Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Omar Issa Kombo (23 total)

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamona na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini je, kwa vile tunafahamu kwamba, vijana hawa wanaokwenda JKT takribani wengi wao ni kutoka katika familia maskini na wanatumia gharama kubwa mpaka kufikia kwenye makambi. Je, Serikali iko tayari kuweka utaratibu pindi inapotokea dosari kama hii kuwarejeshea gharama ambazo wanatumia kwa ajili ya safari hizo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyosema kwamba, lengo la kuwarudisha vijana ilikuwa ni kuhakikisha kwamba, tunaweka utaratibu mzuri. Nafikiri Mheshimiwa Mbunge akubaliane na mimi kwamba na kwa haraka utaratibu ukikamilika tutawahitaji tena vijana kwa sababu, yako manufaa makubwa sana kwa mafunzo ambayo yanatolewa kwa vijana kwa sababu, hawa vijana tunawaandaa, kuna mafunzo ambayo yanawasaidia pia kwenda kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kwamba, tutoe ushirikiano kwa Serikali, tutoe ushirikiano kwa Wizara kama wazazi. Kama anavyosema hata tulivyowarudisha tulizingatia kuona kwamba, vijana hawa wanarudi kwa kufuata utaratibu ambao tumeuweka. Tutaendelea kuona namna nzuri ya kuwasaidia vijana kupitia utaratibu ambao nilikuwa nimeutoa katika jibu langu la msingi.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri bado nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tumeona jitihada mbalimbali za wananchi wakizichukua kwa makusudi katika kupanda mikoko kwa lengo na madhumuni ya kuhifadhi mazingira, kuongeza mazalia ya samaki lakini kuzuia maji ya bahari kupanda nchi kavu. Mfano mzuri ni wananchi wa Kijiji cha Mjini Wingwi na Sizini Wilaya ya Micheweni. Swali la kwanza, je, Serikali inawapa matumaini gani wananchi hawa wa Mjini Wingwi na Sizini kwa kuwapatia misaada ya kifedha na vifaa kama boti kwa ajili ya patrol kama sehemu ya kuhamasisha na kuwapa moyo kuendelea na jitihada hizo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kufuatana nami baada ya Bunge hili mpaka kwenye Kijiji cha Mjini Wingwi na Sizini kwa lengo la kwenda kuona jitihada za wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu maswali haya, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Omar Issa kwa juhudi yake ya kutunza mazingira katika maeneo yake.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anauliza Serikali itawapa matumaini gani wananchi? Serikali kwa sababu inasikiliza na inathamini juhudi za wananchi, naomba hili tulichukue na baadaye tutakaa pamoja naye na wataalamu wetu tuone namna gani tunawapatia motisha wananchi ambao wanajitahidi kutunza mazingira.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili mimi niko tayari kabisa kufuatana naye baada ya Bunge hili kwenda kuona na kutafuta njia sahihi ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu, lakini pamoja na majibu mazuri nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengine Wabunge kutoka Zanzibar, pamoja na majukumu mengine tunatakiwa kuwaeleza wananchi wa Zanzibar juu ya umuhimu na faida za Muungano wetu. Kwa kujua hilo, je, Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haioni ipo haja ya kuwashirikisha Wabunge kutoka Zanzibar katika uibuaji wa vipaumbele vya miradi inayotokana na fedha za Muungano?

Pili, Mheshimiwa Waziri katika Mkutano wa Nne aliniahidi kwenda Jimboni kwangu kutembelea vijiji vya Mjini Wingwi na Sizini.

