakaa lakini tunayo majengo ambayo yamekosa hadhi, kwa maana ya uhalisia wa miradi tuliyonayo kwa mwaka huu ambao unakwenda kumalizika tulikuwa tulikuwa na miradi 22, mwaka ujao tutakuwa na miradi 13 na inawezekana kabisa katika mwaka ujao ukawa umeingia kwenye mpango wa kuangalia uwezekano wa kujengewa Mahakama nyingine. Kwa hiyo, naomba tu Mbunge awe na utulivu katika kipindi hiki kwa sababu miradi yote mpaka kufikia 2025 tutakuwa tumekamilisha majengo yote ya ngazi ya Wilaya. Ahsante.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya Nanganga – Nachingwea kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, katika jibu la msingi nilisema kwamba barabara ya Nachingwea – Nanganga ipo katika hatua za mwisho na tunategemea katika zile barabara ambazo tunategemea kuzisainia kwa pamoja hiyo barabara ni mojawapo ya Nanganga – Nachingwea. Ahsante.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Ziko Leseni zimetolewa kwa ajili ya shughuli za utafiti kwenye maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Jimboni Nachingewa lakini wahusika hawajafanya shughuli hiyo iliyokusudiwa kwa muda mrefu sasa.

Je, Serikali haioni sasa iko haja ya kupitia sheria yetu ili kuweza kuondoa utitiri wa hawa watafiti ambao kimsingi hawatimizi majukumu hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi baada ya kipindi hiki cha Bunge ili kwenda Jimboni Nachingwea kuona halihalisi iliyoko na kuwatia moyo wachimbaji wadogo wadogo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Chinguile, Mbunge makini wa Nachingwea, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu waliopewa leseni na wamezilaza hawazifanyii kazi; mwezi wa tisa na mwezi wa kumi tulitoa kama ndiyo kipindi cha mwisho, waweze aidha kufanyia leseni zao kazi au zifutwe. Tangu tangazo hilo litoke, zaidi ya leseni 7,000 zimeshahuishwa na kuna wale ambao hawajaweza kuhuisha mpaka tarehe 30 mwezi uliopita, mchakato wa kuzifutia hizo leseni unaendelea. Hatukuishia hapo, zilizokwishaharibiwa kwa kutofanyiwa kazi huko nyuma, maeneo zaidi ya 48 zimegawiwa kwa wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Spika, hivyo hata katika jimbo lake, wale ambao watashindwa kuendeleza leseni kwa mujibu wa tangazo hilo la Serikali kupitia Wizara ya Madini, watarudisha hizo leseni na tutawapa wale ambao wako tayari.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili, mimi niko tayari baada ya Bunge hili, nitampangia ratiba. Tutafika huko tuwatie moyo wachimbaji wadogo wanaofanya shughuli zao na kuwahamasisha wengine watumie fursa zilizoko katika Wizara ya Madini kupata uwekezaji ambao utawainua katika Maisha yao. ahsante sana. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Je, ni lini Serikali itajenga mtambo kwa ajili ya usikivu wa TBC, katika Tarafa ya Kilimarondo, Jimbo la Nachingwea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika swali la Mheshimiwa Justin, tunao ujenzi wa vituo takribani 14 ambavyo vinaendelea, vilevile katika bajeti ijayo tunatarajia kuongeza vituo vingine nimuombe sasa Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu ni eneo specific ambalo sikutarajia angeweza kuligusia, akitoka hapa tukutane ili niangalie kama lipo katika vile vituo 14 ama vile vituo ambavyo tunaenda kuviongeza ili tuhakikishe kwamba tunakuwa na majibu ya uhakika kwa ajili ya wananchi wake wa Jimbo la Nachingwea. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kwa kuwa viwanda hivi tayari vilipata wawekezaji ambao walishindwa kuendeleza kama mkataba ulivyodai, je, ni hatua gani zimechukuliwa na Serikali kwa wawekezaji hawa ambao walishindwa kufanya kazi iliyokusudiwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, zao la korosho ni zao la kibiashara na linatuingizia kama Taifa fedha nyingi za kigeni, kwa kufufua viwanda hivi vya kubangua korosho tutakuwa tunaongeza thamani ya zao lenyewe, lakini pia tutakuwa tunainua uchumi wa wakulima na kuongeza pato la Taifa. Ni mkakati gani wa Serikali kuhakikisha korosho haziuzwi zikiwa ghafi badala yake kufufua viwanda vingi vya kubangua korosho ili tuweze kuinua ubora wa zao hilo na kuongeza thamani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Chinguile kwa ufuatiliaji kuhusu uongezaji thamani wa mazao mbalimbali ikiwemo korosho katika Mkoa wa Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya hatua ambazo Serikali imechukua kwa swali