Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Nicodemas Henry Maganga (18 total)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA Aliuliza:-

Je ni lini Serikali itajenga chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2019/2020, Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya halmashauri. Majengo yaliyohusika katika awamu ya kwanza ni jengo la wagonjwa wa nje na maabara. Ujenzi wa majengo hayo upo katika hatua ya ukamilishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 60.5 ambapo kiasi cha shilingi 33.5 ni kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali za halmashauri 67 nchini na kiasi cha shilingi bilioni 27 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za halmashauri 27 mpya ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe iliyotengewa kiasi cha shilingi bilioni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe inaelekezwa pamoja na majengo mengine, kujenga jengo la kuhifadhia maiti pindi itakapopokea fedha za ujenzi kwa kuwa tayari ina majengo mawili kati ya majengo saba yanayotakiwa kujengwa na hivyo fedha iliyotengwa kwenye bajeti ya mwaka 2020/2021 itakuwa sehemu ya fedha ya kujenga jengo la kuhifadhia maiti.
MHE. NICODEMUS H. MAGANGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Wilayani Mbogwe maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya matumizi ya Wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemus Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Wilaya ya Mbogwe ni wastani wa asilimia 55. Huduma hiyo ya maji inapatikana kupitia miradi minne ya skimu, visima virefu 26, visima vifupi 460 na matanki 55 ya kuvuna maji ya mvua, vituo vya kuchotea maji 61 na maunganisho ya nyumbani 192.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha huduma za maji, Serikali katika mwaka wa fedha 2020/2021, ilitenga jumla ya shilingi bilioni 2.9 kwa ajili ya upanuzi wa miradi ya maji Lulembela na Nyakafuru, ujenzi wa miradi mipya ya maji Mbogwe, Nanda na Kabanga-Nhomolwa. Hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 1.8 zimetolewa, ambapo kazi zilizofanyika ni ujenzi wa nyumba ya pampu ya kusukuma maji, matenki matano, vituo vya kuchotea maji 48 na ulazaji wa bomba lenye urefu wa kilometa 31. Utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Aprili, 2021 na kuongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kufika asilimia 61 ifikapo mwezi Disemba, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali kupitia Mpango wa Mradi wa Maziwa Makuu kupitia Ziwa Victoria, katika Wilaya ya Mbogwe itatekeleza miradi katika Vijiji vya Kagera, Ilolangulu, Buningozi, Ngemo, Isungabula na Iponya.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kufuta madeni ya muda mrefu kwa wafanyabiashara wa ndani yatokanayo na ukosefu wa elimu juu ya matumizi sahihi ya mashine za EFD wanayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali ilitoa msamaha kwa wadaiwa wa kodi ili kuongeza makusanyo. Msamaha huu ulihusisha riba na adhabu zilizoambatana na madeni yote yaliyolimbikizwa kwa miaka ya nyuma. Msamaha huu ulilenga kusamehe malimbikizo ya nyuma ya riba na adhabu kwa kiwango cha asilimia 100 kwa wafanyabiasha wote hapa nchini ambao walikuwa na malimbikizo ya madeni ya kodi. Msamaha huo ulitolewa kwa kipindi cha miezi sita kilichoanzia tarehe 1 Julai, 2018 mpaka tarehe 31 Desemba, 2018 ambapo kutokana na kusuasua kwa utekelezaji wake, Serikali iliongeza muda wa msamaha huo kwa miezi sita ili wafanyabiashara waliokuwa na madeni hayo kuweza kukamilisha malipo husika yaliyotokana na msamaha huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hiyo ya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi Sura 438 ilitarajiwa kuongeza mapato ya Serikali na kukusanya malimbikizo ya madeni ya nyuma ya kodi pamoja na kuinua kiwango cha ulipaji kodi kwa hiyari kwa zaidi ya asilimia 10.