Je, ananiahidi ni lini tutakwenda kutekeleza ahadi hiyo?Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nikiri wazi kwamba kwa kweli Wabunge kutoka Zanzibar wamekuwa na kipaumbele sana cha kushughulikia changamoto za wananchi wa Zanzibar akiwemo ndugu yangu Omar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwamba niliahidi kwenda ni kweli, bahati nzuri nilishafika Zanzibar mpaka Jimbo la Nungwi, Jimbo la Amani na maeneo mengine, lakini nikuhakikishie kwamba ahadi yangu ya kufika katika eneo lako la kazi lipo pale pale tutaenda kuchapa kazi ondoa hofu katika hilo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kushirikisha Wabunge wa Zanzibar naomba niwashukuru, hata hii ajenda ukiangalia fedha za Covid, Wabunge wa Zanzibar mlileta fedha mahsusi hapa wakati mchakato wa barabara ulipokuwa ukifanyika ndiyo maana hata suala zima la fedha za Covid unaona kwamba zaidi ya shilingi bilioni 231 zimeenda upande wa Zanzibar lengo ni kuona kwamba hisia za Wabunge wa Zanzibar zimeonekana kuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba yale Wabunge wanayoyachangia humu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo lazima iwe shirikishi.

Mheshimiwa Spika, hiyo, hilo jambo ni zuri, tutaendelea kuboresha zaidi jinsi gani Wabunge watashiriki vizuri katika kuibua hoja mbalimbali. (Makofi)
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itamalizia na kukarabati ujenzi wa nyumba za polisi katika kituo cha polisi Wilaya ya Micheweni? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwisha jibu katika swali langu la msingi, Micheweni ambako kunahitajika pia ujenzi wa nyumba na kuboresha kituo ni miongoni mwa vituo ambavyo vitaimarishwa kulingana na mpango wetu wa kukarabati nyumba na vituo chakavu. Nashukuru. (Makofi)
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni nimeona baadhi ya wananchi wakifutwa kwenye mpango wakati bado hali zao ni mbaya sana, na naomba nimtaje mwananchi ambaye ni mfano, anaitwa Ndugu Hamad Faki Hamad maarufu Fofofo kutoka Shehia ya Mjini Wingwi, hali yake ni mbaya sana lakini amefutwa.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anatoa kauli gani kwa TASAF dhidi ya hali kama hizi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali inatoa kauli gani dhidi ya taarifa ambazo zinasambaa kwa wananchi ambazo zinaleta wasiwasi kwamba wanakwenda kufutwa kwenye mpango wakati hali zao bado ni mbaya. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya taarifa hizi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza yeye mwenyewe Mheshimiwa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kwa sababu pia ni mjumbe wa Kamati ya USEMI ambayo inasimamia Wizara yetu hii Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na amekuwa akifuatilia sana masuala haya ya TASAF hasa jimboni kwake kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikienda kwenye maswali yake anauliza ni vigezo gani ambavyo hata huyu amemtaja Mzee Hamad Faki vimemuacha. Sijui hasa kwenye kesi hiyo kama individual na nitakaa naye Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kujua kwa nini Mzee Faki alitoka katika mpango wa TASAF, tukitoka hapa nitakutana naye ili tuweze kulijua.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme jambo moja katika mradi huu awamu hii ya pili imekuwa ina component mbili; component ya kwanza ni ile ambayo tulikuwa tumeizoea kwenye awamu ya kwanza ya mradi huu wa TASAF, ni ule wa cash kwenda kwenye kaya hizi, lakini component ya pili ni public works. Kwamba kaya huenda ina watu watano, na mkuu wa kaya anaweza akawa ni mtu mzima labda ana miaka 70 lakini ndani ya kaya ile kuna watu wenye uwezo wa kufanya kazi. Basi watafanya kazi na kulipwa ujira kutoka kwenye mradi wa TASAF, kwenye miradi ile ambayo wameibua wao wenyewe katika maeneo yao husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, ya taarifa hizi kwamba wanufaika wanaenda kufutwa. Niseme taarifa hizi si za kweli, walengwa hawa hawaendi kufutwa, na tulifanya uhakiki kabla ya kuingia kwenye awamu ya pili ya mpango huu na kaya zimeongezwa. Serikali hii ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake mwenyewe alielekeza tuongeze idadi ya kaya kwenye mpango huu wa TASAF, na kaya zimeongezwa na hauendi kufutwa.
MHE. ISSA OMAR KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi, kwanza naomba nikumbushe tu kwamba kwa Zanzibar tunatumia Wadi siyo Kata. Kwa hiyo, hii ni Wadi ya Kiuyu.

