MHE. MBAROUK JUMA KHATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
(a) Je, hatuoni kuna haja ya kuharakisha ujenzi huu kutokana na uhalifu ambao unajitokeza?
(b) Je, Serikali haioni haja ya kuongeza nguvu ya askari na gari kwa ajili ya doria? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, najibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khatibu, Mbunge wa Jimbo la Bumbwini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua fursa hii kumpongeza sana kwa kazi nzuri anayoifanya; lakini kikubwa nimwambie tu kwamba kuna haja ya kufanya haraka ya kituo hiki ipo na tayari Jeshi la Polisi kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tumeshawasiliana na wenzetu wa Mamlaka ya Bandari – Zanzibar ili ikiwezekana haraka waweze kuanza ujenzi wa kituo hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie tu siyo kituo hiki, pale bandarini ni lazima pale pawe na watu wa uhamiaji, pawe na ofisi za fire na hicho kituo cha polisi ili lengo na madhumuni ni huduma za ulinzi na usalama katika eneo lile zipatikane.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, haja ya kuongeza askari ipo. Nimwambie tu Mheshimiwa awe na subira kidogo kwa sababu, vijana wetu bado wapo kwenye mafunzo. Juzi tu Jeshi la Polisi walitangaza nafasi nyingine ili lengo na madhumuni tuongeze nguvu ya ulinzi na usalama katika maeneo yetu yote ya Tanzania, ninakushukuru.