Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mohamed Lujuo Monni (67 total)

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka miwili iliyopita Waziri wa Nishati alitembelea Kituo cha Afya cha Makorongo na kwa sababu ya umuhimu wa Kituo kile cha Afya alielekeza umeme uwekwe. Kituo kile kinahudumia Kata tano lakini mpaka leo hii kituo kile hakijapata umeme. Naomba sasa kujua, ni lini Wizara itatekeleza agizo lile la Waziri wa Nishati na Madini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni, Mbunge Chemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo ya Waziri yalitakiwa yatekelezwe na kwa vyovyote vile yatakuwa katika hatua za utekelezaji kwa sababu uunganishaji wa umeme siyo jambo la siku moja. Naomba tulichukue na tukalifanyie kazi na kuhakikisha katika muda mfupi umeme unawashwa katika Kituo hicho cha Afya kwa ajili ya kuhudumia wananchi.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, changamoto ya Hanang inafanana sana na changamoto iliyopo kwenye mji wetu wa Chemba. Ni bahati mbaya sana uwezo wa Halmashauri yetu, ni mdogo: sasa naomba kujua, ni lini Serikali itajenga stendi kwenye Mji wetu wa Chemba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, nieleze tu kwa kifupi kwamba, ile miradi ya kimkakati katika Halmashauri ilikuwa na vigezo kwa kila Halmashauri kupata. Tuliainisha vigezo 13 ambavyo Halmashauri ikivikamilisha inapata ile miradi. Moja ya vigezo ikiwemo ni; katika miaka mitatu mfululizo, Halmashauri hiyo iwe imepata hati safi. Kwa hiyo, kama ulikuwa unakosa baadhi ya vigezo, basi ulikuwa hau-qualify kupata hiyo miradi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba Waheshimiwa Wabunge kuhimiza Halmashauri zenu kutimiza vigezo vyote. Vigezo ambavyo vimekamilishwa, vinaletwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI nasi tukiona kwamba Halmashauri ina-qualify, basi tunawa-guarantee kupata huo mradi kwa ajili ya kusaidia Halmashauri zetu kuongeza mapato yao ya ndani. Ahsante sana.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Kwanza kabisa, nimshukuru Waziri na Naibu Waziri wake kwa namna ya kipekee kabisa, kwa namna ambavyo wananipa ushirikiano. Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alipokuja kwenye ziara ya kuomba kura, alisema atahakikisha anachagua Waziri ambaye anawaza nje ya box na hakika watu hawa wanafanya hivyo. Sasa swali langu, nawashukuruni pamoja na kunipa mabwawa manne, lakini nataka kujua sasa, ni lini ujenzi huo wa hayo mabwawa utaanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, mabwawa haya manne yatajengwa kwa nyakati tofauti kulingana na fedha tutakavyokuwa tunazipata, ninaamini Mheshimiwa Mbunge wewe ni shahidi mzuri pale Chemba tumepatendea haki sana, hivi majuzi tu tumetoka kuchimba visima na hata haya mabwawa tunakuja kujenga mwaka ujao wa fedha lakini tutaanza kwa awamu taratibu mpaka kuhakikisha mabwawa yote yanakamilika. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali hili limeulizwa mara mbili kwa mujibu wa Taarifa mbalimbali kutoka Bunge lako majibu yamekua ya kitolewa hayo hayo, sasa naomba kujua hata hizo bilioni 6 ambazo zimetengwa kwa ajili ya mwaka unaoishia mwenzi mmoja ujao hazijawahi kutumika mpaka leo. Naomba kujua lini sasa hizi bilioni 6 sasa zinaanza kufanya ujenzi kwenye barabara ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni nini commitment ya Serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwasababu Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye ziara ya kuomba kura aliahidi itajengwa kwa kiwango cha lami, naomba kujua…

NAIBU SPIKA: umeshauliza Mheshimiwa, ahsante sana.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumshukuru Mbunge kwa jinsi ambavyo ifuatilia barabara hii barabara ndefu na kweli ni kiunganishi cha mikoa tangu Singida hadi Tanga na imepangiwa katika bajeti bilioni 6.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumuahidi Mbunge huyu kwamba kabla ya bajeti hii kwisha barabara hii itatangazwa katika kipande ambacho kimepangiwa kilomita 20. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. MOHAMED M. LUJUO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa muda ili niulize swali langu la nyongeza. Barabara inayounganisha Wilaya ya Kiteto na Makao Makuu ya Mkoa wao wa Manyara inapita kwenye Jimbo langu, lakini sehemu ya barabara hiyo Kijiji cha Kelema Maziwani daraja limekatika na ni miezi sita sasa. Sasa, naomba kujua ni lini daraja hili litajengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Moni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, TANROADS wanafanya tathmini ya barabara zote ambazo zimepata changamoto ya mvua ikiwa ni pamoja na madaraja. Wizara kupitia TANROADS kutokana na uzoefu uliotokea miaka miwili, mitatu iliyopita tumeandaa madaraja ya muda kwa ajili ya kutatua changamoto za madaraja ambayo yamesombwa ama kuharibika. Sasa hivi inakuwa ni ngumu kurekebisha hayo madaraja kwa sababu yanahitaji kutengeneza tuta halafu madaraja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hata ungeweka sasa hivi ni wazi kwamba daraja hilo litasombwa kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba daraja hilo ambalo liko katika hiyo barabara ya Kiteto Manyara litakuwa ni kati ya madaraja ambayo yatahakikishwa kwamba yanajengwa ili kurudisha mawasiliano ambayo yamekatika kwa kipindi alichokitaja Mbunge. Ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nasikitika sana swali langu halijajibiwa, swali limeuliza juu ya kilometa 58.2, nimejibiwa juu ya kilometa 23 tu. Naomba nirudi tena, ni lini Serikali itajenga barabara yote ya kilometa 58.2 kwa sababu sehemu kubwa ya barabara hiyo tayari imekatika kwa sababu ya mvua?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; barabara pia ya Larta – Lahoda – Handa imekatika kabisa hakuna namna watu wanaweza kupita. Naomba kupata majibu ya Serikali barabara hizi ni lini pia zitajengwa ili watu wapiti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza kwamba ni lini barabara inayopitia Lahoda na maeneo ambayo ameyaainisha kwamba itajengwa. Kama nilivyoeleza katika jibu la msingi kwamba katika mwaka huu wa fedha 2021/2022, TARURA kwa maana ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini umepanga kufanya tathmini ya barabara zote nchini pamoja na madaraja ili tuweze kuwa na database ya kutosha kuangalia zile barabara ambazo zinaharibika sana tuzipe kipaumbele katika mipango yetu inayokuja. Ndiyo maana nimeahidi kwamba moja ya barabara ambayo tutaipa kipaumbele ni hizi barabara ambazo ameitaja ikiwemo hii barabara ya Kwa Mtoro -Sanzawa – Mpendo ambayo tulikuwa tunaijenga kwa awamu kulingana na fedha inavyopatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, Serikali ipo kazini na hatupo hapa kwa ajili ya kumdanganya mtu yeyote, lengo la Serikali ni kuwahudumia wananchi ili waweze kupata huduma bora kabisa ya usafiri na usafirishaji. Ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, shule ya Sekondari Farukwa ilipandishwa hadhi na ikawa ya kidato cha tano na sita lakini baadaye wakasitisha na sababu walizofanya wasitishe tumezimaliza tayari ni lini sasa wataturudishia shule yetu ya kidato cha tano na sita. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika,
naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Monni Mbunge wa Chemba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, anasema kwamba Shule ya Farukwa ambayo ipo katika Jimbo la Chemba wameshamaliza zile changamoto kwa hiyo wanataka kujua ni lini sasa Serikali itairudisha ile shule ili sasa ianze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tutawatuma wataalam kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI watakuja kukagua kujiridhisha kama hizo vile vigezo vyote mmeshamaliza na kama itakuwa imekamilika basi nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mwaka unaokuja hiyo shule itafunguliwa na wanafunzi wataenda kusoma hapo. Ahsante sana.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Changamoto iliyopo kwenye Jimbo la Kyerwa inafanana kabisa na changamoto zilizopo Wilaya ya Chemba. Changamoto kubwa ni miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naishukuru sana Serikali kwa kupitia Wizara ya Maji, nami ni shabiki mkubwa wa Mheshimiwa Waziri Jumaa Aweso. Yale maneno ambayo Ndugu yangu Mheshimiwa Jerry Silaa alisema, nami nayathibitisha kwamba anapaswa kupewa zile Ph.D ambazo zinatolewa, tena apewe Tanzania. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu sasa. Pamoja na kuwa tumepata visima vitano na vimechimbwa zaidi ya miaka miwili, vingine mmoja, lakini bado havifanyi kazi kwa sababu miundombinu yake haipo tayari: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, ni lini sasa Serikali kupitia Wizara ya Maji itaweka miundombinu ili watu wale nao waanze kupata maji? Ahsante sana.(Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, kwa kweli nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Chemba kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa muda mfupi katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni kweli tulishafika Chemba, hali ya Chemba ilikuwa siyo nzuri. Maelekezo ya kwanza ambayo tumeyafanya ni katika kuhakikisha kwamba tunachimba visima vya dharura ili wananchi wa Chemba waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Nataka nimhakikishie katika mfuko wa mwezi huu tutatoa fedha ya uanzaji wa miradi ile ili wananchi wa Chemba waweze kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumaliza kabisa tatizo la Maji Chemba, siyo maeneo yote ambayo utachimba ukapata huduma ya maji. Eneo la Chemba limetupa experience baadhi ya maeneo yamekuwa na ukame. Tunakwenda kuchimba bwawa kubwa katika kuhakikisha wananchi wa Chemba wanaendelea kunufaika na maji. Tunaona mvua zinazonyesha maji yanapotea tu. Mkakati wa Wizara na mageuzi ya Wizara ni kuhakikisha tunachimba mabwawa makubwa ili kuvuna maji na wananchi wa Chemba waendelee kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona, maana nimesimama muda mrefu sana.