Mheshimiwa Spika, naomba niulize swali moja la nyongeza kama ifuatanyo; ni miaka miwili sasa tumekuwa tukipata matumaini haya ya Serikali kwamba tutajengewa ofisi, lakini kiukweli hali ni mbaya. Kwa NIDA Micheweni wanatumia vyumba viwili walivyoazimwa na Wizara ya Afya ambapo vyumba hivyo viwili wanatumia Ofisi ya DRO, Ofisi ya Picha, store na jiko. Kwa kweli hali mbaya sana, hata ufanisi unakuwa ni mdogo sana.

Mheshimiwa Spika, tunaomba commitment ya Serikali; je, ni quarter gani ya mwaka wa fedha husika tutaanza kujengewa ofisi hii wananchi wa Wilaya ya Micheweni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kombo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kweli narekebisha, badala ya kuita Kata ya Kiuyu, ni Wadi ya Kiuyu, ahsante sana.

Kuhusu kuwapa matumaini na kwamba hali ya ofisi hizo ni mbaya sana, nakubaliana naye. Ndiyo maana tunasema katika mwaka 2023/2024 tutaweka fedha kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hii.

Mheshimiwa Spika, commitment ninayoitoa, ni kazi ndogo tu. Bunge lako tukufu likiidhinisha bajeti hii ambayo itakuwa imebeba pia dhima ya kujenga hizo ofisi 31, ni kwa uhakika kabisa jimbo lake litanufaika na ujenzi huo, ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kweli nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri. Kwa kweli ni matumaini yangu kwamba wananchi wa Micheweni watafarajika pindi watakaposikia majibu haya ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo nina swali moja la nyongeza. Mara nyingi imezoeleka katika Shirika la Posta wakati wanapotoa ajira wanachukua waajiriwa kutoka katika maeneo mengine. Je, Mheshimiwa Waziri ananihakikishiaje, pindi watakapofungua ofisi hii katika ajira ambazo watatoa watazingatia kipaumbele au wataweka kipaumbele kwa wananchi wa Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi ambayo anaifanya kwa ajili ya wananchi wa Wingwi. Lakini vilevile ameendelea kuhakikisha kwamba anatupatia changamoto zinazoendelea ndani ya jimbo lake. Sisi kama Serikali tunaendelea kuzipokea na kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini pili suala la ajira linafahamika kabisa kwamba mashirika yetu haya yanaajiri kwa kupitia utaratibu wa utumishi wa umma. Hivyo basi, tunaamini kabisa kwamba mfanyakazi yeyote, au yeyote ambaye ni Mtanzania ana haki sawa kuomba kazi na kupatiwa kazi kulingana na vigezo ambavyo vitakuwa vimewekwa.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina swali dogo tu la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni awamu ya pili hii kuambiwa tumetengewa fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hiki. Na kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba kwa kweli uchakavu ni wa hali mbaya sana. Tunaomba commitment ya Serikali; kama ni kweli kituo hiki kitajengwa kwenye bajeti ya mwaka unaokuja, ni quarter ipi wamepanga kufanya ukarabati wa kituo hiki?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, atakumbuka Mheshimiwa Kombo kwamba nilitembelea Kituo hiki cha Micheweni nikajionea hali halisi; na kwa msingi huo tukakubaliana ndani ya Wizara na Jeshi la Polisi kutenga fedha. Atakumbuka kwamba miaka iliyopita hata kama alipewa ahadi hakuna fedha iliyotengwa lakini mwaka ujao namhakikishia fedha imetengwa na tutahakikisha tutakapopata fedha za maendeleo basi kituo hiki tutakipa kipaumbele, nashukuru.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Hadi sasa katika Wilaya ya Micheweni hakuna nyumba za askari ambazo ujenzi unaendelea. Pamoja na hili sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kituo cha polisi Wilaya ya Micheweni ndiyo Makao Makuu ya Polisi Wilaya ya Micheweni. Je, Serikali ina mkakati gani wakujenga nyumba za polisi katika Wilaya ya Micheweni? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika kituo cha polisi cha Wilaya ya Micheweni kuna hanga la Jeshi la Polisi ambalo lilijengwa kutokana na nguvu za wananchi miaka kumi iliyopita hadi sasa hanga hili kutokana na kwamba halikumaliziwa tayari limeanza kuharibika ikiwemo paa kuvuja na saruji kuharika. Je, Serikali haioni haja kuunga mkono jitihada hizi za wananchi kwa kumalizia jengo hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati nimeusema ni kuendelea kutenga fedha kujenga nyumba za askari na maofisa kutegemea upatikanaji wake hata hivyo alichosema kwamba ujenzi umesimama kule Micheweni Mheshimiwa Mbunge ni kweli ndiyo maana kwenye jibu la msingi nimesema zinahitajika milioni 60 ili kumalizia jengo hilo na fedha hizi zinatengwa kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 kutoka Mfuko wa Tuzo na Tozo. Kwa hiyo, Mheshimiwa eneo hilo litakamilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uendelezaji wa ujenzi wa nyumba, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi tutaendelea kujenga nyumba za askari kadri tunavyopata pesa kwenye bajeti yetu au pale tunaposhirikiana na wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Waziri, swali la kwanza; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema kwamba uko mdaki mmoja utafungwa katika eneo la Azam Sea Link, tunataka kujua, ni lini mdaki huu utakwenda kufungwa ili kuondoa adha kwa wananchi wanaotumia eneo hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa vilevile Mheshimiwa Waziri amesema kwenye bajeti ya mwaka huu, wametenga fedha kwa ajili ya kununua midaki mingine. Je, ni midaki mingapi itakwenda kunuliwa kwa ajili ya eneo la Azam Sea Link ili kuendelea kuboresha eneo hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kuhusu lini, ni ndani ya Mwaka huu wa Fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu ni midaki mingapi itajengwa kwenye eneo hili ni kwamba hakuna mpango wa kuongeza kwenye eneo la Azam Link kwa sababu tayari umeshapatikana mmoja na kama kutakuwa na uhitaji tutakwenda kwenye maeneo mengine yenye uhitaji mkubwa.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa vile Waziri amekiri kwamba kituo hiki kutokana na uchakavu tayari kimeondoka; na tayari kutokana na mahitaji na eneo lile ni kubwa, kuna miradi mikubwa ya Serikali ambayo ipo sasa: -

