Primary Questions from Hon. Daniel Awack Tlemai (10 total)
MHE. DANIEL A. TLEMAI Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua mgogoro wa mpaka kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Kata ya Mbulumbulu katika Kijiji cha Lositete?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Awack Tlemai, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mgogoro wa mpaka kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Kata ya Mbulumbulu katika Kijiji cha Lositete ulidumu kwa muda mrefu. Mgogoro huu ulitatuliwa kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali zikiwemo:-
(i) Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya ya Karatu, Monduli na Ngorongoro;
(ii) Wataalam kutoka Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha; na
(iii) Wataalam kutoka Ofisi ya Katibu Tawala ya Wilaya za Karatu, Monduli na Ngorongoro; na Wahifadhi kutoka Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka hizi zote zilishiriki kutafsiri GN iliyoanzisha mipaka ya maeneo hayo kisheria.
Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Lositete kiko katika Wilaya ya Karatu na sio Wilaya ya Ngorongoro ambapo wananchi wa kutoka kijiji hicho walivamia eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na taratibu za kuwaondoa zilifanyika na kuwarudisha katika maeneo yao. Pamoja na kuwa Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro inaruhusu matumizi mseto, sheria hii iliwekwa kwa ajili ya wenyeji waliomo ndani ya hifadhi. Aidha, ndani ya hifadhi pia kuna maeneo ambayo yanasimamiwa Serikali ili kulinda uoto wa asili likiwemo eneo hili.
Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa msisitizo kwa jamii zote zinazozunguka mipaka ya hifadhi kuheshimu maeneo yote yaliyohifadhiwa kwa faida ya jamii na maslahi ya Taifa kwa ujumla. Ahsante.
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua mgogoro wa Wananchi wa Bugeli na Hifadhi ya Manyara pamoja na mauaji ya Wananchi yanayotokea mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Tlemai Awack, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Bugeli, hasa wafugaji wanapoingiza mifugo hifadhini na kukamatwa na Askari wa Hifadhi, wamekuwa na tabia ya kukataa kutii sheria bila shuruti na kupiga yowe maalum ijulikanayo kama “hayodaa” ikiwa ni kiashiria cha hatari kubwa kwa kabila la Kiiraki. Hivyo, baada ya yowe hiyo kupigwa, wananchi wengi hupata morali na kujitokeza wakiwa na silaha za jadi zikiwemo fimbo, mishale, mapanga na mikuki ili kupinga ukamataji huo wa mifugo na kuchukua mifugo yao kwa kutumia nguvu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kumekuwepo na baadhi ya matukio ya Askari kunyang’anywa silaha au mifugo iliyokamatwa hifadhini na wananchi ambapo husababisha kutokuelewana kati ya Askari wa Hifadhi na wananchi. Pamoja na taharuki hizo, kumekuwepo pia na mauaji ya Askari wapatao wawili na majeruhi kwa Askari watatu katika eneo hilo. Aidha, matukio kama haya yamekuwa yakijitokeza katika maeneo mengine yanayozunguka hifadhi mbalimbali hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiunda Kamati mbalimbali kuchunguza matukio hayo ili kubaini chanzo cha changamoto hizo. Kwa ujumla, imebainika kuwa tatizo kubwa ni wananchi kutoheshimu makubaliano ambayo yamekuwa yakifanywa mara kwa mara kati ya Uongozi wa Wilaya, Hifadhi, Serikali ya Kijiji na wananchi kuhusu taratibu za kufuatwa na wananchi hao pindi wao wenyewe au mifugo yao inapokamatwa ndani ya hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kwa dhati kuleta mahusiano mazuri kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi kwa kuchukua hatua mbalimbali, zikiwemo kufanya vikao vya kutafuta suluhu pamoja na kupanga matumizi bora ya ardhi katika maeneo husika. Katika kutekeleza azma hiyo, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itahakiki mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara na kuandaa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi kwa Kijiji cha Bugeli. Utekelezaji wake kwa sasa upo katika hatua za kukabidhi hati kwa wananchi wa kijiji husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa rai kwa wananchi wanaopakana na maeneo yaliyohifadhiwa kuepuka uvunjifu wa sheria za nchi na za uhifadhi na hivyo kudumisha amani kwa jamii husika na Taifa kwa ujumla.
