Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo (41 total)

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Wizara, ninayo maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, wakati wananchi wa Muleba wakisubiria hizi hatua ambazo Wizara inazichukua, je, Serikali iko tayari kuiongezea nguvu Ofisi ya TANESCO iliyopo kwa sasa kwa kuiongezea wafanyakazi na vitendea kazi ili wakati tunaendelea kusubiria iendelee kutoa huduma stahiki kwa wananchi wa Wilaya ya Muleba? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wilaya ya Muleba inavyo visiwa 39 na kati ya hivyo, visiwa 25 vinakaliwa na wavuvi ambao wanachangia pato la taifa. Je, Wizara na Serikali ni lini itavipelekea umeme wa uhakika na wa bei nafuu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TANESCO imeendelea kutoa huduma kwa wananchi na kuhakikisha kwamba huduma ya umeme inapatikana kwa uhakika. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini kwamba tutaendelea kupeleka huduma ya umeme kwa wananchi na kuhakikisha kwamba ofisi ya TANESCO Muleba lakini na maeneo mengine yote nchini zinafanya kazi vizuri kabisa. Serikali tayari imeshaongeza nguvu kazi katika maeneo mbalimbali kwa kupeleka watumishi na vifaa mbalimbali ikiwemo vitendea kazi na magari. Tunaahidi kwamba tutaendelea kuboresha utendaji katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, kama nilivyokuwa nimetangulia kusema kwamba miradi inayopeleka umeme visiwani ni miradi inayoitwa off grid, maeneo ambapo Gridi ya Taifa haijafika na Muleba ni mojawapo ya maeneo ambayo ina visiwa vingi vinavyokaliwa na watu vinavyohitaji kupata huduma ya umeme. Tayari wako watu ambao walikuwa wanapeleka umeme huko ikiwemo kampuni ya JUMEME lakini gharama yake ilikuwa ni kubwa na Serikali ilitoa maelekezo kwamba gharama hiyo ya unit 1 kwa Sh.3,500 ishuke na kufikia shilingi
100. Maelekezo hayo tayari yameshaanza kutekelezwa. Kama bado kuna tatizo katika maeneo hayo basi tunaomba taarifa hiyo itolewa ofisini ili tuendelee kusimamia vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Serikali inao mpango wa kufikisha umeme wa TANESCO katika maeneo hayo kwa kadri bajeti itakavyoruhusu au kuweza kusimamia ile miradi ili iweze kutoa umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu kwa wananchi wote wanaoishi visiwani.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi wa maji wa Wilaya ya Muleba ambao unalenga kusaidia kata sita ambao umefanyiwa usanifu tangu mwaka 2018. Je, Wizara itaujenga lini na utakamilika lini kwa ajili ya kuwahudumia wakazi wa Wilaya ya Muleba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daktari, Mbunge kutoka Muleba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ambao usanifu wake umekamilika nao tayari Wizara tunaendelea na michakato kuona kwamba mradi huu tunakuja kuutekeleza ndani ya wakati.

Waheshimiwa Wabunge pale tunaposema kwamba, maji ni uhai, Wizara tunasimamia kuhakikisha kuona kwamba, wananchi wote wanaenda kupata maji safi na salama ya kutosheleza kwa lengo la kulinda uhai wa wananchi. Hivyo, Mheshimiwa Daktari nikuhakikishie kwamba, namna usanifu umekwenda vizuri na utekelezaji wake nao unakuja vizuri namna hiyo.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa lengo la Serikali ni kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 561,383 ya mwaka 2020 hadi kufikia hekta 1,200,000. Je, Serikali haioni busara kuhakikisha kwamba hii miradi ambayo imeshaanza badala ya kukimbilia kuanzisha miradi mipya tuhakikishe inakamilishwa ili wananchi waweze kuzalisha kwa wingi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mkoa wa Kagera kwa historia yake na jiografia yake ni Mkoa pekee ambao unapakana na nchi nne na nchi hizo nne zina uhaba mkubwa wa ardhi na hivyo uhaba mkubwa wa chakula. Je, Serikali haioni busara kuendeleza hili bonde kuhakikisha kwamba Mkoa wa Kagera sasa unakuwa soko la chakula kwa hizi nchi ambazo zinapakana na Mkoa huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Kikoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kama Wizara priority yetu ya kwanza sasa hivi tunachokifanya na Waheshimiwa Wabunge tutakapokuja kwenye bajeti wataona, ni kufanya tathmini na kukamilisha miradi ya umwagiliaji na tathmini tunazofanya ni za aina mbili; moja kuangalia efficiency ya miradi ya umwagiliaji iliyopo sasa hivi kama inafanya kazi kwa kiwango ambacho kinatarajiwa na kufanya marekebisho pale ambapo tunahitaji kufanya marekebisho. Pia kukamilisha miradi ya umwagiliaji ambayo tumeshaianza. Hatutakuja na mradi mpya wa umwagiliaji isipokuwa kukamilisha miradi tuliyoianza.

Mheshimiwa Naibu Spika, priority ya tatu ni kuwekeza umwagiliaji katika uzalishaji wa mbegu, Serikali ina mashamba 13 ambayo hayana mifumo ya umwagiliaji, mashamba haya 13 ndiyo tutakayoyapa kipaumbele katika bajeti ya mwaka kesho kuwekeza fedha ili yaweze kufanya kazi yote at optimal level ili kuweza kuzalisha mbegu bora na kwa wakati na kuondokana na tatizo la wakulima kutokupata mbegu za uhakika na kuyaacha mashamba idle ambayo hayatumiki. Kwa hiyo hivi ndiyo vipaumbele. Niseme tu ndani ya Bunge kwmaba kipaumbele chetu ni kukamilisha hiyo miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Mto Ngono na umuhimu wa Mkoa wa Kagera, kwetu sisi kama Wizara ya Kilimo na Serikali Mkoa wa Kagera ni moja kati ya mikoa ambayo tunaipa kipaumbele sana na ndiyo tutakapoelekeza nguvu zetu katika kipindi cha miaka mitano. Sababu ya kufanya hivi, mkoa huu strategically umeungana na nchi kama alivyozitaja nne, lakini vile vile ni lango kubwa la kuuza mazao katika nchi ya South Sudan. Kwa hiyo Mto Ngono tutaupa priority kama tulivyosema katika jibu letu la msingi kwamba tunatafuta fedha na tutawekeza katika hizo hekta 11,700 ili waweze kuzalisha mwaka mzima. (Makofi)
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Pamoja na nia njema ya Serikali yetu kutoa tiba bure kwa wazee wetu, lakini zoezi zima limegubikwa na ukiritimba wa kutoa tiba kwa wazee wetu.