a) Je, Serikali haioni haja ya kuweka kituo cha dharura katika eneo hili la Tumbe?

b) Je, Wizara iko tayari kwenda kukaa na ofisi ya mkuu wa wilaya pamoja na halmashauri kuangalia eneo kubwa au kupatiwa eneo ambalo litatosha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi, ni kweli kabisa kwamba eneo hili lina matumizi makubwa kwa kuwa pia kuna miradi mikubwa ambayo inahitaji kituo cha polisi. Lakini kituo cha polisi cha dharura kinaweza kikapatikana endapo tu mamlaka za halmashauri husika zitatenga jengo ambalo litakuwa na sifa ya kutumika kama kituo cha polisi.

Mheshimiwa Spika, suala la eneo; kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi, ni jukumu la halmashauri sasa kutafuta eneo ambalo tunakwenda kujenga kituo kipya. Na Wizara iko tayari kutoa ushirikiano kwa mamlaka za halmashauri hiyo ili kituo hicho kiweze kujengwa haraka sana.
MHE. OMAR ISSA. KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante je, ni lini Serikali itawajengea nyumba za kuishi Jeshi la Polisi Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kadri ambavyo tutapata fedha tutaendelea kuimarisha na kujenga Vituo vya Polisi na Makazi ya Askari. Kwa hiyo, Micheweni ni moja ya eneo litakalozingatiwa katika ujenzi wa nyumba za askari, ahsante. (Makofi)