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba mwaka wa Fedha uliopita tulikuwa na miradi mitatu mikubwa. Mradi wa Machiga, Mradi wa Chandama na Mradi wa Visima 13, lakini mpaka leo wakandarasi wote hawako site; naomba kujua kauli ya Serikali juu ya Wakandarasi hawa. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Monni tumekuwa tukifanya kazi kwa pamoja na amefika Wizarani mara nyingi, nampongeza kwenye hilo. Miradi hii mikubwa ninaamini ameshaongea na Mheshimiwa Waziri, ameshaongea na Mheshimiwa Katibu Mkuu, tunakuja kutekeleza na Wakandarasi watafuata namna ambavyo wamesaini mikataba yao.(Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nasikitika kidogo kwa majibu ambayo Serikali imetoa, anakubaliana kwamba uhakiki umekamilika tangu 2015 na sasa ni miaka nane mpaka leo watumishi wale hawajalipwa hata shilingi moja. Hata hivyo, kinachosikitisha zaidi, wapo waliostaafu lakini pia wapo ambao wamekufa. Nataka kujua nini hatima ya hao waliostaafu na hao waliokufa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kulipa madai yoyote ya watumishi lazima uhakiki kujiridhisha zaidi ya shaka kwamba wanaodai wanadai kiwango halali na wanastahili kulipwa malipo hayo. Ni kweli kwamba uhakiki ulianza mwaka 2015/2016, lakini kuna dosari nyingi za madai zilionekana miongoni mwa wale ambao walitakiwa kulipwa na Serikali isingeweza kuwalipa kabla ya kujiridhisha kwamba kiasi ambacho wanadai wanatakiwa kulipwa. Kwa hiyo, baada ya Mkaguzi wa Ndani kutoka Makao Makuu kufanya ukaguzi, ikaonekana madai yale yameshuka na ndiyo maana yamechelewa kuanza kulipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mwaka ujao inatengwa fedha, lakini kila mwaka tutatenga fedha kuhakikisha wote waliostaafu, walioko kazini na hata ambao wametangulia mbele za haki wanalipwa kwa kupitia wale ndugu ambao ni wategemezi wa hao waliotangulia mbele za haki.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Mwaka 2008 Serikali ilianza ujenzi wa jengo la mama na mtoto kwenye zahanati ya Kijiji cha Msada, Kata ya Msada, lakini mpaka leo ni miaka 14 lipo kwenye renter. Naomba kujua ni lini sasa Serikali itatoa fedha za kumalizia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali iliweka utaratibu wa kutumia fedha kutoka Serikali Kuu na pia kutumia fedha kutoka mapato ya ndani halmashauri kukamilisha baadhi ya majengo na hususan majengo katika ngazi ya zahanati. Kwa hiyo, naomba nichukue fursa hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, kuhakikisha wanatenga fedha katika asilimia 40 ya miradi ya maendeleo kukamilisha jengo la mama na mtoto katika zahanati ambayo Mheshimiwa Mbunge ametaja. Ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Barabara ya Zamahero-Babayo- Makorongo hadi Donsee ndicho kipande pekee yake kitakuwa sasa hakina lami, ukizingatia barabara ya Kibarashi - Handeni hadi Singida inajengwa na ni kibarabara cha kilometa 18 tu, nataka kujua Serikali mna mpango gani wa kutumalizia hiko kibarabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, alichosema ni kweli, barabara hii tutaijenga kwa kiwango cha lami lakini itategemea na upatikanaji wa bajeti. Kwa hiyo, Serikali inalifahamu na inaendelea kutafuta fedha ili kukamilisha hicho kipande ambacho ndicho kilichobaki. Ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Chemba ujenzi wake umesimama kwa miaka minne sasa, naomba kumuuliza Waziri ni lini sasa watatoa fedha za kumalizia? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika utaratibu wa kumaliza vituo vya Polisi tumekuwa tukitumia njia mbalimbali ikiwemo kutumia Mfuko wetu wa Tuzo na Tozo ambao upo chini ya Jeshi la Polisi, ambao katika mwaka huu wa fedha tumeshaufanyia ujenzi na ukarabati wa vituo kadhaa katika maeneo mbalimbali nchini. Hivyo basi nichukua hoja hii ya kituo cha Chemba tuona kama tunaweza kumaliza kupitia Mfuko wa Tuzo na Tozo katika kipindi cha mwaka huu wa fedha unaokuja.

