Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Innocent Sebba Bilakwate (60 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza nichukue nafasi hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Kyerwa ambao wamenichagua kuwa Mbunge wao. Nachowaahidi wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa sitawaangusha.
Nimejipanga vizuri na najua yanayoendelea kule Jimboni lakini mimi ndiye Mbunge wa Jimbo la Kyerwa hakuna mwingine. Hao wanaojipanga wanasema wanasubiri siku mbili, sijui miezi miwili hakuna lolote mimi ndiye Mbunge wa Jimbo la Kyerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kwanza kupongeza hotuba ya Waziri na niipongeze hotuba ya Mheshimiwa Rais ambapo aligusia maeneo mengi mazuri yanayomlenga Mtanzania halisi. Kwa kweli mimi nasema Mpango huu ni mzuri na nauunga mkono lakini kuna maeneo ambayo nataka nijikite. Maeneo ambayo nataka kujikita, niiombe Serikali, Mpango huu umlenge mwananchi wa kawaida, twende kule chini. Tunaongelea kujenga viwanda lakini tunapoelekea kwenye kujenga viwanda vikubwa tusipoangalia huyu mwananchi wa chini ambaye hali yake ni mbaya hatutaweza kufikia malengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema tunaenda kwenye uchumi wa kati lazima tuende huku chini, huyu mwananchi ambaye hali yake ni mbaya tunamuinuaje kwanza. Tuna vitu ambavyo lazima tuviangalie, kwa mfano, mimi natoka maeneo ya wakulima. Kule kwetu Mkoa wa Kagera na Jimbo langu la Kyerwa tuna uwezo wa kulima kwa mwaka mpaka mara tatu lakini hawa watu wanapolima hawana pa kuuza mazao, hawana soko la uhakika. Lazima tuwawekee mazingira rafiki wanapolima wapate mahali pa kuuza mazao yao, ndipo tutaweza kumuinua mwananchi na ndipo tutaweza kusema tunaingia kwenye uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali na Wizara ya Kilimo, kwa mfano kule Kyerwa kuna masoko ya kimataifa yanajengwa pale Mkwenda na Mrongo mpakani na Uganda lakini masoko haya hayaendelei. Tulitegemea masoko haya yangekamilika mwananchi wa hali ya chini angeweza kuuza mazao yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni kuhusu miundombinu. Kwa kweli naomba niiambie Serikali ni kama kuna maeneo ya Watanzania na mengine labda siyo Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kule kwetu Kyerwa hakuna hata kilomita moja ya barabara iliyojengwa kwa kiwango cha lami, hali ni mbaya. Barabara inayotoka Murshaka - Nkwenda - Isingilo - Murongo ni mbaya sana haipitiki. Tulipotoka kwenye uchaguzi, nimefanya utafiti magari yote yanayopita kwenye barabara hii yote yamepasuka vioo kila baada ya wiki moja ni kwenda kufanya service, hali ni mbaya.
Naiomba sana Serikali kama wanaweza kutusaidia watusaidie barabara hii inayotoka Murshaka mpaka mpakani na Uganda. Hii ndiyo barabara muhimu na tunayoitegemea. Watu wanaotoka Uganda - Murshaka - Kayanga - Bukoba hii ndiyo barabara tunayotumia. Niombe sana Serikali na niwaombe hao wataalam mnaowatumia, kuna barabara inayotoka Mgakolongo - Kigalama - Bugomola – Uganda, mmesema itajengwa kwa kiwango cha lami, niiulize Serikali ni lini barabara hii itaanza kujengwa? Vilevile barabara hii ya Murshaka - Mulongo itaanza kujengwa lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema tunataka kwenda kwenye uchumi wa kati lazima tuangalie, wananchi wa Jimbo langu la Kyerwa hawana maji safi na salama, hatufiki hata asilimia 10. Nimuombe Waziri wa Maji na Serikali yangu, najua hii ni Serikali sikivu, wananchi wa Kyerwa tuangaliwe na sisi ni sehemu ya Watanzania, kile kidogo tunachokipata wote tufaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuna suala la afya, Wilaya yangu ya Kyerwa ni mpya hatuna Hospitali ya Wilaya. Wilaya hii tuna vituo vya afya vinne tu ambavyo havina dawa na hata kwenye zahanati hakuna dawa. Haya mambo ameyazungumzia sana Mheshimiwa Rais, niiombe sana Serikali tunapopeleka dawa ziwafikie wananchi. Naiomba sana Serikali katika hilo itufikirie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda niliongelee ni kuhusu hawa vijana wetu wa bodaboda. Serikali iliweka utaratibu wa kusajili pikipiki baadaye wamesema pikipiki hizi zitabadilishwa namba. Ninyi mwanzoni mmesema mmesajili kwa kutumia namba „T‟ leo mnasema mnataka kutumia namba nyingine, gharama hizi zinabebwa na nani? Leo wananchi wanapigwa, wananyanyaswa wakasajili pikipiki upya lakini makosa haya yalifanywa na nani? Niiombe sana Serikali tunapofanya makosa sisi kama gharama za kusajili pikipiki tukasajili sisi bila kuwabebesha mzigo hawa vijana wa bodaboda, hili siyo sawa. Lazima tuangalie hawa vijana wamejiajiri leo wako mitaani wananyanyaswa, wanapigwa, wanaambiwa sajili mara ya pili hili siyo sawa. Niiombe Serikali iliangalie suala hili na ilitolee ufafanuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ndugu zangu nataka kusema tumemaliza uchaguzi, kila chama kilipeleka Ilani kwa wananchi na chama walichoona ni bora ni Chama cha Mapinduzi. Hakuna chama kingine ambacho kimepewa kuongoza Tanzania ni Chama cha Mapinduzi. Sasa tusije hapa tukaleta mbwembwe, tukaanza kuitukana Serikali sisi ndiyo tunaotawala lazima muwe wapole. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema ndugu zangu hapa kuna maagizo, tunataka tuonekane mbele ya Watanzania kuwa sisi tunajua kupanga, tunajua kuongea lakini Watanzania wana akili. Tumekuwa tukisikiliza hapa Bungeni mkisema vitu mbalimbali, uovu ulio ndani ya Chama cha Mapinduzi ni kweli ulikuwepo lakini Chama cha Mapinduzi kimeamua kufanya mageuzi. Hao mliokuwa mnawataja leo wako kwenu. Sasa hivi ninyi mna ujasiri wa kusimama mbele ya Watanzania kusema mafisadi?
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Huo ujasiri mmeutoa wapi maana mmewabeba ninyi, mliwasema wako kwetu leo wako kwenu. Kwa hiyo, msije hapa kwa mbwembwe Watanzania wana akili, wanajua kinachofanyika na wamepima wameona hamfai.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Habari ndiyo hiyo. (Kicheko/Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niwaambie, hawa Watanzania wana macho wanaona, wana masikio wanasikia.
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha usiendelee.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. INNOCENT S. BILAKATWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu. Nakushukuru kunipa nafasi hii kuchangia. Kwanza nampongeza sana Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ambayo ameiwasilisha mahali hapa. Ni hotuba nzuri ambayo inaongelea kila kitu; hakuna mahali ambapo hakugusa. Kabla sijafika huko, kwanza naipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutumbua majipu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi ndiyo inayotumbua majipu. Kwanza majibu yalianza kutumbuliwa pale walipoanza kukata jina la fisadi namba moja. Hili nalisema kwa sababu hao hao ndio waliosema ni fisadi, hatukuanzisha sisi.
MBUNGE FULANI: Kweli!
MHE. JOHN H. WEGESA: Kwa hiyo, naipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi na nawapongeza Mawaziri, songeni mbele. Tuko nyuma yenu, tutapigana usiku na mchana mpaka kitaeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Rais wetu kwa ujasiri mkubwa kwa kazi nzuri anayoifanya na Serikali nzima kwa ujumla. Niwaambie Waheshimiwa Mawaziri na Waziri wetu Mkuu, msiogope. Siku zote unapokwenda kwenye kituo cha mabasi au cha daladala, kuna watu wanaitwa wapiga debe. Siku zote wapiga debe huwa sio wasafiri. Waacheni wapiga debe wakapige debe, wanaosafiri wanajua wanakoenda. Sisi tunajua tunakoipeleka nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nijikite kwenye michango yangu. Naipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo inajitahidi kukusanya mapato. Naiomba Serikali yetu, bado Watanzania wanahitaji elimu kuhusu kutumia hizi mashine za electronic. Ukienda maeneo mengi ya vijijini, hizi mashine hakuna. Tunapoteza mapato mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwa muda mfupi huu tuliotoka kwenye shilingi bilioni mia nane na kitu, kwenda kwenye shilingi trilioni 1.3 tunaweza kuvuka hata tukaelekea kwenye trilioni mbili.
Naomba tuongeze juhudi za kuwaelimisha Watanzania, kila tunachokinunua tupate risiti. Naiomba sana Serikali hasa katika suala la umeme, kuna maeneo mengine ambayo hawataweza kutumia mashine hizi; hakuna mitandao, hakuna umeme. Kwa mfano, kama kule kwetu Kyerwa, kuna maeneo mengi hakuna mitandao na hizi mashine hazitafika. Naomba Serikali ipeleke mitandao mahali ambapo hakuna mitandao ili tuweze kukusanya mapato mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nijikite kuipongeza Serikali; inasema tunaenda kwenye nchi ya viwanda; ili tuweze kufika kwenye nchi ya viwanda, kuna vitu ambavyo tunahitaji kwanza tuviangalie.
Kwanza, tuongeze nguvu kwenye umeme. Tunataka huu umeme wetu unaokwenda vijijini uweze kuwasaidia vijana wetu. Tunayo makundi mbalimbali, uzalishaji mkubwa uko vijijini; kilimo, kila kitu kinapatikana huko vijijini. Tukiweka umeme wa kutosha, tutaweza kufungua viwanda vidogo vidogo na vijana wetu ambao ndio nguvukazi wataweza kupata ajira. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali izingatie hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu. Tunayo mitambo mikubwa, tuna viwanda vikubwa, hivi viwanda vinahitaji kutumia umeme. Serikali ijikite kuongeza nguvu kwenye kuzalisha umeme, tunataka mitambo inayochimba madini iunganishwe kwenye grid ya Taifa. Itakapounganishwa kwenye grid ya Taifa, mapato yetu yataongezeka kwa sababu uzalishaji ambao wanatumia sasa hivi generator utapungua na mapato yataongezeka. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, tunao uwezo wa kuongeza umeme kwa sababu tayari tunayo gesi nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, tunaposema tunaenda kwenye uchumi wa kati, uchumi wa viwanda, ni lazima tuboreshe miundombinu yetu iwe mizuri. Huwezi ukasema utajenga viwanda wakati miundombinu haiko vizuri. Kwa mfano, kama kule kwetu Kyerwa tunazalisha kila kitu lakini barabara ni mbovu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, hili mliangalie. Kuna barabara inayotoka Murushaka kwenda Nkwenda mpaka Mulongo mpakani na Uganda. Hii barabara imesuswa kwa muda mrefu, lakini unapoongelea uchumi wa Kyerwa ni pamoja na barabara hii. Hii ndiyo namba moja Kyerwa. Naiomba sana Serikali iliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, kuna hao wananchi ambao wanazalisha, kwa mfano, kama kule kwetu, kuna masoko ambayo yameanza kujengwa pale Nkwenda na Mulongo; haya masoko yamesahaulika. Serikali iliyajenga, yamefikia nusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali, haya masoko yaendelezwe ili wananchi wawe na soko la uhakika. Siyo wanalima halafu wakishalima mazao yanaozea mashambani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali ijitahidi sana kuboresha miundombinu ili mazao haya yaweze kuuzwa mahali panapohusika. Mwananchi anapolima ajue nina uhakika wa kupeleka mazao yangu sokoni na kupata pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia maiomba Serikali hii ihakikishe inawakumbuka vijana wetu wa bodaboda. Hawa ni vijana wanaojiajiri, lakini hawa vijana wamekuwa kwenye mazingira ambayo siyo mazuri; vijana hawa wakati mwingine wanapata mateso mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti naiomba sana Serikali, kuwapa elimu hawa vijana na sisi wanasiasa ambao tuko humu Bungeni, tuwape elimu hawa vijana waweze kuwa na Bima ya Afya wapate matibabu. Vijana wengi wanapata ajali, wengine wanakatika miguu na mikono lakini hakuna Bima ya Afya. Mwingine hana pa kutibiwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukaanzisha Mfuko hawa vijana wakawa na kitu kidogo ambacho wanaweka ili hata inapotokea, wanapopata ajali, anakuwa na pesa sehemu fulani ameiweka; siyo wanatumia tu. Wanahitaji elimu na nawaomba Wanasiasa wenzangu tuhakikishe hawa vijana wetu tunawapa elimu ili wajue ile ni ajira kama sisi wengine ambavyo tunajiwekea akiba na hawa vijana waweze kujiwekea akiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nilizungumzie, ili tuweze kufanikiwa haya yote ambayo tunayasema, tunahitaji kuboresha maslahi ya Watumishi wetu. Kuna watumishi wengine wanafanya kazi kwenye mazingira magumu. Mazingira yanakatisha tamaa. (Makofi)
Kwa mfano, kama kule kwetu Kyerwa kwenye Halmashauri, kuna gari moja tu. Hiyo gari ya Mkurugenzi, mara wanakwenda kwenye miradi; hawawezi wakafanya kazi vizuri. Kwa hiyo, naomba tuboreshe mazingira yawe mazuri waweze kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ili tuweze kwenda kwenye uchumi mzuri na maisha yawe mazuri, lazima Watanzania wapate maji safi na salama. Katika maeneo mengi hakuna maji. Tunaposema tunataka uchumi wa Mtanzania upande, ni pamoja na kuondoa hivi vitu ambavyo mnamfanya Mtanzania; kwa mfano, kuna mahali pengine mtu anakwenda kuchota maji masaa matano. Huyu mtu atafanyaje shughuli za maendeleo aweze kujipatia kipato?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya tuyaangalie. Naiomba sana Serikali, tunapofanya haya, tusiangalie sehemu moja tu, hawa ni Watanzania, wote wafaidi kile kidogo tunachokipata. Unakuta miradi inaelekezwa eneo moja tu. Tuelekeze maeneo yote, tugawane kidogo, mwisho wa siku wote tufanikiwe maana wote ni Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, suala la afya ni muhimu. Namwomba Waziri Afya, Kyerwa hatuna Hospitali ya Wilaya, lakini hata vile Vituo vya Afya vilivyopo havina madawa, naamini hii ni Serikali sikivu; na majipu haya ambayo wenzetu wa upande wa pili waliyapandikiza, tumewagundua, tunayatumbua kila siku; yanaondoka. Tunaamini wao ndio wanayapandikiza kwa sababu tunapoanza kuyatumbua, tunaona wanalalamika, maana wale ni wenzao. Kwa hiyo, tutaendelea kuyatumbua na Serikali imejipanga vizuri tutapata Watumishi waaminifu ambao hawakupandikizwa. Serikai hii itapaa sana!
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naishukuru Serikali yangu na naamini ni sikivu. Kwa hayo machache, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukupongeza Mheshimiwa Waziri na Serikali yetu kwa hotuba nzuri kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda. Hotuba hii inaongelea mambo mazuri sana na kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda jambo ambalo litaleta fursa ya ajira kwa vijana wetu ambao wako mitaani, hawana ajira, pia tukiwa na viwanda tutainua kipato cha mwananchi na kipato cha Taifa kitaongezeka na uchumi wetu utakua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kufanikiwa ni lazima tuhakikishe tunaweka mazingira rafiki ambayo yatawapa fursa wawekezaji kuja kuwekeza nchini kwetu bila usumbufu yaani tuondoe urasimu uliopo, pia viwanda ambavyo vipo tuhakikishe tunavilinda. Niiombe Serikali yangu ili tuweze kufanikiwa na tuingie kwenye uchumi wa viwanda wa kati tuhakikishe tunakuwa na umeme wa kutosha ili viwanda vyetu vitumie umeme wetu kupunguza gharama za uzalishaji na ndipo kipato cha Taifa kitaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuwekeza kwenye kilimo cha kisasa ili kupata malighafi za kupeleka kwenye hivyo viwanda, tuweke mazingira rafiki ili huyu mkulima anacholima kiwe na ubora kwa ajili ya viwanda vyetu hatuwezi kufanikiwa. Mheshimiwa Waziri tutumie huu umeme wa REA ambao umefika vijijini, tuwawezeshe na kuwapa elimu vijana wetu kufungua viwanda vidogo vidogo wapate ajira na kuongeza kipato cha Taifa.
Namuomba Mheshimiwa Waziri, Kyerwa kuna kahawa ambayo ni zao muhimu linaloingizia Taifa kipato. Serikali iongeze Benki zetu hasa hasa Benki ya TIB ipunguze riba ili wananchi wakopeshwe mashine za kukoboa kahawa, hili litaongeza kipato kwa mwananchi kitu ambacho kitapunguza wizi wa kahawa inayopelekwa nchi jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kufikiria kufungua kiwanda Kyerwa cha kusafisha Tini ili kuinua kipato cha wachimbaji wadogo wadogo na hili litaondoa Tini nyingi inayovushwa kupeleka nchi jirani maana karibu asilimia 75 ya Tini inayochimbwa Kyerwa inanufaisha nchi jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali ipeleke viwanda maeneo husika ili kuongeza ajira kwa maeneo husika mfano, viwanda vipelekwe maeneo ya uzalishaji pamba, matunda, tumbaku na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa neema ya gesi tunaweza kuzalisha vitu vingi. Niiombe Serikali tusiishie kwenye kuzalisha gesi kwa ajili ya umeme tu, bali kila kitu kinachotoka kwenye gesi maana gesi tunaweza kuzalisha vitu vingi sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mungu kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwa maandishi na pia kunipa uhai na afya njema ya kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. Nichukue fursa hii kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, mwanzo ni mzuri, inatia moyo, ikiwemo Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Murushaka – Murongo; Mheshimiwa Waziri katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika ukurasa wa 59 imeelezwa kufanyiwa upembuzi na usanifu yakinifu, lakini kwenye bajeti yako sijaiona. Mheshimiwa Waziri, kusema ukweli barabara hii ndiyo barabara ya kiuchumi namba moja Kyerwa, ndiyo tegemeo la Wanakyerwa ikipitia Makao Makuu ya Wilaya na kuunganisha Wilaya jirani ya Karagwe na kuunganisha Mkoa wa Kagera. Pia barabara hii inaunganisha nchi jirani za Uganda na Rwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri pia Mheshimiwa Rais akiwa Kata ya Nkwenda Wilayani Kyerwa aliitaja barabara hii na umuhimu wake na akaahidi itajengwa kwa kiwango cha lami na akatoa zawadi ya kuahidi kilometa 20 kwa kuanzia, wakati taratibu zingine zikiendelea, lakini cha ajabu ahadi ya kilometa hizo 20 haionekani katika Bajeti yako. Mheshimiwa Waziri, naomba kupewa jibu kwa nini hiyo barabara haipo kwenye upembuzi na hizo kilometa 20 alizoahidi kwa kuanzia, hazikuwekwa kwenye bajeti yako?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kwa umuhimu wa barabara hii na mateso wanayoyapata wananchi isipowekwa kwenye bajeti au Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano, tujiandae jimbo kuondoka. Maana wamekuwa wakiahidiwa maneno ya uongo kuwa itatengenezwa tangu Serikali ya Awamu ya Nne na Rais Kikwete akiwa Nkwenda kwenye mkutano wa hadhara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mgakorongo – Kigalama – Murongo; Mheshimiwa Waziri, naomba kujua barabara ya Mkagorongo – Kigalama mpaka Murongo, taarifa nilizozipata tayari imefanyiwa upembuzi yakinifu, ninachotaka kujua ni lini barabara hii ujenzi utaanza? Maana, sikuona kwenye bajeti yako pesa ya ujenzi kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana, nimejitahidi sana kukuandikia mpaka nimefika ofisini kwako kukueleza kuhusu barabara hizi na umuhimu wake. Naomba sana kufikiriwa, tumeachwa muda mrefu, tumekuwa yatima, hatukuwa na mtu wa kutusemea. Pia nikuombe sana, pata nafasi ufanye ziara ya kutembelea Jimbo la Kyerwa ili ujionee mwenyewe umuhimu wa barabara hii; maana inaonyesha wakati mwingine mnaletewa taarifa za uongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipewe majibu kama nilivyooomba kwenye maandishi yangu. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa nafasi hii na uhai nilionao naamini uko mikononi mwake. Pia nichukue nafasi hii kukupongeza wewe Mwenyekiti, nafikiri makofi yaliyokupokea yanaonyesha jinsi gani Waheshimiwa Wabunge wanavyokuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kweli mwanzo ni mzuri. Mimi niwatie moyo, songeni mbele, kazi yenu tunaiona, juhudi zenu tunaziona na sisi tuko nyuma yenu, tutawaunga mkono. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwa kweli hawa bado ni vijana wanafanya kazi nzuri tuwaunge mkono tusibeze, huu ni mwanzo tu. Mtu anapofanya vizuri hata kama upo upande wa pili hebu muungeni mkono. Haya yote tunayoyafanya ni kwa ajili ya nchi yetu siyo kwa ajili ya wana CCM tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la afya. Ndugu zangu tuko hapa Bungeni kwa sababu afya zetu ni nzuri, Wizara ya Afya ndiyo kila kitu. Katika kuchangia kwangu niiombe Serikali wamekuwa wakileta bajeti kwenye vitabu lakini inapelekwa asilimia kidogo sana. Tuiombe sasa hivi Serikali tuwe makini sana, hili ni jambo muhimu ambalo linahitaji kuungwa mkono na kila mtu. Tunahitaji afya zetu ziwe nzuri ili tuweze kuwatumikia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema kuingia kwenye nchi ya viwanda na uchumi wa kati lazima afya zetu ziwe nzuri. Hao Watanzania wawe na afya nzuri waweze kuzalisha, bila kuwa na afya nzuri hatuwezi tukafanikiwa hayo tunayoyalenga. Ili tuweze kufanikiwa kwenye kilimo chetu, kiwe kizuri lazima tuwe na afya nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara hii tuiunge mkono na kama wengine walivyochangia kwa kweli namuunga mkono Mheshimiwa Bashe ambaye amesema Wabunge wote bila kujali tunatoka chama gani tuungane akinamama waweze kupatiwa bima za afya. Kwa kweli hili ni jambo muhimu, akinamama wengi wanakufa si kwa sababu ya magonjwa ni kwa sababu hawapatiwi huduma nzuri. Kwa mfano, kama kule kwetu Kyerwa hakuna huduma nzuri za afya, hali ni mbaya. Kule vijijini hali ni mbaya sana, hii mikoa ya huku pembezoni ndiyo kabisa unaweza ukafikiri Serikali haipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ukija kwetu Kyerwa kuna watumishi watano tu na hao wako wilayani, kwenye kata hakuna mtaalam hata mmoja. Hawa watu mnawahesabia wapi? Naiomba Serikali tusiangalie mijini tu twende mpaka vijijini na hao wataalam ambao wako maofisini wasikae makao makuu tu waende vijijini wakaone hali ilivyo. Mara nyingi wataalam wamekuwa wakiuliza huko vipi, fikeni mkaone hali ilivyo. Nimwombe Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu na Ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla wafike Kyerwa waone hali halisi ilivyo, hali ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye zahanati zetu hakuna dawa kabisa. Hawa wazee mnaosema wakate bima ya afya, wanakata bima ya afya, lakini ni aibu kwanza tumalize kitu kimoja. Huyu mzee unamwambia akakate bima ya afya, anakwenda anamwona Daktari anamwandikia, akishamwandikia anamwambia dawa hakuna, dawa muhimu Kyerwa asilimia kubwa hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, tunaposema hao wazee watibiwe bure, watoto wenye umri chini ya miaka mitano wapate huduma bure, akinamama wajawazito wapate huduma bure lazima tuhakikishe yale mahitaji yote yapo, tuhakikishe dawa zipo, huduma zote zipo siyo tunasema tunawapa huduma bure wakati hakuna vitendea kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, tunalo tatizo la watumishi, hakuna watumishi, hakuna Madaktari. Kwa mfano, kule kwetu Kyerwa na naamini ni maeneo mengi hakuna Madaktari. Ndugu zangu, niwaombe na niiombe Serikali tusipange mipango mingi, hebu tupange mipango michache tuweze kuitimiza ndiyo twende kwenye mipango mingine. Tusiseme tutafanya vitu asilimia mia moja halafu mwisho wa siku tunakuja kufanya asilimia tano ni aibu. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali ishughulike suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka niseme, huwezi ukazaa mtoto ukampa mtu mwingine akulelee. Mwenye uchungu na afya ya Mtanzania ni Wizara ya Afya. Huyu ndiye mzazi! Unampaje huyu mtoto mtu mwingine amjengee wodi, amletee vifaa? Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, ifike wakati hizi sheria zinatungwa humu ndani tukazibadilishe. Mwenye uchungu ni Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Wizara yake na Watendaji wenzake; huyu ndiye anayehudumia afya za Watanzania. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge, hizi sheria tuzibadilishe, tusiseme kila kitu tumejaza huku TAMISEMI, kila kitu TAMISEMI, lakini mwisho wa siku afya za Watanzania zikiwa mbaya anayeulizwa ni nani? Ni Wizara ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, Serikali tujipange vizuri, tufikishe madawa kwa wananchi. Hakuna madawa, tunahimiza hapa Watanzania wakate Bima ya Afya, dawa watazipata wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, hawa wa MSD nasikia wanadai pesa kibao! Serikali iwapelekee pesa ili Watanzania waweze kupata madawa, kwa sababu hata tukisema tumejenga vituo, tumejenga maduka ya madawa, mwisho wa siku hawa MSD pesa watazitoa wapi? Sasa tunaomba Serikali ijipange, zamu hii Watanzania wale ambao wanapata huduma hizi bure wanapokwenda siyo anaandikiwa na Daktari cheti halafu mwisho wa siku anakwenda kununua dawa dukani; wengine hawana uwezo. Wakati mwingine tunaanza kwetu, sisi wenyewe Wabunge mbona hatuendi kununua dawa kwa pesa yetu? Si tumepewa Bima ya Afya na tunapata dawa? Lazima tusimame tuhakikishe tunawatetea wananchi wetu, tusiangalie mambo yetu wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni kuhusu vifo vya akinamama. Kuna maeneo mengine miundombinu ni mibovu, kama kule kwetu Kyerwa mtu unatoka tuseme labda Kaisho uende kutibiwa Hospitali ya Nyakahanga, ni mwendo mrefu, barabara mbovu, huyo mama kama ni mjamzito mimba itatoka tu. Kwa hiyo, naiomba Serikali, hivi vitu vyote hatuwezi tukavitenganisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, namwomba Mheshimiwa Waziri, hata kama haihusiani na huko, ninachojua wewe ni Waziri wa Afya unashughulikia afya za Watanzania. Tunacho Kituo chetu cha Afya pale Nkwenda; hiki kituo tunaomba Mheshimiwa Waziri, bado kina upungufu, lakini hiki kituo tunaomba kiwe hospitali kamili. Hatuna Hospitali ya Wilaya, hospitali tunayoitegemea ni Hospitali ya Mission ambayo wananchi hawawezi kumudu gharama za matibabu, ni kubwa sana. Nilishaiandikia Serikali mwaka 2015 nilipokuwa hapa Bungeni kuiomba hii Hospitali ya Mission…
MWENYEKITI: Ahsante!
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa nafasi hii na uhai kuwepo katika Bunge hili, maana tunaishi kwa neema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Sospeter Muhongo wewe ni jembe tu hata wakipiga kelele, tunakuamini wewe pamoja na Naibu Waziri wako na watendaji wengine wote wa Wizara, kazi mnayoifanya inaonekana, hapa tulipofikia pamoja na figisufigisu zilizofanywa, lakini tumefika hapa tulipo kwa sababu ya kazi yako kubwa uliyoifanya. Watanzania wanajua, ndiyo maana wanakuunga mkono na ninaamini watu wenye akili hakuna atakayesimama kukupinga wewe. Kwa hiyo, ninampongeza sana, songa mbele, jeshi kubwa liko mbele yako na nyuma yako, tunakulinda kwa nguvu zetu zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kuhusu Wizara hii, kwa kweli nina kila sababu za kuwapongeza Wizara hii imeonesha dhamira kubwa ya kutaka kutusogeza mbele. Ukisoma hii bajeti fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo ni fedha kubwa, hii ni dhamira nzuri ya Serikali kutaka kuinua uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini umeme ndiyo kila kitu, hata Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Mwijage anaposema anataka Tanzania ya viwanda kila kona, tusipokuwa na umeme wa uhakika hatuwezi kuwa na viwanda. Kwa hiyo, hizi Wizara zinategemeana, niendelee kusema juhudi zenu ni nzuri na tunakuunga mkono, ukiangalia kwa mfano upande wa REA imeongezeka karibu asilimia 150 utoka shilingi bilioni 350 mpaka shilingi bilioni 535, kwa kweli hii ni dhamira ya dhati kwa Wizara hii. Mimi ninawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho ninaomba kwa Mheshimiwa Waziri na Serikali hizi fedha zinapotengwa zitolewe, siyo leo tunapitisha bajeti mwisho wa siku zinatolewa asilimia tano.
Ninaiomba Serikali ijitahidi hizi pesa zitolewe Watanzania wanahitaji kupata umeme wa uhakika, umeme wa kutosha. Kwa mfano, kule kwetu Kyerwa tangu uhuru ndiyo tumeanza kuona umeme wengine walikuwa wanashangaa umeme ulipowashwa. Bado haujafika mbali, umeme kule kwetu Kyerwa umepita maeneo machache, Mheshimiwa Waziri umefika Kyerwa umeona Watanzania wa Kyerwa namna walivyo na uhitaji wa umeme. Maeneo mengi ya vijijini ndiyo kuna uzalishaji, tunaposema tunataka kujenga viwanda tukipata umeme wa uhakika, hivi viwanda vinaweza vikajengwa vijijini tukazalisha huko vijijini, tukafungua viwanda vidogovidogo na tukaongeza ajira kwa vijana wetu ambao wako mitaani hawana ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninakuomba Mheshimiwa Waziri, jambo hili ninakusifu sana kwa kutotenga vijiji hapa maana kuna kuchomekeana sana hapa, kuna wengine wanapita mlango wa nyuma, kwa sababu hukutaja vijiji ninakuomba wote tukagawane mkate huu sawa, Watanzania ni wamoja na wote tupewe sawa siyo wa kupendelewa, kuna upendeleo na hili naomba mlisimamie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wengine wakati mwingine wanatoa pesa ili wapewe miradi hilo lipo, ndiyo maana unakuta mwingine amepitishiwa vijiji vyote kwingine hakuna, naomba Mheshimiwa Waziri hata hao watendaji wako hao uwaangalie vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri suala la umeme ni muhimu sana na ili Tanzania iweze kuendelea tuweze kufanikisha malengo tuliyonayo tunahitaji umeme wa uhakika, siyo umeme huu tunasema tunafunga umeme lakini umeme huo siyo wa uhakika. Kwa mfano, kwetu Kyerwa, umeme unawaka lakini huwezi ukawasha mtambo wowote mkubwa, umeme unawaka na kuzimika, kule tunapewa umeme masaa mawili, matatu. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri huu umeme usiangalie mijini tu hata huko vijijini ni muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la gesi, Mheshimiwa Waziri suala la gesi ni muhimu sana kwa Taifa letu na tumshukuru Mungu kwa jinsi ambavyo tumepata gesi ya uhakika. Hii gesi isijikite kwenye umeme tu wataalam wanasema gesi tunaweza tukaitumia kwenye umeme asilimia kumi, kuna vitu vingi ambavyo tunaweza tukavipata kupitia umeme kwa mfano plastiki, kuna nguo ambazo zinazalishwa kupitia gesi naongelea gesi kuna mbolea na vitu vingine hii gesi isije ikapotea bure. Kama tunaweza kuzalisha umeme asilimia kumi, je, hii asilimia 90 tumejiandaa vipi? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri na hili lazima uliangalie tusije tukasema tuna gesi kumbe gesi yenyewe tunaitumia asilimia kumi tu, kwa hiyo ninaomba mliangalie.
Mhehsimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Mheshimiwa Waziri nataka nilisemee Kyerwa tuna madini ya tin, haya madini kule kwetu Kyerwa majirani zetu ndiyo wanaoyafaidi, asilimia kubwa hatuyafaidi Watanzania yanavushwa na hilo Mheshimiwa Waziri unalijua, naomba tulisimamie vizuri ili tukafaidi haya madini ni ya Watanzania siyo ya nchi jirani. Serikali hili mnalijua sijui mmejiandaa vipi kwa ajili ya kulisimamia vizuri ili haya madini yasiendelee kupotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuhusu madini Mheshimiwa Waziri ulifika kule Kyerwa, vijana wetu ambao wanachimba madini wako kwenye mazingira ambayo siyo mazuri tuwaboreshee mazingira yawe rafiki, tutenge maeneo ambayo ni kwa ajili ya vijana wetu hao wachimbaji wadogo wadogo.
Wakati mwingine hawa vijana wanafanya utafiti, wakishagundua madini hawa wakubwa wanakuja wananunua yale maeneo wale vijana ambao wameanzisha wanaondolewa.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri kama ulivyoongea na wale vijana ukasema utatuma wataalam, waje wapime watenge maeneo kwa ajili ya hawa vijana nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, ninakumini wewe ni mchapakazi ninaomba hili ulisimamie kwa ajili ya vijana wetu...
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza, nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uhai kuwemo katika Bunge hili kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Kyerwa. Nichukue nafasi hii kipekee kukupongeza kwa kazi nzuri unayoifanya kwa ujasiri ambao umeuonesha kama mwanamke. Kwa kweli tunakupongeza na tunakuombea Mungu akupe nguvu, akupe afya na azidi kukuinua kila siku akupandishe juu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kipekee kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kazi nzuri ambayo anaifanya ya kukusanya mapato. Kwa kweli kwa kipindi kifupi ameonesha kazi nzuri ambayo Wizara ya Fedha imeifanya na dhamira ya Serikali yetu kukusanya mapato. Kwa kweli nampongeza na nimtie moyo katika hili asitegemee atapendwa. Mtu yeyote ambaye anakusanya mapato, anakusanya kodi hapendwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, Mheshimiwa Waziri asije akategemea atapongezwa, atabeba lawama nyingi sana. Hata hivyo, katika hili wale wanaoitakia mema nchi yetu ni vizuri tukaungana naye hata sisi Wabunge tukaendelea kuwahimiza wananchi wetu namna ya kuchangia Taifa letu kwa kukusanya kodi kutoka kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wengi sio walipa kodi na sisi Wabunge ambao tumepitia bajeti hii tunahitaji kuwapa elimu, tunaona mambo mazuri ambayo Serikali imeyapanga. Sisi tuwahimize wananchi wetu ili waweze kushiriki, kuendeleza uchumi wa Taifa letu kwa kulipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuongelea mikoa maskini. Kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha, nimekuwa nikifuatilia sana hii mikoa maskini ni mikoa ipi? Kwa mfano Mikoa kama ya Kagera na Kigoma, ni mikoa ambayo ina uzalishaji mkubwa. Kwa mfano, kama kule kwetu Kyerwa, sisi tuna uwezo wa kulima mara tatu kwa mwaka, kila zao kule linastawi, ni kwa nini tumekuwa maskini? Hili ni jambo ambalo ni la kujiuliza na nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha anapokuja hapa atueleze ni namna gani wamejipanga kuinua hii mikoa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kuangalia hii mikoa ambayo ni maskini ni mikoa ambayo ni kama Serikali imeitenga, Serikali haiihudumii, haiwezekani Mkoa kama wa Kagera ambao tuna kila kitu, tuna zao la kahawa ambalo ni zao kubwa leo tunaitwa mkoa maskini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejaza tozo kibao, leo Waziri wa Fedha hajatuambia hizo tozo wameziondoa halafu bado anatangaza hii ni mikoa maskini, hili halikubaliki. Kitu kinachofanywa na Serikali mimi nashangaa! Badala ya kuondoa hizi kodi, walichofanya wamejaza askari kila mpaka ili wakulima wasipeleke kahawa Uganda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hamuwezi kuondoa hizi tozo zote waruhusuni wananchi wakauze kahawa wanakotaka. Lazima tujenge mazingira ambayo ni mazuri kwa wananchi wetu. Lazima tujiulize kwa nini hawa watu wanakwenda kuuza kahawa Uganda na sisi tutafute jibu ambalo litawasadia wananchi wetu wauze kahawa nchini kwetu, siyo tunajaza maaskari kila kona ili wazuie kahawa zisiende, hawa wananchi tutaendelea kuwafanya wawe maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukija kuangalia mikoa hii, Mkoa wa Kagera sisi tuko nyuma, tuna maji mengi, tuna vyanzo vingi vya maji, lakini hatuna maji safi na salama. Ni mikoa ambayo imenyimwa miradi mikubwa ya maji. Ukija kwenye umeme kwetu Kyerwa miaka 50 ya uhuru sasa hivi ndipo tunaanza kuona umeme, umeme wenyewe uliokuja unawaka masaa mawili, huyu mwananchi tutamwendelezaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitegemea nione kwenye bajeti mikoa hii ambayo ni maskini ndiko tuweke miradi mikubwa. Mikoa hii ambayo ni maskini ndiyo imenyimwa barabara, hilo halikubaliki, kwa nini hii mikoa inatengwa kwani sisi sio sehemu ya Watanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Mheshimiwa Waziri, hili waliangalie, lakini mikoa hii ambayo ni maskini huduma za afya ni duni, huyu mwananchi afya yake haiko vizuri ataweza kuzalisha vipi? Mtu anakwenda kuchota maji anakwenda kuanzia asubuhi mpaka saa tano, huyu mwananchi unategemea ataweza kuinuka? Haya mambo lazima tuyaangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali, nimwombe Waziri haya mambo ya kupeleka miradi wale walionacho wanazidi kuongezewa, sio sawa. Lazima tuangalie namna tutakavyowainua hao wananchi wetu ambao wana kipato cha chini. Katika hii mikoa, kwa mfano kama Kagera, tukiweka miundombinu vizuri, tukaweka mazingira mazuri tunaweza tukaliingizia Taifa mapato makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwahiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri hili aliangalie na atuambie anapokuja hapa, suala la kahawa, sasa hivi ni kipindi cha msimu, wananchi wanahitaji kusikia kauli ya Rais aliyoitoa kwenye kampeni; akasema hizi tozo zote ataziondoa. Tunataka tusikie bei nzuri vinginevyo waacheni wananchi wakauze kahawa wanakotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la bodaboda. Hawa Vijana wetu wanafanya kazi kwenye mazingira magumu. Leo tunawabebesha na kuwaongezea mzigo tena badala ya kuwaandalia kwanza mazingira ambayo ni mazuri waweze kufanya shughuli zao vizuri ndipo tutawaongezea kodi.
Unawawekea kodi wakati bado wako kwenye mazingira ambayo ni magumu, hili sio sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuangalie vyanzo vingine ambavyo tunaweza kupata mapato, tuwawekee mazingira mazuri wananchi wetu ndipo twende tukawakamue. Wewe ng‟ombe hujamlisha halafu unaenda kumkamua atapata maziwa wapi? Mheshimiwa Waziri lazima aliangalie jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ni suala la Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Nasema hili jambo inawezekana ni mtego ambao aidha wamemtega Mheshimiwa Waziri ili kuzuia juhudi za Mheshimiwa Rais wetu za kutaka kuwabana mafisadi ndiyo maana mmepunguza pesa. Rais wetu ana nia nzuri ndiyo maana anasema mahakama tayari inakwenda kuanza, TAKUKURU wameipa pesa, lakini hili jicho ambalo linaona huyu mwizi limlete mahakamani wamelinyima pesa, hili jambo sio sawa. Vinginevyo Mheshimiwa Waziri, aidha waliomshauri wamemshauri vibaya ili wasimamishe juhudi za Rais wetu za kupeleka mafisadi mahakamani, lazima aongezewe pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo Mheshimiwa Waziri wamemshauri, hizi Sh. 50 za kuongeza kwenye mafuta, watu wanahitaji maji, hata kwake Kigoma anajua watu wanahitaji maji, watu wanahitaji zahanati, kwa nini anakuwa mgumu kuongeza hizi pesa? Hata Kamati ya Bajeti imeshauri kwa nini hakusikia? Hili ni jambo ambalo ni zuri. Sisi Wabunge leo tuko tayari, tunasema tukatwe hizo pesa wananchi wetu wapate maji, wananchi wetu wapate zahanati. Naomba alifikirie, vinginevyo Waheshimiwa Wabunge tusimame hapa tusiipitishe hii bajeti. Tunahitaji maji, tunahitaji zahanati, hali ni mbaya ndugu zangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nitaunga mkono hoja pale ambapo atapitisha mambo muhimu. Ahsante kwa kunisikiliza.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuchangia.
Kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa jinsi ambavyo imeendelea kushughulikia tatizo la tetemeko katika Mkoa wa Kagera, tunaipongeza sana Serikali yetu kwa jitihada zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali kwa jinsi ambavyo imeshughulikia suala la ukame ambalo limeupata Mkoa wetu, tayari Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali sikivu imeshaleta chakula kuonyesha jinsi gani inavyowajali wana Kagera na wana Kyerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali lakini ombi langu niendelee kuiomba Serikali sisi Mkoa wa Kagera hatujawahi kupata njaa kiasi hiki, Serikali iendelee kuliangalia na ione ni namna gani ya kusaidia. Chakula kilicholetwa Kyerwa kilisaidia asilimia ifike hata asilimia kumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali bado tunahitaji chakula cha gharama nafuu. Lakini kuhusiana na suala la tetemeko niombe Serikali kuna wananchi ambao wanauwezo wa kuweza kujenga nyumba zao, lakini wananchi wengi hawana uwezo na ukilinganisha hali halisi ambayo tumeipata ya ukame.
Mimi niiombe Serikali bado tunahitaji wananchi wasaidiwe wale ambao hawana uwezo Serikali ione namna gani ambavyo inaweza kuwasaidia hasa hasa wale ambao hawajiwezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mpango niipongeze Serikali, mpango huu ni mzuri, una mambo ambayo ni mazuri. Lakini kuna mambo ambayo nataka nishauri, tunaposema tunataka kuingia Tanzania iwe ni ya viwanda kuna mambo ambayo tunabidi tuyaangalie; kwa mfano, suala la wakulima, sijaona kama limepewa nafasi kubwa nchi hii asilimia kubwa tunategemea kilimo, lakini hiki kilimo bado hatujawa na kilimo ambacho ni cha kisasa. Asilimia kubwa ya Watanzania wanategemea kilimo cha kutumia jembe ya mkono, lakini mazingira yenyewe haya ya kilimo wananchi bado sio mazuri, mwananchi anapolima bado hana soko la uhakika. Niiombe Serikali katika mpango wake iweke mazingira ambayo ni mazuri, mwananchi anapolima apate mahala pakuuza mazao yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine sasa hivi nchi yetu wametangaza maeneo mengi tutakumbwa na ukame. Tanzania tuna vyanzo vingi vya maji hata ukija kwetu kule Kagera, niombe Serikali iwekeze nguvu kubwa kwenye kilimo cha umwagiliaji, tutapata chakula kingi lakini tutaweza kupata chakula hata cha kuuza. Ninaamini tukiwekeza kwenye kilimo tutapata pesa nyingi ambayo itainua uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye upande wa ardhi niombe Serikali kama ambavyo imekuwa ikiendelea kushughulikia matatizo ya migogoro ya ardhi, Serikali ili iweze kufanikiwa katika mpango wake lazima tupambane na hizi kero ambazo ziko kwa wananchi wetu, tuainishe yale maeneo ambayo tayari yalishatengwa na Serikali kwa ajili ya wakulima yajulikane na yale ambayo yalishatengwa kwa ajili ya wafugaji yajulikane. Kwa mfano kama kule kwetu Kyerwa kuna mgogoro mkubwa wa ardhi, kuna ardhi ambayo ilishatengwa kwa ajili ya wafugaji. Ardhi hii imeporwa na wezi, wameingia humo tayari Serikali ilishatangaza kuwa hili eneo ni la wafugaji, lakini wameingia watu wamejiwekea fensi humo, wananchi hawana maeneo ya kufugia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini haya maeneo yatakapotengwa wafugaji wakapata maeneo ya kufugia tutapata maziwa, tutaweza kuanzisha viwanda. Niiombe sana Serikali tunaposema tunaingia kwenye Serikali ya viwanda tuhakikishe hii migogoro inaondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ili tuweze kufanikiwa lazima wananchi wetu wawe na afya nzuri. Kwa upande wa afya bado tuseme ukweli tatizo bado lipo, wananchi hawana dawa, lakini wananchi hao hao ambao hakuna dawa za kutosha kwenye zahanati, hatuna maji ya uhakika. Hawa wananchi hawana maji safi na salama, hawana dawa za kutosha hospitalini wanapoumwa watapelekwa wapi? Niiombe Serikali tuwekeze nguvu kubwa kwenye zahanati zetu, kwenye maji ili maisha ya wananchi yaweze kuwa mazuri. Tunaposema tunaingia kwenye... (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: ...vizuri wananchi wetu wakawa na afya bora, tuboreshe…
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nipongeze Kamati zote. Hata hivyo, kabla sijaanza kuchangia, naomba nieleze jambo hili. Suala la vita ya madawa ya kulevya ni janga la Kitaifa. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwamba mtu yeyote anayesimama kuanza kupambana na vita ya madawa ya kulevya aidha awe ni mwizi au vyovyote atakavyokuwa kwa pamoja tuungane mkono na tumuunge mkono mtu huyo. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo mimi nimekuwa nikijiuliza, hivi huyu Makonda mali wanazosema alikuwa nazo kabla hajaanza kupambana na vita ya madawa ya kulevya mbona hamkumleta Bungeni? Waheshimiwa Wabunge tuwe makini kuna mchezo unaendelea na huu mchezo tuugundue, tuukatae, tuungane na Makonda kwa nguvu zetu zote kupambana na vita ya madawa ya kulevya. Mlikuwa wapi? Kwa nini hamkumleta Bungeni kusema ni mwizi, kusema ana mali kibao? Huo mchezo tumeugundua na hatukubali tunaungana na Makonda kama ana upungufu, atawajibika kwa upungufu wake, lakini vita ya madawa ya kulevya tutaendelea naye. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niongelee suala la ulinzi na usalama. Niombe Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani tuangalie mazingira wanayofanyia kazi ya jeshi letu la polisi kwa kweli sio mazuri. Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine sisi ambao tuko pembezoni tunaomba kwa kweli ulinzi uimarishwe kwenye mipaka yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza napongeza Kamati zote kwa taarifa ambazo wamezileta. Kabla sijaanza kuchangia naiomba Serikali, tunakuja hapa tunachangia maeneo mengi, tunashauri lakini unakuta vitu vingi tunavyoshauri mara nyingi havichukuliwi maanani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, tunakuja hapa tunatumia kodi ya wananchi ambao tunawawakilisha, naiomba sana Serikali muwe wasikivu tunapotoa ushauri muuzingatie, haiwezekani tunapiga kelele hapa halafu mwisho wa siku hakuna kinachofanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mazao ya biashara. Ukisoma kwenye taarifa ya Kamati katika ukurasa wa 13 inaeleza katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni mazao haya yamekuwa na uzalishaji usioridhisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo pamoja na ufanisi mdogo wa vyama vya ushirika na matumizi duni ya teknolojia ya pembejeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesahau haya mazao yamekuwa yanaendelea kupotea na wakulima wamekata tamaa. Wakulima wanakata tamaa kwa sababu Mheshimiwa Rais mwenyewe wakati wa kampeni na baada ya kupata nafasi ya Urais amekuwa akizungumzia sana hizi tozo na kodi ambazo mmeweka. Wakulima wamefika sehemu wanakata tamaa. Mimi nitoe mfano Mkoa wa Kagera, haya mazao kwa mfano zao kuu la kahawa siyo Mkoa wa Kagera tu, zao kwa kweli watu hawaoni faida yoyote ya kuliendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali na nimuombe Waziri wa Fedha na Waziri wa Kilimo, kabla hatujaingia kwenye bajeti na sisi Mkoa wa Kagera tumetoa azimio na ninaomba Mikoa mingine mtuunge mkono hatutakuwa tayari kuunga mkono bajeti kama hamtaondoa hizi tozo na kodi ambazo zimewekwa. Tunataka wakulima hawa wafaidi. Hili ninaomba Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono. Haiwezekani mkulima analima hapati faida yoyote, ni lazima tujenge mazingira mazuri hata mkulima anapolima aweze kupata faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni maji. Kama wengine walivyochangia kwa kweli suala la maji ni tatizo na janga kubwa la Kitaifa. Tuliishauri hapa Serikali tukasema iongeze tozo lakini Serikali ikakataa ikaja na sababu, leo hakuna Mbunge ambaye anaweza akasimama akasema kwenye Jimbo lake kuna pesa ya maji ambayo imepelekwa angalau hata asilimia 30. Mimi ninaiomba Serikali tunaposhauri muwe mnazingatia. Ninajua mna nia njema lakini kuna mambo mengine lazima muwe mnatusikiliza na sisi tunaposhauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tukasimama tukaitetea Serikali wakati Serikali hampeleki pesa, kwenye Majimbo yetu wananchi wanateseka hali ni ngumu. Tunahitaji maji, Mheshimiwa Waziri wa Maji, Kyerwa wananchi wamenituma maji sitakutetea hapa usiponiletea maji, na kuna miradi ambayo tayari tumeshaibuni iko kwenye usanifu, hiyo miradi inahitaji pesa. Kuna miradi mingine ambayo ipo ya miaka ya mingi, hii miradi ipo tu wananchi wanakuuliza tunakosa hata majibu. Kwa hiyo, niombe Serikali izingatie hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niongelee migogoro ya ardhi. Kuna migogoro ya ardhi maeneo mengi. Kwa kweli kwa hapa nimpongeze Waziri kwa kazi wanayoifanya, lakini bado kazi ni kubwa na migogoro hii ni mikubwa, isije ikatokea sasa mauaji yanatokea kila kona. Mimi niwaombe kwa mfano kule Kyerwa kuna eneo ambalo lilishatengwa na Serikali ikatangaza kuwa hili eneo ni la wafugaji. Lakini eneo hili linaloitwa Sina limevamiwa na watu, wengine hawakufuata hata taratibu wameingia wameweka fence ni kama Serikali haioni. Haiwezekani wanaweka hivi vitu Serikali inaona na inajua hili eneo ilishalitenga kwa ajili ya shughuli fulani. Mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri wa Ardhi uje Kyerwa utatue huu mgogoro uishe, tujue nani ana haki ya kuwa kwenye hili eneo kihalali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niiombe sana Serikali, mje hapa mtueleze Waheshimiwa Wabunge kwa nini mpaka sasa hamjapeleka pesa kwenye miradi ya maendeleo. Mlete sababu ambazo tutawaelewa kuliko kukaa kimya pesa haiendi na sisi hatujui kinachoendelea, hata wananchi wanapotuuliza, tunakosa jibu. Ni afadhali mkatueleza kama pesa haipo tujue pesa haipo hilo tukawaambie wananchi, kuliko tunakaa hapa tu kila mtu anazungumzia pesa ya maendeleo na hakuna kitu kinachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali, ninajua nia ya Rais wetu na dhamira yake, kwa kweli tunamuunga mkono, lakini tunataka pesa. Hatuwezi tukaunga mkono tu kitu kinasemwa, kinasemwa halafu hatuoni kinachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine niongelee uharibu wa mazingira. Mazingira yetu kwa kweli yameharibiwa sana. Na niombe sana Waheshimiwa Wabunge katika hili, tushirikiane wote kwa pamoja ili tuweze kunusuru mazingira yetu ambayo yameharibiwa. Vyanzo vya maji vimeingiliwa, wakulima wanaingia humo humo, milima na misitu yetu leo haipo tena, leo tunaongelea janga la kitaifa tunasema kuna njaa, kuna ukame. Ukame umesababishwa na sisi viongozi tukiwepo ni hatua zipi ambazo tumechukua ili kunusuru mazingira yetu yawe salama? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tufike wakati sasa siyo kulinda tena kura, wakati mwingine Waheshimiwa wanasiasa mnalinda nafasi zenu hamtaki kuingilia kwenye mambo ambayo ni ya msingi. Watu wanapoharibu mazingira unasema nikisema hapa nitajiharibia kura, unajiharibia wewe. Mwisho wa siku tunakuja kuomba chakula cha njaa, tuhakikishe tunaenda kwa wananchi wetu tuyalinde mazingira yetu ili mazingira yawe salama. Haya mambo ya kusema tunalinda kura wakati nchi inaharibika, tunakoelekea ni kubaya. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge hili tupambane nalo kwa nguvu zetu zote kuhakikisha mazingira yetu tunayarudisha kwenye hali ambayo ni sawa, ili tupate mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la mwisho watu wanatangaza janga la njaa, kweli njaa ipo lakini siyo kama…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Bilakwate.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nipongeze Kamati zote. Hata hivyo, kabla sijaanza kuchangia, naomba nieleze jambo hili. Suala la vita ya madawa ya kulevya ni janga la Kitaifa. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwamba mtu yeyote anayesimama kuanza kupambana na vita ya madawa ya kulevya aidha awe ni mwizi au vyovyote atakavyokuwa kwa pamoja tuungane mkono na tumuunge mkono mtu huyo. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo mimi nimekuwa nikijiuliza, hivi huyu Makonda mali wanazosema alikuwa nazo kabla hajaanza kupambana na vita ya madawa ya kulevya mbona hamkumleta Bungeni? Waheshimiwa Wabunge tuwe makini kuna mchezo unaendelea na huu mchezo tuugundue, tuukatae, tuungane na Makonda kwa nguvu zetu zote kupambana na vita ya madawa ya kulevya. Mlikuwa wapi? Kwa nini hamkumleta Bungeni kusema ni mwizi, kusema ana mali kibao? Huo mchezo tumeugundua na hatukubali tunaungana na Makonda kama ana upungufu, atawajibika kwa upungufu wake, lakini vita ya madawa ya kulevya tutaendelea naye. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niongelee suala la ulinzi na usalama. Niombe Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani tuangalie mazingira wanayofanyia kazi ya jeshi letu la polisi kwa kweli sio mazuri. Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine sisi ambao tuko pembezoni tunaomba kwa kweli ulinzi uimarishwe kwenye mipaka yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mungu ambaye amenipa nafasi hii kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambayo ni muhimu kwa Taifa letu. Pia naipongeza Serikali yangu kwa kazi nzuri zinazofanyika. Nampongeza kipekee Rais wangu na timu yake kwa muda mfupi, wameonesha uwezo mkubwa kuwatumikia Watanzania hasa hasa wanyonge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Watendaji wote kwa kazi nzuri wanazozifanya. Kweli naiona Tanzania mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kwa sababu sisi ni mashahidi, muda mfupi tumeona hostel za Chuo Kikuu Dar es Salaam zimekamilika, usafiri wa mwendo kasi, barabara za juu Dar es Salaam, tumeshuhudia reli ya standard gauge, zinaanza kujengwa na mengine mengi. Hakika hapa kazi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jimbo la Kyerwa, naongelea suala la mawasiliano siyo mazuri. Upande wa mawasiliano ya simu, maeneo mengine hakuna mtandao wa simu, mawasiliano yote yanaenda au yanaingiliwa na mitandao ya nchi jirani, yaani nchi ya Uganda na Rwanda. Naomba sana Wizara ishughulikie tatizo hili ili tupate mawasiliano ya uhakika ukilinganisha na umuhimu wa mawasiliano na ya kuwa tunapakana na nchi jirani jambo ambalo kiusalama siyo nzuri kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la barabara zangu za Wilaya ya Kyerwa. Nikumbushe ahadi ya ujenzi wa barabara ya Mgakorongo - Kigarama mpaka Murongo wa kiwango cha lami, ambapo Mheshimiwa Waziri akijibu swali nililouliza; ni lini ujenzi utaanza na ahadi ya Mheshimiwa Waziri alisema before June, 2017 ujenzi utakuwa umeanza. Namwomba Mheshimiwa Waziri ahadi hiyo itimizwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara iangalie kwa makini matengenezo ya barabara ya Murushaka mpaka Murongo ambapo barabara hii imekuwa ikisahaulika sana kufanyiwa matengenezo. Kwa sababu barabara ya Murushaka mpaka Murongo ni ya kiuchumi zaidi ya asilimia 75 ya magari yanayotumia barabara hiyo, ingawa imepewa kipaumbele cha pili kujengwa kwa kiwango cha lami. Naiomba Wizara barabara hii kwa sababu ya umuhimu wake katika kipindi hiki ambacho haijafikiwa kujengwa kiwango cha lami, Serikali iweke changarawe kuepusha usumbufu tunaoupata katika kipindi cha mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alipokuja Kyerwa aliwaahidi Wanakyerwa kilometa tano zijengwe Kata ya Nkwenda; nimejaribu kufuatilia lakini mpaka sasa hakuna mwenye jibu kamili. Naomba sana Mheshimiwa Waziri atupatie lami, hizi kilometa tano zijengwe ili kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais na lami hii ni muhimu kisiasa. Pia namwomba sana Mheshimiwa Waziri atukamilishie kuweka lami kwenye mlima Rubunuka pande zote kuondoa usumbufu wa magari kukwama kipindi cha Mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuipunguzia mzigo Halmashauri, tunayo barabara ya Nkwenda mpaka Mabila ambayo imejengwa kwa kiwango cha changarawe. Tunaomba ipelekwe TANROADs kwa sababu ya umuhimu wake kwa Wanakyerwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuandika hayo, narudia kuipongeza Wizara kwa kazi nzuri inazofanya. Tunawaombea sana Mungu awafanikishe katika yote mpate fedha ili na sisi Kyerwa tuone lami halisi katika barabara ya Mugakorongo – Murongo - Murushaka na Murongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara hii muhimu. Kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na nguvu na kuweza kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kipekee kumpongeza Rais wetu, kwa kazi nzuri anayoifanya, hakika imeonekana mbele ya Watanzania kuwa huyu ni Rais mtetezi wa wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Waziri wetu Mheshimiwa Ummy, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote kwa kweli kazi mnayoifanya ni nzuri, Mheshimiwa Ummy na timu yako ninasema msonge mbele na Mungu atawafanikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia bajeti. Kwanza niipongeze Wizara ya Afya kwa kuboresha kituo chetu cha afya cha Nkwenda. Kituo hiki sasa hivi akina mama wanapata huduma nzuri, kituo hiki kimeboreshwa, Mheshimiwa Ummy nakushukuru sana umetupatia ambulance, tulikuwa na hali mbaya. Sasa hivi kile kituo kwa kweli ni cha kisasa ingawa bado wananchi wanahitaji huduma zaidi kwa sababu ukilinganisha na jiografia ya jimbo langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kwa upande wa dawa. Kwa kweli Serikali inajitahidi lakini bado mahitaji ni mengi na dawa bado haziwafikii wananchi wetu. Niombe Serikali iongeze nguvu na tumeona kwenye bajeti imetenga hela nyingi lakini bado. Niiombe Serikali, Mheshimiwa Waziri hizi dawa mnazopeleka hebu zisimamiwe vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengine mimi bado ninaamini pesa inayotengwa dawa zinanunuliwa lakini zile dawa zinachakachuliwa zinauzwa mitaani. Mimi nitoe mfano kama kule kwangu Kyerwa. Ukimuuliza DMO atakwambia dawa zipo, lakini unapooenda kwa wananchi wanakwambia kila tunapoenda kituo cha afya hatupati dawa za uhakika. Kwa hiyo, mimi niombe Mheshimiwa Waziri uweke utaratibu ambao tunaweza kufuatilia hizo dawa tukajua kwa siku ni watu wangapi, ikiwezekana hata majina yale waliotibiwa na kupewa dawa yawe yanabandikwa ili tupate uhakika hizi dawa zinaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuiomba Serikali yangu, bado wananchi wanahitaji sana kwa upande wa vituo vya afya, Serikali inajitahidi kuboresha, lakini bado kuna maboma ambayo wananchi wameanzisha wao wenyewe, mengine yamekaa muda mrefu miaka mitano mpaka kumi. Niiombe sana Serikali, hawa wananchi tusije tukawakatisha tamaa, tujitahidi kumalizia haya maboma ili wananchi wetu waweze kupata huduma. Lakini kuna jambo ambalo mimi nishauri, kwenye ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi tunasema kituo cha afya kila kata na zahanati kila kijiji. Hili jambo ni zuri lakini mimi niishauri Serikali, kwa kipindi hiki ambacho bado hatujaweza kufikia hapo hebu tupeleke nguvu yetu kila kituo cha afya kila tarafa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mimi nina tarafa nne, katika tarafa nne nilizonazo mimi nina kituo cha afya kimoja ambacho kina uhakika. Tunaposema tunapeleka kwenye kila kata nina uhakika hatutaweza kufikia hayo malengo kwa wakati tulioupanga; lakini tukipeleka kwenye kila tarafa ikapata kituo cha afya mimi ninaamini wananchi wetu tutaweza kuwasogezea huduma kwa ukaribu. Kwa hiyo, huo ni ushauri Mheshimiwa Waziri uuchukue na iwe kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwenye majimbo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la watumishi. Mheshimiwa Waziri bado watumishi ni wachache, wananchi wanakosa huduma kwa sababu ya watumishi. Kwa mfano mimi kwenye kituo changu pale Nkwenda tuna watumishi wachache sana. Nimuombe Mheshimiwa Waziri Ummy, mmetangaza ajira kwa ajili ya madaktari, hebu tuangalie haya majimbo ambayo yako pembezoni kama kwetu Kyerwa, kwa kweli hali ni mbaya sana. Tusiangalie maeneo ya mijini hebu tuangalie na huku pembezoni ili Watanzania wote waweze kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la bima ya afya. Suala la bima ya afya ni zuri sana, niombe sana Serikali tuendelee kuwahamasisha wananchi ili kila mwananchi aweze kupata bima ya afya. Vilevile tuangalie hawa wazee wetu ambao tumesema wapate matibabu bure, bado huduma hii ni ngumu, wazee wetu bado hawapati huduma bure. Wanapokwenda kwenye zahanati au hospitali wanahudumiwa na daktari lakini mwisho wanaambiwa waende kununua pharmacy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wazee kama tumesema wapate huduma bure, Mheshimiwa Waziri hebu tuweke utaratibu ili waweze kupata huduma bure ili na wao wafurahie matunda ya taifa lao wakati wanaelekea jioni kuaga dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi michango yangu sehemu kubwa ni hiyo, lakini niombe sana Mheshimiwa Ummy, kwa kweli umekuwa ukitoa ushirikiano pale tunapokuja kwako kuleta matatizo ya wananchi wetu. Nikuombe sana Mheshimiwa Ummy na Mheshimiwa Kigwangalla moyo huo uendelee bado wananchi wetu wanayo mahitaji mengi, bado huduma za afya hazijaweza kukidhi viwango vinavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja, ninaishukuru sana Serikali yetu kwa kazi zinazofanyika, ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninamshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu, pia kuniwezesha kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. Nichukue nafsi hii kipekee kumpongeza Mheshimiwa Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mchango wangu kuiomba Wizara kufuatilia vivutio ambavyo vinaonekana vidogo vidogo, lakini vikiwekewa mazingira mazuri, miundombinu na kuvitangaza, vinaweza kuwavutia watalii kuja kuvitembelea na kuiingizia Serikali pesa nyingi na kuinua uchumi wa Taifa letu. Nasema hivi kwa sababu mfano kule kwetu Kyerwa, tuna vivutio vingi ambavyo vikitangazwa vitaingizia Wizara pesa za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna maji ya moto ya Omokitagata, maji haya watu wanapoyaoga au wanapokanyaga kwenye maji hayo hupokea uponyaji wa magonjwa mbalimbali. Pia tuna Hifadhi ya Rumanyika Orugundu, tuna maporomoko ya Mto Kagera ambavyo ni vivutio, ninaomba Wizara kuvitembelea na vyenyewe viwe kwenye vivutio vya Taifa ili kuongeza wigo mpana wa utalii kuliko kila wakati wanapelekwa maneo yale yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, kwa tatizo lilijitokeza kwenye Hifadhi ya Rumanyika Orugundu, kutokana na chanzo cha maji kilicho kilometa moja ndani ya hifadhi ambacho kilikuwa kinatumiwa na wananchi wa kata ya Bugomora na sehemu ya Kata ya Kibale. Chanzo hiki kimekuwa mkombozi wa wananchi wa kata hizo kuwapatia maji safi na salama, lakini baadae Meneja alivunja kisima hicho kilichojengwa na wafadhili na kuwazuia wananchi kutumia chanzo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumweleza Mheshimiwa Waziri na kuona umuhimu wa kuwapatia wananchi maji safi na salama kwa sababu ndicho chanzo pekee cha kuwapatia maji, Mheshimiwa Waziri aliruhusu wananchi wangu kuendelea kutumia chanzo hicho cha maji, nakushukuru sana kwa kuwajali wananchi wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondoa muingiliano wa wananchi na hifadhi, naomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu wananchi hao hawana chanzo kingine cha kuwapatia maji safi na salama na ili kuendeleza ujirani mwema kati ya wahifadhi na wananchi walio jirani na hifadhi, Wizara ione namna ya kuwasogezea maji ya chanzo hicho karibu na wananchi kwa kutumia chanzo hicho, au kama inawezekana eneo hilo la kilometa moja lirudishwe kwa wananchi kama ilivyokuwa mwanzo, maana chanzo hicho mwanzo kilikuwa kwa wananchi na ndio maana wafadhili waliweza kukijengea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee juu ya hifadhi zetu; hifadhi zetu lazima zitunzwe bila kuingiliwa na kitu chochote. Nchi yetu tunakabiliwa na janga la ukame kwa sababu ya uharibifu wa mazingira, tusipokuwa makini nchi yetu inaelekea kuwa jangwa kwa sababu ya baadhi yetu kutosimama kwenye nafasi zetu tulizopewa kusimamia hifadhi zetu ambazo zilitengwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wafugaji wanakosa maeneo ya kufugia kwa sababu maeneo yaliyotengwa na Serikali yaliachwa bila usimamizi na yakaingiliwa bila kufuata sheria zilizowekwa, ndiyo maana leo hii tunasema Serikali iruhusu hifadhi zetu ziingizwe mifugo, hili siyo sahihi na halikubaliki. Mfano kwangu Kyerwa mwaka 1987 Serikali ilitenga maeneo ya wafugaji na yakatangazwa kwenye Gazeti la Serikali na kupewa GN 620. Maeneo haya yamevamiwa na kubadilishwa matumizi wafugaji hawana maeneo ya kufugia, tunadai Serikali iruhusu mifugo kuingizwa kwenye mapori ya hifadhi zetu, naiomba Serikali kufuatilia maeneo yote yaliyotengwa ili yarudishwe kwenye matumizi ya mwanzo ndipo tutaondoa mgogoro wa ukosefu wa maeneo ya kufugia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kunipa uhai na nguvu za kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. Pili, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya kuendelea kuijenga nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo ambalo napenda kulizungumzia ni kuhusu hii operation inayoendelea. Mheshimiwa Mpina mimi naamini unafanya kazi nzuri na historia yako kila mmoja anaijua. Waheshimiwa Wabunge wamechangia mambo mengi niombe uyazingatie.