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali ingawa hayaleti matumaini kwa wananchi wa Wilaya ya Micheweni, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na hali ya kituo kilivyo hali ni mbaya sana mpaka paa zake kuvunja. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka na wa dharura kukarabati Kituo hiki cha Micheweni?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili kuambatana na mimi mpaka Micheweni kwenda kujionea hali halisi ilivyo kwa sababu hanga hili la polisi limejengwa kwa nguvu za wananchi takribani miaka minane iliyopita na sasa hivi tayari limeanza kuvuja. Je, uko tayari kuambatana na mimi kwenda kujionea hali halisi ilivyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kombo kama ifuatavyo:-

Kwanza nakubaliana naye kwamba hali ni mbaya ndiyo maana tathmini yetu imefanyika na kubaini gharama zinazohitajika. Kwa kuwa bajeti ya mwaka huu imepita, naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika maeneo yatakayopewa vipaumbele katika mwaka ujao basi tutazingatia hili eneo pia la Micheweni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umuhimu wa kuambatana naye niko tayari na mara nyingi natekeleza ahadi baada ya Bunge hili tutapanga tuone lini kuweza kuitembelea Micheweni kubaini kiwango cha uharibifu na nakubaliana naye pamoja namna ya kutekeleza ukarabati huo, nakushukuru.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali ilifanya tathmini kwa kuzingatia vigezo hivi sambamba na mgawanyo wa fedha za majimbo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, tunashuhudia baadhi ya majimbo yakipata fedha kidogo ukizingatia kwamba vigezo alivyovieleza Mheshimiwa Waziri ni vikubwa zaidi ukilinganisha na Majimbo mengine na hata hali ya umaskini ni kubwa zaidi. Mfano mzuri ni Jimbo langu la Wingwi: Je, Serikali haioni iko haja ya kufanyia tathmini vigezo hivi, kwa kuzingatia sensa ya mwaka 2022? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ni kwamba Serikali inafanya tathmini ya vigezo hivi mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba vinakidhi uhitaji wa fedha za Mfuko wa Jimbo katika Majimbo yetu na pia kuona namna nzuri ya kuendelea kuboresha formula za hivi vigezo ili kuweza kutoa fedha kwa ajili ya maendeleo ya Mfuko wa Jimbo kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kufanya tathmini mara kwa mara, na mara itakapoona kuna maeneo ambayo vigezo vinahitaji kuongezwa au kupitiwa upya, basi suala hilo litafanyika.

Mheshimiwa Spika, pili, ni kweli kwamba fedha za Mfuko wa Jimbo zinatofautiana kutoka Jimbo moja na Jimbo lingine kwa kuzingatia vigezo hivi. Kama nilivyosema, asilimia 45 ya idadi ya watu katika Jimbo husika; kwa hiyo, Majimbo yenye idadi kubwa ya watu automatically yatakuwa na fedha nyingi zaidi, lakini kiwango cha umaskini kwa asilimia 20 pia na ukubwa wa eneo la kijiografia kwa asilimia 10, ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwenye majibu Serikali imesema itavifanyia tathimini vijiji vilivyobakia je ni lini tathimini hii itaanza?

Mheshimiwa Spika, vilevile asilimia kubwa ya wananchi wa Wilaya ya Micheweni hutumia mitandao ya simu ya halotel na tigo lakini huduma zake zimekuwa ni hafifu mitandao hii. Je, Serikali inachukua jitihada gani kuwaondolea usumbufu wananchi wa maeneo ya vijiji hivi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kombo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kipengele cha kwanza ni lini tutafanya tathimini? Tayari tumeishamaliza kufanya tathimini katika vijiji 2,116 na hivyo naelekeza timu ya wataalam kutoka Wizarani kwetu wakishirikiana na UCSAF waende wakafanye tathimini mara moja katika kata ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziomba.

