Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Soud Mohammed Jumah (21 total)

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH Aliuliza: -

Je, ni fedha kiasi gani Tanzania imeomba na kupatiwa kutoka katika mfuko wa fedha za kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kwa kuwa, ndio mara yangu ya kwanza kusimama kwenye Bunge lako tukufu naomba kwa kibali chako niruhusu niseme angalau maneno mawili kabla ya kwenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, la kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na uzima, lakini la pili nashukuru sana Chama Cha Mapinduzi, chama changu kuendelea kunianimi na kunipa dhamana hata kuniruhusu kwenda kugombea kwenye Jimbo la Tarime Vijijini, lakini pia nawashukuru sana wapiga kura wa Tarime Vijijini, Kanda Maalum kule Tarime Mara kwa kunipa ridhaa hii na hatimaye ahadi yangu ambayo nilitoa mbele yako imetimia. Lakini mwisho lakini sio kwa umuhimu namshukuru sana Mheshimiwa Rais kuendelea kuniamini kuniteua kama Naibu Waziri. Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya maelezo hayo mafupi ninaomba kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, nijibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeomba na kupokea fedha kiasi cha dola za Marekani 8,488,564 kutoka katika Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi. Fedha kutoka Mfuko huo huombwa kwa kuandaa miradi inayokidhi vigezo vilivyokubalika. Fedha huombwa kupitia taasisi ya utekelezaji ya kitaifa au kimataifa, fedha hizo husajiliwa na Bodi ya Mfuko huo. Kwa Tanzania taasisi ya kitaifa iliyosajiliwa na Mfuko huo ni Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambao walipata ithibati ya Mfuko huo Oktoba, 2017.

Mheshimiwa Spika, hadi sasa miradi ifuatayo imeomba na kupata fedha kutoka mfuko huo wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi kwa ajili ya utekelezaji hapa nchini.

Mradi wa kwanza ni Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Mkoa wa Dar es Salaam. Gharama za mradi huo ni dola za Marekani 5,008,564. Mradi ulitekelezwa mwaka 2013 hadi 2019 na Fedha zilizotolewa kupitia UNEP. Kazi zilizofanyika ni ujenzi wa ukuta wa kukinga maji ya bahari Kigamboni na Barabara ya Barrack Obama na ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua Ilala na Temeke na kupanda mikoko maeneo ya Mbweni na Kigamboni, Dar es Salaam.

Mradi wa pili ni Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa jamii za pwani ya Zanzibar. Gharama za mradi huo ni dola za Kimarekani 1,000,000. Mradi uliidhinishwa na Bodi ya AF na kiasi cha dola za Marekani 30,000 kilitolewa kwa ajili ya kuandika andiko la mradi. Fedha zitatolewa kupitia NEMC ambayo iliwasilisha kwa mtekelezaji wa mradi huo ambaye ni Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar. Aidha, andiko la mradi liliidhinishwa na sasa taratibu za kusaini mkataba kati ya NEMC na Mfuko wa Adaption Fund zinaendelea chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Mradi wa tatu ni Mradi wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi kwa Jamii za Wakulima na Wafugaji Wilaya ya Kongwa. Gharama za mradi ni dola za Marekani 1,200,000. Mradi umeidhinishwa na Bodi ya AF na kiasi cha dola za Marekani 30,000 kimetolewa kwa ajili ya kuandika andiko la mradi. Fedha zitatolewa NEMC na kuwasilishwa kwa mtekelezaji ambaye ni NGO ya Foundation for Energy Climate and Environment.

Mradi wa nne ni Mradi wa Kimkakati wa Teknolojia ya Kuvuna Maji Kuimarisha Uwezo wa Jamii za Vijijini katika Maeneo Kame ya Mikoa ya Singida, Tabora na Dodoma. Gharama za mradi ni dola za Marekani 1,280,000. Mradi umeidhinishwa na Bodi ya AF na kiasi cha dola za Marekani 30,000 kimetolewa kwa ajili ya kuandika andiko la mradi.

