Supplementary Questions from Hon. Abdallah Jafari Chaurembo (47 total)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga chuo cha VETA katika Kata ya Chamazi eneo ambalo limetolewa bure na UVIKYUTA zaidi ya ekari 30 ili kuwawezesha vijana wengi wa Kitanzania kuweza kujiajiri na kuweza kupata ajira katika fani mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi Serikali ina mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba katika kila mkoa na katika kila wilaya tunakuwa na Chuo cha VETA. Katika awamu ya kwanza tumefanya ujenzi ambao mpaka hivi ssa unaendelea katika wilaya 29, lakini katika awamu ijayo tunatarajia katika kila wilaya kupeleka vyuo hivyo. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika kila wilaya tutafikia kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni nini kauli ya Serikali kwa kumalizia kipande cha Mbande – Kisewe ambacho kimekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa Kata ya Chamazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, barabara ya Zakhem – Mbagala Kuu imepata fedha za Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar-Es-Salaam na imeshindwa kujengwa kwa sababu ya uwepo wa bomba la mafuta la TAZAMA. Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia walao corridor ya mita saba ili barabara hiyo ambayo tayari inayo fedha iweze kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi tunavyoongea sasa hivi, Mheshimiwa Chaurembo ni shahidi, tulikuwa na kilometa 6.05; kilometa moja imeshakamilika zimebaki kilometa 5.06. Nimhakikishie Mheshimiwa Chaurembo katika mwaka huu wa bajeti, kupitia fedha ya matengenezo, sasa tutaanza barabara ya kutoka Mbande kuja Msongola ambapo tunajenga kilometa 1.5 kwa kiwango cha lami. Pia kwa fedha ya maendeleo tutaendelea kutoka Msongola kwenda Mbande kilometa 1. Kwa hiyo, tutabakiwa kama na kilometa 2.5 ambazo zitakuwa bado hazijakamilika na fedha itakapopatikana tutaendelea kukamilisha barabara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kuhamisha bomba ama barabara Serikali imelipokea na itakwenda kulifanyia kazi tuone kama tutahamisha kwa sababu inapita karibu na bomba. Tutaangalia namna ya kufanya ili barabara ile muhimu sana iweze kuanza kujengwa. Pia kwa sababu suala hili siyo la Idara yangu pekee kwa maana ya Wizara ya Ujenzi ni Wizara nyingi, kwa hiyo, tumelipokea na tutakwenda kulifanyia kazi kuona ni namna gani tufanye kuhamisha barabara hiyo. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa umeme unaozalishwa katika Sub-station ya Mbagala ni chini ya asilimia 20 tu unaotumika Mbagala na asilimia zaidi ya 80 unaenda kutumika Mkuranga. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga sub-station kule Mkuranga ili kuwapoza watu wa Mbagala waendelee kutumia umeme wao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Jimbo la Mbagala ndiyo Jimbo ambalo lina watumiaji wengi wa umeme ukilinganisha na mikoa mingine ya Ki-TANESCO, je, Serikali ina mpango gani wa kulifanya Jimbo la Mbagala kuwa mkoa wa Ki-TANESCO?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Mbagala tunayo Sub- station inayozalisha Megawatts 48 na Megawatts 40 zinakwenda Mkuranga kama alivyosema kwa sababu kuna viwanda vingi sana pale zinabaki Megawatts 8 tu. Tunapata umeme wa Mbagala kutoka Ubungo kupitia Gongolamboto lakini tunapata umeme mwingine kutoka Kurasini. Pale Kurasini tunapata Megawatts kama 26 hivi, zinazoenda kujazia pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba umeme unapungua katika eneo la Mbagala kwa sababu mahitaji yamekuwa makubwa. Hata hivyo, kama tulivyosema kwenye swali la msingi, tunaongeza uwezo wa kituo hicho cha Mbagala kwa kuweka MVA 50 lakini pia cha Kinyerezi ambacho pia kitaleta umeme pale Mbagala.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali hilohilo ni kwamba tayari Serikali inafanya feasibility study ya kujenga sub-station nyingine kumi na kuziboresha nyingine kadhaa katika maeneo yetu ya Tanzania. Mkuranga kwa sababu ya umuhimu wake wa kuwa na viwanda vingi sana ni eneo mojawapo ambalo litapelekewa sub-station katika siku za hivi karibuni ili kupunguza mzigo mkubwa ambao vituo vyetu vya Mbagala na Kinyerezi vinaupata.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, Mkoa wa Dar es Salaam mpaka sasa unayo mikoa ya ki-TANESCO minne na hivi karibuni yamekuja maombi ya Kigamboni kuwa ni Mkoa wa ki-TANESCO na bado yanafanyiwa kazi. Niombe kwamba kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge amelisema, tutaenda kuangalia vigezo kwa sababu kuna kuangalia idadi ya wateja, makusanyo, line ya umeme mkubwa na mdogo katika eneo husika, vigezo vikikidhi basi, mamlaka husika zitaamua na huduma zitapelekwa karibu zaidi na wananchi.