Je, Serikali haioni busara kuoanisha vitambulisho hivi vinavyotolewa kwa wazee na Bima ya Afya ili wazee wetu wapate tiba stahiki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme, Serikali imeendelea kuhakikisha inapunguza changamoto ambazo Mheshimiwa anaziita ukiritimba wa Matibabu kwa Wazee Bila Malipo na ndiyo maana tumeainisha utaratibu wa kuainisha, kuwatambua wazee wetu na kuwapa vitambulisho. Hiyo ni sehemu ya jitihada ya Serikali kuhakikisha ule ukiritimba unapungua na kuwawezesha wazee wetu kupata matibabu bila malipo na bila changamoto yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupokea wazo lake la kuunganisha vitambulisho pamoja na sehemu ya matibabu kwa wazee ili Serikali iweze kulifanyia tathmini na kuona uwezekano wa kufanya hivyo au uwezekano wa kuendelea kuboresha utaratibu uliopo ili tuweze kuboresha huduma.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nilitaka kuongeza kwenye swali la Dkt. Kikoyo kwenye suala la ku-link huduma za matibabu kwa wazee na Bima ya Afya. Jambo moja ambalo lilituchelewesha labda kuleta kwenye Bunge lako Muswada wa Bima ya Afya kwa wote ilikuwa ni kuweka utaratibu kama huo ambao ukishafanya Bima ya Afya ni compulsory, maana yake lazima Serikali ije na utaratibu wa kuona ni jinsi gani Bima za Afya zitapatikana kwa watu hao kama wazee, akina mama wajawazito pamoja na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, swali la Dkt. Kikoyo ni zuri. Pale ambapo Serikali italeta Muswaada wa Bima ya Afya, pia itaweka sasa utaratibu ambao utaondoa hizi changamoto za matibabu bure kwa wazee.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Dkt. Kikoyo kwamba tukimaliza, nadhani tutakuwa tumepata mwarobaini wa tatizo hili. (Makofi)
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Lakini ninalo swali moja tu la nyongeza. Kutokana na uhaba mkubwa wa maji katika Wilaya ya Muleba na jiografia ya Wilaya ya Muleba inapakana na Ziwa Victoria. Serikali inao mpango wowote wa kutumia Ziwa Victoria kuvuta maji kwa ajili ya Wilaya ya Muleba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mhehsmiwa Naibu Spika, Mradi wa Ziwa Victoria ni mradi wa kimkakati na ni mradi ambao tunautarajia uhudumie maeneo mengi sana kwasababu ni mradi unaopita katika majimbo mengi na mikoa mbalimbali. Hivyo niweze kumwambia Mhehimiwa Mbunge kwamba maeneo yake ambayo bomba hili kubwa litakuwa likipita basi na yeye atanufaika katika vijiji vile ambavyo viko kilometa 12 kutoka kwenye bomba kwa pande zote kulia na kushoto.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipatia nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Muleba iko pembezoni mwa Ziwa Victoria, lakini inalo tatizo kubwa la uhaba wa maji na tunao mradi mkubwa ambao usanifu na upembuzi yakinifu umekamilika.

Je, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwa ajili ya kata sita za Wilaya ya Muleba; Kata ya Gwanseri, Kata ya Muleba Mjini, Kata ya Magata Karutanga, Kikuku, Kagoma na Buleza?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Muleba kwa namna bora na nzuri ambayo kwa kufuatilia wananchi wake waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa ambalo sisi kama Wizara na Bunge lako tukufu, sisi kama Wizara ya Maji tumesema hatuna sababu tena ya Watanzania kulalamika suala la maji. Mwenyezi Mungu ametupa rasilimali toshelevu, tuna rasilimali ya maji mita za ujazo zaidi ya bilioni 126. Tuna mita za ujazo bilioni 105 juu ya ardhi ikiwemo mito pamoja na mabonde na bilioni 21 ambayo iliyokuwa chini ya ardhi.

Kwa hiyo, mkakati ambao tumeuweka sisi kama Wizara na katika bajeti yetu kutumia maziwa, rasilimali toshelevu, kuhakikisha kwamba tunatatua tatizo la maji na moja ya maeneo ambayo ya kipaumbele ni vijiji ambavyo vipo kandokando ya mito ama maziwa. Nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi ni Wizara ya Maji si Wizara ya ukame. Tunakwenda kutatua tatizo la maji kwa wananchi wako, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Mkoa wa Kagera kwa muda mrefu kumekuwa na uwanja wetu wa ndege wa kimataifa Omukajunguti.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua ni lini uwanja huu wa Omukajunguzi utajengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni kuboresha uwanja wa ndege wa Bukoba, uwanja wa kimataifa na kwenye bajeti ya mwaka ambayo imepitishwa mwezi uliopita tarehe 27 na tarehe 28. Uwanja ule tunatarajia kujenga jengo la abiria maarufu kama VIP, lakini pia na kuongeza runway ili ndege nyingi kubwa ziweze kutoa katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka huu wa fedha Mheshimiwa Mbunge watu wa Bukoba na maeneo ya jirani muwe na Amani tunajenga uwanja ule jengo la abiria maarufu lakini pia na run way utapata usafiri.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Tume ya Ushindani, kama zilivyo mamlaka zote za udhibiti hapa nchini, zina mamlaka ya kimahakama quasi- judicial organs. Je, Serikali haioni kuunganisha ushindani na kumlinda mtumiaji zinafifisha dhana nzima ya ushindani na inafifisha dhana nzima ya kumlinda mtumiaji wa Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Dhana ya mtumiaji hapa nchini inaakisiwa kwenye sheria mbalimbali ambazo hazina dhana nzima ya kumlinsda mtumiaji na kuakisi haki nane za mtumiaji kama zilizvyoainishwa na Umoja wa Mataifa. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kutunga sheria, a standalone law ya kumlinda mtumiaji wa Kitanzania?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli FCC au Tume ya Ushindani inasimama kama tume ambayo inahusika kama ya kimahakama, kwa maana ya quasi-judicial organ na ndiyo maana katika majukumu yake yale mawili ya kulinda ushindani pamoja na ya kumlinda mlaji tumeamua sasa ile National Consumer Advocacy Council ambayo ilikuwa ni sehemu, kama section katika taasisi hii ikae sasa independent ili sasa tuwe na uhakika kwamba, mlaji anasimamiwa ipasavyo badala ya kuwa chini ya Tume hii ya Ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, miongoni mwa majukumu ambayo tunaenda kufanya, sasa tunataka tuanze kutunga sera ya kumlinda mlaji; na ndani ya sera hiyo sasa tutatengeneza pia sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, kama nilivyosema, pia ili kumlinda mlaji maana yake sasa tunataka tuwe na sheria ambayo yenyewe moja kwa moja itahakikisha inasimamia kumlinda mlaji tu ikiwa nje ya FCC ambayo inafanya majukumu mawili ya kusimamia ushindani, lakini pia na kumlinda mlaji.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, matatizo ya zao la kahawa ya Mkoa wa Kilimanjaro yanafanana sana na matatizo ya kahawa ya Mkoa wa Kagera. Mavuno ya kahawa katika Mkoa wa Kagera huanza mwezi Aprili hadi Mei, lakini mpaka juzi Vyama vya Msingi vilikuwa havijafungua msimu wa kahawa.

