Primary Questions from Hon. Amour Khamis Mbarouk (10 total)
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha vikundi vya wananchi ili kuhamasisha uhifadhi wa mazingira hasa katika fukwe za Bahari ya Hindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali tayari ina mpango wa kushirikisha wananchi kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais. Pia Serikali imeandaa mkakati wa kuhifadhi mazingira ya Bahari, Ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa. Aidha, kufuatia utekelezaji wa mkakati huu na kwa kutambua umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika kuhifadhi mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanzisha vikundi vya usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi vinavyofahamika kwa jina la “Beach Management Units” – BMUs. Vikundi hivi vimeanzishwa katika ngazi ya Kijiji/Mtaa kwa mujibu wa Kifungu cha 18 cha Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003. Ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi una jumla ya vikundi 157 ambapo Tanga ina vikundi (31), Pwani (46), Dar es Salaam (23), Lindi (46) na Mtwara (11). Ahsante. (Makofi)
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -
Je, Serikali inakusanyaje ushuru kwenye Boti zinazoondoka saa moja kamili asubuhi katika Bandari ya Dar es Salaam ilhali watumishi hufika kazini kuanzia saa moja na nusu na zaidi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), pamoja na wadau wote muhimu ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hutoa huduma za kibandari kwa saa 24 kwa siku saba za juma katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, Kanuni za Utumishi kwa Wafanyakazi wa Bandari za mwaka 2019 zimetoa Mwongozo wa Muda wa Kuwa Kazini, ambapo wafanyakazi wote wa Bandari wanaopangiwa maeneo ya kutoa huduma kwa meli ama boti za mizigo hupaswa kuingia kazini kwa zamu (shifts) tatu kama ifuatavyo; saa 1:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri; shift ya kwanza; saa 9:00 alasiri hadi saa 5:00 Usiku; shift ya pili na saa 5:00 Usiku hadi saa 1:00 asubuhi shift ya tatu.
Mheshimiwa Spika, aidha, watumishi wa TPA wanaopangiwa zamu katika eneo la boti zinazosafiri kati ya Dar es Salaam na Zanzibar wanapaswa kuwepo kwenye eneo la kazi na kuhakikisha kuwa huduma zote muhimu za kibandari zinatolewa ikiwemo ukusanyaji wa mapato ya Bandari. Nitumie fursa hii kuitaka TPA kusimamia kwa karibu utaratibu uliowekwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -
Je, kuna Wavumbuzi wangapi na wa teknolojia gani kwani Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa una lengo la kuchochea uvumbuzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mchango wa uvumbuzi na ubunifu kama nyenzo muhimu katika kuchochea ushindani na uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya watu kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuibua, kutambua na kuendeleza uvumbuzi, ubunifu na maarifa asili ya Tanzania kupitia mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) na programu ya kutambua teknolojia zinazozalishwa ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa Serikali imetambua wavumbuzi na wabunifu wapatao 2,735 katika sekta za Afya, Viwanda, Elimu, Kilimo, TEHAMA, Usafirishaji, Nishati, Madini, Mazingira, na Uvuvi. Aidha, Teknolojia 479 zimeweza kuibuliwa, kutambuliwa na kuhakikiwa. Wabunifu 376 wanaendelezwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Kati ya bunifu zilizoendelezwa, 35 zimefikia hatua za ubiasharishaji. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -
Je, ni kwa nini mizigo ya wasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kwa kutumia meli kubwa inapekuliwa na mbwa badala ya scanner?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mizigo yote ya wasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kupitia Bandari ya Dar es Salaam inakaguliwa kwa mdaki (scanner). Katika kuimarisha usalama wa bandari, wasafiri pamoja na mizigo inayosafishwa kwenda Zanzibar, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) iko kwenye hatua za manunuzi ya mdaki (scanner) mwingine mpya kwa ajili ya eneo la meli zifanyazo safari kati ya Dar es Salaam na Zanzibar ili kupunguza muda unaotumika kukagua mizigo na hivyo kufanya eneo hilo kuwa na Midaki miwili. Mdaki mpya unaonunuliwa unatarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwezi Aprili, 2023.
Mheshimiwa Spika, matumizi ya mbwa katika Bandari ya Dar es Salaam hufanyika kwa ukaguzi maalum wa mizigo baada ya mizigo hiyo kukaguliwa kwa kutumia mdaki na kuonekana si salama kuruhusiwa kupita, ahsante.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaboresha jengo la Kituo cha Polisi Konde, Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk Mbunge wa Tumbe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uchakavu wa jengo la Kituo cha Polisi cha Konde kilichopo Wilaya ya Micheweni. Tathmini ya uchakavu ili kufanya ukarabati imefanyika mwezi Novemba, 2022 na kiasi cha fedha shilingi 92,000,000 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati huo. Fedha hizo zitatengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -
Je, Tanzania inapokea watalii wa aina ngapi kutoka nje na sekta hii inachangia kiasi gani katika Pato laTaifa kwa mwaka?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe, kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa ikipokea watalii mbalimbali kutoka masoko ya Kimataifa ikiwemo nchi za Bara la Afrika, Amerika, Asia na Pasifiki, Ulaya, na Mashariki ya Kati. Watalii hao wamekuwa wakitembelea Tanzania kwa madhumuni tofauti, ikiwa ni pamoja na mapumziko, kutembelea ndugu na jamaa, biashara, mikutano, matukio, na sababu nyinginezo ikiwemo ziara za kujifunza na matibabu.