Mheshimiwa Spika, operation hii uliianzisha kwa nia njema lakini naamini kwa michango ya Waheshimiwa Wabunge baadhi ya watendaji wako wanakuangusha. Wana nia mbaya ya kutaka kuharibu lile zuri ambalo umeliandaa ili lisiweze kufanikiwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mpina ushauri wangu ninaokushauri, hebu fuatilia maoni ya Wabunge, baadhi naamini ni mazuri yanaweza kukusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine ambalo napenda kulisema kwa Waheshimiwa Wabunge, tumekuwa na hoja zinajitokeza hapa Bungeni, linapotoka jambo linafanyika Mheshimiwa Mbunge anasimama anasema wapiga kura wangu. Mimi nikuombe Mheshimiwa Mpina, simamia sheria, fuata taratibu, kile ambacho kinamgusa mwananchi ambaye hakufuata taratibu lazima twende kwenye mstari ulio sahihi. Nchi hii imefika hapa tulipo, mimi ninalisema hili, mimi ni mwanasiasa, lakini mambo mengi yamechangiwa na wanasiasa. Hata kama mtaona ni baya lakini wanasiasa tumehusika kuharibu nchi hii. Ukitaka kugusa hapa wanasema wapiga kura, ukitaka kugusa hapa hao watu wangu, mambo mengi ambayo yameharibika sisi ndiyo tumesababisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshauri Mheshimiwa Mpina jambo lingine, hili suala la ng’ombe kuchomwa moto kwa kweli siyo zuri. Hata kule kwangu nina ng’ombe wengi lakini wengine wana vidonda, yaani unajaribu kujiuliza hivi hawa ni wataalam ni watu gani ambao wametoa ushauri huu? Hili jambo sio sawa, angalia namna nyingine ambayo mnaweza kuwatambua hawa ng’ombe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine nikushauri Mheshimiwa Mpina, yako maeneo ambayo yalitengwa kwa ajili ya wafugaji lakini yamevamiwa. Kule kwangu kuna eneo limetengwa na Serikali likapewa GN. No. 620 ya mwaka 1987, eneo hili limevamiwa, wameingia watu wenye pesa, wameingia mpaka wengine kutoka nje ya nchi, wafugaji hawana pa kufugia wanahangaika. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Mpina ulifuatilie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mungu kwa kunipa uhai na nguvu za kuwepo mahali hapa na kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. Pia namshukuru Mungu kuweza kuchangia Wizara hii muhimu kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri zinazofanyika, kuisimamia vizuri Wizara hii muhimu hakika matunda yake yanaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi la kutoa elimu bure, kwa kweli imewapunguzia mzigo wazazi na matokeo yameonekana watoto wengi wanapelekwa shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeza Wizara baada ya tetemeko lililoupata Mkoa wetu wa Kagera, Mheshimiwa Naibu Waziri alifika Kyerwa na kuahidi kusaidia miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko, namshukuru sana Naibu Waziri kwa msaada huo mkubwa kwa wananchi Kyerwa ingawa bado tunaendelea kuomba msaada wa kusaidiwa miundombinu mingi Kyerwa imechakaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kyerwa miundombinu mingi ya shule zetu imechakaa sana, kitu kinachosababisha watoto wetu kusoma kwenye mazingira magumu sana. Mfano, shule ambayo namuomba sana Mheshimiwa Waziri kutusaidia kuboresha miundombinu ni shule za msingi Kaisho, Mabila, Murongo, Businde, Songambele, Nyakatuntu, Bugomora na Isigiro ambazo shule hizo zina upungufu wa vyumba vya madarasa ni 94 vyenye gharama ya shilingi 1,880,000,000. Kwa upande wa vyoo kwenye shule hizo ni mbaya sana mapungufu ni matundu ni 198 yenye thamani ya shilingi 217,800,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sekondari na kwenyewe hali ni mbaya tunaomba kusaidiwa na kuomba sana Waziri Mheshimiwa Ndalichako, naomba sana msaada wako maana sehemu kubwa wananchi ndiyo waliochangia kuweka hiyo miundombinu, ninaiomba kusaidiwa angalau ili kuunga mkono juhudi za wananchi Kyerwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamejitahidi sana lakini mahitaji ni makubwa sana kitu kinachopelekea shule nyingine wanafunzi wanasomea nje. Mfano, shule ya msingi Maendeleo iko katika Kata ya Businde, walimu sita wako kwenye nyumba moja kitu ambacho kimesababisha kushindwa kuleta familia zao hasa wenza wao. Naiomba sana Wizara kuziangalia shule za namna hii jinsi ya kuzisaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee shule za sekondari za kata, wananchi wamejitahidi maeneo mengi kujenga madarasa na maabara lakini zaidi ya asilimia 85 hazina vifaa vinavyotakiwa kwenye maabara, naiomba sana Wizara kuzipatia vifaa hizo shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kyerwa hatuna Chuo cha Ufundi, niiombe sana Serikali inapoangalia maeneo ambayo hawana vyuo vya ufundi naomba Kyerwa tuangaliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika michango yangu naweza nikawa nimeongelea masuala yanayohusu Wizara ya TAMISEMI, lakini Wizara ya Elimu ndiye bosi wa elimu nchini. Miundombinu ikiwa mizuri, maabara zikiwa na vifaa vinavyotakiwa, tukapata walimu wa sayansi, elimu itakuwa nzuri na Wizara ya Elimu itakuwa imefanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Wizara kwa motisha wanayopewa walimu, lakini bado walimu wanadai stahiki zao, niombe sana walimu wanaodai walipwe ili waweze kutulia na kuwafundisha watoto wetu bila usumbufu wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee utaratibu wa Chuo Kikuu Huria ambao ulikuwa unawapa nafasi wale ambao hawakufanikiwa kufaulu kidato cha nne kwenda kidato cha sita, utaratibu wa kusoma foundation mwaka mmoja halafu mtu akifaulu anaenda kusoma digrii. Hili jambo limewasaidia wengi wakiwemo wanasiasa ambao wengi wao humu ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Waziri suala hili liruhusiwe lakini lisiwe vyuo vyote ila Chuo Kikuu Huria kiendelee kutoa elimu hii ambayo wengi leo hii chuo hiki kimepata Profesa, Madaktari na wengine wengi wamepitia chuo hiki. Wako Wabunge wengi ambao wanataka kujiendeleza lakini kwa zuio la Mheshimiwa Waziri tumeshindwa. Ninakuomba Waziri uliangalie ili kutusaidia wanasiasa tujiendeleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo narudia kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wa Wizara kwa kazi nzuri inayofanyika tunawaombea kwa Mungu awape hekima katika kutimiza majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na nguvu ya kuwatumikia wananchi wangu wa Kyerwa. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wa Wizara hii muhimu kwa kazi nzuri na hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa; ni nzuri ingawa baadhi ya watendaji wenye nia mbaya wamegeuza baadhi ya hatua za kupambana na uvuvi haramu kuwa biashara ya kujinufaisha na uvuvi kuichafua Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, niishauri Serikali kusimamia vizuri sekta ya mifugo na uvuvi ili tuweze kuongeza kipato kwa Serikali yetu. Ni jambo la kusikitisha nchi yetu ina mifugo mingi, tuna maziwa na bahari zimetuzunguka, lakini hatuoni faida inayolingana na kile tulichonacho.