Mheshimiwa Spika, na tatizo kubwa lililopo hasa Wilaya ya Muleba, wananchi wanabugudhiwa na task force ambayo imeundwa ambayo inajumuisha watu wa PCCB, Usalama wa Taifa na watu wa Kilimo. Kila anayekutana naye anatoka shambani ana gunia moja anakamatwa na kupelekwa kituo cha polisi.

Naomba kauli ya Serikali, je, ni nini kauli ya Serikali kukomesha vitendo viovu hivi ambavyo vinawabugudhi wakulima kwa kisingizo kwamba wanalangua kahawa ilhali wako kwenye Wilaya yao, wako kwenye tarafa yao na vijiji vyao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Muleba Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza, niseme na nirudie tena, tumefanya vikao na viongozi wa Mkoa wa Kagera, tumefanya vikao na vyama vikuu vya ushirika vya Kagera, tumefanya vikao na wanunuzi binafsi; la kwanza, hatumzuii mkulima yeyote kupitia chama chake cha msingi kuuza mazao yake kwa mfanyabiashara katika level ya chama cha msingi. Hili ni jambo la kwanza, na tumeruhusu na tumetoa leseni. Na msimu umeshafunguliwa. Na wiki iliyopita tulikuwa na mkutano hapa Dodoma wa wadau wote wa kahawa.

Mheshimiwa Spika, la pili, tuwaombe viongozi katika ngazi za Halmashauri na Wilaya. Sekta ya kilimo haiwezi kusimamiwa kimabavu, sekta ya kilimo inasimamiwa kwa misingi ya win-win. Mkulima anayevuna mazao yake kutoka shambani kuyapeleka kwenye nyumba yake ama kuyapeleka kwenye chama chake cha msingi, naomba kupitia Bunge lako niwaombe viongozi walioko katika Halmashauri na Wilaya wasiwabughudhi.

Mheshimiwa Spika, lakini haturuhusu vilevile wafanyabiashara wanaowafuata wakulima mashambani kwenda kununua mazao chini ya bei ya soko, halafu wao kupeleka kwenye minada na Chama cha Msingi ili waweze ku-benefit na bei. Hilo hatutaruhusu na wala hatutaruhusu mfanyabiashara yeyote anayechepusha mazao kuvusha kwenye mpaka wa Tanzania na Uganda.

Mheshimiwa Spika, tunawataka na nitumie Bunge lako kuwaomba Waheshimiwa Wabunge, kama mna wanunuzi kutoka Uganda ambao wana uwezo wa kutupa bei nzuri, waleteni Wizarani tutawapa leseni, watakwenda kununua katika mfumo rasmi bila kubugudhiwa na mtu yeyote.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii. Matatizo ya Ludewa yanafanana sana na matatizo ya Wilaya ya Muleba. Wilaya ya Muleba ni kubwa yenye watoto wengi wanaohitimu darasa la saba, form four na kidato cha sita.

Je, ni lini Serikali itatujengea Chuo cha VETA katika Wilaya ya Muleba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba sasa kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kikoyo, Mbunge wa Muleba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwa upande wa Kilolo, Serikali inaendelea kutafuta fedha baada ya ukamilishaji wa vyuo hivi 29 katika wilaya 29 ambayo tumeanza kwa awamu ya kwanza kuweza kuzifikia wilaya nyingine ikiwemo na Wilaya ya Muleba. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Kikoyo katika muda mfupi ujao baada ya Serikali kupata fedha tutahakikisha kwamba kila wilaya tunaifikia ikiwemo na wilaya ya Muleba. Ahsante sana.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Kwa kuwa, idadi ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita inaongezeka mwaka hadi mwaka; na kwa kuwa, bajeti yetu na uwezo wetu wa kuwagharimia kupata mikopo sio mkubwa sana. Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka kuanza maongezi na mazungumzo na benki za kibiashara, ili Serikali iwadhamini vijana wetu ambao wanakosa mikopo, ili wapate mikopo kupitia benki za biashara kwa riba nafuu ambayo Serikali itaweza kuwadhamini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kikoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile ametuletea pendekezo, ametuletea wazo. Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge naomba nilihakikishie Bunge lako tunaomba tulibebe pendekezo hili la Mheshimiwa Dkt. Kikoyo twende tukakae chini, tulifanyie kazi, tufanye tathmini ya kina na pindi tutakapoona kwamba, jambo hili linafaa, basi tutakuja kulieleza kwenye Bunge lako Tukufu ni namna gani ya kuliendea jambo hili. Ahsante sana.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipatia fursa ya kuuliza maswali mawili madogo nyongeza.

Mheshimiwa Spika, hizi Skimu za Buhangaza, Kyota na Kyamyorwa ni za muda mrefu, zilijengwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania lakini hazijakamilika kwa maana hiyo tumezamisha fedha za walipa kodi lakini hakuna tunachokipata.

Je, hizi skimu nataka kupata commitment ya Serikali ni lini zitakamilishwa ili ziweze kutumika kama ilivyokusudiwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Kagera tumebarikiwa kuwa na bonde Mto Ngono, ni bonde kubwa linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji maji. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanza kulitumia hilo Bonde la Mto Ngono kwa kilimo cha umwagiliaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika majibu yangu ya msingi nimeeleza mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwanza tumefanya tathmini ya kina ya skimu hizi kufahamu gharama halisi na baadaye utekelezaji wake utaanzia mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili la kuhusiana na Bonde la Mto Ngono, niliwahi kutoa maelezo hapa naomba niyarudie; ukiangalia katika jedwali la saba katika kitabu cha bajeti cha Wizara ya Kilimo tumeainisha mabonde 22 ambayo Serikali itakwenda kuyapitia kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina likiwemo Bonde la Mto Ngono.

Mheshimiwa Spika, nataka niwaondoe hofu Waheshimiwa Wabunge wanaotoka Mkoa wa Kagera nafahamu hili ni eneo ambalo mmekuwa mkilipa kipaumbele kikubwa sana, tumeanza na upembuzi yakinifu tutajenga skimu katika Mto Ngono na umwagiliaji utafanyika na wananchi wa Kagera watanufaika na bonde hilo. (Makofi)
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipatia fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru kwa majibu ya Serikali yenye kutia moyo. Lakini tungependa kujua kutokana na wingi wa abiria katika Mkoa wa Kagera.

Je, ni lini shughuli ya kuwalipa fidia wakazi wa eneo lile kama mchakato wa kuanza ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa Omukajunguti itafanyika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutokana na wingi wa abiria unaokabili Uwanja wa Ndege wa Bukoba, je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha miruko zaidi ya mmoja ili kukabiliana na mahitaji ya usafiri wa anga kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba kuna timu iliundwa na mwezi uliopita ilienda kutembelea eneo la Uwanja wa Omukajunguti ili kujiridhisha kama una uvamizi kiasi gani, ikiwa ni maandalizi ya kuanza kulipa fidia. Kwa hiyo taarifa itakavyotoka taraibu zitaanza ili wananchi waweze kulipwa na maandalizi ya ujenzi wa uwanja huu uanze.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la pili linalohusu miruko, suala la ndege ni biashara pia ni huduma. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Shirika la Air Tanzania wamesikia na watafanya tathmini kuona kama kuna umuhimu wa kuongeza safari zingine.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, pamoja na nia nzuri ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na wingi wa abiria wanaotumia uwanja wa ndege wa Bukoba na kutokana na ufinyu na huduma hafifu za uwanja wa ndege wa Bukoba. Uwanja wa Bukoba mwaka 2020 tulipokea abiria zaidi ya 44,000 na mwaka 2021 tumepokea abiria 45,000.

Je, Serikali haioni kuna uharaka wa kujenga Uwanja wa Ndege wa Omukajunguti?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika majibu ya Serikali imesema wamefanya tathmini ya kulipa watu watakaopisha ujenzi wa uwanja huo.

Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa wakazi wa eneo lile wa Mkajunguti ili waweze kupisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Omukajunguti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na idadi kubwa ya abiria ambao ndio wanatumia uwanja wa Bukoba ndiyo maana Serikali imeamua kwamba kuna haja ya kujenga uwanja mkubwa zaidi kwa sababu uwanja wa Bukoba kwa mahali ulipo hauwezi kuendelezwa kwa maana ya kuipanua na ndio maana Serikali imetafuta eneo jipya ambalo uwanja mkubwa unaweza kujengwa ili kuruhusu ndege kubwa hasa tukizingatia umuhimu wa uwanja huo na abiria walivyo wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la fidia, Serikali ilishafanya tathmini ya awali ambayo kwa mujibu wa fidia hatuwezi kuitumia tulifanya tathimini ilikuwa inaenda kwenye bilioni tisa. Kwa hiyo, kuna utaratibu tunaufanya tuweze kurudia ile tathmini twende na hali ya sasa na mara tutakapokamilisha basi fidia italipwa kabla ya kuanza ujenzi wa uwanja huo wa ndege wa Omkajunguti. Ahsante.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali. Kutokana na Takwimu za Serikali yenyewe, hali ya Ziwa Victoria hususani upatikanaji wa mazao ya samaki ni mbaya sana. Kulingana na viwango ambavyo tumejiwekea katika Ziwa lolote samaki wazazi wanapaswa kuwa kati ya asilimia 3-5 lakini kwa Takwimu ambazo zimetolewa na Serikali hii katika Ziwa Victoria samaki wazazi wako chini ya asilimia 0.85. Swali la kwanza; sasa naomba Serikali inipe majibu upungufu huo hausiani na uvuvi haramu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Task Force zimekuwa zikiendelea Ziwa Victoria, hawa ambao wanatumwa kwenda kufanya hiyo kazi ni wasomi, lakini hawana weledi wowote na masuala ya uvuvi. Matokeo yake wamekuwa wakikamata hizo zana haramu wanawapiga faini zisizo na Kanuni wala Sheria wala sijui nini, baada ya kuwapiga faini wanawarudishia zile zana haramu ambazo zinasadikiwa kuwa ni zana haramu.

Je, Serikali haioni kwamba inaendekeza huo uvuvi wa haramu kwa kutumia pesa ya walipakodi wa Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, upungufu hauhusiani na uvuvi haramu? Kwa namna yeyote ile upungufu wa samaki wazazi unahusiana na uvuvi haramu na ndiyo maana tumeweka mkakati shirikishi kama Serikali kupitia Vyombo vyetu vyote na sasa tunakwenda katika kutekeleza mkakati ule ambao utakwenda kunusuru na kulinda moja; samaki wazazi lakini mbili rasilimali nzima na kwa hivyo itapelekea kupatikana kwa uendelevu wa rasilimali hii muhimu kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, amehusianisha juu ya vitendo vya baadhi ya maafisa wetu wasiokuwa waaminifu na waadilifu. Nakiri yawezekana wako maafisa wanaofanya vitendo vya kinyume na maelekezo na maagizo ya Serikali. Tuko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge, ikiwa anafahamu watumishi wanaofanya hivyo, Taratibu, Sheria na Kanuni za Kiutumishi zipo, nataka nimuahidi yeye kwamba tutachukua hatua madhubuti kwa yeyote ambaye anashiriki katika kuharibu operations na shughuli za Kiserikali zenye lengo jema kabisa la kulinda rasilimali za nchi hii, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, zaidi ya 85% ya wakazi wa Wilaya ya Muleba hawana maji safi na salama; je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya Wilaya ya Muleba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar, Mbunge wa Muleba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi ule wa mradi kutoka Ziwa Victoria upo kwenye mpango wa Wizara. Mara tutakapopata fedha tutaendelea kuzileta kwa mafungu ili mradi huu tuanze kuutekeleza.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza. Mazingira ya Kyerwa na Muleba yanafanana kutokana na mvua nyingi, milima na mabonde. Tuna barabara nyingi ambazo hazipitiki hasa kipindi cha mvua. Tulileta ombi letu kwa ajili ya barabara ya Kimea Burigi na Luhanga- Kiholele. Je, ni lini Serikali itatupatia pesa kwa ajili ya kutengeneza hizo barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oscar Kikoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba jimbo hili pia lina changamoto ya milima, mabonde na linahitaji kupata fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizi na ni kweli kwamba Mheshimiwa Mbunge alileta ombi maalum. Nimhakikishie kwamba maombi maalum yote yaliyoletwa yanafanyiwa tathmini na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA na tutahakikisha yanatafutiwa fedha ili yaweze kufanyiwa kazi. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba tutalipa kipaumbele pia eneo ambalo wameomba maombi maalum. Ahsante.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Wilaya ya Muleba iko kando kando mwa ya Ziwa Victoria, na tuna mradi wa kuvuta maji kwa ajili ya Kata sita za Wilaya ya Muleba; usanifu umekamilika.

Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza huo mradi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali Mheshimiwa Mbunge wa Muleba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mara usanifu wa mradi unapokamilika, tunatarajia tuwe na kipindi kifupi cha mwezi mmoja au miwili kuona sasa tunatumia maandiko ya Mhandisi Mshauri ili mradi uanze kutekelezeka. Hivyo, kwa
sababu usanifu umekamilika, tupo katika utaratibu wa kuona sasa tunapata mkandarasi aje kutekeleza huu mradi.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana; Mkoa wa Kagera unafahamika kwa uzalishaji wa zao la kahawa, na ni zao la kimkakati, na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imejikita kuboresha na kuongeza thamani ya zao la kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya wabia wa Kiwanda cha TANICA Serikali ni mbia na kuna hisa za zaidi bilioni 8.6 ambazo hazijalipiwa. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakisha kwamba hizo hisa ambazo hazijalipiwa za bilioni 8.6 zinalipiwa ?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, Serikali iliunda kamati maalum kwa ajili ya kuangalia namna ya kukikwamua kiwanda hiki muhimu sana cha kuzalisha kahawa katika Mkoa wa Kagera; hivyo tuko katika hatua za mwisho za kuona namna gani ya kupata fedha hizo pia kuona wanahisa wanaongeza hitaji ili, moja, kupata hizo fedha ambazo ni mtaji muhimu pili, kupata teknolojia ya kisasa ambayo itasaidia uzalishaji wenye tija wa kiwanda hicho; kwa sababu moja ya changamoto tuliyonayo ni uchakavu wa mitambo au mashine zilizofungwa tangia mwaka 1967.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Serikali inafanyia kazi na fedha zitakazopatikana tutaweza kuboresha kiwanda hiki pia kuhakikisha uzalishaji unakuwa na tija kwa ajili ya manufaa Taifa hili na Mkoa wa Kagera, nakushukuru.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru nina maswali mawili ya nyongeza. Ningependa kupata kauli ya Serikali, kule kwetu Muleba wakulima wanafukuzwa wanakamatwa wakisafirisha kahawa kutoka kata moja hadi kata nyingine na katika tarafa hadi tarafa nini kauli ya Serikali?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; nilitaka kujua kahawa ni mali ya nani? Ni mali ya Serikali au ni mali ya mkulima? Na ni lini ile hadhi inabadilika? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge Dkt. Kikoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kauli ya Serikali ni marufuku kwa wakulima wa kahawa walioko katika eneo moja kukamatwa na kuzuiwa kufanya biashara yao kwa sababu biashara hii inafanyika kwa mujibu wa Sheria Na. 23 ya mwaka 2001.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, zao la kahawa kama alivyouliza Mheshimiwa Mbunge, katika hali yake ya kawaida Serikali inafanya uratibu lakini mazao haya ni ya wakulima. Najua alikuwa anaelekea wapi, lakini lengo kubwa la Serikali ni kuhakikisha kwamba tunasimamia na kumfanya mkulima wa kahawa aweze kunufaika. Kwa hiyo kama Serikali tutaendelea kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira wezeshi ili mkulima wa kahawa aweze kunufaika.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali ni majibu mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia idadi ya Maprofesa nchini imeporomoka sana kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita. Chuo Kikuu pekee cha Dar es Salaam kinahitaji Maprofesa 161 lakini wapo Maprofesa tisa. Sasa kwa nini Serikali isibadili umri wa kustaafu kutoka miaka 65 mpaka miaka 70 ili kutunza hao wachache tulionao? (Makofi)

Swali la pili, kwa nini Serikali sasa kwa kuwa tunao uhitaji mkubwa wa Maprofesa isitoe package nzuri ili kuwavutia vijana wengi wakajitahidi kufanya research ili waweze kufikia hiyo hatua ya Uprofesa kwa ajili ya kutunza vyuo vyetu vikuu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Kikoyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kukabiliana na upungufu wa watumishi na taaluma katika vyuo vyetu vikuu vya umma nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kufanya mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, tunaendelea kuongeza nafasi za ajira kwa Wahadhiri pamoja na Wanataaluma katika vyuo vyetu. Jambo la pili, tunaendelea kuruhusu uhamisho wa watumishi wenye sifa kutoka taasisi nyingine za Serikali ili kuweza kuingia katika Vyuo Vikuu na kuhudumu kama Wahadhiri pamoja na kwenda kwenye nafasi za juu za Uprofesa. Jambo la tatu, tunaendelea kusomesha Wahadhiri ndani na nje ya nchi ikiwa na lengo pana la kuhakikisha tunaongeza idadi ya watumishi au wanataaluma hawa katika vyuo vikuu. naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itaendelea kufanya mambo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika mradi wetu wa HEET wa miaka mitano ambao tunaendeleanao. Serikali inaenda kusomesha Wanataaluma zaidi ya 600 ambapo tunaamini kabisa katika usomeshaji huu tutaweza kupata maprofesa wengi. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi juhudi hizi zinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo hili la kuongeza umri kwa wanataaluma hawa hasa Maprofesa, uliongezwa kutoka miaka 60 mpaka miaka 65. Mheshimiwa Mbunge hapa anashauri kwamba tuongeza tena iwe miaka 70. Tunachukua ushauri huu, tutakwenda kuufanyia kazi tuweze kuangalia namna bora ya kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili kuhusu kuongeza maslahi Serikali imekuwa ikifanya hivyo. Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea na jambo hili vizuri kabisa na imeendelea kuboresha maslahi ya watumishi wakiwemo na wenzetu wanataaluma katika vyuo vikuu na tutaendelea kufanya hivyo kwa kadri ya bajeti itakavyoruhusu, nakushukuru.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipatia fursa hii kuuliza swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi kubwa kujenga vyuo vya VETA sehemu mbalimbali. Je, Serikali ina mkakati gani kufungamanisha mitaala ya vyuo vya VETA na sehemu vilikojengwa? Kwa mfano Kagera tumepata Chuo cha VETA, tunaishukuru Serikali, kufungamanisha mtaala wa VETA na uchumi wa Mkoa wa Kagera kama kusindika kahawa, uvuvi na maeneo mengine kama madini? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba, Vyuo vya VETA vinawaandaa watu kwa ajili ya ajira na kuweza kumudu mazingira ambayo wapo. Na mkakati wa Serikali ni kwamba, pamoja na zile kozi mbalimbali za VETA ambazo kwa kweli zina-cut across kwa mfano kusoma wiring, electrical wiring au mechanics, n.k., lakini kila Chuo cha VETA kinashauriwa kufanya kazi na maeneo yale pale, ili kuchagua baadhi ya masomo ambayo yanakidhi matakwa ya eneo lile ambalo wanafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, najua kwa mfano, chuo ambacho kinajengwa pale Mkuranga kutakuwa na mazungumzo na wanaojenga viwanda katika eneo lile kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, mafunzo yanayofanyika pale yanaendana na mahitaji. Kwa hiyo, kadhalika hata cha Kagera na sehemu nyingine tutaendelea kufanya hivyo.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini Wizara ya Maji itaanza kujenga au kutekeleza Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya Wilaya ya Muleba?

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kikoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Ziwa Victoria kwa Muleba Mheshimiwa Mbunge alikuja tukaongea na menejimenti, tulishakubaliana mwaka ujao wa fedha tunakwenda kukamilisha usanifu na kuanza kuona uwezekano wa kufanya mradi huu.
MHE. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Wilaya ya Muleba ni Wilaya kongwe hapa nchini lakini haina hospitali ya Wilaya na mwaka jana Mheshimiwa Rais alitupatia fedha kuanza ujenzi wa hospitali hiyo.

Je ni lini sasa ujenzi utakamilika wa Hosoitali ya Wilaya ya Muleba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Hospitali hizi za Wilaya huwa unaenda kwa awamu na fedha hutolewa kwa awamu.

Awamu ya kwanza hutolewa milioni mia tano ama wakati mwingine bilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi huo; na katika kila mwaka wa fedha Serikali hutenga fedha kwa ajili ya kuendelea na kumalizia ujenzi wa Hospitali hizi za Wilaya. Nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge, tutakaa na wenzetu wa Wizara ya Fedha kuona katika mipango yao wameweka kiasi gani katika mwaka wa fedha unao fata ili ziweze kwenda Muleba kule kwa ajili ya ukamilishaiji wa Hospitali hii ya Wilaya.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Barabara ya Kagoma – Biharamulo katika Mji wa Muleba pale, walielekeza maji kwenye makazi yatu ambapo wamechimba mtaro mkubwa ambao unajulikana kama Buhimba, lakini Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano wakati wa Kampeni 2020 - 2025 alitoa maelekezo mahususi kwamba Mamlaka zinazohusika wakae tumalize hilo tatizo: -

Je ni lini Mamlaka ya TANROADS itakuja kumaliza tatizo la maji katika eneo la Buhimba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa sababu yalikuwa ni maelekezo mahususi na kuhusu eneo mahususi, naomba pia kutumia nafasi hii kumwelekeza Meneja wa Mkoa wa Kagera aende kwenye eneo lililokuwa limetolewa maelekezo na Mheshimiwa Rais, kutoa ama kuyatoa maji yaliyokuwa yameelekezwa kwenye makazi ya watu na kuyapitisha kwenye njia sahihi. Nimwombe atakapokuwa anafanya hivyo aweze kuwasiliana na Mheshimiwa Mbunge ambaye ametoa hoja hii, ahsante. (Makofi)

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri yenye kutia matumaini kwenye hizi kata ambazo kwa kweli zina changamoto kubwa ya mawasiliano.

Je, niombe kupata commitment ya Serikali ni lini sasa kama zimetiwa kwenye mpango, ujenzi wa minara hii utafanyika kwa ajili ya hizo kata tajwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) K.n.y. WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi minara hii itaanza kujengwa kwa mujibu wa sheria kwa kuwa tutatangaza kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha huu, kwa hiyo, tunaamini mchakato umeshaanza na mara mzabuni atakapoanza basi minara hii itaanza kujengwa kufuata na taratibu za manunuzi ahsante.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa Mikoa mikubwa sana hapa nchini na wenye wanafunzi wengi. Je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu katika Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza Mheshimiwa Dkt. Kikoyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wakati najibu swali la msingi nimezungumza mradi wetu wa HEET, kwamba pamoja na mambo mengine unakwenda vilevile kujenga vyuo katika Mikoa ya pembezoni na miongoni mwa Mikoa ambayo niliitaja ni pamoja na Mkoa wa Kagera. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nadhani Mkoa huu upo na upo kwenye program hii HEET tutakwenda kujenga chuo katika Mkoa huo wa Kagera pamoja na Mikoa mingine ya pembezoni. Nakushukuru sana.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Wilaya ya Muleba ni kati ya wilaya kubwa lakini haina gari la zimamoto. Ni lini Serikali itatupatia gari la zimamoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu ya msingi nimeeleza mpango wa Serikali kutumia zaidi ya dola za Kimarekani milioni 100 kununua magari ya kuzima moto na vifaa vingine kwa ajili ya uokoaji, na tutakapokuwa tumepata mkopo huo na kununua magari hayo, Wilaya ya Muleba anapotoka Mheshimiwa Kikoyo itazingatiwa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Muleba na hili swali nimeuliza mara nyingi sana hapa Bungeni. Tunapakana na Ziwa Victoria na Wilaya ya Muleba ina matatizo makubwa sana ya maji pamoja na kwamba tupo kando kando ya Ziwa Victoria. Tuna mradi ambao usanifu na upembuzi yakinifu umekamilika wa kuchota maji kutoka ziwa Victoria na kuyasambaza kwenye Kata sita za Gwanseli, Magata, Kabuganga, Muleba Mjini, Buleza, Kagoma na Kikuku. Je, ni lini utekelezaji wa huo mradi utaanza kwa ajili ya wananchi wa Wilaya ya Muleba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ishengoma Kikoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru kwa kukiri kwamba pamoja na changamoto hizo lakini kazi zinaendelea kufanyika ndani ya Jimbo lake na hizo kata zote alizozitaja tunaendelea kuzifanyia kazi. Mimi na Mheshimiwa Mbunge tulitembelea chanzo kile kingine pale Kizuri ambacho kinatoa maji mengi na tunakiboresha. Kutumia maji ya Ziwa Victoria tutayatupia kwenye maeneo haya yote ambayo yapo mbali na vyanzo vingine. Maeneo yale ambayo Mheshimiwa Mbunge tumeshaongea mara nyingi na nimefika pale, ambayo yanapata maji tutaendelea kutumia vyanzo vilivyopo. Kwa maeneo ambayo ni muhimu kutumia maji ya Ziwa Victoria, tunakwenda kufanya kazi nzuri na maeneo haya yote aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge tutahakikisha maji yanapatikana.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, Muleba ni moja ya miji yenye hadhi ya miji midogo tangu mwaka 2008. Ni lini itapata hadhi ya kuwa Halmashauri ya Mji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali ilishafanya tathmini kwenye Mamlaka za Miji Midogo kote nchini. Zipo mamlaka ambazo zinakidhi vigezo vya kupanda kuwa Halmashauri za Miji, lakini zipo mamlaka nyingi ambazo pia bado hazijakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi kuwa Hamashauri za Miji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kikoyo kwamba Halmashauri ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Muleba ni moja ya mamlaka ambazo zinafanyiwa tathmini ya vigezo na mara tutakapokuwa tumefanya tathmini na pale Serikali itakapokuwa ipo tayari kwa ajili ya kuanza kupandisha hadhi Mamlaka za Miji kuwa Halmashauri za Miji tutakwenda kufanya hivyo, ahsante.
MHE. DKT.OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na ninaishukuru Serikali kutupa Kituo cha Ndolage.