Mheshimiwa Spika, kipengele cha pili ni cha kiufundi na kibiashara, pia ni cha kisheria, kwa sababu kinaangukia katika upande wa sheria kwa mujibu wa Sheria Namba 12 ya Mwaka 2003, na kwa kanuni zetu za mwaka 2018 inampatia TCRA mamlaka ya kuhakikisha kwamba inaangalia ubora wa huduma ya mawasiliano. Hivyo, basi nitumie fursa hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri kuwaelekeza TCRA kwenda kufanya tathmini na kujiridhisha na quality of service katika maeneo hayo ili tujue ni hatua gani tunazichukua kulingana na majibu ambayo watayaleta, nakushukuru.
MHE. OMARI ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. changamoto iliyopo kwenye Jimbo la Kilolo, ni sawa na changamoto iliyopo Mkoa wa Kaskazini Pemba, juu ya usikivu wa TBC. Je, Serikali inatoa kauli gani kuwatolea wananchi changamoto hii, ukizingatia TBC ni Redio ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kupokea changamoto ya Mheshimiwa Mbunge ili Serikali tukaifanyie kazi na baada ya hapo tutamshirikisha Mheshimiwa Mbunge ili atupatie ushirikiano specific katika maeneo ambayo ameyataja. Nakushukuru.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini kabla sijauliza naomba kusahihisha, ni Mkoa wa Kaskazini Pemba, Wilaya ya Micheweni, siyo Mkoa wa Kaskazini Unguja. Sasa, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza Sheria mbalimbali ambazo zinakata kodi kwa Mfuko huu wa Majimbo kwa upande wa Zanzibar, ikiwemo upande wa Jamhuri na ile ya upande wa Serikali ya Zanzibar. Je, Serikali zote mbili hazioni haja ya kukaa pamoja na kuona namna ya kupunguza au kuondoa kabisa kodi hizi kwa ukizingatia kwamba, mifuko hii inakwenda kuwahudumia wananchi moja kwa moja?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Serikali haioni haja ya kutoa maelekezo kwa Halmashauri za Zanzibar kwamba, wasitumie fedha hizi kama vyanzo vyao vingine vya mapato ya halmashauri kwa vile fedha hizi vilevile zinawahudumia wananchi wa Zanzibar kwenye majimbo yetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kombo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka Waheshimiwa Wabunge wote wafahamu kwamba, makato ya fedha hizi yapo kisheria, yanakatwa kwa mujibu wa Sheria. Maana yake ni kwamba, uwepo wa hizi kodi ni kwa sababu, Sheria zipo na zinawaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri, wa Majiji, wa Mabaraza ya Miji kwamba, fedha hizi zinazotumika kununua vifaa kwa ajili ya Mfuko wa Jimbo ni lazima zikatwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli fedha hizi ni kidogo, lakini zinatumika kwenye miradi ya jamii, mahitaji ya fedha hizi ni mengi uki-compare na zinazotoka. Waheshimiwa Wabunge, ni lazima tukubaliane kwamba, fedha hizi ni lazima zikatwe kodi, ili halmashauri zetu ziweze kupata kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ninachotaka kuwaambia Waheshimiwa, ni tumefanya vikao mara kadhaa na Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmashauri, wa Majiji, wa Mabaraza ya Miji na taasisi zinazokusanya fedha, zikiwemo ZRA na ZRB, lengo na madhumuni ni kuona namna ambavyo tunawaelimisha Waheshimiwa Wabunge na wengine ili waweze kufahamu hilo.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, mweleze kwa kifupi.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama alivyoshauri basi tutalichukua na kwenda kuyafanyia kazi yale ambayo ameshauri.