Mheshimiwa Spika, wafugaji wamekuwa kama yatima, hawana mtetezi yeyote. Hata pale wanapotengewa maeneo wamekuwa wakinyang’anywa, wamekuwa ni watu wa kutangatanga. Kule Kyerwa miaka ya 1987 Serikali ilitenga eneo la Sirina, Ibada 1 na Rutifa Katabe kuwa maeneo ya wafugaji na yakatangazwa kwenye Gazeti la Serikali na kupewa GN 620. Hata hivyo maeneo haya inatafsiriwa wameingia na kujimilikisha kwa kuwahonga baadhi ya watumishi wabaya na leo hii wafugaji wananyanyasika na ng’ombe, akiingia kwenye maeneo yao waliyoyapora ng’ombe wanatozwa faini ya pesa nyingi na wengine kuwakata mapanga.

Mheshimiwa Spika, nimuombe sana katika hili Mheshimiwa Waziri aingilie kati kuwaokoa wafugaji wa Kyerwa ambao wamenyang’anywa na kuonewa miaka mingi, wanahangaika kwa kutangatanga bila kupata msaada wowote.

Mheshimiwa Spika, niko tayari kutoa ushirikiano kwa Mheshimiwa Waziri kwa sababu jambo hili limekuwa kero ya miaka mingi. Kila kiongozi anayekuja ananunuliwa lakini mimi sinunuliwi kwa gharama yoyote.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya nimtakie Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri mafanikio katika vita hii ambayo watakutana na vipingamizi vingi, tunawaombea kusonga mbele mungu akiwa upande wao.

Mheshmiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote namshukuru Mungu kwa kunipa uhai na nguvu za kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. Pia namshukuru Mungu kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa moyo wake wa dhati wa kusimamia ahadi ya kufanya Tanzania kuwa ya viwanda ili kuinua uchumi wa viwanda. Nchi zilizoendelea kiuchumi ziliwekeza sana katika uchumi wa viwanda maana hapo ndipo penye mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mwijage, Katibu Mkuu na Watendaji wengine kwa kusimamia kikamilifu sera ya Tanzania ya viwanda, kweli kasi inayoendelea inaonekana. Nawashauri wasikatishwe tamaa na kelele za wasioitakia mema nchi yetu.

MheshimiwaMwenyekiti, ili kuinua uchumi wa nchi yetu haraka na kuwanufaisha Watanzania wengi, nashauri Wizara kuwekeza sana katika viwanda ambavyo malighafi zake zinapatikana hapa nchini mfano malighafi zinazotokana na mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi. Pia nchi yetu imejaliwa kuwa na madini mengi sana tuombe Serikali kuwavutia wawekezaji kuwekeza viwanda ambavyo tutatumia madini yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano Kyerwa tumejaliwa madini ya tini ambayo yanapatikana maeneo mengi ya Wilaya. Madini haya yamekuwa yakinufaisha nchi majirani zetu kwa njia ya magendo. Niombe Wizara kuwavutia wawekezaji kuwekeza Kyerwa kwa sababu mahitaji ya mabati ni mengi na hii itainua uchumi wa nchi yetu na kuwapa ajira wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa na Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, sera na mkakati wa Serikali yetu ni kuwawezesha wananchi kwa kuwawekea mazingira rafiki wakulima wetu ili wanapolima wawe na uhakika na soko la bidhaa zao. Wananchi wetu wanajitahidi sana kulima lakini hakuna soko la uhakika. Jimbo langu la Kyerwa liko mpakani, Serikali imekuwa ikikosa mapato kwa sababu ya biashara ya magendo ya kupeleka bidhaa nchi jirani kwa sababu wananchi hawana sehemu ya kuuza bidhaa zao. Ili kuepuka kuikosesha Serikali mapato na kuwaondolea wananchi usumbufu na wale wanaopoteza maisha Mto Kagera kwa biashara ya magendo, naiomba sana Serikali kufufua masoko ya Kimataifa yaliyojengwa Murongo na Nkwenda ambayo yametelekezwa bila kukamilika na mpaka sasa hatujui nini kinaendelea na nani msimamizi wa masoko haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, masoko haya yakikamilika wananchi wetu watakuwa na soko la uhakika kitu ambacho kitainua kipato chao na uchumi wa nchi yetu utaongezeka na tutaepusha biashara ya magendo na madhara wanayoyapata. Naomba Mheshimiwa Waziri anapohitimisha awaambie Wanakyerwa nini hatma ya haya masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe na kuishauri Serikali yangu tunayowavutia wawekezaji kuwekeza ufugaji na viwanda vya nyama, mfano Mkoa wa Kagera tuna mifugo mingi niwaombe Wizara kuwakaribisha wawekezaji wawekeze Kyerwa kiwanda cha nyama na maziwa tunao ng‘ombe wengi, mbuzi na mifugo mingine ili kuwainua wananchi wetu kimapato na uchumi wa Taifa letu utaongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili Watanzania waendelee kuwa sawa lazima tuwavutie wawekezaji maeneo yote ili isionekane maeneo fulani ndiyo tumewekeza nguvu halafu maeneo mengine yameachwa. Nasema hili kwa sababu inaonesha mfano Mkoa kama Kagera umesahaulika kiuwekezaji wakati kuna fursa nyingi na ndiyo wazalishaji wakubwa wa ndizi, uvuvi, madini, ufugaji na kadhalika. Mkoa wa Kagera tumejaliwa kila kitu na tunaweza kulima na kuvuna zaidi ya mara mbili kwa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwekeza kwenye viwanda vikubwa ambavyo vinaajiri sehemu ndogo ya Watanzania lakini pia tuweke kipaumbele katika kuweka mazingira wezeshi kwa viwanda vinavyoajiri watu wengi kama viwanda vitakavyotumia malighafi zinazopatikana ndani mfano kahawa, alizeti, pamba, korosho na kadhalika. Kwa kufanya hivyo tutainua kipato cha wananchi wetu na uchumi wa Taifa na tutapata baraka maana hapa wataguswa Watanzania wengi na watanufaika sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, narudia kumpongeza Mheshimiwa Waziri hakika kazi anaiweza sana tumuunge mkono Watanzania kwa umoja wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii muhimu. Kwanza naunga mkono asilimia 100 kwa sababu kupandisha hadhi mapori haya ni muhimu sana hasa kwa sisi tunaotoka Kagera. Tulikuwa tunapata wakati mgumu kupita kwenye mapori ya Biharamulo, hali ilikuwa mbaya lazima muwe na Polisi vinginevyo mlikuwa mnavamiwa. Baada ya kupandisha hadhi mapori haya tunaamini usalama utakuwepo na tutasafiri salama. Pia wale majangili ambao walikuwa kwenye yale mapori tunaamini hawatakuwepo tena na usalama utakuwa mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono pia kwa sababu mapori mawili ya Ibanda na Rumanyika yako Kyerwa. Mapori haya ni muhimu na yana wanyama ambao kwa kweli ni muhimu sana. Ninaamini Serikali baada ya kupandisha hadhi mapori haya sasa tutaenda kupata watalii na Serikali inaenda kuongeza kipato tutakapokuwa tumeweka mazingira mazuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya kupandisha hadhi mapori haya tunatamani tuone wananchi wetu wanapata elimu ya kutosha ili wasiweze kuvamia tena mapori yale kwa sababu wengine walikuwa wanategemea kwenda kutafuta kuni na kadhalika. Kwa mfano, kule Kyerwa kwangu kuna miti inaitwa Emisambyia, ni miti muhimu sana na ni mirefu sana ikilindwa mazingira yetu yatakuwa mazuri. Nachoomba sana Serikali iendelee kutoa elimu ili wananchi wajue umuhimu wa kupandishwa hadhi mapori haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine tunatamani waweke mazingira rafiki hata kwa watalii wanaokuja. Pawepo na barabara, mahoteli mazuri ili kuwavutia watalii kufika kwenye maeneo yale. Tunatamani hata wananchi ambao wanazunguka maeneo haya waweze kunufaika. Wananchi waone shule zinajengwa kupitia mapori haya na miundombinu mingine mizuri inaimarishwa ili wananchi waendelee kuiunga mkono Serikali na kuyalinda mapori haya kwa sababu tunajua wananchi wengi ndiyo wamezunguka mapori haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, mimi naiunga sana mkono Serikali kwa kupandisha hadhi mapori haya. Kule kwangu kuna Majimoto Mtagata, niwakaribishe sana Waheshimiwa Wabunge yale maji yanatoa moto na watu wengi wamekuwa wakienda pale wakiamini katika yale maji kupokea uponyaji. Tunawakaribisha sana Waheshimiwa Wabunge mfike Kyerwa, mjionee maajabu ya Mungu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mungu kwa kupata nafasi hii ya kuchangia Wizara hii muhimu sana kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi ya kipekee kumshukuru Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri na watendaji wote kwa kutimiza ahadi ya kuondoa kodi/tozo ambazo zilikuwa zinamdidimiza mkulima. Mheshimiwa Rais wetu kila anapoahidi lazima atekeleze, namshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu, tunapoongelea Tanzania ya viwanda na kwenda kwenye uchumi wa kati lazima tuwekeze nguvu yetu kwenye kilimo cha kisasa, kilimo kilichofanyiwa utafiti, kilimo chenye kumuwezesha mkulima kupata mbegu bora, kilimo ambacho kitamuwezesha Mtanzania kupata soko la uhakika lazima tuweke miundombinu wezeshi kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hayo kwa sababu Watanzania zaidi ya asilimia 65 ni wakulima. Pamoja na hayo ukweli ni kwamba sekta hii imesahaulika kabisa hasa hasa maeneo ya vijijini ambako wakulima wamekata tamaa. Kilimo ndio uchumi wa Taifa, ninaamini tukiwekeza nguvu yetu kwenye kilimo Taifa letu litainuka kwa muda mfupi. Taifa letu limejaliwa maji mengi sana yaliyo ardhini lakini pia tuna vipindi vingi vya mvua, karibu nchi nzima tunapata mvua ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwa kodi na tozo mbalimbali zilizoondolewa kwenye mazao. Hata hivyo bado zipo kodi nyingine ambazo hazijaondolewa. Niombe Serikali kuziondoa ili mkulima aweze kufaidi bei nzuri za mazao. Pia niiombe Serikali kutoa bei elekezi kwa kila zao kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kujifunza katika mataifa mengine ambayo mataifa hayo ni yenye ukame, lakini mataifa hayo yametumia kilimo cha umwagiliaji ambacho kimeinua mataifa hayo yamepaa sana kiuchumi kupitia sekta hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee ufugaji, kama tunataka kuondoa migogoro mingi ya wakulima na wafugaji lazima tuhakikishe tunalinda maeneo ambayo yalitengwa kwa ajili ya wafugaji na wakulima ili wananchi wetu wasiendelee kuuana na kuondoa chuki kati yao ambayo inaendelea kukua na kuleta matatizo makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongelea hili kwa sababu maeneo mengi yaliyotengwa yamevamiwa na watu, Serikali ipo na inaiona migogoro hii ambayo mpaka leo hii ni mikubwa. Nasema haya nikiwa na ushahidi, kwenye Jimbo langu Serikali ilitenga maeneo ya wafugaji, yakatangazwa kwenye Gazeti la Serikali na kupewa GN. 620 ya mwaka 1987, lakini maeneo hayo yamevamiwa na matajiri na kuzungushia uzio na tayari wamepatiwa hatimiliki ya miaka 99, Serikali imekaa kimya wafugaji wanateseka hawana maeneo ya kufugia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri kulifuatilia jambo hili ambalo limeleta mgogoro mkubwa Jimboni kwangu. Pia nataka kujua eneo ambalo lilitangazwa na Serikali na kupewa GN linawezaje kubadilishwa matumizi bila tangazo lingine la kubadilisha tangazo la kwanza? Tusipomaliza migogoro hii italeta matatizo makubwa kwa Taifa letu.

Mheshimwia Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja.
TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI NDUGU PROF. MUSSA ASSAD, MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaingia kwenye hoja, naomba nisome andiko katika Amosi 3:3 ambalo linasema: “Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema neno hilo sasa niingie kuchangia hoja hii. Mimi ni Mwanakamati wa Kamati ya Maadili kwa jinsi ambavyo tulimhoji CAG na jinsi ambavyo alionyesha kwa kweli dharau kubwa ya kulidharau Bunge na hakuonyesha kujutia kitendo kile.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini CAG ni jicho la Bunge na Serikali. CAG ni mtu ambaye anaanimika sana. Mimi nilikuwa najiuliza swali moja, hivi jicho linaweza likauambia mwili wewe hufai? Kitendo cha CAG kusema Bunge ni dhaifu ni pamoja na kusema Rais wa nchi hii ni dhaifu kwa sababu Rais ni sehemu ya Bunge, Waziri Mkuu ni sehemu ya Bunge lakini na sisi Wabunge hapa ni sehemu ya Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kitendo alichokionyesha CAG ni cha dharau, kulidhalilisha Bunge na kuidhalilisha Serikali yetu. Kwa hiyo, naungana na hoja ambayo imeletwa mbele yetu kwa kweli hatuwezi kuendelea kufanya naye kazi kwa sababu hakulidhalilisha Bunge peke yake ni pamoja na Mheshimiwa aliyemteua kwa sababu na yeye ni sehemu ya Bunge lakini na Mawaziri wote ni sehemu ya Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme CAG hakuonyesha uzalendo wowote. Tumekuwa tukiona Mataifa mengine haijawahi kutokea kiongozi mkubwa namna hii hata kama kuna upungufu kusimama na kuanza kuidhalilisha Serikali namna hii.

Kwa hiyo, kitendo alichokionyesha CAG kinakiuka hata maadili ya kiapo chake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mungu kwa kunijalia afya na nguvu za kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kipekee kuipongeza Serikali yangu kwa kazi nzuri inayofanyika kuanzia Rais wetu, Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla. Nampongeza sana Waziri wa Maji, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii muhimu sana kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la maji ni kubwa sana kwa Taifa letu, maeneo mengi hawana maji safi na salama, pia hata wale wanaopata maji wanayapata kwa umbali mrefu sana zaidi ya kilometa kumi mpaka 20. Kitu ambacho kinarudisha nyuma shughuli za maendeleo na kushusha uchumi wa Taifa na katika hili waathirika wakubwa ni wale walio vijijini ambao ni wakulima zaidi ya asilimia 70 na ndiyo wazalishaji wakubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Wizara ikiwezekana iongeze pesa kwenye bajeti kwa sababu bajeti hii imeshuka sana kulingana na mahitaji ni makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Jimbo langu hali ni mbaya sana ya upatikanaji wa maji safi na salama, niishukuru sana Serikali kwa miradi ya zamani ya miaka ya 1970 ambayo ilikuwa imechakaa sana. Kazi ya kuboresha miundombinu imeanza katika kata ya Mabila, mradi wa Kilela - Isingiro, Kagenyi, Lukurayo na miradi mingine midogo. Miradi hii ni sehemu ndogo sana ya mahitaji ambayo ikikamilika itasaidia kama asilimia 15.

Mheshimiwa Naibu Spika, suluhisho la kuwapatia wananchi wa Kyerwa maji, niendelee kushukuru Serikali kwa mradi mkubwa wa vijiji 57 kwenye kata 15 ambao uko kwenye hatua ya usanifu ambao hatua hii itakamilika mwezi wa Septemba, 2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulileta mapendekezo kuomba shilingi bilioni 12 kama kianzio ili tunapomaliza usanifu kazi ianze kuwanusuru wananchi wa Kyerwa na tatizo la upatikanji wa maji safi na salama, pia kuwandolea wananchi usumbufu wa kufuata maji mbali zaidi ya kilometa 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika sana kuona kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018 mapendekezo yetu hayajakubalika kitu ambacho kitasababisha kusubiri mwaka 2018/2019. Naiomba sana Wizara, niko chini ya miguu yenu na kwa unyenyekevu mkubwa nakuomba Mheshimiwa Waziri uangalie namna yoyote ya kupata pesa ili tunapomaliza usanifu kazi ianze haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyoshauri Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuongeza shilingi 100 kwenye mafuta na mimi nashauri Serikali yetu ikubali ili kuwaokoa Watanzania wanaopata mateso makubwa ya ukosefu wa maji safi na salama. Pia umbali wanaoupata kufuata maji mbali na baada ya kukubali ombi hilo na Kyerwa maombi yetu yapokelewe ya kutengewa shilingi bilioni 12 ili kuanza mradi wetu mkubwa wa vijiji vyetu 57 na kata 15, naomba sana Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maombi hayo bado kuna kata zingine ambazo hazijafikiwa na mradi mkubwa wa vijiji 57, niendelee kuiomba Serikali kututengea pesa ili kuwapatia huduma hii muhimu wapiga kura wangu. Najua Serikgu yatazingatiwa na kupewa umuhimu sana.