Hata hivyo, licha ya nia nzuri ya Serikali ya kufuta riba na adhabu ili kuwawezesha walipa kodi wenye madeni sugu ya kodi kuyalipa kwa awamu ili kurahisisha mwendelezo wa biashara zao, wengi wao hawakulipa kodi hizo hata baada ya kuingia mikataba na TRA na hata baada ya Serikali kuongeza muda wa ziada wa kufanya malipo ya kodi husika yaliyotokana na msamaha huo. (Makofi)
MHE. NICODEMUS H. MAGANGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza barabara zote mbovu zilizopo katika Jimbo la Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemus Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbogwe lipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe lina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 1,344.3. Serikali imekuwa ikifanyia matengenezo ya barabara mbovu, pamoja na matengenezo ya kawaida kwa barabara zenye hali nzuri kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika mwaka wa fedha 2019/2020, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe iliidhinishiwa shilingi bilioni 1.30 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 78.6, makalvati mistari 27, boksi kalvati moja pamoja na ujenzi wa barabara ya Mang’ombe – Magetini mpaka Kona nne, yenye urefu wa kilometa 1.2. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, jumla ya shilingi bilioni 1.64 ziliidhinishwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 46.6, makalvati mistari 18 pamoja na ujenzi wa barabara ya Masumbwe – Iponya yenye urefu wa kilometa moja kwa kiwango cha lami na barabara ya Mang’ombe, Magetini – Kona nne, yenye urefu wa kilomita 0.8 kwa kiwango cha lami, ujenzi wa barabara hizo umekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, Katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.14 kwa ajili ya matengenezo ya barabara yenye urefu wa kilometa 74.96, Mtaro wa mawe kilometa 1.2 na ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa moja kwa kiwango cha lami katika Mji wa Masumbwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matengenezo yaliyofanyika katika mwaka wa fedha 2019/2020 na 2020/2021, yamejumuisha barabara muhimu zilizokuwa mbovu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, zikiwemo barabara ya Shenda - Mwabomba yenye urefu wa kilometa 17, barabara ya Isebya-Lwamgas yenye urefu wa kilometa 10. Barabara ya Ushirika-Kadoke-Ntono yenye urefu wa kilomita 5.5, barabara ya Ikunguigazi – Isabya - Nyashinge yenye urefu wa kilometa 15, barabara ya kanegere – Prison-Nyakasaluma- Bunyihuna yenye urefu wa kilometa 19.46, barabara ya Ishigamva-Busabaga-Ilolangu yenye urefu wa kilometa 15 na barabara ya Ilolangu -Kisumo-Bukombe boda yenye urefu wa kilomita 17.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, ili kuhakikisha zinapitika katika majira yote ya mwaka na kuwezesha huduma za usafiri na usafirishaji.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba ikiwemo x-ray pamoja na vifaa vingine vya kupima wagonjwa katika hospitali zilizojengwa hivi karibuni hasa katika Wilaya mpya ikwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Jimbo la Mbogwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetoa shilingi bilioni 34 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali 67 za Halmashauri zilizoanza kujengwa katika mwaka wa fedha 2018/2019. Fedha hizo zimepelekwa Bohari Kuu ya Dawa na utaratibu za kupeleka vifaa tiba katika Hospitali 67 zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali mpya ya Halmashauri.

Aidha, mwezi Mei, 2021 Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ambapo majengo mapya matano yamejengwa na yameyakamilika. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali na shilingi milioni 487 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe. Ahsante.
MHE. NICODEMUS H. MAGANGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia Wananchi Pori la Kanegere kwa matumizi ya Wafugaji kwa kuwa Pori hilo limepoteza sifa ya kuwa Hifadhi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Henry Maganga, Nicodemus, Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, kama ifatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Pori la Kanegere lina ukubwa wa hekta 725.24 na lipo kwenye Kijiji cha Kanegere ambacho kina eneo lenye ukubwa wa hekta 4,443.35. Kijiji hicho tayari kimeandaa Mpango wa Matumizi ya Ardhi kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Kijiji Na.5 ya mwaka 1999 na Sheria ya Matumizi Ardhi Na.6 ya Mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika, Pori la Kanegere linamilikiwa na kijiji na sehemu kubwa ya pori hilo ipo katika safu ya milima. Eneo hilo halifai kwa ajili ya shughuli za ufugaji kwani ni eneo lenye miinuko mikubwa ya milima.

Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango wa Matumizi ya Ardhi ulioandaliwa, wananchi wamelitenga eneo hilo kwa ajili ya kuhifadhi na kupunguza mmonyoko wa udongo unaoathiri mazingira ya kijiji kwa ujumla wake. Aidha, kwa upande wa wafugaji mpango huo umetenga eneo la malisho lenye ukubwa wa hekta 405.02 ambalo inashauriwa wafugaji kulitumia kwa ajili ya mifugo yao.

Mheshimiwa Spika, hivyo, natoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe kushirikiana na Mamalaka husika ili kukamilisha taratibu za pori hilo kutangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali kwa manufaa mapana ya Kijiji, Halmashauri na nchi kwa ujumla. Ahsante.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza: -

Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya askari wa misitu wanaopiga na kuwanyang’anya mkaa wananchi wa Mbogwe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Askari wa Uhifadhi wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo ya viongozi mbalimbali ikiwemo ya Waheshimiwa Wabunge pamoja na kuzingatia haki za binadamu. Endapo kuna uvunjaji wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo, Wizara haitosita kuwachukulia hatua watumishi wake wanaohusika na uvunjaji huo wa sheria.

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na wimbi la uvunaji wa mazao ya misitu, ukataji na uchomaji wa mkaa bila kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia biashara hii. Hali hii imesababisha kutoweka kwa kasi kwa maeneo ya misitu na hatimaye kujitokeza kwa athari za mabadiliko ya tabia nchi. Hivyo, inapotokea mwananchi anasafirisha mazao ya misitu (mkaa) bila kufuata utaratibu, mazao hayo hutaifishwa na Serikali. Nitoe rai kwa wananchi wanaojishughulisha na biashara hiyo kufuata sheria, kanuni na taratibu husika.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Skimu za Umwagiliaji katika Jimbo la Mbogwe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na zoezi la utambuzi na uhakiki wa maeneo zaidi yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe. Hadi sasa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na wananchi wa Mbogwe wameweza kuibua Skimu ya Mugelele yenye eneo la ukubwa wa hekta 300. Aidha, baada ya zoezi hilo kukamilika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itatenga fedha katika bajeti ya mwaka 2023/2024 kwa ajili ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia Watu Wenye Ulemavu mitaji katika Jimbo la Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ilitenga shilingi milioni 56 kwa ajili ya mikopo ya watu wenye ulemavu. Hadi kufikia mwezi marchi, 2023 jumla ya vikundi 6 vya watu wenye ulemavu vimekopeshwa kiasi cha shilingi milioni 34. Fedha hizi zimewezesha vikundi vya watu wenye ulemavu kuanzisha biashara na kujiongezea kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe imetenga shilingi milioni 56.19 kwa ajili ya mikopo isio na riba kwa vikundi vya watu wenye ulemavu. Fedha hizi zitatolewa kupitia mfumo ulioboreshwa wa asilimia 10, ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI K.n.y. MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itatatua tatizo la ukosefu wa maji katika Jimbo la Mbogwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemus Henry Maganga Mbunge wa Jimbo la Mbogwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji Wilayani Mbongwe ni wastani wa asilimia 55. Katika kupunguza kero ya maji kwa wananchi wa Wilaya hiyo, Serikali ina mipango ya muda mfupi na muda mrefu, ambapo Katika mpango wa muda mfupi Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji ya Iponya, Kagera, Kanegere na Lugunga-Luhala. Miradi hiyo imeanza kutoa huduma kwa wananchi. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itachimba visima virefu 28 sambamba na kufanya upanuzi wa miradi ya maji ya Lulembela, Kagera, Kanegere na ujenzi wa miradi mipya ya maji katika vijiji vya Kisumo, Nyang’holongo, Ikobe, Ngemo, Bwendamwizo, Isebya, Ushirika, Mlale, Kadoke, na Mpakali. Kukamilika kwa Miradi hiyo kutaongeza huduma ya maji kufikia wastani wa asilimi 75.