Mheshimiwa Spika, tuangalie kimefikia kiwango gani na mahitaji ni kiasi gani na uwezo wa fedha zilizopo ni kiasi gani na vipaumbele vilivyopo ni vipi.(Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Magari ya vituo vya afya vya Mrijo, kwa Mtoro na Makorongo yamechakaa kabisa na hayafanyi kazi. Naomba commitment ya Serikali sasa kama tunaweza kufanyiwa ukarabati au kama tunaweza kupata magari mapya. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshemiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nampongeza sana kwa kazi kubwa anayoifanya kwa wananchi wa Chemba. Nimhakikishie kwamba magari ya wagonjwa ambayo ni chakavu, Serikali inaweka mpango wa kutafuta magari mengine ya wagonjwa ili kuhakikishwa huduma za afya zinaenda vizuri na tutatoa kipaumbele katika vituo vya afya ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante./ Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuishukuru sana Wizara ya Maji wamefanya kazi kubwa, lakini nina swali moja la nyongeza. Kijiji cha Ombiri kilikuwa na bwawa la asili ambalo sababu ya mvua kubwa kingo zake zimekatika. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wanarudisha bwawa lile kwa ajili ya watu wa kijiji kile? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunafahamu bwawa la Ombiri katika Kijiji cha Ombiri, limepata matatizo, sisi kama Wizara kwa umuhimu wa bwawa namna ambavyo tunaendelea kuyajenga, kwa hiyo, bwawa hili ambalo limepata hitalafu sisi kama Wizara tumelipa kipaumbele, tutakuja kulitekeleza kwa kulikarabati vizuri.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nilitaka kujua kuna barabara yetu ya Chemba - Soya ambayo kwa muda mrefu imekuwa na shida kubwa na mara kadhaa viongozi walipokuja waliahidi kuijenga walau kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, naomba kujua commitment ya Serikali katika hili.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ahadi zote ambazo viongozi wamezianisha zipo katika mpango. Kwa hiyo, hata hii ambayo barabara ameiainisha Mheshimiwa Mbunge ya kutoka Chemba mpaka Soya ni miongoni mwa barabara zetu, zipo katika mipango yetu. Ahsante sana.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kata ya Tumbakose na kata ya Kimaha mawasiliano ni hafifu sana, naomba kujua commitment ya Serikali kwenda kujenga mnara maeneo hayo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Monni, Mbunge wa Chemba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo hayana kabisa huduma ya mawasiliano tunatumia Sheria yetu Namba 11 ya mwaka 2006 iliyoanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa wote kwenda kufikisha mawasiliano kwenye eneo hilo. Lakini kama mawasiliano ni hafifu na kuna changamoto ya ubora wa mawasiliano kwa Sheria yetu Namba 12 ya mwaka 2003 iliyoanzisha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, tunaielekeza Mamlaka ya Mawasiliano TCRA iende ikapime ubora wa mawsiliano ili tujiridhishe changamoto ipo wapi, ili tuhakikishe kwamba wananchi wa Chemba wanapata mawasiliano ya hakika na ubora unaotakiwa, ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Vijiji vya Ombiri, Muungano, Golopaguma, Dalayi navyo vina matatizo makubwa ya majosho kwa ajili ya mifugo. Na ikumbukwe kwa Mkoa wa Dodoma Wilaya ya Chemba ndiyo yenye mifugo mingi. Naomba kujua commitment ya Serikali sasa ni lini tutaenda kujenga majosho kwenye vijiji hivyo? Ahsante sana.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Wilaya na Mkoa wa Dodoma kwa ujumla una mifugo mingi sana. Kwa mwaka huu wa fedha tunaoenda nao angalau kila wilaya tulikuwa tumewapangia majosho si chini ya manne, tuliwapa upendeleo kidogo. Sasa safari ijayo tutaangalia pia hasa kwa Jimbo la Mheshimiwa Mbunge wa Chemba, tuone ni kwa namna gani tunaweza kupanga kujenga majosho mengine ili Mheshimiwa Mbunge na wafugaji wake waweze pia kufaidika.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mwezi mmoja uliopita nilisoma kwenye vyombo vya Habari kwamba vyombo vya ADB imepitisha zaidi ya bilioni 250 kwa ajili ya Bwawa la Farkwa. Sasa nataka kujua ni lini mradi huo utaanza? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge amekuwa mfuatiliaji mkubwa sana juu ya ujenzi huo wa mradi huo wa Bwawa la Farkwa. Utekelezaji wa miradi ya maji inategemea na fedha na hapa, nitumie nafasi hii kumpongeza sana nakumshukuru Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake mahususi kabisa, African Development Bank bodi yake imeridhia sasa kutupatia fedha ya kuhakikisha ujenzi wa bwawa lile unatekelezeka. Kwa hiyo, suala la mikopo lina taratibu zake, lakini kikubwa tutaliharakisha ili kuhakikisha mradi ule unaenda kuanza na wananchi wa Farukwa kwa maana ya Jimbo lake la Chemba na wananchi wa Jiji la Dodoma waende kupata huduma ya maji safi na salama.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Chemba ina jumla ya shule za msingi 103 za Serikali na tumeongeza shule nane kwa matokeo ya fedha za UVIKO, lakini asilimia 70 ya shule zote hizi zipo vijijini ambavyo ni ngumu sana kupata nyumba za kupanga, naomba kujua mna mkakati gani wa maksudi wa kujenga nyumba za Walimu kwenye shule hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Monni Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Serikali ni kujenga nyumba maeneo ya pembezoni na miongoni mwa mikakati ambayo nimeainisha ni pamoja na kutenga fedha, vilevile tuna miradi mbalimbali ambayo tumeiainisha ikiwemo BUST, EP4R, EQUIP 2 yote hii lengo lake ni kuhakikisha kwamba tunapunguza hiyo adha kwa hiyo tutazingatia maeneo hayo ikiwemo Jimbo la Chemba. Ahsante. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Nina swali moja tu la nyongeza. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali kwa sababu mradi huu umeanza muda mrefu sana. Wilaya yetu ya Chemba miji yake mingi ipo pembezoni na ni ukweli kwamba eneo la mjini lina watu wachache sana. Sasa nataka kujua nini mpango wa Serikali wa kupeleka hii huduma ya Vituo vya Polisi kwenye miji hiyo mikubwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Wilaya ya Chemba sehemu kubwa ni Wilaya ya Vijijini na ina miji inayozunguka mji wenyewe wa Chemba, pale panahitajika pia utaratibu wa kuimarisha ulinzi kwenye maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimwahidi tu Mheshimiwa Monni kwamba tulikubaliana nitafanya ziara, moja ya lengo ni kuangalia maendeleo ya ujenzi huu, lakini la pili ni kuangalia maeneo ambayo kimkakati yanastahili kupewa huduma za kipolisi ili kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Tutakapofika huko Mheshimiwa tutakubaliana ni maeneo gani yapewe kipaumbele. Ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, boma la zahanati ya Isusumya limekuwa la muda mrefu sana na tulileta maombi maalum. Nataka kujua sasa mpaka leo hatujajua nini kinaendelea, nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba zahanati hiyo imekamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimuelekeze Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chemba kutenga fedha za ukamilishaji wa Boma shilingi milioni 50 kwenye mwaka wa fedha ujao ili kukamilisha boma hili ambalo halmashauri imeona ni kipaumbele na tayari imeshaleta maombi maalum kwa ajili ya ukamilishaji.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ujenzi wa Chuo cha VETA Chemba umekamilika, nataka kujua ni lini sasa kitafunguliwa ili kidahili wanafunzi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli ujenzi wa vyuo 25 vile vya Wilaya awamu ya kwanza pamoja na vinne vya Mikoa, tayari ujenzi umekamilika. Jukumu letu tulilonalo sasa hivi ni utafutaji wa vifaa na kuajiri walimu kwa ajili ya kwenda kufundisha kwenye maeneo hayo. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, mwaka ujao wa fedha kuanzia mwezi Julai tutaanza kutoa kozi za muda mfupi lakini kuanzia Mwezi wa Kumi tutafanya usahili sasa kwa ajili ya kozi za muda mrefu sambamba na upelekaji wa vifaa vya kufundishia kwenye maeneo hayo kwa sababu samani tayari tumeshapeleka.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara ya Kiberashi – Chemba – Singida kandarasi yake imetangazwa lakini kuna kipande cha kama kilometa 18 kutoka Goima hadi Kondoa. Nataka kujua commitment ya Serikali ya kujenga kipande hicho. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Goima – Bicha ni barabara ambayo sasa tumewaagiza Mkoa wa Dodoma waweze kufanya usanifu, maana yake ilikuwa haijafanyiwa usanifu, wafanye usanifu ili iwe ni link kati ya barabara ndefu ambayo tutaijenga ya Kiberashi – Singida halafu hiyo itakuwa ni link. Mwaka huu tumepanga waanze kufanya usanifu ikiwa ni maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Moja, barabara hii inaunganisha Mikoa Mitatu. Inaunganisha Mkoa wa Singida, Dodoma na Manyara. Naomba kujua ni kwa nini, barabara hii tusiipandishe hadhi iwe TANROADS ili iweze kuhudumiwa kwa urahisi zaidi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Naibu Waziri Jimbo Lake na Jimbo langu linaunganishwa na barabara chafu kweli kweli, kati ya Seya na Zajiro kwake. Nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha barabara hiyo inatengenezwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu kupandisha hadhi barabara hii ambayo inaunganisha Mikoa Mitatu ya Singida Dodoma na Manyara, utaratibu upo wa kisheria kwa maana lazima vikao vianze katika ngazi ya Wilaya, vikitoka kwenye Wilaya viende kwenye Bodi ya Barabara ya Mkoa na baada ya kutoka Bodi ya Barabara ya Mkoa viende RCC na ndipo hadhi ya barabara hii iweze kupandishwa.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili. Nikiri ni kweli barabara hii inayounganisha kati ya Jimbo la Mheshimiwa Monni na Jimbo langu mimi la Chamwino na tayari maelekezo yalikuwa yameshakwenda kwa Mameneja wote wa TARURA wa Mikoa, kuhakikisha kwamba wanatenga fedha ya kuhakikisha vipande vya barabara hii vinaanza kutengenezwa. Katika mwaka huu wa fedha tuliouombea wa 2023/2024 barabara hii vilevile imo katika barabara zilizoombewa fedha. Naomba kuwasilisha.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mji wa chemba unakuwa kwa kasi lakini hauna soko kabisa. Naomba kujua mkakati wa Serikali wa kujenga soko pale kwenye mji wa Chemba, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Monni Mbunge wa Jimbo la Chemba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nielekeze Mkurugenzi wa halmashauri ya Chemba kuainisha na kuandaa eneo kwa ajili ya ujenzi wa soko na kuleta andiko la kuona uwezo wa halmashauri kwa mapato ya ndani yanafikia eneo gani ili Serikali Kuu iweze kuona sehemu gani inahitaji kuchangia ili kujenga soko katika mji huu wa Chemba, ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahasante sana. Shule ya sekondari Ifaru iko katika jimbo la Chemba mwanzoni ilikuwa na kidato cha tano na sita baadaye wakasitisha kwa sababu ya uchakavu wa miundombinu. Sasa uchakavu ule tayari Serikali imefanya ukarabati. Ni lini sasa itarejesha kusajili wanafunzi wa kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mohamed Monni Mbunge wa Chemba kwamba Ofisi ya Rais TAMISEMI imelipokea jambo hilo na italifanyia kazi; kwa sababu moja ya malengo ya Ofisi ya Rais TAMISEMI ni kuhakikisha halmashauri zote nchini zinakuwa na shule za kidato cha tano na cha sita kwa sababu ya ongezeko kubwa la wanafunzi ambao wanawekwa sasa, kwa hiyo lipo katika mchakato na linafanyiwa kazi.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kata ya Msaada kuna jengo ambalo lilikuwa likijengwa kwa mpango wa MAMM tangu mwaka 2008 mpaka leo halijakamilika. Naomba kujua, ni lini Serikali itamalizia jengo hilo, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni kuhusu Kata ya Msaada, Serikali itamalizia jengo la Msaada hapa kadri ya upatikanaji wa fedha. Tutaangalia katika mwaka wa fedha huu ambao umeshapitishwa na Bunge lako Tukufu, kuona kama kuna fedha imetengwa kwa ajili ya Msaada lakini kama haipo, basi tutatenga fedha kwenye mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru Serikali kwa barabara yetu ya Kiberashi – Handeni – Chemba hadi Singida lakini ili barabara hiyo iweze kutumika vizuri kuna interchange mbili. Kwanza ni kutoka Zamahelo mpaka Donsee nyingine ni kutoka Goima hadi Bicha. Sasa nataka kujua mkakati wa Serikali wa kuhakikisha interchange hizo zinajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Monni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, pongezi za Serikali nazipokea kwa niaba lakini pongezi hizi ziende kwa Mheshimiwa Rais, maana yeye ndiye anayetoa hizi fedha na hususani katika ujenzi wa barabara hii ambayo Mheshimiwa Mbunge umeizungumzia. Kwa kuanzia kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii nafikiri itakuwa vema zaidi tukianza kama ambavyo Serikali imepanga ndipo tuanze na hizo zingine kwa kuwa hii ndio itakuwa lango muhimu