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuendeleza mashamba ya Karatu –Bendhu pamoja na kuwalipa wafanyakazi wa mashamba hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Awack Tlemai, Mbunge wa Jimbo la Karatu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu ina jumla ya mashamba 33 yanayomilikiwa na wawekezaji katika tasnia ya mazao ya biashara na chakula. Kati ya mashamba hayo 33 mojawapo ni Shamba la Bendhu lililopo Kata ya Oldeani lenye ukubwa wa hekta 472, Mwekezaji wa shamba hilo aliyemilikishwa kwa miaka 99 kuanzia 1948 hadi 2047, ameliendeleza kwa asilimia 49 kwa kilimo cha mazao ya ngano na kahawa. Aidha asilimia 45 ya shamba linalimwa na wafanyakazi kwa ajili ya kujikimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mashamba yote 33, Shamba la Bendhu ndiyo lenye mgogoro wa mirathi iliyotangazwa kupitia Gazeti la Serikali Na.6 la tarehe 5 Februari, 2021 katika ukurasa wa 13. Kutokana na mgogoro huo uzalishaji wa mazao katika shamba hilo uliyumba na kusababisha malipo kwa wafanyakazi kutofanyika kwa wakati. Aidha, wafanyakazi wa shamba hilo walifungua kesi Na.8 ya mwaka 2015 katika Kamisheni ya Usuluhishi na Maamuzi (CMA) Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na majadiliano ya kesi hiyo, mwezi Desemba, 2020 yalifikiwa makubaliano kwamba wafanyakazi wataendelea kulipwa kadri ya mapato yatakavyokuwa yanapatikana kutokana na uzalishaji katika shamba hilo. Pia, utekelezaji wa makubaliano hayo unasimamiwa na Chama cha Wafanyakazi. Aidha, nia ya Serikali ni kuona utekelezaji wa makubaliano hayo unafanyika bila changamoto yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na shauri la mirathi kuwa mahakamani, Serikali inasubiri maamuzi ya Mahakama juu ya shauri hilo. Aidha, hakuna migogoro iliyopo katika mashamba mengine 32 ya Karatu. Hata hivyo mkakati wa Serikali ni kuendelea kufuatilia mashamba yote ya uwekezaji yaliyopo Wilayani Karatu na kwingineko nchini ili kuhakikisha mashamba hayo yanaendelezwa na kuzalisha kwa maslahi ya nchi. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI K.n.y. MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kurekebisha miundombinu ya Skimu ya maji katika Kijiji cha Mbuganyekundu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Awack Tlemai, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kujenga miundombinu ya umwagiliaji ya skimu zilizopo katika bonde la Eyasi zenye jumla ya hekta 5,000 ikiwemo skimu ya Mbuganyekundu. Taratibu za kuwapata wakandarasi wa ujenzi wa skimu hizo unaendelea ambapo zabuni zimeshatangazwa.
MHE. DANIEL T. AWACK aliuliza: -
Je, ni lini itatolewa bei elekezi ya maji katika Karatu ili kuondoa tofauti kati ya KARUWASA wanaouza unit 1 Sh.1,700 na KAVIWASU unit 1 Sh.3,000?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Tlemai Awack, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha hakuna changamoto katika ulipaji wa bili za maji kwa wananchi. Hivyo, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023, imeviunganisha vyombo vya usimamizi wa huduma ya maji KARUWASA na KAVIWASU na kuunda chombo kimoja cha KARUWASA ambacho kitakuwa imara ili kiweze kutoa huduma ya maji kwa ufanisi katika eneo lote la Mji wa Karatu.
Mheshimiwa Spika, bei elekezi ya kuanzia kwa uniti moja ya maji imeshatolewa na inatumika. Aidha, marekebisho yataendelea kufanyika kwa kuzingatia miongozo kutoka EWURA.
