Primary Questions from Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo (20 total)
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO Aliuliza:-
Ofisi ya TANESCO Wilaya ya Muleba inazidiwa na wingi wa wateja kutokana na miradi ya REA.
Je, ni lini Wilaya hiyo itapewa hadhi ya Mkoa wa TANESCO ili iweze kutoa huduma kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Umeme nchini (TANESCO) limekuwa likiweka ofisi za Mikoa katika maeneo mbalimbali kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ongezeko la shughuli za kiutendaji za Shirika na mahitaji ya umeme pamoja na wateja.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kusogeza huduma kwa wateja karibu Wilayani Muleba, TANESCO imefungua ofisi ndogo (sub-office) eneo la Kamachumu na imeshaanza kutoa huduma kwa wateja wa Kamachumu katika Jimbo la Muleba Kaskazini na maeneo mengine ya jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, TANESCO inatarajia kufungua ofisi ndogo (sub-office) nyingine eneo la Kyamyorwa na Bulyage ili kusogeza karibu zaidi huduma kwa wateja wa maeneo hayo na jirani. Ofisi hizo zitakuwa na wafanyakazi pamoja na vitendea kazi vyote vinavyohitajika ikiwa ni pamoja na usafiri.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -
(a) Je, ni lini miradi ya kilimo cha umwagiliaji ya Kyamyorwa na Buhangaza iliyopo Wilaya ya Muleba itakamilika na kuanza kutumika?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza Bonde la Mto Ngono kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini kwa Pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Skimu ya Buhangaza na Skimu ya Kyamyorwa zilizoko Muleba Kusini zote mbili kwa ujumla zina eneo la ekari 700. Wizara ya Kilimo imeshafanya kuendeleza jumla ya ekari 215 na ili kuhakikisha kwamba miradi ya kilimo cha umwagiliaji inakamilika na kuanza kutumika ikiwemo miradi hiyo miwili, Wizara imeweka vipaumbele. Cha kwanza, ni kuhakikisha kwamba miradi yote ambayo ni kiporo iliyokwishajengwa ili kubaini kama kuna upungufu unaosababisha kushuka kwa ufanisi wa uzalishaji na kufanyia tathmini, kuhuisha usanifu uliofanyika awali kwa utaratibu wa kutumia wakandarasi na kuiweka kwenye mfumo wa usanifu na ujenzi kwa maana ya utaratibu wa force account. Kwa hiyo tathmini ya awali inafanyika ili kuweza kuangalia mahitaji halisi ya skimu hizo mbili kuweza kuzikamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uendelezaji wa bonde la Mto Ngono, katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, Serikali ilifanya upembuzi yakinifu katika bonde hilo lililopo katika Wilaya za Misenyi na Bukoba Vijijini na kubaini eneo lenye hekta 11,700 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kuendeleza bonde la Mto Ngono kwa kuanza na ujenzi wa Bwawa la Kalebe lenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo milioni 268 ambazo zitaweza kumwagilia eneo lote la hekta 11,700. Bwawa hilo litatumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, kuzalisha umeme, maji ya mifugo, ufugaji wa samaki na kuzuia mafuriko. Aidha, Andiko la Mradi limewasilishwa kwa wadau wa Maendeleo na majadiliano ya kupata fedha za utekelezaji wa mradi yanaendelea. (Makofi)
MHE. OSCAR I. KIKOYO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Katerela kwa ajili ya Kata za Kasharunga na Rulanda?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante. kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini Kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jitihada za kuhakikisha wananchi Wilayani Muleba wanapata huduma ya maji, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imekamilisha miradi ya maji ya Bulembo, Kasharunga, Ruteme, Ilogero na Kyota. Pia, utekelezaji wa miradi ya Nshamba, Kishamba na Kashansha unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Mei, 2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia RUWASA katika mwaka wa fedha 2021/2022 imepanga kuanza ujenzi wa mradi wa maji kutoka chanzo cha maji Katerela utakaowanufaisha wakazi wapatao 19,619 katika Kata za Kasharunga na Rulanda. Mradi huu unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi million 700 ambapo utahusisha ujenzi wa chanzo cha maji, ujenzi wa matanki mawili ya maji ukubwa wa lita 200,000 na lita 300,000, ujenzi wa nyumba ya mtambo, vituo vya kuchotea maji 25 na ujenzi wa mtambo wa bomba za maji umbali wa mita 40,130.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -
Mihimili muhimu ya uchumi wa soko ni Mamlaka za Udhibiti, Tume ya Ushindani na Mamlaka ya kulinda haki na maslahi ya Watumiaji: -
(a) Je, ni lini Serikali itaunda mamlaka yenye nguvu ya kulinda haki na maslahi ya watumiaji nchini?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kutunga Sheria ya kuwalinda Watumiaji?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kumlinda Mlaji/Mtumiaji na inatekeleza jukumu hilo kupitia Sheria ya Ushindani Namba 8 ya Mwaka 2003 (The Fair Competition Act). Sheria hiyo ndiyo iliyounda Tume ya Ushindani (Fair Competition Commission – FCC) ambayo ndiyo mamlaka ya kuwalinda walaji/watumiaji wa bidhaa na huduma nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Sheria hii, Serikali imekamilisha uundaji wa Baraza la Kumtetea na Kumlinda Mlaji (National Consumer Advocacy Council) ambalo litakuwa na jukumu la kisheria kusimamia haki za mlaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kuhakikisha Baraza hilo linaanzishwa ili liweze kujitegemea nje ya FCC, ili liweze kufanya kazi zake kwa ufasaha.
Aidha, Serikali inakamilisha maandalizi ya Sera ya Ubora ambayo pia ni muhimu katika kulinda haki za walaji/ watumiaji.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inazo sheria mbalimbali za kumlinda mlaji. Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Ushindani Namba 8 ya Mwaka 2003, Sheria ya Viwango ya Mwaka 1975, Sheria ya Vipimo ya Mwaka 1982, Sheria ya Usalama Mahali pa Kazi ya Mwaka 2003, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Sheria ya Chakula, Madawa na Vipodozi ya mwaka 2003. Chini ya sheria hizo walaji mbalimbali hulindwa.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani mahsusi wa kuhakikisha vijana wote wanaoomba mikopo ya Elimu ya Juu wanapata mikopo hiyo kama walivyoomba?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kugharamia utoaji wa mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo iliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi wa Elimu ya Juu mhitaji anapata mkopo kwa ajili ya kugharamia masomo yake. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imekua ikiongeza fedha za bajeti ya mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kila mwaka. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 570 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu ikiwa ni ongezeko la bilioni 106 kutoka bilioni 464 ya mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ongezeko hilo la fedha za bajeti, wanufaika wa mikopo ya Elimu ya Juu wamekuwa wakiongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo katika mwaka 2021/2022 wanafunzi wanufaika wa mikopo ya Elimu ya Juu walikua 176,617 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 27,228 kutoka wanafunzi 149,389 wa mwaka 2020/ 2021.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuongeza fedha za mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kulingana na ongezeko la fedha katika bajeti yake ili kuhakikisha vijana wote wanaoomba mikopo ya Elimu ya Juu wanapata mikopo hiyo kama walivyoomba. Ahsante sana.
MHE. DKT.OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa skimu za umwagiliaji Wilayani Muleba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Kamati Shirikishi ya Umwagiliaji Mkoa na Ofisi ya Kilimo Wilaya ya Muleba imekamilisha tathmini ya kina ya mahitaji ya sasa ya skimu za umwagiliaji za Buyaga hekta 120, Kyamyorwa hekta 500, Kyota hekta 120 na Buhangaza hekta 600 na kupata gharama halisi za umaliziaji wa ujenzi wa skimu hizo. Serikali inaendelea na zoezi la kuainisha maeneo mengine yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji Wilayani Muleba likiwemo Bonde la Buligi lenye takribani hekta 5,000.
