Primary Questions from Hon. Omar Ali Omar (9 total)
MHE. OMAR ALI OMAR Aliuliza:-
Je ni lini Serikali itatoa ajira kwa Jeshi la Polisi, hasa ikizingatiwa kuwa haijatoa ajira tangu mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Omar Ali Omar, Mbunge wa Jimbo la Wete kutoka Mkoa wa Kaskazini Pemba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuajiri na kuongeza idadi ya askari polisi hapa nchini kwani idadi yao hupungua kutokana na askari kustaafu, kufariki dunia, kufukuzwa kazi na wengine kuacha kazi, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali kupitia bajeti yake ya mwaka 2021/2022 imetoa kibali cha ajira kwa askari polisi 3,103 ambapo mchakato wake unaendelea hivi sasa. Nakushukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuliza: -
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati jengo kongwe la Polisi Wete ambalo lipo katika hali mbaya?
(b) Je, ni lini Serikali itayatengeneza magari ya polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo kwa sasa ni gari moja tu linafanya kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, tena kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Ali Omar, Mbunge wa Jimbo la Wete swali lake lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uchakavu wa jengo la Kituo cha Polisi Wete ambalo limejengwa mwaka
1973. Tathmini kwa ajili ya ukarabati ilifanyika mwaka 2021 na kubaini kwamba kiasi cha shilingi 52,760,000 kinahitajika ili kugharamia ubadilishaji paa, mfumo wa umeme, ceiling board pamoja na kupaka rangi. Hivi sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Kaskazini Pemba kuna magari ya polisi 12 na yanayofanya kazi ni magari matano na magari saba ni mabovu. Tayari magari hayo yameshafanyiwa tathmini ya ubovu na kubainika kuwa kiasi cha shilingi 44,254,000 kinahitajika kwa ajili ya ukarabati. Aidha, ukarabati huo utafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha. Nakushukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuliza: -
Je, wanafunzi wangapi kutoka Zanzibar wamepata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2020/2021?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Omar Ali Omar, Mbunge wa Wete kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imekuwa ikitoa mikopo kwa wanafunzi wote wa Kitanzania wenye uhitaji bila kuangalia mwombaji anatoka upande upi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, takwimu za mwaka 2020/2021 zinaonesha kuwa wanafunzi Watanzania wapatao 1,492 wanaosoma katika taasisi sita za elimu ya juu zilizopo Zanzibar walipangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 5.3. Aidha, kwa mwaka 2021/2022 jumla ya wanafunzi wa Tanzania 1,929 wanaosoma katika taasisi za elimu ya juu Zanzibar walipangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 5.8. Nakushukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuliza: -
Je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na uharibifu unaotokana na ukataji mikoko na uvunaji wa matumbawe ili kuvinusuru visiwa visitoweke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Ali Omar, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto iliyoainishwa na Mheshimiwa Mbunge Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimekuwa zikichukua juhudi mbalimbali za kisera, kisheria pamoja na kuandaa miongozo mbalimbali ya utunzaji wa mazingira ya baharini ili kuhakikisha uharibifu wa mazingira ya bahari unadhibitiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa juhudi hizo ni kama zifuatazo: -
Kwanza, kujenga uelewa kwa wanajamii juu ya utunzaji wa mazingira na rasilimali za bahari ikiwemo uhifadhi wa mikoko na matumbawe.
Pili, upandaji wa mikoko na matumbawe katika maeneo yaliyoathirika kwa kutumia njia mbalimbali endelevu na za kitaalamu. Kwa mfano upandaji wa hekta Saba za mikoko Unguja na hekta 10 Pemba kwa mwaka 2020 – 2021 pamoja na kuweka matumbawe bandia 90 Unguja na Pemba.
