Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Asia Abdulkarim Halamga (70 total)

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza kwa kuwa Barabara ya Rujewa – Madibira inafanana na ile barabara ya Arusha – Simanjiro – Kiteto pamoja na Kongwa kilometa 430 ambayo imeahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 - 2025 pamoja na hotuba ya Mheshimiwa Rais. Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jibu langu la msingi na bado natambua kwamba, barabara anayoulizia, kama mwenyewe alivyosema, iko kwenye ilani lakini pia iko kwenye ahadi ya Rais, lakini pia iko kwenye hotuba ya Rais.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, barabara hiyo pia, kadiri Serikali itakavyoendelea kutafuta na kadiri fedha zitakavyopatikana ni kati ya barabara ambazo tunategemea kuzikamilisha ili tuweze kuunganisha wilaya zote, mikoa yote kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali tayari Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba halimashauri 85 hazijaweza kutekeleza kwa asilimia mia moja utoaji wa mikopo. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuanzishwa kwa benki ya vijana ili iweze kusimamiwa na vijana wenyewe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali ina mpango gani juu ya kuwakopesha vijana mmoja mmoja kwa sababu vijana wengi wanaopewa mikopo hii haiendi kuwanufaisha kwa kuwa mawazo yanakuwa tofauti? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asia Abdukarim Halamga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tumeona tangu kuanzishwa kwa mpango huu wa mikopo asilimia kumi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kazi ya ukopeshaji katika ngazi ya halmashauri katika miaka mitatu iliyopita imeongezeka zaidi ya mara tatu. Kwa hivyo, kwa hatua hii bado Serikali inaendelea kutekeleza vizuri, lakini ni kweli kwamba bado kuna changamoto kwenye baadhi ya halmashauri kutokana na uwezo wa ukusanyaji wa mapato na ndiyo maana Serikali imeendelea kusisitiza halmashauri kuboresha vyanzo vya mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na wazo la Mheshimiwa Mbunge kuanzisha benki ya vijana, naomba tulichukue kama Serikali, tukalifanyie tathmini na kuona njia bora zaidi ya kulitekeleza. Kuhusiana na mikopo ya vijana kwa maana kijana mmoja mmoja, pia ni wazo la Mheshimiwa Mbunge na sisi ni kazi yetu kuchukua mawazo ya Waheshimiwa Wabunge, kuyatathmini, kuyafanyia kazi na kuona uwezekano wa kutekeleza hilo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inapokea mawazo hayo na tutakwenda kuyafanyia kazi na kuona njia bora zaidi ya kuyatekeleza.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo majibu ya Serikali yameweza kukiri kwamba, mfumo wa sasa wa elimu bado haujakuwa suluhisho la vijana wengi wanaomaliza na kwenda kujiajiri wao wenyewe.

Je, ni lini hasa Serikali itakamilisha mchakato wa mabadiliko haya, ili tuweze kwenda na mfumo kama ambavyo Serikali imeweza kukiri kwamba, hatuko kwenye mfumo wa kidunia, hatujaweza kukimbizana nao?

Je, Serikali ni lini itakamilisha mchakato huo ili kuwasaidia vijana wengi wanaotoka kwenye shule waweze kwenda kujiajiri wao wenyewe? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi kwamba, sasa tuko katika mjadala wa kitaifa wa kuhakikisha kwamba, tunaboresha mitaala yetu hii, ili kuingiza stadi za kazi, lakini vilevile kuingiza mambo yote yanayoonekana ni muhimu kuhakikisha kwamba, tunajenga umahiri wa vijana wetu. Mchakato huo tumeanza na tumeanza katika Mkoa wa Dar es Salaam, lakini vilevile tulifanya mjadala mpana hapa Dodoma na tuna website ya kuhakikisha kwamba, tunakusanya maoni hayo.

Mheshimiwa Spika, tutaendelea na mchakato huu wa kukusanya maoni. Na ndani ya mwaka huu wa fedha tunakadiria au tunakusudia kuhakikisha mchakato huu uweze kukamilika, ili tuweze kupata mitaala ile ambayo nchi yetu inayohitaji. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nitumie nafasi hii kushukuru majibu mazuri sana ya Serikali. Swali langu la nyongeza;

Je, Serikali ina mpango gani wa kutambua kundi la Video Vixens kama makundi mengine ya sanaa kupitia Sheria Na. 7 ya Mwaka 1999; kwa sababu Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba tayari kundi hili halitambuliki rasmi bali kundi linalotambulika ni kundi la wanamuziki; na kwamba mikataba ya watu hawa haitambuliki, kwamba inayotambulika ni ya kundi la wanamuziki pamoja na makundi mengine, na siyo kundi la Video Vixens? Je, kupitia Sheria hiyo Na. 7 ya Mwaka 1999 tunawasaidiaje vijana hawa kuweza kutambulika?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa kundi la Video Vixens ambalo linachukua Video Kings pamoja na Queens, na kwamba ni kundi linalochukua vijana wengi zaidi; sasa Serikali haioni haja ya kuwasaidia kuwatengenezea mikataba mizuri ili vijana hawa wasipitie changamoto wanazozipitia; kwa sasa hivi kwa sababu wanafanya kazi kubwa lakini wanalipwa ujira mdogo na wananyanyasika?

Nikisema wananyanyasika nadhani Waheshimiwa Wabunge tunaelewana. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asia kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwenye majibu yangu ya awali na ya msingi nilieleza kwamba kwenye Sheria yetu ya Mwaka 1999 vijana hawa walikuwa hawajatambuliwa, lakini kwa sababu ya umuhimu wa kazi yao; ilibidi sheria hii tuirekebishe mwaka 2019, Kifungu na. 47(b) ndicho kikatambua sasa ikaingiza mkataba, kwamba ni lazima hawa vijana ambao wana-perform na wale owners wa kazi ile waweze kutambuliwa, na mikataba yao COSOTA iiangalie.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilihakikishie Bunge lako Tukufu na wasanii kwamba hawa vijana hawajaachwa, sheria inawatambua. Na hata pale ambapo vijana hawa wanadhulumiwa COSOTA inaingilia kati kwa sababu ile mikataba inakuwa imeshapitia kwao. Mimi niwahakikishie kwamba wakati tunafanya marejeo ya kanuni maoni yamechukuliwa kote na hatujapata malalamiko so far kwamba wanaonewa.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa kuendelea kuwalinda kwa sababu – swali lake la pili – tunapitia Kanuni yetu ya mwaka 2003 kuona jinsi gani tuboreshe mpaka hata mgawanyo tunaotoa wa fedha kwa wamiliki au wasanii wetu; maana kama kuna jambo lolote within marekebisho yale Mheshimiwa Mbunge, yatakwenda kuangaliwa wakati Kanuni hiyo haijafika mwisho, maana wana nafasi ya kutoa tena maoni yao.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa barabara hii ya Mtwara inafanana kabisa na ahadi ya Serikali kupitia Ilani ya Uchaguzi katika barabara ya kujengwa kwa kiwango cha lami kuanzia Babati kupitia Sukuru – Olkasmenti - Simanjiro – Kibaya, Wilaya ya Kiteto. Je, Serikali ni lini itaanza ujenzi wa barabara hii ili kurahisisha huduma kwa wananchi wa Manyara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA
M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, Mbunge wa Vijana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tu kwamba kazi inaendelea ilikwishaanza baadhi ya barabara tathmini imekamilika na ujenzi unaendelea. Zile barabara ambazo hazikufanyika mwaka wa fedha 2020/2021, zimewekewa mpango mkakati wa bajeti ijayo 2021/2022. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge wa Vijana, Mkoa wa Manyara, watu wa Manyara wasiwe na wasiwasi mpaka Simanjiro, tutatekeleza Ilani ya Uchaguzi kama ilivyoelekezwa na kama ambavyo ndio maagizo ya Viongozi wetu Wakuu hasa Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa ahadi hii ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara kule Kakonko inafanana kabisa na ahadi ya Mheshimiwa Rais katika barabara ya Boay – Gidas hadi Getasam, Wilaya ya Hanang, lakini barabara ya Boay –Gidas, barabara ya Babati Vijijini: Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi huu wa barabara kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Spika, kwa sababu, sasa hivi barabara hiyo imekuwa ni chakavu kabisa na haiwezi kupitika: Je, Serikali inatuahidi nini hata kutusaidia kwa kiwango cha changarawe? Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ambacho amejaribu kukiainisha Mheshimiwa Mbunge; ni lini Serikali itaanza kukamilisha ahadi za Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na Marais wote waliotangulia na hapa amejaribu kuainisha barabara katika maeneo ya Hanang na Babati Vijijini.

Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie kwamba mpaka sasa hivi Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Serikali kwa ujumla tumeanza mchakato wa kuziainisha ahadi zote zilizotolewa na viongozi wakubwa nchini. Baada ya hapo tutazifanyia tathmini, tutazitenga katika mipango yetu na kuziwekea bajeti ili kuhakikisha kila ahadi ambayo kiongozi mkubwa aliahidi inatekelezwa na kwa wakati ili kuhakikisha kwamba tunawasaidia wananchi, hususan maeneo yale ambayo yana-involve sana uzalishaji mkubwa kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Wilaya ya Hanang wanategemea sana kilimo katika masuala mazima ya uchumi. Lakini katika kilimo hiki tunategemea sana shamba letu kubwa, shamba la NAFCO ambalo kwa sasa lina mwekezaji. Shamba lile lina hekari takriban 40,000. Mwekezaji analima asilimia 20 na eneo analoliacha wazi anawanyanyasa sana wananchi. Je, Serikali inatuambia nini juu ya kurudisha shamba lile Serikalini au kuwagawia wananchi ili tuweze kuingiza kipato katika Serikali na kwa mwananchi mmoja mmoja. Ahsante sana kwa kunipatia nafasi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Halamga na Mheshimiwa Mbunge wa Hanang kwa ufuatiliaji wa eneo ambalo lilibinafsishwa kwa Kampuni ya Ngano Limited. Lile eneo kwa mujibu wa sheria alibinafsishiwa huyu bwana na alilinunua. Sisi kama Wizara ya Kilimo pamoja na Waziri wa Kilimo tumekutana naye na wawakilishi wake na tumefanya nao mkutano. Tumewapa ultimatum ya mwaka mmoja na wao wanafahamu kwamba wasipotekeleza makubaliano tuliyofanya na wao, Serikali itachukua hatua ambazo tumekubaliana nao wao. Kwa hiyo, tuwaombe wananchi wa Wilaya ya Hanang kuweni na Subira. Tumeanza safari ya ngano pamoja na mmeona matokeo na sasa tuwaahidi, tatizo la ngano limited linaenda kuisha.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Serikali ina mpango gani wa kuutangaza utalii wa ndani kwa kutumia Wabunge pamoja na Halmashauri zetu? Naomba kuwasilisha. (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nimpongeze Mheshimia Asia kwa swali lake hilo zuri pia nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango mkakati kabisa wa kushirikiana na Halmashauri zote na Serikali za Mikoa na Wilaya katika kutangaza Utalii ikiwemo kuwatumia Wabunge pia katika kutangaza utalii. Ni wazi umeona tayari Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na baadhi ya Wabunge tumeshaanza kushirikiana nao kuhakikisha kwamba tunatangaza utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiongezea kwenye majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwamba maelekezo ya Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli yalikuwa ni kwamba tupunguze gharama za utalii ili kuwezesha Watanzania wengi zaidi na watalii wengi zaidi kwenda kwenye sehemu za vivutio vya Utalii, zoezi hili tumeshalianza tunaamini gharama hizo zitashuka na Watanzania waweze kufaidi maliasili zao. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali.

Serikali imekamilisha mradi wa maji katika Mji wa Kateshi mradi wenye thamani ya shilingi bilioni 2.5 lakini mpaka sasa mradi huo haujaanza kufanya kazi.

Je, ni lini Serikali itaanza kusambaza maji ili wananchi wa mji wa Katesh lakini maeneo ya Mogito ambayo chanzo kimeanzia pamoja na maeneo mradi unapopita watanufaika na maji haya katika miji hii na kata hizi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mradi wowote ukishakamilika sisi kama Wizara tunapenda kuona maji yanawafikia wananchi kwenye vituo vya kuchotea maji, hivyo mara miundombinu yote itakapokamilika maji mara moja yataanza kutoka katika mradi huu wa Katesh. Tunafahamu tumeshatumia fedha nyingi za Serikali ambazo ni jasho la wananchi, hivyo hatuko tayari kuona fedha imeshatumika halafu kile tunachokitarajia kisipatikane. Pia niendelee kukupongeza Mheshimiwa Asia mwendo wako ni mzuri wewe unawakilisha vizuri vijana na sisi kama Wizara hatutakuwa kikwazo kuona kwamba unafika mbali. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi naomba kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mji Mdogo wa Matui Wilaya ya Kiteto una wakazi wengi na unaendelea kukua kwa kasi.

Nini kauli ya Serikali juu ya upatikanaji wa uhakika wa maji safi na salama kwa wananchi wa Matui pamoja na viunga vyake?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Mbunge wa Viti Maalum vijana kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya ya Matui huko Kiteto nayyo ni miongoni mwa maeneo ambayo Wizara imetoa jicho la kipekee kabisa. Tunafahamu kuwa ni maeneo ambayo watu wameongezeka sana, hivyo mwaka ujao wa fedha kila eneo tutalitupia jicho, na kwa eneo hili la Matui pia tutalipa kipaumbele.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Sibiti hadi Hydom kwa kiwango cha lami kwa sababu tayari ipo kwenye bajeti? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyouliza Mheshimiwa Flatei ndio mwendelezo wa barabara kutoka Hydom kwenda Daraja la Sibiti. Ni barabara ambayo inafanya kama kilomita 300 na kitu ambayo inaanzia Kolandoto, Lalago, Sibiti, Hydom, Mbulu hadi Karatu. Tayari tumeshaanza ujenzi, kwa maana ya daraja na kilomita zake takriban 25; na kwa hiyo kadri tutakavyoendelea kupata hela barabara hii tutaiunganisha yote kuwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto kubwa katika Mkoa wa Manyara ya upandishwaji wa gharama za umeme kutoka kwa wananchi kutoka unit zero mpaka kupelekwa unit one. Changamoto hiyo imetokea wananchi walikuwa wanalipa umeme wa shilingi 5,000 wanapata unit 41, na kwa sasa hivi wananchi wakinunua umeme shilingi 5,000 wanapata umeme unit 14; na Wilaya zilizoathirika ni Wilaya za Hanang, Mbulu, Babati, Simanjiro kwa ujumla wake mkoa mzima wa Manyara.

Nini kauli ya Serikali juu ya kuwapa umeme kwa bei ya kawaida wananchi wa Manyara ili waweze kujiinua kiuchumi na wasilale giza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Taifa Vijana kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba gharama za umeme ziko juu hata hizo zinazosemwa ni ndogo sisi bado tunaziona ziko juu. Nia ya Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha umeme unakuwa wa gharama nafuu na kila mmoja anaweza kuupata kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi pia na ya kijamii.

Mheshimiwa Spika, tariff tunazozitumia sasa zilitengenezwa mwaka 2016 na EWURA ndiyo msimamizi wa gharama za utoaji wa umeme kwa watu mbalimbali. Sasa naomba nieleze kinachotokea; zile tariff, ile kanuni ya gharama inasema mtu anayetumia unit sifuri mpaka unit 75 atakuwa-charged shilingi 100 kwa unit moja, yule anayetumia zaidi ya unit 75 na kuendelea gharama zake ni shilingi 200 hadi 350 kulingana na yuko kwenye tariff I, tariff II au tariff III.

Sasa kuna kifungu kwenye kanuni ile kiliwekwa kwamba wananchi wote wanaotumia umeme wakiwa maeneo ya vijijini wapate gharama hiyo ya unit moja shilingi moja na wanaozidi 75 waendelee kwingine. Wale ambao sio wa maeneo ya vijijini hawapati nafuu ya punguzo hilo la gharama.

Mheshimiwa Spika, lakini baada ya kuona kwamba kanuni hizo zilitengenezwa kipindi ambacho kulikuwa na shida sana ya upatikanaji wa umeme wa gharama nafuu kwa maana ya kutumia mafuta mazito na mitambo mingine, lakini sasa tuanzalisha umeme kutoka kwenye maji ambako ni nafuu, tunayo gesi yetu ya kutosha kabisa kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Mheshimiwa Spika, tumekubaliana na wenzetu wa TANESCO, wakae chini, wa-review hizo gharama za kuuza umeme ili tuweze kupata umeme mwingi zaidi na tukauuza kwa gharama ndogo.

Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Asia pamoja na Waheshimiwa wengine watuvumilie kidogo, tuko katika mapitio mazuri kabisa ya kushusha gharama za kuuza umeme na kila mmoja atapata gharama hiyo ya umeme nzuri kabisa kwa ajili ya maendeleo kwenye maeneo yetu ya mijini na maeneo ya vijijini ili ile nia ya uwekezaji ambayo Mheshimiwa Rais anaitaka kwa Watanzania wote iweze kufikiwa kwa kila mmoja. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa Wilaya ya Hanang’ ni wakulima wakubwa sana wa kilimo cha ngano na wanalima haswa, shayiri na waliingia mkataba na TBL kwa kipindi kirefu juu ya kuwapa mbegu lakini baadae kuwauzia. Kwa hiyo, kuwa na soko la uhakika lakini pia upatikanaji wa mbegu wa uhakika. Mpaka sasa TBL imekaa kimya kwa wakulima na wakulima wamekuwa na taharuki kubwa kwa sababu, msimu umefika na TBL wamekaa kimya.

Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya kuwaondoa hofu wakulima wa shayiri wa Wilaya ya Hanang’? Tunaomba majibu ya Serikali. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halamga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kauli ya Serikali. TBL hana excuse yoyote kuondoa mfumo wa contract farming wa zao la shayiri. Mwaka jana walitaka ku-withdraw tulikaa nao tukasaini nao makubaliano na walinunua jumla ya tani 8,000 kutoka katika maeneo yenu na leo nimeongea na management ya TBL mimi mwenyewe baada ya kupigiwa simu na Mkuu wa Wilaya watarudi kununua. Kwa sababu, mahitaji yao yote ya incentive package waliyotaka kwa ajili ya kujenga kiwanda hapa Dodoma Serikali imewapatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie Bunge lako hili Tukufu kuwaambia TBL warudi wakasaini mikataba na wakulima wa Kanda ya Kaskazini kwa ajili ya zao la shayiri kwa sababu, kilio chao Serikali ilisikiliza na tuliwapatia incentive package walizotaka na watapata msamaha wa kodi, tofauti na mzalishaji yeyote wa kinywaji wanachozalisha atakayeagiza shayiri kutoka nje. Hatutoruhusu kuagiza shayiri kutoka nje kabla ya shayiri ya ndani ya nchi kununuliwa. Huu ndiyo msimamo wa Serikali. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Tarafa ya Simbayi na Tarafa ya Basuto katika Jimbo la Hanang tuna changamoto kubwa sana kwanza ya umbali na hakuna gari la wagonjwa; je, ni lini Serikali sasa itapeleka magari ya wagonjwa katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga, Mbunge wa Viti Maalumu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tarafa hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja alikwishazileta na pia kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge Hhayuma wamekuwa wakishirikiana kwa karibu sana na kuona wananchi wa Hanang wanapata huduma hizi na nimhakikishie tu kwamba Mheshimiwa Mbunge tumeshafanya tathinini ya kuona uwezekano wa kupeleka la wagonjwa lakini gari moja la wagonjwa jipya litaletwa Hanang ili muweze kupeleka katika tarafa hizo, ashante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vya Kata ya Kiru na Magara, Jimbo la Babati Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, umeme vijijini katika eneo alilolitaja utakamilika mwezi Desemba, Mkandarasi wa Giza Cable Industries Limited ambaye anapeleka umeme katika Mkoa wa Manyara, anaendelea na kazi na tutaendelea kusukumana naye ili akamilishe kazi kwa wakati.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga Minara ya simu katika Kata ya Makame na Raiseli katika jimbo la Kiteto?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halanga, Mbunge Viti Maalum Manyara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kwelli kabisa kuna changamoto ya Mawasiliano katika jimbo la Kiteto. Na bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto, ndugu yangu wakili msomi Olelekaita pamoja na Mheshimiwa Asia, kwa kweli tunashirikiana vizuri sana na wao katika kuhakikisha tunatatua changamoto hii. Bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge anafahamu kabisa kuwa orodha ya vijiji vyake vyote vipo kwenye bajeti ya mwaka huu. Hivyo niwaombe Waheshimiwa Wabunge wa Manyoni pamoja na Kiteto, tuhakikishe kwamba tunashirikiana katika kutoa maeneo ili kukamilisha ujenzi wa miradi hii. Ahsante sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa changamoto iliyoko Busega inafanana kabisa na changamoto iliyoko Wilaya ya Kiteto: Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za ujenzi wa vituo vya afya katika Tarafa zifuatazo: Tarafa ya Dosidosi, Tarafa ya Makame pamoja na Tarafa ya Kibaya? Ahsante sana kwa kunipa nafasi.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, yeye ameomba kwamba, vituo vitatu katika Tarafa tatu ambazo ameziainisha hapo.

Mheshimiwa Spika, unatambua kabisa kwamba Serikali ya Awamu ya Sita, moja ya kazi kubwa ambayo tumeifanya sasa hivi ni kuhakikisha Tarafa zote ambazo hazikuwa na vituo vya afya, tumepeleka fedha na ujenzi unaanza.

Kwa hiyo, miongoni mwa maeneo ambayo ameyataja, zipo baadhi ya Kata, sehemu ya hizi Tarafa alizozitaja, tumepeleka vituo vya afya na ujenzi unaendelea. Kwa hiyo, nimwondoe shaka kwamba hivyo vituo vitakamilika na tutaleta na vifaa tiba ili kuhakikisha wale wananchi wanapata huduma ya afya kama ambavyo Serikali imekusudia. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza; je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Skimu ya Kata ya Endagaw ilhali tayari ilishatoa zaidi ya shilingi milioni 800 na bado haijaanza kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Skimu aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge ipo katika utekelezaji wa Bajeti ya mwaka huu, zoezi la utekelezaji linaendelea.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano katika Vijiji vya Katesh, Endagulda pamoja na Yaeda Jimbo la Mbulu Vijijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Manyara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Katesh, Endagulda pamoja na Hhayeda ambayo yanatoka katika Jimbo la Mheshimiwa Flatei Massay, kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Asia Halamga kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kufuatilia katika Mkoa wa Manyara, kuhakikisha kwamba huduma ya mawasiliano inaimarishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, maeneo yote haya yote matatu ambayo ameyataja Mheshimiwa Asia Halamga tayari tumeyaingiza katika mradi wetu wa minara 763.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza, nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya kuweza kuwavutia wawekezaji.

Je, nini mpango wa Serikali katika kuajiri watumishi wa kada ya mazingira katika miradi yote mikubwa ambayo inatekelezwa na Serikali?

Swali langu la pili; je, kwa kuwa nchi yetu kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya tabia nchi, kwa mwaka huu wa fedha, Serikali imepanga ajira ngapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Asia Halamga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa amekuwa hodari sana kufuatilia masuala mbalimbali ya ajira za kada mbalimbali ambazo zinahusu mkoa wake na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la kwanza la je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri watu kwenye miradi hii mikubwa; Niseme tu kwamba Serikali inaajiri kwa kuzingatia ukomo wa bajeti kama ambavyo inaidhinishwa na Bunge lako hili Tukufu. Kwa hiyo, tutaendelea kuzitenga kwenye bajeti na kuleta hapa Bungeni kuona namna gani nafsi hizi zitaongezwa Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili:Je, Serikali ilitenga jumla ya ajira ngapi? Kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga jumla ya ajira 30,000 kwa kada zote na taasisi mbalimbali za Serikali nchini na hiyo pia kama nilivyojibu katika jibu langu la nyongeza la kwanza kwamba ni kutokana ukomo wa bajeti ambao tulipatiwa. Hata hivyo tutaendelea kutenga na kuona namna gani tunaweza kuangalia hizi kada zote zikapata watumishi wa kutosha.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, kwenye jibu lako unasema ajira ambazo Serikali ilitoa vibali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ajira 223 utekelezaji bado unaendelea. Ni kwamba wale waombaji hakuna, au yaani mwaka ule uliopita kipindi kile mpaka sasa hivi bado mnaendelea au kuna changamoto kwenye sekretarieti ya ajira?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, Hapana, siyo kwamba kuna changamoto kwenye sekretarieti ya ajira, lakini hizi nafasi zote 223 zinatokana na taasisi mbalimbali za Serikali. Kwa hiyo, sekretarieti ya ajira inaanza mchakato pale tu zile taasisi zilizoidhinishiwa vibali vyao vya kuajiri zinapoanza mchakato wao kupeleka sekretarieti ya ajira. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana ni Asia Halamga, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Naibu Waziri amewahi kuja kukagua eneo la ujenzi wa uwanja wa ndege lililopo kata ya Mwada eneo lenye takribani ya hekari 600 na halina mgogoro wowote.

