Primary Questions from Hon. Dorothy George Kilave (15 total)
MHE. DOROTHY G. KILAVE Aliuliza:-
Serikali ilitenga eneo la Kurasini EPZ tangu mwaka 2014 kwa ajili ya uwekezaji lakini hadi sasa eneo hilo halijaendelezwa kama ilivyokusudiwa.
Je, kwa nini Serikali isirejeshe eneo hilo kwa Halmashauri ya Temeke ili lipangiwe shughuli za maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy Kilave, Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Serikali kupitia Mamlaka ya EPZ ilianza mchakato wa kutwaa ardhi eneo la Kurasini mwaka 2014 kwa madhumuni ya kujenga Kituo cha Biashara na Ugavi wa Vifaa. Hatua mbalimbali za kuendeleza eneo hilo zimefanyika zikiwemo ulipaji wa fidia, kusafisha eneo kwa kubomoa majengo yaliyokuwepo, kufanyika kwa upembuzi yakinifu wa awali na kupatikana kwa hatimiliki. Hatua inayoendelea sasa ni tathmini ya mazingira na maandalizi ya mpango kabambe (conceptual master plan) inayofanywa kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa.
MheshimiwaNaibu Spika, Wizara katika Bajeti yake ya mwaka 2020/2021 imetenga fedha kwa ajili ya uendelezaji wa miundombinu ya mradi awamu ya kwanza ikiwemo ujenzi wa uzio kuzunguka eneo la mradi. Tayari Mamlaka ya EPZ imeingia mkataba na Kitengo cha Ujenzi cha Jeshi la Kujenga Taifa kwa ajili ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa nia ya Serikali katika kutekeleza mradi huu wa kielelezo kwa mujibu wa Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa iko pale pale na pia nitumie fursa hii kuomba ushirikiano wake na Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kwa ujumla ili kufikia azma ya Serikali kupitia uendelezaji wa mradi huu kwa malengo yaliyokusudiwa. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dorothy Kilave swali la nyongeza.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Waziri, lakini naomba sasa niseme kwamba sasa ni miaka karibu saba tangu mmelitwaa hili eneo.
Je, haiwezekani kwamba mtachukua tena miaka saba kwa ajili ya kulirekebisha na kuweka mpango huo? Niombe basi kama nilivyosema kwamba wananchi wa Temeke tunatamani kujenga shule za sekondari na msingi kwa sababu tunazaliana sana na maeneo mijini sasa hivi hakuna. Niseme tu kwamba tuombe sasa Wizara yako itupe eneo hili ili sisi katika miaka hii ambayo tumeambiwa tujenge shule za sekondari pamoja na msingi basi tuyapate kwa sababu naona mtakwenda tena miaka saba ijayo katika kutengeneza hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; je, Serikali yetu sasa ina mpango gani wa kumalizia fidia kwa wananchi wa maeneo ya jirani karibu na pale ambapo mmetwaa lile eneo lakini yapo maeneo Shimo la Udongo ambapo mlitakiwa kuyatwaa lakini bado hamjalipa fidia. Naomba maswali yangu haya mawili tuweze kujibiwa. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE Aliuliza: -
Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Buza/Nzasa – Kilungule pamoja na daraja litamalizika hasa ikizingatiwa kuwa barabara hiyo inawaunganisha wananchi wa Temeke na Mbagala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave Mbunge wa Jimbo la Temeke kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mradi unatekelezwa kupitia DMDP, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke inatekeleza Mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Nzasa – Kilungule – Buza yenye urefu wa kilometa 7.6. Kati ya hizo kilometa 5.4 zinajengwa kwa kiwango cha lami na kilometa 2.2 kwa kiwango cha zege; na ujenzi wa stendi ya mabasi Buza fungu namba 14 wenye thamani ya shilingi bilioni 19.13 bila VAT, chini ya Mkandarasi Mjenzi Group Six International Ltd. Fedha hizi ni Mkopo wa Serikali kutoka Benki ya Dunia na unaotekelezwa kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa mradi huu ulianza kutekelezwa tarehe 01 Aprili, 2020 na unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Oktoba, 2021. Mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 69 na fedha kiasi cha shilingi bilioni 8.05 zimelipwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kufanya matengenezo ya miundombinu ya barabara za Jimbo la Temeke kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaajiri Walimu wa Sayansi katika Shule za Sekondari za Kata Wilaya ya Temeke pamoja na kumaliza tatizo la uhaba wa Vifaa vya Maabara kwenye shule hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Temeke, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 iliajiri Walimu 6,949 ambapo kati yao asilimia 79 walikuwa Walimu wa sayansi ambao walipangiwa vituo katika Shule za Sekondari za Serikali, kipaumbele kikiwa ni shule zenye upungufu mkubwa kulingana na mahitaji ya wakati huo. Serikali imefanya tathmini ya mahitaji ya Walimu wa sayansi katika shule za sekondari na kubaini kuwa Manispaa ya Temeke ina upungufu wa Walimu wa Sayansi 631, sawa na asilimia 71.05 ya mahitaji. Serikali itaendelea kuajiri Walimu wa fani zote na kuwapangia vituo kulingana na mahitaji ya shule za sekondari zote nchini, zikiwemo Shule za Sekondari za Manispaa ya Temeke.