la kuunganisha kati ya Mkoa wa Dodoma na Mkoa jirani, ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza ninaishukuru Serikali kwa majibu mazuri sana, kwamba tayari kandarasi imeshatangazwa, pamoja na majibu hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, tangu 2019 daraja lilipokatika walitengeneza diversion ambayo magari yote yalikuwa yanapita pale lakini kwa bahati mbaya sasa ile diversion imeharibika kabisa.

Nini mkakati wa Serikali wa kuimarisha hiyo barabara ya mchepuo?

Swali la pili, katika barabara hiyo kutoka Kijiji cha Kalema Maziwani mpaka Mondo, mkandarasi aliyepewa kazi ya kuweka mifereji aliweka chini ya kiwango na hivyo kipindi cha masika maji yale yanaharibu kabisa barabara. Nini kauli ya Serikali juu ya mkandarasi huyu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu diversion naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa tayari tumeshatangaza tenda na Mkandarasi atakwenda site ni wazi pia kwamba wakati anajenga lazima hiyo diversion aiimarishe. Kwa hiyo, pia nitoe maagizo na maelekezo kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma kuhakikisha kwamba anakwenda kuimarisha hiyo diversion ili wananchi na wasafiri wanaopita pale waweze kupita sehemu salama ambapo sasa ni kiangazi, naamini ataitengeneza hiyo diversion.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mifereji. Ni kweli barabara hii tunatengeneza mifereji kwa awamu, tumeendelea kutenga bajeti na hata mwaka huu wa fedha tunakokwenda mifereji itaendelea kutengenezwa. Kwa hiyo, pia nimuagize Meneja wa Mkoa wa Dodoma, kwamba kipindi hiki cha kiangazi ndicho kipindi sahihi cha kutengeneza mifereji, pia niwaombe wananchi wa Chemba kutokufanya shughuli za kijamii karibu na barabara na kuweza kusababisha baadhi ya mifereji kuziba na kuleta changamoto kwenye miundombinu ya barabara. Ahsante. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mji wa Chemba ni Mji ambao unakuwa kwa kasi sana lakini hauna soko, naomba kujua nini mkakati wa Serikali kujenga soko katika Mji wa Chemba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali unaanza na wao wenyewe Halmashauri ya Wilaya, hatuwezi tukakaa Ofisi ya Rais, TAMISEMI tukajua kuna uhitaji wa soko katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, ni wao kupitia Baraza lao la Madiwani liibue mradi huu na kisha kufanya andiko kupitia Mkurugenzi na Afisa Mipango wake na kuwasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tuweze kutafuta fedha kwa ajili ya kuwajengea soko wananchi wa Chemba.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kituo cha Afya cha Makorongo kimeanza kutumika, lakini baadhi ya majengo hayajakamilika. Mfano, jengo la maabara. Nini kauli ya Serikali ya kukamilisha ujenzi huu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kituo kile kimeanza kutoa huduma za afya lakini jengo la maabara na baadhi ya majengo hayajakamilika na ujenzi huu tunakwenda kwa awamu. Nikuhakikishie kwamba Serikali inatafuta fedha kupitia mapato ya ndani lakini pia kupitia Serikali kuu ili kukamilisha majengo haya, kituo kiweze kutoa huduma vizuri zaidi, ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Katika mpango huo vipo vijiji vinne ambavyo havikuwekwa kwenye mpango, sijui sababu ni nini. Vijiji hivyo ni Kelemakuu, Birise, Muungano na Sankaleti. Nataka kujua, Serikali ina mpango gani sasa wa kuviingiza vijiji hivyo kwenye mpango wa REA? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vijiji hivyo vinne vya Kilemakuu pamoja na vingine vyote vipo katika hivyo vijiji 12 ambavyo vimebakia katika utekelezaji wa mradi na kufikia hiyo tarehe 31 Oktoba vitakuwa pia vimewashiwa umeme. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofanya ziara kwenye Wilaya ya Chemba kwenye Kijiji cha Itwalo aliahidi Serikali kujenga kituo cha afya, lakini hivyo hivyo kwenye Kata ya Tarangi. Naomba kujua ni lini utekelezaji wa ujenzi huu utafanyika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni kwanza nilitaarifu Bunge lako kwamba, Serikali inatoa kipaumbele cha kukamilisha ahadi zote za Viongozi wetu wa Kitaifa kuanzia Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi tutaangalia katika kata hizi mbili ambazo Mheshimiwa Monni amezitaja ni namna gani tunaweza tukatenga fedha ama kama imetengewa fedha kwenye mwaka huu wa fedha unaoenda kuanza wa 2023/2024, tuweze kuanza ujenzi huu mara moja na kama fedha haijatengwa, basi tutenge fedha kwenye mwaka wa fedha wa 2024/2025.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Chemba imetenga maeneo kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu na tafiti, na tunafahamu Taifa hili lina changamoto ya upungufu wa mbegu;