Wilaya ya Muleba ni miongoni mwa Wilaya kubwa hapa nchini yenye Majimbo mawili ya uchaguzi na ina shule nyingi za sekondari zaidi ya 67. Kila mwaka zaidi ya watoto 3,000 hawaendelei na Kidato cha Tano baada ya Kidato cha Nne. Ninaomba kupata commitment ya Serikali ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA chenye hadhi ya Wilaya kama zilivyo Wilaya nyingine? (Makofi)

Swali la pili, Serikali ina mkakati gani wa kutupatia Vyuo vya VETA ambavyo vinamilikiwa na Taasisi za Dini na watu binafsi kuvipatia ruzuku ya kujiendesha ili viendelee kuwasaidia na kuwaelimisha watoto wetu katika Wilaya zetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishaeleza kwenye majibu ya msingi kwamba Serikali inafanya ujenzi wa Vyuo hivi kwa awamu. Nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Muleba Kusini kwamba katika bajeti ya Serikali imetengwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyuo 36 vya VETA katika Wilaya mbalimbali nchini. Kwa vile tunakwenda kuweka vigezo vya namna gani tunaweza kwenda kugawa vyuo vile 36, ninampa tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba Wilaya hii ya Muleba ina Majimbo karibu matatu na idadi ya wananchi ni kubwa na hivyo ni miongoni mwa vigezo ambavyo tutaviweka kulingana na ule uhitaji. Kwa hiyo nikuondoe wasiwasi katika mwaka ujao wa fedha kati ya vyuo vile 36 na Muleba itakuwa ni miongoni mwa hizo.

Mheshimiwa Spika, katika eneo lake la pili kuhusu vyuo vya binafsi kuvipa uwezo au ruzuku ya kujiendesha, utaratibu huu haukuwepo lakini Mheshimiwa Mbunge kwa vile ametoa hapa mapendekezo, naomba tuchukue mapendekezo haya tuende tukayafanyie tathmini ili tuweze kuangalia namna gani Serikali inaweza cheap in kwa sababu wanaosoma humu ni watoto wa Kitanzania.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Jina langu ni Kikoyo siyo Chikoyo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kikoyo.

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali la nyongeza. Wilaya ya Muleba tumejenga zaidi ya shule 30 mpya, lakini walimu wamebaki wale wale. Serikali ina mpango gani mahususi kwa Wilaya ya Muleba kutupatia walimu wa ziada?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba kumekuwa na shule nyingi mpya ambazo zimejengwa ambazo zina uhitaji mkubwa wa walimu. Tayari Serikali imeanza mikakati mbalimbali ikiwemo kufanya msawazo wa walimu kutoka kwenye shule zile za zamani kuwahamishia kwenye shule hizi mpya. Pia Serikali inatumia njia ya kuajiri walimu ili kufidia upungufu katika maeneo ya shule hizi mpya na hata zile shule za zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali itaendelea na mikakati hii ili kuhakikisha shule zote zinazojengwa zinaweza kupata walimu ili wanafunzi waweze kupata elimu iliyo bora.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Jimbo la Muleba Kusini ina vijiji vitatu ambavyo havijapata umeme; Kijiji cha Kiholele, Burungura na Bihanga. Ni lini Serikali itapeleka umeme katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hivi vijiji vitatu kwenye Jimbo la Mheshimiwa Dkt. Kikoyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mkandarasi yupo site. Tutaendelea kumsimamia ili aongeze kasi kuhakikisha vijiji hivi vinawaka umeme.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, Kijiji cha Kisana tunajenga zahanati ambayo imetumia zaidi ya miaka 10 haijakamilika. Ni lini Serikali itatoa hela ya kumalizia hilo boma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka wa bajeti kwa ajili ya kuhakikisha inakamilisha miundombinu ambayo haijakamika kwenye vituo vyetu vya kutoa huduma ya afya msingi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali imetenga bajeti, pia itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha inaendelea kukamilisha miundombinu ambayo haijakamilika kwenye vituo vyetu vya kutoa huduma ya afya msingi ikiwemo katika zahanati hii katika Kijiji cha Kisana.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Zahanati ya Kihwera iliyopo katika Kata ya Kabilizi itapandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya, kwa sababu inahudumia watu wengi zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ili zahanati ipandishwe hadhi kuwa kituo cha afya kuna vigezo ambavyo vinazingatiwa, ikiwemo idadi ya wananchi wanaohudumiwa, ukubwa wa eneo, lakini pia uwepo wa miundombinu inayotosheleza kituo cha afya. Kwa hiyo, ninaomba nilichukue jambo hili ili Ofisi ya Rais, TAMISEMI iweze kufuatilia. Lakini nimwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Muleba kuleta taarifa rasmi kama eneo lile linakidhi vigezo na zahanati ile inakidhi vigezo vya kupandishwa kuwa kituo cha afya, ahsante.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali yenye kutia matumaini. Sitakuwa na swali la nyongeza ila naipongeza Serikali kwa kuliona hilo na niwaombe sasa wakajenge hiyo hospitali kwa ajili ya wananchi wa Wilaya ya Muleba. Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ametoa pongezi kwa Serikali kwa kuendeleza ujenzi wa miundombinu hii muhimu na sisi kama Serikali tunapokea pongezi hizo.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini hata hivyo soko letu limejaa bidhaa nyingi hafifu zisizofaa kwa watumiaji na nyingi zinatokana na udhaifu wa Sheria ya Ushindani tuliyonayo. Je, Serikali haioni ni muda muafaka sasa kuleta hapa Bungeni, tukatunga sheria mahsusi ya kumlinda mtumiaji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namba mbili, kuzagaa kwa bidhaa hafifu hasa vinywaji, sekta ya dawa na sekta ya ujenzi, huoni kwamba Sheria ya Ushindani tuliyonayo, aidha imeelemewa au ni ya zamani sana hivyo Serikali kutunga Sheria na kutenganisha hizi dhana mbili? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana kwa sababu suala la kulinda bidhaa au kumlinda mteja ni jambo la msingi, lakini hata hivyo, ombi lake la kwamba tuone namna gani ya kulinda sheria, bahati nzuri siyo muda mrefu katika Bunge hili tutakuja na sheria ambayo mwisho wa siku ni kwamba sheria hii itaona jinsi gani ya kushughulikia mambo hayo.