Mheshimiwa Spika, skimu hizo zitaingizwa katika mpango wa ujenzi na ukamilishaji wa skimu za umwagiliaji katika kipindi cha mwaka 2023/2024 na 2024/2025.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Uwanja wa Ndege Kimataifa wa Omukajunguti ili kuruhusu ndege kubwa kutua Bukoba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kujenga kiwanja kipya cha ndege katika eneo la Omukajunguti, Mkoani Kagera ili kuwezesha ndege kubwa ziweze kuruka na kutua.
Mheshimiwa Naibu Spika, Uthamini wa awali kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi watakaoathirika na utekelezaji wa mradi ulishafanyika. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi ya kuanza kwa ujenzi wa kiwanja hicho cha ndege. Ahsante.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza:-
Je, ni kwa kiwango gani task forces zimepunguza tatizo la uvuvi haramu katika Ziwa Victoria kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2017/2018 - 2019/2020, Kikosi Kazi kilifanya doria na operesheni katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Ziwa Victoria. Utekelezaji wa doria hizo uliwezesha kukamatwa kwa zana haramu zilizokuwa zikitumika katika shughuli za uvuvi ikiwemo nyavu za makila, makokoro, nyavu za timba (monofilament) na nyavu za dagaa. Pia, vifaa vilivyokuwa vinatumika kwenye uvuvi haramu na utoroshaji wa mazao ya uvuvi ikiwemo injini pamoja na boti na magari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa doria hizo katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria uliwezesha kupungua kwa vitendo vya uvuvi haramu, biashara ya samaki wachanga na utoroshaji wa mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi kwa asilimia takribani 80; ahsante.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kukiongezea mtaji kiwanda cha Kahawa cha TANICA?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mwenendo wa kibiashara usioridhisha wa Kiwanda cha Tanganyika Instant Coffee Company Limited (TANICA) unaochangiwa na changamoto ya ukosefu wa mtaji, uchakavu wa mitambo, matumizi ya teknolojia iliyopitwa na wakati na kiwanda kuwa na madeni makubwa. Kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, Serikali imefanya upembuzi yakinifu wa mahitaji ya rasilimali fedha kwa ajili ya kuendesha kiwanda hicho, ambapo imebainika kuwa zinahitajika takribani dola za Marekani milioni 1.31.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali inafanya mashauriano na wanahisa wa kiwanda ili wawekeze kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kukiboresha na kuendesha kiwanda hicho. Serikali ina nia ya dhati kuhakikisha kuwa kiwanda hicho kinafanya kazi kwa ufanisi na tija ili kuendeleza zao la kahawa ambalo linalimwa kwa wingi katika Mkoa wa Kagera, nakushukuru.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaachia bei ya zao la kahawa kuamuliwa kwa nguvu ya soko?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, bei ya kahawa duniani hutegemea mwenendo wa bei katika masoko ya rejea ya kahawa duniani ambayo ni soko la bidhaa la New York (ICE) kwa kahawa za arabika na euronest LIFFE ya London kwa kahawa aina ya robusta. Mabadiliko ya mwenendo wa bei katika masoko hayo huchochewa na kiasi cha kahawa kilichozalishwa duniani na mahitaji kwa wakati husika.
Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya mwenendo wa bei ya kahawa katika masoko rejea yana athari za moja kwa moja kwenye bei za kahawa katika masoko ya kahawa hapa nchini na duniani kwa ujumla. Hivyo, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi yanayoleta ushindani wa kutosha ili kuchochea bei ya kahawa nchini.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza:-
Je, ni maprofesa wangapi wanaozalishwa kila mwaka na ni wangapi wanastaafu kwa kipindi hicho?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Profesa ni ngazi ya kitaaluma ambapo Mhadhiri au Mtumishi wa Taasisi za Elimu ya Juu hufikia baada ya matokeo ya kazi za kitaaluma ikiwemo kufanya machapisho na ufundishaji. Hivyo, kupanda cheo cha mwanataaluma kunatokana na jitihada za mhusika katika ufundishaji, kufanya tafiti na kuchapisha maandiko yake katika majarida yanayotambulika Kitaifa na Kimataifa. Hivyo, kuongezeka kwa idadi yao kunategemea zaidi jitihadi za mtu binafsi katika utekelezaji wa majukumu yake na kukubalika kwa jitihada hizo kwa wanataaluma wenziwe kwa kuzingatia miongozo waliyojiwekea. Hadi kufikia Mwaka 2022 tulikuwa na jumla ya Maprofesa 226 kati yao 163 wakiwa ni Maprofesa Washiriki (Associate Professors) na 63 ni Maprofesa Kamili (Full Professors).