Je, nini mkakati wa Serikali wa kuyatumia maeneo haya?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Chemba kwa utayari wao wa kutenga ardhi kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu na utafiti. Hivi sasa tuko nao katika mazungumzo ya mwisho kwa ajili ya kuanza kuanzisha shamba kubwa la uzalishaji wa Mbegu za mtama mfupi ambao una soko kubwa kwa kampuni ya bia Tanzania pamoja WFP na wakulima wakubwa wanapatikana ndani ya Mkoa wa Dodoma na Singida. Kwa hiyo shamba hili ndani ya Chemba litakuwa kama mwokozi kwa wakulima wa kanda ya kati.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kata ya Lahoda, Kata ya Jangalo na Kata ya Kinyamshindo zote zipo mpakani mwa Singida pia na Manyara. Je, ni lini mkakati wa Serikali wa kujenga vituo vya afya katika Kata hizo? ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata hii ya Lahoda, Jangalo na nyinginezo zilizokuwepo pembezoni katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Serikali itaweka kipaumbele kuhakikisha kwamba tunaanza ujenzi wa majengo ambayo yanahitajika kwenye vituo hivi vya afya na tutaangalia katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ili tuweze kupeleka fedha hizi kuanza ujenzi wa vituo hivi vya afya.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana:-

Mheshimiwa Spika, katika Kijiji cha Takwa, Kata ya Kinyomshindo, Jimbo la Chemba, kuna skimu ambayo imetelekezwa sasahivi. Siku za nyuma imepata fedha kutoka Serikalini. Ni nini mkakati wa Serikali wa kuifufua skimu ile ya umwagiliaji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nitahakikisha nashirikiana na Mheshimiwa Mbunge pamoja na wataalam wangu kwa sababu, ipo karibu hapa twende tukaiangalie muda wowote tutakaopata nafasi katikati hapa, ili tuweze kutoa maamuzi sahihi ya utekelezaji wa skimu hii, lakini lengo kubwa la Serikali ni kuhakikisha kwamba, skimu zote zinafanya kazi, ndio dhamira kuu. Kwa hiyo, kama hiyo ndio dhamira kuu maana yake hiyo skimu aliyoitaja ipo ndani ya mpango wa Serikali, baada ya kukaa na wataalamu wetu kuona namna ya kuweza kutekeleza mradi huo.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza; Hospitali ya Wilaya ya Chemba tayari imefungwa mashine za x-ray na ultra-sound lakini hakuna mtaalam hata mmoja. Naomba kujua ni lini Serikali itapeleka wataalam hao ili mashine hizo zifanye kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Kituo hicho hicho cha Afya cha Mrijo kinahudumia Kata nne zikiwemo Kata za Wilaya ya Kiteto. Naomba kujua ni lini sasa watapeleka gari la wagonjwa ili liweze kuhudumia kituo hicho?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohamed Lujio Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza hili la wataalam wa mionzi katika Hospitali ya Wilaya. Nimtoe mashaka Mheshimiwa Monni, Serikali inaendelea kutafuta wataalam hawa hata katika ajira ambazo zilikuwa zimetangazwa na Serikali katika upungufu ambao tulipata kwa kutokuwa na watu walioomba nafasi, ni nafasi kama hizi za wataalam wa mionzi, lakini Serikali itaendelea kuweka jitihada kubwa kwa ajili ya kuajiri wataalam hawa ili Hospitali ya Wilaya ya Chemba nayo iweze kupata watumishi watakaosaidia katika kutumia mashine hizi za x-ray na nyinginezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la Kituo cha Afya Kata ya Mrijo ambacho kinahudumia kata nne kama alivyosema Mheshimiwa Monni. Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika sekta hii ya afya vilevile na tayari fedha imeshatolewa kwa ajili ya ununuzi wa magari ya kubebea wagonjwa ambapo kila halmashauri hapa nchini ikiwepo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba itapata magari mawili kwa ajili ya kubebea wagonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haikuishia hapo, Mheshimiwa Rais bado aliona kuna umuhimu wa kupata magari kwa ajili ya supervision, kwa ajili ya watalaam wetu kutembelea zahanati zetu na vituo vya afya ambavyo vipo katika Halmashauri hizi, kwa hiyo pia halmashauri hizi zitapata angalau gari moja kwa ajili ya supervision.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Wilaya ya Chemba ni Wilaya ambayo ina maeneo mazuri na ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji, lakini bahati nzuri sana tupo katikati ya Barabara ya c2c. Wizara ya Uwekezaji ina mpango gani wa kuwekeza kwenye Wilaya ya Chemba ambayo iko karibu kabisa na Makao Makuu ya Nchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Monni ni kweli Chemba ni sehemu ya kimkakati kwa sababu iko katika barabara Kuu tunasema South – North Corridor ambayo tunaamini sasa kwa kufungua njia hizi kutakuwa na fursa nyingi za uwekezaji katika maeneo ya Chemba kama ilivyo Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie kwamba Serikali inaendelea kufanya jitihada za kuwatafuta wawekezaji, lakini nitumie fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge kushirikiana na halmashauri kuanza kutenga maeneo mahususi kwa ajili ya uwekezaji ili tunapopata wawekezaji wasipate kikwazo kwa maana ya kupata ardhi ambayo iko tayari kwa ajili ya uwekezaji katika sekta mbalimbali katika Jimbo la Mbunge.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, mwaka 2018, Serikali ilichimba kisima kwenye Kijiji cha Mayi lakini mpaka leo hakijaweka miundombinu na hivyo hakitumiki, nini kauli ya Serikali?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mwaka wa 2021/2022 Serikali ilitangaza kandarasi ya visima 13, mpaka leo imechimba vitatu tu na hivyo tunawadanganya wananchi. Naomba kujua Waziri anasema nini juu ya visima hivyo ambavyo havijachimbwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Monni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kisima kilichochimbwa mwaka 2018, Mheshimiwa Mbunge tutakisimamia kuhakikisha tunaleta usambazaji kwa wanufaika wote kwenye kile kisima. Kwa visima hivi ambavyo tulivipitisha mwaka wa fedha 2022, Mheshimiwa Mbunge Serikali haiwezi kudanganya kwa sababu suala letu sisi ni kuhakikisha tunapeleka huduma kwa wananchi. Kwa hiyo, vile visima vilivyobaki lazima tuvifanyie kazi tutakuja kuvichimba kadiri tunavyopata fedha katika mwaka wa fedha 2023/2024.