lake la kwanza, ni kupitia kama nilivyosema na kufanya tathmini ya viwanda vyote ambavyo vilibinafsishwa na havifanyi kazi. Hatua ya kwanza ilikuwa ni kuvirejesha na ndiyo maana viwanda zaidi ya 20 vimesharejeshwa na vingine tunaendelea utaratibu kukamilisha urejeshwaji, zaidi ya viwanda 33 na hiyo ndiyo hatua ya kwanza kwamba wale ambao wameshindwa kuviendeleza viwanda hivi, vyote vitanyang’anywa ili tuweze kutafuta wawekezaji wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, katika hilo tunataka wale ambao sasa huenda walifanya hujuma kwenye viwanda vile ambavyo walipewa vilikuwa labda na mitambo na vifaa mbalimbali vya mashine za viwanda hivyo ambavyo either wameng’oa au wamefanya hujuma yeyote, basi nao kulingana na mikataba ile nao watachukuliwa hatua mbalimbali za kisheria kulingana na mikataba ambayo tuliingia nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la pili, ni kweli Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha bidhaa, mazao ya kilimo yanaongezwa thamani ikiwemo korosho ambayo inaingizia Serikali fedha nyingi za kigeni. Lengo sasa ni kuhakikisha korosho inaanza kuuzwa ikiwa imebanguliwa badala ya kuwa ghafi na ndiyo maana tumeanza moja, kurejesha hivi viwanda na kuvifufua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Wizara kupitia taasisi zetu, tunaandaa mashine, teknolojia rahisi ya viwanda vidogo vidogo ambavyo vitawasaidia wakulima wadogo wadogo na wajasiriamali waweze kubangua katika ngazi ya chini ili tuhakikishe tunauza korosho ambayo imebanguliwa badala ya kuendelea kuuza korosho ghafi, nakushukuru. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, zao la karanga na soya lilimwa kwa wingi miaka ya zamani kwenye Jimbo langu la Nachingwea. Kwa kuzingatia mahitaji ya sasa ya mazao haya kwenye soko la dunia, ni nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha inafufua zao hili kwenye Jimbo la Nachingwea na maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuhakikisha tunafufua mazao yote ambayo yamekuwa na tija kubwa kwa wananchi, ikiwemo soya ambayo sasa hivi inapelekwa sana nchini China ambao wamekuwa ni waagizaji wakubwa wa zao hili. Kwa hiyo, jambo hili lipo katika mpango na tumeshazielekeza taasisi zetu za kitafiti ziongeze utafiti na uzalishaji wa mbegu ili tuwafikishie wananchi. Kwa hiyo, wananchi wa Nachingwea wakae tayari kwa jambo hilo kwa sababu liko katika mipango yetu, ahsante. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia Mto Ruvuma kumaliza kabisa tatizo la maji katika Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa mradi huu ni mradi wa kimkakati kwa Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi, kwa kutambua umuhimu huo na Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakifuatilia sana akiwemo Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea, Serikali inaendelea na mapitio ya usanifu wa mradi huu wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma ili yafike mpaka Lindi na Mtwara.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Serikali imeshafikia katika hatua nzuri na tuombe tu kwamba pindi tutakapoenda katika hatua ya utekelezaji Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kushirikiana kuhakikisha kwamba waweze kutoa ushauri, michango na maoni yao tutayapokea na kuyaingiza katika utekelezaji halisi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nipongeze kwanza Serikali, wamesema sasa walau wameshusha kwa ngazi ya mkoa, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza: Je, Serikali haioni iko haja sasa ya kutambua mahitaji ya nafasi hizi za kazi kwa kila jimbo ili kutoa msawazo sawa na baadaye kuratibiwa kitaifa ili kulinda utaifa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, wako vijana ambao walihitimu vyuo mbalimbali kuanzia 2015 mpaka 2020 na kwa sasa kwa kutumia mfumo hawa vijana ni kana kwamba mfumo unawakataa. Je, Serikali haioni iko haja sasa ya kutoa upendeleo maalum kwa hawa vijana ambao kwa sasa kwa sababu ya umri unavyokwenda wanaachwa sasa kwenye mfumo wa ajira? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Amandus kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza ametaka kujua kwamba Serikali ina mpango gani wa juu ya kushusha hizi ajira katika ngazi ya majimbo kwa maana hiyo. Bunge lako Tukufu lilitoa maelekezo kwa Serikali kwamba wahakikishe ajira hizi zinashuka katika ngazi za mikoa. Katika kutekeleza hilo na commitment ambayo Serikali ilitoa ndani ya Bunge hili, tayari utekelezaji huo umeanza ambao tumeanza katika ngazi ya mkoa na usaili utafanyika katika ngazi ya mkoa ambapo utahusisha Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, baadaye kwa kuwa safari ni hatua, tayari Serikali itaendelea kujipanga kwa namna ya kushuka katika ngazi ya wilaya. Kwa hiyo, nimwondolee shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imekuwa ikisikiliza maelekezo ya Bunge na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge na ushauri wake tunaupokea, tutaingiza katika utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ameuliza habari ya kwamba ni namna gani Serikali imejipanga sasa kuangalia wale waliohitimu kwa miaka ya nyuma. Ni kweli katika nyakati mbalimbali Serikali imetumia hiyo approach ya kuchukua wale wa miaka ya nyuma na ndani ya Bunge humu tulipata ushauri huo, lakini kiukweli ukiangalia wale wanaohitimu na namna ambavyo Serikali imekuwa ikitoa ajira nafasi zinakuwa ni chache. Kwa hiyo, ukienda kwa mtindo huo unaweza ukakuta tunakaa ndani ya mwaka mmoja.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka mmoja, kwa mfano waliohitimu 2015 tunakaa tunaajiri ndani ya miaka sita, kwa hiyo, tatizo litakuwa pale pale, ndiyo maana tumerejea kufuata kwenye Sera ya Ajira na Utumishi kwamba sasa waende kwenye ushindani na katika ushindani ili kuzingatia pia waliomaliza kwa miaka ya nyuma, Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kwamba kama endapo waliokuwa kwenye ushindani wamefungana kwa marks na yule ambaye ana umri mkubwa atapewa kipaumbele, nashukuru. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Nanganga – Nachingwea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Nanganga – Nachingwea yenye urefu wa kilometa 45 Serikali ilishakamilisha usanifu wa kina. Tunaendelea kutafuta fedha ili tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami ili kuwasaidia wananchi wa Nachingwea kufika Makao Makuu ya Mji wa Lindi kwa barabara ya lami, ahsante. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Sekondari Amandus Chinguile ipo Nachingwea Mjini na imezungukwa na makazi ya watu, je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kujenga uzio katika shule hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu yangu ya msingi kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa zina wajibu wa msingi wa kutafuta fedha, kutafuta mapato na kutenga kwenye bajeti zake fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya muhimu ikiwemo ujenzi wa uzio katika shule zetu. Kwa hiyo, niendelee kumkumbusha Mkurugenzi aweze kuweka katika mipango ya kibajeti katika halmashauri yake ili aweze kutenga fedha kwa kadiri ya vipaumbele na kwa kadiri ya mahitaji kwa ajili ya ujenzi wa fence katika shule hii ya Amandus Chinguile. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali yanayoonesha namna wanavyojali wastaafu, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wastaafu ambao wanaishi vijijini na mbali sana na makao makuu ya halmashauri na afya zao wakati mwingine siyo nzuri, wakati Serikali inatengeneza mfumo mpya wa kidigitali, je, haioni haja sasa ya kuwasogezea huduma wazee hawa wastaafu ambao hali zao siyo nzuri kwa kutumia watendaji wa kata na vijiji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, ni mshahara gani hutumika katika kutengeneza pension hizi za wastaafu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kabla ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge ninaomba nimpongeze sana kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, kwa kufuatilia jambo hili siku hadi siku. Ni mara kadhaa tunakutana ofisini kujadili suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nichukue swali lake la kwanza kama ni ushauri, hivyo ushauri wake umepokelewa, tunaenda kuufanyia kazi, kwa sababu Serikali imeona hilo na ndiyo maana tukasema tunaenda kuanzisha mfumo maalumu wa kidigitali ambao utawawezesha wastaafu kujihakiki wenyewe kupitia simu zao za mkononi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, mshahara ambao unazingatiwa wakati wa kutengeneza pension ni ule mshahara wa mwisho wa mtumishi. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mamlaka ya Mji Mdogo Nachingwea imekuwa zaidi ya miaka 10 sasa na tumefuata taratibu zote ambazo tulipaswa kufuata.