Mhesali yangu na Mheshimiwa Waziri wangu ni sikivu, maombi yanhimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi na mimi kuchangia Wizara hii muhimu. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa nguvu kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa kazi nzuri wanayoifanya lakini pia nimpongeze kwa unyenyekevu ambao kwa kweli amekuwa akiuonesha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ni Wizara ambayo ni muhimu mimi naweza nikasema ndiyo moyo wa nchi, ni Wizara ambayo imetuletea heshima kubwa ndani na nje ya nchi kwa kweli Jeshi letu linasifika sana na ninawapongeza na niseme moyo huo wa kujitolea kuhakikisha Taifa linakuwa salama, uendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo machache ambayo mimi nitashauri; kwa upande wangu mimi ninapakana na nchi ya Rwanda na Uganda, mipaka yetu iko salama, lakini nilikuwa ninaomba kuna Kata ya Kitwechenkula pale kuna mambo ambayo yanafanyika kwenye mpaka wetu kwa raia wetu siyo mambo mazuri. Niliombe Jeshi letu liangalie na ikiwezekana pale hatapawepo na kambi itapendeza kwa sababu wenzetu upande wa pili wao wana kambi na sisi tukiweka pale kambi nafikiri tutaheshimiana vizuri. Kwa hiyo niombe sana Serikali na Wizara hii iliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo mimi nilete pale kwenye Kata ya Kaisho kuna kambi isiyo rasmi, ile kambi iko katikati ya raia na unajua raia hawajazoea kuona majeshi kama hakuna ulazima wa ile kambi kuwepo pale iko barabarani kwanza hata kwa wanajeshi wetu inaweza wasiwe salama kwa sababu wako katikati ya wananchi hakuna uzio ni barabarani kwahiyo niombe sana Wizara iliangalie kama hakuna ulazima wa kambi ile kuwepo pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine Jeshi letu limefanyakazi kubwa sana na mkiona Taifa hili liko salama ni kwa sababu ya kazi nzuri inayofanywa na Jeshi letu sasa mimi nilikuwa ninaomba wakati mwingine wameeleza hapa ukiangalia nyumba za askari wetu kwa kweli unajiuliza hawa watu wanaosababisha Taifa liwe salama leo hii tuko hapa tumetulia kwasababu ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama mipaka yetu iko salama. Nchi nyingine hawawezi wakakutana namna hii hebu tuangalie namna gani tunaweza tukaboresha makazi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nimekuja na hoja nyingine ikiwezekana hawa wanajeshi wanapostaafu wawe na bima ya maisha, kwa sababu tumeshawatumikisha wamechoka wanapostaafu hata hawana uwezo tena hawana nguvu kwa sababu nguvu kubwa wameiwekeza huku kupigana na kuhakikisha mataifa mengine yanakuwa salama. Kwa hiyo, tuhakikishe tunawapa bima ya maisha kama zawadi kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Kwa hiyo hilo ndilo ombi langu ambalo nimelileta kwenu na Waziri aliangalie pamoja na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na nguvu kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa na ninachowaahidi sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia Wizara hii kwanza kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya. Kwa kweli ameonesha huyu ni mtetezi wa wanyonge. Ninachowaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania, Mheshimiwa Rais anafanya kazi ambayo anahitaji msaada wa Mungu pekee ili ampe ulinzi. Hili jambo si la kawaida na halikuwahi kusikika kwenye masikio ya Watanzania, naomba tumwombee sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara ya Ardhi kwa kazi nzuri wanayoifanya. Ingawa kwa upande wangu kwenye Jimbo la Kyerwa bado hajafika lakini nasikia kwingine anafanya vizuri, kwa hiyo nampongeza; na naamini huko Kyerwa atafika, kwa sababu yanayojiri huko Kyerwa anayajua na anayafahamu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee Jimbo langu la Kyerwa. Kwa kweli, tunayo matatizo ambayo ni makubwa kutokana na kwamba ile Wilaya bado ni mpya. Mheshimiwa Waziri bado hatujapata watendaji wa kutosha wa kuweza kupima maeneo ya wananchi, hasa yale maeneo ambayo ni ya Mji ule wa Rubwela na miji mingine midogo ambayo tumeitenga. Naamini wananchi wangu hawa watakapopimiwa ardhi yao tutaweza kuinua uchumi wao, wataweza kwenda kukopa. Pia maeneo haya yakipimwa naamini hata uchumi wa Taifa utainuka kwa sababu watakapopata pesa watafanya shughuli ambazo zitawapatia kipato na Serikali itapata sehemu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna watumishi wachache pale kwenye halmashauri yetu, kwa hiyo niombe Mheshimiwa Waziri aliangalie. Hata hivyo, si watumishi wachache tu, Idara ya Ardhi hawana hata gari, hawana hata pikipiki na jiografia ya wilaya yangu kwa kweli si nzuri. Kwa hiyo, hili tuliangalie, tusiwapeleke tu kule watumishi halafu tukawa-dump kule, hawana vitendea kazi halafu tutegemee hatimaye wanaweza wakawapimia wananchi ardhi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Mheshimiwa Waziri naomba alisikilize ni kwamba, bado maeneo ya vijijini wananchi wanalalamika wanasema gharama za upimaji ni kubwa. Tuliangalie hili, tusije tukalinganisha na maeneo ambayo ni ya mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo mimi nimekuwa nikishangaa sana na nimekuwa nikijiuliza maswali mengi. Mara nyingi hapa Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukiongelea migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, lakini nimejiuliza jambo moja, hivi vipindi vyote ambavyo vimepita Serikali haikutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji na wakulima? Nimejiuliza sana, lakini hatimaye katika kufuatilia kwangu nimegundua Serikali ilitenga maeneo kwa ajili ya wafugaji lakini maeneo haya kwa sababu ya viongozi ambao wamejaa tamaa, viongozi ambao hawawezi kusimamia majukumu yao maeneo haya wameyagawa, watu wengine wameingia na hatimaye tunasababisha migogoro mikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kule kwangu Kyerwa. Kuna eneo ambalo lilitengwa kwa ajili ya wafugaji mwaka 87. Eneo hili lilitangazwa kwenye Gazeti la Serikali likapewa GN Number 620, lakini eneo hilo leo watu wameingia kiholela bila kufuata utaratibu, wamegawana hovyo hovyo. Sasa unajiuliza hili eneo ambalo lilitangazwa na Serikali bila kutolewa tangazo lingine la kubadilisha matumizi, leo unaweza kuingizaje watu wengine waweze kujimilikisha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri; hili najua ugumu wake na mimi kama Mbunge nimetumwa na wananchi kwa ajili ya kuwatetea, hivyo sitanyamaza wala sitatulia katika hili, lazima tuondoe hii migogoro ambayo hatimaye inaleta uadui kati ya wakulima na wafugaji. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana, jambo hili siwezi kulinyamazia wakati linaendelea kuleta mgogoro mkubwa kati ya wakulima na wafugaji, lazima litolewe ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengine kule kwangu, kwa mfano Kata ya Nkwenda, kuna Kijiji kimoja cha Nyarutuntu; maeneo ya vijiji yanachukuliwa hovyo na wanakijiji hawana msaada, wanapofuatilia hawapati msaada. Naomba Mheshimiwa Waziri aandike, kwenye Kata ya Mgwenda, Kijiji cha Nyarutuntu kuna mgogoro. Huyu bwana amekuwa akiwatumia viongozi wakubwa kwa ajili ya kuteka ile ardhi ambayo ni ya wananchi; hivi vitu ndivyo vinaleta shida kubwa kwa wananchi wetu, naomba tuyafuatilie hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kwenye Mabaraza ya Ardhi. Haya Mabaraza ya Ardhi ni mazuri lakini maeneo mengine yamekuwa kero, hawatendi haki. Kwa mfano maeneo ya vijijini hawana elimu ya kutosha ili waweze kutimiza majukumu yao. Nimwombe Mheshimiwa Waziri tusiishie mijini hebu twende na huko vijijini tuweze kuwapa elimu ili wawatendee haki Wanakyerwa na Watanzania ambao hawajatendewa haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina mengi ya kusema lakini naomba nirudie, namwomba sana Mheshimiwa sana afike Kyerwa kama anavyofika katika maeneo mengine ili aweze kutatua migogoro ya ardhi ili yule anayestahili haki akapewe haki yake na hatimaye tuweze kukaa vizuri na wakulima na wafugaji wetu kama ndugu na kama marafiki kama ilivyo siku zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia kwenye bajeti hii muhimu. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uhai na nguvu kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wa Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kwa kweli nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kipekee kumpongeza Mheshimiwa Rais, Jemedari wetu kwa kazi nzuri ambayo kwa kweli anaifanya katika Taifa hili. Kwa kweli tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu amlinde, ampe afya njema, ampe nguvu, aendelee kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya ambazo zinaonekana. Kuna watu wengine walikuwa wanasema aah, ndiyo tunaanza, siyo kusema ndiyo tunaanza, Mheshimiwa Rais ameshaonesha mfano mkubwa kwa kazi ambazo amezifanya, sina haja ya kuzieleza, wenye masikio wanasikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Mheshimiwa Rais, kazi ambayo anaifanya mtu yeyote mwenye akili timamu ambaye ni mzalendo na Mtanzania, lazima apongeze kazi hii. Inasikitisha ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, anaposimama mtu ambaye anaona kazi kubwa iliyofanyika halafu anasema kilichofanyika ni upuuzi. Ni kitu ambacho kwa kweli mimi nimejiuliza sana Waheshimiwa Wabunge sijui kama na nyie mmejiuliza. Hawa watu wanadai wao ndio waliokuwa na hoja ya kusema hii mikataba mibovu haifai. Leo ni nini kilichowabadilisha? Wakati mwingine tunaweza tukaamini maneno ambayo yanayosemwa huko nje kuwa wengine kuna sehemu mmepelekwa ndiyo maana leo mmegeuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea leo mseme kwa kweli tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa hoja ambayo tulikujanayo, sasa leo ameishikilia na sisi tunaenda naye. Leo mmegeuka, nini kilichowageuza wenzangu? Ni nani aliyewaloga? Huo upofu umetoka wapi leo? Watanzania wenye akili wanajua Rais anachokifanya na wanamuunga mkono na wanamwombea. Naamini Waheshimiwa Wabunge katika vita hii Mheshimiwa Rais atalindwa atatunzwa na hakuna kitakachomdhuru kwa sababu ni wakati wa Mungu kuitengeneza Tanzania. Ni wakati wa Mungu kurudisha vile ambavyo viliibiwa, ndiyo maana mmeona Mwenyekiti mwenyewe wa hiyo kampuni amekuja kwa ndege binafsi. Huu ni wakati wa Mungu, kwa hiyo, nyamazeni, Mungu yuko kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee bajeti yetu. Bajeti yetu kwa kweli ni nzuri, naipongeza sana, lakini niiombe Wizara, Mheshimiwa Waziri Mpango kuna vitu ambavyo tukiwekeza nguvu Taifa hili litainuka kwa muda mfupi. Sehemu kubwa ya Watanzania, wakulima ndio walio wengi, lakini nguvu ambayo tumeiwekeza kwenye kilimo ni ndogo sana. Naiomba sana Wizara, tunasema tunaingia kwenye Tanzania ya viwanda, hivi viwanda vitapata malighafi wapi tusipowekeza kwenye kilimo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuwekeze kwenye kilimo ili tuweze kumwinua mkulima. Kuna mazao ambayo ni muhimu, kwa mfano, kuna mazao kama kahawa. Mazao haya tumeyaacha kwa muda mrefu, lakini mazao haya kama kahawa, korosho, tumbaku na mazao mengine yanaweza kuliingizia Taifa hili pesa nyingi na tukamwinua mkulima na kipato cha Serikali kikaongezeka. Kwa hiyo, naomba sana hilo tuliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la viwanda. Nchi hii tumejipanga kwenda kwenye viwanda. Naomba sana Wizara yangu, ili tuwe na viwanda lazima tuwe na umeme wa uhakika ambao utaweza kuendesha viwanda vyetu; lakini ukiangalia bado uzalishaji wa umeme ni mdogo kulinganisha na jinsi ambavyo tumejipanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Wizara iweze kuongeza nguvu tuweze kuzalisha umeme, tuwe na umeme wa uhakika ndipo tutafanikisha Tanzania ya viwanda na tunapowakaribisha wawekezaji ili kuwekeza kwenye viwanda, pawepo na umeme wa uhakika. Kitu kingine kwenye viwanda, tuweke mazingira ambayo ni rafiki, mazingira ambayo hata wawekezaji wakija waweze kuvutiwa na mazingira ambayo ni rafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa hizi tozo ambazo wameondoa kwenye mazao mbalimbali kama korosho na kahawa. Hili ni jambo ambalo ni zuri na litaweza kumwinua mkulima. Bado zipo tozo kwa upande wa kahawa na mazao mengine. Huyu mkulima amesahaulika sana na tunasema kilimo ni uti wa mgogo, lakini uti huu wa mgongo umesahaulika.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.

Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa nguvu na afya kuwepo mahali hapa, lakini nichukue pia nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri zinazofanyika. Ndugu zangu Watanzania wanaona yale yanayofanyika. Kwa hiyo, ninampongeza Mheshimiwa Rais, anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua kipindi hiki kama Watanzania tuko kwenye vita na ni vita ya kiuchumi. Vita ya kiuchumi kuna watu ambao watatu-support, lakini wapo watu wengine ambao watabeza, lakini kitu cha muhimu sisi tuangalie ni wapi tunakoenda na lile ambalo tumelikusudia. Hao wapiga debe tuachane nao, siku zote nilishawahi kusema hapa Bungeni, mara nyingi wapiga debe huwa sio wasafiri. Ukiwa kwenye kituo cha mabasi utaona watu wanasema twende, twende lakini mwisho wa kusafiri hawaendi. Hao wapiga debe tuachane nao tusonge mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii niongelee kwanza upande wa afya. Niipongeze Serikali yangu, Kyerwa tulikuwa hatuna kituo cha afya hata kimoja, lakini sasa hivi tuna kituo cha afya kimekamilika, kiko vizuri na niishukuru Serikali wamenipa shilingi milioni 700 kwa ajili ya kuboresha kituo cha Mlongo. Kwa hiyo, nina kila sababu ya kupongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali, bado tuna upungufu wa watumishi na ukilinganisha kwa mfano Wilaya yangu ya Kyerwa bado tunahitaji zaidi huduma za afya. Nina Kata 24, naomba sana Serikali kwenye mgao huu ambao mnaenda kugawa Hospitali za Wilaya 67, naomba na Wilaya yangu ya Kyerwa ipewe mgao kwa sababu tunahitaji sana huduma ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende upande wa maji, wengine tunapopongeza wanasema tunajipendekeza lakini mambo kama yamefanyika lazima tupongeze. Kwenye Wilaya yangu ya Kyerwa nimepewa zaidi ya bilioni mbili na milioni 900. Sasa hivi tumeweza kuboresha miradi midogo kwa mfano mradi wa Kaishori, Rutunguru na Isingilo, mradi wa Mabira, hii ni miradi ambayo itawahudumia wananchi lakini kwa muda mfupi tumeweza kufanya usanifu wa mradi mkubwa ambao huu mradi utaweza kuwahudumia wananchi wa Kata 15 kati ya 24.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe sana Serikali bado tuna uhitaji sana wa huduma ya maji. Kama walivyoshauri Waheshimiwa Wabunge wenzangu, niiombe sana Serikali ile shilingi 50 ambayo tumeomba iongezwe bado uhitaji wa maji kwa wananchi wetu ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe sana Serikali ilizingatie na iweze kuliongeza. Niiombe sana Serikali, kwenye mradi wetu ambao tumeshafanyia usanifu tutakapomaliza kutangaza tender ninaamini Serikali yetu ni sikivu tutapatiwa pesa kwa ajili ya kukamilisha huu mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la TARURA, Waheshimiwa Wabunge, tulikuwa tunaongea sana hapa Bungeni tunasema miradi inaharibika kwenye Halmashauri, haisimamiwi vizuri. Serikali imeleta chombo kizuri ambacho ni TARURA. Mimi niwaeleze ukweli Waheshimiwa Wabunge, Mbunge una uwezo wa kukaa na yule Meneja wa TARURA mkajadiliana miradi ambayo unayo kwenye jimbo lako, lakini ninashangaa leo Wabunge ninyi ndiyo mnashauri irudishwe kwenye Halmashauri, kwa nini mlikuwa mnapiga kelele? Hili niiombe Serikali, ushauri mwingine tusiusikilize. TARURA wameanza vizuri, kwa muda mfupi kwenye jimbo langu wameonesha jambo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo niishauri Serikali tuongeze, badala ya asilimia 70 kwenye TANROADs tufanye nusu kwa nusu au kama ikishindikana tufanye asilimia 45 kwa 55 kwa sababu barabara nyingi ziko vijijini na wazalishaji wakubwa wako vijijini. Kwa hiyo, niombe sana Serikali hili ilizingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la umeme. Tunahitaji umeme, kule kwetu Kyerwa bado kabisa, kwa hiyo, niombe sana waendelee kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme ili wananchi wetu wapatiwe umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilizungumzie ni suala la kahawa. Ninaamini Serikali yetu ina nia njema kwa ajili ya kuwakomboa wakulima hao ambao wameachwa muda mrefu. Wakulima hawa walikuwa wanauza kahawa kwa butura ambayo butura wanauza 20,000 na yule anayenunua anakuja kupata zaidi ya 100,000. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali, ilisimamie hili kwa karibu kwa sababu hii na yenyewe ni kama vita. Wale waliokuwa wananunua na wao wangetamani hili la Serikali lisifanikiwe. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ambalo niishauri Serikali kama walivyochangia Wabunge wengine, hawa wananchi walishazoea kahawa kabla haijakomaa wanaweza kuuza butura sasa kukomesha biashara ya butura, tuanzishe SACCOS ambazo zitaweza kuwahudumia hao wananchi kabla kahawa haijakomaa aweze kutatua matatizo yake. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali iweze kulizingatia tuweze kuwakomba wakulima ambao wameachw amuda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nishauri kwa upande wa kahawa. Kuna madeni ambayo walikuwa wanadaiwa hawa KDCU, KCU, haya madeni yasije yakahusishwa na wananchi wanapouza kahawa zao. Madeni watafute namna ya kuwalipa, lakini sio wananchi wanaenda kulipa madeni, wananchi hawakusababisha haya madeni. Kwa hiyo, kama Mbunge ambaye natoka Mkoa unaolima kahawa, suala hili lisije likahusishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nishauri Serikali katika zao hili la kahawa. Kama kuna uwezekano waajiri watu kuliko haya mambo ya kuchaguana. Ndiyo maana wanachagua hata watu wengine ambao hawana uwezo, mwisho wa siku wanakuja kuharibu. Kwa kuwa, Serikali ina nia ya dhati niiombe sana Serikali wawekwe waajiriwa ambao wana uwezo kama ni wahasibu, kama ni mameneja ambao wataweza kusimamia haya mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa MWenyekiti, kitu kingine tuombe sana Serikali iwezeshe hivi vyama vya msingi kwa sababu sasa hivi hawana pesa na walikuwa hawajajiandaa ni kama wameshtukizwa. Sasa jamno ambalo wameshtukizwa leo unawaambia wanunue kahawa na huko kwenye mabenki wanadaiwa. Hii itakuwa ngumu na inaweza ikasababisha chuki kwa wananchi kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niendelee kuipongeza Serikali na niendelee kuwatia moyo. Serikali songeni mbele, kazi mnayoifanya ni kubwa, Watanzania wanaona na kwa muda mfupi kwa kweli mmeonesha mabadiliko makubwa. Watanzania wako wengi wanawaunga mkono. Hizi kelele tuachane nazo tusonge mbele. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na nguvu kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuendelea kumpongeza Jemedari wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli pamoja na Waziri Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara ya Afya kwa kazi nzuri wanayoifanya, hakika Serikali yetu imejipanga kuhakikisha inaboresha huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, wako watu wengi wanabeza mara hakuna kilichofanyika sasa mimi ngoja niwaambie baada ya kuwasemea wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa ni nini kimefanyika Kyerwa. Wakati naingia hapa Bungeni nilikuwa nina kituo cha afya kimoja ambacho huduma zake hazikuwa nzuri kituo cha Nkwenda leo kimeboreshwa akina mama wanapata huduma ya upasuaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana nimepokea shilingi milioni 700 kwa ajili ya Kituo cha Afya Mlongo, hiyo ni kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya John Pombe Magufuli. Mwaka huu kwenye bajeti ya TAMISEMI nimepokea bilioni moja na milioni mia tano (1,500,000,000) kwa ajili ya hospitali ya Wilaya, nani kama John Pombe Magufuli?

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi ni kazi nzuri zinazofanywa na Serikali ya John Pombe Magufuli, wenye macho wanaona na wenye masikio wanasikia. Pamoja na kazi hizi zinazofanyika bado tunazo changamoto za watumishi, niendelee kuiomba sana Serikali yetu, Kyerwa watumishi wa afya ni wachache sana, ninaomba tunapotoa mgao kama Serikali na Kyerwa muiangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa ajili ya huduma za matibabu ya kibingwa, kwa kweli tumepiga hatua nzuri sana. Mimi nimefika pale Muhimbili kwenye Hospitali ya Jakaya Mrisho Kikwete ya Moyo, kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana inatia moyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo haya tulikuwa tunasikia yanafanyika nje, lakini leo tunaona yanafanyika Tanzania, nimpongeze Daktari wetu Profesa Janabi, lakini na madaktari wengine ambao wanaboresha huduma za afya. Ninachoiomba Serikali yangu sikivu tujitahidi kama tunavyofanya maamuzi magumu kwenye mambo mengine, hebu tufanye maamuzi magumu kuboresha huduma za afya kwa upande wa matibabu ya kibingwa ili tuweze kuokoa pesa nyingi zinazoenda nje ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu nilimpeleka Mzee wangu India, Watanzania ni wengi wanaotibiwa India na wanatumia gharama kubwa sana. Kama mtu mmoja tuliweza kutumia zaidi ya milioni 30 kuna mama mmoja alikuwa anafanyiwa upasuaji pale Hospitali ya Apollo anahitaji zaidi ya dola 30,000 hizi pesa zote tukiboresha huduma za afya zitaingia Tanzania na tutaongeza kipato cha Wizara ya Afya. Ninaiomba sana Serikali iongeze vifaa, iongeze nguvu ninaamini tunao wataalam wengi sana lakini tatizo bado vifaa havitoshi kuweza kuboresha huduma hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la upatikanaji wa madawa. Kwa kweli Serikali inafanya kazi nzuri, tumetoka bilioni 30 leo tunaongelea bilioni 200, ni kazi kubwa inayofanyika kwa kweli tuna kila sababu ya kuipongeza Serikali yetu kwa kuhakikisha inaboresha huduma za afya na Watanzania wanakaa sawa. Ninachoomba Mheshimiwa Ummy tumeona ukiongea na wadau mbalimbali hili jambo na lenyewe iwe ni sehemu ya kufanya maamuzi magumu ili tuweze kuwa na viwanda vya madawa hapa Tanzania na hii itasaidia, hizi pesa nyingi zinaenda nje lakini zingebaki ndani zingeweza kuboresha huduma za afya na ninaamini tutapiga hatua kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la Bima ya Afya, hili suala ni jambo ambalo ni muhimu Watanzania hawawezi kuwa na pesa ya kujitibu, lakini tunapokuwa na bima ya afya itasaidia. Niiombe sana Serikali iongeze nguvu na waendelee kuwahamasisha Watanzania kila mmoja awe na bima ya afya, hii itasaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania wa Mwaka 2022
MHE. INNOCENT S BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu ambae amenipa afya na nguvu kuwepo katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, awali ya yote niipongeze Serikali Muswada huu ambao ni muhimu na kwa kweli niseme ulichelewa. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kuwa tayari kupokea maoni ya Kamati pia maoni ya wadau, hakukuwa na mvutano wowote ule na Serikali ilitoa ushirikiano mzuri sana.

Mheshimiwa Spika, kama walivyochangia Waheshimiwa Wabunge, Muswada huu ni muhimu sana. Tumekuwa tukishuhudia mambo mengi ambayo yanafanyika kwenye mitandao, tunashuhudia vitu ambavyo ni vya ajabu, ninaamini kuletwa kwa Muswada huu unaenda kulinda maadili ya Watanzania. Leo hii ukifungua kwenye mitandao, unakutana na vituko vya ajabu na mitandao hii inafunguliwa na watoto wetu, wanajifunza vitu ambavyo kwa kweli vinaondoa maadili yetu lakini ninaamini kwa Muswada huu sasa tunaweza kudhibiti hata wale ambao wanaleta taarifa ambazo zinaweza zikaondoa maadili yetu katika Taifa letu. Kwa hiyo, Muswada huu ni mzuri sana ninawaomba Waheshimiwa Wabunge, tuunge mkono Muswada huu kwa sababu unaenda kulinda utu wetu na unaenda kulinda taarifa zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine niliseme ni kwamba Muswada huu ni mzuri sana lakini ni lazima tujue chanzo cha mapato cha kuweza kuendeleza Muswada huu, maana tunaweza tukawa tumetunga Muswada lakini hatuna chanzo chochote cha mapato. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri utueleze hapa utakapokuwa una-wind hapa utuambie ni chanzo kipi ambacho tutaweza kupata mapato? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine niliseme ni kwamba Muswada huu unaenda kuinua biashara ya kimtandao, kwa sababu hawa wanaofanya biashara kwenye mtandao watakuwa na uhakika wa taarifa zao kulindwa na huu Muswada. Jambo lingine ambalo ningependa kuliongelea ni kwamba, tumekuwa tukipitisha Sheria nzuri, nyingi na kwa kweli ukisikia Wabunge wanapokuwa wakichangia hapa Sheria zinakuwa ni nzuri lakini kwenye utekelezaji, wakati wa kutunga Kanuni zinakuwa Sheria za ajabu, tunaonekana Wabunge tumetunga Sheria za ajabu, tumefanya vitu vya ajabu. Hata mambo yaliyojitokeza kwenye tozo, tukaonekana Wabunge hakuna kitu chochote tulichotunga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ninashauri Bunge hili kama ndiyo tunaoletewa Miswada hii kuipitisha iwe Sheria sasa tuwe na nguvu ya kuleta Kanuni hizi ambazo Serikali inaenda kuzitunga ili tujue kile ambacho sisi tumekipika, kinapakuliwa vipi, siyo tunakuja hapa, tunajadili Muswada, tunauweka vizuri halafu mwisho wa siku tunakuja kuletewa Kanuni za ajabu. Kwa hiyo, ninaomba sana hili jambo lazima liangaliwe, Bunge lazima lisimame kuhakikisha Sheria tunazozitunga na Kanuni zake zinakwenda kuwa nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo. Ninakushuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia Wizara hii muhimu. Kwanza nimpongeze Waziri Mwigulu kwa kazi nzuri anayoifanya. Lakini pia nilipongeze na Jeshi la Polisi, wanafanya kazi nzuri. Naamini Taifa hili limetulia kwa sababu ya mchango mkubwa wa Jeshi la Polisi, kwa hiyo, tunawapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii inaongozwa kwa mujibu wa sheria na mtu yeyote anayetaka kuishi kwenye Taifa letu kwa amani, kwa furaha, lazima afuate sheria za nchi hii, vinginevyo Jeshi letu la Polisi fanyeni kazi kwa mujibu wa sheria, washughulikieni wote ambao wanaenda kinyume na sheria ya nchi hii. Katika hili haijalishi ni kiongozi wa dini, haijalishi ni kiongozi wa kisiasa, hebu washughulikieni, Taifa hili lina amani kwa sababu wanafanya kazi nzuri na hizi kelele zinazopigwa zisije zikawatisha wakaacha kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunawaunga mkono na naamini mtu ambaye ametulia kwenye Taifa anafuata sheria, hawezi kusumbuliwa wala kubugudhiwa kwa namna yoyote. Wewe ukiona unasumbuliwa ujue una shida, ukiona wanavamia kwako, mara unalala magereza, mara unalala ndani, ujue una shida, fuata sheria uishi kwa furaha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wengi ambao wanajidai kumtaja Mungu lakini maandiko yanasema katika Tito, kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu. Kama unataka Mheshimiwa Rais afanye kazi vizuri pamoja na wewe mtii kwa sababu huyo ameletwa na Mungu na maandiko yanasema hivi, hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu hata hiyo iliyopo imeamuliwa na Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unataka kuishi kwa imani itii hiyo mamlaka; ujumbe umefika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kulisemea Jeshi letu la Polisi kwa upande wa Kyerwa. Nimwombe sana Mheshimiwa Mwigulu na watendaji wote wa Mambo ya Ndani, kwa kweli Jeshi letu la Polisi Kyerwa wanafanya kazi kwenye mazingira magumu, hawana kituo cha polisi, wanafanya kazi kwenye ofisi ya kata ambayo ofisi yenyewe hali yake ni mbaya. Kwa hiyo, niombe polisi wetu hawa ambao wanafanya kazi kwenye maeneo ya mipakani wapewe vitendea kazi lakini wapewe ofisi ambayo inafanana na hadhi ya polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo ambazo nimewapa polisi, upo upungufu ambao naamini kila binadamu anao upungufu; hivyo tunashauriana, tunarekebishana, tunasonga mbele. Kwa upande wa bodaboda niwaombe sana Jeshi la Polisi; mazingira, namna ambavyo wanaendesha hawa vijana wetu wa bodaboda kwa kweli haipendezi. Kwa upande wetu kule Kyerwa bodaboda wakati mwingine wanakimbizwa mpaka kwenye migomba, wakati mwingine wanapata ajali, kwa hiyo, niwaombe sana polisi hili mliangalie tusije tukaanza kusema mambo mengine makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa Magereza kuna eneo ambalo Magereza walichukua pale Kyerwa na wakawaahidi wananchi kuwapa fidia. Wananchi hawa bado hawajafidiwa na wanasubiri kwa muda mrefu na maeneo yao wamezuiwa wasiyaendeleze. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Mwigulu hili aliangalie na walisimamie ili wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa waweze kupewa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niongelee upande wa uandikishaji unaoendelea. Kule kwenye Jimbo langu la Kyerwa wananchi wangu wengi unakuta unapomhoji saa mbili, tatu kwa Kiswahili inakuwa ni shida. Sasa kwenye mahojiano yale unakuta wanapowahoji wananchi mwingine anaposhindwa kujibu maswali mawili matatu kwa Kiswahili wanaanza kusema huyu ni mhamiaji haramu. Kwa hiyo, niombe sana hili waliangalie ili uandikishaji huu uweze kufanyika vizuri na kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilisemee, Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukipita sana eneo la Mikese na eneo lile kituo cha polisi mara nyingi tunapata ajali, tunakuwa na matatizo mbalimbali. Hebu nimwombe Mheshimiwa Mwigulu, kile kituo cha polisi kipewe vitendea kazi, wana gari moja ambalo haliwasaidii. Kwa hiyo, niombe sana kile kituo Waheshimiwa Wabunge wengi tumekuwa tukipata msaada pale, kwa hiyo na chenyewe wakikumbuke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikushukuru na niendelee kusema Mheshimiwa Mwigulu asonge mbele, Rais wetu anafanya kazi nzuri, hebu wamuunge mkono na Jeshi letu la Polisi kazi kubwa waliyoifanya Kibiti imedhihirisha Jeshi la Polisi wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa Mwaka 2022
MHE. INNOCENT S BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu ambae amenipa afya na nguvu kuwepo katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, awali ya yote niipongeze Serikali Muswada huu ambao ni muhimu na kwa kweli niseme ulichelewa. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kuwa tayari kupokea maoni ya Kamati pia maoni ya wadau, hakukuwa na mvutano wowote ule na Serikali ilitoa ushirikiano mzuri sana.