Mradi wa mwisho na wa tano ni Mradi wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi wilaya ya Bunda. Gharama za mradi n dola za Marekani 1,400,000. Mradi huu bado haujaidhinishwa na Bodi ya EF, lakini kiasi cha dola za Marekani 30,000 kimetolewa kwa ajili ya kuandika andiko la mradi. Naomba kuwasilisha.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuiwezesha Mifuko ya Kuendeleza Utalii na Wanyamapori na kufikia lengo la watalii milioni tano ifikapo 2025?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Tozo ya Maendeleo ya Utalii (TDL) ulianzishwa kwa Sheria ya Utalii Na. 29 ya Mwaka 2008, Kifungu cha 59(2). Lengo la Tozo hiyo ni kuendeleza mazao ya utalii; kudhibiti ubora wa huduma za biashara za utalii; kukuza na kutangaza vivutio vya utalii; kujenga uwezo katika sekta ya utalii; na kuwezesha tafiti na shughuli nyingine yoyote kwa ajili ya maendeleo na kuboresha sekta ya utalii.
Kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2020, vyanzo vya tozo hii kwa sasa vinakusanywa na Wizara kwa kushirikiana na TRA na makusanyo hayo huingizwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa wanyamapori, upo Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania ambao ulianzishwa kwa Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura 283, Kifungu cha 91(2). Mfuko huo unawezesha shughuli za kuhifadhi wanyamapori ndani na nje ya maeneo ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wanyamapori wanaendelea kulindwa na kusimamiwa kwa ajili ya kuendeleza utalii nchini, mifuko ya utalii na wanyamapori imekuwa ikiwezeshwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Pamoja na vyanzo vya mapato vya mifuko hii kukusanywa na kupelekwa kwenye Mfuko Mkuu (Hazina), Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imetenga fedha kupitia bajeti kuu ya Serikali kwa ajili ya kutekeleza kazi za mifuko husika. Hivyo, kazi zilizokuwa zinafanywa na mifuko hii sasa zitatekelezwa kupitia bajeti kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza:-