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kata ya Lahoda ndio kata maarufu sana kwa uzalishaji wa ufuta na alizeti kwa Kanda ya Mashariki, lakini barabara yao ya kutoka Ilasee, Lahoda hadi Handa na kuunganisha na Singida ni mbovu sana. Naomba kujua nini mkakati wa Serikali wa kuboresha barabara hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana kwa kazi nzuri anayoifanya kwa Jimbo la Chemba na nimhakikishie kwamba Serikali imeweka mkakati mzuri sana kuhakikisha maeneo yote yenye mazao ya kimkakati kama alizeti, ufuta na kata ambazo amezitaja, kutenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha kwamba barabara zile zinajengwa vizuri zinapitika vizuri ili wananchi waweze kusafirisha vizuri mazao yao. Kwa hiyo nitoe maelekezo kwa Meneja wa TARURA Chemba, wafanye tathmini ya bajeti iliyopo na kuweka kipaumbele kwenye maeneo yenye uzalishaji mkubwa kama haya ili barabara ziweze kupitika vizuri. Ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Bakorongo kilikamilika na kufunguliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, mwaka 2007, tangu hapo maelekezo yamekuwa yakitolewa kiwekewe umeme na hakijawekewa.

Mheshimiwa Spika, nataka kujua nini kauli ya Serikali kuhusu kuweka umeme katika kituo hicho cha afya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tunayo maeneo mengi ya taasisi za umma ambayo hayajafikiwa na umeme, kwenye vituo vya afya, vyanzo vya maji, shule na taasisi za dini. Baada ya kuona mahitaji makubwa wenzetu wa REA wamekuja na mkakati na mradi maalum ambao tutapeleka umeme katika vyanzo vya maji, vituo vya afya na migodi ili kuharakisha na kurahisisha ufikaji wa miundombinu ya umeme katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, naomba baada ya kutoka hapa basi nizungumze na Mheshimiwa Mbunge ili tuone kama liko captured kwenye huo mradi wetu ambao tunatarajia unaweza ukaanza mwishoni mwa mwaka huu. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Waziri Mkuu alipotembelea Kata ya Jangalu kwenye Kijiji cha Itolwa aliahidi kujengwa kituo cha afya. Naomba kujua ni lini sasa kituo hicho kitajengwa maana sasa ni miaka minne, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo ya Serikali kwanza ilikuwa ni kuhakikisha tunamaliza ujenzi katika Tarafa zote, lakini lengo la pili, ni kuhakikisha zile Kata ambazo hazifikiwa na zenyewe tunazijengea vituo vya afya. Kwa hiyo, hayo ndiyo malengo ya Serikali. Tatu, ahadi zote za Viongozi ambazo zimetolewa ziko katika mpango wetu tutahakikisha kabisa kwamba zinafikiwa ikiwemo katika Jimbo la Chemba, ahsante. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Kumekuwa na michango mingi sana hasa kwa hawa wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Tano. Nina mwanafunzi ambaye hana wazazi hana familia, alikuwa anaenda Bwiru Sekondari, nimelazimika kutoa fedha nyingi mara nne zaidi ya ile fedha ya ada.

Nini sasa tamko la Serikali leo juu ya shule hizo ambazo michango ni mikubwa mara Nne zaidi ya fedha ambazo unatozwa za ada?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monnie Mbunge wa Jimbo la Chemba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kwamba yote lazima iwe imepitishwa kwa kuzingatia mazingira yaliyopo. Kama kuna shule ama kuna eneo lolote lina michango mikubwa tunaomba taarifa hizo ofisi ya Rais TAMISEMI ili tuweze kuchukua hatua katika hayo maeneo ambayo wamezidisha michango.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, michango ambayo imezidi kiwango ni michango ambayo haikubaliki na Serikali tulishatoa kauli yetu.(Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kijiji cha Kidoka na Takwa wanayo miradi maarufu ya umwagiliaji lakini mpaka leo Serikali haijawekeza chochote. Naomba kujua commitment ya Serikali katika kuwekeza kwenye miradi ya vijiji hivyo, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Monni Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikirudia mara nyingi kusema ya kwamba tumedhamiria kuyagusa maeneo mengi ambayo yanafaa kwa ajili ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao katika nchi yetu ya Tanzania, hatua ambayo inafanyika hivi sasa ni kwamba timu yetu imeendelea kuyapitia maeneo yote kufahamu status ya kila maeneo ambayo yanafaa kwa ajili ya umwagiliaji. Katika eneo ambalo Mheshimiwa amelitaja la Kidoka mimi na yeye tutatafuta muda hapa katikati tutaongozana pamoja na wataalam kwenda kulitembelea na kuona uwezekano wa kufanya uwekezaji katika eneo hilo. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, Mto Bubu umekata katikati kati ya Kijiji cha Mpendo - Hamia na hivyo kipindi cha mvua kuna na ugumu sana wa kupata mawasiliano ya barabara kuja Dodoma.

Nini mkakati wa Serikali walau wa kujenga daraja la muda ili watu wapate mawasiliano? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni, Mbunge wa Chemba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tumelipokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na tutatuma wataalam wetu waende wakafanye tathmnini waone ni namna gani linaweza likatekelezeka ndani ya muda mfupi. Ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Wananchi wa Kata ya Dalai walijihamisha wakaanza ujenzi wa kituo cha afya. Lini sasa Serikali nayo itaweka nguvu zao ili kituo kile kimalizike? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa sababu wananchi wameanza ujenzi wa kituo cha afya kwa nguvu zao, tumewapongeza kwa juhudi hizo, lakini Serikali itaendelea kutafuta fedha kama ilivyo kwa majimbo mengine yote ili kuchangia nguvu za wananchi kukamilisha vituo ambavyo vimeanza ujenzi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira kwamba Serikali inatambua hilo na italifanyia kazi. Ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Boma la Zahanati la Isusumia limemalizika tangu mwaka 2016. Naomba kujua ni lini sasa Serikali itatenga fedha ili boma lile liweze kumalizika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Wilaya ya Chemba kwa ujumla ina maeneo makubwa ya kilimo na hivyo kuna wahamiaji wengi sana. Nini mkakati wa Serikali wa kujenga zahanati kwenye maeneo yale sasa wamehamia watu wengi wa kutosha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na boma la Zahanati ya Lusubi ambayo limekamilika tangu mwaka 2016; nitoe maelekezo kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya kote nchini akiwepo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, majengo yote ya kutolea huduma za afya yakikamilika ni wajibu wao kufuatilia usajili wa zahanati zile, lakini kuweka vifaa tiba vya kuanzia ilia Zahanati zianze kutoa huduma wakati tunasubiri fedha Serikali Kuu kwa ajili ya kuanza kutoa huduma kwenye vituo hivyo kwa maana ya vifaa vya ziada vinavyohitajika.

Kwa hiyo zahanati hii, itafutiwe vifaatiba mapema iwezekanavyo kupitia mapato ya ndani, lakini pia isajiliwe ili ianze kutoa huduma mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na maeneo ya Chemba ambayo yana wananchi wengi, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha tunaendelea kujenga zahanati na vituo vya afya kwa maeneo ya kimkakati. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aainishe maeneo hayo ya kimkakati Serikali ifanye tathmini na kuona mpango wa utekelezaji. Ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Kumekuwa na michango mingi sana hasa kwa hawa wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Tano. Nina mwanafunzi ambaye hana wazazi hana familia, alikuwa anaenda Bwiru Sekondari, nimelazimika kutoa fedha nyingi mara nne zaidi ya ile fedha ya ada.