Mheshimiwa Spika, kama walivyochangia Waheshimiwa Wabunge, Muswada huu ni muhimu sana. Tumekuwa tukishuhudia mambo mengi ambayo yanafanyika kwenye mitandao, tunashuhudia vitu ambavyo ni vya ajabu, ninaamini kuletwa kwa Muswada huu unaenda kulinda maadili ya Watanzania. Leo hii ukifungua kwenye mitandao, unakutana na vituko vya ajabu na mitandao hii inafunguliwa na watoto wetu, wanajifunza vitu ambavyo kwa kweli vinaondoa maadili yetu lakini ninaamini kwa Muswada huu sasa tunaweza kudhibiti hata wale ambao wanaleta taarifa ambazo zinaweza zikaondoa maadili yetu katika Taifa letu. Kwa hiyo, Muswada huu ni mzuri sana ninawaomba Waheshimiwa Wabunge, tuunge mkono Muswada huu kwa sababu unaenda kulinda utu wetu na unaenda kulinda taarifa zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine niliseme ni kwamba Muswada huu ni mzuri sana lakini ni lazima tujue chanzo cha mapato cha kuweza kuendeleza Muswada huu, maana tunaweza tukawa tumetunga Muswada lakini hatuna chanzo chochote cha mapato. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri utueleze hapa utakapokuwa una-wind hapa utuambie ni chanzo kipi ambacho tutaweza kupata mapato? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine niliseme ni kwamba Muswada huu unaenda kuinua biashara ya kimtandao, kwa sababu hawa wanaofanya biashara kwenye mtandao watakuwa na uhakika wa taarifa zao kulindwa na huu Muswada. Jambo lingine ambalo ningependa kuliongelea ni kwamba, tumekuwa tukipitisha Sheria nzuri, nyingi na kwa kweli ukisikia Wabunge wanapokuwa wakichangia hapa Sheria zinakuwa ni nzuri lakini kwenye utekelezaji, wakati wa kutunga Kanuni zinakuwa Sheria za ajabu, tunaonekana Wabunge tumetunga Sheria za ajabu, tumefanya vitu vya ajabu. Hata mambo yaliyojitokeza kwenye tozo, tukaonekana Wabunge hakuna kitu chochote tulichotunga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ninashauri Bunge hili kama ndiyo tunaoletewa Miswada hii kuipitisha iwe Sheria sasa tuwe na nguvu ya kuleta Kanuni hizi ambazo Serikali inaenda kuzitunga ili tujue kile ambacho sisi tumekipika, kinapakuliwa vipi, siyo tunakuja hapa, tunajadili Muswada, tunauweka vizuri halafu mwisho wa siku tunakuja kuletewa Kanuni za ajabu. Kwa hiyo, ninaomba sana hili jambo lazima liangaliwe, Bunge lazima lisimame kuhakikisha Sheria tunazozitunga na Kanuni zake zinakwenda kuwa nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo. Ninakushuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. Pia nikushukuru wewe binafsi kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wangu, Waziri, Naibu Waziri na watendaji wake wote kwa kazi nzuri zinazofanyika kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji kwa Watanzania, yaani kumtua mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni muhimu sana na ni ukweli usiopingika Serikali inafanya kazi kubwa sana ingawa ziko changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa pesa pamoja na wataalam wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii pia kuishukuru Wizara ya Maji kwa pesa ambayo tumetengewa mwaka 2017/2018 shilingi bilioni 2.1 ambazo zimetusaidia kuboresha miradi mbalimbali kama mradi wa Mabila, Kaisho, Isiringiro, Rutunguru, Kagenyi na mengineyo midogo midogo. Lakini pia tumeweza kuanza mradi mpya wa vijiji 57 ambavyo utakuwa mkombozi kwa Wanakyerwa ambao utaweza kuhudumia zaidi watu 200,000 utakapokuwa umekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huo mkubwa tumefikia hatua ya kutangaza tender, namuomba sana Mheshimiwa Waziri na watendaji wake wa Wizara kutufuta machozi ya kilio cha muda mrefu cha kukosa maji kwa wana Kyerwa ambao hali yao ya upatikanaji ni mbaya sana. Kwa kweli naomba sana Serikali imetuweka kwenye bajeti tumetengewa shilingi bilioni moja tu ambapo mradi unahitaji zaidi ya shilingi bilioni 140. Natambua sana hatua hii tuliyofikia ya usanifu na design Wizara imefanya kazi kubwa. Waziri, Mkurugenzi wa Maji Vijijini kuhakikisha tunafikia hapa, bado imani yangu ni kubwa sana kwao mpaka mradi huo unakamlilika na Wanakyerwa wanapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji inafanya kazi nzuri na kubwa sana lakini miradi inayosimamiwa na Halmashauri ni kampuni za mifukoni na za kupeana kiurafiki, na hatimaye miradi ni ya hovyo. Mfano miradi ya Itera, Mradi wa Rutunguru, Kaisho na Isingiro mpaka sasa hakuna kinachoendelea. Kuna mradi kata ya Rukuraijo vifaa vimeibiwa kama solar na vingine, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa na maradi wa Kigorogoro ambao una zaidi ya miaka kumi lakini hakuna kinachoendelea. Niiombe Wizara kufuatilia miradi kujua kinachoendelea, lakini pia kukagua kazi iliyofanyika, kwamba ni sawa na pesa iliyotolewa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Wabunge wengi walivyoshauri kuongezwa shilingi 50 kwenye mafuta ili mradi kama wetu ambao ni mkubwa uongezewe pesa na hii itasaidia Wizara kuendelea angalu kuongeza bajeti yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na usimamizi usioridhisha wa baadhi ya Halmashauri kwenye sekta ya maji kama ilivyokuwa kwenye upande wa barabara zilizokuwa zinasimamiwa na Halmashauri na ikaundwa TARURA, tuombe sana Serikali kuunda chombo ambacho kitasimamia maji vijijini yaani Wakala wa Maji Vijijini hii itasaidia sana Wizara kuongeza ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo niendelee kumshukuru Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wake wote wa Wizara kutusaidia kufika hapo tulipofika kuanzisha mradi wa vijiji 57 ushirikiano umekuwa mkubwa sana. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uhai ili kuendelea kuwatumikia wananchi wetu. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuifanya kuhakikisha haya madini yanawanufaisha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri. Hatua ambazo Mheshimiwa Rais anazichukua kwa huyu Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa uadilifu wenu tunaamini mtasimamia sekta hii muhimu ili iweze kuwanufaisha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niongelee Wilaya yangu ya Kyerwa. Wilaya ya Kyerwa tuna madini ya tin, madini haya ni muhimu. Naamini Serikali ikiona na ikayasimamia yanaweza kuliingizia Taifa hili kipato kikubwa pia tunaweza tukatengeneza mabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo napenda kulizungumzia mwaka 2016, Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo alifika pale na akajionea mazingira yalivyo. Maeneo yale bado utafiti haujafanyika kuweza kubainisha yale maeneo ambayo yana madini ya bati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Wizara hii imechukua muda mrefu, tangu 2016 walikuja wataalam mara moja na hawajarudi tena. Nimwombe Mheshimiwa Waziri atueleze hatua hizi zitachukuliwa lini ili tuweze kujua ni kiasi gani cha madini tuliyonayo kwa sababu mpaka sasa hivi uchimbaji unaoendelea, wachimbaji wadogo wadogo wanachimba lakini sehemu kubwa ya madini yetu Mheshimiwa Waziri naamini anajua hatuyafaidi bali yanawafaidisha majirani zetu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri pawepo na mkakati na hatua za haraka ili kuweza kunusuru haya madini ambayo ni ya muhimu yasiende kuwanufaisha majirani zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wachimbaji wadogo wadogo, naishukuru Serikali angalau imeweza kuwatengea maeneo lakini siyo wote, bado wanapata usumbufu sana wanapofanya utafiti wao wakapata sehemu ambayo ina madini wanakuja hawa watu ambao ni wakubwa wanasema haya maeneo ni yetu. Hivyo, wanataabika, bado hawajatengewa maeneo ambayo yataweza kuwasaidia. Niwaombe Serikali, Mheshimiwa Kairuki naamini wewe pamoja na wasaidizi wako ni wasikivu, mtakapokuja kupima yale maeneo ili kujua ambayo yana madini muweze kuwatengea wachimbaji wadogo wadogo ili wawe na uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuna wawekezaji ambao walifika pale wamekuja kujenga viwanda vya uchenjuaji. Kuna mmoja ambaye alikuwa hajafuata taratibu Serikali imemsimamisha ili aweze kufuata utaratibu. Niiombe Serikali huyu mwekezaji anapokuja na ninyi muweze kumsaidia haraka ili hawa wachimbaji wetu waweze kupata uhakika wa kuchenjua hayo madini wanayochimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wale wachimbaji wanapochimba hawana uhakika wa soko, wale ambao wana leseni ya maeneo yale ndiyo wanaochukua yale madini. Wanachukua kwa pesa ni ndogo kwa hiyo wachimbaji wadogo hawapati pesa ambayo inalingana na thamani ya yale madini. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri tuwe na uhakika wa soko na haya madini yatambuliwe. Majirani zetu ndiyo wanayatumia sana lakini sehemu kubwa inatoka kwetu. Tuweke mkakati ambao utaweza kuyatambua haya madini na ikiwezekana tuyatangaze. Bado tunaweza kufungua viwanda ambavyo vinaweza kukusanya madini haya na yakatunufaisha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka kujua hii STAMICO ndiyo iliyokuwepo kipindi kile madini haya yanaibiwa na kupotea hovyo. Je, STAMICO hii ambayo mnaendelea nayo na naona mnatenga hela kwa ajili ya kuiendeleza, ni STAMICO mpya au ni ile ya zamani? Inawezekana hawa watendaji bado ni walewale. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri lazima achukue hatua, kama tunataka kubadilika lazima tubadilishe mfumo wote vinginevyo huku juu mtachukua hatua lakini bado wale wale wanaendelea kufanya uharibifu uliokuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, Mwenyezi Mungu ametujaalia madini mengi sana na ninaamini tukiyasimamia tunaweza kuliingizia Taifa kipato kikubwa sana. Kwa hiyo, niombe sana, hawa wanaosema sijui haya madini yana mapepo, majini na vitu vingine, mimi naamini hilo halipo. Hatuhitaji kwenda kwa waganga, hii rasilimali tumepewa na Mwenyezi Mungu tuisimamie, tuwapate watu ambao ni wazuri kwa msaada wa Mungu aliyetupa rasilimali hizi zitaweza kunufaisha Taifa letu. Ashukuriwe Mungu ametupatia Mheshimiwa John Pombe Magufuli ambaye ameanza kusimama vizuri na ametupa Mawaziri wazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi niwatakie kila la kheri Waheshimiwa Mawaziri, Watendaji Wakuu wote wa Wizara lakini hii ni vita lazima tupambane kuhakikisha madini haya yanawanufaisha Watanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu. Awali ya yote nimshukuru kwanza Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na nguvu kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anazozifanya. Kwa kweli nampongeza sana, tumeona mabadiliko makubwa ambayo amekuwa akiyafanya, kwa kweli tunampongeza pamoja na wasaidizi wake, wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia mimi nilipongeze Jeshi letu la Polisi, kwa kweli pamoja na baadhi ya wenzetu kubeza na kusema hakuna chochote kinachofanyika na wengine wamefika mbali kusema maneno magumu, wanasema Jeshi la Polisi ni kansa, kitu ambacho kwa kweli si jambo zuri na sikutegemea kama Mbunge angeweza kusimama na kusema neno la namna hii. Tuko hapa kwa sababu ya kazi nzuri zinazofanywa na Jeshi letu la Polisi. Ndugu zangu tunaweza tukawa hatuelewi lakini ukiongea na majirani zetu ambao wanapita kwenye nyakati ngumu, ndiyo mnaweza mkajua umuhimu wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunalala wenzetu wako nje wanang’atwa na mbu na mambo mengine wanayoyafanya. Leo hii tuko hapa tumetulia, hali ni nzuri, ukienda nchi za wenzetu, tulienda kule Burundi, kila mnapozunguka mnatembea na mitutu ya bunduki lakini nendeni pale nje hata bunduki hatuzioni ni kwa sababu ya amani iliyopo katika Taifa letu.

MHE. JOHN W. HECHE:Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, kuhusu utaratibu, nisaidie Kanuni.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 64(1)(a), Mbunge hatatoa Bungeni maneno yasiyokuwa na ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Bungeni tuko hapa kwa ajili ya….

MWENYEKITI: Maneno ambayo siyo ya ukweli ni uongo, si ndiyo?

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo uwongo huo. Hakuna miongoni mwetu hapa ambaye anabeza kazi ya Jeshi la Polisi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, anachojitungia na kutaka kujipa uhalali kwamba Jeshi la Polisi sisi tunalibeza, hatulitaki au…

MWENYEKITI: Mheshimiwanimekuelewa, sababu ya muda, nimekuelewa, kaa tu, sitaki usimame. Anachosema Mheshimiwa Bilakwate, nimemsikia vizuri sana halafu asubuhi nilimsamehe sana huyu Mheshimiwa Sophia Mwakagenda alitumia neno, Jeshi la Polisi ni kansa, nilimvumilia.Sasa Mheshimiwa Bilakwate anajibu kwa namna hiyo, ndiyo maana sitaki mimi niliendeleze suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Bilakwate,hoja yako imesikika lakini nalikataza hilo, sitaki kufika huko.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Niombe sanaWizara ya Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Waziri lakini Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Jeshi letu la Polisi kwa kazi nzuri wanazozifanya waweze kupewa yale ambayo ni mahitaji yao lakini bajeti yao izingatiwe ili waweze kuendelea kutimiza majukumu yao. Vinginevyo tusipowajali hawa wenzetu wanaosema wao wako wengi siku wakianzisha vita, tusipowapa vitendea kazi vizuri ili waweze kuwadhibiti watakapoanzisha vita, tutakuwa tunakwenda pabaya. Kwa hiyo, niombe sana tuwasaidie Polisi wetu kwani wanayo mahitaji mengi ili waweze kutimiza majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Mheshimiwa Waziri ulifika Kerwa, ulionamazingira ambayo Polisi wetu wanafanya kazi. Uliona Kituo chaPolisi siyo kizuri na kituo kile ni ofisi za kata, nikuombe sana hili ulizingatie. Sisi tuko mpakani, tunakutana na watu wengi, majirani zetu wanaingia, tusipoimarisha vizuri Jeshi la Polisi mipakani, tunaweza tukaingiza mambo mengine ambayo baadaye yanaweza kuhatarisha amani ya taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ni kwa upande wa NIDA. Kerwa tupo kwenye utaratibu wa kuanza kusajili vitambulisho vya NIDA, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, hii mikoa ambayo iko pembezoni muweze kuiangalia kwa umakini sana kwa sababu wako wenzetu wanatamani kuwa Watanzania ambao hawana sifa. Suala hili tuliangalie ilitusijetukaingiza watu ambao hawana sifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine tunahitaji hata kuhubiriana injili au kukemeana mapepo. Naomba nisome hili nenona mwenye akili ataelewa. Nasoma Kitabu cha Warumi 13:1-7, inasema: “Kila mtu naaitii mamlaka iliyo kuu;kwa maanahakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo imeamuriwa na Mungu. Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana naagizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu. Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka?Fanya mema, naweutapata sifa kwake. Kwa kuwa yeye nimtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa sababu ni mtumishi wa Mungu, amlipiziaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu. Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile gadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MWENYEKITI: Kanuni gani?

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 64(1)(a), inasema: “...hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli”.

MWENYEKITI:Hicho ni Kitabu Kitakatifu, Mheshimiwa endelea.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sijasema sababu.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.Niendelee kusoma mstari, nilikuwa nimefika mstari wa6 unasema: “Kwa sababu hiyo tena mwalipa kodi; kwa kuwa wao ni wahudumu wa Mungu, wakidumu katika kazi iyo hiyo. Wapeni wote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru;astahiliye hofu, hofu; asitahiliye heshima, heshima”.Haleluya.(Makofi)

WABUNGE FULANI: Ameen.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya nafikiri kila mtu ameelewa, kama mnataka Jeshi la Polisi lisiwapige na lisizuie mikutano lazima muwe watii.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA:Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Nyie mnasema mnaonewa kila sehemu, mnaonewa wapi nikwa sababu hamtendi mema. Mabaya mnayoyatenda ndiyo yanayowageuka, tendeni mema muone kama na ninyi hamtatendewa mema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa nguvu kuendelea kuwatumia wananchi wa Jimbo la Kyerwa. Pia nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara ya Maji kwa kazi nzuri inazozifanya. Pamoja na changamoto ambazo wameeleza, lakini tumeona Mheshimiwa Waziri na timu yake wakienda maeneo mbalimbali kutatua kero ya maji. Kwa hiyo, tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri na tunaamini juhudi hizo zitaendelea ili kuhakikisha tunapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, pamoja na changamoto ambazo zipo, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa miradi ambayo inaendelea kule Jimboni kwangu Kyerwa. Tunao mradi mkubwa ambao tumemaliza usanifu, mradi wa kimkakati wa Kata 18 kwenye vijiji 57. Mradi huu tunaamini mpaka hatua tuliyofikia ya usanifu, sasa kazi iliyobaki ni kazi ya kutangazwa tenda na kuutafutia pesa ili mradi huu uweze kuanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba sana Mheshimiwa Waziri, hali ni mbaya kwa Wanakyerwa, naomba sana mradi huu uangaliwe ili wananchi waweze kupata maji safi na salama. Tunajua maji ni uhai, maji ni kila kitu, maji ni uchumi. Bila kuwa na maji safi na salama mambo mengine hayawezi yakaenda hata tunaposema tunaingia kwenye uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uchumi wetu uweze kustawi, uweze kusonga mbele ni pale ambapo tutakuwa na maji safi na salama kwa sababu tunategemea kule vijijini ndiko kuna uzalishaji mkubwa na hawa wananchi wakipata maji safi na salama ule usumbufu wa kuamka usiku kwenda kutafuta maji utaondoka na wataingia kwenye shughuli za uzalishaji na uchumi wa Taifa letu utaweza kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri mradi huu nimeshakutana na wewe ofisini, nimeshakutana na Naibu Waziri, nimeshakutana na Katibu Mkuu lakini nimekutana pia na Waziri wa Fedha, ninaamini Mungu atasaidia mradi huu utapatiwa pesa ili uweze kuanza na wananchi wa Kyerwa waweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilisemee kwa upande wa Kyerwa, tunao mradi wa Kata ya Mabira unaendelea vizuri lakini kuna mradi wa Kata ya Kaisho, Rutunguru na Isingiro, mradi huu Naibu Waziri ulipofika Kyerwa walikueleza Mkandarasi kwa kweli hana uwezo na uliamuru Mkandarasi yule asimamishwe lakini tangu umetoka kule hakuna kazi inayoendelea, mradi umesimama na huyu Mkandarasi kwa kweli mimi niombe asije Wizarani kuwadanganya, hana uwezo kabisa. Wakati mwingine unajiuliza, hivi hawa Wakandarasi wanapatikanaje? Mtu ambaye anaendesha kampuni yeye na mke wake ndio unakuta wako site, ndio wanaofanya kazi, yaani hakuna kitu kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli naomba sana na Mheshimiwa Waziri ikiwezekana muunde Tume ya kwenda kukagua hii miradi na kuangalia uwezo wa hawa Wakandarasi kweli uwezo wao ni mdogo na wanakwamisha hii miradi isiweze kukamilika. Hili Wabunge wengi wameliongelea, maeneo mengi kwa kweli Wakandarasi hawana uwezo na wakati mwingine unaweza ukafikiri labda hizi kampuni wanapeana ni zile za urafiki au za kutafuta 10 percent ili waweze kupata chao waondoke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tuna nia ya dhati ya kuweza kuwapa maji safi na salama Watanzania, lazima tuhakikishe tuna wataalam wenye uwezo wa kuweza kusimamia miradi hii, lakini pia hata wale wanaotoa hizi tenda tuwafuatilie kwa karibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunamwamini Mheshimiwa Waziri, anafanyakazi zake vizuri pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu yote lakini lazima waangalie wataalam walionao kule chini, wanaweza wakawakwamisha ili wasiweze kufanikisha zile juhudi zao. Kwa hiyo, naomba sana hili waliangalie na pia kwa mfano, kama kule kwangu Kyerwa kuna watalaam wawili, Mzee moja ambaye ni Injinia kwa kweli ni mzee ambaye afya yake haijakaa vizuri, anahitaji msaada. Kwa hiyo, Kyerwa ni kama tuna mtaalam mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri hili aliangalie. Tunaposema tunataka tuwe na chombo ambacho kinajisimamia kuhusiana na maji, lazima tuwe na wataalam wa uhakika. Hata tukisema tutaunda chombo, bila ya kuwa na wataalam, tutakuwa tunapoteza muda. Nawaomba sana hilo tuliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano ni kwenye Wizara ya TAMISEMI, wameunda TARURA. Kwa muda mfupi TARURA wamefanya kazi nzuri sana, ni kwa sababu wamepeleka wataalam wenye uwezo. Nami nawaomba sana wapeleke wataalam ili waweze kuwapatia wananchi maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Waheshimiwa Wabunge wameongea sana kwamba ili tuweze kutatua tatizo la maji, tumeomba sana huu mfuko wa maji uweze kuongezewa fedha. Bunge lilishaazimia shilingi 50/=, lakini nashindwa kuelewa, ni kwa nini hili jambo linapata shida sana? Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aeleze kweli tuweze kuridhika. Hatuwezi tukaridhika kwa maneno tu, tunahitaji wananchi wetu waweze kupatiwa maji safi na salama ndiyo tunaweza kuelewa. Vinginevyo kwa kweli Jumatatu wakati unahitimisha, kama hutakuwa na majibu ya kuongeza shilingi 50/= kwa kweli hatutaelewana kama Wabunge wote walivyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nilikuwa najiuliza, hivi tukiamua leo Watanzania, maana tumeamua kuwapatia huduma Watanzania; tukiamua kila vocha ya shilingi 1,000/= ikatwe shilingi mbili tu, hebu jaribu kupiga mahesabu ni vocha ngapi ambazo zinaweza kuingizia pesa nyingi kwenye mfuko wa maji na tukaweza kutatua tatizo la maji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana, tunavyo vyanzo ambavyo vinaweza vikatupatia maji safi na salama. Watanzania tumeamua kupiga hatua, ni pamoja na kujifunga mkanda. Vinginevyo, tutakuja hapa tutaeleza mambo ya siasa, tutasema tunawapelekea maji lakini hakuna hatua yoyote ambayo tutachukua. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri hili uliangalie tuweze kuwafikishia wananchi wetu maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli baada ya kusema hayo, naishukuru Serikali, wanasema hata kwa kile kidogo uweze kushukuru. Kwa Kyerwa kwa kweli Awamu ya Tano angalau tunaweza tukasema kuna chochote tunachokiona, kama nilivyosema tunao mradi wa kimkakati wa vijiji 57 kwenye Kata 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuomba sana, Mheshimiwa Waziri mradi huu ndiyo unaweza ukawa mkombozi kwa wananchi wa Kyerwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi kuchangia kwenye mpango huu kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kunipa uhai na nguvu kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kutuletea mpango huu pia kwa ujasiri ambao ameendelea nao kusimama imara kuhakikisha anaisimamia wizara yetu inafanya vizuri kwa kweli tunampongeza hajatetereka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa maamuzi magumu ambayo amekuwa akiyachukua kwenye mambo mbalimbali ambayo ameyafanya na watanzania wanaona kwa kweli tunampongeza sana tunaendelea kumwombea afya njema, Mwenyezi Mungu amlinde aweze kutimiza majukumu yake ya kuwatumikia watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kuchangia kwenye mpango huu kuna mambo ambayo nitaishauri Serikali, nishauri upande wa miundombinu. Maeneo mengi ya uzalishaji ni vijijini tunaposema tunaingia kwenye Tanzania ya viwanda lazima tuangalie kule vijijini ambako tunategemea kuzalisha ambako kuna wakulima wengi zaidi ya asilimia 70 lakini ukija kwa upande wa miundombinu kama barabara kwa kweli Serikali pamoja na jitihada ambazo imekuwa ikionyesha lakini bado kuna maeneo mengi ambayo hayajafikiwa vizuri, mimi nitoe mfano kama kule kwangu Kyerwa, Kyerwa tunazalisha sana kwa mwaka sisi tunalima zaidi ya mara tatu lakini ukija kuangalia barabara zetu kwa kweli sio nzuri na ukienda upande wa pili kwa kweli ukaangalia barabara za wenzetu na ukaja kidogo kwenye upande wa Kyerwa kwa kweli inasikitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri tuwekeze nguvu sana kwenye miundombinu ili hawa wakulima wanapozalisha mazao yao yaweze kufika sokoni kirahisi ndipo tutaweza kuinua kwanza kipato cha mkulima pia kuinua kipato cha Serikali. Kwa hiyo, niombe hilo Mheshimiwa Waziri uliangalie tunazo barabara zetu za Mgakorongo kwenda Murongo mpaka Uganda lakini tunayo barabara ya Mulushaka kwenda Nkwenda Murongo hizi ni barabara ambazo ni muhimu ukilinganisha na uzalishaji ambao tunaupata kule Kyerwa kwa hiyo niombe sana hilo tuliangalie hatuwezi tukasema tunaingia kwenye uchumi wa viwanda wakati miundombinu ambayo tunategemea kupata mazao yaje kwenye viwanda vyetu kama sio mizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilizungumzie tunayo mazao yetu ya kimkakati tunategemea kuwa viwanda vingi lakini hivi viwanda lazima tuhakikishe malighafi zinatoka hapa ndani kama tunataka kuinua uchumi wa Taifa lakini tukitegemea malighafi zinazotoka nje tutakuwa tunawanufaisha wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana nchi yetu Mungu ameibariki tunaweza kulima maeneo mengine kama nilivyosema kule kwetu tunalima mara tatu kwa mwaka sasa niombe sana tuwekeze sana kwenye kilimo. Tumekuwa tukiongelea suala la mazao ya kimkakati, kahawa na haya mazao mengine lakini hatuoni jitihada za Serikali kuongeza uzalishaji wa hizi kahawa. Kwa hiyo, niombe sana kwenye haya mazao ambayo ni ya kimkakati ambayo tunategemea yeweze kuleta malighafi kwenye viwanda vyetu kama hatujawekeza nguvu. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri hili uliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine lisemee ni kwa upande wa afya, Pamoja na jitihada za Serikali kuwekeza kwenye vituo vya afya, kuwekeza kwenye hospitali lakini bado hatuna madaktari wa kutosha, tunategemea tuwe na madaktari tuwe na wataalam wa kutosha ili watanzania wawe na afya nzuri ndipo tutaweza kuwa na uzalishaji ambao ni mzuri. Kwa hiyo, niliombe sana Mheshimiwa Waziri hili mliangalie na muwekeze nguvu lakini pia pamoja na jitihada za Serikali tuna vituo vingi vya afya ambavyo vimeongezeka nchini pamoja na hospitali za Wilaya lakini bado vifaa havitoshi. Kwa hiyo, niombe sana hili la lenyewe tuliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ili tuweze kufika kwenye uchumi wa viwanda lazima tuwe na maji safi na salama kwa wananchi wetu. Wananchi wetu wanatumia muda mwingi kwenda kutafuta maji wakati mwingine masaa hata mawili, matatu lakini hakuna maji ambayo yanaweza kuwasaidia wananchi wetu waweze kuzalisha. Mwananchi ameondoka saa 11 ameenda kutafuta maji halafu unategemea atarudi saa nne aweze kwenda shambani kulima, na hao wakulima ndio tunaowategemea waweze kuzalisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyeiti, kwa hiyo, niombe sana Serikali pamoja na jitihada zake niombe sana muendelee kuwekeza upatikanaji wa maji safi na salama na nimwombe sana Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikikusumbua sana kwenye miradi ambayo iko kule Kyerwa tunao mradi wa vijiji 57 niombe sana miradi hii iangaliwe ili wananchi wetu ambao hawa tunategemea ndio wawe wazalishaji wakubwa kuinua uchumia wa Taifa letu waweze kuwa na muda mwingi wa kwenda kuzalisha kuliko kuwa na muda mwingi wa kwenda kutafuta maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona sana huu mpango ni mzuri lakini haya mengine tukiyazingatia nimeongelea suala la maji, miundombinu, kilimo hivi vitu vikiangaliwa vizuri ninaamini tutapiga hatua kutoka hapa tulipo na uchumi wa Taifa letu utaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru asante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu na bajeti ambayo kwa kweli kila mmoja ambaye ameisoma bajeti hii kwa kweli inagusa maisha ya Watanzania na imekuwa bajeti ya mfano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunipa afya na nguvu lakini pia nimpongeze Waziri Dkt. Mpango kwa kazi nzuri unayoifanya na tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kukupa afya nikutie moyo kelele hizi unazozisikia kutoka kwa wenzetu usitegemee zitaisha, wewe unaposikia kelele ujue mambo yanakuwa mazuri songa mbele uendelee kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii kwa jinsi ambavyo imeletwa kama tutaisimamia vizuri ninaamini uchumi wa Taifa letu unaenda kuinuka na tunaenda kuona mambo makubwa ambayo hatujawahi kuyaona katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiongelee kwa upande wa kilimo, pamoja na jitihada za Serikali bado hatuja wekeza nguvu kubwa ya kutosha kwenye kilimo. Nasema hivi kwa sababu tunataka kuingia kwenye uchumi wa viwanda ili viwanda vyetu viweze kupata nguvu kubwa lazima tuwe na malighafi ambazo zinapatikana katika nchi yetu, tusitegemee kupata malighafi ambazo zitatoka nje kuendeleza viwanda vyetu. Kwa hiyo, tujikite kwenye kilimo ambacho kitainua kwanza kipato cha Mtanzania na asilimia kubwa zaidi ya 80 ni wakulima, tukiwekeza kwenye kilimo kwa mfano wakapata mbegu bora wakawa na masoko ya uhakika, dawa na pembejeo ninaamini tunaweza uchumi wa Taifa letu ukainuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Serikali imejikita kwenye mazao ya kimkakati ambayo ni korosho, pamba, chai, kahawa mazao haya tukiyasimamia ninaamini yanaweza yakainua kipato cha nchi yetu pia kipato cha mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la zao la kahawa ambalo tukilisimamia vizuri linaweza kuingiiza pesa nzuri na nyingi kwenye Taifa letu, lakini pamoja na kuondoa zile tozo ambazo zilikuwepo bado kahawa haijaweza kumnufaisha mkulima. Zao la kahawa siyo linalimwa Kagera tu zao la kahawa linalimwa maeneo mengi katika nchi yetu, niiombe sana Serikali ilisimamie.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiki ni kitu cha kushangaza pale kwangu Kyerwa ukivuka tu mpaka hata ukiita wanasikia, ukivuka tu mpaka ukienda Uganda kahawa ni shilingi 2000 lakini ukija kwetu ni shilingi 1100. Ukienda kwenye nchi ya Rwanda kahawa ni shilingi 3000. Ninaiomba sana Serikali hawa wenzetu hii kahawa wanaiuza wapi tuangalie huko wanakouza kahawa na njia wanazotumia ili tuweze kuinua kipato cha mkulima lakini kipato cha Serikali yetu ninaamini hili litasimamiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la kahawa kuna watu ambao mimi ninaamini bila kuingilia kati, Serikali ikaingilia na Waziri wa Kilimo angekuwepo hili akalisikia, kuna Bodi ya Kahawa, unasema unaunda Bodi ya Kahawa hii angelisikia kuna Bodi ya Kahawa, wewe unasema unaunda Bodi ya kahawa hii bodi inawakilisha wafanyabiashara hakuna mkulima hata mmoja ambaye anawakilishwa mnategemea hawa wakulima ni nani atakayewasemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na vikwanzo vingi kwa mfano mwaka jana tulipata KDCU ambao ni Chama cha Ushirika walipata mteja kwa kununua kahawa lakini ilichukua siku 28 kutoa kibali, hii ndiyo bodi ya kahawa na ofisi ya Mrajisi. Mwaka huu tunatangaza msimu wa kahawa mwezi wa Tano mpaka sasa hivi bado kibali hakijatolewa na Benki ya Kilimo ipo tayari kutoa pesa imetenga zaidi ya bilioni 40, lakini bado ofisi ya Mrajisi haitoi kibali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ni vikwazo ambavyo haviwezi vikainua kilimo kwa sababu huyu mkulima anakata tamaa, lakini kama tukiondoa hivi vikwazo ambavyo vipo kwenye Tume ya Ushirika vipo kwenye Bodi ya Kahawa na vipo kwenye ofisi ya Mrajisi, nanaamini mkulima ataongeza kilimo na pato la Taifa litaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nnaipongeza sana Serikali kwa kuwekeza katika mradi mkubwa huu wa umeme, tunasema tunaingia kwenye uchumi wa viwanda hatuwezi tukaingia kwenye uchumi wa viwanda kama hatuna umeme wa uhakika. Hatuwezi tukawakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza kwenye nchi yetu kama hatuna umeme wa uhakika. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa maamuzi makubwa na mazito ambayo imeendelea kuyachukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi Wabunge tulikuwa tunalalamika tunasema Serikali inashika huku, inashika huku haileti miradi ambayo inaweza ikasimamia sasa Serikali imekuja na miradi hii mikubwa nilitegemea kama Wabunge wote tuungane kwa pamoja tuiunge mkono
Serikali kuona hii miradi inakamilika, sasa hivi tunashauri, sasa Serikali ikifaya wenyewe tunageuka! Kwa kweli huu niseme ni kama uwendawazimu au ni kama uigizaji, tufanye mambo ambayo tunashauri Serikali, Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi ni Serikali sikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine watu walikuwa wanalalamika wanasema tumewekeza kwenye mradi wa Stigler’s Gorge. Huu mradi ninaamini tumekuwa tukilalamika Wabunge tunasema barabara zetu zinaharibika kwa sababu ya mizigo, huu mradi utakapokuwa umekamilika tunaamini barabara zetu zitakuwa salama na usafirishaji utakuwa mzuri kuongeza kipato cha Taifa. Tunaboresha bandari, bandari tunapoiboresha tunategemea mzigo tena ije ipite barabarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niendelee kuipongeza sana Serikali kwa kazi hii inayofanyika, tusitegemee wenzetu kuwa watasifia kwa sababu yale ambayo walikuwa wanashauri ndiyo leo tunayoyafanya, kwa hiyo wamekosa hoja hawana jambo jingine ambalo wanaweza kuja nalo jipya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze sana Serikali na niiombe sana Serikali Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango bajeti hii kama ulivyoileta Mungu akuwezeshe uweze kuisimamia vizuri na ninaamini tunakoenda tunaenda kuzuri, Tanzania tunavyopiga hatua siyo kama Tanzania ya miaka 20 iliyopita na mtakuja kujionea wenyewe kwenye Uchaguzi Mkuu unaokuja uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mtaona mambo makubwa ambayo Watanzania wanayaona wakati mwingine mnaweza mkafikiri Watanzania hawasikii, Watanzania wanasikia na wanaona mambo makubwa yanayofanyika katika Taifa hili na ndio maana kila kona tunakoenda Mheshimiwa Rais anaungwa mkono na Serikali yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya ninakushuru, ahsante sana.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nimshukuru kwanza Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na nguvu ya kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo wa Kyerwa. Nichukue nafasi hii kwanza kukupongeza wewe binafsi kwa miaka hii kwa kweli umeonesha uchapaji kazi mkubwa kwenye Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mimi kama unavyosema kama mchungaji naendelea kukuombea Mwenyezi Mungu akupe afya na nguvu ili urudi tena uendelee kuchapa kazi hii ambayo umeichapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake. Ni ukweli usiopingika Mheshimiwa Waziri Mkuu amechapa kazi kubwa na amekuwa msaada mkubwa kwa Mheshimiwa Rais kwa ziara nyingi ambazo amekuwa akizifanya hata kule kwetu Kagera, ziara ambazo amekuwa akizifanya wale ambao walikuwa wakionekana ni Mungu watu siku hizi wamekuwa wapole. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichangie kwa upande wa sekta ya kilimo; kwenye hotuba ya Waziri Mkuu sekta ya kilimo ni muhimu sana na ndiyo sekta ambayo ina wazalishaji wakubwa. Niiombe sana Serikali imefanya mambo makubwa sana, lakini katika sekta hii bado hatujaweka nguvu kubwa. Tunasema hii nchi ni Tanzania ya viwanda, lakini hivi viwanda lazima vipate malighafi kutoka kwa hao wakulima, tusipowekeza nguvu kubwa tutaendelea kuleta malighafi kutoka nje na tutaendelea kunufahisha Mataifa mengine wakati hizi malighafi zingeweza kuzalishwa hapa kwetu. Kwa hiyo, niombe sana pamoja na jitihada za Serikali, lakini iongeze nguvu, kwa kweli bado kabisa hatujaona nguvu kubwa kama ambavyo tumewekeza kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kwa mfano suala la mazao haya ya kimkakati. Haya mazao ya kimkakati naamini tukiweka nguvu kubwa yatatusaidia sana kuongeza pato la Taifa na ndiyo mazao ambayo ni muhimu lakini pia yanaweza kutuingizia pesa ya kigeni kwa mfano, niseme kahawa, hili ni zao la muhimu sana. Pamoja na jitihada za Serikali za kuturudisha kwenye ushirika bado bado, mimi niseme kama mkulima ambaye natoka kwenye mkoa ambo tunalima kahawa bado hatujaona jitihada kubwa sana kubwa sana ambazo Serikali imeweka.