Je, Serikali itawasaidiaje Wafanyabiashara wa Dagaa wanaofuata Masoko nchi jirani ambao hutozwa ushuru Zanzibar na Tunduma kwa upande wa Tanzania Bara?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mazao ya uvuvi yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi au yanayoingizwa nchini kwa upande wa Tanzania Bara yanalipishwa ushuru stahiki wa Serikali kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Uvuvi pamoja na Sheria nyingine za Nchi. Aidha, dagaa wanaotoka Zanzibar kwenda nchi jirani kupitia mpaka wa Tunduma hawalipishwi ushuru wowote katika Bandari ya Dar es Salaam na wanapokuwa wamefikishwa Tunduma kuelekea nchi jirani.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeweka Maafisa katika Bandari ya Dar es Salaam na maeneo ya mipakani kwa ajili ya kudhibiti utoroshaji na biashara haramu ya mazao ya uvuvi nchini. Hata hivyo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuona umuhimu wa kulinda na kuendeleza rasilimali za uvuvi, itakutana na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuangalia namna bora ya kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani katika kutatua changamoto zinazohusu masuala ya uvuvi.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, Taasisis ngapi zimeweza kujisajili hadi sasa na Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) nchini, na miradi mingapi imeshaombewa kupitiwa mfuko huo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira). Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge Jimbo la Donge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) ulianzishwa mwaka 2010 na kuanza kufanya kazi mwaka 2015. Taasisi inayotaka kuomba fedha kutoka katika Mfuko huu, ni lazima iwe imesajiliwa au kupata ithibati chini ya Mfuko huu. Ithibati au usajili hutolewa baada ya taasisi husika kutimiza vigezo stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko wa mabadiliko ya Tabianchi unaruhusu taasisi za kitaifa, kikanda na kimataifa, kusajiliwa ili kuweza kuomba fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya mabadiliko ya tabianchi. Hadi kufikia mwezi Machi 2021, mfuko huu ulikuwa umesajili jumla ya taaisis 74 ulimwenguni kote. Hapa nchini, taasisi iliyopata usajili ni moja tu, ambayo ni Benki ya CRDB. Tunaipongeza Benki ya CRDB kwa kuweza kupata ithibati ya mfuko huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa usajili wa taasisi katika mfuko huu wa mabadiliko ya Tabianchi hauna ukomo. Serikali inaendelea kuhamasisha taasisi nyingine za hapa nchini kujisajili na mfuko huu, ili kuwa na uwezo wa kupata fedha na kutekeleza miradi mbalimbali ya mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi, hadi sasa jumla ya miradi sita imeombewa fedha kutoka Mfuko huu kupitia taasisi mbalimbali. Hata hivyo, ni miradi miwili tu ambayo fedha yake imeidhinishwa. Miradi hiyo ni Pamoja na mradi wa Maji kwa Kuwezesha uhimili katika Mkoa wa Simiyu (Dola za Marekani millioni 120), na mradi wa pili, ni mradi wa kuandaa Uwezo wa CRDB (Dola za Marekani 560,000) ahsante.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani ya kupunguza au kuondosha kabisa wizi wa mazao ya kilimo na mifugo katika maeneo ya Unguja na Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Donge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi nchini ndilo lenye jukumu la kulinda maisha na mali za wananchi na linatambua suala la uhalifu na wizi wa mifugo na wizi wa mazao ya kilimo unaosumbua wananchi wa Zanzibar, katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Septemba 2021 jumla ya matukio 72 ya wizi wa mifugo na 85 ya wizi wa mazao umeripotiwa katika vituo vya Polisi. Watuhumiwa 48 wa wizi wa mifugo na 52 wa wizi mazao wamekamatwa na kesi 22 za wizi wa mifugo na 36 za wizi wa mazao zinaendelea mahakamani na ziko kwenye hatua mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuanzisha na kushiriki kwenye vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuzuia uhalifu na Jeshi la Polisi litaendelea kufanya doria kwenye maeneo yote ili kudhibiti na kutokomeza uhalifu hapa nchini. Nakushukuru.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha usajili wa Taasisi ya NEMC katika Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Green Climate Fund (GCF) ili kuipatia nchi fursa za fedha za mabadiliko ya tabianchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa wananchi wa Jimbo la Donge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ni Ofisi kiungo ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi Kitaifa ililiteua Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili liweze kuanza mchakato wa kupata Ithibati na kuwa mratibu wa fedha za Mfuko wa GCF.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Mei, 2021, NEMC iliwasilisha maombi rasmi kulingana na taratibu na baada ya GCF kujiridhisha mwezi Julai, 2021 walitoa invoice kwa ajili ya kulipa ada ya kufanyiwa Ithibati. Ada hiyo imelipwa mwezi Agosti, 2021 na hivi sasa GCF kwa barua ya tarehe 10 Januari, 2022 wameiarifu NEMC kwamba maombi yao yanafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kwa sasa suala hili liko GCF, naomba tuwe na subira wakati GCF wanaendelea na taratibu zao za mapitio. Aidha, nitoe wito kwa taasisi zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuata taratibu ili ziweze kupata ithibati kwenye Mfuko huo wa Green Climate Fund. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, kuna mpango gani kuboresha The National Herbarium of Tanzania Arusha ili
kuimarisha huduma za utafiti na uhifadhi wa Mimea nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, The National Herbarium of Tanzania ilianzishwa kwa Sheria ya TPRI ya Mwaka 1979. Ili kuimarisha utendaji wa Taasisi za Wizara, Serikali imeunda Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) iliyoanzishwa kwa Sheria Na. 04 ya Mwaka 2020 kwa kuunganisha Sehemu ya Afya ya Mimea iliyokuwa chini ya Wizara ya Kilimo na Mamlaka ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kitropiki (TPRI).

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha The National Herbarium of Tanzania na kuimarisha Huduma za Utafiti na Uhifadhi wa Mimea, Serikali imepanga kuendeleza kuimarisha kanzidata ya mimea ya Tanzania inayohifadhi sampuli kavu ndani ya National Herbarium of Tanzania (NHT) pale Arusha, Mweka, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine na TAFORI. Aidha, Serikali kupitia TPHPA inaendelea Kuorodhesha, kukusanya na kutambua sampuli za mimea katika misitu ya hifadhi nne ambazo ni Mlima Hanang, Chenene, Salanga na Chemichemi, katika mikoa ya Manyara na Dodoma.
MHE. MOHAMED JUMAH SOUD aliuliza: -

Je, Kampeni ya AFR 100 imetekelezwa kwa kiasi gani na maendeleo gani yamefikiwa hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Jumah Soud, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara imefikia hatua zifuatazo katika utekelezaji wa Kampeni ya AFR 100: kuondoa wavamizi na kurejesha ardhi iliyoathiriwa; Kuimarisha usimamizi wa misitu ya mikoko; Kutoa elimu ya kudhibiti moto wa msituni ili kulinda uoto wa asili; na Kutekeleza Mpango wa Dodoma ya Kijani.