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo yanatia moyo, sasa nataka kujua; kwa kuwa Sera ya Serikali ni kuwa na Sekondari katika kila Kata: Je, ni lini sasa Serikali itajenga Shule za Sekondari katika Kata ya Mbagala, Kilungule na Kibonde Maji ambapo Kata hizo hazina Sekondari kabisa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuongozana nami kwenda katika Jimbo la Mbagala kujionea hali ya msongamano wa wanafunzi darasani katika Shule ya Mbande, Chamazi, Mianzini, Kilamba, Nzasa, Mbagala, Rangi Tatu, Mbagala Kuu, Mzinga, Kilungule na Kijichi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameainisha baadhi ya Kata hususan Kata ya Mbagala, Kilungule pamoja na Kibonde Maji ambazo mpaka sasa hivi hazina Sekondari; na Sera ya Serikali ni kwamba kila Kata lazima iwe na Sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Jimbo la Mbagala ambako anawapigania kwamba hizo Kata zote zitapata Sekondari za Kata ambazo zipo katika mpango wetu. Kwa sababu sasa hivi Serikali tuna mpango wa kujenga sekondari 1,000 nchi nzima katika zile Kata zote ambazo hazina sekondari. Kwa hiyo, miongoni mwa Kata tutapeleka Shule za Sekondari ni pamoja na Kata alizoziainisha; Kata ya Mbagala, Kilungule pamoja na Kiponde Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Mbunge alikuwa anaomba tuongozane tukaone msongamano katika shule ambazo ameziainisha hapa ikiwemo Mbande, Chamazi, Rangi Tatu, Mbagala Kuu, Mzinga, Kijichi na Kilungule; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, nipo tayari, hata akisema baada ya maswali na majibu twende, mimi nitakwenda kwa ajili ya hiyo kazi ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mchakato wa kuhakiki mali za wananchi pamoja na majedwali haya ya fidia ulianza toka mwaka 2018, je, wananchi wa Kokoto hadi Kongowe wanataka kujua wavumilie mpaka lini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, ni nini hatma ya wananchi wa Mbagala Rangitatu eneo la Charambe hadi kule Mbande ambao wamewekewa mawe ya hifadhi ya barabara toka mwaka 2010 na bila kupewa maelezo yoyote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaurembo, Mbunge wa Mbagala kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Mbunge wa Mbagala ambaye ni Meya Mstaafu wa Manispaa ya Temeke kilio chako kimesikika Mheshimiwa Mbunge na ndio maana Mheshimiwa Rais alitembelea katika eneo lako na ametoa maelekezo. Kiongozi Mkuu wa nchi akitembelea nchi hayo ni maelekezo sisi ni watekelezaji.
Mheshimiwa Spika, kilichofanyika ni kwamba ni fidia imefanyika, mkandarasi yupo pale site ataleta taarifa, watu wa TANROADS Mkoa wa Dar es salaam watapitia taarifa hiyo, tutafanya joint verification kwa maana ya Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Fedha na Valuer wa Serikali baada ya hapo wananchi wale watalipwa fidia. Maelekezo ni kwamba ujenzi hautaanza mpaka tuondoe vikwazo vya kulalamikiwa na wananchi baada ya kulipwa haki zao. Kwa hiyo, naomba wavute subira katika jambo hilo tunalifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili Mheshimiwa Mbunge anauliza habari ya mawe ambayo imewekwa pale katika road reserve ya Mbande kwenda Msongola mpaka Mvuti. Ni kweli kwamba wananchi baadhi walilipwa wakati huo, lakini tumekubaliana kwamba tukianza upanuzi wa barabara hiyo, yule mwananchi ambaye anafikiwa kwa wakati huo atakuwa analipwa fidia yake, hayo ndio majibu ya Serikali, ahsante sana.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa mgawanyo wa mali iliyokuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam haukuhusisha wadau wakiwepo Waheshimiwa Wabunge: -
Je, Serikali haioni sasa haja ya kuu-review ule mgao hasa katika ile mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu?
NAIBU SPIKA: Nataka kuamini ukisema Wabunge, unamaanisha pia na Madiwani hawakushirikishwa. Kwa sababu kama walishirikishwa Madiwani halafu Wabunge ndio hamkuwepo, ni ninyi ambao hamkuwepo. Hebu fafanua kidogo.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam hayakushirikishwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Jambo alilolita Mheshimiwa Abdallah Chaurembo ni kubwa sana ambalo linahitaji kwanza tufuatilie, tujiridhishe kwa sababu ninaamini kila jambo linapofanyika kunakuwa na muhtasari ambao huwa unaandikwa na vikao na idadi ya watu waliohudhuria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, endapo jambo hilo halikufanyika, basi ninaamini Ofisi ya Rais, TAMISEMI itazingatia namna bora kabisa ambayo itasaidia jambo hili liweze kufanyika kikamilifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunalipokea na tutakwenda kulifanyia kazi, ahsante sana.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Halmashauri ndiyo Mamlaka za Upangaji: ni lini Wizara ya Ardhi itakabidhi viwanja vya mradi wa viwanja 20,000 kwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ili kuyapangia matumizi mengine maeneo yote ya Taasisi ambayo hayakuendelezwa katika Kata ya Tuangoma na Kibada hasa katika Kiwanja kilichopo Goroka Block D, Block 10 Kiwanja Na. 219, Changanyikeni Block 9 Kiwanja Na. 215, mashamba pori ya NSSF ya Mtaa wa Masuliza, Mwapemba, Vikunai na Changanyikeni? (Makofi)