Mheshimiwa Spika, niombe sana tuendelee kuweka jitihada ili huyu mkulima ambaye anazalisha aendelee kuongeza uzalishaji. Mimi naamini tusipoweka nguvu kubwa katika mazao ya kimkakati wakulima hawa watakata tamaa. Maeneo mengine hata kule kwetu Kagera watu wameanza kukata tamaa sehemu zingine ile mibuni wanaikata wanaweka mazao mengine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe sana Serikali iongeze nguvu lakini ni pamoja na kuwa na soko la uhakika. Hawa wakulima wanapolima mazao yao wapate soko la uhakika lakini pia wapate bei nzuri.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kahawa kumekuwa na sintofahamu. Majirani zetu Uganda inasemekana wana bei kubwa na hili limeleta changamoto kubwa kwenye Mkoa wa Kagera na hasa kwenye Jimbo langu. Alipokuja Mheshimiwa Naibu Waziri alipofika kule akasema wamefanya utafiti Uganda wamekuta wana bei kubwa. Sasa baada ya kusema wana bei kubwa nini kinafuata?

Mheshimiwa Spika, mimi nafikiri kama kweli wana bei kubwa kwa nini tusiwaruhusu hawa wananchi tukaweka utaratibu kahawa hii hawa Waganda wakaja wakanunua wakatupa bei nzuri kuliko kuja unawaambia wananchi halafu unaondoka. Hata hivyo, Naibu Waziri mwingine anasema tatizo la bei ya kahawa ni soko la dunia. Kwa hiyo, hii inawachanganya wananchi hata sisi ambao ni wawakilishi tunakosa majibu ya kuwaambia wananchi wetu. Kwa hiyo, kama Uganda kuna bei kubwa ambayo inaizidi ya Tanzania na changamoto kama sio soko la dunia niombe sana Mheshimiwa Waziri basi hawa Waganda wawekewe utaratibu waje wanunue kahawa yetu ili wakulime wapate bei nzuri na wasiendelee kulalamika na mwisho wa siku wakakata tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi kama mwakilishi furaha yangu ni kuona wananchi wangu wanapata bei nzuri ya kahawa na wanajengewa ambayo mazuri kuweza kuuza kahawa yao. Haijalishi ni nani atakayenunua hata kama anatoka Uganda au Ulaya, cha muhimu Serikali iweke utaratibu mzuri.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuliongelea ni suala la miundombinu. TARURA wana barabara nyingi ukilinganisha na TANROADS na ndiyo wako vijijini ambako ndiko kuna uzalishaji mkubwa. Hawa TARURA tunaendelea kuwapa asilimia 30 wahudumie mtandao mkubwa ambao hata TANROADS hawafikii nusu, hili kwa kweli halijakaa sawa. Niombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu aliangalie jambo hili na ikiwezekana msiwaachie hawa Mawaziri kwa sababu kila mmoja anavutia upande wake. Mheshimiwa Waziri Mkuu aingilie kati hili jambo TARURA wapewe pesa ya kutosha ili waweze kuhudumia barabara zetu. Vinginevyo wananchi hawa wanapozalisha hawatakuwa na miundombinu rafiki ya kusafirisha mazao yao kufika kwenye masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mikoa mingine ambayo kwa kweli tumejaliwa, ukiondoa hii mvua iliyokuja kipindi hiki lakini sisi kwetu Kagera, kwa mfano kwangu Kyerwa miezi karibu kumi yote sisi tuna mvua, sasa huku barabara zinaharibika sana. Niombe sana Serikali maeneo haya ambayo yana mvua kipindi kirefu yaongezewe pesa ili barabara ziweze kutengenezwa. Kwa kweli nipongeze kwani Serikali imejitahidi TARURA wanafanya kazi nzuri wakiongezewa pesa naamini watafanya kazi nzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee suala la Corona. Mimi niipongeze kwa kweli Serikali imejitahidi sana na huyu mama yetu Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na msaidizi wake wanafanya kazi nzuri na tumeona Waziri Mkuu kazi anayoifanya. Hawa wanaobeza siku zote wanasema mpiga debe huwa si msafiri acha wanaosafiri waendelee kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za Serikali lakini wengine walikuwa wanashauri sijui kuna kujifukiza na kadhalika, lakini mimi nije mbele yako na niombe hili neno kama litapata kibali chako lifanyike kwa sababu una mamlaka ya kuamua jambo lolote ukiwa kwenye Kiti chako. Ukisoma kwenye Maandiko Matakatifu magonjwa yote yaliporuhusiwa na Mungu ilikuwa ni dhambi. Dhambi ndiyo imesababisha magonjwa haya yaje yatupate kwa sababu Mungu hawezi kuruhusu watu wake waguswe na adui kama hawajatenda dhambi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi pamoja na juhudi hizi zinazofanyika niombe sana, sisi hapa Bungeni ni wawakilishi wa wananchi wa Watanzania wote, Kiti chako kama kitaridhia tutoe dakika hata tano tusimame mbele ya Bunge hili tukatubu kwa ajili ya Taifa la Tanzania. Mheshimiwa Rais alishaonesha mfano mzuri na akatoa Maandiko sasa niombe sana na wewe utupe kibali kutoka kwenye Kiti chako tusimame tutubu kwa ajili ya dhambi ya Tanzania. Ninaamini Mungu ataturehemu na ataliponya Taifa letu tutakuwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni suala la NIDA ambalo kwa kweli halijakaa vizuri na limeleta vurugu. Wewe unawaambia wananchi simu zitafungwa wakati NIDA hawajatoa vitambulisho, hivi huyu mwananchi unayemfungia simu zake hujampa kitambulisho, hujampa huduma kosa lake ni lipi?

Mheshimiwa Spika, niombe hili jambo Serikali iliangalie na ikiwezekana wakae wajipange, halijakaa sawa. Kule kwetu limeleta mpaka rushwa, imekuwa ni biashara, anayekuwa na pesa nyingi ndiye anaweza kupata kitambulisho, haliko vizuri kwa ujumla. Niombe sana Serikali ijipange jambo hili iliangalie na ikiwezekana wafuatilie maeneo mengine waone linaendaje.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kabla sijachangia nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa nguvu na uhai kuwepo katika Bunge hili. Kipekee, niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa ambao wameniamini tena kwa mara nyingine na kunipa kura nyingi za kishindo ambazo zimenirudisha katika jengo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikichangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais, kwa kweli niseme ukisikia na ukisoma vizuri kwenye hotuba hii, hotuba hii imejaa matumaini na neema kubwa sana kwa Watanzania. Mimi nachosema wasaidizi wake ambao Mheshimiwa Rais amewaamini, niombe wachukue hatua ambazo zitaibeba hotuba hii na kuifanyia kazi. Kwa nini nasema hivyo? Mara nyingi wakati mwingine viongozi wetu wanaongea mambo mazuri na makubwa lakini yanaishia kwenye vitabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwanza niongelee upande wa kilimo, tunaongelea Tanzania ya viwanda. Wazalishaji wakubwa wako vijijini, lazima tuwekeze nguvu kubwa kwa wakulima wa hali ya chini na ili tuweze kufanikiwa lazima tuandae miundombinu mizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wamekuwa wakichangia kuhusu TARURA, ni ukweli usiopingika kuwa mtandao wa barabara nyingi sana uko kule kwa wananchi wa hali ya chini na ndiyo wazalishaji wakubwa. Mimi nashindwa kuelewa, kwa nini hili jambo tumeshauri muda mrefu toka Bunge lililopita lakini bado halijatatuliwa naomba Serikali ilione hili jambo ni la muhimu. Tunaongelea Tanzania ya viwanda, hatuwezi tukafanikiwa kwenye viwanda vyetu kama hatutaboresha miundombinu mizuri kwa wananchi wetu wa hali ya chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwa mfano kule vijijini, mimi niongelee kwa mfano Kyerwa, barabara hali ni mbaya lakini haohao ndiyo wazalishaji wakubwa. Ukienda kwa Mkoa wa Kagera, ndizi zinazotoka Kagera ndizo zinalisha nusu ya Tanzania. Tusipoboresha mazingira haya yawe mazuri huyu mkulima akaweza kusafirisha mazao yake vizuri, hatutaweza kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini siyo hilo tu; malighafi nyingi tunategemea zitoke kwa hawa wananchi wa hali ya chini. Tusipoboresha haya mazingira mazuri, tukaweka miundombinu mizuri, tutaishia kuchukua malighafi kule nje kuwanufaisha watu wa nje badala ya kutumia malighafi ambazo zinazalishwa hapa kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana Mawaziri ambao wanahusika suala la TARURA walitilie mkazo.niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, suala hili ni kwa faida yetu sote. Tuombe sana Wizara inayohusika na TARURA itengewe pesa, kama haitatengewa pesa sisi ndiyo tunaopitisha bajeti, haiwezekani tukae tunazungumza mambo hayafanyiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, nimekuwa nikishangaa, ukienda kwenye vyuo vyetu, kwa mfano kile Chuo cha NIT, tuna wataalam ambao wanaweza wakatengenezwa pale kusimamia miradi yetu mikubwa. Leo hii tunao Mradi wa SGR, mradi huu unajengwa na watu kutoka nje lakini Serikali imejipanga vipi kuandaa wataalam ili hawa waliojenga huu mradi wakishaondoka tupate wataalam wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiwasikiliza wale watu wa NIT wanakwambia mtaalam mmoja kwenda kusoma nje anatumia zaidi ya milioni 200, lakini wao kumuandaa mtaalam huyohuyo wanatumia milioni 25, lakini unakuta chuo hichohicho Serikali bado haijawekeza nguvu. Sasa hili na lenyewe lazima tuliangalie, vinginevyo hii miradi mwisho wa siku itakosa wataalam wetu wa kusimamia. Jambo ambalo unalisimamia wewe mwenyewe hata kama mradi ni wako unakuwa na ule uzalendo. Haya masuala ya miradi kusimamiwa na watu wengine, tunakwenda kutafuta wataalam nje, hili jambo halijakaa sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake amezungumzia miradi mingi ya maji. Kwa kweli tuseme ule ukweli, miradi mingi ya maji bado haijafanikiwa. Unakuta hapa wamedonoa kidogo, hapa wamegusa kidogo. Niiombe sana Serikali tusianze kufanya usanifu miradi mipya, tukamilishe ile miradi ya zamani ndiyo tuanze na mingine. Hili suala la kushika hapa kidogo tuonekana tuna miradi mingi ambayo haina manufaa hatutaweza kufika mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Kyerwa tuna mradi wa maji wa vijiji hamsini na zaidi, mradi huu ukikamilika naamini utanufaisha wananchi zaidi ya laki mbili. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali, tunapoanzisha miradi hasa hii ya maji basi ikamilike kuliko tunagusa kidogo, Serikali inaonekana tuna miradi mingi sana lakini mwisho wa siku hatuikamilishi. Kwa hiyo, niombe hili na lenyewe tuliangalie. Tutakapokuwa tumehakikisha hawa wananchi wetu wamepata maji, nina uhakika hata uzalishaji utakuwa mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho napenda kukiongelea ni barabara zetu kuu, kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha. Ukienda kwa mfano mpakani kwetu na Uganda ni aibu. Kule kwetu unaweza ukafikiri ni uchochoro kule kwao ni Ulaya. Hizi barabara ambazo zinaunganisha nchi na nchi niombe sana tuweze kuzikamilisha ili na sisi tuonekane ni sehemu ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na nguvu kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kabla sijaanza kuchangia, kipekee nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya. Ni ukweli usiopingika, kazi kubwa zilizofanywa na Awamu ya Tano huwezi ukamweka pembeni Makamu wa Rais ambaye leo hii ni Rais wetu na pia na Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nakushukuru kwa ziara yako uliyoifanya Wilaya ya Kyerwa ambayo mimi kama Mbunge nimeanza kuona matunda yake. Mheshimiwa Waziri Mkuu, nakushukuru sana. Kabla sijaanza kuchangia, nikukumbushe ahadi ambazo tulikueleza na wewe ukaahidi. Mheshimiwa Waziri Mkuu ulipokuja, kabla hujafika kwenye Kituo cha Mkutano, ulipita Kata ya Nkwenda. Pale Nkwenda kuna upungufu wa kukamilisha jengo la mama na mtoto, nawe uliahidi ukiwa pale kwenye Kata ya Nkwenda, kuwa jengo hili litakamilishwa na ukaahidi pia kuongeza Vituo vya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine Mheshimiwa Waziri Mkuu, ulipopita kwenye barabara ya Murushaka kwenda mpaka Mulongo ulijionea na wewe mwenyewe ukaahidi barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami. Nashukuru kazi imeanza. Mheshimiwa Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipofika, aliahidi kilometa 50. Nimpe majibu dada yangu aliyekuwa anasema kuna sintofahamu; hakuna sintofahamu yoyote, barabara inajengwa kuanzia Rubwera kwenda Karagwe. Kwa hiyo, hilo nimpe majibu. Jambo lingine ukitaka kuuliza, mwulize mwenye nyumba, anaweza akakupa majibu kuliko kumwuliza mpangaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni upande wa maji. Nashukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja, tulimweleza changamoto tunayoipata kwenye maji na ninaishukuru Serikali kwa jitihada ambazo zinaendelea. Kwa kweli kwa sasa hivi tuna hatua nzuri. Tumeshakutana na Waziri na Katibu Mkuu; kwa kweli mimi kama Mbunge naridhika na ninawaahidi wananchi wa Jimbo la Kyerwa kuwa nimejipanga vizuri pamoja na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuwapelekea majisafi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la umeme Mkoa wa Kagera. Kwa kweli tunayo changamoto kubwa kwenye Mkoa wa Kagera. Umeme wetu ni umeme ambao kwa kweli hautabiriki, unaweza ukawaka asubuhi, saa nne umezimika, saa sita unawaka. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali hili suala la umeme Mkoa wa Kagera lipatiwe majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la kilimo. Tumekuwa tukiongea sana hapa kuhusiana na kilimo, lakini mimi niseme zipo jitihada ambazo kwa kweli bado hazijaridhisha. Ni jambo ambalo linasikitisha, ukiangalia nchi nyingine ambazo zimeendelea na nchi hizi hazina mvua ya kutosha, lakini ukija kwetu tuna mvua nyingi, Mungu ametujaalia ardhi yenye rutuba, lakini hatujaona hii neema ambayo tunayo ni namna gani tunaweza kuitumia. Naiomba sana Wizara ya Kilimo, tujikite kwenye kufanya utafiti, ni kitu gani ambacho tunahitaji kukifanya ili kilimo chetu kiwe na tija? Vinginevyo tutakuwa hapa tunaimba bila kuwa na majibu ambayo ni sahihi. Kilimo ni afya, kilimo ni uhai, kilimo ni biashara na kilimo ni viwanda. Leo hii tunasema tumeanzisha viwanda, viwanda viko vingi zaidi ya 8,000, lakini hivi viwanda vinahitaji malighafi. Tutaenda kutafuta malighafi nje wakati tungeweza kuzalisha kwetu na neema ipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwenye mazao ya kimkakati. Mazao haya hayajapewa kipaumbele. Pamoja na kusema haya mazao tumeyatenga kimkakati, lakini mimi niseme bado hayajapewa kipaumbele. Kwa mfano, kwenye zao la Kahawa; pamoja na kulima hili zao, bado hatuna soko la uhakika. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara tujikite kutafuta masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeondoa biashara ya butura na mimi kama Mbunge ninajua biashara hii ilikuwa inawanyonya wakulima. Ni mkakati upi ambao tumekuja nao kama Serikali? Huyu mkulima anapolima kabla hajaenda kuvuna kupeleka hii Kahawa kwenye soko, anapataje pesa ya kumsaidia ili aweze kuhudumia hii Kahawa? Tunasubiri mwishoni ndiyo tunakuja kwa mkulima na huyu mkulima hatujamsaidia mwanzo. Kwa hiyo, naomba sana tutafute masoko. Wizara tokeni mkatafute masoko. Naomba hili tuliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, ili kilimo chetu kiende vizuri, lazima tuboreshe miundombinu ya barabara. Barabara zetu ambapo huku kwa mkulima ndio kuna mzalishaji siyo nzuri, hali ni mbaya. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iboreshe barabara za TARURA ambako huku ndiyo kuna mzalishaji mkubwa. Kwa hiyo, naomba sana hili tuliangalie ili tuweze kumsaidia mkulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo nilisemee…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na nguvu kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa.

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee suala la NIDA, suala hili kwa kweli limekuwa ni kero. Mimi kama Mbunge naunga mkono Serikali kusema kila raia awe na kitambulisho cha NIDA, lakini ni jambo ambalo linashangaza, Serikali inatangaza wananchi hao wawe na vitambulisho, lakini ninachokiona hiki kilichotangazwa, Serikali ilikuwa haijajiandaa. Hawa wananchi wanasema sisi tupo tayari, mtupe vitambulisho, wanakwenda kwenye Ofisi za NIDA hawapati vitambulisho wanaambiwa shida ni mtandao, kwa kweli hili jambo halijakaa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe sana Serikali iliangalie na nishauri kama Serikali katika hili bado haijajipanga vizuri, ni afadhali kulisitisha kuliko wananchi kuendelea kukosa huduma. Kwa sababu limekuwa ni kero kubwa sana na ukilinganisha kwa mfano mazingira ya kule kwetu Kyerwa, wananchi wanatoka maeneo ya mbali anakwenda wilayani zaidi ya kilomita 30, anashinda pale, hajapata kitambulisho anarudi nyumbani, imekuwa ni kero kubwa sana. Kwa hiyo niiombe sana Serikali ili iliangalie, ikiwezekana kama bado haijajipanga isitishe.

Mheshimiwa Spika, kule kwangu kuna shida, ukienda kwenye Ofisi za NIDA wanasema shida ni mtandao, mtandao mpaka wafuate Wilaya nyingine ya Karagwe. Kwa hiyo niombe zile wilaya ambazo zipo pembezeni na hakuna mtandao wangeacha hili jambo kwa sababu limekuwa ni kero kubwa sana, yaani kule kwetu ukiongelea NIDA wanasema hii ni hatari. Kwa hiyo niombe sana hili liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka nilizungumzie ni suala la watu wa Uhamiaji, kubainisha wale ambao ni raia na sio raia. Mazingira ya kule kwetu ukisema mwananchi aende wilayani ni kero kubwa. Ushauri wangu ninaotoa, Maafisa hawa wa Uhamiaji wawatumie Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji. Waende kule site wakawatumie hawa ndio wanaweza kutambua raia ni nani, haiwezekani Afisa Uhamiaji umetoka Dar es Salaam au Dodoma, unafika Kyerwa unasema huyu siyo raia, hili sio sawa. Wawatumie viongozi ambao wananchi wamewachagua Maafisa Watendaji, Wenyeviti wa Vijiji ili waweze kujua ni nani ambaye ni raia au siyo raia, vinginevyo hii biashara ni kama kuwaneemesha watu. Kwa hiyo hilo niombe sana tuliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalotaka kulizungumzia ni kuhusu hawa mapolisi wetu, pamoja na mambo mengine ambayo yanazungumzwa lakini wanafanya kazi kwenye mazingira magumu sana. Ukifika kule kwangu, sasa hivi wilaya ina zaidi ya miaka saba hawana ofisi, wanafanyakazi kwenye Ofisi ya Kijiji. Tulivyomaliza uchaguzi nilikwenda kuikagua ile ofisi inadondoka wakati wowote, imebidi nichukue fedha niwape milioni 10 angalau tuweze kuboresha ile ofisi ambayo ni ya kata. Kwa hiyo niombe sana, hili liangaliwe. Pia hawana nyumba, wanaishi kwenye mazingira magumu, yaani ni kama kundi fulani ambalo limetelekezwa. Kwa hiyo niombe sana tuliangalie, tuweze kuboresha mazingira wanayofanyia kazi, kwa sababu wanafanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninaloomba, kule kwetu kuna kitu kinaitwa gongo, ile gongo inatokana na ndizi, hizi ndizi zinatengenezwa wanapata gongo. Serikali tunaomba ifanye utafiti hii gongo iweze kuhalalishwa. Kama tunaruhusu ndizi na hiki kitu kinatokana na ndizi, kwa sababu kuna gongo nyingine inatokana na vitu vya ajabu ajabu, lakini hii inatokana na ndizi. Kwa hiyo, naomba kwa Mheshimiwa Waziri, Wanakyerwa wamenituma, hili jambo liangaliwe. Kwa sababu imekuwa ni biashara ya watu…

SPIKA: Yaani hiyo hoja ni muhimu sana, kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mchungaji anaomba gongo hii.

MHE. CHARLES P. MWIJAGE: Taarifa.

SPIKA: Na kuna taarifa juu ya hayo. Taarifa ipo upande gani! Haya endelea.

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, napenda nimpe taarifa ndugu yangu Mheshimiwa Bilakwate, wanachotengeneza Kagera sio gongo ni enkonyagi au Kaliinya. Kwa hiyo, enkonyagi ni tofauti na gongo, gongo ni haramu enkonyagi sio haramu. (Makofi)

SPIKA: Pokea taarifa Mheshimiwa Bilakwate.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, Ahsante hiyo taarifa nimeipokea kwa kweli inaitwa enkonyagi. Kwa hiyo hili niombe sana, Serikali iliangalie namna gani wanaweza kutafiti kwenye kinywaji hiki ili kiweze kuruhusiwa kwa sababu hata ukimuuliza Mheshimiwa Mwijage na Waheshimiwa wengine wanaotoka Kagera, wote wamesomeshwa kutokana na hiyo akaguri, akakonyagi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine niongelee suala la bodaboda. Hawa vijana wamejiajiri, hebu niombe sana Polisi wetu wajikite kuwapa elimu kuliko kukimbizana nao kila sehemu. Wanafanya kazi kwenye mazingira ambayo ni magumu, unamkamata bodaboda ambaye kwa siku akipata faida kubwa ni shilingi 30,000, unamtoza shilingi 50,000, unamtoza shilingi 200,000; hili kundi tutaendelea kulifanya kuwa maskini. Kwa hiyo niombe sana hili liangaliwe.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Spika, kwanza, niwapongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Kipekee hizi pongezi sio za kubahatisha, Mheshimiwa Waziri unafanya kazi nzuri sana. Kitu kinachotia moyo ni namna ambavyo unawasilikiza Wabunge wanapoleta hoja zinazotoka kwenye majimbo yao. Mimi nikushukuru kwanza kwa miradi ambayo tumekaa pamoja na watendaji wenzako na nimeona kwenye bajeti umeiweka. Ni jambo zuri na mimi niseme kwa Kyerwa maeneo mengi kwa kweli hatuna maji safi na salama na wewe hili umeliunga mkono kwa kuweka vijiji vyote, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti tunaona mipango mizuri lakini jambo lingine hii fedha inaletwa? Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri ili kazi yako iendelee kuwa nzuri hizi fedha ziletwe. Kuna maeneo ambayo kwa kweli kwangu yana shida kubwa sana, ukienda kwenye Kata kama za Bugala, Businde, Murongo kwa kweli hali ni ngumu sana. Nishukuru nimeona vijiji vya Bugala na Businde kule mmetenga fedha kwa ajili ya kuchimba visima lakini maeneo mengine kama Kibale ule mradi wa Kigologolo kuuongezea uwezo ili uweze kusambaza maji kwenye vijiji vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine tuliongelea mradi wa vijiji 57, mradi huu ni mzuri sana na ndio mkombozi kwa wananchi wa Kyerwa. Kwa hiyo, niombe sana fedha ambayo mmeitenga iwafikie ili wananchi wa Jimbo la Kyerwa waweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, RUWASA bado ni wachanga na ukija kule kwangu hawana gari wala ofisi, hawa watu wanawezaje kufanya kazi? Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri waongezee uwezo ili waweze kufanya kazi nzuri. Mimi niseme kwa upande wa Kyerwa yule kijana ambaye mmeleta pale anafanya kazi nzuri lakini anafanya kazi kwenye mazingira magumu. Kwa Kyerwa ni kipindi kirefu cha mvua hata kwa pikipiki huwezi kwenda kukagua miradi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii miradi tunayoitengea fedha kama haitapata usimamizi mzuri tutakuwa tunafanya kazi bure. Tutakuwa tunapeleka fedha nyingi lakini fedha ambayo hatuoni inachokifanya kwa sababu hakuna usimamizi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge hapa wamekuwa wakiongelea suala la kubambikiziwa bili. Hili lipo kila maeneo hata hapa Dodoma, mimi nimekutana na watu wengi pale ofisini kwa Waziri wanalalamika. Nimekwenda Karatu, kule ukitaka kuchota maji unaingiza kadi kama ulivyolipia ndivyo unavyopata maji. Naomba hili lifanyike nchi nzima ili tuondoe suala la kubambikizia watu bili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mama mmoja nilimkuta ofisini kwa Waziri wamemletea bili milioni 1 na hana hata biashara na hili limekuwa likifanyika maeneo mengi. Hata mimi nyumba ninayokaa hapa Dodoma wameleta bili ya ajabu kwelikweli tena kipindi ambacho sisi hatukuwepo…

T A A R I F A

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa, endelea nakuruhusu.

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa
Spika, nataka kumpa taarifa tu ndugu yangu anayezungumza kwamba hata kwenye nyumba ya baba yangu mzazi Mzee Gwajima ambapo anaishi yeye mwenyewe bili inakuja shilingi 600,000 kila mwezi. Anachosema ni kweli na ni sahihi.

SPIKA: Unapokea taarifa hiyo Mheshimiwa Bilakwate?

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo naipokea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo lazima waje na mpango mtu analipia kutokana na matumizi yake, kama ilivyo LUKU, tutakuwa tumemaliza hili suala la kubambikizia watu bili. Sijui kuna nini kinaendelea pale, mpaka watu wengine wakawa wanasema wanakusanya fedha ili waweze kujilipa vizuri, suala hili linaichafua Wizara lazima Waziri aliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la mwisho ambalo napenda kuchangia ni kuhusu RUWASA. RUWASA ni ofisi ambayo inajitegemea, kwa upande wa Kagera hakuna Bodi ya Manunuzi wanategemea BUWASA. Kwa hiyo, niombe sana suala hili liangaliwe wawezeshwe ili wawe na Bodi yao waweze kuwa manunuzi yao kuliko kutegemea ile ya Bukoba Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na nguvu kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, bajeti yake ni nzuri na naamini hii ndio bajeti ya kwanza kuwasilisha. Ninachoomba kwa Mheshimiwa Waziri, Wabunge wamekuwa wakisema kumekuwepo na upendeleo na ukweli nakiri, ukiangalia huu upendeleo umekuwepo kwa sababu kuna maeneo mengine unaona ndio yanayotajwa kila mara. Sasa tumwombe Waziri kwa sababu ni bajeti yake ya kwanza ajitahidi sana huu upendeleo usiwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumizie suala la barabara, barabara ni uchumi na ndio kila kitu. Niombe nizungumzie barabara ambazo ni za kiuchumi; niongelee barabara ya Murushaka kwenda mpaka Murongo, hii ni barabara muhimu sana kiuchumi. Kwenye Nchi ya Tanzania hakuna wilaya ambayo inalima kahawa nyingi kama Wilaya ya Kyerwa, lakini ukija kuangalia hizi barabara ndizo barabara ambazo zimeachwa kwa muda mrefu na imekuwa ni ahadi ya muda mrefu lakini hazitengenezwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine nimekuwa nikishangaa, wanasema Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa maskini. Lakini jambo ambalo linasikitisha ni kwamba hii mikoa ambayo imenyimwa miundombinu lazima itaendelea kuwa mikoa maskini lakini kwa upande mwingine ninajiuliza, Serikali hili hailioni?

