Primary Questions from Hon. Asia Abdulkarim Halamga (13 total)
MHE. ASIA A. HALAMGA Aliuliza:-
Ni Halmashauri ngapi nchi zimetekeleza kwa asilimia 100 sheria ya utoaji mikopo asilimia 10 ya makusanyo ya ndani kwa makundi ya vijana, akinamama na watu wenye mahitaji maalum?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-
Mheshimwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarim Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimwa Naibu Spika, kwa mujibu wa takwimu zilizopo hali ya utoaji wa mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu katika Halmashauri nchini imeimarika hasa baada ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 yaliyofanyika Julai, 2018 kwa kuongeza Kifungu cha 37A kuhusu Mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.
Mheshimwa Naibu Spika, tangu kuanza kutumika kwa Sheria hii mwaka wa fedha 2018/2019 na 2019/2020 Halmashauri 79 zimetoa mikopo kwa asilimia 100 na Halmashauri 54 zimetekeleza kwa asilimia zaidi ya 85.
Mheshimwa Naibu Spika, utekelezaji wa shughuli hizi za mikopo umewezesha kuongezeka kwa mikopo inayotolewa na halmashauri nchini ikilinganishwa na kipindi kabla ya kufanya marekebisho ya sheria. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 (kabla ya marekebisho ya sheria) shilingi bilioni 26.1 zilitolewa; mwaka wa fedha 2018/2019 (baada ya marekebisho ya sheria) shilingi bilioni 42.06 zilitolewa; na mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya mikopo iliyotolewa ilikuwa ni shilingi bilioni 40.7 zilitolewa.
Mheshimwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kifungu namba cha 24(2) cha Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za mwaka 2019, Mkurugenzi yeyote ambaye atashindwa kusimamia utekelezaji wa Kanuni hizi atakuwa ametenda kosa la kinidhamu na mamlaka yake ya nidhamu inaweza, kwa kadri itakavyoona inafaa, kumchukulia hatua za kinidhamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naomba kutoa rai kwa Wakurugenzi wote nchini kote kuhakikisha kwamba wanazingatia takwa hilo la kisheria.
MHE. ASIA A. HALAMGA Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa muda mrefu wa kuwatambua na kulinda maslahi ya vijana waliojiajiri katika sanaa ya burudani kama Video Vixen na Video King?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, Kundi la Vijana kutoka Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Video Vixens na Video Kings ni walimbwende, wachezaji, waigizaji, wanamitindo au watu wengine maarufu ambao hushiriki kwenye Sanaa hasa katika muziki wa video (audio-visual) kwa lengo la kuiongezea mvuto kazi husika. Hawa hushirikishwa na wamiliki wa kazi husika kwa makubaliano maalum.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Na. 7 ya mwaka 1999, anaepaswa kulipwa mrabaha wa kazi ya sanaa ni mtunzi, mbunifu na mtayarishaji (producer) wa kazi ya sanaa husika.
Mheshimiwa Spika, ili kuweza kuifikia na kuivutia hadhira yake, Sanaa hii imekuwa ikiwashirikisha Video Vixen na Video Kings, Serikali ilifanya marekebisho ya Sheria hii kifungu cha 47(b) mwaka 2019 ili kuipa COSOTA mamlaka ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mikataba ya kimaslahi kati ya wenye kazi hiyo ya sanaa na vijana wetu hawa.
Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa wadau wote wa sanaa ya burudani kuishirikisha COSOTA ili maslahi yao yaweze kulindwa kupitia mikataba.
