Contributions by Hon. Amina Ali Mzee (3 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. AMINA ALI MZEE: Mheshimiwa Spika, naomba Serikali iwatumie wanafunzi wa Kitivo cha Kilimo SUA kufanya tafiti mbalimbali za kilimo.
Kwa nini tunakuwa watumwa wa sayansi? Ikiwa wataalamu waliosomea sayansi hawawezi kuitumia sayansi kubadilisha mwelekeo wa idara wanazozifanyia kazi basi wanasayansi hao hawasaidii Serikali na inabidi Serikali ichue hatua.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iwaandae vijana kuweza kuwaendeleza kwenye kilimo kwa kupatiwa elimu, mikopo na masoko kuweza kujikwamua kiuchumi na kuzalisha ajira nyingi nchi.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. AMINA ALI MZEE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nami sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia taarifa ya Kamati hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina budi kumshukuru Mwenyezi Allah Subhana Wa Ta’ala, lakini nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika bajeti ya Wizara hii ilitutengea jumla ya bilioni moja katika sekta ya uchukuzi katika ununuzi wa mitambo ndani ya Chuo cha DMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru Mama yetu Kipenzi, Mama Samia Suluhu Hassan ndani ya chuo hichi mtambo huu wa scanner umefika ndani ya chuo na tayari wanafunzi wanaendelea kufaidika na mtambo huu kwa ajili ya kujisomea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite katika mchango wa kamati, changamoto ya kamati yetu zinaonyesha suala la madeni ndani ya taasisi za Serikali. Taasisi nyingi za Serikali zinaonyesha bado zina madeni. TBA inadai madeni mengi katika taasisi za Serikali, kupitia Wakala wa Madeni tuliweza kukusanya jumla ya trilioni saba kwa ajili ya ulipaji wa madeni. Jumla tulikuwa tuna deni la bilioni 25. Tuipongeze TBA kwa kuhakikisha kuendelea kulipa madeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tutoe wito kwa Serikali kwa kupitia taasisi zake, Wizara mbalimbali za Serikali zinadaiwa na TBA. Kama sera yetu ya mashirika inavyosema tuhakikishe mashirika yanaendelea kujitegemea kiuchumi na kujiendesha kibiashara na faida. Taasisi za Serikali zijitahidi kulipa madeni ili kuhakikisha Shirika letu la TBA linaendelea kunyanyuka na kuendeleza biashara zake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto pia iliyoelezwa suala la upungufu wa watumishi; ndani ya sekta yetu ya uchukuzi tuna takribani upungufu wa watumishi 18,000 lakini mpaka sasa Serikali imeendelea kuajiri watumishi 12,000, tuna upungufu wa watumishi 6,000. Serikali yetu tukufu inayoongozwa na Mama yetu mpendwa, tunaiomba Serikali yetu upungufu wa watumishi 6,000 kuhakikisha kuziba gap ili watumishi wengi wazidi kupata nafasi. Sekta ya uchukuzi tunafahamu, tuna vyuo, tuna bandari, sekta tofauti tofauti lakini upungufu huu unasababisha kuzorotesha kazi zetu ndani ya sekta yetu ya uchukuzi. Tunaiomba sana Serikali iweze kupunguza upungufu huo wa watumishi ili tupate watumishi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. AMINA ALI MZEE: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kunipa nafasi hii, nami nishukuru kwa nafasi ya kuchangia ya Wizara ya Ujenzi. Nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kuendelea kutoa fedha nyingi ndani ya Sekta hii ya Ujenzi. Tunaona mtandao mkubwa wa barabara ndani ya nchi hii; Mheshimiwa Rais anatoa fedha nyingi ili mtandao uendelee kuenea na kuendeleza demokrasia ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niipongeze Wizara kwa kuendelea kuwapa wakandarasi vijana na wanawake ambao wanamaliza chuoni pale high court kuwajengea uwezo wa miaka mitatu ili waweze kujiajiri katika kazi mbalimbali za barabara ambazo zinaendelea ndani ya nchi hii, niipongeze sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze mchango wangu kwa kuchangia kuhusu kuwawezesha Shirika la TBA. Serikali ilitazame kwa jicho la huruma Shirika hili la TBA. Shirika letu la TBA linajitahidi sana kuhakikisha kwamba linajenga nyumba kwa ajili ya wananchi na watumishi wanaoishi ndani ya Dodoma hii na maeneo mengine ya Taifa hili. Serikali itazame basi haja, kama Kamati ilivyoshauri, kuomba shilingi bilioni 50 ili shirika hili nao wapatiwe ili waweze kujiendesha kibiashara na waweze kuzalisha faida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, taasisi nyingi za Serikali zinadaiwa na Shirika hili la TBA, taasisi hizi zinalikwamisha shirika letu kujiendesha kwa faida na kibiashara. Wapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge na wananchi ambao pia wanadaiwa na shirika hili. Nitoe wito kwa wananchi na taasisi za Serikali, zilipe madeni ambayo wanadaiwa na TBA. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee na mchango wangu kwa taasisi ya TEMESA. Tunaelewa kuwa taasisi nyingi za Serikali pamoja na Wizara wanapeleka magari yao ya halmashauri TEMESA; lakini wakishapeleka huko TEMESA wanaigeuza shamba la bibi. Wakishapeleka magari yao na yakishakuwa yamefika na kwamba wamepewa huduma, wakishamaliza kupewa huduma tu wanaondoka na magari yao, lakini taasisi yetu ya TEMESA hailipwi. Ninaomba taasisi za Serikali zilipe madeni yao wanayodaiwa na TEMESA. Tunajua kwamba TEMESA inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa vifaa kama vile vipuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali basi ione haja ya kuweza kuwapatia mtaji TEMESA ili waweze kununua spare wenyewe bila kutegemea spare kutoka kwa wafanyabiashara, maana sasa hivi wanachukua spare kutoka kwa wafanyabiashara. Wafanyabiashara hawa wakishawapa spare inawezekana hizo spare wanawapa nzima, inawezekana hizo spare fake, kwa hiyo wakija kutengeneza baada ya siku kadhaa gari za Serikali zinaharibika. Kwa hiyo tunaiomba Serikali iwape mtaji TEMESA ili waweze kujiendesha na wao kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.
Mheshimiwa Spika, tumeona taarifa ya Kamati pia inaeleza juu ya wananchi wengi ambao wanadai fidia. Serikali yetu Tukufu, Mheshimiwa Waziri kijana, Naibu wake Waziri pamoja na Katibu Mkuu wetu mwanamke Mheshimiwa Aisha, tuchukue basi hatua na jitihada za haraka kuhakikisha kwamba wananchi wetu waliopisha maeneo kwa ajili ya ujenzi wa barabara nao wanalipwa fidia ili nao waweze kupisha maendeleo ya nchi yetu na ujenzi wa barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sina mengi zaidi, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)