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni kazi gani zimefanyika kwenye shilingi 1,250,000,000 ambazo Serikali imepeleka kwenye Wilaya ya Micheweni kama jibu la msingi la Mheshimiwa Naibu Waziri linavyosema?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu, pengine Mheshimiwa Mbunge hajasikia vizuri, ni kwamba katika mwaka wa fedha huu wa 2023/2024 baada ya kusaini mkataba huu sasa, itaanza kazi ya ujenzi wa nyumba za makazi za askari hawa wa Uhamiaji. Kwa hiyo, kiasi hicho kilichotengwa cha shilingi 1,250,000,000 kitaanza utekelezaji wake mara baada ya kusaini mkataba.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri ambayo kwa kweli yamekuwa ni majibu ya kufanana siku zote na wala hayaleti matumaini kwa Wabunge wote kutoka Zanzibar, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali mmekiri kwamba changamoto ni sheria na sisi ndio watunga sheria: Ni lini mtaleta Muswada hapa Bungeni ili kubadilisha sheria hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba Mfuko huu unakatwa tozo kwa sheria mbili; Sheria ya Zanzibar na Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania: Je, hamuoni haja ya kukaa pamoja ili kuangalia ni namna gani ya kutatua changamoto hii ili iweze kukatwa tozo kwa upande mmoja tu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar Issa Kombo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimwambie tu kwamba awe na matumaini kwa sababu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, inafuata kabisa misingi ya Mwanafalsafa Bentham, mtaalamu wa sheria aliyesema, “Laws should provide minimum pain and provide maximum pleasure.” Kwa msingi huo ni kwamba, sheria hizi zilizotungwa siyo Msahafu wala Biblia Takatifu. Zinaweza kubadilishwa kulingana na mahitaji yaliyopo, lakini pia kutatua changamoto ambazo zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa lugha ya Kilatini wanasema, “Ubi societas, ibi jus, ibi ius ubi societas” kwa maana ya kwamba sheria ni zao la jamii na jamii ndiyo inayozaa sheria. Sasa Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ameleta hoja hii ndani ya Bunge na utakumbuka vizuri katika Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mheshimiwa Waziri alijibu hapa na akaeleza kwamba suala hilo walilitolea ufafanuzi. Pia, akasema Serikali iko tayari kukaa na wataalamu kwa upande wa Zanzibar, kukaa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar; ZRA, TRA na Ofisi yetu ya Wizara ya Fedha ili kuweza kuangalia ni sehemu gani wanaweza wakarekebisha na kuhakikisha kwamba pande hizi zote wanapata nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mwisho wa siku fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ni kwa ajili ya maendeleo ya mwananchi. Pia kodi inayokatwa ni kwa ajili ya maendeleo ya mwananchi na nchi kwa ujumla. Kwa hiyo, hivi vyote kwa pamoja tutaweza kuviangalia. Nimtoe wasiwasi kwamba Serikali iko makini na tutalishughulikia ili kuweza kuhakikisha tuna-provide maximum pleasure na tunaondoa hizo minimum pain, ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naipongeza Serikali kwa majibu, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Ilani imeelekeza kwamba ununuzi wa meli hizi ni kwa kuzingatia pande mbili za Muungano na Mheshimiwa Waziri amesema kuna mchakato wa ununuzi wa meli mbili.