Mheshimiwa Spika, sekta ya utalii kabla ya mlipuko wa janga la UVIKO - 19 ilikuwa ikichangia wastani wa asilimia 17.2 ya Pato la Taifa, asilimia 25 ya fedha za kigeni, asilimia 60 ya biashara za huduma na kuzalisha ajira takribani Milioni 1.5, ikiwa ni ajira za moja kwa moja na zile zisizo za moja kwa moja.
Mheshimiwa Spika, mlipuko wa janga la UVIKO-19 ulioikumba Dunia mwishoni mwa mwaka 2019 ulisababisha kupungua kwa idadi ya watalii kutoka 1,527,230 mwaka 2019 hadi watalii 620,867 mwaka 2020. Mapato kutoka Dola za Marekani Bilioni 2.6 hadi Dola za Marekani Bilioni 0.7.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -
Je, kwa mujibu wa master plan ya miundombinu ya barabara Tanzania, tunahitaji fedha kiasi gani kukamilisha miundombinu hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu kilometa 36,760.29, kati hizo kilometa 12,223.04 ni barabara kuu (Trunk Roads) na kilometa 24,537.25 ni barabara za mkoa (Regional Roads). Kati ya kilometa 36,760.29, kilometa 11,587.82 sawa na asilimia 31.50 zimejengwa kwa kiwango cha lami na kilometa 25,172.48 zilizobaki ni za changarawe, sawa na asilimia
68.50. Ili kujenga kwa kiwango cha lami kilometa 25,172.48 zilizobaki, inakadiriwa kiasi cha shilingi trilioni 45.3 zinahitajika kwa wastani wa gharama za ujenzi bilioni 1.8 kwa kilometa kilometa moja, ahsante.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawaendeleza wavuvi kwa kuanzisha uvuvi unaotumia dira maalum inayoelekeza samaki walipo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) K.n.y WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tanzania Fisheries Research Institute - TAFIRI), imeshaanza kuteleleza mradi wa kutambua maeneo yenye samaki yanayofaa kwa uvuvi (Potential Fishing Zones - PFZs) katika Bahari ya Hindi ili kuwasaidia wavuvi kujua maeneo yenye samaki wengi. Aidha, katika mradi huu, wavuvi wanawezeshwa kufanya uvuvi unaotumia dira maalum kwa kupewa taarifa za kijiografia (GPS) kupitia simu za mkononi ili kujua maeneo yenye samaki kwa wakati husika. Mradi huu wa majaribio ulifanyika kwa mafanikio kwa kushirikiana na wavuvi wa maeneo ya Mafia na Tanga kwa upande wa Tanzania Bara na Unguja na Pemba kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa TAFIRI inatengeneza programu maalumu (mobile app) ambayo itawawezesha wavuvi kupata taarifa za maeneo ya uvuvi ambako samaki wanapatikana kwa wingi. Aidha, programu hiyo imekamilika kwa asilimia 90. Ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO K.n.y. MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -
Je, kwa nini Serikali imehamisha Kituo Kidogo cha Polisi Tumbe?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, shughuli na huduma za Kituo cha Polisi Tumbe kilichopo Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, zimehamishwa toka Tumbe kwenda Kituo cha Polisi Konde. Sababu ya kufanya hivyo ni uchakavu wa jengo lililokuwa linatumika kama kituo cha polisi ambalo ni mali ya Shehia ya Tumbe Mashariki. Jengo hilo halifai tena kwa matumizi ya kazi za polisi. Eneo hilo pia ni finyu na limezingirwa na nyumba za makazi ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kutumia fursa hii kumshauri Mheshimiwa Mbunge kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni kupata eneo kubwa zaidi lenye angalau ukubwa wa square meters 3,000 kwa ajili ya kujenga kituo cha polisi eneo hilo la Tumbe. Wizara kupitia Jeshi la Polisi itaunga mkono katika ujenzi wa kituo hicho kipya, ahsante.
MHE. KHAMIS MBAROUK AMOUR aliuliza: -
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuwasaidia wamachinga ili waondokane na umachinga na kuongeza mapato ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khamis Mbarouk Amour, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, wamachinga ni fursa sahihi ya kujenga uchumi, Serikali itaendelea kusaidia wajasiriamali kifedha na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara, miundombinu na kurasimisha wajasiriamali ikiwemo wamachinga. Nakushukuru.