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kustaafu linahusu zaidi Vyuo Vikuu vya Umma ambao umri wa kustaafu ni miaka 65. Kwa takwimu za mwaka 2022 idadi ya maprofesa kamili waliostaafu ni wanne na wanaotarajia kustaafu kwa mwaka 2023 ni watano, kwa mwaka 2024 ni Wawili, na mwaka 2025 ni sita. Maprofesa Washiriki waliostaafu kwa mwaka 2022 ni mmoja na wanaotarajiwa kustaafu kwa mwaka 2023 ni 18, mwaka 2024 ni wanne, na mwaka 2025 ni sita. Ninakushukuru.
MHE. FLORENT L. KYOMBO K.n.y. MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -
Je, kwa nini Serikali isiruhusu wafanyabiashara wazawa wa kusindika kahawa Mkoa wa Kagera kununua kutoka kwa wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka utaratibu wa uuzaji na ununuzi wa kahawa za wakulima kupitia vyama ya ushirika ili kuondoa uuzaji wa kahawa katika mifumo isiyo rasmi na kuimarisha biashara ya mazao nchini. Aidha, kupitia mfumo huo wafanyabiashara wazawa waliowekeza kwenye viwanda vya kuongeza thamani na kusindika kahawa Mkoani Kagera wanaruhusiwa kununua kahawa kwenye minada ghafi inayoendeshwa na Bodi ya Kahawa. Kupitia utaratibu huo wanunuzi wazawa wanapata nafasi ya kushindana kununua kahawa moja kwa moja kwa wakulima kama ilivyowasilishwa na vyama vyao vya msingi (AMCOS).
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuinusuru Benki ya Wakulima Mkoa wa Kagera ambayo ipo chini ya uangalizi wa BOT?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 4 Januari, 2018 Benki Kuu ya Tanzania iliifutia leseni ya kufanya biashara Benki ya Wakulima Mkoa wa Kagera baada ya kushindwa kutimiza masharti ya leseni. Sambamba na uamuzi wa kuifutia leseni, Benki Kuu iliamua kuiweka benki hii chini ya ufilisi na iliiteua Bodi ya Bima ya Amana (Deposit Insurance Board - DIB) kuwa mfilisi wa benki hiyo. Kwa muktadha huo, iliyokuwa Benki ya Kagera Farmers’ Cooperative Bank Limited haipo chini ya uangalizi wa Benki Kuu ila ipo chini ya ufilisi wa DIB baada ya kufutiwa leseni ya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha, 2006, benki ikishafutiwa leseni na kuwekwa chini ya ufilisi hakuna tena uwezekano wa benki kuendelea kuwepo na hivyo Serikali haina mpango wa kuifufua benki hiyo ila inafanya ufuatiliaji ili kuhakikisha kuwa zoezi la ufilisi linakamilika. Hadi Machi 2023, Bodi ya Bima ya Amana ilikuwa imelipa fidia ya bima ya amana jumla ya shilingi milioni 846.11 kwa wateja 1,389 waliokuwa na amana kwenye Benki ya Wakulima ya Kagera kati ya jumla ya shilingi milioni 899.56 zilizopaswa kulipwa kwa wateja 2,797 kulingana na matakwa ya sheria, ahsante.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano katika Kata za Karambi, Mubunda, Ngenge na Rutoro katika Wilaya ya Muleba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) K.n.y. WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Disemba, 2021 Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ilifanya tathmini ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu katika Kata za Karambi, Mubunda, Ngenge na Rutoro.
Mheshimiwa Spika, Kufuatia tathmini hiyo, kata tajwa zilibainika kuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu na hivyo zimejumuishwa katika zabuni inayotarajiwa kutangazwa kabla ya mwaka wa fedha 2021/2022 kukamilika, ahsante.