Je, ni lini Serikali sasa italeta fedha kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli uwanja huu utajengwa eneo linaloitwa Mwaga na sasa hivi tunavyoendelea ni kwamba tuko kwenye hatua ya utwaaji wa eneo hilo na pia lilikuwa ni agizo la Mheshimiwa Makamu wa Rais wakati anafungua daraja la Magala kwamba kazi hiyo ifanyike haraka. Kwa hiyo Serikali tuko tunaendelea kulifanyia kazi tuweze kutoa na kuwalipa fidia halafu ujenzi uanze.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Umeme Wilaya ya Hanang kwa kuwa kwa sasa kituo kinachotumika ni cha Babati na hivyo inaendelea kuleta changamoto kubwa kwa watumiaji wa umeme ndani ya Wilaya ya Hanang?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilifanya utafiti na kubaini maeneo yanayohitaji Vituo vya Kupoza Umeme na vimetengwa katika awamu tatu. Kuna wale ambao wana mahitaji makubwa sana tumewaweka kwenye group la kwanza; kuna wale ambao mahitaji yao kidogo yanaweza kuvumilika wako group la pili; na kuna wale amabo wananaweza wakasubiri mpaka baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mradi ambao niliotangulia kuutaja wa Grid Imara ambao unakaribia jumla ya trilioni moja na bilioni 900 unatekelezwa kwa miaka minne. Kwa kuanzia tumepewa bilioni 500 na tutajenga Vituo vya Kupoza Umeme 15 katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda kuangalia kama eneo la Hanang ni eneo mojawapo ambalo limeoneka lina uhitaji wa kituo cha kujengwa haraka namna hii au kitakuja baadaye kidogo. Hata hivyo, nitoe taarifa njema kwa Waheshimiwa Wabunge, mradi huu utakapokamilika 2025/2026, tunatarajia kila wilaya itakuwa ina Kituo cha Kupoza Umeme cha Gridi katika wilaya husika ili kuzuia waya kuitembea kwa muda mrefu na hivyo umeme kupotea.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Jengo la Polisi Mkoa wa Manyara kwa kuwa takribani ni miaka 10 sasa lipo katika hatua ya msingi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum Manyara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli nasi tumebaini kwamba jengo hilo limekaa muda mrefu na lilikuwa halijapangiwa bajeti lakini nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika bajeti ya mwaka 2023/2024, Jeshi la Polisi limeweka kituo hicho katika mpango wake wa ujenzi.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa kumekuwa na changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa mbegu za shayiri. Je, Serikali haioni sasa haja ya kuanzisha kituo cha uzalishaji wa mbegu katika shamba la NAFCO lililoko Wilaya ya Hanang?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba tu kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba shamba la Bassotu kama Wizara, tunaligeuza kuwa ni center of excellence kwa ajili ya kuzalisha ngano na shairi.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mwongozo huu ulitoka mwaka 2019 na sasa ni mwaka 2022; je, Serikali imefanya tathmini na kugundua changamoto zipi juu ya mwongozo huo, na nini majibu ya Serikali baada ya kugundua changamoto zilizopo katika mwongozo huo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; ni lini Serikali itakamilisha uandaaji wa Sera mpya ya Elimu ya Sekondari ili kumpunguzia kijana wa Kitanzania mzigo wa kukaa muda mrefu shuleni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asia kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tunakumbuka Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Aprili, 2021 akihutubia Bunge hili tukufu alituagiza Wizara ya Elimu kuweza kufanya mapitio ya sera, sheria pamoja na mitaala yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi hilo ndilo ambalo linaendelea hivi sasa na katika mapitio haya ya sera, sheria pamoja na mitaala, suala la miongozo hii kufanyiwa tathmini nalo limeingizwa ambapo tutafanya tathmini ya kina kuona namna gani miongozo hii tunaweza kuirekebisha kulingana na wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, anauliza muda gani tutatumia; naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa mpaka kufika mwaka wa fedha ujao tutakuwa tumekamilisha utaratibu wa mapitio ya sera, sheria pamoja na mitaala hii ili iweze kuanza kutumika. Nakushukuru sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kutenga shilingi 1,140,000,000 kwa ajili ya kujengwa shule 57 katika Jimbo la Kiteto.

Je, Serikali ni lini itaharakisha sasa usajili wa shule hizi ili wananchi waweze kupata huduma kama ambavyo nia ya Mheshimiwa Rais imeweza kulenga kutatua changamoto?

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kufuatana na Mbunge wa Jimbo la Kiteto ili kwenda kuona hali halisi ya vituo hivi ambavyo vinajengwa kwa sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha kwanza kabisa niseme kwamba napongeza kazi nzuri anayoifanya, na nimhakikishie tu kwamba Serikali ipo tayari kusajili shule zote ambazo zimekamilika na maeneo yote ambayo yanahitaji. Kwa hiyo, wayafuate tu yale maelekezo ambayo tumeyatoa na sisi tutazisajili.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo pamoja na Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kuhakikisha tukajionee hizo kero za wananchi. Ahsante sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuulizwa swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzuia simba na tembo wanaoharibu mazao pamoja na mifugo katika Kata ya Magugu pamoja na Vilima Vitatu Jimbo la Babati Vijijini pamoja na Jimbo la Kiteto? Ahsante.
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika Kijiji cha Magugu tulikuwa na changamoto ya simba ambayo sisi tuliiona ni changamoto ngeni sana kwa sababu tumezoea ni tembo, mamba na viboko; lakini tulipeleka askari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto tunayoipata ni kwamba hawa wenyeji baada ya kuonesha kwamba mipaka ya hifadhi inakuwa maeneo fulani wenyeji wanasogea karibu sana wanaweka mazizi kando kando ya hifadhi. Sasa Simba anapotoka cha kwanza anaona kitoweo kiko karibu, kwa hiyo ‘mimi niwaombe wananchi wanaoishi maeneo hayo kwamba tunapoweka kando kando ya hifadhi beacon hii unaweka zizi la ng’ombe hapa. Na hili limekuwa ni changamoto kubwa kwa sababu hao hao wanatega ikifika maeneo kadhaa basi anaingiza hata ng’ombe hifadhini anaweza wanapata chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niwaombe wafugaji, kwamba kuweka zizi kando kando ya hifadhi ni kuleta hatarishi ya wanyama wakali kusababisha kuliwa hii mifugo na wanyama hatarishi kama simba. Lakini tumeendelea kutoa ushirikiano na askari wataendelea kuwepo katika maeneo hayo ili kudhibiti simba wanaotamani kula mifugo.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kata ya Endago ya Wilaya ya Hanang ina wakazi zaidi ya 5,600 lakini haijawahi kuwa na Kituo cha Afya wala Zahanati. Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya afya katika Kata hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Kata hii ina idadi kubwa ya wananchi zaidi ya 5,000 lakini haina zahanati. Nimhakikishie kwamba tunaweka mpango wa kutafuta fedha kwenda kujenga zahanati katika eneo lile, ikibidi tunaweza tukaona uwezekano wa kujenga Kituo cha Afya baada ya tathmini kuona inakidhi vigezo. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kutoa huduma ya afya bure kwa wafungwa, lakini kwa kuwa Waziri amekiri kwamba, suluhisho la matatizo yote ya afya ni kupitishwa kwa muswada wa bima ya afya;