MHE. ZAYTUN S. SWAI K.n.y. MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa Barabara ya Matala – Mwanhuzi – Lalago kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Tlemai Awack, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya barabara ya Matala – Mwanhuzi – Lalago yenye kilometa 148.4 ya kutoka Lalago – Mwanhuzi – Sibiti – Nyahaha imo kwenye mradi wa ujenzi wa Barabara ya Maswa – Lalago - Sibiti River – Haydom – Mbulu – Karatu yenye urefu wa kilometa 339 ambao utatekelezwa kwa utaratibu wa Engineering, Procurement and Construction plus Financing (EPC+F) ambao hadi sasa mkandarasi amepatikana na mkataba wa ujenzi utakuwa umesainiwa kabla ya mwishoni mwa mwezi Juni, 2023. Kwa sehemu ya Nyahaha kwenda Matala (kilometa 25) Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Njia Panda - Mangola - Matala hadi Lalago kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Tlemai Awack, Mbunge wa Karatu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Njia Panda kuanzia Karatu – Mang’ola – Matala – Sibiti River hadi Lalago, yenye urefu wa kilometa 328 inayojulikana kama Eyasi Route.
Mheshimiwa Spika, sehemu ya kuanzia Sibiti River hadi Lalago yenye urefu wa kilometa 121 imejumuishwa kwenye mradi wa EPC+F kupitia barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti River – Lalago hadi Maswa ambayo ina jumla ya kilomita 389 ambapo mkataba wake wa ujenzi umesainiwa. Kwa sehemu iliyobaki ya Njia Panda – Mang’ola hadi Matala kilometa 137, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, ahsante (Makofi)
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatoa bei moja elekezi kwa kila unit moja ya maji Wilayani ya Karatu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Awack Tlemai, Mbunge wa Jimbo la Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma ya majisafi na usafi wa mazingira mjini Karatu inatolewa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Karatu (Karatu Urban Water Supply and Sanitation Authority - KARUWASA). Awali kulikuwa na changamoto ya kuwepo kwa Taasisi mbili zinazotoa huduma ya maji ambazo ni Karatu Village Water Supply (KAVIWASU) na KARUWASA na kila moja ilikuwa na bei yake. Mwezi Agosti 2022, Serikali iliziunganisha taasisi hizo na kuwa na taasisi moja inayoitwa KARUWASA na kutoa bei elekezi ya maji ya shilingi 1,300 kwa unit moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa eneo la Karatu Vijijini linalohudumiwa na RUWASA, Serikali ilitoa bei elekezi kulingana na teknolojia inayotumika kuwafikishia wananchi maji na bei hizo zinafuatwa.
MHE. ZAYTUN S. SWAI K.n.y. MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza:-
Je, lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa barabara ya Karatu – Mbulu – Singida kilometa 190?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Awack Tlemai, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Karatu – Mbulu – Singida ni sehemu ya barabara ya Karatu – Mbulu – Hydom – Sibiti River – Lalago – Maswa yenye urefu wa kilometa 389. Serikali imeanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii ambapo sehemu ya Mbulu – Garbabi kilometa 25 kazi zinaendelea, sehemu ya Labay – Hydom kilometa 25) mkataba wa ujenzi umesainiwa tarehe 19 Mei, 2023 na sehemu iliyobaki itajengwa kupitia Mpango wa EPC + F wa barabara ya Karatu – Mbulu – Hydom – Sibiti River – Lalago – Maswa ambapo mkandarasi amepatikana na mkataba wa kuanza ujenzi umesainiwa tarehe 16 Juni, 2023, ahsante. (Makofi)
MHE. DANIEL T. AWACK aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa barabara za ndani za kilometa 10 katika Mji wa Karatu kwa kiwango cha lami iliyotolewa na Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Tlemai Awack, Mbunge wa Jimbo Karatu, kama ifuatvyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 barabara NBC - Kudu yenye urefu wa kilometa 0.6 ilijengwa kwa gharama ya shilingi milioni 350. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, ujenzi wa barabara za Tarafa - Ari Mpya, TRA - Mahakamani na NBC - Kudu zenye urefu wa kilometa 0.9 kwa gharama ya shilingi milioni 499.99 ambapo hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 78 na zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2022.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za Canivo - Buchani kilometa 0.53; Posta - Maliasili kilometa 0.10 na Bambras - Continental kilometa 0.100 zenye jumla ya urefu wa kilometa 0.73 zinaendelea kutekelezwa ambapo hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 70. Kwa upande wa mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya shilingi milioni 500 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara kilometa 0.62 kwa kiwango cha lami kwa barabara za Gorwa, Posta – Mailimbili, Bampras Continental na Rhotia Pharmacy. Serikali itaendelea kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara za Mji wa Karatu kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha.