Contributions by Hon. Amour Khamis Mbarouk (10 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, Bismillah Rahman Rahimu, nakushukuru sana kwa fursa hii na kwasababu leo ni siku ya kwanza kabisa kusimama katika Bunge lako hili na Mwenyezi Mungu amejaalia kwamba ni siku ya mwanzo katika siku za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, basi nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu Sub-hanallah wa taala kwa kutuwezesha sisi wote huku kuwa Wabunge na kuhudhuria kwenye nyumba hii. Pili Chama changu Chama Cha Mapinduzi CCM lakini hasa hasa viongozi wake Mahsusi Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli kwakuwa yeye alikiongoza Chama Cha Mapinduzi hadi leo nipo hapa kwenye Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Mama Samia kama msaidizi wake naamini walishauriana sana katika kupitisha majina yetu, kwa hiyo, nachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Mama Samia Mwenyezi Mungu ampe maisha marefu yenye manufaa ya duniani na akhera.
WABUNGE FULANI: Amin!
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nisiwasahau Katibu Mkuu na Katibu wa Itikadi na Uenezi hawa ndio walitumwa kabisa kabla ya kampeni za uchaguzi walitumwa na Hayati Dkt. Magufuli kuja kupeleka ujumbe na ku-test mitambo pale Pemba kwa hiyo, tuwashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niwashukuru Spika na Naibu Spika kwa namna mnavyotuongoza kiasi ambacho leo najisikia kusimama hapa na kusema chochote yote hii ni kwasababu ya uongozi wenu. Katika hotuba hii ya Waziri Mkuu ambayo ni ya bajeti ya Wizara yake, naomba nichangie mambo machache sana..
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie jambo la kwanza ni Kilimo, kwa fikra yangu ili kilimo kiendelee ndani ya Tanzania, lazima tuwekeze fedha nyingi sana, na ili fedha hizi zipatikane lazima benki waondoshe riba kwa wakulima. Kwa sababu mkulima anapolima kule shambani alafu ukaja ukamkata riba, na shambani mazao yake akiyaondoa au akiyapeleka sokoni lazima pia kodi atoe kwa hiyo, tunakuwa tunamkata juu na chini kiasi ambacho tunamfanya mkulima akate tamaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana hii riba kutoka kwenye Benki iondolewe, na hili pia Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli alilisema katika hotuba yake hii ni kuonesha kwamba riba kidogo inarudisha nyuma maendeleo. Katika kilimo hiki hiki kuna tafiti, watu wengi wamezungumzia kuhusu tafiti. Nilikuwa naomba kama kuna tafiti zozote basi zipelekwe kule vyuo vikuu wanafunzi waliopo pale watusaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halafu fedha ambazo zimepangwa kwenye Mawizara kwa ajili ya tafiti wapewe wanafunzi wetu wa vyuo vikuu kule ziwasaidie, sasa itakuwa sisi vyuo vikuu vinamanufaa gani kwetu ikiwa hadi sasa hatujaweza kusimamia tafiti zetu wenyewe kwa kupunguza gharama. Naomba sana hizi tafiti zipelekwe vyuo vikuu tunavyo vingi na fani tofauti kozi tofauti zinasomwa, naamini vijana wanaweza kufanya kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili katika hotuba ya Waziri Mkuu nilikuwa naombi sana na ombi hili ni kuhusiana na sina hakika nitakachosema nipo kwenye sheria au vinginevyo. Lakini sisi tuna mifuko ile ya Jimbo na ile mifuko kwa upande wetu kule Pemba au Zanzibar inapatikana kidogo sana, na hapa kuna ahadi ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ya kumsaidia Rais wa Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, inaonaje Serikali kwamba itaongezea katika kusaidia hili kumsaidia Rais wa Zanzibar kama hii mifuko itaongezwa kiwango pengine kutoka Milioni 20 zilizopo sasa hivi au pengine Milioni 50 kwa majimbo mengine bila kujali formula kwamba Jimbo lina watu wengi wapewe kiwango kikubwa basi sisi tuongezewe zile fedha angalau ifike Milioni 100 kwa Jimbo pale Zanzibar na iwe specially kwa Zanzibar. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, hizo hupati mzee.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine katika hili angalau bajeti tunazozizungumza hapa katika kumsaidia Rais wa Zanzibar pale angalau asilimia 10 kila Wizara ingekuwa inafikiriwa kupelekwa pale Zanzibar, Zanzibar leo ingekuwa Ulaya na watu wengi wangeipenda sana.
MBUNGE FULANI: Hamjashauriana kwa kweli!
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuchangia mambo haya naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, mimi nawaomba Waziri na Naibu Waziri wajitambue na watambue kwamba nafasi walizoaminiwa na Rais si nafasi za kazi bali ni nafasi za kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kimaendeleo katika jamii ya Watanzania, na ili mabadiliko hayo yaonekane na kila Mtanzania ni wajibu kufanya kazi zitakazobadilisha fikra za Watanzania hasa hasa wakulima; na ili fikra za Watanzania zibadilike, ni lazima Watanzania hao washirikishwe katika mambo yanayowahusu na wakati huo huo Mawaziri wanatakiwa washiriki katika shughuli za wakulima moja kwa moja katika maeneo wanayofanya kazi, waache kabisa maofisi.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, wangeamua kuanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa kwenda kwenye maeneo wakawaomba wananchi kuchimba mitaro wenyewe akiwepo Waziri au Naibu Waziri na wataalam wa ndani ya Wizara. Jambo hili lingejenga ujasiri na ufanisi wa uongozi, lingewajengea heshima Serikali, lingewasaidia wananchi ambao ni wakulima na lingepunguza matumizi makubwa ya fedha za Serikali.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iwe na takwimu mahsusi ya wakulima wa kila zao linalolimwa Tanzania, kisha wafanye tathmini ya malengo ya Serikali waliojiwekea. Je, malengo na idadi ya wakulima italingana? Baadaye wafanye marekebisho yanayohitajika.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iweke mitandao ya masoko kwa kuweka wafanyabiashara wakubwa watano hadi kumi watakaoishi nchi mbalimbali ambao watauza bidhaa za Tanzania za kilimo na hata za viwanda nje ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, soko lingine lipo ndani, Watanzania ni milioni 65, Serikali iwatumie Watanzania hawa kama soko, hivi inakuaje Zanzibar wawe wanatumia mchele wa mapembe kutoka India na nchi nyingine ambao ni rahisi na isitumie mchele kutoka Tanga. Serikali iondoe mifumo itakayosababisha mchele wa Mbeya na bidhaa nyingine na bei kubwa huko Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali izuie vijana kucheza betting na badala yake Serikali iwaandae kuwa wakulima, fedha ambazo vijana wanazitoa kuwapa Wachina ni nyingi mno na iwapo vijana hao wangezitumia fedha hizo kwenye kilimo Tanzania ingepaa angani kwa utajiri.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja nikiamini kuwa kilimo ni uti wa mgongo, kwa maana ndio axis ya maendeleo ya nchi yoyote. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na hii Wizara kwa kweli viongozi wake wamekwenda shule sana. Nawaombea Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala awaongoze, lakini pia awape mwelekeo mwema katika kutuongoza Jamhuri hii ya Muungano.
Mheshimiwa Spika, niishukuru Jamhuri hii ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa hata jimboni kwangu pale wamenisaidia sana. Kuna majengo mazuri sana ambayo yamefadhiliwa na UAE na haya tumeletewa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kweli, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni njema sana kwetu na tunaishukuru sana na tunashukuru viongozi wa Tanzania kwa kutufikiria jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naamini kwa kuwa wamekuwa na imani ya kutusaidia jambo hili, kuna mambo mengine mazuri wanaweza wakatusaidia kama vile barabara na hata ile bandari inayotegemewa kuwa bandari ya samaki kwa ajili ya zile meli nane zile zinazotegemewa kununuliwa kwa Tanzania, naamini itajengwa Tumbe kwa kwa sababu, pale itarahisisha sana biashara baina ya Tanzania na Kenya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nataka nichangie kuhusiana na mazingira. Jimbo la Tumbe na Jimbo la Konde yameathiriwa sana na bahari. Jimbo la Tumbe bahari imeshafika kwenye soko pale na lile soko limejengwa kwa gharama sana. Katika mchango wa lile soko ni Jamhuri ya Muungano ndio imechangia pale, lakini maji yakipanda juu lile soko linafikwa sasa hivi, kwa hiyo, wakati wowote ile bahari itachukua eneo kubwa la ardhi. Kwa hiyo, naomba sana Wizara hii ya Muungano ifikirie jambo hilo.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri juzi alipokuwa akijibu swali alisema kwamba, kuzuia mambo yale ni kwa gharama kubwa sana, lakini naamini kutuhamisha Pemba sio gharama kubwa sana. Kwa hiyo, atutafutie hata eneo lingine hapa Tanzania bara na ndio neema za Muungano hizo kwamba kile kisiwa kikizama sisi tuwe na mahali pa kukimbilia huku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika jambo hilohilo la mazingira, mimi sijui kule kwetu kuna tatizo gani la mazingira kwa sababu, mikorosho inakatwa ovyo na Wizara hii ipo, miembe inakatwa ovyo. Yaani miti inakatwa kimsingi na hakuna ule ufuatiliaji wowote.
Sasa mazingira haya tunayozungumza hapa, sina hakika kwamba yanahusika huko, lakini kama yanahusika, namwomba sana kabisa Waziri na Naibu wake na kwa sababu Naibu Waziri yupo Pemba pale, basi siku moja aje Jimbo la Tumbe tuangalie namna zao la mikorosho linavyoathiriwa na miembe inavyokatwa. Sasa hivi wakati wowote kutakuwa jangwa na kukiwa jangwa maana yake ni kusema kwamba, bahari itaongeza speed ya kupanda juu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wazazi wetu, wazee wetu, waasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume, walivyofanya jambo hili la Muungano maana yake walifanya kwa nia safi kabisa. Huwezi ukafanya umoja kama huna nia safi. Hawa walikuwa na nia safi kabisa na wakawashawishi Watanzania waliokuwepo wakati ule wote wakaridhia kwamba, wafanye Muungano huu.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa nina masikitiko kidogo kwamba, watu wametumia nguvu kubwa sana kuuchafua Muungano huu. Sasa naiomba sana Serikali ifikirie namna kwanza ya kutupa, kwa sababu Bunge hili ni jipya sana, kutupa semina angalau mtu asishindwe cha kujibu wakati akiulizwa. Pia naiomba Wizara hii inayohusika na mambo ya Muungano kwa sababu, nilisoma eneo katika kanuni zetu kwamba, ile Mifuko ya Jimbo ikishapelekwa Zanzibar watu wanatakiwa ku-report nini kimefanyika kutokana na hiyo Mifuko.
Mheshimiwa Spika, sasa Mifuko ile imetumika katika miaka 25 hii iliyopita, kuanzia mwaka 1995 mpaka juzi kwa kweli, hatujaona faida yake. Sasa Mheshimiwa Waziri akija hapa atatueleza labda angalau kwa lile Jimbo la Tumbe tu ambalo natoka niwaambie nini kwamba, Jamhuri ya Muungano hapa ilileta fedha shilingi milioni 20 kila mwaka na ilifanyiwa jambo gani. Fedha hizi hizi ndio zilizotumika kuwashawishi wananchi kule Pemba na Zanzibar kwamba, Jamhuri ya Muungano ndio adui wa Wazanzibari. Limefanyika sana jambo hilo mpaka sasa hivi sawa na kusema tu kwamba, yani wengi wa wananchi wanaamini kwamba…
MBUNGE FULANI: Taarifa.
SPIKA: Bahati mbaya muda umeisha.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana niwapongeza sana viongozi wa Wizara hii Mama Mheshimiwa Prof. Ndalichako na mwenzake na hii ni Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ambayo tunategemea sana kwamba mambo yake yangekwenda kwa Sayansi na Teknolojia na ninaamini wangeanza na walimu na kwasababu ni mwalimu naomba nianze na walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Elimu ni Wizara muhimu sana katika nchi yeyote ndio tuliitegemea ilete mabadiliko yote ndani ya nchi kwasababu wao ndio wana deal na elimu na elimu ndio maendeleo. Lakini ninasikitika sana na walimu kwamba wamewekwa nyuma sana kwa hiyo ninaiomba hii Wizara na Serikali kwa ujumla waangalie walimu kwa jicho la huruma sana kwasababu mwalimu anafanya kazi nyingi sana akiwepo shule ana lea mwalimu, anafundisha, anatoa kazi, anazisimamia yote haya ingekuwa ni mtu mwingine mkubwa mkubwa basi yote haya angepangiwa allowances kwamba labda akisahihisha kuna allowance akitoa homework kuna allowance akitoa home text ana allowance lakini akitoa termina test ana allowance akitoa examination ana allowance. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwasababu ni walimu bado halijafikiriwa jambo hili naomba sana walimu wafikiriwe sana kazi wanayoifanya ni ngumu mno. Nafikiria hata kuwaombea hawa kwamba wangekuwa na wao wanapewa afya, yaani huduma za Afya bure ingependeza sana, na ninaiomba sana Wizara ya Elimu iwatumie sana Walimu. Ninakumbuka mwaka 2009 kuna mwalimu ndio amegundua mchanga fulani pale uliokuwa unapelekwa Kenya kwamba ule ndio mchanga ambao una dhahabu, Mheshimiwa Dkt. Magufuli Hayati Mwenyezi Mungu amrehemu akhera alipo huko amekuja kuuzuia baadaye.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaamini sana kama tungewatumia walimu vizuri basi hata wanafunzi wa darasa la sita leo wangeweza kutusaidia sana katika tafiti mbalimbali hata ulinzi wa yale madini kwa mfano madini yanayoibiwa kule basi walimu wangeandaa wanafunzi hata wakienda kucheza mchezo fulani tu pale wakawa wamevaa nguo tofauti za wanafunzi basi wakagundua kuna madini yanaibiwa na nani anaiba, Watoto wangesema, lakini kwasababu bado walimu hatujawatumia vizuri naomba sana Wizara ya Elimu iangalie jambo hili..
Mheshimiwa Naibu Spika, ni juzi tu hapa wiki iliyopita amekuja mama mmoja alinieleza kwamba anatoka Arusha yule mama alilalamika sana kwamba wamezuiwa yale mahitaji yao yaani increment zao zimezuiwa sijui kupandishwa madaraja yamezuiwa kwa muda wa miaka sita. Anashukuru sasa kwamba wanakwenda kupandishwa madaraja ila wao wamestaafu wamestaafu mwaka jana mwezi Novemba sasa anahofu kwamba yale madaraja wao hayatawahusu na ile arrear yao ya haya madaraja wanayotaka kupandishwa sijui itakuwaje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini yote haya ni kwasababu tulimchukulia mwalimu ni mfanyakazi tu peke yake. Kwa hiyo, ilivyokuja kwamba wafanyakazi wote zimezuiwa increment na mwalimu tukamzuia, kumbe mwalimu ni zaidi ya mfanyakazi sisi wote humu tumekuja humu kwasababu walimu wametutengeneza leo tumekuwepo hapa kwasababu walimu wametengeneza future zetu lakini sisi tuliotengenezewa future hatuangali nani wametutengenezea future hizi. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ya Elimu iwaangalie sana walimu sio vibaya walimu sasa kununuliwa hadi vile viatu vya kuingia shule sio tatizo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba Waziri wa Elimu aangalie pia suala la masomo haya kila unapofungua kwenye mtandao mtu anapotaka kujiunga na chuo anaambiwa awe na mfano awe na credit nne lakini non- religious subject. Nilikuwa ninamuomba Waziri afikirie kwamba sisi pamoja na uhai wetu wote duniani hapa ipo siku tutaondoka duniani, na kwasababu tutaondoka duniani kila mtu anategemea kwamba kuwe na watu nyuma watakaosema mwanga wa bwana uwashiwe kule akhera sijui kuyasema vizuri haya maneno lakini sisi tunaomba dua ziombwe hawa watakaotuombe dua ni nani ikiwa leo mwanafunzi anaambiwa somo lako hili la dini halitazingatiwa katika udahili wa vyuo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hili somo la dini halitamsaidia kule anakokwenda kwamba atasoma chemistry lakini halitamwongezea halita mchupisha amepata A ya chemisty amepata A ya biology amepata A ya physics lakini ameshindwa kupata B nyingine amekuja kupata D ya Bible knowledge na Islamic knowledge si itamsaidia kuingia advance, atakwenda kusomea chemistry lakini hapa imemsaidia lakini in-directly kwamba huyu mtoto umemfanya asome dini kwa hiyo kesho atakuwa padri kesho kutwa atakuwa shekhe atakuwa mwalimu wa Madrasa kwasababu ya elimu ile ile. (Makofi)
Mheshimiwa Niabu Spika, kwa hiyo sasa hivi mwanafunzi hasomi tena dini kwasababu anaona Serikali haizingatii hiyo credit yake. Kwa hiyo ninamuomba sana Waziri ninaiomba sana Serikali ifikirie jambo hili ni jambo kubwa na kwasababu sisi Watanzania wote kila mtu ana dini yake ninamuomba sana aangalie sana juu ya kurudisha ile hadhi ya somo la dini katika udahili wa vyuo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba pia Waziri afikirie namna ya kujenga uzalendo wa watanzania kwa kupitia Wizara hii ya Elimu leo watu wengi tumesoma lakini matatizo yameongezeka ukiangalia huku mara mtu anakwambia sijui nini kimeibiwa sijui hichi kimeibiwa tatizo nini, tatizo ni kwamba kila mtu hapendelei kwamba nchi ipate nini, anapendelea yeye mwenyewe apate nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mtu atakuwa na madaraka miaka mitano, sita, kumi yeye akiwa na madaraka ndani ya siku tano ni tajiri… (Makofi)
NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa ahsante sana.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, Naunga mkono hoja ninashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nikupongeze kwa namna unavyotuongoza, lakini pia niwapongeza sana Waziri wa Wizara hii na Naibu wake kwa kazi nzuri sana wanayoifanya ndani ya nchi yetu na kwa kufuata Ilani ya Chama chetu Cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia habari ya wavuvi na wafugaji, mimi ni mvuvi niliwahi kuvua kwa miaka mingi sana. Kwa hiyo, najua kwamba wavuvi hawana elimu maalum, wavuvi wetu wengi sana wanavua kwa mirathi yani kwa elimu ya mirathi. Jinsi mtu alivyomkukuta baba yake anavua ndivyo hivyo anavyovua na yeye na sina hakika kwamba wizara hii imeweka siku kwamba itakutana na wavuvi ana kwa ana kuwasiliza changamoto zao kule waliko au wataandaa mafunzo juu ya uvuvi. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, ni kwamba hawa wavuvi wengi hawavui kwa sababu ni kazi anayoipenda kwa sababu uvuvi ni kazi hatari sana, ni sawasawa na mtu anapopanda mnazi yaani wakati wowote unaweza kusikia chochote na hasa kwa kuzingatia vyombo wanavyovitumia, kuelekea katika mazingira hayo ya uvuvi. Kwa hiyo, naiomba Serikali sana, badala ya kuchukua maamuzi ya kuchoma tu nyavu au kutunga tu sheria ngumu walikuwa wafikirie sana namna ya kuwaendeleza wavuvi. Nasema hivyo kwa sababu, kwa mfano, Serikali inapotaka kupitisha njia eneo inapitisha barabara wanafika mahali wakikuta kibanda cha mtu kwa sababu ya kuthamini binadamu yule wanaamua kumlipa fidia. Lakini kwa bahati mbaya sana mvuvi hafanyiwi hivyo inachukuliwa tu nyavu kwa sababu ya kigezo cha uvuvi haramu inachomwa au kitu kingine chochote kinaangamizwa bila kufikiria kumbe Serikali ilitakiwa ikinunue kile kwa sababu na yeye ndio maisha yake. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, sawa sawa na nyumba au ardhi inayopatikana wakati inapopitishwa barabara. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali iwahurumie sana wavuvi wanafanya kazi hatari sana na sisi kama Serikali hatujafikia kiwango cha kuwaendeleza moja kwa moja. Huwa nachukulia mfano ingekuwa yule mvuvi ni mtoto wangu siningempa mtaji nikamnunulia chombo kizuri sana mashine nzuri, mitego mizuri lakini Serikali inatakiwa ijue kwamba wale wavuvi ni kwa ajili ya mapato ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo na wao ipo haja ya kuwaandalia utaratibu wa kuendesha maisha yao lakini pia na pato kwa Serikali. Jimbo langu sehemu kubwa sana imepakana na bahari ya Hindi na pale kuna wavuvi na mara nyingi sana wavuvi hawa wanaenda kuvua mbali sana lakini Serikali bado haijaweza kuweka ulinzi huko wanakokwenda, sina hakika kwamba Serikali hapa Tanzania Bara kwa mfano imeweka vyombo maalum huko baharini kwamba wavuvi wakipata tatizo lolote wanaenda kuokolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halipo naomba sana Serikali ifanye hivyo kwa sababu uvuvi ni kazi hatari sana na sisi wote naamini kila anayemsomesha mwanae uvuvi hampi chombo kwenda kuvua baharini bali anamtafutia eneo zuri kwenye Serikali awe mhudumu ofisini ili awasimamie wavuvi. Kwa hiyo, bado uvuvi na changamoto kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndipo tunapotakiwa sasa kutumia sayansi yetu tumesoma sayansi kwa muda mrefu sana na Tanzania wanasifiwa sana kwa wanasayansi, na hapa ndio tunatakiwa kuitumia vizuri sana kwa kuelewa ni eneo gani lina Samaki ili Serikali ipate faida kubwa zaidi, kama hautujaweza kutengeneza vifaa vitakavyotuonesha kwamba hapa hili eneo kuna, Samaki tukawatayarisha wavuvi wetu wawe katika utaratibu huo, elimu hiyo, basi tusitegeme kwamba sekta hii ya uvuvi itakuwa nzuri. Kwa sababu mpaka sasa hivi wavuvi wetu wanavua kwa kubahatisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ana ring net anaenda kuzungusha anavua hamna kitu mara mbili tatu, bado tunabahatisha. Haya maeneo tajiri sana sisi watanzania Mwenyezi Mungu ametubariki sana maeneo haya ya uvuvi tuna maziwa mengi, lakini tuna bahari kubwa sana ya Hindi. Kwa nini hadi leo hatujafikia mahali bahari ya Hindi ikatuneemesha? Na kila mtu anajua kwamba bahari ni tajiri mbali ya Samaki kuna mambo mengi sana ambayo ni ya kufanya nchi yetu iwe tajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, bado Serikali haijafikia maamuzi ya kuandaa utaratibu wa kuwanufaisha wavuvi, na wahudumu wengine wa bahari lakini pia kwa kupata mapato makubwa zaidi. Naomba sana Serikali iwafanye wavuvi ni watoto wao lakini pia ni waajiwa wao kama vile wanavyohudumiwa walimu sisi Wabunge na wafanyakazi wengine ndivyo wahudumiwe wavuvi, kama kweli tunahitaji wavuvi walete tija ndani ya nchi hii vinginevyo tutawapelekea wavuvi hasara ndio maana hapa nina tarehe 3 Novemba, 2018 kuna wavuvi walikamatwa kesi yao haijulikani iko wapi lakini walipelekwa mahakami ni watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaelekeze lakini pia Serikali kuna wavuvi walipigwa mpaka risasi kwa nini?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naunga mkono hoja na nawatakia heri sana Waziri na Naibu wake na wewe mwenyewe, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhana Wataalah kwa kuwa yeye ndiye aliyetuumba kuwa wanadamu na hakutuumba Wanyama, kwa hiyo, ametuumba wanadamu tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu Alhamdullilah. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana na kumshukuru sana Rais wa nchi hii ya Tanzania, mama yetu Samia Suluhu Hassan, mwanamke wa kwanza Afrika Mashariki kuwa Rais na ninampongeza pamoja na wote wafuasi wake wanaomsaidia Dkt. Mpango, Makamu wa Rais na Mawaziri wote na Naibu Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza kwa pongezi za kipekee kwa kutuletea hotuba hii au bajeti hii ambayo ni nzuri sana. Bajeti hii imewachukua mpaka wale ambao ni wachache kwenye Bunge hili wakadiriki kusema kwamba ile yaani inawasababisha kupata raha mpaka wanasema kwamba inawatekenyatekenya, inawafinyafinya, kwa kweli mimi nilijisikia faraja sana. Namuomba Mwenyezi Mungu ampe nguvu sana Mama yetu Mama Samia, nguvu za kipekee za kutuongoza kule tunakokuhitaji na amuepushe kabisa na maadui na mahasidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ndio itaenda kutekeleza Ilani yetu ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025 na ninaimani kwamba mwaka 2025 Bunge hili linaweza likawa la Chama cha Mapinduzi peke yake kwa sababu reference mama yetu Mama Samia alivyokuwa Makamu wa Rais wakashauriana vizuri na Mheshimiwa Magufuli ambaye ni Hayati sasa hivi, walitekeleza ilani ipasavyo wakatufanya hata sisi Wabunge kutoka Pemba wa CCM tukawepo hapa. Leo tunajivunia sana kuwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kuwemo ndani ya Bunge hili kutoka Pemba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni tabia tu kama alivyokuwa akilalamikia hapa Mbunge kutoka upinzani hapo, alikuwa akilalamikia kwamba, hakuna haki, lakini inavyoonekana kwamba haki lazima wapate wao ndio tatizo lao pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza pia mama kwa kutupatia zile shilingi milioni 500 kwa kila Jimbo, namshukuru sana na watu wasiwe na wasiwasi jamani, hizi zilivyotajwa zilitajwa kwamba kila jimbo. Unapofanya wasiwasi kwamba sisi wapemba, sijui sisi Wazanzibari hatutapewa, maana yake una wasiwasi kwamba kule hakuna majimbo. Hizi fedha zitatoka jamani, msiwe na wasiwasi, haya maneno kasema mama, mna wasiwasi na mama? (Makofi)
MBUNGE FULANI: Hatuna.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sasa kuhusiana na hii nyongeza ya shilingi 100 katika mafuta, lakini pia katika mitandao ya simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi 100 hizi mimi najiuliza hivi zitakuwa na alarm? Yaani zitakuwa na sauti zitakapoingizwa? Kiasi kwamba ikifika kwa mfano saa 6:00 ya usiku itamueleza Waziri wetu Mheshimiwa Miwgulu Nchemba kwamba leo kumeingia kiasi fulani cha fedha? Kwa sababu mwenzangu aliyepita kuchangia sasa hivi alikuwa anasema kwamba Waziri Mkuu alitumbua watu kwenye Wizara ya Fedha kwa sababu ya matumizi mabaya, sijui wanajilipa shilingi milioni 400 kwa siku na hizi zitakuwa na usalama gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamuomba Waziri ajue kwamba yeye ndio kaka yetu katika familia hii ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini katika Chama cha Mapinduzi na ajue kwamba yeye ndio kaka mwenye fedha anatakiwa awe makini sana na mfuatiliaji sana na msimamizi sana wa hizi fedha. Kwa sababu wananchi wetu wako tayari kuchangia tena kwa heshima ya Serikali hii tukufu, lakini kwa heshima ya Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo na sisi Wabunge tunalipa baraka jambo hili ila tunaomba kile kilichokusudiwa kitendeke. Na si eneo hili tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuna eneo lingine ungeweza kulitumia vizuri lingeweza kutusaidia sana hata katika tiketi za mabasi makubwa yale yanayokwenda mikoani ingetusaidia kama utafanya kifungu kidogo, kwenye tiketi za usafiri wa ndege, kwenye tiketi za boti; unaweza kuongeza hapo, lakini je, kweli itakwenda kuwanufaisha Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hicho ndio kitu cha kuzingatia. Kadri tutakavyokuwa tukilichangia jambo hili tuhakikishe kwamba, kile kichokusudiwa ndio kinaenda kutendeka kwa sababu nina imani kwamba Tanzania hii tukishatandika barabara zote hizi kodi zitapunguzwa pia, wananchi wetu watapungua kwenye kulipia kodi. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali ifikirie namna gani ya kuzisimamia kodi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi hizi zikikusanywa vizuri tutaondokana kabisa na madeni nje kwa sababu tunavyokopa au kadri tunavyopewa misaada hata wanafunzi wa darasa la sita najua plus minus is equal to minus, kwa maana sisi kadri tunavyokuwa tunapokea misaada ndio tunatoa yaani tunapoteza. Ni logic ndogo ambayo inatumiwa na wanafunzi wa darasa la saba, darasa la tisa, darasa la kumi, kwa hiyo ninaamini Mheshimiwa Waziri anaijua hii hajaisahau kwamba plus minus is equal to minus kwa kadri tunavyokuwa tunapokea misaada ndio tunavyokuwa tunatoa. Kwa hiyo namwomba sana Waziri wetu, kiongozi wetu, kaka yetu katika familia hii, atuongoze katika jambo la kujitegemea na si kuendelea sana kukopa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niishauri Serikali kwamba katika mikakati iliyowekwa kuhakikisha bajeti hii inapatikana inayosimamiwa sikuona, inawezekana imo lakini sikuona kwamba kunahitajika kuwe na usalama wa nchi. Nilimsikia Mheshimiwa Noah hapa akieleza orodha ya matukio ya ujambazi ambayo yapo, ambayo yangeweza kufanya wafanyabiashara kama walikuwa wanafanya biashara mpaka saa sita ya usiku, sasa wataogopa kwa sababu kuna ujambazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili naomba sana Serikali ilifanyie utafiti ni muhimu sana kufanyia utafiti. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini kwanza nianze kwa kuwashukuru viongozi wetu wakuu wa nchi ambao ni Mama Samia, mwanamke pekee katika Afrika Mashariki anayetuongoza kwa wema sana na kwa heri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia nishukuru na nimpongeze Makamu wetu wa Rais Dkt. Philip Mpango kwa kumshauri vizuri mama na leo mafanikio yake tunayaona sana. Lakini nimshukuru pia na kumpongeza Waziri Mkuu kwa namna anavyosimamia Serikali hii ya Mama Samia nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika na Naibu Spika kwa namna ambavyo mnavyotuongoza na katika muongozo ambao naushukuru sana ni kwamba leo mimi nipo kwenye Kamati hii ya Sheria Ndogo, najisifia kujua mambo mengi sana katika nchi hii ya Tanzania ambayo nilikuwa siyajui ni kwa sababu tu umechukua jukumu la kunipanga katika Kamati ya Sheria Ndogo, nakushukuru sana, Mwenyezi Mungu akupe uhai mrefu wenye manufaa hapa duniani na akhera, lakini akupe busara na hekima za kuliongoza Bunge hili mpaka pale Mwenyezi Mungu atakaposema basi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sheria ndiyo kitu muhimu sana katika hii dunia na kila kinachofanikiwa katika dunia ni kwa sababu kimewekewa sheria madhubuti, lakini pia kusimamiwa sheria hiyo, ndiyo maana hata dini zetu uislamu, ukristo na dini nyingine zinaendelea vizuri au zinafanikiwa kwa sababu ya sheria. Kwa hiyo, tunashukuru sana leo kwamba sisi tupo kwenye Kamati ya Sheria Ndogo na tunasimamia sheria hizi ili nchi iende vizuri, tunashukuru sana na tunawaomba wanaohusika sasa na sheria wazitekeleze kwa wema sana.
Mheshimiwa Spika, mimi ninamambo machache sana yaani ninayoyaomba katika mchango wangu huu; kwanza katika mijadala yetu mingi sana tulikuwa tunashuhudia kwamba ushirikishwaji wa wadau ulikuwa mdogo sana au ulikuwa hakuna katika kila sheria iliyotungwa, kwa sababu unapomshirikisha mdau maana yake anatoa zile concern zake, zile hisia zako anazitoa kwako kwamba mkituambia hivi tutakuwa kuna tatizo hili, tatizo hili litajitokeza, lakini kwa vyovyote vile ukimshirikisha mdau utapunguza changamoto katika sheria, utapunguza makali katika sheria, lakini jambo hili limekosekana, unakuta kwamba sasa badala ya kwamba tunatunga sheria ili Serikali ipate mapato, lakini iende vizuri unakuta sasa kuna malalamiko ndani ya nchi. Jambo hili tunawaomba sana wale waliokasimiwa madaraka ya kutunga sheria na hasa hizi sheria ndogo ambazo sisi ndiyo tunazisimamia tunawaomba sana waweze kuwashirikisha wadau ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ambalo mimi ninapenda nishauri na niombe ni kuweka uwiano baina ya sheria mama kwa sababu sheria zote zinazoitwa ndogo maana yake kuna sheria kubwa ambayo tunaita sheria mama, ni muhimu sana tunavyoamini ni kwamba wale wanaotunga sheria ndogo wameaminiwa na tunaamini kwamba wamesomea zile sheria, kwa nini wasifanye ile sisi tunaita murajaa, kwa nini wasirudie kwenye zile sheria mama wakajua kwamba hiki ninachokifanya kinalingana na sheria mama. Sheria mama inasema adhabu ni shilingi 20,000 wao wanasema shilingi 200,000; haiendani kabisa yaani kama kwamba hawakusoma kabisa kwenye ile Katiba au sheria mama, sasa hii inapelekea kuleta image mbaya kufikiria kwamba waliotunga hii sheria walikuwa wana-interest gani kwenye hiyo sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, ni kukomoana yaani kuna sheria unahisi hasa kwamba hii sheria imetungwa kwa kuwakomoa watu Fulani, sasa mimi nilikuwa naomba sana wanaotunga hizi sheria wasitunge kwa kukomoa au kwa sababu mtu fulani tu tunataka kumlinda kwenye hiyo sheria. Kwa mfano, hata Mheshimiwa Ramadhani alikuwa anasema hapa anatoa mfano wa shilingi 1,000 lakini hata bajaji wakati mwingine hata, kila ikiingia itoe kwa mfano shilingi 500 au shilingi 3,000 sawa sina gari, ila basi wanatoa 40 sasa hii inapelekea kujiona wale wengine kwamba ni inferiority na hawana haki katika nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa mimi nilikuwa naomba sana wale wanaopewa madaraka haya ya kukasimu/ waliokasimiwa madaraka kwa ajili ya kutunga sheria ndogo wajitahidi sana watu wengine wasione kwamba tunawakomoa kwa sababu kazi hii waliyopewa, wamepewa na Bunge, wanaliwakilisha Bunge na sisi Wabunge tumechaguliwa na wananchi hao hao ambao wao ndiyo wanawatungia sheria. (Makofi)
Sasa ikionekana sisi leo tumechaguliwa na wananchi, halafu Wabunge wanakuja kupitisha sheria ambayo imewakandamiza wao, wao watatuonaje. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana wanaokasimiwa madaraka wajitahidi sana kuangalia kutokuwakomoa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kupata fursa hii, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja hii iliyotolewa na Kamati ya Sheria Ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria yoyote duniani ipo kwa ajili ya kudhibiti hisia za wanadamu kwa kuwa mwanadamu anaweza kuamka leo vizuri, kesho vibaya, anaweza kukasirika, anaweza kufurahi sana akatoa maamuzi ambayo siyo sahihi. Sasa baadhi ya sheria ndogo zinaeleza kabisa kwamba jambo hili lililokosewa ataachiwa Mkurugenzi labda wa halmashauri fulani aamue kwa namna atakavyoliona kosa. Sasa nadhani tuiombe Serikali ifikirie kipengele hiki. Mwanadamu yeyote anaweza akamhukumu mtu vibaya kwa sababu tu hata ya mwonekano wake. Kwa hiyo tukiruhusu kwamba tumuache tu Mkurugenzi ahukumu atakavyoona naona haitakuwa sahihi. Kwa hiyo naiomba sana Serikali jambo hili wafikirie kwamba lengo la sheria ni kudhibiti hisia za wanadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kwamba kuna sheria hii ya madawa yaliyoharibika au yaliyo-expire, yasiyofaa, kufanya recall, kwamba labda yameathiri huko au yanaonekana yana madhara yakarejeshwa, Serikali ikaamua kurejesha zile dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria mama, mtu aliyefanya kosa hili anatakiwa alipe faini ya shilingi milioni moja. Hata wale wadau wa sheria hii walikuwa wanaona kwamba adhabu hii ni ndogo sana kulinganisha na kosa hili kwa sabbau hapa ni maisha ya mtu. Anaweza akala dawa ikamgharimu kuondoa maisha yake duniani au akapata athari kubwa ikamsababishia ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu anaweza kulifanya kosa hili kwa sababu tu hakutegemea kwamba atapigwa faini ya shilingi milioni moja ambayo dawa ile ikiuzwa anaweza kupata hata milioni 100 ya faida. Ni vyema sasa sheria hii ikaangalia vizuri au ikaangaliwa upya ili sheria ndogo zinazotungwa zikaweza kupata unafuu wa adhabu angalau watu wakapata hofu ya kujali maisha ya wengine ambao ni wanyonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii naihisi kama vile ni kama sheria ile ya mpira, mtu mpirani anaweza kuvunjwa mguu kabisa, lakini aliyevunja mguu hukumu yake aoneshwe tu kadi nyekundu, yaani anaoneshwa tu. Sasa nadhani Waziri na Serikali ifikirie maslahi ya wanaotumia dawa, kwamba wanaweza kuondoa maisha kwa sababu ya sheria kama hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, naiomba Serikali ione huruma sana juu ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Chama hiki ni chama kinachopenda wanyonge sana, kinachopenda kuondoa kabisa ubaguzi, hakina ubaguzi kabisa; watu wenye ulemavu, wasio na ulemavu, wanadamu wote ni sawa. Sasa inapotungwa sheria ya kuwadhibiti ombaomba halafu ukaainisha kabisa mtu mwenye ulemavu, sijui unawafikiriaje hawa ambao ni viongozi wetu wa Chama cha Mapinduzi, viongozi wenye busara, viongozi mashujaa, mahiri sana, unawafikiriaje hawa na Ndiyo chama kinachoongoza Serikali hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa najiuliza mpaka tunafikia kutunga sheria ya kudhibiti ombaomba, hawa Maafisa wa Serikali waliopo pale wilayani, kuna Mkurugenzi na wasaidizi wake, kuna Mkuu wa Wilaya na wasaidizi wake, hawa wote wana maafisa wanaowasaidia. Sasa malengo ya kuweko maafisa wengi hawa ni nini kama siyo kuwasaidia hawa wengine ambao ni wanyonge?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo dogo tu. Kama ni ombaomba, wewe ndio Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, fanya utafiti; hawa ni ombaomba kwa uzururaji, kwa ulemavu, kwa ugonjwa au kivipi? Maana yake mpaka unafika kutoa hii sheria ya kuwadhibiti ni kwa sababu gani unafanya hilo jambo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ombaomba wamo walemavu ambao sheria ya halmashauri inasema kwamba wewe uwapatie asilimia mbili ili kuwawezesha. Tungetegemea sasa halmashauri imwombe Waziri au itengeneze sheria kuliomba Bunge kwamba sasa hawa ile ruzuku wanayopewa kwa mkopo basi wapewe tu bila kurejesha kwa sababu ni walemavu, lakini leo halmashauri inasema inataka kuwadhibiti. Inakuwaje Serikali yetu ya wapenda wanyonge inayoongozwa na viongozi wenye busara sana, leo unasema kwamba ombamba wadhibitiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Sheria kama itatekelezwa, maana yake haitamalizia hapo. Kuna watu wataharibikiwa na safari njiani, wataenda kwenye taasisi za dini; kuna mtu ataenda Kanisani, mwingine ataenda Msikitini ataomba, jamani nimekuja hapa nimeharibikiwa na safari; na watu wakiwa na roho mbaya wanaweza kumshitaki, kwa sababu ni ombaomba pia. Kuna watu wanaojenga taasisi za dini kwa kupitia michango ya wanadini wenzao, watu wakiwa na roho mbaya wanaweza kumshitaki kwa sababu sheria hii ya kudhibiti ombaomba ipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba sana waliotunga sheria hii watuonee huruma sana, hasa Chama chetu cha Mapinduzi kinachopenda wanyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi ya kuchangia katika wasilisho hili la sheria ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakushukuru kwa kutuchagua pia katika jambo hili au katika Kamati hii ya Sheria Ndogo, tunakushukuru sana wewe na Mheshimiwa Spika kwa sababu Kamati ya Sheria Ndogo kimsingi ndiyo Kamati inayoendeleza Miji, Halmashauri, Vijiji, kuna sheria nyingi hapa ambazo sisi zitatufanya tuelewe kila kitu kinachokwenda ndani ya nchi hii, tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, mama msikivu, muadilifu, mwenye hekima, mwenye huruma kubwa sana kwa wananchi wake na hii ni kwa sababu anatoka kwenye Chama cha Mapinduzi, chama ambacho kinatekeleza Ilani yake kwa uangalifu na uadilifu sana. Mama huyu ukilalamika tu tozo yeye anaondoa, sijui halmashauri hii haina shule anakuletea, hakuna hospitali mahali analeta, huyo ndiyo Mama Samia kutoka Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka Mama Samia anafikia kwenye maamuzi hayo au kwenye sifa hizo ni kwa sababu Tanzania ni nchi tunayoisifu na inayosifika duniani kwamba ni nchi yenye utawala bora. Na nchi hii yenye utawala bora ni utawala wa sheria, na sheria hizi ndiyo tupo kwenye sheria ndogo, sheria zinazoongoza huko vijijini na kwenye halmashauri mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaomba sana wale ambao wamekasimiwa madaraka na Bunge kutunga sheria hizi tunazoziita sheria ndogo basi wawe makini sana kwa sababu hizi sheria tunaziita ndogo, lakini ndiyo zinazowafanya watu wawe jela, ndizo zinazowafanya watu watozwe faini. Kwa hiyo, si sheria ndogo kama tunavyosaini ni sheria hasa za nchi. Kwa hiyo, tunawaomba sana wawe makini sana na hii ni kwa sababu Waarabu wana msemo wao wanasema dawamulhali minalmuhali (mtu hadumu kwa kwa hali moja Maisha) na sheria hizi zinaenda kusimamiwa na watu mahakamani, leo hakimu anaweza kuwa na hasira akatumia sheria ndogo hii hii akamuonea mtu. Kwa hiyo, ili tumdhibiti hasira zake, furaha yake, huzuni yake lazima tuweke sheria ambayo itamuongoza asije akaongozwa kwa hisia zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina mfano hapa wa sheria inayoitwa Electricity Act, Sura 131; kuna sheria ndogo inasema Electrical Installation Services hii imetoa adhabu mbili; adhabu ya kwanza kwa mtu ambaye hana leseni ya kufanya installation ni faini isiyozidi shilingi milioni moja au kifungo kisichozidi miaka mitano au vyote viwili, lakini mtu mwingine anayo leseni, lakini atafanya jambo nje ya leseni yake, leseni imekwambia wewe kazi yako ni kuweka waya tu hautakiwi baada ya waya kuweka meter kwa mfano, kuweka plug, yeye kwa sababu ya ubinadamu wake akapitiwa akaweka vile vitu, kwa hiyo, yeye anatakiwa alipe shilingi 200,000; lakini amefanya kitu ambacho ni nje ya leseni yake maana yake ni kwamba tuna mli- guard kwamba huyu leseni pia hana jambo alilofanya hana leseni, lakini sheria imemfanya kwamba yeye alipe faini shilingi 200,000. Sasa lazima tuwe waangalifu tusiwe na bias kwamba huyu yupo hivi yupo hivi, lazima tufike mahali wananchi wetu wote ni wamoja tuwe na huruma kama alivyo Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wale tunaomwakilisha lazima tuwe makini katika jambo hilo. Lakini sawa ulishaliona tatizo hili sheria ndogo ilishaona tatizo tumeitana na tunawasifu Mawaziri Mashallah Alhamdulillah, ni wasikivu sana wanalichukua tunakubaliana tunaenda kulirekebisha hasa hiyo kurekebisha hiyo huku sheria ipo mtaani inafanyakazi, lakini hapa muda wa kurekebisha watu wanaumia field, hairekebishwi inatuchukua muda mrefu sana mpaka kurekebishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, alikuwa ametoa wazo kwamba Bunge hili liazimie kwamba sasa kazi inapotolewa hii ya kurekebisha iwe na muda maalum. Kwa hiyo, tunaliomba sana Bunge lifanye hivyo kwasababu hizi sheria ndiyo zinaumiza watu wetu kule field. Tuwafikirie watu wetu kwamba wao ndiyo wanaumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii kuwa mchangiaji wa mwanzo kabisa katika jambo hili la Kamati hii ya Kudumu ya Sheria Ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Allah Subhana Wa ta’ala muumba mbingu na ardhi, akatuwezesha sisi kuwa Wabunge mahiri tunaofanya kazi zetu kwa umakini sana. Lakini pia nitumie fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri sana anayoifanya. Amefika kila eneo, kila jimbo, kila kata kupeleka maendeleo. Tunamshukuru sana, tunampongeza sana, tunampa moyo sana, ili aendelee kufanya kazi hii adhimu ya Taifa hili, kazi ya uzalendo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashukuru pia kuwemo kwenye Kamati hii, Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo. Katika vipengele ambavyo vimetajwa leo hapo na Mwenyekiti wakati akiwasilisha mada yake ni kutokutekelezwa kwa Maazimio ya Bunge. Sisi hapa tumekaa tunapitisha maazimio leo. Mfano leo, tumeshasoma na tutapitisha maazimio, kama yalivyoelekezwa katika uwasilishaji wake, na Bunge linaazimia kwamba, jambo hili lirekebishwe, litengenezwe, halafu anatokea mtu hafanyi hilo jambo kwa hiyo, hatekelezi Maazimio ya Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi siamini kwamba kuna mtu ana nguvu hiyo, lakini labda huwa nafikiri labda amesahau au hakusikia au sijui niseme neno gani zuri. Maana maazimio tunayatoa kwa pamoja tunakuwepo humu Bungeni, watu wanasikia, wafau wenzetu wanasheria wanayachukua wanakubaliana na sisi, miezi inapita, mitatu, minne, mpaka miezi sita hajatekeleza, lengo lake huwa ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, labda wanafikiria kwamba Kamati hii ya Sheria Ndogo labda si Kamati ya kisekta, mimi huwa nafikiria vitu kama hivyo, labda si Kamati ya kisekta kwa hiyo, hawajibiki sana hivi, hana wajibu wa kuwajibika wa kutekeleza Maazimio ya Bunge kwa sababu ni watu wa sheria ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ifahamike kwamba, Kamati ya Sheria Ndogo ni sawa na kamati nyingine yoyote ya Bunge na tunaliwakilisha Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, siamini na wala sitaki kuamini kwamba kuna mtu anatubeza kiasi hicho. Sasa, kama yupo tunamuomba aache hilo jambo, aache kabisa, kwa sababu hizi tunazozitengeneza ni sheria na tunazitengeneza kwa ajili ya wananchi wenzetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, utawala bora ni utawala wa sheria. Maana yake ni kwamba, kama sheria ni mbovu, zimerekebishwa na wewe hautaki, maana yake ni kwamba unabomoa utawala wa sheria ambao ndio utawala bora, kazi ambayo itakuwa inatukwaza, si jambo zuri. Na bahati nzuri sana ni kwamba, hizi sheria tayari ziko mtaani na zinawaumiza watu, ni wananchi wenzetu na sisi ni miongoni mwa wananchi. Kwa hiyo tunawaomba wale wanaohusika, wale wadau wenzetu wa sheria wanaohusika na kurekebisha warekebishe. Si vizuri mpaka Bunge lingine linakuja maazimio ya Bunge hayajatekelezwa, si jambo zuri. Lakini mimi ninaamini labda watu wanafanya hivyo kwa sababu ya yale madaraka yao, labda wale wanataka kuyalinda yale madaraka, kwamba hiyo sheria ikibadilishwa inamfanya madaraka yake yapotee.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi naomba tena kwa heshima na taadhima wale wanaohusika na kutekeleza Maazimio ya Bunge baada ya Bunge kupitisha maazimio hayo wayatekeleze. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo naunga mkono hoja na ninakushukuru kwa nafasi; ahsante. (Makofi)