Swali la pili: Je, ni lini Wizara ya Ardhi itaweka miundombinu ya barabara katika mradi wa viwanja 20,000 katika maeneo yote ya Kata ya Tuangoma. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula, nataka tu niwaeleze Waheshimiwa Wabunge, alichosema Mheshimiwa Chaurembo ni kweli kwamba kwa mujibu wa Sheria Mamlaka za Upangaji wa Ardhi ni Halmashauri. Kwa hiyo, sisi kama Madiwani ni sehemu ya Mamlaka ya Upangaji wa Ardhi. Kila Halmashauri inapanga yenyewe matumizi ya ardhi yake. Ingawa tunashirikiana katika kuthibitisha ule upangaji, lazima uthibitishwe na Wizara ya Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dar es Salaam kuna mradi ulianzishwa miaka ya nyuma ya viwanja 20,000. Sasa leo nataka niseme hapa mbele ya Mheshimiwa Mbunge, viwanja 20,000 vilivyopimwa katika Wilaya ya Temeke, kwa mfano hivi vya Tuangoma iliyokuwa miradi 20,000 na Kibada, nimeshaagiza na ninarudia tena kuagiza, Wizara ya Ardhi ikabidhi michoro ya viwanja hivi 20,000 kwa Manispaa ya Temeke na wiki hii lazima makabidhiano yafanyike ili wananchi na Wilaya ya Kigamboni waweze kusimamia ipasavyo miradi hii ya viwanja 20,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, ulikuwa ni mradi ndani ya Wilaya ya Temeke, sasa michoro yote na taarifa zote za umiliki ziwe ni open space, maeneo ambayo hayajaendelezwa, Temeke liwe ni jukumu lao kufuatilia. Kama kuna watu hawajaendeleza Temeke ni Mamlaka halisi. Pekuweni tutoe notice kwa watu ambao hawajaendeleza tuchukue hatua mchukue ardhi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naagiza Kamishina wa Ardhi akabidhi michoro na taarifa zote. Kuanzia leo, eneo lote la Viwanja 20,000 la Kibada na Tuangoma lazima liwe chini ya Mamlaka ya Manispaa ya Temeke. Hayo mengine mtafanya wenyewe. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilini Serikali itajenga substation ya kule Mkuranga sambamba na kuweka transformer ya NVA 90 pale katika substation ya Mbagala ili kuondoa tatizo la ukatikaji wa umeme mara kwa mara katika jimbo la Mbagala?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jimbo la Mbagala linalo substation ndogo kama alivyosema ambayo ina transformer yenye uwezo wa AVA 50 NA substation hiyo inapeleka umeme mpaka maeneo ya mkulanga na kwa bahati nzuri ambayo inakuwa mbaya kwa upande mwingine. Eneo la Mkulanga limekuwa na viwanda vingi sana na hivyo linachukua umeme mwingi sana kutoka eneo la Mbagala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshaanza upembuzi wa kujenga kituo cha kupoza umeme eneo la Mkulanga ambacho kitakuwa kina zaidi ya Megawatt 100 lakini taratibu za kukamilisha ununuzi wa transformer ya AVA 90 itakayokuja kufungwa pale Mbagala zinakamilika na tunaamini kabla yam waka huu kuisha kituo cha Mbagala kitakuwa kimeongezewa uwezo wakati kule Mkulanga substation ikiwa inapatikana fedha kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nataka kujua wananchi wa Kokoto, Mzinga mpaka Kongowe ambao walithaminiwa zaidi ya miaka minne sasa, je, ni lini sasa Serikali itawalipa fidia zao ili ujenzi wa barabara hiyo uanze? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chaurembo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kokoto, Zinga, Kongowe ni kweli inasubiri fidia zifanyike ili barabara ianze ujenzi. Naomba nimhakikishie taratibu zinaendelea na Serikali, ili tukishapata tathmini na kupata fidia kamili tutaanza kuwalipa na utaratibu wa ujenzi wa barabara hii utaanza. Kwa sababu, hatuwezi kuanza ujenzi kabla ya fidia. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ina upungufu wa Walimu 6,300. Je, Serikali haioni haja ya kuleta Walimu wapya kujaza nafasi zote za Walimu waliofariki na kustaafu wa Manispaa ya Temeke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chaurembo Abdallah, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, watumishi wetu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na maeneo mengine ya Serikali, wale ambao kwa sababu moja ama nyingine wanastaafu ama kufariki dunia, utaratibu wa kujaza nafasi zao unafuata utaratibu wa ajira za kawaida, lakini kwa kuzingatia uhitaji katika halmashauri husika.