Mheshimiwa Spika, mpango wa muda mrefu ni kutekeleza mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Wilaya ya Mbogwe ambapo usanifu wa mradi huo unaendelea na utakamilikaji katika mwaka wa fedha 2023/2024 na ujenzi kuanza.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuza: -

Je, kuna mpango gani wa kuongeza thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na nchi jirani za Afrika Mashariki?
WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kulinda thamani ya shilingi ya Tanzania kwa hatua zifuatazo: -

(i) Kushirikisha sekta binafsi katika kuimarisha mikakati ya kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi;

(ii) Kuhimiza wananchi kuongeza matumizi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa hapa nchini ili kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni;

(iii) Kusimamia kwa karibu wazalishaji wa ndani ili kuongeza ubora katika uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa lengo la kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi;

(iv) Kuendelea kusimamia utekelezaji wa kifungu 7(3) na 13(1) cha Kanuni za Fedha za Kigeni za mwaka 2022, zinazoelekeza wafanyabiashara kuweka katika benki zilizopo nchini fedha za mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi ndani ya siku 90 tangu siku ya kusafirisha bidhaa au kutoa huduma na wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje kufanya malipo kwa kutumia benki na taasisi nyingine za fedha zilizopo nchini;

(v) Kuongeza vyanzo vya upatikanaji wa fedha za kigeni ikiwemo ununuzi wa dhahabu;

(vi) Kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji kutoka nje; na

(vii) Kusimamia utekelezaji wa sera ya fedha ili kuhakikisha utulivu wa mfumuko wa bei hapa nchini.
MHE. NICODEMUS H. MAGANGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha pesheni za wastaafu zinalipwa kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemus Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwneyekiti, pensheni ni mafao wanayolipwa wanachama waliostaafu kwa kila mwezi katika kipindi chote cha maisha yao. Katika kuhakikisha wastaafu wanalipwa pensheni zao kwa wakati, Serikali kupitia Mifuko ya Pensheni ya PSSSF na NSSF imeweka utaratibu mahsusi wa kufanya malipo kwa njia ya kielektroniki kupitia kwenye akaunti zao za benki kila au ifikapo tarehe 25 ya kila mwezi. Hadi kufikia mwezi Machi, 2023 idadi ya wastaafu wanaolipwa pensheni katika Mifuko ya PSSSF na NSSF imefikia 186,605 ikijumuisha PSSSF wastaafu 158,735 na NSSF wastaafu 27,870.

Mheshimiwa Mwneyekiti, mifuko inaendelea kuimarisha mifumo ya ndani ya ulipaji wa mafao ili kuhakikisha maombi ya wastaafu wapya yanafanyiwa kazi kwa haraka na kuanza kulipwa pensheni ndani ya kipindi kisichozidi siku 60 kama sheria inavyotaka, ahsante.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia mikopo katika Wilaya ya Mbogwe?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo mwanzo Serikali ilikuwa na utaratibu wa kuwapatia mikopo wachimbaji wadogo kwa lengo la kuwaongezea mitaji ili kuwafanya wafanye shughuli zao kwa tija. Baadaye tathmini ilifanyika na ilionesha upotevu wa fedha hizo. Kufuatia tathmini hiyo, Serikali inaendelea kuangalia namna bora ya kuwapatia mikopo wachimbaji wadogo nchini wakiwemo wa Wilaya ya Mbogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hatua hiyo, Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeingia makubaliano (MoU) na Benki za CRDB, NMB na KCB kwa ajili ya kuwapatia mikopo wachimbaji wadogo.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza: -

Je, ni lini mradi wa barabara wa kilometa 96 unaofadhiliwa na Benki ya Dunia utafika Mbogwe?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Henry Nicodemas Maganga, Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Tanzania, kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), inatekeleza Mradi wa Maendeleo ya Barabara kwa Ushirikishaji Jamii na Ufunguaji Fursa za Kijamii na Kiuchumi Vijijini (Roads to Inclusion and Socioeconomic Opportunities - RISE). Mradi huu utagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 350, ambapo, kiasi cha milioni 300 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na milioni 50 ni mchango wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ni miongoni mwa Halmashauri zitakazonufaika na Mradi wa RISE ambapo jumla ya kilometa 96 zinaratajiwa kujengwa. Kwa sasa TARURA ipo kwenye hatua ya manunuzi ya Mtaalamu Mshauri wa kufanya usanifu wa kina (detailed engineering design) wa barabara zilizopendekezwa. Ujenzi unatarajiwa kuanza ndani ya mwaka wa fedha 2022/2023 baada ya usanifu kukamilika, ahsante.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kwa Watumishi wanaohusika kutumia vibaya fedha za miradi ya Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia masuala ya nidhamu katika Utumishi wa Umma kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 6(1)(b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 ambacho kimewapa Mamlaka Wakuu wa Taasisi kusimamia masuala ya nidhamu kwa watumishi walio chini yao pale wanapokiuka kiapo cha ahadi ya uadilifu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia uvunjifu wa maadili katika utekelezaji wa majukumu ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Serikali imeendelea kuwachukulia hatua mbalimbali za kinidhamu Watumishi wa Umma wanaotumia vibaya fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo kuwasimamisha kazi na kuwaanzishia mashauri ya kinidhamu.