(b) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/ 2021, Serikali ilinunua na kusambaza vifaa vya maabara katika Shule za Sekondari za Kata zipatazo 1,258 nchini zikiwemo shule 14 Manispaa ya Temeke ili kuwafanya wanafunzi waweze kujifunza kwa vitendo masomo ya Sayansi. Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ya Elimu nchini itaendelea kununua na kusambaza shuleni vifaa vya maabara katika shule za sekondari nchini, zikiwemo Shule za Sekondari za Manispaa ya Temeke. Ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -
Je ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa Ardhi kati ya Wananchi na Serikali katika Kata ya Yombo Vituka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na Serikali ili kupisha ujenzi na upanuzi wa Shule ya Msingi Uwanja wa Ndege, ulihitimishwa tarehe 26 Septemba, 2022 baada Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali Shauri la Rufaa Na. 116/2019 lililofunguliwa na walalamikaji 56 ambao walishindwa kuthibitisha madai yao.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka Madaktari Bingwa na Wataalam wa Vifaa Tiba katika Hospitali ya Malawi ambayo ipo Kata ya Buza Temeke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kituo cha kutolea huduma za Afya cha Malawi bado hakijapandishwa hadhi kuwa Hospitali. Kwa sasa Kituo hicho kinatambulika kama Kituo cha Afya - Malawi ambacho hakijakidhi vigezo vya hitaji la kupelekewa Madaktari Bingwa kwa kuzingatia mwongozo wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa sasa inaendelea na taratibu za kuongeza Vifaa Tiba kwenye Kituo hicho. Aidha, Halmashari inaelekezwa kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu inayohitajika ili kiendane na hadhi ya Hospitali na kuombewa kupandishwa hadhi.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza gharama za malipo kwa Akinamama wanaojifungua kawaida na wale wa operesheni?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya inaendelea kutekeleza Sera ya Afya ya mwaka 2007 inayoelekeza kutoa huduma za matibabu bure kwa makundi maalum, ikiwemo akinamama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano. (Kipengere 5.3.4 chenye Tamko linalosema “Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inayotoa huduma bila faida na mashirika ya Kimataifa itaendelea kutoa huduma bila malipo kwa wanawake wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano”).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vituo vya binafsi visivyo na ubia na Serikali ukamilishaji wa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote utakapopitishwa utakuwa suluhisho la tatizo hili.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -
Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi waliohamishwa kupisha maegesho ya malori eneo la Kurasini tangu mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa uthamini uliofanyika mwaka 2013 na ulipaji wa fidia kufanyika Mwaka 2015, Mwekezaji katika mradi huo alitoa shilingi bilioni 16.83 kwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa ajili kulipa fidia ambapo wananchi 165 waliofanyiwa uthamini ili kupisha mradi huo wamelipwa fedha zao kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya malipo hayo kukamilika, wananchi 44 kati ya 165 waliolipwa fidia hawakuridhika na malipo yaliyofanyika, hivyo wakafungua kesi ya madai ya mapunjo ya shilingi bilioni 3.198 katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kupitia Shauri Namba 50 la mwaka 2016. Tarehe 28 Mei, 2021, Mahakama ilitupilia mbali shauri hilo baada ya wananchi hao kushindwa kuthibitisha madai yao, hivyo, hakuna fidia inayodaiwa na maeneo yaliyotwaliwa kupisha ujenzi wa maegesho ya malori katika eneo la Kurasini kwani wananchi wote wamelipwa kwa mujibu wa sheria, ahsante.
