Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Asia Abdulkarim Halamga (2 total)

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ya Tanzania imeweza kusaidia baadhi ya nchi za Afrika kujikomboa katika uhuru wa nchi zao. Moja ya nchi hizo ikiwa ni Afrika ya Kusini, Angola, Zimbabwe, Msumbiji na maeneo mengine. Katika nchi yetu ya Tanzania, maeneo ambayo yalishiriki katika mkakati huo wa kuzisaidia nchi hizo ni pamoja na Kongwa, Mazimbu Morogoro, Nachingwea na maeneo mengine. Nini kauli ya Serikali kwa Mataifa haya kuhusu kuchangia maendeleo katika maeneo haya ambayo nimeyataja nchini kwetu.

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, najua swali hili una maslahi nalo kwa sababu Kongwa ni moja kati ya maeneo ambayo wanaharakati hawa wa kupata uhuru kwenye nchi zao waliishi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali na Taifa letu la Tanzania limefanya kazi kubwa sana kuhakikisha kuwa nchi zetu za Bara la Afrika zinapata ukombozi kwa kukaribisha hapa wanaharakati wao kuja kuweka mikakati ya kwenda kukomboa nchi zao na nchi nyingi zimefanikiwa. Mkakati huu ulisimamiwa sana na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye pia alikuwa na ndoto ya kuona Afrika imejitawala na tunaiona imefikiwa, Bara la Afrika kwa kweli sasa hivi kila nchi imejitawala yenyewe na inaendelea na shughuli zake.

Mheshimiwa Spika, sasa maeneo yaliyotumiwa na hawa wapigania uhuru kwenye nchi yetu ikiwemo na Kongwa kama alivyosema lakini pia Dakawa, Wilaya ya Kilosa, pale Mazimbu Morogoro hata kule Nachingwea Mkoani Lindi yametoa mchango mkubwa sana ya ukombozi wa maeneo ambayo wapigania uhuru walikuja hapa. Maeneo haya namna ambavyo yanaendelezwa hayana mchango mkubwa sana kutoka kwao lakini tunaendelea kufanya mawasiliano nao kwa utaratibu ule wa kujenga mahusiano na nchi hizi.