Mheshimiwa Spika, mathalan, katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Desemba, 2023, TAKUKURU ilifuatilia matumizi ya rasilimali za umma kwenye utekelezaji wa miradi 2,541 yenye thamani ya shilingi trillioni 8.26, ambapo miradi 467 ilibainika kuwa na upungufu mbalimbali ikiwemo uvujaji na kutokuwa na thamani ya fedha. Kutokana na matokeo hayo, hatua kadhaa zilichukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura 329, ikiwa ni pamoja na kuanzisha uchunguzi kwa miradi 274 ambapo watumishi 51 walichukuliwa hatua za kinidhamu.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza:-

Je, lini barabara za lami zinazofadhiliwa na Benki ya Dunia zitaanza kujengwa Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa RISE katika Wilaya ya Mbogwe zina jumla ya urefu wa kilometa 102. Barabara zitakazojengwa kwenye Mradi huo ni Masumbwe – Iponya - Nyashimba (kilometa 20), Lulembela – Kiseke – Isebya (kilometa 17), Mkweni – Nhomolwa - Nyanhwiga (kilometa 21), Ishigamva – Busabaga – Ilolangulu (kilometa 14) na Ivumwa – Ushirika - Shibutwe (kilometa 30).

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huu utafanyika kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa Barabara za Masumbwe – Iponya – Nyashimba (kilometa 20), Lulembela – Kiseke – Isebya (kilometa 17), Ishigamva – Busabaga – Ilolangulu (kilometa 14) na Mkweni – Nhomolwa – Nyanhwiga (kilometa 21). Aidha, kazi za usanifu wa barabara za awamu ya kwanza zilianza Januari, 2024 na zinatarajiwa kukamilika Agosti, 2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kazi ya usanifu wa barabara kukamilika Serikali kupitia TARURA itatangaza zabuni na kumpata mkandarasi wa kujenga barabara za awamu ya kwanza kwa kiwango cha lami.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuchimba malambo kwa ajili ya mifugo ili kurahisisha shughuli za ufugaji Mbogwe?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo katika Jimbo la Mbogwe. Aidha, pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali za kujenga mabwawa na kuchimba visima virefu kwa ajili ya maji ya mifugo, bado mahitaji ni makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuchimba malambo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe lipo kwenye Mipango ya Serikali. Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa bajeti halikuweza kuzingatiwa kuingizwa kwenye vipaumbele vya mwaka 2024/2025. Pamoja na hayo, Serikali inaendelea kuliweka suala hili kwenye mipango ijayo ya utekelezaji wa bajeti kwa kadri ya upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha Raia wa Kigeni hawashiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288 na kanuni zake za mwaka 2024, raia wa Tanzania ndio wenye haki ya kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu kwa kupiga kura au kuchaguliwa kuwa Viongozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kusimamia vipindi vyote wakati wa uchaguzi, Serikali imekuwa ikitoa elimu ya uraia kwa watendaji (waandikishaji na wasimamizi wa uchaguzi) ili kuhakikisha raia wa Tanzania wenye sifa ndio wanaoshiriki katika chaguzi na sio raia wa kigeni. Aidha, inapobainika kwamba kuna mtu anadiriki kujiandikisha ama kutafuta fursa ya kugombea na zipo taarifa au tuhuma, kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Uchaguzi, mhusika huyo huwekewa pingamizi na ikithibitika mtu huyo huchukuliwa hatua za kisheria ikiwepo kuondolewa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura sanjari na kufikishwa Mahakamani, ahsante.