Je, Zanzibar inakwenda kunufaika vipi kutokana na ununuzi wa meli hizo mbili za awali?

Swali la pili, je, kuna ushirikiano gani kati ya ZAFICO na TAFICO katika ununuzi wa meli hizo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na hili la kwanza, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua Zanzibar inanufaika vipi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi meli ziko nane na meli hizi zimegawanywa katika pande zote mbili, Bara meli nne na Zanzibar meli nne. Kama nilivyosema kupitia TAFICO tayari meli mbili zabuni zimeshatangazwa na kwa bahati nzuri sana kule Zanzibar tayari wao walishafika mbali zaidi kwenye mchakato wa manunuzi wa meli hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kupitia taratibu za kimanunuzi Zanzibar wao wanaendelea na utaratibu wao na kwa sababu tulishagawana meli hizi na huku Bara nao wanaendelea na utaratibu wao. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba meli hizi zitakaponunuliwa pande zote mbili zitanufaika na manunuzi ya meli hizi na kila kitu kitakwenda sawa sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uhusiano kati ya ZAFICO na TAFICO, mashirika haya ni ya umma, yanashirikiana katika kubadilishana utaalam, kufanya utafiti na mambo mengine, lakini kazi kwa maana ya kazi hizi za uvuvi na shughuli zote zinazohusiana na masuala ya uvuvi ushirikiano wa mashirika haya ni mkubwa na wanashirikiana kwa karibu sana, ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo; nimeona mikakati ya Serikali na ni mizuri, lakini sijaona mkakati wa kuishirikisha jamii yenyewe katika ulinzi dhidi ya vitendo vya udhalilishaji. Sasa, je, Serikali haioni haja ya kuishirikisha jamii moja kwa moja katika ulinzi dhidi ya vitendo hivi kama ambavyo wanafanya wenzetu wa Jeshi la Polisi katika dhana ya ulinzi shirikishi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa, vitendo hivi kwenye jamii vinatokea mara nyingi, Watanzania wenzetu wanapoteza Maisha. Je, Serikali haioni haja ya kushirikiana na viongozi wa dini katika kuwapa elimu wananchi kwa sababu, vitendo vinasababishwa na mmong’onyoko wa maadili vilevile na hofu ya wananchi kupoteza hofu ya Mungu na wanaojenga hofu ya Mungu na maadili ni viongozi wetu wa dini, sasa Serikali haioni haja ya kushirikisha viongozi wa dini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo. Swali lake la kwanza, Serikali imekuwa ikishirikiana na jamii katika kutekeleza afua za ulinzi na usalama katika jamii. Ndiyo maana Kamati zetu zinaanzia katika vijiji, Mwenyekiti wa Kijiji hadi Taifa, ili kuhakikisha kuwapa elimu ya ulinzi na usalama kwa jamii, ili wananchi wawe na uelewa kuhakikisha kwamba, usalama katika nchi unakuwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Wizara inashirikiana na viongozi wa dini katika kutekeleza Mpango wa Pili, MTAKUWWA, ambao viongozi wa dini wamo katika Kamati ya Ulinzi na Usalama. Kamati hiyo inaanzia Vijijini hadi Taifa kuhakikisha Mpango wa Pili wa Taifa wa MTAKUWWA unakamilisha Sheria na hatua zake na viongozi wa dini kuhakikisha kwamba, wanatoa miongozo na makongamano katika jamii, kutoa elimu ya kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na migogoro ya msongo wa mawazo. Ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni muda gani wa mwisho ulifanyika upembuzi yakinifu kwa benki hizi katika Wilaya yetu ya Micheweni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, kuna maombi yoyote ya ufunguzi wa matawi mapya ya benki katika Wilaya yetu ya Micheweni yaliyopelekwa, ukizingatia kazi kubwa ya maeneo ya uwekezaji inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ally Mwinyi katika Wilaya yetu ya Micheweni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar Issa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kujibu ninaomba kumpongeza sana yeye pamoja na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Micheweni kwa namna wanavyopambana ili huduma za kibenki kupatikana ndani ya Wilaya ya Micheweni hasa makao makuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba uridhie nijibu maswali yote mawili kwa pamoja kuwa hadi sasa bado Serikali haijapokea maombi kwa Benki za NMB na CRDB kufungua tawi jipya pale makao makuu ya Wilaya ya Micheweni, lakini kutokana na uwekezaji ambao umewekwa na Serikali ya Awamu ya Nane, inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi katika Wilaya ya Micheweni, mfano, kama ujenzi wa bandari mpya ya kisasa na viwanda mbalimbali na ni eneo husika la uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba benki zetu za NMB na CRDB na benki nyingine, waende kuangalia fursa hii na wafanye upembuzi yakinifu kwa ajili ya kufungua tawi katika makao makuu ya Wilaya ya Micheweni. (Makofi)
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itafanyia ukarabati Kituo cha Polisi Wilaya ya Micheweni wakati ni mara nyingi wametuahidi, lakini bado mpaka leo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Kombo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ni kukarabati vituo vyote vya Polisi ambavyo ni chakavu na kujenga vipya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kituo chake hicho alichokitaja kipo kwenye mpango na tayari tumefanya ukarabati ili wananchi wetu waweze kuhudumiwa kwa maana ya usalama wa raia na mali zao katika eneo lake. Ahsante sana. (Makofi)