MHE. JANEJELLY J. NTATE K.n.y. MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -
Je, nini tamko la Serikali kuhusu Kitambulisho cha Taifa kuwekwa ukomo wa kutumika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vitambulisho vya Taifa vilivyotolewa hadi mwaka 2022 vilikuwa na tarehe ya ukomo wa kutumika. Serikali imefanya marekebisho ya Kanuni za Usajili na Utambuzi wa Watu za mwaka 2014 ikiwemo Kanuni ya 7(3)(a) ambayo inaainisha taarifa zilizopo katika uso wa Kitambulisho cha Taifa zinazohusiana na tarehe ya ukomo wa muda wa matumizi ya Kitambulisho cha Taifa. Ili kuondoa ukomo wa matumizi, marekebisho hayo yalitangazwa rasmi katika Tangazo la Serikali (GN) Na. 96 la tarehe 17 Februari, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ina maana kwamba, Vitambulisho vya Taifa kwa raia ili kuwezesha Vitambulisho vinavyofikia ukomo wake baada ya kipindi cha miaka kumi vitaendelea kutumika baada ya muda huo. Napenda kufafanua zaidi kwamba Namba za Utambulisho (NIN) zilizopo katika vitambulisho hivyo, hazina ukomo wa muda wa matumizi. Aidha, marekebisho hayo hayatahusu muda wa matumizi ya Vitambulisho vya Taifa kwa Wageni Wakaazi (Legal Residents) na Wakimbizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa wito kwa watoa huduma wanaotumia vitambulisho vya Taifa kuwatambua wateja wao, kuendelea kutambua vitambulisho vyenye tarehe za ukomo, nakushukuru.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka huduma ya maji ya DAWASA katika Kata za Buza, Vituka, Makangarawe na Sandali - Temeke?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha wananchi wa Kata za Buza, Vituka, Makangarawe na Sandali katika Manispaa ya Temeke wanapata huduma ya maji, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Maji wa JET-Buza ambao hadi kufikia mwezi Agosti, 2023, utekelezaji umeweza kufikia asilimia 30 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2024. Mradi huo utanufaisha wananchi zaidi ya 173,810 wa Kata hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika kuboresha huduma ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam, Serikali katika mwaka wa fedha 2023/2024 itaanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji utakaonufaisha Jimbo la uchaguzi la Temeke, Kata za Buza, Vituka, Makangarawe na Sandali pamoja na Majimbo mengine matano ya uchaguzi ya Kibamba, Ubungo, Kinyerezi, Ukonga na Ilala. Kazi zilizopangwa kufanyika ni pamoja na ujenzi wa tenki la lita milioni tisa eneo la Bangulo na ulazi wa mtandao wa mabomba wa umbali wa kilometa 124. Mradi huo unatarijiwa kukamilika ifikapo Desemba, 2024.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Ofisi za kisasa za Walimu katika kila shule nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Miradi ya Kuboresha Elimu ya Msingi (BOOST) na Sekondari (SEQUIP) imeendelea na azma ya kuboresha Sekta ya Elimu Nchini kwa kujenga shule mpya za msingi na sekondari, ambapo hadi sasa shule 231 za sekondari zimeshajengwa na ndani yake kuna majengo ya utawala ambayo ni ofisi za Walimu za kisasa, vivyo hivyo kwa shule za msingi, shule zote mpya ambazo zinaanza kujengwa, hitaji hili limezingatiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mradi wa BOOST shule nane za zamani zinakarabatiwa sambamba na uboreshaji wa Ofisi za Walimu. Uboreshaji utaendelea kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -
Je, Serikali ina mikakati gani ya kupanua wigo wa miradi ya kuboresha barabara za mitaa ya Manispaa ya Temeke hasa Jimbo la Temeke kupitia DMDP?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mradi wa DMDP Awamu ya Kwanza inajenga mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 48.243 kwa gharama ya shilingi billion 60.9 katika Jimbo la Temeke kwa Kata za Mtoni kilometa 9.623; Makangarawe kilometa 10.402; Yombo vituka kilometa 7.710; Kilakala kilometa 10.53; Keko kilometa 0.462; Buza kilometa 1.7; na Kata za Changombe, Sandali, Temeke na Azimio zimejengwa kilometa 7.8. Kwa sasa kilometa 46.543 zimekamilika na zinatumika na kilometa 1.7 za Buza zilizosalia zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Septemba, 2022.