Mheshimiwa Naibu Spika, hii mikoa ambayo ina uzalishaji mkubwa wa kahawa, hii mikoa ambayo ndiyo ina uzalishaji mkubwa wa ndizi, hata ukienda Ulaya watakwambia ndizi ya Bukoba. Lakini nenda uangalie barabara zake zilivyo! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo niombe, nimeona umeweka pesa kidogo, nimesema hiki ni kama kishika uchumba, hii pesa bilioni tatu ambazo umeweka, Biblia inasema kila mtu aseme kweli na Jirani yake, na ndiyo yenu iwe ndiyo na hapana iwe hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu kwako Mheshimiwa Waziri; hii bilioni tatu uliyoitenga barabara hii unanihakikishia utaanza kuijenga! Na ni ahadi ambayo Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, aliahidi na akatoa maelekezo kwamba ijengwe kilometa 50 kwa kuanzia. Sasa nimeona mmeweka bilioni tatu, kwa kweli niseme hili jambo sijaridhika nalo lakini wewe nikuombe wakati unajumuisha hapa utuambie hii barabara unaijenga lini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mgakorongo kwenda mpaka Mrongo. Hii ni barabara ambayo ni muhimu, inaunganisha Nchi jirani ya Uganda. Ukiangalia upande wa wenzetu ni jambo ambalo linasikitisha, kule kwa wenzetu ni kama Ulaya lakini huku kwetu ni kama uchochoroni. Sasa hizi barabara ambazo zinaunganisha nchi na nchi lazima tuzipe kipaumbele. Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo nikuombe sana barabara hizi ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, ni jambo ambalo linasikitisha unapita kwenye barabara unaona bado ni nzuri lakini wanakwambia tunaondoa hii lami kwa sababu muda wake wa kuishi umekwisha. Kule kwetu tunatamani hata hiyo mliyoiondoa mngetupa sisi, lakini hatuipati. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri hili uliangalie sana na huu upendeleo uondoke kabisa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshalia Mheshimiwa.

MHE. INNOCENT S. BILAKATWE: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilisemee…

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ni Mwanakamati wa Miundombinu…

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara imeleta bajeti ambayo ina mambo mengi mazuri, lakini mimi niseme kama hatuna soko la uhakika, tunapoteza muda na hapa tunafanya ngonjera tu. Huu umekuwa ni wimbo wa kila siku na wewe Spika ni shahidi tumekuwa tukiambiwa tunaleta mbolea, mbegu bora, miche, lakini soko la haya mazao liko wapi? Kwa hiyo, hii ni changamoto kubwa na Wizara lazima ijipange kuhakikisha tunapata masoko. Mkulima amekuwa analima kilimo cha kubahatisha tu, anasema mwaka huu nimelima, lakini sina uhakika wapi nitauza mazao yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni muumini wa ushirika na hii iko kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi, lakini niseme kama ushirika hawatakuja na mbinu ambayo itaweza kumnufaisha mkulima, mimi sitaiunga mkono. Tunataka ushirika ambapo mkulima anapopeleka mazao yake aweze kupata pesa yake. Tunataka ushirika ambapo mkulima aweze kutatuliwa matatizo yake sio mkulima anaenda kukopwa. Kwa hiyo, lazima Wizara muwe wabunifu, ukitaka kuleta jambo jema na zuri, lazima uweke vitu ambavyo vitawavutia wale unaowaletea.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi ni kipindi cha msimu wa kahawa. Asubuhi nimepiga simu kuuliza bei ya Uganda kahawa ni shilingi ngapi? Kahawa Uganda sasa hivi ni shilingi 3,500 ya Uganda ambayo kwa kwetu ni shilingi 2,300, lakini kwetu kahawa hiyohiyo ya arabika wanakwambia ni shilingi 1,500. Ukija kwenye kahawa ya robusta ambayo Uganda ni shilingi 2,500 kwetu ukipiga hesabu hela ya Tanzania ni shilingi 1,500 kwetu ni shilingi 1,100.

Mheshimiwa Spika, kitu ambacho mimi ninakishangaa huyu mkulima wakati anaanza kulima, anaanza kuandaa hii kahawa Serikali huioni popote, lakini kipindi cha msimu unapoanza utashangaa askari wanapelekwa mpakani. Sasa ninataka nikuulize Mheshimiwa Waziri, wewe unasema Uganda hawana bei nzuri, askari wale mnapeleka wa nini mpakani kahawa isiende Uganda? Wewe unasema majirani zetu hawana bei nzuri, sawa ninakubaliana na wewe; kwa nini msimu unapofika ndio mnapeleka maaskari, maana yake kule kuna bei nzuri ndio maana mkulima anakimbilia kule. Kipindi cha msimu kikifika ni kama vita, hili jambo halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe sana haya mambo ya kuanza kukamata wananchi wanapoanza kuvuna kahawa, ooh, kahawa sijui haijaiva, sisi kule kwetu mtu ana mashamba zaidi ya matatu, analima kwenye kata hii na kwenye kata nyingine, sasa wakikuta unahamisha kahawa yako kuitoa kwenye kata nyingine ambako una shamba unaipeleka kuianika kwako wanasema kahawa unaipeleka Uganda, hili jambo halikubaliki. Kwa hiyo, niombe sana Serikali ijipange kuleta bei nzuri ya kahawa. Tuwe na masoko ya uhakika vinginevyo tunapoteza muda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kiwanda cha TANICA, hiki kiwanda kiboresheni. Mtakapoboresha hiki kiwanda nina uhakika kitaweza kuongeza bei ya kahawa. Kiwanda kinaendelea kubaki vilevile, lakini ninyi kazi yenu ni kutegeshea msimu umefika mnatafuta pesa yenu ya Serikali, hili jambo sio sawa. Kwa hiyo, niombe sana Serikali iboreshe kwanda cha TANICA ili hiki kiwanda kiweze kuongeza bei nzuri kwa mkulima, vinginevyo niombe sana Serikali kama hamjajipanga waacheni wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi kitu ambacho siungi mkono ni suala la butura. Hilo mnapambana nalo kwa nguvu zote kwa sababu linamnyonya mkulima, lakini wapeni uhuru wananchi kuuza kahawa wanavyotaka…

T A A R I F A

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa, Mheshimiwa.

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nalazimika kumpa Taarifa mzungumzaji, mtumishi wa bwana, butura inaingia kwa sababu ya ku-fail kwa mfumo wa ushirika. Butura kwa kwetu ni continuous cash flow, mkulima anahitaji continuous cash flow, anahitaji chenji. Kwa hiyo, akikosa chenji atachukua alichonacho kusudi apate pesa ya kutimiza majukumu yake, anaweza kuuza hata kitanda. Sasa yeye hauzi kitanda anauza kahawa aliyonayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali ilete cash flow, ilete chenji, Wahaya walikuwa wanaita nyantakorakorwa, BCU ilikuwa ina kitu kinaitwa chenji, nyantakorakorwa ndio iliondoa butura. Bila nyantakorakorwa butura itaendelea kuwepo. (Makofi)

SPIKA: Taarifa hiyo inayohusu nyantakorakorwa? (Kicheko)

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, mimi ninachosema napokea hii Taarifa, lakini naishauri Serikali lazima ije na mpango wa kumsaidia huyu mkulima kabla hajauza kahawa yake aweze kupata pesa ya kumsaidia kuendeleza zao hili.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo mimi nasita kusema naunga mkono hoja kwa sababu bado wakulima wangu wanateseka. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kunipa nafasi ya kuchangia lakini pia, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye ananipa afya na nguvu kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na wasaidizi wake, lakini kipekee nimtaje Mkurugenzi wa REA, huyu mtu amekuwa ni mtu wa pekee, ukimtafuta wakati wowote anapatikana na ni mtu ambaye kwa kweli ni msikivu, nimpongeze sana na aendelee hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umeme ni ajira, umeme ni viwanda, umeme ni uchumi, umeme ni maendeleo. Niongelee umeme kwa upande wa Mkoa wa Kagera, kwa kweli pamoja na juhudi za Serikali, Mkoa wa Kagera tumekuwa tukipata taabu sana tuna umeme ambao hauna uhakika. Kwa siku moja unaweza ukakatika zaidi hata ya mara 20, lakini pia umeme huu umekuwa ni umeme ambao nguvu yake ni kidogo. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali Mheshimiwa Waziri unafanya kazi nzuri mpambane iwezekanavyo, ili Mkoa wa Kagera uweze kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa. Kwa sababu, umeme tunaoutumia sasa hivi, ni umeme ambao unatoka katika nchi Jirani na hatuna uhakika nao kwa sababu, sio wa kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri hili upambane nalo, ili Mkoa wa Kagera na sisi tuwe na umeme wa uhakika na ninaamini, hiki kinaweza kikawa kinachangia kwa Mkoa wa Kagera kuwa miongoni mwa mikoa ambayo ni masikini. Na ukija kuangalia mikoa yote kama Kigoma, Kagera na mikoa mingine ambayo iko kwenye orodha ya mikoa masikini, ni mikoa ambayo haina umeme wa uhakika. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri hili ulifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikija kwa upande wa Kyerwa Mheshimiwa Waziri, nikushukuru tumekaa mara nyingi, ninakuomba sana kwa ajili ya vijiji vyangu ambavyo havijafikiwa. Nina vijiji 99, vijiji 29 bado havijapatiwa umeme. Lakini tumekaa tumezungumza muda mrefu umenipatia vijiji 19 bado vijiji 10 havijapatiwa umeme na nikuombe sana kwenye kata hizi ambazo zilikuwa hazijapatiwa umeme, yaani umeme haujawahi kugusa kabisa. Kwa mfano, ukienda kwenye Kata ya Bugala kuna Kijiji cha Bugala, Mugaba kwenye Kata ya Businde kuna Businde, Nyakashenyi, kwenye Kata ya Kibale kuna Kibale, Kijumbura, Kigorogoro, kwenye Kata ya Rukuraijo kuna Kijiji cha Mkombozi pamoja na Mgorogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia, Kata ya Bugomora kuna Kijiji cha Nyakatera, vijiji hivi havijawekwa kwenye orodha ya kupatiwa umeme. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri hili ulipe kipaumbele, hawa watu wanahitaji umeme muda mrefu na nilitegemea mkandarasi anapoenda anapeleka umeme maeneo yote. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri vijiji hivi ambavyo nimevitaja, viweze kupatiwa umeme, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri. Lakini jambo lingine mimi nina vitongoji 670, vitongoji 503 bado havijapata umeme, kwa hiyo, unaposema mmepeleka umeme kwenye vijiji bado vitongoji vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa Kyerwa naweza nikasema umeme haujafika hata asilimia 30 kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hili uliangalie. Mnasema mmepeleka umeme kwenye vijiji vingi, lakini vitongoji vingi havijafikiwa. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri hivi vitongoji 503 kati ya vitongoji 607, niombe sana vipelekewe umeme. Na umeme wa kwanza ulipokuja ile REA ya kwanza walipitisha nguzo juu, lakini vitongoji vyote ambavyo viko chini pale havikuweza kupatiwa umeme.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine Mheshimiwa Waziri, ulitoa maelekezo ukasema TANESCO wapeleke umeme kwenye taasisi za dini, kwenye mashule, kwenye vituo vya afya, maeneo mengi hayajafikiwa kwa upande wa Kyerwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri hili na lenyewe uliangalie. Jambo lingine ni suala la wananchi kuuziwa nguzo. Hili bado lipo Mheshimiwa Waziri na ikiwezekana niombe utoe maelekezo kwa maandishi, kila Mbunge awe na hii barua tuipeleke kwa wananchi. Kwa sababu, wanapopima wanakuambia mwananchi uko nje ya ramani ambayo tumepewa. Kwa hiyo, wewe unatakiwa ulipie nguzo tatu au nne. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri hili uliangalie.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, pale Kyerwa kwenye Kata ya Mulongo mpakani na Uganda, kuna mradi wa Kikagati, ule mradi Mheshimiwa Waziri sisi kama wana Kyerwa au wana Kagera, hatuelewi nini kinaendelea! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu, unaona upande wa pili ndio wanashughulika, lakini sisi hata ukienda pale kupata taarifa, haupewi taarifa inayohusiana na ule mradi. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri tujue sisi kama Kagera kwasababu, ule mradi ni wa Uganda pamoja na Tanzania. Tujue sisi kama Kagera tunapata nini? Lakini mradi huu unakamilika lini Mheshimiwa Waziri?

Mheshimiwa Spika, ninaamini mradi huu utakapokamilika ndio unaweza kuwa mkombozi, wakati Mkoa wa Kagera bado hatujaunganishwa kwenye gridi ya Taifa. Mradi huu unaweza ukasaidia angalau kutupunguzia yale makali tunayoyapata kwenye kukatika umeme kila mara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nimpongeze Waziri na nisemee mradi wa Julius Mwalimu Nyerere. Mradi huu ni mradi ambao kwa kweli Mheshimiwa Waziri, Serikali yetu itapata heshima kubwa, lakini pia wewe mwenyewe Mheshimiwa Waziri, ninaamini mradi huu umeuanzisha wewe na mradi huu utakupa heshima kubwa na jina lako litakumbukwa milele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninakushukuru ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa afya na nguvu. Jambo la pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kwa bajeti hii ambayo ni nzuri kwa kweli, inatia moyo. Kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu, kwa kasi aliyoanza nayo kwanza ya kuibua miradi mipya, lakini pia kuendeleza miradi ile ambayo iliachwa na mtangulizi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa ambalo linaelekea kujitegemea, lazima tuhakikishe tunawekeza kwenye mapato ya ndani, hasa hasa upande wa kukusanya kodi. Ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, mapato ambayo yanakusanywa kutokana na kodi ni asilimia 4.5 ambayo inatoka kwa watu milioni 2.7. Kwa kweli bado tunayo kazi kubwa ya kuhamasisha Watanzania kulipa kodi. Hili jambo Waheshimiwa Wabunge, tusiiachie Serikali, tunahitaji kuwa mstari wa mbele. Tunakuja hapa tunahitaji maendeleo, tunahitaji barabara, tunahitaji maji na huduma mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya yote hayo, lakini tusipohamasisha Watanzania kukusanya kodi, siku moja mara mbili hivi, nimeenda kule Kariakoo. Ukinunua vitu vya milioni mbili, unashangaa wanakwambia tuandike shilingi 300,000, sasa ni wangapi ambao wanafanya hivi? Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania, lazima tuwe mstari wa mbele kuhakikisha tunawahamasisha Watanzania kukusanya kodi, ndio tutaweza kufika kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Serikali imekuwa ikiweka nguvu sana kwenye viwanda. Hapa niishauri Serikali, viwanda hivi viendane na kilimo, ili viwanda vyetu viweze kupata malighafi ambazo zinatoka ndani. Kwa sababu, tutakapopata malighafi zinazotoka ndani nina uhakika uzalishaji utapungua. Kwa hiyo, hili lazima Serikali iliangalie, tuwekeze sana kwenye kilimo. Tumekuwa tukiimba, Mungu ametujalia Taifa lina ardhi nzuri, tuna vipindi virefu vya mvua, hebu tutumie fursa hii au nafasi hii, ambayo Mungu ametujaalia kuweza kuwekeza kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo hiki ili kiwe na faida, lazima tuhakikishe tuna soko la uhakika, wataalam watoke waende kutafuta masoko. Tusiishie kukaa ndani, tukaishia kukaa maofisini bila kutafuta masoko na ili tutakapotafuta masoko, nina uhakika uzalishaji utaongezeka, kwa sababu, mkulima atakuwa na uhakika ni wapi anaenda kuuza mazao yake. Kwa hiyo, hili nalo tulipe kipaumbele tuliangalie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilisemee, niipongeze Serikali kwa upande wa vijana wetu hawa wa bodaboda. Hii ni ajira, niiombe sana Serikali pamoja na kupunguza hii kodi, bado niiombe Serikali upande wa Polisi tusijikite kutoza faini. Tutoe elimu kwa vijana hawa na hili naamini litawasaidia kwa sababu, hii ni ofisi kama zilivyo ofisi nyingine. Vijana hawa wanafanya kazi kwenye mazingira magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilisemee, niipongeze Serikali kwa upande Madiwani. Tumefanya kazi nzuri, lakini Madiwani hawa wamechaguliwa kama sisi. Pamoja na malipo yao kulipwa na Serikali kuu, lakini niiombe sana Serikali, iangalie namna gani ya kuboresha posho ya hawa Madiwani ili iweze kuendana na kazi wanazozifanya. Waheshimiwa Wabunge leo hii sisi tupo hapa, lakini wanaofanya kazi kubwa ni Waheshimiwa Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni kwamba, tunao hawa watu wetu Wenyeviti wa Vijiji. Kwa kweli niseme Serikali hili jambo lazima iliangalie, inaitwa Serikali ya Vijiji, ni Serikali gani ambayo Mwenyekiti wa Kijiji halipwi, hakuna chochote anachokipata. Kwa hiyo, niombe, tumeboresha kwa Watendaji, tumeboresha kwa Madiwani, hebu twende kuangalia, Wenyeviti wetu wanafanya kazi kwenye mazingira magumu. Mwenyekiti yuko ofisini lakini hakuna anachopata. Mwisho wa siku ndio maana hawa Wenyeviti wa Vijiji wanaanza kuwaibia wananchi. Kwa sababu, hana kipato mwananchi akija kupata huduma, anachomwambia lazima uache Sh.20,000/=. Kwa hiyo, niombe sana Serikali hili iliangalie na lenyewe ilipe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niipongeze Serikali, leo hii tumepata chanzo cha mapato kwenye barabara zetu. Niombe na niishauri Serikali, tunataka tuone hizi fedha zinaenda kufanya kazi kwa wananchi. Nina uhakika wananchi wetu hawana shida kwa sababu, hizi fedha zitakapokatwa kwenye simu, zinaenda kutoa huduma kwa wananchi wetu. Zinaenda kujenga barabara, zinaenda kuboresha miradi ya maji na afya na tunaenda kupata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamefanya kazi kubwa, kama wameweza kujenga maboma ya mamilioni, leo hii ukiwaambia Watanzania wachangie miradi ya maji, wachangie umeme, wachangie barabara, sidhani kama lina shida. Kinachotakiwa, hizi fedha lazima ziwekwe kwenye Mfuko Maalum, ziende kufanya kazi iliyokusudia, watu waone huduma za maji, watu waone umeme, watu waone barabara. Kwa hiyo, niombe sana Serikali hili nalo iliangalie sio mnaweka tu, maana kuna fedha nyingine inaweza ikakusanywa, lakini mwisho wa siku ikatumika tofauti na ilivyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie jambo lingine la Corona, niipongeze Serikali kwa juhudi ambazo zimekuwa zikifanyika. Hata hivyo, niwaambie ndugu zangu, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania, Taifa hili ni Taifa la Mungu na ninyi mtakuwa mashahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majirani zetu wanaotuzunguka sio kusema hawachukui hatua kama sisi, lakini Mungu analo kusudi na Taifa la Tanzania. Kama italazimika kutumia barakoa, tutazitumia, kama italazimika kupata chanjo tutazipata, lakini nataka niwaambie Watanzania, kama tusipoendelea kumpa nafasi Mungu, ambaye amelilinda Taifa hili, wenzetu wanakufa, lakini Taifa hili lipo salama. Hatua zote tuchukue, lakini lazima tutambue, Mungu ndiye namba moja. Tusipompa Mungu nafasi namba moja, tutachoma hizo chanjo, tutavaa barakoa hizo na tutakufa. Taifa hili liko salama kwa sababu, Mungu analo kusudi na Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuchangia. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na nguvu ya kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. Pia nichukue nafasi hii kipekee kuishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri zinazofanywa chini ya mama yetu Samia Suluhu, hasa hasa kuleta pesa nyingi ya maendeleo kwa wananchi wetu. Ni ukweli usiopingika pesa inakuja na miradi inaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa nataka nizungumzie kwanza upandaji wa bidhaa. Ni vizuri tukaeleza hapa ukweli. Nilikuwa najaribu kufuatilia taarifa za EWURA; ukifuatilia taarifa za EWURA mara nyingi Waheshimiwa Mawaziri na wengine wamekuwa wakisema bidhaa zimepanda kwa sababu ya mafuta. Hebu tuangalie taarifa za EWURA zinasemaje kuanzia mwezi wa 12 mpaka sasa.

Mwezi wa 12 mwaka jana bei ya mafuta kwa Dar es Salaam ilikuwa ni shilingi 2510 na kwa Kigoma kule Uvinza ilikuwa ni shilingi 2754 mwezi wa pili mwaka huu bei ya mafuta ilishuka ikawa shilingi 2480 kwa Dar es Salaam na kule Uvinza Kigoma ikawa 2720, maana yake ilishuka kwa shilingi 30. Tukaja mpaka mwezi wa tatu bei ya mafuta ilikuwa ni shilingi 2500 kwa Dar es Salaam mpaka 2784 kwa Uvinza kule Kigoma.

Sasa Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wanaotusikiliza lazima tueleze ukweli. Bidhaa zilizopanda mimi niseme ukweli hazitokani na upandaji wa mafuta. Kwa sababu ukija kuangalia hapa hizi takwimu za EWURA haiwezekani hii shilingi 60 ambayo imepanda kwenye soko la mafuta ndiyo iongeze bei kiasi hiki. Mimi nitoe mfano, kule kwangu kuna sabuni mbili tunazozitumia, kule Kyerwa. Sabuni ya nyota mwezi Januari ilikuwa inauzwa shilingi 1,000 lakini mpaka sasa ile sabuni inauzwa shilingi 3,500. Sabuni ya mkwano ilikuwa inauzwa shilingi 2,000 leo hii hiyo sabuni inauzwa shilingi 5,000. Hivi hii shilingi 60 iliyoongezeka kwenye soko la mafuta ndiyo imepandisha bidhaa kiasi hiki?

Mheshimiwa Spika, lakini ukija kwenye mafuta ya kula ni jambo ambalo ni la ajabu. Mafuta yaliyokuwa yanauzwa shilingi 1,700 leo hii haya mafuta ni shilingi 3,500. Yaani hii haikubaliki. Ukienda kwenye vifaa hivi vya ujenzi, mimi mwaka jana mwezi wa 12 niliagiza pale kwenye vifaa vya ujenzi vya aluminum; pale nilivyoagiza wakanipa quotation ya shilingi milioni 18. Nimekwenda juzi wananiambia hivyo vifaa bei imebadilika ni milioni 35. Waheshimiwa Wabunge na Watanzania lazima tuwaeleze ukweli. Suala la kusema mafuta yamepanda tuongee tarehe sita juzi, siyo miezi hii miwili mitatu iliyopita, hili haliko sawa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi ninachokiona kwenye suala la upandaji wa mafuta tunaongelea kipindi hiki cha juzi, lakini miezi mitatu kule nyuma mafuta yalikuwa hayajapanda kiasi hiki cha kuweza kupandisha bidhaa zikapanda namna hii hili haliko sawa. Mimi nilichokiona baada ya kufuatilia hawa wanaouza wameachiwa uhuru wameamua kujitawala kufanya wanavyotaka.

Mimi niombe tumsaidie Mheshimiwa Rais, tusiende na hoja ya kusema bidhaa zimepanda kwa sababu ya mafuta. Leo hii tukianza kutangaza sawa kwa sababu mafuta yameongezeka takriban kwa 500 zaidi. Kwa hiyo mimi ninapinga suala la kusema bidhaa zimepanda kwa sababu ya mafuta kupanda.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilisemee ni kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa maamuzi ambayo ameyafanya kule Kagera kwenye suala la kahawa. Kwa uchumi wa mkoa wa Kagera tunategemea sana kahawa, na hawa wakulima wamesahaulika kwa muda mrefu. Kwa hiyo mimi nipongeze Serikali kwa hatua ambayo umechukua na kuruhusu kahawa kuuzwa kwenye AMCOS.

Mheshimiwa Spika, kahawa ilikuwa inauzwa kwenye Vyama Vikuu, wanakusanya na ndio wanauza, lakini Vyama Vikuu kimekuwa ni kichaka cha kuwanyonya wakulima na kuwaibia. Sasa niombe sana Waheshimiwa Wabunge wale ambao wanatoka kwenye mikoa inayolima kahawa tuunge mkono utaratibu huu. Mimi mwaka jana niliiomba Serikali, nikaomba huu utaratibu utumike angalau waangalie unaendaje. Mwaka jana tumeujaribu, utaratibu huu ni mzuri wa kuuza kahawa kwenye vyama vya msingi; kwa hiyo ninapongeza sana Serikali kwa hatua hii ambayo imefikia.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine, ili nchi hii iweze kuwa, pamoja na vipaumbele vingine, tunaona Serikali imeanza kuwekeza kwenye kilimo ambacho kimesahaulika kwa muda mrefu. Niiombe sana Serikali wampe nguvu Mheshimiwa Bashe, kazi anayoifanya ni nzuri. Serikali iongeze pesa tuingie kwenye kilimo ambacho kina tija kilimo ambacho kitakuwa na faida kwa nchi lakini pia kwa mkulima. Leo hii ukienda kwenye viwanda vyetu tunaagiza bidhaa na malighafi nje kwaajili ya kuleta kwenye viwanda vyetu.

Mheshimiwa Spika, fedha za kigeni zinaenda nje, kitu ambacho hakijakaa sawa. Hii nchi Mungu ameijalia, tuna vipindi virefu vya mvua, tuna udongo mzuri, ukiingia kule kwetu Kyerwa ni raha tupu. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, tuwekeze kwenye Kilimo ambacho mkulima akihitaji mbolea anaipata kwa wakati, mkulima akihitaji mbegu bora, azipate kwa wakati. Ninaamini nchi hii tunaweza tukatumia kilimo na kikaongeza fedha nyingi kwenye uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la kusemea ni hawa watumishi wanaojitolea. Juzi Serikali imetangaza kuajiri. Kuna watumishi wamekuwa wakijitolea muda mrefu. Hawa watumishi inapofika wakati Serikali inapotaka kuajiri, hao wanaojitolea huwa wanaachwa. Sasa naiomba sana Serikali, hao watumishi ambao wamejitolea muda mrefu, Serikali iwape kipaumbele ndio waanze kupewa nafasi. Kwa hiyo, hili naomba Serikali iliangalie, kwa sababu hili jambo ni muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo linguine, MSD wameshindwa, lazima tueleze ukweli. Sijui pale kuna mdudu gani? Kipindi cha nyuma alikuwepo yule kijana anaitwa Laurian, alikuwa anafanya vizuri, tunapata dawa kwa wakati. Wakaingiza fitina, sijui nini na nini, hata kesi yenyewe aliyofunguliwa hatuioni, lakini madudu tunayoyaona ndiyo haya. Hakuna dawa, hali ni mbaya huko vijijini. Kwa hiyo, naomba sana Waziri anayehusika, huyu bwana waliyemweka pale, kama ameshindwa, wamweke pembeni watafute mtu ambaye anaweza akawapatia wananchi dawa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya mambo ya kulea watu, huko vijijini hali ni mbaya. Hili haliwezekani, ni lazima tuelezane ukweli. Mtu kama ameshindwa kazi, akae pembeni, wanaoweza kazi waendelee.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru, ahsanteni sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango wa Serikali 2022/23. Kwanza nipongeze kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais, kwa kweli ameonesha uwezo mkubwa kama Kiongozi wa Nchi, kila mmoja ni shahidi. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na timu yake kwa Mpango mzuri ambao wametuletea na leo tunaujadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia ninalo swali kwa Mheshimiwa Waziri ambalo anaweza akatujibu wakati anahitimisha Mpango huu. Tumekuwa tukipitisha mipango, tumekuwa na Mpango Mkubwa wa Miaka Mitano, lakini leo hii tuna mpango wa mwaka mmoja ambao ni Mpango wa Tatu; swali langu kwa Mheshimiwa Waziri, ni vizuri tukajiuliza mipango ambayo tumeipitisha hii miaka mitatu tumefanikiwa au bado hatujafanikiwa? Na kama hatujafanikiwa ni kitu gani ambacho tunatakiwa tukifanye ili Mpango huu tunaoujadili leo usije ukashindwa kama mipango mingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukipitisha mipango na tumekuwa na Mpango mkubwa wa miaka Mitano lakini leo hii tunao mpango wa mwaka Mmoja ambao ni mpango wa Tatu, swali langu kwa Mheshimiwa Waziri ni vizuri tukajiuliza mipango ambayo tumeipitisha hii miaka Mitatu tumefanikiwa au hatujafanikiwa? kama hatujafanikiwa ni kitu gani tunachotakiwa tukifanye ili mpango huu leo tunaoujadili usije ukashindwa kama mipango mingine? Ninaamini hili ninalosema kila Mbunge analo jibu, kwa kweli kwa sehemu kubwa bado hatujafanikiwa kile ambacho tumekipitisha kwenye mpango uliopita. Kwa hiyo, Mheshimwa Waziri hilo ni suala ambalo naomba utujibu kama Wabunge kwa sababu tusiwe tunapitisha mipango mizuri, Wabunge wanatoa ushauri mzuri lakini mwisho wa siku majibu yanayotoka ni asilimia Thelathini, Hamsini hatufiki hata asilimia Sabini Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nipongeze sana Serikali, tumesoma kwenye mpango kwa habari ya SGR, SGR ni mradi mzuri sana kwa Taifa kwa sababu umeeleza unavyoenda kuunganisha nchi ya DRC na huko ndiko kwenye biashara kubwa. Ushauri wangu ni kwamba, ili SGR iwe na faida kubwa ni lazima tuwe na mzigo wa kutosha, hatuwezi tukajenga SGR lwa mabilioni halafu hatuna mzigo ambao tutaweza kuupitisha na kurudisha fedha hii ambayo tumekopa. Ili tuweze kuwa na mzigo wa kutosha wakati tunaendelea na mpango wa kujenga kufika kwenye hizo nchi ni lazima tuje na mkakati wa kuboresha bandari yetu. Bandari yetu ya Dar Es Salaam ndiyo tunayoitegemea kwa sehemu kubwa ili tupate mzigo ambao tutapitisha kupeleka nchi jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kwa upande wa bandari, pamoja na uboreshaji unaoendelea bandari ya Dar es Salaam imezidiwa. Bandari ya Dar es Salaam hatuna eneo lingine ambalo tunaweza tukapanua na kuwa na Bandari kubwa, lazima tuje na mpango kabambe wa kuhakikisha tunajenga Bandari ya Bagamoyo. Bagamoyo ndiyo Bandari muhimu itakayoenda kuinua uchumi wa nchi hii. Mimi naamini tukiwa serious tukakubali kukaa kwenye meza tukapanga mipango mizuri na tukaisimamia Bandari ya Bagamoyo itainua Taifa hili. Kwa hiyo niombe sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kujenga Bandari ya Bagamoyo lazima tuongeze ufanisi, ni lazima wakati tunaboresha Bandari yetu ya Dar es Salaam tuangalie hawa washindani wetu ambao kwetu Mungu ametujalia, tunayo mazingira mazuri, tumezungukwa na nchi nyingi majirani, ni kitu gani kinachosababisha wengine wakimbilie Mombasa wengine wakimbilie kwenye nchi nyingine ambako ni mzunguko mkubwa kupeleka mizigo kwenye nchi zao? Hivyo ni lazima tuingie kwenye ushindani na biashara ni ushindani, lazima unapofanya biashara uangalie mwenzako ameboresha wapi ili na wewe uweze kufanya vizuri zaidi. Kwa hiyo, niombe sana hilo tuliangalie kwa ajili ya kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ili SGR isije ikawa ni mzigo umekaa tu, kwa sababu kama SGR tunategemea kupeleka abiria tu hakuna chochote ambacho tutafanikiwa, Kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri hili mliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niongelee kilimo, kilimo ni biashara, kilimo ni maisha na kilimo ni uchumi. Mungu ameijalia nchi hii mpaka wakati mwingine huwa najiuliza hivi kweli tunaona hii fursa ambayo Mungu ametupatia na tunaitumia ilivyo? Ukiangalia nchi hii imejaliwa vipindi virefu vya mvua, pamoja na mvua bado tunayo maji ya kutosha kwenye maziwa na kwenye mito, hizi fursa na hii neema ambayo Mungu ametupa tunaitumiaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumetokea COVID, imetokea vita ya Urusi na Ukraine kule hii fursa tumeitumiaje? Tungekuja na mpango kabambe wa kilimo cha umwagiliaji, tukatenga Kanda. Nimpongeze Mheshimiwa Bashe kule kwetu ameanza na mazao haya ya kimkakati kuanza kuzalisha miche, lakini lazima tutenge kikanda, tuseme Kanda hii itazalisha mpunga, Kanda hii ni korosho na Kanda hii ni mahindi halafu haya mazao tunayoyapata ndiyo tuende kuyauza kwa majirani zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, Kyerwa peke yake tunailisha Uganda ndizi, yaani ni foleni ndizi iliyokuwa inauzwa shilingi 3,000 leo ni 20,000! Sasa hizi fursa lazima tuziangalie na tuzifanyie kazi, siyo kila siku kinakuja hiki kinaisha, kinakuja hiki hakiishi tunakatia katikati tunakwenda. Kwa hiyo, niombe sana tutumie fursa hii ili tuweze kuboresha kilimo chetu kiwe na tija lakini ili tuwe na kilimo ambacho ni kizuri lazima wakulima hawa tuwaboreshee mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeeleza kwenye mpango kuhusu kuboresha barabara zetu za TARURA, ni kweli barabara zimeanza kuboreshwa lakini bado lazima tujue wakulima wengi wako vijijini, unaongelea barabara 25,000 ambazo Serikali tayari imeshaziboresha. Sehemu kubwa barabara nyingi Waheshimiwa Wabunge ninyi ni mashahidi ni za udongo. Serikali iwekeze kwenye barabara za changarawe ili hawa wananchi ambao ni wazalishaji wakubwa waweze kupeleka mazao yao sokoni na mazao yao yanapokwenda sokoni Serikali inaongeza kipato. Kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali kwenye mpango huu ili tuboreshe kilimo tunahitaji barabara nzuri, tunahitaji mazingira mazuri kwa wakulima wetu na ili tuboreshe kilimo kiwe kizuri na tuweze kupata kipato ni lazima tuwe na soko la uhakika. Kwa hiyo ninaomba sana Serikali iliangalie jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilisemee, tunalo janga la Kitaifa sijui wenzangu mnaliona, mabadiliko ya tabianchi lakini pia na uharibifu unaoendelea tunaoufanya sisi kwa kuharibu vyanzo vya maji, kukata miti na kuchoma mkaa, nchi hii inaenda kuwa jangwa. Serikali lazima ije na mpango kwa kila Halmashauri kuzalisha miti na kuigawa kwa wananchi ili tuende kuboresha yale mazingira ambayo yameharibika vinginevyo tunakoelekea hali ni mbaya. Ninakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa afya na nguvu kuendelea kuwatumikia wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kipekee kuishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri zinazofanyika chini ya mama yetu Samia yenye matumaini makubwa ya kumtua ndoo mama kichwani. Kwa kweli ninasema hivi nilikuwa najaribu kuangalia bajeti zilizopita kwa kweli inaweza ikawa ni bajeti ya kwanza ile bajeti tuliyopitisha mwaka jana ambayo imeweza kutekelezwa kwa asilimia kubwa asilimia 95 ukijaribu kuangalia pesa ambayo ilikuwa imetengwa bilioni 778 lakini pesa ambayo tayari imeshatolewa ni bilioni 743 kwa kweli ni hatua nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Maji kwa kazi kubwa mnayoifanya. Kwa kweli mnafanyakazi kubwa lakini kikubwa ambacho niwapongeze kwa namna ambavyo mnatupa sisi ushirikiano wa Bunge tunapowaletea mahitaji ya wananchi wetu. Kwa kweli kipekee ninasema mmekuwa mkinipa ushirikiano mkubwa na leo hii ninaposema ninapongeza kwa kweli napongeza kwa dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa najaribu kuangalia mara nyingi wanasema Wabunge wa CCM wanapongeza lakini sasa kazi zinapofanyika lazima tupongeze. Nilikuwa najaribu kuangalia bajeti ambayo tumepitisha mwaka jana kwa Kyerwa tuna mradi mmoja wa Kaisho, Isingiro kuna bilioni 1.3 tuna mradi wa Kimuri, Chakarisa Rwanyango bilioni 2.1, tuna mradi wa Nyamiega Nyakatera ambao una bilioni 1.3 mradi wa Runyinya Chanya bilioni 4.6 mradi wa Kaisho Isingiro bilioni 1.9, mradi wa Murongo milioni 738, mradi wa Karongo milioni 734. Mradi wa kuchimba visima milioni 630.