Mheshimiwa Spika, maendeleo yaliyofikiwa ni pamoja na kusainiwa kwa makubaliano ya Kurejesha Mandhari ya Kiafrika – (AFR 100) na Mbinu ya Tathmini ya Fursa ya Marejesho. Aidha, Tanzania imefanikiwa kuandaa na kukamilisha Mkakati wa Kitaifa wa Kurejesha Mandhari ya Misitu. Mkakati huu unatarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano wa Nchi Wanachama wa kujadili masuala ya Mazingira (COP 27).
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuanzisha mfuko wa mabadiliko ya tabianchi kusaidia kupambana na athari za mabadiliko ya Tabianchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge na mtumishi wa wananchi wa Jimbo la Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa uwepo wa vyanzo vya fedha vya uhakika ili kuimarisha jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kufuatia kupitishwa kwa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021, Serikali kwa sasa inafanya mapitio ya Sheria ya Mazingira, Sura ya 191 ikiwemo taratibu za kuanzisha Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira. Mfuko huu ukianzishwa, pamoja na mambo mengine utazingatia ufadhili wa shughuli za mabadiliko ya tabianchi nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, Serikali inatumia vigezo gani kuanzisha vituo vya polisi katika maeneo ambayo idadi ya watu na vitendo vya uhalifu vinaongezeka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohammed Jumah Soud, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vigezo vinavyotumika kuanzisha vituo vya polisi ni ongezeko la watu, ongezeko la matukio ya uhalifu, umbali kati ya kituo kimoja cha polisi na kingine, uwepo wa miundombinu ya Serikali, shughuli za kibiashara pamoja na maeneo ya kimkakati kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi, likini pia uwezo wa kibajeti na utayari wa wananchi na mamlaka zao za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, nia ya uanzishwaji wa kituo cha polisi huwasilishwa kwenye Kamati ya Usalama ya Wilaya. Kikao kikiridhia, hoja hupelekwa kwenye Kamati ya Usalama ya Mkoa, kisha ushauri wao huwasilishwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya utekelezaji ikiwa ni pamoja na mipango ya ujenzi, kupeleka Askari na vitendea kazi. Nashukuru.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza ajali zinazosababishwa na magari ya mchanga Wilaya ya Kaskazini B - Unguja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la Kaskazini A na B – Unguja ajali zilizotokea kuanzia Januari, 2021 hadi Desemba, 2021 ni tatu ambazo zimesababisha vifo vya watu wanne na majeruhi mmoja. Ajali zilizotokea kuanzia Januari, 2022 hadi Machi, 2023 ni moja na imesababisha kifo cha mtu mmoja. Kwa jumla kesi zilizofikishwa mahakamani ni nne na zilizopata hukumu ni tatu na kesi moja inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajali zinazosababishwa na magari ya kubeba mchanga zimeendelea kupungua kutokana na Serikali kuweka alama za matumizi ya barabara, kuweka Kituo cha Ukaguzi wa Magari, kukagua leseni za madereva, kuweka utaratibu wa kupima macho na kutoa elimu ya matumizi bora na sahihi ya barabara kwa watumiaji wote, nashukuru.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, kuna mikakati gani ya kudhibiti mifugo katika Bonde la Ihefu na Mto Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Jimbo la Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Oktoba, 2022 Serikali kupitia Kamati ya Mawaziri Nane wa Kisekta inayoshughulikia migogoro ya ardhi katika vijiji 975 nchini, ilitoa tamko kuhusu utatuzi wa mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Taifa Ruaha na baadhi ya vijiji vya Wilaya za Mbarali na Chunya. Ili kudhibiti mifugo katika Bonde la Ihefu na Mto Kilombero, jumla ya vijiji 16 vimeandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji na kutenga maeneo kwa ajili ya malisho ili kuwezesha ufugaji katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kudhibiti mifugo kutoka katika maeneo mengine kwenda kwenye Bonde la Mto Kilombero kutafuta malisho na maji katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali inajenga mabwawa ya maji kwa ajili ya mifugo katika Halmashauri za Morogoro DC Kijiji cha Kongwa na Kibaha DC Kijiji cha Viyenze. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imeanzisha mashamba darasa 100 ya malisho katika Halmashauri 44 zikiwemo Halmashauri zinazopakana na Bonde la Ihefu na Mto Kilombero ili wafugaji waweze kujifunza kuzalisha malisho na hivyo kutulia katika maeneo yao ya ufugaji.
MHE. MOHAMED JUMAH SOUD aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kupunguza upoteaji wa Uoto wa Asili nchini unaosababisha kupoteza hadhi kwa Hifadhi na Mapori ya Akiba?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Jumah Soud, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kubwa ya kupotea kwa uoto wa asili katika Hifadhi na Mapori ya akiba ni ongezeko la mimea vamizi katika maeneo hayo. Mimea hiyo husababisha mabadiliko ya aina ya mimea katika maeneo yaliyohifadhiwa kwa kutoa fursa kwa mimea isiyoliwa na wanyamapori kustawi zaidi, kuongezeka na kupunguza uoto wa asili ambao ni tegemeo la wanyamapori. Hadi sasa, tafiti zimebaini aina 47 za mimea vamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa. Sababu zinazopelekea kushamiri kwa mimea vamizi ni pamoja na uingizaji wa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa, mabadiliko ya tabianchi, shughuli za binadamu na viumbepori wahamao.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jitihada za kudhibiti mimea vamizi, Wizara kupitia Taasisi za uhifadhi inatekeleza mkakati wa kukabiliana na mimea vamizi katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kuondoa kwa kung’oa mimea husika katika hifadhi. Aidha, mikakati mingine ni kuimarisha ulinzi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa kudhibiti shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na uingizwaji wa mifugo hifadhini sambamba na kuwekeza zaidi katika utafiti ili kupata suluhisho la kudumu.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, kwa miaka mitano iliyopita, Tanzania ilipata kiasi gani kutoka katika Mfuko wa Fedha za Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa (LDCF) ?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge Wa Donge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi sasa imeweza kutekeleza miradi minne ambayo inatekelezwa pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Fedha tulizo pokea ndani ya miaka mitano kutoka Mfuko wa Nchi Zinazoendelea (Least Development Countries Climate Fund-LDCF) ni Kiasi cha Dola za Marekani Milioni 19,343,743.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa za miradi yote minne kwa kina inapatikana katika tovuti ya Ofisi ya Makamu wa Rais www.vpo.go.tz.
Aidha, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kutafuta fedha zaidi kutoka kwenye Mfuko wa LDCF ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kadri fursa zinapopatikana kwa pande mbili za Muungano wetu.
MHE. MOHAMED JUMAH SOUD aliuliza: -