Je, changamoto wanazokutananazo kwa sasa wafungwa juu ya huduma za afya, Serikali haioni haja ya kukaa na kupitia utaratibu ambao imeuweka kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, lakini nianze kwa kusema kwanza ni wakati muafaka sisi Wabunge na sisi viongozi wote kujirudi na kutafakari kwa makini muswada wa bima ya afya kwa watu wote, moja hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa leo tu ukienda pale Mirembe wako wafungwa wa namna hiyo zaidi ya 270 na wanahudumiwa na wanapewa tiba bure na Serikali. Lakini pia, kweli kumekuwepo maeneo kama unavyosema Mheshimiwa Mbunge ambayo wakati mwingine akifika mfungwa anatakiwa kupewa huduma, anapewa zote bure, lakini kuna dawa inakosekana, saa nyingine ndugu anatafutwa kununua hiyo dawa iliyokosekana. Waziri wa Afya ameshatoa maelekezo kuhakikisha kwa kutumia watu wetu wa ustawi wa jamii mfungwa huyo anapitia kwenye utaratibu hata kwenye mapato ya ndani mfungwa huyo anatafutiwa dawa wakati tukishirikisna na Wizara ya Mambo ya Ndani kuona tunafanya nini, ili hilo tatizo lisiwepo.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza. Serikali imewahi kwenda kutoa elimu ya ufugaji wa vizimba vya samaki kwa wananchi wanaozunguka Ziwa Basutu. Je, kwa kuwa imekwishakuwa ni muda mrefu ni lini Serikali itapeleka fedha ili wananchi hao waweze kunufaika na mafunzo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tayari wananchi wa Basutu wamekwishapata elimu naomba nimuahidi kuwa Serikali inalichukua jambo hili na kwenyewe tutakwenda kufanya tathimini ya kimazingira ili waweze kunufaika na program hii na kujiongezea kipato na kutengeneza ajira. Ahsante sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kutenga zaidi shilingi milioni 900 kwa ajili ya ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Endagaw. Kwa sasa mkandarasi ameweza kusimamishwa. Je, ni lini Serikali itatuletea mkandarasi ili aweze kukamilisha ujenzi wa skimu hiyo na uweze kuleta tija kwa fedha za Serikali lakini kwa wananchi pia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mbunge amekuwa mfuatiliaji mzuri katika eneo hili. Ni kweli mkandarasi aliyekuwepo Endagaw tulimsimamisha na kumwondoa lakini tuko katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi mwingine ambaye atakwenda kukamilisha kazi hiyo kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge wape tu matumaini wakulima wako kwamba kazi itakamilika na watafanya kilimo cha umwagiliaji.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa kero za Muungano, ingawa Mheshimiwa Waziri hapa amejibu, anasema kwamba kero ya bandari imetatuliwa; lakini hadi jana nimepokea simu kutoka kwa wananchi ambao wamesafiri kutoka Zanzibar wamekuja Dar es Salaam na wamezuiwa mizigo yao midogo midogo bandarini. Nataka kujua, Serikali ituambie hapa;

Je, ni lini watalikomesha jambo hili na kero hii kuisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO
NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu suala la nyongeza la Mheshimiwa Asia Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika kikao chetu ambacho tulikaa tarehe 6 Disemba, 2022, miongoni mwa maazimio ambayo tuliazimia, kwa sababu kama nilivyosema kwamba suala la utatuzi wa changamoto za Muungano limeundiwa Kamati Maalum, kuna Kamati ya Wataalam, kuna Kamati ya Makatibu Wakuu lakini kuna Kamati ya Mawaziri. Kwa hiyo, mpaka tarehe hii tulipokaa tulikubaliana na tukatoa maelekezo kwa TRA na ZRA na Wizara zinazohusika kulifanyia kazi suala hili na kutoa mapendekezo ya ni kipi kinatakiwa kilipiwe na kipi ambacho hakitakiwi kilipiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwa na subira, hili jambo tunalifuatilia na tunahisi tunapokwenda kwenye kikao kijacho tutalipatia ufumbuzi. Nawaomba Watanzania waendelee kuwa na subira, Serikali zote mbili zinazifanyia kazi hizi changamoto za Muungano.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Galapo, Orkasmet hadi Kibaya Kiteto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, tunapoongea sasa hivi, barabara aliyoitaja ndiyo tunakamilisha usanifu wa kina na baada ya hapo tutatafuta fedha kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza nachukua nafasi kwa kuipongeza Serikali kwa kujengwa kwa hospitali za mMikoa;

Je, ni lini Hospitali hizo za Mikoa zitaanza huduma za dialysis?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili. Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba gharama za matibabu ziko juu;

Je, nini kauli ya Serikali juu ya kuwasaidia wale wananchi masikini ambao hawana uwezo wa kukidhi gharama hizo za matibabu?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kwa namna ambavyo anashirikiana na Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Manyara kufutilia shughuli mbalimbali za afya katika mkoa huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza linahusu huduma kwenye hospitali zetu za mikoa. Kati ya bilioni 290.9 ambazo Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu amezileta zimetumika kununua vifaa kwa ajili ya dialysis kwa hospitali zote za mikoa. Na hata Mkoa wako wa Manyara vifaa tayari vimefika na nategemea mpaka sasa kazi hiyo imeanza na watu wanapata huduma pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili linahusu suala la gharama. Ni kweli ni gharama kubwa sana kwenye eneo la kutibu figo, na nilisema juzi hapa. Tunafikiri kwamba bei yake inaweza ikashuka kuanzia tisini hadi 150,000, hapo inawezekana kushusha. Lakini kuna utaratibu wa exemption kwa watu ambao wananshindwa kulipa. Kama yuko kule Manyara kwenye kata yake akiwa na barua ya mtendaji wake wa kata, akifika hospitali anastahili kutibiwa bure.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nichukue nafasi hii mimi pamoja na wananchi wa Kata ya Endagaw na wananchi wa Wilaya ya Hanang, kuiomba Serikali kuhakikisha kwamba ujenzi huo wa mifereji unafanyika sasa na sio kipindi cha masika kwa sababu sisi tunajua uhalisia wa jiografia tunapotoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Hanang ni wananchi ambao wanalima sana. Je, Serikali haioni haja sasa ya kuendelea kuongeza mabwawa ili wananchi wa Wilaya ya Hanang waweze kulima kilimo cha uhakika na chenye tija? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, baada ya kumwondoa mkandarasi aliyeshindwa kufanya kazi yake vizuri, hivi sasa tunahakikisha kwamba mkandarasi ambaye tutamtangaza aifanye kazi hii kwa haraka na kuwahi msimu huo ambao umekuwa na athari kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Waziri, la pili, ni kweli Wilaya ya Hanang ina wakulima wengi. Katika mpango wa Serikali, mwaka huu wa fedha tutakwenda kuchimba bwawa eneo la Laganga ambapo zaidi ya hekta 600 za umwagiliaji zitapatikana na wakulima wa eneo la Hanang watapata maeneo ya kilimo chao cha umwagiliaji. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na ukubwa wa jiografia wa Wilaya ya Hanang; je, ni lini Serikali itaongeza watumishi wa afya katika Hospitali ya Wilaya pamoja na vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halamga kuhusu Hanang na vituo vya afya, zahanati, hospitali ya wilaya na vituo vya afya ambavyo vina upungufu wa watumishi, kama nilivyokwishakusema kwenye majibu yangu ya msingi katika ajira hizi zilizotangazwa na Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu ajira 8,070 nitahakikisha pia Hanang wanapata watumishi wa afya.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza. Mkandarasi aliyekabidhiwa vijiji 15 vya Wilaya ya Hanang’ kasi yake inasuasua sana: Je, nini kauli ya Serikali juu ya Mkandarasi huyu ili kuwapa matumaini wananchi wa Wilaya ya Hanang’?