Kwa hiyo, wale watumishi ambao katika Halmashauri ya Temeke wamestaafu, wanafahamika idadi yao, lakini waliofariki idadi yao inafahamika na wakati wa vibali vya ajira moja ya maeneo ambayo yanawekewa kipaumbele ni kujaza nafasi hizo. Nakushukuru.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi; nataka nijue ni lini ujenzi wa barabara wa Mbande - Kisewe - Msongola utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii itaanza kujengwa kama tulivyoipanga kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, kutokana na majibu hayo ya Serikali: Je, Serikali haioni ipo haja sasa ya kutoa ufafanuzi kwa wananchi hao ya tofauti kati ya fidia na kifuta machozi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili: Je, kutokana na malalamiko ya wananchi hao kuwa mengi, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuongozana nami jimboni ili kwenda kuwasikiliza wananchi hao na hatimaye kutatua matatizo hayo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaurembo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nianze na swali la pili kwamba niko tayari wakati wowote kufuatana na Mheshimiwa Mbunge ili kwenda kuwasikiliza wananchi. Bahati nzuri nilipata fursa ya kukutana na baadhi yao na kwa niaba yangu alikutana nao Mheshimiwa Jafo Dar es Salaam, na tulipokea barua yao na baadhi yao tunaendelea kuwasiliana nao. Tutafanya hivyo ili tukawasilikilize kule kule kwa sababu ndiyo kazi ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni ufafanuzi wa tofauti ya maafa au fidia na kifuta machozi. Maafa yanasababisha na majanga, majanga na huwa si jambo lililopangwa au kutarajiwa, majanga yanaweza kutokana na nguvu za asili, inaweza ikawa na mafuriko, au Tsunami, pia majanga yanaweza yakatokana na matokeo mbalimbali ya nguvu ambazo siyo za kawaida. Inaweza ikawa ni mlipuko wa magonjwa, na yenyewe hayo pia ni majanga.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, yanapotokea maafa, huwezi ukayawekea utaratibu wa kulipa fidia. Kwa hiyo, hakuna utaratibu wa fidia kwa majanga, bali ambacho hutokea, jamii au Serikali huweza kutoa kifuta machozi au mkono wa pole kwa walioathirika. Kwa hiyo, Serikali ilifanya hivyo na iliwalipa kifuta machozi. Pia Serikali ililipa kifuta machozi kiasi cha Shilingi 17,464,944,954/=, fedha hizi ni nyingi.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali ilishughulikia mazishi ya wale ambao walifariki katika tukio lile. Naomba kuwasilisha.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa kutoka Mbagala Kokoto mpaka Kongowe ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo ambayo umetengewa fedha katika mwaka huu wa fedha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chaurembo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ya Kokoto kwenda Kongowe, hawa wananchi watalipwa fidia pale ambapo barabara hii itaanza kujengwa, ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua ni lini ujenzi wa kipande cha barabara kutoka Mbande - Kisewe mpaka Msongola utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chaurembo Mbunge wa Mbagala kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja iko kwenye mpango na tunategemea utekelezaji utaanza mwaka huu wa bajeti.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la uhalifu katika Mikoa mbalimbali nchini. Je,Serikali ina mkakati gani wa kuunga mkono juhudi za wananchi nchi nzima ambao wameanzisha ujenzi wa Vituo vya Polisi ili kuweza kuvimalizia na hatimaye ulinzi uweze kuwa imara?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chaurembo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza uwepo wa wimbi la uhalifu ambao tumekuwa tukisema hapa uhalifu ni matokeo ya tabia na mwenedo wa jamii tunaupiga vita kwa nguvu zetu zote. Ndiyo maana yalivyojitokeza matukio haya ya panya road, ni jeshi halikulala hatimaye nchi imekuwa tulivu pia niwapongeze wananchi kwa kujenga Vituo vya Polisi mahala vinakohitajika ili mapolisi wawe karibu na wananchi.
Mheshimiwa Spika, kama nivyosema kwenye majiibu yangu ya msingi ya maswali yaliyopita, pale ambapo wananchi wamefanya kazi niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuwasiliane na ma-OCD wetu na ma-RPC kwenye Mikoa yetu waweze kufanya tathmini kwenye kiwango cha ujenzi kilicho fikiwa na nini kinatakiwa kukamilisha, ili tuweze kuingiza kwenye mpango wa ugaramiaji kitaifa. Tukilifanya hilo itakuwa rahisi kuingizwa kwenye mipango. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muda wa ujenzi wa barabara hii umekwisha, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha barabara hii inaisha haraka ili kuondoa msongamano katika Barabara ya Kilwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, ni lini Serikali itamalizia kwa kiwango cha lami kipande cha kilometa tano cha Mbande- Kisewe mpaka Msongora?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaurembo Abdallah, Mbunge wa Mbagala, kwa pamoja, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza tutahakikisha kwamba barabara ile kipande ambacho kimebaki cha kilomita tano chote tunakijenga kwa kiwango cha lami ikiwa ni pamoja na kukamilisha daraja ambalo limeshakamilika na sasa tunachoendelea ni kuweka lami pale juu kwenye daraja ambalo tunalijenga.
Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kufikia mwakani barabara ile yote tutakuwa tumeijenga kwa kiwango cha lami ikiwa ni pamoja na kukamilisha hilo daraja ambalo lilikuwa ni changamoto kubwa sana kwa wananchi ambao wanatumia barabara hiyo.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Wizara inafahamu kwamba baadhi ya maeneo mtandao wa maji haujafika; je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia maji wananchi hawa kwa dharaura?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Naibu Waziri yupo tayari kuongozana nami kwenda kuona adha kubwa wananchi wa kata hizi wanazopata katika kukosa maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali yake mawili, Mheshimiwa Abdallah Chaurembo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mkakati wa dharura, mara zote DAWASA imekuwa ikijitahidi kuona inafanya kila linalowezekana wananchi wasikose maji kabisa, lakini nawaomba uvumilivu kwa sababu visima tisa ambavyo tunatarajia kuja kuvichimba katika maeneo yale ya Kimbiji; na tutajenga tenki kubwa maeneo ya Lugwadu la Shilingi milioni 15. Haya matatizo yatakoma kabisa.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi jitihada ndogo ndogo zinazoendelea kufanywa na DAWASA, naomba tuendelee kuwavumilia. Kuongozana nawe ni sehemu ya majukumu yangu, hakuna neno, tutakwenda kufanya kazi. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nilitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kulipatia Jimbo la Mbagala maji safi na salama yenye uhakika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Chaurembo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, maeneo hayo ya Mheshimiwa Mbunge tayari kuna miradi inayoendelea, ipo kwenye utekelezaji hatua za mwisho. Hivi punde maji safi na salama yataunganishwa katika existing lines ili wingi wa maji uweze kuongezeka kwa wananchi. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nataka kujua ni lini Serikali itajenga kipande cha Barabara kutoka Mbande Kisewe mpaka Msongola ili kuunganisha Wilaya ya Temeke na Wilaya ya Ilala?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chaurembo, Mbunge wa Mbagala kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama tulivyoongea barabara hii imeshakabidhiwa kwa Manager wa Mkoa wa Dar es Salaam kukamilisha hicho kipande kidogo sana ambacho kimebaki kwa kiwango cha lami.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua sasa barabara ya kutoka Kokoto mpaka Kongowe ni lini upanuzi wake utaanza?
Mheshimiwa Naibu Spika, na swali la pili, Je, ni lini sasa barabara ile ya kutoka Mbande Kisee mpaka Msongora ambayo imekuwa ni adha kwa wapiga kura wa Dar es Salaam ujenzi wake utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na barabara ya pili Mbande kwenda Msongora kilomita hizo tatu ambazo zimebaki tunategemea zitaanza kutekelezwa katika bajeti hii tunayoanza kuikamilisha. Na barabara hii ya Kokoto kwenda Kongowe upanuzi wake, naomba Mheshimiwa Mbunge asubiri tuone kwenye bajeti tumependekeza tufanye nini. Tunajua tayari kuna changamoto kubwa tuweze kuitekeleza hii barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati barabara ambazo zimeathirika na mvua katika Jimbo la Mbagala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni mkakati wa Serikali kutengeneza barabara hizi na ndiyo maana TARURA walikuwa na emergency fund ya shilingi bilioni 11 na sasa wameomba tena nyongeza iweze kufika shilingi bilioni 46 kwa ajili ya kutengeneza barabara hizi za Mbagala na za maeneo mengine ya Waheshimiwa Wabunge ambayo yameathiriwa na mvua ambazo zimeendelea kunyesha hapa nchini.
MHE. MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara nyingi za Jiji la Dar es Salaam, hasa zile zilizo chini ya TARURA huhitaji matengenezo ya mara kwa mara. Je, Serikali haioni ipo haja kwa TARURA kuwa na kitengo maalum cha matengenezo badala ya kuwatumia Wakandarasi?
Swali la pili, kwa kuwa Jimbo la Kinondoni linazungukwa na mito midogo midogo ambayo husababisha mafuriko hasa katika Kata za Mwanayamala, Kijitonyama, Tandale, Kigogo na Ndugumbi. Je, Serikali ipo tayari kufanya upembuzi wa kitaalam ili kubaini njia bora za kukabiliana na hali hii ya mafuriko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la kwanza la Mheshimiwa Tarimba la je, TARURA ipo tayari kuanzisha kitengo maalum kwa ajili ya kuangalia ukarabati wa barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuanzisha kitengo maalum kunahitaji rasilimali fedha, rasilimali watu na vifaa. Hivyo basi, kwa sasa TARURA inaona ni bora kufanya outsourcing kwa sekta binafsi. Hii pia inasaidia kutoa ajira kwa Watanzania wengine ambao wanafanya kazi katika sekta binafsi. Vilevile ina-assure quality control na kunakuwa kuna checks and balances akipewa mtu na TARURA wakamkagua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, tayari mito ya Jimbo la Kinondoni imetengewa fedha kwenye Mradi wa DMDP II ambao utaanza Novemba, mwaka huu 2023. Kwenye DMDP I tayari walikuwa wameshatengenezewa Mto Ng’ombe ambayo imezuia mafuriko makubwa sana katika maeneo yanayozunguka barabara hizi na makazi ya watu wa Jimbo la Kinondoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ni lini mabomba yaliyosambazwa katika Kata mbalimbali ya Jimbo la Mbagala yataanza kutoa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chaurembo, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mabomba yaliyosambazwa lazima mwisho wa siku yatoe maji, miradi yetu sisi inapokamilika lazima mwisho wa siku itoe maji. Hivyo nikutoe hofu Mheshimiwa Mbunge maeneo yote ambayo tumeshasambaza unafahamu kazi nzuri ya DAWASA inayoendelea kufanyika, kuna matenki makubwa yameshakamilika na sasa hivi yamebakia kwenye hatua za mwisho kabisa ili yaweze kufikia maeneo yote ambayo tayari yana mtandao.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri. Naomba kuuliza, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuokoa wananchi wa Mikwambe hasa Mtaa wa Zahanati, Rushe, Chambaruba A na B ambao wanaathirika na kutokuwa na mifereji katika barabara hiyo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni upi mkakati wa Serikali wa kujenga mifereji katika barabara zote za lami zilizopo katika Jimbo la Mbagala?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaurembo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza na la pili Mheshimiwa Chaurembo anaulizia mkakati wa kuhakikisha barabara ambazo tunaweka lami hasa hasa kwenye majiji ni barabara ambazo ni kama barabara za mitaa. Mpango wetu ni upi katika kuhakikisha tunajega mifereji ama mitaro?