Mheshimiwa Spika, kupitia Mradi wa DMDP Awamu ya Pili katika Jimbo la Temeke imependekezwa kujengwa mtandao wa barabara wa jumla ya kilometa 53.10 kwa kiwango cha lami zinazokadiriwa kugharimu shilingi billioni 69.5. Ofisi ya Rais – TAMISEMI imewasilisha mapendekezo hayo Wizara ya Fedha na Mipango ili iwe sehemu ya mzunguko wa 20 wa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia katika Mkoa wa Dar es Salaam unaotarajia kuanza mwezi Julai, 2022.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kununua Magari ya Zimamoto kwa ajili ya Kituo cha Zimamoto na Uokoaji Mchicha – Temeke?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, masuala ya “kwa niaba, na jina la Mbunge” yameshatolewa. Kwa hiyo, nenda moja kwa moja kwenye jibu.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunikumbusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea na jitihada za kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limepata jumla ya magari 12 ya Zimamoto na Uokoaji yaliyopatikana kutoka katika mkopo wa Euro milioni 4.9 kutoka katika Serikali ya Austria ambapo yatasambazwa katika vituo vilivyoainishwa, kikiwemo Kituo cha Temeke. Vituo vingine vitakavyonufaika ni pamoja na Ilala, Kinondoni, Dodoma, Mwanza, Morogoro, Mbeya, Arusha na Kilimanjaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha taratibu zote za mkopo wenye masharti nafuu wa thamani ya Dola za Marekani milioni 100 kutoka Taasisi ya ADEX iliyopo Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa ajili ya kupata vitendea kazi mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa magari 150 ya zimamoto na uokoaji kwa matumizi ya nchi nzima. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka mita za maji kama za LUKU ili kuwawezesha wananchi kulipa bili za maji kulingana na matumizi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imeendelea na ufungaji wa dira za malipo ya kabla (pre paid water meters) ambapo hadi kufikia mwezi Juni, 2024 jumla ya dira 14,914 zilikuwa zimefungwa kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini pamoja na RUWASA ambapo kati ya hizo, dira 11,861 zilifungwa kwa Mamlaka ya Maji Safi na Miji Mikuu ya Mikoa, dira 325 zilifungwa na Mamlaka za Miradi ya Kitaifa, dira 692 zilifungwa na Mamlaka ya Maji ya Miji Mikuu ya Wilaya na dira 50 Mamlaka za Miji Midogo. Vilevile kwa upande wa vijjijni jumla ya dira 1,986 zilifungwa kwa Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali imekamilisha uandaaji wa andiko dhana (concept note) pamoja na mpango mkakati sambamba na kutengeneza mfumo wa ankara wa kuendesha dira za malipo ya kabla ifikapo Julai, 2025. Aidha, Serikali inaendelea kusimamia, kusisitiza na kuziwezesha Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira pamoja na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha zinaongeza kasi ya ufungaji wa dira za malipo ya kabla ili kuwawezesha wananchi kulipa ankara za maji kulingana na matumizi na kuboresha usimamizi wa mauzo na makusanyo.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza:-
Je, kuna mpango gani wa kujenga kwa zege barabara zinazoingia Bandari Kavu – Temeke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2024/2025 Serikali kupitia Mradi wa DMDP Awamu ya Pili imepanga kutumia shilingi bilioni 1.8 kufanya ujenzi kwa kiwango cha zege barabara ya Markas kilometa 0.48 iliyoko Bandari Kavu Namba 20 na kujenga mfereji mkubwa wenye urefu wa kilometa 1.16 wa kutoa maji ya mvua ambayo yamekuwa yakisababisha mafuriko kwenye makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kupitia fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mwaka 2024/2025, Serikali imepanga kujenga kwa kiwango cha zege barabara ya Saza kilometa 0.550 iliyoko Bandari Kavu ya Kontena Tupu, Fantuzz Chang’ombe kwa gharama ya shilingi milioni 750 na mkandarasi tayari yuko site.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wafanyabiashara kulipwa madai na riba pindi wanapocheleweshewa malipo?
WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulipaji wa madai yanayotokana na kupokelewa kwa bidhaa au huduma huzingatia masharti ya mikataba ya zabuni au kandarasi iliyoingiwa baina ya Serikali na mtoa huduma. Hivyo, Serikali hulipa au hulipwa riba pindi masharti ya mikataba ya zabuni au kandarasi yanapokiukwa.