MHE. NG’WASI D. KAMANI K.n.y. MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Wakandarasi wa Tanzania wanapata fursa ya kujenga Mnara wa Mwalimu Nyerere katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika hasa ikizingatiwa kuwa Serikali ya Tanzania ndio inasimamia ujenzi wa mnara huo?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, zabuni Na. SADC/NYERERE ST/02 ilipotangazwa kati ya mwezi Mei na Julai, 2021 ilitoa fursa sawa kwa wakandarasi wote kutoka nchi Wanachama wa SADC. Serikali kupitia Baraza la Sanaa la Taifa ilichukua jitihada za kuwatangazia na kuwahamasisha wadau wote nchini kupitia Shirikisho la Sanaa za Ufundi na Idara za Sanaa za Vyuo Vikuu mbalimbali nchini ili wenye vigezo vilivyoainishwa kwenye zabuni waweze kuomba kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu wapo wakandarasi wa Kitanzania walioomba kazi hii sambamba na wenzao kutoka mataifa wanachama wa SADC. Hivi sasa SADC imekamilisha uchambuzi wa nyaraka na muda wowote mshindi atatangazwa baada ya kusaini mkataba.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaajiri wahitimu wa kada ya mazingira waliomaliza katika vyuo vikuu nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha wahitimu wa kada ya Mazingira na kada ya Afya ya Mazingira (Environmental Health Officers) wanaajiriwa ili kuimarisha jitihada za kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali ilitoa jumla ya vibali vya ajira 223 kwa kada ya Mazingira katika taasisi zipatazo 124 ambapo utekelezaji wa ajira hizo unaendelea. Aidha, katika mwaka huu wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga nafasi 73 za ajira kwa Wataalam wa Mazingira kwa ajili ya taasisi za Serikali zikiwemo Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hatua za utekelezaji wa ajira hizi zote zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu wa fedha 2022/2023.
Mheshimwa Spika, jitihada hizi ni endelevu kutokana na umuhimu wa suala la utunzaji wa mazingira ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya nchi na dunia kwa ujumla ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kutoa bima za afya kwa wafungwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdulkarim Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hakuna mpango mahususi wa bima ya afya kwa kundi la wafungwa. Katika kuhakikisha kuwa wafungwa wanapata haki yao ya msingi ya kupata huduma ya afya, Serikali imeweka utaratibu maalum wa kutoa huduma za matibabu kwa wafungwa katika magereza mbalimbali nchini kupitia vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakamilisha Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote, ambapo utakapokamilika utakuwa suluhisho la upatikanaji wa huduma za afya kwa makundi yote ya kijamii wakiwemo wafungwa. Naomba kuwasilisha.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -
Je, hadi sasa hali ya ugonjwa wa figo ipoje nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarim Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa utafiti uliofanyika hapa nchini Tanzania katika jamii ulionyesha kuwa asilimia saba ya Watanzania wanaishi na ugonjwa wa figo, ambao kwa kiasi kikubwa unahusishwa na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa sukari na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe rai kwa wananchi kupima afya mara kwa mara kwani kwa kuchelewa kutambua tatizo la afya madhara yake ni makubwa na gharama ya matitabu inakuwa kubwa.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Banio la Maji, Kata ya Endagau, Wilaya ya Hanang?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji Endagaw iliyopo katika Mkoa wa Manyara, Wilaya ya Hanang ulianza mwaka wa fedha 2021/2022. Hadi sasa Serikali imeshakamilisha ujenzi wa baadhi ya maeneo ikiwemo ujenzi wa ukuta wa bwawa wenye takribani mita 270 pamoja na punguza maji (Spillway) na baadhi ya maumbo ya mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kukamilisha ujenzi wa kazi zote zilizobaki, hii ni baada ya kukamilisha mapitio ya usanifu wa mradi huu, ikiwemo mfereji wa Onjae pamoja na maumbo yake.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana wakati wote katika hospitali, vituo vya afya na zahanati nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha dawa zinapatikana wakati wote kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, Serikali inatekeleza na kusimamia yafuatayo:-
i. Kuiwezesha MSD mtaji ili iweze kufanya kazi kama bohari ya dawa badala ya kufanya kazi kama idara ya manunuzi,
ii. Utoaji wa fedha za kununua, kutunza na kusambaza dawa kila mwezi kiasi cha shilingi bilioni 16,
iii. Kuboresha utendaji wa MSD na kuiwezesha kuwa na mikataba ya muda mrefu ya ununuzi wa dawa,
iv. Kuboresha maoteo ya bidhaa za afya na kuchukua hatua kwa upungufu unaobainika,
v. Kufunga mifumo ya kielektroniki ili kuimarisha usimamizi wa dawa na kuwezesha dawa kutolewa kulingana na wagonjwa husika,
vi. Kusimamia Muongozo wa matibabu katika kuhakikisha dawa zinazonunuliwa, kutunzwa na kuandikwa na Madaktari zinazingatia muongozo wa matibabu,