Mheshimiwa Spika, bado tuna mahusiano na nchi zote ambazo zimepata uhuru kwa kuwa na wapigania uhuru wao hapa nchini na wao wanatambua mchango huu ingawa mchango wa kuboresha maeneo haya si mkubwa sana kwa sababu ya kubadilika kwa vizazi kwenye nchi zao na kutambua umuhimu wa Tanzania kwenye ushiriki wa ukombozi wa nchi zao. Hata hivyo, tumeimarisha sana kwenye sekta ya kiuchumi, kisiasa lakini pia kijamii pale ambapo tumefungua Balozi kwenye nchi zao, tunayo mawasiliano na nchi nyingi zipo kwenye Jumuiya ya SADC ambayo pia tunakutana mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya viongozi wa nchi hizo wanapokuja Tanzania wanapata hamu ya kwenda kutembelea maeneo haya. Wote mnakumbuka mwaka 2020 kulikuwa na Mkutano wa SADC hapa na Mheshimiwa Rais Ramaphosa miongoni mwa Marais waliokuja, alipata nafasi ya kwenda Mazimbu na mimi niliandamana naye kwenda kuona eneo lile na akaambiwa changamoto zilizopo pale na ahadi ambazo amezitoa. Tunaamini viongozi hawa ambao bado wana kumbukumbu sahihi na kuona uthamani wa Tanzania kwenye uhuru wao wataendelea kuutambua mchango wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini na sisi tunayo namna ya kuwakumbusha, tunapokuwa na matukio tunawakumbusha na wao wakiwa na matukio yao ya uhuru wanakumbuka nchi yetu Tanzania. Ni vile utofauti sasa wa yule aliyeshiriki kwenye ukombozi namna alivyokuwa anathamini nchi yetu; wote mnakumbuka Mheshimiwa Mandela alipotoka gerezani nchi ya kwanza kuitembelea ilikuwa Tanzania, hii ni kwa sababu alikuwa anajua umuhimu wa Tanzania na uhuru uliopo sasa Afrika Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatarajia pia na Marais wengine kupitia taratibu zetu za Kidiplomasia wataendelea kuitambua nchi yetu na maeneo ambayo wamepatia uhuru kwa kuungana na maeneo hayo kuyaboresha na kuweza kuyafanya kuwa endelevu kama maeneo ya kumbukumbu kwao na sisi pia. Kwa hiyo, tunaendelea kushirikiana na nchi hizo ili kujenga mahusiano ya karibu zaidi kwa Bara la Afrika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kumekuwa na ongezeko kubwa sana la vijana nchini wenye uwezo wa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kupitia fani mbalimbali katika halmashauri zetu, kutokana na uimara wa sera. Je, ni upi mpango wa Serikali kutambua vijana hawa katika halmashauri zote nchini?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli vijana wetu sasa ndio nguvu kazi yetu. Wako vijana wabunifu na wana ujuzi, lakini wapo ambao bado hawajapata ujuzi. Serikali yetu imeandaa mkakati wa kuwawezesha vijana kitaaluma. Kupitia mpango huu, Serikali kupitia Sera yetu ya Vijana na Uwezeshaji imesisitiza na kuhamasisha vijana kushiriki katika shughuli ambazo zinaweza kuleta ujuzi, pia tumehamasisha ubunifu kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina mpango ambao sasa unatekelezwa mpaka kwenye halmashauri zetu, kuhakikisha kwamba vijana wenye ujuzi, lakini ambao hawana ujuzi kupata ujuzi. Serikali tumeendelea kujenga Vyuo vya Ufundi, ambavyo vitakuwa vinafundisha masomo mengi ili kuwapa ujuzi vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wako ambao hawajasoma, lakini ni wabunifu wameweza kubuni kazi zao. Wizara ya Elimu imebuni mfumo wa kuitisha pamoja wabunifu na kuandaa maonesho ya ubunifu, ambapo vijana na Mtanzania yoyote atapata nafasi ya kwenda kuonesha kazi yake. Hawa vijana wote wanatoka kwenye halmashauri na katika halmashauri ndiko ambako tumejenga VETA zetu ili kutoa nafasi ya karibu kwa vijana hawa kwenda kujifunza na kupata ujuzi.

Mheshimiwa Spika, ambacho kinafanywa sasa kama ambavyo Mheshimiwa Asia ametaka ni kwamba, halmashauri baada ya kuwa wamepata wabunifu inawabeba kuwapeleka kuonesha ubunifu kwenye maonesho mbalimbali. Baada ya maonesho yale, hawa wabunifu wanatambuliwa, wanawezeshwa aina ya utambuzi wao ili waweze kuendeleza ubunifu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaendelea kuziagiza halmashauri, kuendelea kusimamia ufundishaji wa taaluma zenye ujuzi ili kupata vijana wengi ambao watapata taaluma za ujuzi, pamoja na wale wabunifu ambao mtu mmoja mmoja anaweza kubuni kazi yake waziendeleze, halafu waratibiwe na kutambulika. Tutajua huyu mjuzi yuko wapi, amefanya kazi gani, aina gani na kumtafutia hata uwezekano wa kuwa na masoko pindi ubunifu huo au ujuzi huo unaweza kumuingiza kwenye masoko na maeneo mengine ya ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, halmashauri zetu ziendelee kuratibu vijana hawa kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamiii ambayo tunayo katika kila halmashauri, tuweze kuwatambua. Wale ambao wanafanya kazi ya aina moja waundiwe vikundi ili wawezeshwe kupata hata mitaji kupitia mikopo ya halmashauri au mifuko yote au Taasisi za Fedha, waweze kuendeleza ujuzi huu.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba, vijana hawa tunawaweka pamoja kwenye maeneo hayo. Nawaagiza sasa wahakikishe kwamba, kila halmashauri inakuwa na kanzidata ya kuwatambua hawa vijana ili kuwawezesha kushiriki kwenye maonesho makubwa na kuboresha kazi zao na kuwapa mitaji ya kuendeleza kazi hiyo. Hayo ndio maelezo ya swali hili. Ahsante sana. (Makofi)