Je, Serikali ipo tayari sasa kupandisha Mamlaka ya Mji Mdogo Nachingwea iwe Mji kamili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsnate sana. Serikali ilikwishafanya tathmini ya Mamlaka za Miji Midogo kote nchini. Zipo Mamlaka ambazo zina sifa au zinakidhi vigezo vya kupanda kuwa Halmashauri, mamalaka hizo zinasubiri muda na taratibu nyingine zipandishwe hadhi kuwa Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, pia zipo Mamlaka ambazo kimsingi hazikidhi vigezo vya kuwa Halmashauri, kwa hiyo, Serikali inafanya utaratibu wa kuona hatua zaidi za kuchukua kwa zile Mamlaka ambazo hazikidhi na hazina sifa za kuwa Halmashauri na bado zipo na taarifa rasmi itatolewa na Serikali kuhusiana na hatua ambazo zitafuata. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Chinguile tutalifanyia kazi suala la Nachingwea tuone kama linaangukia kwenye category gani na hatua gani inafuata, baada ya hapo utapata taarifa rasmi, ahsante. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kwa kuwa viwanda hivi tayari vilipata wawekezaji ambao walishindwa kuendeleza kama mkataba ulivyodai, je, ni hatua gani zimechukuliwa na Serikali kwa wawekezaji hawa ambao walishindwa kufanya kazi iliyokusudiwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, zao la korosho ni zao la kibiashara na linatuingizia kama Taifa fedha nyingi za kigeni, kwa kufufua viwanda hivi vya kubangua korosho tutakuwa tunaongeza thamani ya zao lenyewe, lakini pia tutakuwa tunainua uchumi wa wakulima na kuongeza pato la Taifa. Ni mkakati gani wa Serikali kuhakikisha korosho haziuzwi zikiwa ghafi badala yake kufufua viwanda vingi vya kubangua korosho ili tuweze kuinua ubora wa zao hilo na kuongeza thamani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Chinguile kwa ufuatiliaji kuhusu uongezaji thamani wa mazao mbalimbali ikiwemo korosho katika Mkoa wa Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya hatua ambazo Serikali imechukua kwa swali lake la kwanza, ni kupitia kama nilivyosema na kufanya tathmini ya viwanda vyote ambavyo vilibinafsishwa na havifanyi kazi. Hatua ya kwanza ilikuwa ni kuvirejesha na ndiyo maana viwanda zaidi ya 20 vimesharejeshwa na vingine tunaendelea utaratibu kukamilisha urejeshwaji, zaidi ya viwanda 33 na hiyo ndiyo hatua ya kwanza kwamba wale ambao wameshindwa kuviendeleza viwanda hivi, vyote vitanyang’anywa ili tuweze kutafuta wawekezaji wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, katika hilo tunataka wale ambao sasa huenda walifanya hujuma kwenye viwanda vile ambavyo walipewa vilikuwa labda na mitambo na vifaa mbalimbali vya mashine za viwanda hivyo ambavyo either wameng’oa au wamefanya hujuma yeyote, basi nao kulingana na mikataba ile nao watachukuliwa hatua mbalimbali za kisheria kulingana na mikataba ambayo tuliingia nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la pili, ni kweli Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha bidhaa, mazao ya kilimo yanaongezwa thamani ikiwemo korosho ambayo inaingizia Serikali fedha nyingi za kigeni. Lengo sasa ni kuhakikisha korosho inaanza kuuzwa ikiwa imebanguliwa badala ya kuwa ghafi na ndiyo maana tumeanza moja, kurejesha hivi viwanda na kuvifufua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Wizara kupitia taasisi zetu, tunaandaa mashine, teknolojia rahisi ya viwanda vidogo vidogo ambavyo vitawasaidia wakulima wadogo wadogo na wajasiriamali waweze kubangua katika ngazi ya chini ili tuhakikishe tunauza korosho ambayo imebanguliwa badala ya kuendelea kuuza korosho ghafi, nakushukuru. (Makofi)