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkandarasi aliyekuwepo Hanang’ Nakurwa Investment Company ni kweli alikuwa anasuasua lakini tumemsimamia na katika vijiji 15 ambavyo vimebakia, vijiji tisa ameshasambaza nguzo, na tuna imani mpaka ifikapo Desemba, 2023 atakuwa amekamilisha kuweka umeme vijiji vyote, ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano katika Kata ya Sirop, Wilaya ya Hanang?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Manyara kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Kata ya Sirop ina changamoto ya mawasiliano. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge baada ya kikao hiki cha Bunge tukutane ili nimuunganishe na watalam wetu ili waweze kumpa tarehe ya kufika katika eneo hilo kwa ajili ya kufanya tathmini, nakushukuru sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itasaini mkataba wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, barabara kuanzia Kongwa – Kiteto – Simanjiro hadi Arusha na Tanga – Kiteto hadi Singida? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti tulitaja barabara aliyoitaja Kongwa - Kibaya – Orkesumet - Losinyai hadi Arusha ambayo tunachosubiri sasa ni baada tu ya Bunge hili sasa ambalo tunategemea kabla ya Mwezi Juni barabara hiyo iwe imesainiwa kwa mpango wa EPC + F. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa mpango Mkakati wa kujenga Vyuo vya VETA kila wilaya. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kujenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Simanjiro?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia, Mbunge kutoka Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Simanjiro wenzetu wa Taasisi ya Upendo walijenga chuo kilikuwa hakijakamilika miundombinu yake lakini baada ya kujenga waliikabidhi Serikali. Chuo ambacho kipo katika Wilaya ya Simanjiro kipo katika Kijiji Engalakash katika Kata ya Emboret, lakini kilikuwa kimejengwa kweli na wenzetu wa Upendo na wamekwisha kabidhi Serikali na kilikuwa na miundombinu ifuatayo: Karakana mbili; Madarasa; Bwalo; Mabweni mawili; na Kisima cha maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa fedha Serikali imepeleka pale milioni 190 kwa ajili ya kuongeza miundombinu ambayo tunakwenda kujenga Bweni moja, tunajenga nyumba za watumishi, lakini kulikuwa na changamoto za umeme. Kwa hiyo, tunasambaza umeme ndani ya majengo pamoja na nje ya majengo na tutaendelea kufanya hivi. Kwa hiyo, sasa hiki ndiyo kitakuwa Chuo cha Wilaya ya Simanjiro kinachomilikiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwondoe hofu tutaendelea kuongeza majengo kama tunavyofanya katika maeneo mengine kama vile Urambo, Nanyumbu na maeneo mengine ambayo tulikuwa na vyuo vya zamani vilikuwa na miundombinu ambayo sio toshelezi, tutakwenda kujenga miundombinu ili kutosheleza kutoa huduma ile ya VETA katika maeneo yote ya wilaya zote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia vyanzo vya uhakika vya maji kama maziwa na mito kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, tarehe 20 Machi, 2023 mbele ya Mheshimiwa Rais tulisaini mikataba 22 kwa ajili ya kuyapitia mabonde yote ya kimkakati nchi nzima na hasa yale yenye mito na maziwa. Nataka nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba, tumezingatia hoja ya Wabunge humu ndani na tutalitumia Ziwa Victoria, Mto Malagarasi, Mto Ruhuhu, Mto Songwe, kule Litumbandyosi, pamoja na Kilombero, Mto Ngono, Mto Rufiji, hii yote tutaitumia kuhakikisha kwamba, tunafanya kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi ya maji katika Kata ya Duru na Yasanda, Jimbo la Babati Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maeneo ya Babati Vijijini, Miradi ambayo ipo kwenye utekelezaji tunaendelea kupambana kuona inakamilika ndani ya wakati na maeneo ambayo usanifu umekamilika pia mwaka ujao wa fedha tutaendelea kuongeza nguvu katika maeneo yote ya Babati Vijijini ili kupata maji safi na salama.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Tunaishukuru Serikali kwa kujenga vituo vya afya katika Mkoa wa Manyara. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka wataalam wa kutosha pamoja na vifaatiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni commitment ya Serikali hii ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba ina wataalam wa kutosha wa afya, ndiyo maana hivi karibuni Serikali ilitoa ajira 8,070 kwa wataalamu wa afya kote nchini na Mkoa wa Manyara nao wamepata mgao wao wa wataalam hawa wa afya.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia bonde la Kiru na Magara kwa ajili ya umwagiliaji?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kiambatanisho namba tano cha bajeti yetu tuliyoisoma hapa ndani tumeyataja mabonde 22 moja kati ya mabonde yaliyotajwa ni mabonde ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja na yapo katika hatua ya mshauri mwelekezi hivi sasa akikamilisha kazi tunaanza ujenzi mara moja ili wananchi wa Mkoa wa Manyara waweze kunufaika na skimu hizi za umwagiliaji.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je Serikali ina mpango gani wa kujenga Mahakama ya mwanzo eneo la Minjingu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi naomba sasa kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wetu huu wa bajeti ya mwaka huu miongoni mwa maeneo ambayo yanahitaji ujenzi wa Mahakama ni pamoja na eneo la Minjingu. Mheshimiwa Asia pamoja na wewe mmekuwa mkikumbusha jambo hili naomba niliarifu Bunge hili Tukufu na wananchi wa Babati Vijijini kwamba tutajenga Mahakama pale Minjingu ili wananchi wapate huduma.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nichuke nafasi hii kuipongeza Serikali kwa majibu mazuri, lakini pia nina maswali yangu mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikinunua dawa MSD na inapokosa inanunua kwa mshitiri; je, Serikali inamkaguaje mshitiri ili kuwa na dawa za kutosha pale inapokosekana MSD?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; ni hatua gani zinachukuliwa kwa watoa huduma wa vituo vya afya ambao wanathibitika na upotevu wa madawa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri ambayo yanalenga kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma. Ni kweli kama anavyosema Mbunge kwamba, wakati mwingine inapokuwa MSD hakuna dawa, basi watu wetu wanapewa OS na wanakwenda kununua kwa mshitiri, lakini kuna mikoa ambayo wamemweka mshitiri ambaye ni mmoja na wataalam wetu hawaruhusiwi kunua dawa nje ya yule mshitiri. Kwa hiyo, anapokuwa amekosa MSD, anafika kwa mshitiri, naye mshitiri akiwa hana dawa, kwa hiyo, inafika mahali watu wetu wanateseka hawana dawa na huku fedha wanazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii na hili swali la Mheshimiwa Mbunge kuagiza kwamba, kwanza tusilazimishe hospitali zetu kununua kwa mtu fulani dawa. Ni kwamba tutengeneze biashara huria, duka lolote lenye dawa ambalo limetimiza vigezo, watu wetu waweze kununua kwenye duka lolote la dawa bila kulazimishwa kununua kwa mtu fulani. Kwa sababu nayo hiyo ni aina ya ufisadi mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge, hakika tutakapokuwa tunapita, tutashirikiana naye kushughulikia suala hilo, kwa sababu ukiona mtu mmoja analazimishwa kwenye mkoa mmoja kwamba yeye ndio auze dawa, hiyo ni aina mwingine wa ufisadi na tutausimamia na ku-control.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu tunafanya nini kwa wale wanaobainika kwamba wameiba dawa, kwa kweli kuna sheria na taratibu za utumishi wa umma. Kama unavyojua, nasi ni Wabunge ambao tunatunga sheria hapa, kuna baadhi ya sheria tumetunga ambapo mwizi anakuibia mara moja, lakini ikifika mahali wakati wa kumshughulikia mwizi ambaye una hakika kwamba ameiba, inabidi ufuate taratibu na sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inabidi tutafakari kwa kina namna gani tutawashughulikia watu ambao wanafanya ufisadi kwa sababu wakati mwingine sheria zinawalinda sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Mkandarasi anayeitwa Giza anasuasua sana miradi yake katika Jimbo la Kiteto. Je, ni lini miradi ya umeme ya vijiji vya Kiteto itakamilika?

SPIKA: Ni Mkandarasi wa umeme halafu anaitwa Giza?