Jambo lingine ni ushirikishwaji wa jamii katika kusimamia maeneo ya mikoko na matumbawe ikiwemo kuanzisha hifadhi ndogondogo za kijamii katika maeneo ya Kukuu, Fundo, Makoongwe kwa Kisiwa cha Pemba na maeneo ya Mtende, Tumbatu na Kizimkazi kwa upande wa Kisiwa cha Unguja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuiliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka magari kwa jeshi la polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Ali Omar, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kulipatia Jeshi la Polisi magari kama nyenzo ya kutendea kazi. mwaka 2022, Mkoa wa Kaskazini Pemba ulipatiwa magari matatu (3) yaliyonunuliwa na Serikali ili kupunguza uhaba wa magari katika mkoa huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bajeti yake ya mwaka wa fedha 2022/2023, imetoa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 15 kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kununulia magari na pikipiki. Pindi magari na pikipiki yatakapopokelewa yatagawiwa kwenye mikoa na wilaya zenye uhitaji mkubwa ikiwemo Mkoa wa Kaskazini Pemba, nashukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuliza: -
Je, kwa nini Serikali haipangi kusahihishia mitihani ya kidato cha nne Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Ali Omari, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2021 na 2022 Serikali ilisahihisha mitihani ya Taifa, kidato cha nne (CSEE) katika kituo cha Shule ya Sekondari Hasnuu Makame, Kusini Unguja. Aidha, Serikali itaendelea kusahihisha mitihani Zanzibar kwa vituo vya mitihani vyenye sifa za kulaza watahini wasiopungua 500 kwa wakati mmoja, kuwa na vyumba visivyopungua ishirini vya kazi, na miundombinu ya maji na umeme kwa wakati wote wa kazi ya kusahihisha, nakushukuru sana.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuliza:¬-
Je, lini Serikali itajenga ukuta wa Ikulu Ndogo ya Muungano Pemba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Ali Omar, Mbunge wa Jimbo la Wete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaandaa mipango mahususi ya kutekeleza suala hilo ambapo tathmini ya kitaalamu ya kina imefanyika ili kupata gharama za ukarabati wa Jengo la Ikulu ndogo ya Muungano Pemba ikiwa ni pamoja na ujenzi wa ukuta. Aidha, inategemewa kuwa, utekelezaji utaanza katika mwaka wa fedha 2024/2025, nakushukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuliza: -
Je, sababu gani zinazosababisha Wananchi ambao wamepatiwa Visa kwenda nje ya nchi kutosafiri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiwaruhusu wananchi kwenda nje ya nchi kwa madhumuni mbalimbali baada ya kukamilisha taratibu zote za kuondoka nchini. Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamekuwa wakizuiliwa kuondoka nchini kutokana na sababu kadha wa kadha ikiwemo sababu za kiusalama kutokana na mazuio yanayowekwa na taasisi za kiusalama, kuwa na Visa isiyo halali, kuwepo viashiria vya uhusika katika usafirishaji haramu wa binadamu hasa watoto wadogo na wanawake, kwa wale wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi kushindwa kukidhi vigezo vilivyowekwa na Wizara ya Kazi na Ajira na mwisho ni kutokufuatwa kwa taratibu za kusafiri nje ya nchi kwa watumishi wa umma, ahsante.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya mapitio katika kubaini kaya maskini ili kuondoa malalamiko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, TASAF imekuwa ikitumia utaratibu wa kutambua na kuandikisha kaya maskini kupitia Mkutano Mkuu wa Kijiji, Mtaa au Shehia kwa usimamizi wa watendaji kutoka maeneo ya utekelezaji kwa kuzingatia vigezo vilivyoainishwa na jamii husika.
Mheshimiwa Spika, katika kushughulikia malalamiko ya walengwa, wananchi na viongozi kuhusu utekelezaji wa Mpango wa TASAF imekuwa ikitumia njia mbalimbali ikiwemo kufanya uhakiki ili kuziondoa katika Mpango kaya zilizoimarika kiuchumi. Katika mapitio yaliyofanyika kwenye kaya 750,000 kutoka vijiji, mitaa na shehia 12,000 ilibainika kuwa kaya 394,505 zimeimarika kiuchumi na hivyo kukidhi vigezo vya kuhitimu na kutoka katika Mpango. Aidha, kwa sasa Serikali ipo kwenye maandalizi ya usanifu wa Mpango utakaofuata baada ya Mpango wa sasa kufika katika ukomo hapo Septemba, 2025. Ninashukuru.