Je, ni vigezo gani hutumika kuanzisha Vituo vya Polisi maeneo yenye idadi kubwa ya watu pamoja na vitendo vya uhalifu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Jumah Soud, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vinavyotumika kuanzisha Vituo vya Polisi ni ongezeko la watu, ongezeko la matukio ya uhalifu, umbali kati ya Kituo kimoja cha Polisi na kingine, uwepo wa miundombinu ya Serikali, shughuli za kibiashara pamoja na maeneo ya kimkakati kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi, uwezo wa kibajeti na utayari wa wananchi na Mamlaka zao za Serikali za Mitaa ni vigezo vingine tunavyovitumia. Hatua inayofuata ni mapendekezo ya uanzishwaji wa kituo husika kuwasilishwa kwenye Kamati ya Usalama ya Wilaya, Kamati ya Usalama ya Mkoa na kisha ushauri wao huwasilishwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya utekelezaji. Nashukuru.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, utaratibu gani unaotumika kwa Kamandi mbalimbali nchini kuanzisha miradi ya kibiashara katika maeneo ya Kamandi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Jumah Soud, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, uendeshaji wa miradi ya kibiashara Jeshini ulianzishwa kupitia Mess and Institutes ambayo ilikua na jukumu la kusimamia mabwalo (Mess) ambayo yalikuwa yanauza vinywaji na kuendesha maduka katika vikosi vya Jeshi. Baadaye utaratibu huo ulifanyiwa maboresho kadhaa yaliyopelekea kubuni na kuendesha miradi ya kibiashara Jeshini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu wa sasa Kamandi, Brigedi, Vikosi na Shule zinapaswa kubuni na kuandaa andiko la mradi au biashara na kuwasilisha Makao Makuu ya Jeshi kwa ajili ya kibali. Makao Makuu ya Jeshi huchambua maandiko yaliyowasilishwa kujiridhisha endapo mradi au biashara hizo, hazitaathiri majukumu ya msingi ya Jeshi. Aidha, miradi hiyo huzingatia taratibu za uhifadhi wa mazingira, taratibu za usajili BRELA na taratibu za Mamlaka ya Mapato Nchini.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani wa kupunguza athari hasi zitakazojitokeza kutokana na kuondolewa kwa buffer zone katika hifadhi na mapori?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maeneo ya kinga za hifadhi za wanyamapori husaidia wanyamapori kupata mahitaji yao ikiwemo malisho na hivyo kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori.

Mheshimiwa Spika, katika kupunguza athari za kutokuwa na maeneo ya kinga, Wizara kupitia taasisi zake za uhifadhi (TANAPA, TAWA na NCAA) inatoa elimu kwa wananchi kuhusu kutokuanzisha shughuli za kibinadamu kama vile kilimo na makazi kwenye maeneo ya karibu na hifadhi ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori.

Vilevile kuwaelimisha kuanzisha shughuli rafiki kama vile ufugaji nyuki kwenye maeneo hayo. Sambamba na hatua hiyo, jitihada za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu zinafanyika ili kulinda wananchi na mali zao.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, utaratibu gani unaotumika kwa Kamandi mbalimbali nchini kuanzisha miradi ya kibiashara katika maeneo ya Kamandi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Jumah Soud, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, uendeshaji wa miradi ya kibiashara Jeshini ulianzishwa kupitia Mess and Institutes ambayo ilikua na jukumu la kusimamia mabwalo (Mess) ambayo yalikuwa yanauza vinywaji na kuendesha maduka katika vikosi vya Jeshi. Baadaye utaratibu huo ulifanyiwa maboresho kadhaa yaliyopelekea kubuni na kuendesha miradi ya kibiashara Jeshini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu wa sasa Kamandi, Brigedi, Vikosi na Shule zinapaswa kubuni na kuandaa andiko la mradi au biashara na kuwasilisha Makao Makuu ya Jeshi kwa ajili ya kibali. Makao Makuu ya Jeshi huchambua maandiko yaliyowasilishwa kujiridhisha endapo mradi au biashara hizo, hazitaathiri majukumu ya msingi ya Jeshi. Aidha, miradi hiyo huzingatia taratibu za uhifadhi wa mazingira, taratibu za usajili BRELA na taratibu za Mamlaka ya Mapato Nchini.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani kuimarisha shughuli za TCU Zanzibar ili kupunguza usumbufu kwa wadau wa elimu Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) inatekeleza majukumu yake yote katika pande zote mbili za Muungano. Majukumu hayo yanahusisha utoaji wa mafunzo kwa Viongozi na Wahadhiri wa Vyuo Vikuu vilivyopo Tanzania Bara na Zanzibar kuhusu masuala ya elimu ya chuo kikuu, ikiwemo Uongozi na Usimamizi wa Vyuo Vikuu, Uandaaji wa Mitaala inayokidhi mahitaji ya soko, Mbinu Bora za Ufundishaji na Uthibiti Ubora wa Elimu ya Juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, katika kipindi cha Juni, 2023 hadi Machi, 2024 viongozi na wahadhiri 48 kutoka vyuo vikuu vitatu vilivyopo Zanzibar wamepata mafunzo yaliyojumuisha viongozi na wahadhiri kutoka vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki 49 vilivyosajiliwa chini ya TCU.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TCU kila mwaka hufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu yake. Kutokana na tathmini hiyo, mikakati ya uboreshaji huwekwa kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya TCU katika pande zote za Tanzania Bara na Zanzibar.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza:-

Je, Serikali ina mipango gani wa kuharakisha Miradi ya LNG nchini ili kuchochea uchumi na kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na majadiliano na Kampuni za Nishati za Kimataifa (International Energy Companies - IEC’s) kwa ajili ya Utekelezaji wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG). Aidha, Serikali inaendelea na kazi za awali ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti wa msingi wa kimazingira na kijamii, uelimishaji kwa wananchi juu ya umuhimu na manufaa ya mradi kupitia uhamasishaji wa matumizi ya gesi asilia kwa matumizi mbalimbali ikiwemo matumizi ya majumbani. Ahsante.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, Serikali ina mipango gani wa kuharakisha Miradi ya LNG nchini ili kuchochea uchumi na kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na majadiliano na Kampuni za Nishati za Kimataifa (International Energy Companies - IEC’s) kwa ajili ya Utekelezaji wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG). Aidha, Serikali inaendelea na kazi za awali ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti wa msingi wa kimazingira na kijamii, uelimishaji kwa wananchi juu ya umuhimu na manufaa ya mradi kupitia uhamasishaji wa matumizi ya gesi asilia kwa matumizi mbalimbali ikiwemo matumizi ya majumbani. Ahsante.