Nini sasa tamko la Serikali leo juu ya shule hizo ambazo michango ni mikubwa mara Nne zaidi ya fedha ambazo unatozwa za ada?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monnie Mbunge wa Jimbo la Chemba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kwamba yote lazima iwe imepitishwa kwa kuzingatia mazingira yaliyopo. Kama kuna shule ama kuna eneo lolote lina michango mikubwa tunaomba taarifa hizo ofisi ya Rais TAMISEMI ili tuweze kuchukua hatua katika hayo maeneo ambayo wamezidisha michango.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, michango ambayo imezidi kiwango ni michango ambayo haikubaliki na Serikali tulishatoa kauli yetu.(Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kuna vijiji vya Machiga na Chandama kuna mradi wa maji ambao tayari Kandarasi yake ilitangazwa na Mzabuni akapewa lakini mpaka leo hayupo site. Nini kauli ya Serikali kuhusu Mzabuni huyu kuwepo site? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Monni, Mbunge wa Chemba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wakandarasi wote ambao tumesaini nao mikataba wanafahamu sheria na taratibu na tayari Mheshimiwa Waziri ameshaongea mara nyingi, hatutakawa na mzaha na wale Wakandarasi ambao wanachelewa kufika site hivyo Mheshimiwa Mbunge hili nimelipokea na tutalifanyia kazi kwa karibu.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Barabara ya kutoka Chemba – Soya – Mwailanje – Zajilwa – Dodoma na Zajilwa ni Jimboni kwake, kwa sasa imeharibika sana, naomba sasa commitment ya Naibu Waziri mwenyewe, ni lini barabara ile itajengwa ili ipitike wakati wowote? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni, nikiri kwamba alipotaja Zajilwa na Itiso zimo katika Jimbo langu la Chamwino na barabara hii ya Chemba – Soya – Mwailanje itaanza ukarabati wake mara moja. Ipo katika bajeti ya mwaka huu wa 2023/2024 na tayari Meneja Maganga pamoja na Lamela - Meneja wetu wa Mkoa na Meneja wa TARURA wa Wilaya ya Chemba, wameshakaa na kuona ni namna gani wanaanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara hii, hasa katika maeneo ambayo ni korofi.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Kwanza kabisa, naomba nichukue fursa hii kuishukuru Wizara kwa majosho matano. Nina swali moja tu la nyongeza. Nataka kujua kama Wizara inajua kwa uhakika katika vijiji vyetu vyote 114, mahitaji ya majosho ni kwa kiwango gani, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni kweli kwamba Wizara ina Database ya kujua wapi panahitajika josho lipi, kwa size gani na kwa umuhimu gani? Pia, Mheshimiwa Mbunge kama anaona kuna sehemu ambapo sisi kama Serikali tunapaswa kwenda kujenga josho, alete taarifa zake tuweze kufanyia kazi kwenye maeneo hayo. Hata hivyo, mpaka sasa database ya vijiji ambavyo majosho yanatakiwa kujengwa, Serikali ina hiyo database, ahsante. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Jimbo la Chemba lina Kata tano…

SPIKA: Simamisha kisemeo vizuri.

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, Jimbo la Chemba lina Kata tano ambazo zina vijiji zaidi ya vinane, hivyo imekuwa ni kazi kubwa sana kwa Watendaji wa Kata kufanya kazi. Nini sasa msimamo wa Serikali kugawa Kata hizo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni, nirejee katika majibu yangu ya msingi, pale ambapo miundombinu itajengwa katika maeneo ya kiutawala yaliyopo sasa ya kukidhi mahitaji yote ya wananchi katika maeneo hayo, ndipo Serikali itaenda katika mchakato wa kugawa maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu unapogawa kata, maana yake inabidi shule, zahanati na vituo vya afya na huduma nyinginezo ziweze kujengwa.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa sote ni mashuhuda, Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka fedha nyingi katika kuhakikisha vituo vya afya vinajengwa, shule mpya zinajengwa katika kata ambazo zilikuwa hazina shule za sekondari. Kwa hiyo, mpaka pale mchakato huu utakapokamilika ndipo Serikali itaanzisha maeneo mapya ya kiutawala.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Mpendo na Kijiji cha Amia kinatenganishwa na mto mkubwa ambao unaitwa Mto Bubu. Ni lini sasa Serikali itajenga daraja ili kuunganisha vijiji hivi viwili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyotangulia kusema kwamba ni muhimu sana kuwe kuna mawasiliano na ndiyo kipaumbele katika mipango kazi au utekelezaji wa majukumu ya TARURA kuhakikisha kwamba mawasiliano hayakatiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kadiri alivyoleta maombi yake na kwa kuzingatia vipaumbele na upatikanaji wa fedha, Serikali itamsaidia kwenda kurekebisha miundombinu hii.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itajenga kituo cha afya katika Kata ya Ijangalo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ili kujenga kituo cha afya kuna vigezo ambavyo ni muhimu viwe vimezingatiwa. Kwa hiyo, naomba nitumie fursa hii nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutawasiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chemba ili tuweze kuona kata hiyo kama inakidhi vigezo ili tuanze kutafuta fedha za mapato ya ndani na Serikali Kuu kwa ajili ya kujenga kituo hicho cha afya, ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mvua kubwa zilizonyesha Tanzania nzima pamoja na Chemba, zimeharibu kabisa miundombinu ya barabara. Baadhi ya barabara hizo ambazo kwa sasa hazipitiki ni Barabara ya Kwa Mtoro – Sanzawa – Mpendo, Soya – Chandama, Soya – Magasa na maeneo mengine mengi. Tumeomba fedha za dharura lakini mpaka leo hatujapewa fedha kabisa. Naomba kujua ni ipi commitment ya Serikali kuhakikisha miundombinu inarudi ili watu waendelee na kazi zao kama kawaida? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa barabara zetu hizi za Wilaya. Kwa wakati huu Serikali pia inatambua kwamba barabara zetu hizi nyingi zimeharibika kutokana na mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha na ndiyo maana fedha ya dharura Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan ameongeza bajeti kutoka bajeti ya shilingi bilioni 21 mpaka shilingi bilioni 13, kwa ajili ya kuhudumia Barabara ambazo zinapata uharibifu mkubwa kama huu ili ziweze kutengenezwa kwa udharura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua changamoto ya miundombinu katika Jimbo la Mbunge na itahakikisha kwamba inaleta fedha kwa ajili ya kuhakikisha miundombinu inaimarika katika Jimbo lake.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, hospitali hiyo hiyo ya wilaya haina mtaalam wa maabara. Je, ni lini Serikali italeta mtaalam huyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kituo cha Afya Farkwa kimekamilika lakini hakina wataalam ili kianze kufanya kazi. Je, ni lini Serikali italeta wataalam ili kianze kufanya kazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Monni, kwani amefuatilia mara kadhaa kuhusiana na upatikanaji wa watumishi katika vituo vyake na Hospitali ya Halmashauri. Naomba nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanafanya internal reallocation ya mtaalam wa maabara angalau mmoja ili apelekwe haraka iwezekanavyo katika hospitali hii ya Halmashauri ambayo Mheshimiwa Mbunge anasema haina mtaalam wa maabara ili aanze kutoa huduma wakati tunasubiri vibali vya ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusiana na wataalam kukosekana katika kituo hicho cha Farkwa, naomba nimhakikishie kwamba tunaendelea kuajiri wataalam. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kibali. Kwa hiyo, itakapofika hatua ya kuajiri tutahakikisha kuwa tunapeleka watumishi kwenye kituo hicho ili kianze huduma kwa wananchi, ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Upungufu wa watumishi wa afya Wilaya ya Chemba ni zaidi ya 62%. Nini kauli ya Serikali juu ya hawa watumishi wapya watakaoajiriwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa watumishi katika Halmashauri ya Chemba na maeneo mengine umesababishwa pia na kasi nzuri ya ujenzi wa vituo vya huduma za afya, lakini Serikali katika miaka hii mitatu imeshaajiri watumishi zaidi ya 14,000 na kuwapangia katika Halmashauri ya Chemba na maeneo mengine kote nchini. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Monni kwamba katika ajira hizi ambazo zinaendelea na utaratibu kwa sasa, tutahakikisha pia zahanati hiyo inapata watumishi.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kituo cha Afya cha Soya ni cha muda na hakina gari la wagonjwa. Ni lini sasa Serikali itapeleka gari la wagonjwa katika kituo hicho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu mkubwa sana wa kuwa na magari ya kusafirishia wagonjwa katika vituo vyetu vya kutoa huduma za afya ya msingi imekuwa ikifanya utaratibu wa kununua na kupeleka magari haya. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kwa kadiri ya upatikanaji wa haya magari na kwa kuzingatia vipaumbele vya uhitaji, basi gari hili litafikishwa katika jimbo lako, kwa ajili ya kuhudumia kituo ulichokitaja.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; maeneo ya vijiji vyote vinavyozunguka Mradi wa Bwawa la Farkwa, mradi mkubwa kabisa, Kijiji cha Sakaletwa, Gonga Chini na Gonga vyote havina mawasiliano. Naomba kujua ni lini sasa, Serikali itajenga mnara katika maeneo ya mradi ule unaoendelea ili wafanyakazi wote walioko pale wapate mawasiliano?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Kijiji cha Magasa wataalamu walifika wakaainisha eneo la kujenga mnara, lakini mpaka leo hawajarudi. Naomba kujua ni lini sasa watarudi ili kuendelea na kazi ile? Ahsante.
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Monni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, eneo la Mradi mkubwa wa Bwawa la Farkwa kwenye vijiji alivyovitaja vya Sakaletwa, Gonga na Gonga Chini kuna mahitaji makubwa ya huduma za mawasiliano. Wataalamu wetu walishafika eneo hili na wamefanya uchambuzi na taarifa zipo Wizarani, utaratibu unaendelea kwa ajili ya kuwapatia huduma za mwasiliano kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Kijiji cha Makasa alichokitaja ni katika vijiji ambavyo viliingizwa kwenye mradi ule wa minara 758 na UCSAF waliingia makubaliano na TTCL na tayari walishalipa hela ya awali na wamesaini. Kwa hiyo, kazi itaanza hivi karibuni, wamesaini mkataba huo Mwezi Machi na huu Mwezi Aprili mwishoni kazi itaanza. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina swali moja tu la nyongeza. Tulikuwa na mpango wa ujenzi wa mabwawa mawili kwenye Wilaya ya Chemba, Bwawa la Ndoroboni na Bwawa la Babayu, naomba kujua sasa ujenzi wake utaanza lini? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Monni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kama Serikali tunatangaza jumla ya mabwawa 100 kwa ajili ya kufanya usanifu na kila usanifu unavyokamilika tutakuwa tunatangaza bwawa hilo katika mwaka huo wa fedha au mwaka mwingine wa fedha. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge, mimi na yeye tuonane baadaye tuangalie haya mabwawa mawili kama yamo ndani ya mabwawa 100 ambayo yametangazwa kwa ajili ya kufanyiwa usanifu. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, nina swali moja muhimu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika Kijiji cha Igunga tumechimba maji mara tatu lakini hatujapata maji ardhini. Tumeomba shilingi 300,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kuyatoa Ntomoko kuyaleta kwenye Kijiji cha Igunga. Nini kauli ya Serikali juu ya kuleta fedha hizo ili Watu wa Igunga waweze kupata maji? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Kijiji cha Igunga baada ya kufanya utafiti na kuchimba maeneo kadhaa tukajiridhisha kwamba hakuna maji. Sasa, Serikali ikaangalia chanzo kilichopo Ntomoko na tayari Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekubali kutoa kiasi cha shilingi 350,000,000 kwa ajili ya kuyaleta maji kutoka Ntomoko kuja katika Kijiji cha Igunga. Nakushukuru sana.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, barabara ya kutoka Kwamtoro - Sanzawa - Mpendo yenye kilometa 54 imeharibika sana kwa sababu ya mvua kubwa iliyonyesha, hata hivyo, tumeleta maombi maalum.