vii. Kudhibiti mianya ya upotevu na wizi kwa kuwa na kaguzi za mara kwa mara ili kuhakikisha dawa zinakuwepo vituoni,
viii. Kuanzisha maduka ya dawa ya hospitali za umma yatakayokuwa na dawa muda wote kwa ajili ya wagonjwa wa ndani na nje ya hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuzielekeza Halmashauri na viongozi wote wa vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha wanatumia zaidi ya asilimia 50 ya mapato yao kununua dawa na bidhaa nyinginezo za afya.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha kwa ajili ya kumalizia Miradi ya Afya iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mchango wa wananchi katika ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya kote nchini. Aidha, Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati nchi nzima katika kila jimbo. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali ilitenga fedha Shilingi bilioni 27.75 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati 555 ambapo jumla ya Shilingi bilioni 26.95 zilitolewa na Serikali kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya shilingi bilioni 38.2, zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha maboma ya zahanati 763 yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi ambapo maboma 564 yanakamilishwa kwa fedha ya ruzuku ya Serikali na maboma 199 kwa fedha za halmashauri mapato ya ndani, ambapo jumla ya fedha shilingi bilioni 30.98 zimekwishatolewa mpaka sasa, ikijumuisha shilingi bilioni 26.92 ruzuku ya Serikali na shilingi Bilioni 4.06 mapato ya ndani ya halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati 300.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdulkarimu Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa jengo la Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Manyara ulianza mwaka 2012 kwa kutumia Mkandarasi aitwaye MS Mavonda’s Co. Ltd kwa gharama ya shilingi 862,167,729. Ujenzi huo ulipofikia asilimia 65 zilijitokeza changamoto katika kutekeleza mkataba hali iliyosababisha kuvunjika kwa mkataba huo mwezi Agosti, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga kukamilisha utekelezaji wa mradi huo kwa utaratibu wa nguvu kazi kwa maana ya Force Account ambapo taratibu zote zimekamilika na tayari kiasi cha fedha shilingi 353,986,150 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo zimepokelewa kutoka Hazina. Ujenzi wa jengo hilo unatarajia kukamilika mwezi Oktoba, 2022. Nashukuru.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuwaajiri vijana wa JKT walioshiriki ujenzi wa ukuta wa Mererani, Ikulu na maeneo mengine?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa mwaka 1963 kwa lengo la kutoa mafunzo ya uzalendo, ulinzi na malezi kwa vijana wa Kitanzania. Mafunzo hayo, yanalenga kuwafundisha umoja na mshikamano, ukakamavu na kuwa tayari kulitumikia Taifa lao wakati wote. Katika mafunzo hayo, vijana hufundishwa pia stadi mbalimbali za kazi na maisha. Lengo ni kuwawezesha vijana hao kuwa na uwezo wa kujitegemea baada ya mafunzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania huandikisha askari wapya kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo yanayotolewa mara kwa mara, kama ilivyofafanuliwa katika kanuni ya tano ya Kanuni za Majeshi ya Ulinzi, Juzuu ya Kwanza ya Utawala. Hivyo, vijana wote wanaojiunga na JKT huandikishwa kwa kufuata utaratibu. Hapa wanaojiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, wanaoandikishwa, huandikishwa kwa kufuata utaratibu huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2022, jumla vijana 5,744 waliokuwa na sifa ikiwa ni pamoja na wale walioshiriki katika ujenzi wa ukuta wa Mererani na Ikulu waliandikishwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kufuata utaratibu niliouelezea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka huduma ya Mawasiliano Kata ya Simbay - Hanang’?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeainisha changamoto ya mawasiliano katika Kata ya Simbay (Kijiji cha Simbay) na utekelezaji wa mradi huu utafanyika kwa kadri ya fedha zitakapopatikana. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani kuwapa Vitambulisho vya Taifa wafungwa pamoja na mahabusu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarim Halamga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kusajili na kutambua watu waliopo katika makundi maalum ikiwemo wafungwa na mahabusu ni kupitia maombi maalum kutoka kwa Wakuu wa Gereza katika wilaya husika. Uratibu wa usajili wa makundi hayo unafanywa na NIDA kupitia Wakuu wa Magereza na Maafisa Usajili wa Wilaya husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa baadhi ya wafungwa na mahabusu wamekwisha kusajiliwa walipokuwa uraiani kabla ya vifungo vyao, Serikali kupitia NIDA ipo tayari kufanya usajili na utambuzi kwa watu wote waliokidhi vigezo ikiwemo wafungwa na mahabusu kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza. Ahsante.