Mheshimiwa Spika, Wizara chini ya TANROADS tunayo program ya kuhakikisha barabara ambazo tunaweka lami, tunajenga na mitaro, lakini hata barabara ambazo ni za changarawe pia programu hiyo tunayo.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu Mamlaka ya Hali ya Hewa imetabiri mvua kubwa za El-Nino. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na nitumie nafasi hii kutoa maelekezo kwa Meneja Mkuu wa TANROADS kushirikiana na TARURA kuhakikisha barabara za TANROADS ambazo maji yanaenda kwenye barabara za TARURA wakae mara moja hasa hasa kwenye maeneo ya majiji na manispaa kujiandaa na kuhakikisha tunajitayarisha vyema kuhakikisha mvua za El-Nino zitakazonyesha basi mifereji na mitaro tutakuwa tumeitengeneza vizuri ili kuwaepushia wananchi maafa ambayo yanaweza yakatokea kwa mvua kubwa na mifereji kutokuwa vizuri.
Mheshimiwa Spika, hili la Mheshimiwa Mbunge tumelichukua, lakini nimeona nitoe maelezo ya jumla hasa kwenye majiji na manispaa Mkurugenzi Mtendaji wa TANROADS ajipange na Mkurugenzi Mtendaji wa TARURA ili tuweze kulifanya kwa ufasaha, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga madaraja ya kuunganisha Jimbo la Mbagala na Jimbo la Mkuranga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kujenga madaraja ya kuunganisha Wilaya hizi mbili au Mikoa hii miwili, Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa sasa, tumeweka daraja la Mto Kitonga kuhakikisha katika mradi wa DMDP II ambapo fedha hizi zitakapopatikana kuanzia mwaka wa fedha huu Novemba, 2023 tutaanza utekelezaji wa kujenga daraja hili. Barabara hii ni ya muhimu sana kwa sababu kuna huduma nyingi za mchanga unaotoka katika Wilaya ya Mkuranga kuelekea Mkoa wa Dar es Salaam inapita katika barabara hii.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Barabara ya Kigamboni mpaka Kongowe eneo la Mikwambe lina tatizo ya mifereji: Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mifereji katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja, siyo tu mifereji, bali pia ni barabara ambayo kuna vipande vingi ambavyo vimechoka sana. Kwa hiyo, mpango wa Serikali pamoja na kutengeneza mifereji, pia ni kukarabati yale maeneo yote ambayo yamechakaa sana, ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi. Mtaa wa Mikwambe Kata ya Twaangoma kuna mgogoro wa kisima cha maji ambacho kimejengwa katika kiwanja ambacho amemilikishwa mtu binafsi. Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua mgogoro huo ili wananchi waendelee kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chaurembo kama ifauatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mgogoro huo upo lakini DAWASA tayari wanaufanyia kazi na kwa niaba ya Wizara DAWASA watahakikisha mgogoro huu unaisha kwasababu maeneo ya aina hii yamekuwa mengi na tumekuwa tukimaliza. Kwa hiyo, hata hili pia sisi kama Wizara tutahakikisha linakamilika ili huu mradi uweze kutoa huduma kwa wananchi.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa barabara na kwa kuwa nyumba zilizo mbele ya Barabara hii, viwanja vyake vilipimwa na mamlaka ya upangaji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufidia walau mita sita ili wananchi wa eneo hili wapate Barabara ya uhakika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili nini hatma ya barabara ya Mabwawa ya Samaki na Mlima habarizenu iliyopo katika Kata ya Mianzini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdallah Chaurembo. La kwanza hili la kipande cha mita 400 kilichosalia katika barabara hii ya Zakhiem.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara hii kwa kumbukumbu zangu ni barabara ambayo inaunganika na maandazi road ambayo barabara hii ya Maandazi Road imewekwa katika mpango wa DMDP II. Sasa kwa sababu ni mita chache kutoka pale tutakaa na wenzetu wa Manispaa ya Temeke na vilevile tutakaa na wenzetu wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam kuona ni namna gani tunaweza tukachepusha barabara hizi mita 200 kwa kuona kama tunaweza kuingiza katika mpango wa kulipa fidia. Halmashauri wenyewe baada ya kufanya tathmini walipe fidia kwa ajili ya kuchepusha barabara hii ili iweze nayo kuingizwa katika mipango ya kuwekewa lami au zege ili wananchi hawa waweze kupata huduma sahihi wanayostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili, barabara hii aliyoitaja ya Bwawa la Samaki hadi Kilima cha Habaribzenu. Naomba nitumie nafasi hii kumwelekeza Meneja wa TARURA wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kufika katika barabara hii na kuweza kufanya tathmini na kuona ni namna gani inaweza ikatengewa fedha ya kuweza kutengeneza ili iweze kupitika wakati wote.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Kokoto mpaka Mwandege ndiyo lango kuu la magari yanayotoka Kusini. Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua barabara hiyo ili kupunguza msongamano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Katika bajeti ambayo tumeitenga mwaka ujao na kweli nakubaliana kuna changamoto kubwa sana. Pale ambapo BRT II inaishia mwaka ujao tunaanza kutekeleza mradi wa kujenga kilometa 3.8 kwa barabara hizo nne, lakini mpango ni kwenda mpaka Vikindu kwa ajili ya kujenga hizo barabara nne kupunguza changamoto ya msongamano wa hizo barabara.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua ni lini Serikali itakijenga kwa hadhi ya Kituo cha Polisi Mbagala?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chaurembo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli swali hili ni moja ya maswali ambayo yako kwenye mpango wa kujibiwa, lakini niseme tu kwamba tunajua Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwemo Wilaya ya Temeke, na Majimbo ya Mbagala, na majimbo mengine ya maeneo ya Kigamboni, kuna vituo vidogo vya Polisi vingi kuliko vituo vya ngazi ya wilaya. Tunaendelea na mpango mkakati wa ujenzi wa vituo hivi kwa kuangalia maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa kutokana matukio ya uhalifu ili kuyazingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini Mbagala kwa sababu ya wigi wake wa watu, matukio ya uhalifu pia yatakuwa mengi, tutakizingatia katika mpango huu wa ujenzi.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, wananchi waliokuwa pembeni ya barabara inayotoka Kongowe mpaka Kokoto wamefanyiwa uthamini zaidi ya miaka mitatu sasa.
Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi hao ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Chaurembo, Mbunge wa Mbagala kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wananchi wa Mbagala ambao wamewekewa alama ya kupisha eneo hili la mradi huu kwamba kabla ya kuanza ujenzi Serikali itahakikisha inawalipa fidia yao. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatafuta fedha kwanza kuanza kwa ujenzi na kuwalipa hao wananchi fidia yao. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi. Ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Mbande Kata ya Chamazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdallah Chaurembo Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza tunatambua juhudi za Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo lake Mbagala kwa juhudi wanazofanya katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Kwa kutambua juhudi hizo, nasi kama Serikali kupitia Jeshi la Polisi tutatembelea Kituo cha Mbande kutathmini kiasi gani kinahitajika ili kuweza kumalizia na hivyo kutoa mchango wetu ili kukamilisha kituo hicho kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za wananchi.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itajenga transfoma yenye uwezo wa MVA 90 katika substation ya Mbagala iliyoko katika Jimbo la Mbagala?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chaurembo, Mbunge wa Mbagala kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Jimbo la Mbagala ni moja ya maeneo ambayo yana mahitaji makubwa ya umeme, lakini miundombinu ni finyu, kwa hiyo kumekuwa na changamoto kubwa ambayo Mheshimiwa Mbunge amekuwa anatuletea mara kwa mara, ya kadhia ya kukatika kwa umeme au umeme kuwa na nguvu ndogo.
Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa njema Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Mbagala, kwamba Serikali tayari imekwisha kuagiza transfoma hiyo kubwa kwa ajili ya kufungwa katika kituo cha kupoza umeme Mbagala na kabla ya mwaka ujao wa fedha kwisha transfoma hiyo itakuwa imefungwa na kuweza kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Jimbo la Mbagala, lakini na Majimbo mengine Temeke na mkoa mzima wa Dar es salaam kwa ujumla. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga stendi ya mikoani katika Jimbo la Mbagala hasa Mikoa ya Kusini?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdallah Chaurembo, Mbunge wa Mbagala kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Mbagala ni eneo ambalo wananchi wengi wa Mikoa ya Kusini wanatumia kama sehemu ya kufikia au kuanza safari kuelekea mikoa ya Kusini, kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Mbunge lakini niagize Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kufanya tathimini ya uwezekano wa kutekeleza mradi huu kwa maana ya kupata eneo, lakini pia kufanya makadirio ya gharama ili tuweze kuona kama Serikali nini kinaweza kikafanyika. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, je, Serikali ina mpango gani wa kuzitumia fedha zilizobaki katika utekelezaji wa mradi huu wa DMDP Awamu ya Kwanza katika kuziboresha barabara za Jimbo la Mbagala na Jimbo la Temeke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdallah Chaurembo, Mbunge wa Jimbo la Mbagala kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tumepokea ushauri na tutakwenda kushauriana na wataalam juu ya utekelezaji wa mabaki wa hizo fedha ambazo zimebakia, ahsante sana.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi. Ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Mbande Kata ya Chamazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdallah Chaurembo Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza tunatambua juhudi za Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo lake Mbagala kwa juhudi wanazofanya katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Kwa kutambua juhudi hizo, nasi kama Serikali kupitia Jeshi la Polisi tutatembelea Kituo cha Mbande kutathmini kiasi gani kinahitajika ili kuweza kumalizia na hivyo kutoa mchango wetu ili kukamilisha kituo hicho kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za wananchi.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, ni lini ujenzi wa Barabara ya Mbagala Rangi Tatu mpaka Kongowe ambayo ipo katika bajeti ya mwaka huu utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, barabara hiyo kilometa 3.8 imeshapata kibali cha kutangazwa ili ianze kujengwa. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itasambaza maji yanayotoka kwenye Visima vya Kisarawe Two katika Kata ya Toangoma?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Chaurembo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, visima vya Toangoma tayari DAWASA wanaendelea na jitihada kuona wanakwenda kusambaza maji, wataanza mwaka huu wa fedha na mpaka kufika mwaka ujao wa fedha maeneo yale yote ambayo yapo ndani ya mradi yatakwenda kufikiwa.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, ni lini ujenzi wa Barabara ya Mbagala Rangi Tatu mpaka Kongowe ambayo ipo katika bajeti ya mwaka huu utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, barabara hiyo kilometa 3.8 imeshapata kibali cha kutangazwa ili ianze kujengwa. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, je, kutokana na ongezeko kubwa la watu katika Jimbo la Mbagala, Serikali haioni ipo haja ya kuanzisha Kituo cha Uokoaji na Zimamoto katika Jimbo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Chaurembo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tumezingatia hilo na ndiyo maana unaona katika mpango unaokuja, tunaleta magari karibu 100 yatakayogawiwa nchi nzima na Mbagala tutaiangalia kwa upekee wake. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi zahanati ambazo zimekidhi vigezo kuwa vituo vya afya katika Jimbo la Mbagala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati ambazo zimekidhi vigezo vya kuwa vituo vya afya tumeshaelekeza halmashauri, kwa maana ya Mganga Mkuu wa Halmashauri, Mkurugenzi kupitia kwa Katibu Tawala wa Mkoa kuleta maombi maalum Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili na sisi tuweze kuwasiliana na Wizara ya Afya na kusajili na kupandisha hadhi ikiwa vinakidhi kwa miundombinu na population. Kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kumkumbusha Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke kufuata utaratibu huo mapema iwezekanavyo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa halmashauri nyingi sasa zimeonesha uwezo wa kununua mitambo kwa ajili ya kuchonga barabara, je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha vitengo maalumu vya maintenance katika halmashauri hizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni mawazo mazuri sana ya Mheshimiwa Mbunge, tumeyapokea, tutayachakata na tutayafanyia kazi. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, je, NSSF haioni ipo haja sasa ya kuendelea kujenga madaraja na barabara kwa kutumia mtindo huu kama ilivyofanya katika daraja la Nyerere? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali haioni sasa ipo haja baada ya NSSF kumaliza mkataba wao daraja hili likapitika na wananchi wa Temeke na Mbagala bila kutozwa chochote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Chaurembo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, moja, NSSF itaendelea kuwekeza kwenye miradi yote yenye tija na ile ambayo inaenda kulenga kutoa huduma kwa wananchi na kurahisisha maisha kwa wananchi wote na hasa katika kuangalia pia ulindaji wa thamani ya fedha ya mfuko wa wanachama wa NSSF. Kwa hiyo, tutaendelea kuwekeza kwenye maeneo yote ambayo yatakuwa yana tija lakini pia ambayo yatakuwa yanaenda kuhudumia wananchi walio wengi ili kuweza kuleta ule ustawi wa wananchi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusiana na tozo baada ya gharama za mradi kurejeshwa na daraja hili kukabidhiwa Serikalini, hatua nyingine zitafuata na itakuwa ni mali ya Serikali na maamuzi yatafanyika kwa namna ambayo itaruhusu wananchi wote kuweza kulitumia bila kuwa na gharama, ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha zege Barabara ya Tinyango kuunganisha na Machimbo katika Kata ya Chamazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa ya uwakilishi anayofanya na ya kuwasemea wananchi wake na hasa kwenye masuala ya miundombinu ya barabara. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na barabara hii ya Tinyango anayoitaka ijengwe kwa kiwango cha zege kwamba barabara hii ipo kwenye mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka fedha zinatengwa kwa ajili ya kuendeleza barabara zetu hizi za wilaya na nimhakikishie kwamba ni kwa kadiri ya fedha zitakavyokuwa zinapatikana. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba inafikia barabara zote ikiwemo barabara hii aliyoitaja ya eneo la Tinyango. Kwa hiyo, tutalifikia Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, je, ni lini tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara katika Jimbo la Mbagala litaisha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante, nashukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Abdallah Chaurembo. Nimhakikishie kwa kweli siyo kama ilivyokuwa mwaka jana, kwa kiasi tumepunguza kukatiwa kwa umeme katika Jimbo la Mbagala. Lakini, Mheshimiwa Mbunge, tunatekeleza mradi wa kuongeza transfoma pale kwenye kituo cha kupooza umeme cha Mbagala.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tukimaliza mradi huu wa kupanua kituo kile cha kupooza umeme pale Mbagala, basi tutakuwa tumemaliza kwa kiasi kikubwa changamoto ya kukatika kwa umeme. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge atupe subira kidogo ili tuweze kukamilisha mradi. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itaanza kurekebisha barabara zilizopata athari ya mvua hizi katika Jimbo la Mbagala na ukizingatia mvua sasa zimeisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa Serikali inatambua madhara makubwa ambayo yamejitokeza kwenye barabara zetu hizi kutokana na mvua. Nikupe taarifa bajeti maalum ya bilioni 350 imepatikana kwa ajili ya kuhudumia barabara hizi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge, baada ya mvua kuisha katika mwaka mpya wa fedha, tayari ataanza kuona wakandarasi wanaingia site kwa ajili ya kuanza kufanya marekebisho ya barabara hizo, ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Barabara ya Mwendokasi inayotoka Gerezani, Kariakoo mpaka Mbagala itafunguliwa na mabasi kuanza kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA(MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa sana kwa kujenga Barabara ya Mwendokasi toka Gerezani kwenda Mbagala. Nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara ile iko hatua za mwisho kabisa na hivi karibuni itaanza kutumika kwa ajili ya kusafirisha wananchi katika eneo hilo. Ahsante. (Makofi)