Je, ni lini sasa Serikali italeta fedha ili tuweze kufanya ukarabati wa barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa maombi yake haya sisi tuliyapokea na tunayafanyia kazi ili tuweze kuhakikisha kwamba dhamira ya Rais inatimia ya kuhakikisha Watanzania wanapata barabara zilizo bora ambazo zinapitika katika misimu yote katika mwaka mzima.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunafanyia kazi maoni haya mahsusi kabisa na pindi fedha zitakapopatikana tunakuja kuhakikisha kwamba tunajenga barabara hizi. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Jangalo, Mpendo na Lahoda ni kata za mpakani, mwaka 2003 Serikali ilifanya tathmini kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya, nataka kujua ni lini sasa Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kata zote za kimkakati tayari tumeshazianisha kwa awamu, tulishaanza na awamu ya kwanza mwaka wa fedha 2021/2022, tupo awamu ya pili mwaka wa fedha 2023/2024. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatafuta fedha na kwenda kujenga vituo vya afya hivyo kwa awamu kadiri ambavyo tumeweka mpango mkakati katika nchi nzima, ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, Kata za Mpendo, Jangalo na Lahoda ni kata za mpakani na hakuna kabisa huduma ya vituo vya afya. Naomba kujua, ni lini Serikali itatenga fedha ili kujenga vituo vya afya kwenye kata hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nirejee maelekezo ya Serikali na msisitizo wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwamba Wakurugenzi wote katika Mamlaka za Serikali za Mitaa watambue maeneo ya kimkakati na maeneo ambayo wananchi wako mbali zaidi na vituo vya huduma za afya, waanze kutenga fedha za mapato ya ndani ili kuanza ujenzi wa maeneo hayo. Wakati huo walete tathmini na gharama zinazohitajika Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi, kukamilisha vituo hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kumkumbusha Mkurugenzi wa Chemba kwamba waandae na watenge fedha kwenye bajeti, pia waanze ujenzi. Sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutahakikisha tunakamilisha ujenzi wa kituo hicho, ikiwa eneo hilo linakidhi vigezo vya kuwa na kituo cha afya, ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Chemba unakua kwa kasi sana. Ninataka kujua ni lini sasa Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa stendi, ambapo tayari andiko tumeshaleta kwenye Ofisi ya TAMISEMI. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Chemba walishawasilisha andiko la ujenzi wa stendi na tayari limeshafanyiwa uchambuzi katika ngazi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, na limeshawasilishwa Hazina. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Chemba kwamba Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo la stendi ya Chemba. Ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mradi wa REA, kuna vijiji vitatu vya Wilaya ya Chemba vilisahaulika; Kijiji cha Kelema Kuu, Kijiji cha Birise na Kijiji cha Muungano na bahati nzuri hatuhitaji sisi fidia, tunahitaji umeme tu. Naomba kujua, ni lini sasa vijiji hivyo vitawekewa umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Monni amekuwa akifuatilia kweli vijiji hivi vitatu ambavyo vilisahaulika katika mpango, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeshafanyia kazi na vijiji hivi vya Kelema Kuu, Birise na Muungano, tayari tumeshaongea na mkandarasi kwa ajili ya kumwongezea wigo ili aweze kuanza kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa hakuna kijiji kitaachwa kupelekewa umeme katika mradi huu ambao unaendelea. Kwa hiyo, wakae kwa utulivu, Serikali tumesikia na tutapeleka umeme katika hivi vijiji vitatu, ahsante.