Mheshimiwa Spika, ni kweli wakati mwingine katika suala zima la bidhaa, ukienda bidhaa za ujenzi na mambo mengine, hata upande wa vyakula imekuwa ni changamoto kubwa. Ni imani yetu Waheshimiwa Wabunge katika mjadala wa sheria utakaokuja hivi karibuni katika Bunge hili, tutakuwa pamoja kuhakikisha kwamba tunatengeneza sheria mahsusi kabisa ambayo itasaidia kuwalinda Watanzania hasa katika kuhakikisha kwamba tunapata bidhaa zilizokuwa sahihi kwa ajili ya watumiaji, ahsante.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Utekelezaji wa Miradi ya REA katika Wilaya ya Muleba unasuasua. Serikali ina kauli gani kumuhimiza mkandarasi amalize ile kandarasi aliyopewa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na pia, nashukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Kikoyo. Nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kweli, ni mkakati wetu kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati. Namhakikishia nitafanya ziara katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge, ili kujionea na kuendelea kumsisitiza mkandarasi aweze kuongeza kasi hii ya kupeleka umeme kwenye vijiji ambavyo vimebakia, ili iweze kufanyika kwa haraka wananchi waweze kupata umeme. Ahsante. (Makofi)
MHE. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na commitment ya Serikali kwamba jengo la Muleba litawekwa kwenye bajeti ya mwaka 2025/2026. Wilaya ya Muleba ina majengo mengi ya Mahakama za Mwanzo ambayo yamechakaa. Je, Serikali ina mpango wowote wa kuyakarabati?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Kuna wadau walitupatia majengo kwa ajili kuyaendeleza kidogo na kuyafanyia ukarabati ili yatumike kama Mahakama za Mwanzo. Je, Serikali ililipokea hili jambo; na imepangia pesa kwa ajili ya kulikarabati ambalo liko Kata ya Ijumbi?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mahakama nyingi kama nilivyosema kwenye jibu la msingi hazina hali nzuri. Ni kwa msingi huo ndiyo maana Idara ya Mahakama imeweka Mpango wa Miaka Mitano wa Ujenzi na Ukarabati wa Majengo haya. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango huo unatekelezwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, pia kwa taarifa, kwa ujumla Mahakama za Mwanzo ambazo zimejengwa na kukarabatiwa ni 185, Mahakama za Wilaya ni 66, Mahakama za Ngazi ya Mkoa ni saba na Mahakama Jumuishi ni zaidi ya 12. Kwa hiyo, mpango huu unatekelezwa kila mwaka. Itakapofikiwa Wilaya ya Muleba, pia itanufaika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, ni kwamba majengo tuliyapata kutoka kwa mdau; namwomba tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutawasiliana na Idara ya Mahakama wafanye assessment ya utoshelevu au kufaa kwa hilo jengo kuwa Mahakama ili ikiridhiwa, basi ukarabati ufanyike ili liweze kutumika kama Mahakama kwenye Kata ya Ijumbi, aliyoitaja. Nakushukuru.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali lililotangulia lilikuwa linahusu masuala ya watumiaji na mikopo. Sasa ni lini Serikali kutokana na umuhimu wa watumiaji itatenganisha masuala ya ushindani na masuala ya watumiaji ili tuweze kuwalinda watumiaji wa Tanzania?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Tanzania tunazalisha bidhaa. Ili kuuza ile bidhaa, watumiaji inabidi wanunue. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhamasisha watumiaji wa Tanzania wanunue na kutumia bidhaa na huduma zilizozalishwa hapa nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba sheria hii tuliyoitaja inasimamia ushindani wa haki pamoja na kuwalinda walaji. Uzoefu unaonesha kwamba nchi nyingi duniani zinatumia sheria hii moja ambayo inachukua maeneo mawili kwa maana ya ushindani wa haki katika soko, lakini pia kupitia humo kumlinda mlaji, kwa sababu tunapitia sheria hii, pale ambapo tunaona kuna haja ya kutenganisha kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameshauri, basi Serikali haitasita kufanya hivyo na tunachukua ushauri wake, lakini pia na wadau wengine ambao watatoa maoni wakati tunaihuisha au tunarekebisha Sheria hii Na. 8 ya Mwaka 2003.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, ni kweli sisi kama Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, tayari tuna mikakati mbalimbali. Moja ya kaulimbiu yetu katika kuhakikisha tunakuza Sekta ya Viwanda na Uzalishaji nchini ni, “Nunua Tanzania, Jenga Tanzania,” kwa maana ya nunua bidhaa zilizozalishwa Tanzania ili uweze kuijenga nchi yako Tanzania.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kufanya hivyo, lakini kwa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zina ubora unaotakiwa ili ziweze kushindana na bidhaa zinazotoka nje, kwa sababu ili kuhakikisha Watanzania wanapenda bidhaa zao za ndani, lazima ziwe na ubora ule ambao unalingana na bidhaa nyingine kutoka nje ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaendelea kuhakikisha tunatangaza hilo, lakini kuhakikisha bidhaa zetu zinazalishwa katika ubora unaotakiwa, nakushukuru.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Mradi wa kutoa Maji Ziwa Victoria ulianza kama siyo mwaka 2009 mpaka leo haujaanza kutekelezwa na mwaka jana Serikali ilitenga shilingi milioni 850 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huu hatua kwa hatua. Je, ni kitu gani kimefanyika mpaka leo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba Muleba Magharibi ambayo ina tatizo kubwa la maji inapata maji na wananchi wake wanatokana na adha ya ukosefu wa maji? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Serikali inatambua ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge alichokiongelea kwamba mradi huu ulianza mwaka 2009 na kweli kabisa katika bajeti iliyopita shilingi milioni 850 ilitengwa. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kufuatilia kwa faida ya wananchi wake wa Muleba Kusini nampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Serikali inatenga fedha, lakini pia inaendana na upatikanaji wa fedha. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kuwa mradi huu, Serikali imejizatiti kwa sababu inatambua umuhimu mkubwa sana kwa ajili ya wananchi wa Muleba Kusini kupata maji ya kutoka Ziwa Victoria. Ni jambo ambalo Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiliongelea, kama Tabora wanapata maji ya Ziwa Victoria lakini wao wapo karibu pale na kweli Serikali imelitambua hilo na inaliangalia kwa kina vizuri kabisa na tunaendelea kutafuta fedha ili zikishapatikana tu mradi huu uanze mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna miradi mikubwa, miradi ya kati na miradi ya muda mfupi, tumeanza na maeneo mengine kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi, tumeanza na zile kata zingine ambazo tunaenda kutoa huduma kwa watu wapatao 2,780, lakini pia tunachukua maombi ya Mheshimiwa Mbunge kwa eneo la Muleba Magharibi ili kuhakikisha kwamba tunaliingiza katika utaratibu wa utekelezaji wa miradi yetu ya muda mfupi ili wananchi wa Muleba Magharibi na wao wapate huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.