MHE. DKT.OSCAR I. KIKOYO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Muleba?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Dkt. Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kujenga Vyuo vya VETA katika Mikoa na Wilaya mbalimbali kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Muleba na maeneo mengine, wananchi wa Muleba wanashauriwa kuendelea kutumia Kituo cha Ufundi Stadi katika Wilaya ya Muleba kinachoitwa Ndolage VTC pamoja na vyuo vya VETA na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilivyopo kwa ajili ya kupata elimu na mafunzo ya ufundi.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Muleba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Muleba imetengewa shilingi 1,825,662,000 katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali hiyo. Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya hospitali hiyo mpaka itakapokamilika.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -
Je, lini Serikali itatenganisha dhana ya ushindani na dhana ya kuwalinda watumiaji wa bidhaa na huduma nchini?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kimsingi dhana ya ushindani na kumlinda mlaji zina uhusiano mkubwa kwa sababu ushindani wenye afya katika soko ni mojawapo ya njia bora ya kumlinda mlaji. Kupitia ushindani, mteja hunufaika kwa kupata unafuu wa bei, kuongezeka kwa wigo wa upana, bidhaa bora na chaguo sahihi kwa mlaji, kukuza ubunifu wa uzalishaji wa bidhaa na kudhibiti ukiritimba katika soko.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kusimamia ushindani wa haki na kuwalinda watumiaji wa bidhaa na huduma hapa nchini kwa kutumia Sheria ya Ushindani Na. 8 ya Mwaka 2003 ambayo inatarajiwa kufanyiwa marekebisho katika Mkutano huu wa Bunge kwa lengo la kuongeza tija kwa watumiaji kwa kumlinda mlaji, ahsante sana.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga jengo la Kisasa la Mahakama ya Wilaya ya Muleba?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kujenga majengo mapya na kukarabati yaliyochakaa. Kutokana na uhaba uliopo wa majengo ya Mahakama, majengo hayo yanajengwa na kukarabatiwa kwa awamu kwa kuzingatia mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama kadri fedha zinavyopatikana.
Mheshimiwa Spika, jengo la kisasa la Mahakama ya Wilaya ya Muleba limepangwa kujengwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, ahsante.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -
Je, lini Serikali itawasilisha Bungeni Muswada wa kutunga Sheria ya kuwalinda watumiaji huduma na bidhaa nchini?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Sheria ya kuwalinda watumiaji wa bidhaa na huduma ipo, ambayo ni Sheria ya Ushindani Na. 8 ya Mwaka 2003. Utekelezaji wake unasimamiwa na Tume ya Ushindani (FCC). Kimsingi, sheria hiyo inabeba masuala makuu mawili, ambayo ni ushindani na kumlinda mtumiaji wa huduma na bidhaa katika soko la Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika, pamoja na uwepo wa sheria hiyo, vilevile kuna sheria nyingine za kisekta ambazo zinasaidia kuwalinda watumiaji katika sekta husika. Aidha, Serikali inaendelea na mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Ushindani Na. 8 ya Mwaka 2003 ili iweze kuendana na wakati wa sasa, nakushukuru.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya Kata sita za Wilaya ya Muleba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda kwenye Kata Sita za Muleba, Magata, Kurutanga, Gwanseli, Bureza, Kikuku na Kagoma, Wilayani Muleba Mkoani Kagera. Kwa sasa, Serikali inaendelea na utafutaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika mpango wa muda mfupi wa kuboresha huduma ya maji safi na salama katika kata hizo, Serikali imekamilisha utekelezaji wa Miradi ya Maji minne ya Ilemela, Karutanga, Butembo na Kagoma inayohudumia wananchi 22,279 waishio katika Vijiji nane vya Ilemela, Gwanseli, Bureza, Butembo, Makarwa, Kikuku, Kagoma na sehemu ya Kijiji cha Nsisha. Aidha, upanuzi wa Skimu za Maji za Karutanga na Butembo kwenda Kijiji cha Magata na Kitongoji cha Umdangara Muleba Mjini unaendelea ambapo unatarajia kukamilika mwezi Septemba, 2024 na kunufaisha wananchi 2,780.