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, yes! Na miradi yake inasuasua.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, mkandarasi Giza Cables ni mkandarasi anayetoka Misri na Misri kuna Mji ambao unaitwa Giza na ndio jina lake linapotokea na alikuwa anafanya kazi Manyara na Mara. Ameshakamilisha loti yake ya Manyara na kwa Manyara tunaendelea kumsimamia ili akamilishe kazi yake kabla ya Desemba atakuwa amekamilisha kazi hiyo.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Swali la kwanza; kwa kuwa majibu ya Serikali yanaonesha kabisa fedha iliyotengwa ni ndogo kulinganisha na miradi ya wananchi. Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya kuongeza fedha ili kuweza kumalizia miradi ambayo nguvu za wananchi zimetumika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuona miradi hiyo ama nguvu hizo za wananchi kwa kuanzia tuanze na Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunatambua kwamba wananchi wamefanya kazi kubwa sana ya ujenzi wa maboma na fedha ambayo tumetenga bado haikidhi, lakini Serikali inaendelea kutafuta fedha kuhakikisha kwamba tunakamilisha na kuongeza jitihada ambazo wananchi wamezifanya. Kwa hiyo nimwondoe shaka kwamba, tutaendelea kuongeza kwa mfano mwaka huu na mwakani mwaka wa fedha unaofuatia, Serikali itaongeza fedha ili kuhakikisha maboma hayo yanakamilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, niko tayari kwenda kujionea hiyo miradi Mkoa wa Manyara nikiongozana na Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum pamoja na Wabunge wote wa Mkoa wa Manyara. Ahsante sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza: Je, ni lini ujenzi wa shule 56 za michezo utaanza kama Serikali ambavyo iliahidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato umeshaanza wa kujenga Academy 56 katika shule zetu za Sekondari na tunatarajia katika mwaka huu wa fedha ambao tunauendea, endapo Bunge lako Tukufu litatupitishia fedha, tumetenga kiasi cha Shilingi bilioni mbili kwa kuanza na shule hizo.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi; kwa kuwa kuwa na kitambulisho cha Taifa ni haki ya kila Mtanzania, je, ni nini kauli ya Serikali kwa wafungwa na maabusu wa muda mrefu juu ya kupatiwa huduma hii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba ni haki la kila raia kupata kitambulisho, lakini kwa hawa ambao wamefungwa sidhani kama kuna dharura ya kiasi hicho, kwa sababu hawa wapo jela vitambulisho vinatakiwa kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali ikiwemo elimu, mikopo, safari, passport na kadhalika, sasa huyu mfungwa tuhangaike kumpa kitambulisho anakwenda kukitumia wapi. Lakini tuahidi atakapokuwa amemaliza kifungo chake akirudi uraiani atatambuliwa na kupewa kitambulisho kama inavyopaswa, nashukuru. (Makofi)

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kutengwa kwa kiwango hicho cha fedha na mwezi Oktoba jengo hilo litakuwa limekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la nyongeza; kwa kuwa kwa sasa Mkoa wetu wa Manyara tuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa hati za kusafiria lakini pamoja na hati za makazi. Inatulazimu kupata huduma hiyo Mkoa wa Arusha, Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Singida na siyo Mkoa wa Manyara.

Je, Serikali iko tayari sasa kutufungia elektroniki ili tuweze kupata huduma hiyo ndani ya Mkoa wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili; kwa kuwa Mkoa wa Manyara uko pembezoni na wahamiaji haramu wengi wanatumia kama njia ya kupita kwenda kwenye nchi zingine.

Je, Serikali haioni haja ya kutuongezea watumishi pamoja na usafiri kwa sababu kwa sasa watumishi wetu wanatumia pikipiki badala ya usafiri wa magari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Halamga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kwamba katika Mkoa wa Manyara huduma za kutoa pass kwa electronics zilikuwa hazijafungwa kwenye jengo hili kwa sababu jengo lilikuwa halijakamilika. Hivi sasa watumishi wa ngazi ya Mkoa wako kwenye jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara na mimi nimshukuru Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kuwaweka watumishi hawa kwenye jengo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namuahidi Mheshimiwa Halamga, jengo litakapokamilika mifumo yote ya electronic ya utoaji wa pass zitatolewa kwenye jengo letu la uhamiaji baada ya Oktoba mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nyongeza ya watumishi na magari, nakubali kwamba Mkao wa Manyara unalo gari moja tu aina ya Forde Ranger liliko ngazi ya Mkoa, Wilayani kule tunatumia usafiri wa pikipiki, lakini pia kuna uhaba wa watumishi kama alivyokwishaeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Waheshimiwa Wabunge wanakumbuka wakati wa bajeti tulitamka kwamba wapo watumishi 820 ambao wataajiriwa kama watumishi wapya, wako kwenye mafunzo sasa hivi, wanatarajia kuhitimu mwezi Septemba, 2022. Katika mpango wetu wa ugawaji tutazingatia maeneo yenye upungufu mkubwa zikiwemo Wilaya za Mkoa wa Manyara. Nashukuru.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi; je, Serikali ina mpango gani wa kuokoa Ziwa Babati kwa kuondoa magugu yanayozidi kukua kwa kasi?

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la dada yangu Asia, Mbunge wa Manyara Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Ziwa Babati limekuwa na changamoto na magugu sambamba na maeneo mengine. Serikali tumeandaa mpango maalum hivi sasa kubainisha juhudi tulizonazo juu ya mpango huo lengo kuangalia maeneo ya changamoto mbalimbali. Kwa hiyo, tuko katika stage ya kutafuta fedha siyo Ziwa Babati peke yake lakini na maziwa mengine yanayokabiliana na magugu katika maeneo mbalimbali.


MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa kilometa tano za lami Babati Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, ni lengo la Serikali kuhakikisha ahadi zote za Viongozi wetu Wakuu, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu zinatekelezwa kwa wakati na tutaendelea kuratibu kupitia Ofisi ya TARURA, Mkoa wa Manyara, Ofisi ya TARURA, Wilaya ya Babati, kuona ni kiasi gani kinahitajika ili tuweze kutafuta fedha kuweza kutekeleza ahadi hiyo.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka magari ya wagonjwa katika Jimbo la Mbulu Mji na Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, magari mawili yatanunuliwa na kupelekwa Halmashauri ya Mbulu Mjini na Mbulu Vijijini. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, nini mpango wa Serikali kwa vikundi vya wafugaji wa Simanjiro, Kiteto na Hanang kuleta mbegu ya madume bora?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi, ni kwamba madume bora yapo na katika bajeti ya mwaka huu pia tutaongeza idadi ya madume bora, na Wilaya ya Hanang, Kiteto, Simanjiro na maeneo mengine kote ambako wanahitaji madume bora, tuko tayari kuwapelekea. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kata ya Gehandu kwa sasa wanatumia mnara wa mawasiliano uliopo Kata ya Ishiponga. Je, ni lini Serikali itapeleka mnara wa mawasiliano katika Kata ya Gehandu kwa sababu huu wa Ishiponga katika Jimbo la Hanang unasuasua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga na nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili eneo la Gehandu tayari tunalifanyia kazi, kwanza, kuboresha ule mnara wa jirani kwa sababu masuala ya mawasiliano ni suala la signals kufika. Kwa hiyo, tutaongezea vifaa ili kuona signals zinaweza kufika vizuri zaidi wakati tunajipanga kujenga mnara mpya katika eneo hili la Gehandu. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, je, ni lini Serikali itapeleka mashine ya x-ray katika Vituo vya Afya vya Hirbadau, Mogitu pamoja na Bassotu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 66.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wewe vituo vyako hivi vya afya vitakuwa katika mgao wa manunuzi ya vifaa tiba. Kwa hiyo, utapata mashine hii ya x-ray.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata ya Bassotu, Wilaya ya Hanang umekuwa ni wa muda mrefu sana. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili kukamilisha ujenzi wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Vijana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Bassotu kimetengewa fedha katika mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuweza kukamilika na kutoa huduma kwa wananchi wa Bassotu na Wilaya ya Hanang kwa ujumla.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Afya katika Kata ya Kitwai iliyopo Wilaya ya Simanjiro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tulitoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa Halmashari zetu zote kote nchini kuhakikisha wanatupa maeneo ya kipaumbele vya ujenzi wa Vituo vya Afya vya Kimkakati katika kata zetu. Kwa hivyo, nimwelekeze Mkurugenzi wa Halmashauri hii kuleta maandiko hayo ya mapendekezo ya eneo hili la Kituo cha Afya cha Kitwai kama liko katika eneo la kimkakati Serikali itafute fedha kwa ajili ya utekelezaji. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Afya Galapo Jimbo la Babati Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa bahati njema nilishafanya ziara katika Kituo cha Afya cha Galapo na tulifanya mkutano wa hadhara tukiwa pamoja na Mbunge wa Jimbo, na tayari kituo kile kimeingizwa kwenye mpango wa Benki ya Dunia kwa ajili ya kujengwa. Wakati wowote tunatarajia fedha ikitoka tutakwenda kuanza ujenzi Galapo.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Hanang ina ng’ombe zaidi ya 300,000 na tuna magulio 17. Je, ni lini Serikali itajenga miundombinu kwa Mnada wa Endasak na Katesh walau wa kuanzia?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anavyosema Mheshimiwa Mbunge, Wilaya ya Hanang ina mahitaji makubwa ya ujenzi wa minada, lakini mchakato wa kibajeti huanzia chini. Wananchi wanapoanzisha mradi wao chini kwa mapendekezo katika mpango wa bajeti yakifika huku juu sisi tuko tayari kutekeleza ujenzi wa mnada huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge arudi kule jimboni, awaeleze wananchi kwamba wanaweza kuanzisha mchakato wa mawazo ya kuanza kuingiza kwenye mpango wa bajeti ya mwaka 2024/2025 ili tuweze kuingiza kwenye mpango wa bajeti kuu, ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je ni lini Serikali itaweka vifaa tiba katika majengo ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya Endasak pamoja na Gisambalang Jimbo la Hanang? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, Vituo vya Afya vya Endasak na Gisambalang ni vituo ambavyo Serikali ilipeleka fedha, vituo hivyo vimejengwa vimekamilika vimeanza kutoa huduma za awali. Lakini Mheshimiwa Rais alishapeleka fedha za Vifaa Tiba katika Halmashauri zote 184, tunatambua kwamba Vifaa Tiba vile bado havitoshelezi ikiwemo katika vituo hivi vya Endasak na Gisambalang. Nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha Serikali imetenga zaidi ya bilioni 66.7 ya vifaa tiba na tutahakikisha tunatoa kipaumbele katika vituo hivi vya afya, ahsante. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Priscus Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini. Nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali katika kipindi cha bajeti Mheshimiwa Waziri alitueleza kwamba zimetolewa zaidi ya shilingi bilioni 949 kwa ajili ya ulipaji wa madeni mbalimbali. Tunataka kufahamu katika ulipaji huo wa zile fedha shilingi milioni 949 watoa huduma shuleni na wao wako kwenye huo mpango?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, je, mnatumia muda gani ili wananchi hawa waweze kujua watakaa muda gani na madeni hayo kwa sababu watoa huduma shuleni wengi ni wajasiriamali wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Asia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, bila shaka wazabuni ambao wanatoa huduma shuleni ni sehemu ya fedha ile ambayo ililipwa mwaka uliopita na wanaendelea kulipwa ndani ya mwaka huu na mwaka unaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kwamba ni lini, inategemea upatinaji wa mapato na kukamilika kwa uhakiki. Basi nimwomba Mheshimiwa na Wazabuni wote nchini wawe na Subira, muda ukifika, fedha zao watalipwa.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Dajameda pamoja na Kijiji cha Muungano, Kata ya Laghanga Jimbo la Hanang hakuna maji kabisa na wananchi wanatumia umbali wa kilometa 30 kwenda kata nyingine ya Bassotu kufuata maji, je, ni lini Serikali itawapelekea wananchi hawa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Hanang ni kweli kabisa kwamba kuna changamoto katika vijiji hivyo pamoja na cha Muungano, lakini Serikali kupitia RUWASA tayari wameshafanya utafiti na wataanza kufanya usanifu wa kuvuta maji kutoka Bassotu kuja katika vijiji saba na katika hivyo vijiji saba ni pamoja na Kijiji cha Muungano na kijiji kingine ambacho amekitaja ambacho sijakisikia vizuri. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, je, ni lini Serikali itaanza Ujenzi wa Barabara ya Mbuyu wa Mjerumani hadi Mbulu kwa kiwango cha lami?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, pia barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge, Mbuyu wa Mjerumani kwenda Mbulu imeshakamilisha usanifu na tulichokuwa tunakifanya ni kujenga kwa awamu hasa kwenye ile milima (zile escapement) wakati Serikali inatafuta fedha kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Je, ni lini Serikali itaanza mradi wa usambazaji wa umeme kilometa mbili katika Jimbo la Babati Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari mikakati ipo katika hatua za mwisho kuhakikisha kwamba, umeme unafikishwa katika Jimbo la Babati Vijijini. Namuomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati tunatekeleza jambo hili. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali italeta gari la Zimamoto katika Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, tunanunua magari 150 ambayo tutayapeleka kwenye mikoa yote ambayo haina magari hayo ikiwemo Mkoa wa Manyara, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza ninauliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachukua nafasi hii kuishukuru sana Serikali yetu kwa kuendelea kuwajenga vijana katika misingi ya uzalendo, lakini katika misingi ya stadi za maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, kwa kuwa Serikali iliona kazi maalumu na kubwa ambayo imefanywa na vijana waliofanya kazi hiyo ya operation, waliojenga Ikulu pamoja na ukuta wa Mererani.

Je, Serikali haioni haja ya kuwachukua pia vijana waliojenga Chuo cha Mzumbe, Bwawa la Mwalimu Nyerere, nyumba za Ukonga pamoja na Msomela kwa sababu kazi za operation hazitokei kila mara, ni kazi ambazo zinatokea mara chache. Je, Serikali haioni haja sasa ya kuwachukua na vijana hao waliojenga maeneo mengine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Serikali haioni kuwa kwa kuwa JWTZ itakuwa ina nafasi labda zisizokidhi vijana wote. Serikali haioni haja sasa kuungana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuwa na ile database ya vijana ambao wamefanya kazi maalumu, wakaweza kuwekwa kwenye majeshi mengine? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, swali la kwanza ambalo ameuliza, kuwachukua vijana wengine ambao wameshiriki katika operation mbalimbali alizozitaja, utaratibu wa kuwachukua vijana ni kama nilivyoeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ninafurahi na ninamshukuru kwamba katika swali lake la pili, ameeleza wazi nafasi za kuandikisha vijana jeshini ni chache. Kwa hiyo, tunawachukua vijana kulingana na mahitaji ya wakati huo, kulingana na taaluma walizonazo na vijana wote wanaopenda JKT hushiriki katika operation mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawashukuru sana vijana wetu kwa moyo huo wa kujitolea na kufanya kazi hizi wanazokuwa wamepangiwa kwa umahili wa hali ya juu. Kwa hiyo, kadiri nafasi zinavyopatikana na kadiri mahitaji ya wakati huo yalivyo vijana mbalimbali huchukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuwa na database, database ipo na tunashirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama katika kuainisha vijana kuja kwetu. Kuainisha vijana ambao wana sifa kulingana na mahitaji yao. Kwa hiyo, tunafanya kazi pamoja na database ipo, lakini ikumbukwe tu kwamba Bunge hili lilitoa pia uhitaji au kigezo hicho. Kwa hiyo, pengine ni kulishauri Bunge likaangalia upya kigezo hicho ambacho kiliondolewa, ahsante. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza kabisa, niishukuru Serikali kwa kuendelea kutatua changamoto ya mawasiliano katika nchi yetu. Nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa katika Wilaya ya Hanang’ kwa maeneo kama Sirop, Gisambalang, Gidahababieg, Lalaji pamoja na Hirbadaw bado tuna changamoto kubwa ya mawasiliano. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kuweka Kata hii ya Simbay na haya maeneo niliyoyataja ya Wilaya ya Hanang’ katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kumekuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano katika Kata ya Nkaiti, Vilima Vitatu na Wilaya ya Babati Vijijini. Je, Serikali haioni haja sasa ya kupeleka minara ya mawasiliano katika maeneo haya? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nipende kumpongeza Mheshimiwa Asia Halamga amekuwa mfuatiliaji mzuri katika hili na kama ambavyo mara ya mwisho amekuja Wizarani tukaongea kwa pamoja. Niendelee kumpa matumaini, maeneo haya yote aliyoyataja, mazingira yake tumeelewa na nipende kuiagiza UCSAF katika mwaka ujao wa fedha tuhakikishe tunawafikia wananchi na kuwapatia mawasiliano ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Mbunge kuhusu lini tutajenga mnara katika Kata ya Vilima Vitatu, Nkaiti, Babati Vijijini. Haya maeneo pia tayari wameshafanya survey na sasa wanaelekea kufanya tendering ya hivi vifaa vya kujengea mnara na ndani ya miezi sita tunatarajia katika maeneo haya ya Nkaiti, Babati Vijijini mnara huo utajengwa. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Vijana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli jengo la Mkoa wa Manyara la Kamanda linaendelea, lakini kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, tumetenga shilingi 800,000,000 kwa ajili ya kukamilisha jengo hilo la Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara. Ahsante sana. (Makofi)