Mheshimiwa Waziri kwa kweli ninakushukuru na miradi hii ninayoitaja tayari wakandarasi wamesha saini mkataba na wako kazini wanaendelea. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri mimi nakushukuru sana kwa jinsi ambavyo unaendelea kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapochangia pamoja na miradi hii ambayo imeletwa kwa Kyerwa bado naendelea kuomba Mheshimiwa Waziri juzi tumekutana pamoja na wewe na Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Maji Vijijini tumejadili juu ya mradi wa Kyerwa ambao unaenda Nyaruzumbura unaenda Nyakatuntu mpaka Kamuli.

Mheshimiwa Spika, mradi huu ninausemea sana kwa sababu mradi huu mndiyo utakuja kuwa mkombozi kwa wananchi wa Kyerwa ambao utaenda kuhudumia zaidi ya wananchi karibu elfu arobaini. Lakini tunaposema mradi wa Kyerwa mpaka Kamuri mradi huu utakapokuwa umekamilika tukapeleka maji mpaka kwenye kata ya Kamuri tutaweza kusambaza maji kwenye maeneo ya kata ambazo hazijawahi kufikiwa kabisa tangu nchi hii imekuwepo Kata kama Kikukuru, Kata kama ya Businde, Kata kama ya Bugara kata nyingine zote pamoja na Kibale ambazo hazijawahi kufikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri kama tulivyokubaliana mradi huu ninaomba sana uanze kwa sababu ulipitishwa kwenye bajeti iliyopita na ninaamini kwenye bajeti hii umo. Niwaombe sana mradi huu ni muhimu na ndiyo utaenda kuondoa kero ambayo ipo kwa wananchi wa Kyerwa.

Mheshimiwa Spika, mambo mengine Mheshimiwa Waziri ni pamoja na miradi mingine ambayo tumeleta hii miradi mingine ambayo imepitishwa kwa mfano mradi wa Isingiro Kaisho mradi huu utajengwa kwa awamu. Kwa hiyo, niombe awamu hii inapoisha Mheshimiwa Waziri tupate pesa ili tuweze kukamilisha mradi huu kwa sababu mradi huu ulikuwa wa muda mrefu na ulikuwa ni kero sana kwa wananchi wa Jimbo la Kyerwa.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine niombe sana Mheshimiwa Waziri miradi tayari tumeshasaini mikataba pamoja na wakandarasi niombe sana pesa ije kwa wakati ninaamini wale vijana mliowaweka kijana wangu Tungaraza pale Kyerwa anafanyakazi nzuri sana mleteeni pesa kwa upande wa usimamizi hana shida akishirikiana pamoja na Meneja wa Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine ambalo niliona nichangie nchi hii Mungu ameijaalia sana tuna vyanzo vingi sana vya maji yaani watanzania kukosa maji kwa kweli ni jambo ambalo ni la ajabu lakini tuna vyanzo vingi vya maji. Lakini pia Mungu ametujaalia vipindi virefu vya mvua ukipita pale Dodoma karibu na kwa Mheshimiwa Spika ambaye amestaafu unakuta maji yamevuta mpaka barabara huwa najiuliza Serikali kwa nini hailioni hili? tukavuna haya maji kwanza pale tukitenga yale maji yanaweza kutusaidia kwa mahitaji yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine yale maji inaweza ikawa ni kivutio hata na Dodoma na wao wakaonekana wana kama ziwa yale maji ni mengi sana lakini yanaishia kupotea kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri kwenye mipango yenu mje na mipango ya kuvuna haya maji tuwe na mabwawa makubwa wananchi wa Dodoma waachane na maji ya chumvi ukimaliza kuoga kama umesahau kujipaka mafuta utashangaa ni kama umejipaka poda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri hili na lenyewe uliangalie ili na watu wa Dodoma waweze kupata maji ambayo ni maji yanaitwa maji baridi maji safi ambayo hayana chumvi. Kwa hiyo, niombe sana na hili na lenyewe Serikali iliangalie.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilisemee Mheshimiwa Waziri ule mradi wetu mkubwa ambao tulikubaliana utajengwa kwa awamu huu mradi msije mkausahau mradi wa vijiji 57 tumeanza kuujenga kwa awamu lakini tuendelee kuufikiria ni namna gani tutaendelea kutenga kwenye bajeti ili wana Kyerwa ifike sehemu tuondokane na adha ya kutopata maji wakati mwingine ukifika sehemu nyingine ukiona maji wanayotumia kwa kweli hali ni mbaya.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nirudie tena Mheshimiwa Waziri ninakushukuru sana kwa kazi nzuri unayoifanya na wewe pamoja na Ofisi yako lakini pia ushirikiano ambao mmekuwa mkinipa ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia mpaka sasa kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyelwa. Kabla sijaanza kuchangia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu nataka nisome neno la Mungu katika Zaburi 33:12; “Heri Taifa ambalo Bwana Mungu wao watu waliochaguliwa kuwa urithi wake.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme neno hili Taifa la Tanzania ni Taifa Maalum. Inawezekana watu wasijue lakini Taifa hili Mungu ameliweka kwa ajili ya kusudi maalum. Ni lazima kama Watanzania tutambue kusudi hili ambalo Mungu ameliweka katika Taifa hili na tulilinde kwa nguvu zote na gharama zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Mataifa machache ambayo Mungu ameyachagua na ameyaweka kwa ajili ya kusudi maalum. Kwa hiyo ndugu zangu haya mambo ya haki za binadamu ya kuliondoa kusudi la Mungu katika Taifa letu niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, niwaombe sana Watanzania tupambane nalo kwa nguvu zote. Haiwezekani tukaileta laana katika Taifa hili ambalo Mungu ameliweka kusudi lake. Niombe sana viongozi wetu wa kitaifa hili jambo walichukulie serious na ikiwezekana pawepo na kipindi maalum cha kutubu ili kuondoa dhambi hii katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongea hayo sasa nichangie hotuba ya Waziri Mkuu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Watanzania wanajua kazi kubwa anayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais na aendelee hivyo hivyo, tunamtia moyo na naamini na Mungu atakuwa pamoja naye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea Watanzania fedha nyingi. Kila mahali Mheshimiwa Rais anakokwenda ameleta fedha na kwa kweli hakuna mahali ambapo hajagusa. Kwa hiyo, tunaendelea kumwombea Mheshimiwa Rais aendelee kuwatumikia Watanzania na naamini Watanzania wako pamoja naye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Vitambulisho vya NIDA. Ni haki ya Watanzania kupata vitambulisho vya NIDA kwa sababu ni muhimu, lakini jambo ambalo ni la kusikitisha, ni zaidi ya miaka 10 tangu waanze kutengeneza vitambulisho vya Taifa. Hata hivyo, katika maeneo mengi bado hatujaweza kuwafikia Watanzania wengi ili waweze kupata vitambulisho vya NIDA. Naamini vitambulisho hivi vya NIDA ni haki ya kila Mtanzania. Mtanzania ambaye hana kitambulisho hawezi kusajili simu yake, Mtanzania huyu hawezi hata kusajili biashara yoyote. Kwa hiyo, tunadumaza maendeleo ya Taifa. Hivyo, niiombe sana Serikali haya mambo ya kila siku wanakuja hapa na ngonjera za kutuambia sijui inaletwa mitambo gani, tuombe sasa waje na majibu yaliyo sahihi, Watanzania wapate vitambulisho ili tuondoe usumbufu uliopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile utaratibu wa kupata vitambulisho bado haujakaa vizuri. Kwa maeneo haya ambayo yapo pembezoni kama Mkoa wa Kagera na maeneo mengine, Watanzania wanapata shida sana. Haiwezekani umeenda kumtambua Mtanzania, wewe Afisa uhamiaji uliyetoka Dar es Salaam bila kushirikisha Viongozi wa Vijiji na Vitongoji, wewe unaanza kutambua unasema huyu ni mhamiaji haramu kwa sababu ana pua ndefu, kwa sababu ni mrefu. Niombe sana tushirikishe jamii inayozunguka maeneo hayo ili tuweze kuwatambua wale ambao hawastahili ili Watanzania wanaostahili waweze kupewa Vitambulisho vya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niongelee suala la umeme. Umeme ni maendeleo, umeme ni ajira, lakini pia umeme ni uchumi. Mheshimiwa Rais anapambana sana kuleta pesa kwa ajili ya kuwapa Watanzania umeme, lakini kasi ya kupeleka umeme ni ndogo. Mfano, upande wa Kyerwa, tuna vijiji 28 ambavyo bado havijapatiwa umeme, lakini vijiji hivi tayari Mkandarasi amekwishapewa. Niombe sana Serikali ifuatilie huyu Mkandarasi anayepeleka umeme Mkoa wa Kagera, kwa kweli speed yake ni ndogo. Haiwezekani ndani ya miaka miwili kwenye Wilaya ya Kyelwa ameshindwa hata vijiji vitatu, sasa hivi ni vijiji viwili tu. Kasi yake ni ndogo kwa kweli hairidhishi. Pesa ipo Serikali imetoa, lakini hawa wakandarasi wanaowapa wakati mwingine wawaangalie waone ni wakandarasi wa namna gani. Watanzania wanahitaji umeme kwa sababu ni muhimu sana. Kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu hili aliangalie kama Msimamizi Mkuu wa Shughuli za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niongelee kilimo. Serikali imeweka fedha nyingi kwenye kilimo na tunampongeza Mheshimiwa Waziri Bashe anafanya kazi nzuri. Tulishuhudia hapa wanagawa pikipiki za Maafisa Ugani, lakini niombe sana Mheshimiwa Waziri Bashe hili aliangalie Maafisa Ugani wake wanamwangusha. Hakuna kazi wanayoifanya. Hawa Maafisa Ugani kitu wanachokifanya kwa mfano Kyerwa, wanasubiri msimu wa kahawa, mkulima anaanza kuvuna kahawa ndipo wanakuja kukagua kama ile kahawa imekomaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzoni wakati anaanza kulima, anapalilia, anahudumia hili zao hatumwoni Afisa Ugani lakini ukifika wakati wa kuvuna wanakuja kwa kasi. Wakati mwingine wanakuja kutafuta fedha kwa wakulima, kuwaibia. Kwa hiyo, niombe sana, ni lazima tuweke nguvu kubwa ili mkulima aweze kupata zao ambalo ni zuri na lenye tija. Kwa hiyo, niombe hili Mheshimiwa Bashe aliangalie Maafisa Ugani wake kwa kweli wanamwangusha hawafanyi kazi, wamekaa tu na hizo pikipiki walizowapa sijui wanazifanyia nini? Kwa hiyo niombe sana hili waliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilisemee ni suala la barabara. Barabara ni muhimu sana. Hizi barabara za Wilaya ya Kyerwa zimezungumziwa muda mrefu. Barabara ya Omurushaka kwenda mpaka Murongo, tenda imetangazwa mwaka 2022, Mkandarasi amekwishapatikana, lakini mpaka leo zaidi ya miezi sita hatujaona Mkandarasi. Tunaomba Mkandarasi aje asaini Mkataba, barabara hii ianze kujengwa kwani ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile barabara ya Mugakorongo kwenda mpaka Murongo, hii ni barabra muhimu, ni barabara inayounganisha Nchi ya Uganda na Tanzania. Ni lazima tufanye biashara na hawa wenzetu. Ukienda kwa wenzetu unaangalia ni kama Ulaya, lakini ukija huku kwetu ni kama uchochoro. Niombe sana kwa sababu barabara hii imeshatangazwa, tenda imeshafunguliwa, Mkandarasi apatikane na barabara hii ianze ili Wanakyerwa na wao waweze kujiona kama ni sehemu ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu ambae amenijalia afya na nguvu za kuendelea kuwatumikia mabosi wangu wananchi wa Jimbo la Kyerwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kuona ile ndoto yake ya kuwatua wakinamama ndoo kichwani inatimia. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Aweso, Mdogo wangu pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu, kwa kazi kubwa mnayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa najaribu wakati mwingine unapopata nafasi watu hawa wanaofanya kazi vizuri unaenda mbele ya Mungu kuwaombea. Wakati ninaomba kwa ajili ya Mheshimiwa Aweso pamoja na timu yake nikawa najaribu kumuuliza Mungu, hawa watu yaani ukija kuwangalia nia yao, kusudio lao ni moja yaani wamejipanga vizuri. Ukienda kwa Mheshimiwa Aweso, ni mnyenyekevu mpole, ukienda kwa Naibu Waziri hivyo hivyo, ukienda kwa Katibu Mkuu, hivyo hivyo, ukienda kwa Ndugu yangu Bwire, hivyo hivyo lakini hatujaishia hapo hata hawa watumishi mliowaweka mikoani ndugu yangu Warioba anafanya kazi nzuri pamoja na Tungaraze wanafanya kazi vizuri sana ndio maana mnaona haya mafanikio makubwa tunayoyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati mwingine tunapokuwa tunasifia, tunasifia kwa sababu vitu vimefanyika. Ninataka nieleze kwa upande wa Kyerwa. Miradi inayoendelea upande wa Kyerwa baada ya kukaa na Mheshimiwa Aweso na Katibu Mkuu pamoja na wasaidizi wake nikawaomba sana na ninakumbuka maneno uliyoniambia Mheshimiwa Aweso, ukaniambia hutakuwa kikwazo kutupatia maji wananchi wa Jimbo la Kyerwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye kata ya Murongo, kuna mradi wa milioni 589 mradi huu umekamilika, ukienda kwenye Kata ya Mabira, tuna mradi wa bilioni 768 mradi huu tenda imetangazwa na wiki ijayo mkandarasi anakabidhiwa Mradi. Ukienda kwenye Mradi wa Kata ya Nkwenda, Iteera mpka Rwabwere, Mradi wa bilioni 4 na milioni 600, mradi huu unaendelea vizuri na uko kwenye asilimia 75. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye kata ya Kimuli, mradi wa bilioni 2 milioni 116 unaendelea vizuri. Ukienda kwenye Kata ya Kaisho, Isingiro na Rutunguru, mradi wa bilioni 1 na milioni 900 mradi unaendelea vizuri, tukienda kwenye Kata ya Rwabwere, mradi wa milioni 738 umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Aweso, ninakushukuru sana maana nilikusumbua sana lakini ukasema hautakuwa kikwazo ni hakika maneno yako nimeanza kuyaona. Mungu akubariki na ninasema kama mtumishi wa Mungu kama Mungu wangu aishivyo hatakuacha wala kukupungukia wewe pamoja na timu yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru, pamoja na kupongeza hawa watu namna walivyojipanga, ukiangalia hata wakandarasi wanaowaleta ni wakandarasi ambao wako makini. Mkandarasi mliyempa mradi kule Kyerwa anaitwa JAMTA, mkandarasi huyu ameanza kufanya kazi hata kabla hajaanza kulipwa. Ukiangalia miradi yote inayoendelea yuko karibu asilimia 80 lakini angalia alipolipwa ni kwenye kama asilimia 40 au asilimia 50. Wakandarasi wa namna hii tuwalinde na tuendelee kuwaunga mkono na kuwapa miradi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, tumekaa tena na wewe, Katibu Mkuu lakini pia Waziri wa Fedha. Tunao mradi ambao unakwenda kuhudumia Kata ya Kyerwa, Kata ya Nyaruzumbura, Kata ya Nyakatuntu, Kata ya Kitwe, Kata ya Bugara, Kata ya Kikukuru, Kata ya Kitwechenkura. Mradi huu unahitaji fedha nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekuomba na tumekaa sana na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, mmenihakikishia mradi huu unakwenda kuanza na nimeuona kwenye bajeti mmeuweka. Niombe sana kama ambavyo umekuwa msaada, umekuwa mtu wa karibu kwa wana Kyerwa wewe pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na wasaidizi wako. Nikuombe mradi huu tunapomaliza bajeti uweze kuanza ili wananchi wa Kata hizi ambazo nimezitaja na wao waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Kyerwa mnaweza mkaona ni miradi mingi. Kyerwa tulikuwa mbali sana hatukuwa na miradi, miradi mingi ambayo walikuwa wanapigia mahesabu ile miradi ya zamani. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri, miradi hii iweze kukamilika ili wananchi wangu, mabosi wangu wa Jimbo la Kyerwa na wao waweze kupatiwa maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho nilikuwa nataka nishauri Serikali, ukija kuangalia Mkoa wa Dodoma ni Mkoa ambao tunatumia maji ya kuchimba. Lakini maji haya ni maji ya chumvi, ni maji kiasi gani tunayoyapoteza? Maeneo mengi Mkoa wa Dodoma mafutiko ni mengi. Mheshimiwa Aweso, sisi tunakuamini pamoja na timu yako, hebu angalia ni namna gani tunaweza tukavuna maji yanayopotea ili wananchi wa Mkoa wa Dodoma waweze kupata maji, yanaitwa maji safi, maji laini? Yale maji ambayo sio maji chumvi. Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, niombe sana hili uliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine wameeleza hapa Wabunge, Wizara ya Maji madeni ni mengi mnayodai. Kwa nini msije na mfumo wa mtu kulipia kama tunavyolipia umeme akalipia maji ili kuondoa hii adha ambayo mnaipata ya madeni kuwa mengi? Lazima tuje na ubunifu, mwananchi anakwenda analipia akishamaliza kulipia ndio anapata huduma ya maji. Vinginevyo, Mheshimiwa Aweso, hawa watu wataendelea kukukwamisha pamoja na Waziri wa Fedha. Tunataka tupate pesa hii ili pesa hii iende kuwasaidia wananchi wengine maeneo mengine ambayo bado hawajapata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, nikushukuru tena na nikutakie kila la heri. Lakini ndugu zangu niwaombe, pamoja na hawa watendaji kufanya kazi nzuri hebu tumkumbuke Rais wetu ambae kwa kweli anafanya maajabu katika nchi hii. Tumuombee kwa Mungu ili Mungu aendelee kumlinda, aendelee kumpa afya njema ili aendelee kuwatumikia watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuchangia Wizara hii muhimu. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na nguvu kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kupongeza, Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yako, mnafanya kazi nzuri mimi nimekuwa Mwanakamati wa Wizara yako, hivyo ninajua kazi nyingi na kubwa unazozifanya. Wewe pamoja na timu yako tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nianze kuongelea barabara zangu, Barabara ya Mlushaka kwenda mpaka Murongo; Mheshimiwa Waziri umeandika mwenyewe na hayo umeyasoma mbele ya Bunge, Barabara ya Mlushaka kwenda mpaka Mrongo itasainiwa kabla ya Mwezi wa Saba. Barabara ya Mgakorongo kwenda mpaka Murongo umeahidi itasainiwa kabla ya Mwezi wa Saba. Mheshimiwa Waziri ninakuheshimu sana na nisingependa niongee maneno magumu. Maneno haya umeyasema ndani ya Bunge hili na umeyasema mbele ya Mungu na Mungu amesikia. Niombe sana, hakuna cha kusainia Dodoma, barabara hii ikasainiwe Kyerwa ili Wanakerwa waone kazi kubwa ambayo anaifanya Mama Samia lakini pia waone kazi kubwa anayoifanya Mbunge wao ambaye amekusumbua mara kwa mara. Kwa hiyo ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri uzingatie, tunapomaliza bajeti twende Kyerwa tukasaini barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine kwa upande wa barabara, mimi nipongeze sana Meneja wetu wa Mkoa anafanya kazi nzuri sana. Kijana huyu ni mtulivu na ni msikivu sana. Lakini bajeti ambayo inatengwa kwa Mkoa wa Kagera ni ndogo. Mkoa wa Kagera una vipindi virefu vya mvua, takriban miezi saba yote tuna vipindi vya mvua. Kwa hiyo unakuta barabara za Mkoa wa Kagera hazipitiki kwa sababu bajeti inayotengwa ni kidogo sana. Kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri mnapokuwa mnatenga bajeti angalieni hii mikoa ambayo ina changamoto ya vipindi virefu vya mvua ili iweze kupewa bajeti na barabara ziweze kupitika hasa hasa zile barabara za udogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee suala la uwekezaji kwenye bandari. Bandari yetu mimi niseme ndio moyo wa Taifa, lakini bandari hii ni lango kwa nchi zinazotuzunguka kwa sababu ya umuhimu wake. Hakuna nchi ambayo inatuzunguka haihitaji Bandari ya Dar es Salaam. Lakini bado mimi niseme sijaona nguvu kubwa na juhudi kubwa ambazo mmeziweka kama Serikali kuhakikisha bandari hii inaleta tija katika Taifa letu. Leo hii kila Mbunge anayechangia hapa anaomba maji, anaomba barabara, anaomba umeme na mambo mengine lakini tunachokitega uchumi kimekaa tu. Sasa niombe sana Mheshimiwa Waziri kelele hizi achana nazo. Mimi ninaamimi Serikali kwa kipindi ambacho mmekaa na TICTS mmejifunza mambo mengi, mmeona mapungufu yaliyokuwepo, wapi kama Serikali walikosea sasa ni wakati wa kutafuta mwekezeji ili tuingie ubia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ninaamini ndugu zangu kuna wengine wameshauri wanasema Serikali iwekeze, hivi tutawekeza kwenye vitu vingapi? Na mwisho wa siku tutakachoenda kukifanya lazima tuende kukopa. Leo hii tumekopa kwa ajili ya Mradi wa Mwalimu Nyerere, tumekopa kwa ajili ya SGR na miradi mingine. Tukiendelea kukopa mwisho wa siku yatatokea mambo mengine ambayo tunayasikia kule Kenya. Sasa niombe sana Mheshimiwa Waziri simama imara pamoja na timu yako, tunaamini yule kijana, Mkurugenzi wa Bandari yuko vizuri sana na tumeanza kuona maboresho ambayo ameyafanya. Sasa msije mkasema mambo hayafanyiki, hayafanyiki kwa sababu bado hatujaweza kuwekeza vya kutosha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana wekeza hapo nguvu tafuta mtu ambaye anafaa tuwekeze ili bandari yetu hii iweze kuinua uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii tumejenga SGR na wanafanya vizuri sana, nimpongeze sana Mkurugenzi wa TRC, anafanya kazi nzuri, amesimia miradi inakwenda vizuri. Lakini SGR hii mnategemea ni ya kubeba abiria? Hii si ya kubeba abiria ili tuweze kupata faida na SGR lazima tuwe na mzigo utakaotoka nje na kuingia. Kwa hiyo niombe sana Serikali iendelee kuweka nguvu ili tuone faida ya kujenga SGR. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, hili usimame imara, vita ya kiuchumi inahitaji kujikunja, inahitaji kuwa imara. Ukizubaa kidogo tu kelele hizi zinazopigwa usifikiri watu wanapiga kelele kwa sababu wanakutakia mafanikio. Jambo ambalo tunashauri sisi kama Wabunge tuombe sana hii timu ambayo inatafuta mtu wa kuwekeza ijipange vizuri, tutafute wanasheria ambao ni wazuri. Huyu mwekezaji tutakaye mleta atakaposhindwa pawepo na vifungu ambavyo vitambana akishindwa aondoke, lakini lazima tuweke nguvu sana kwenye bandari yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niendelee sana, nirudie sana kumpongeza sana Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa, na mmesikia Waheshimiwa Wabunge bado hajaona faida, na ninyi Wabunge ni mashahidi, bado hatujaona faida kwenye banda hili. Sasa Mheshimiwa Rais kama ameliona hilo leo hii wanaleta wazo la kuwekeza, kwa nini tusi…

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Bilakwate kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Festo Sanga.

TAARIFA

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba amezungumzia utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwamba ni mzuri na ni kweli ni mzuri na kwenye ripoti iliyotoka leo ya World Bank inaonesha kabisa Bandari ya Dar es Salaam ndiyo inaongoza sasa kwa Afrika Mashariki kufanya kazi vizuri ikiwa ni bandari ya 312 na wenzetu wa Mombasa wako 326, tumeshawapiku. Kwa hiyo, ni kazi nzuri ambayo anafanya Mkurungenzi wa Bandari, Ndugu Mbossa tunampongeza sana sana kwa kile anachokifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

SPIKA: Mheshimiwa Bilakwate unaipokea taarifa hiyo?

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo naipokea na mimi naendelea kumpongeza lakini ili tumpongeze zaidi lazima tulete uwekezaji ambao una tija na tuone matunda ya bandari yetu.

Mheshimiwa Spika, niendelee kusema ndugu zangu, kazi hii inayofanyika katika Taifa hili mnaona uwekezeji mkubwa tulionao, ukienda kwenye umeme, ukiangalia miradi ya barabara iliyotajwa hapa, ukiangalia miradi ya maji ni miradi mikubwa. Mheshimiwa Rais amejipanga kuhakikisha Watanzania wanapata huduma. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge na hili nataka niongee kwa upole sana; kazi hii ina vita katika ulimwengu wa roho na katika ulimwengu wa mwili. Inawezekana msinielewe; lakini vita hii ili tuweze kushinda na Mheshimiwa Rais aendelee kufanya kazi vizuri niombe sana mumuombee, muombeeni, Mheshimiwa Rais ana maono makubwa. Mimi juzi nilivyoenda pale Ikuu, Hayati John Pombe Magufuli wakati anaiacha ile Ikulu haikuwa vile lakini ninyi mmeona. Ukienda kwenye Mradi wa Mwalimu Nyerere unakwenda vizuri, ukienda SGR miradi ambayo iliachwa na Hayati leo hii inakaribia kumalizika na ameongeza miradi mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana tuendelee kumuombea, tuendelee kumtia moyo lakini pamoja na wasaidizi wake ili Tanzania yenye neema iweze kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na nguvu ya kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa, pia nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya ya kutangaza vivutio vyetu na tumeanza kuona faida kubwa ya Royal Tour ambayo imeanza kuleta watalii wengi na kuongeza fedha za kigeni.

Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Waziri sasa hivi hii ni Wizara ya tatu na kila ulikoenda kwa kweli ulienda na matumaini na uliacha matumaini na ninaamini Wizara hii ambayo imeleta makovu mengi, imeleta huzuni na masikitiko kwa watanzania sasa naamini imepata mwenyewe.

Mheshimiwa Spika, tumeongelea suala la tembo, kwa kweli tembo tunawapenda na wanadamu tunawapenda, jambo hili Mheshimiwa Waziri lazima ujipange. Watu wamejeruhiwa, watu wameteseka muda mrefu sasa ni wakati wako kuleta majibu ambayo yanaenda kuponya haya majeraha ya muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapouliza hapa Bungeni wanakwambia tembo hawa ni njia yao walipita miaka 200, lakini jambo ambalo linasikitisha maeneo hayo ambayo yamevamiwa na tembo ni maeneo ambayo yametengwa kwenye vijiji kwa mujibu wa sheria. Wakati wanatenga haya maeneo Serikali haikujua hapa ni njia ya tembo? Kwa nini watenge haya maeneo wawapeleke wananchi, waende kuendeleza maeneo hayo, wana mashamba wamejenga nyumba. Kwa mfano, kule kwangu Kyerwa katika Kata ya Businde, Kata ya Bugara Kata ya Kibare wanaendelea maeneo mengi. Hawa tembo walikuja kama 20 sasa hivi wameshazidi 100, hivi Mheshimiwa Waziri kama mmeshindwa kuwafukuza hata mmeshindwa uzazi wa mpango? Leteni uzazi wa mpango wa hawa tembo, tembo hawa wanaua wananchi, wanatesa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maeneo mengi kwenye kitongoji kimoja wameondoka wananchi zaidi ya 200, walikuwa na mashamba walikuwa wanafanya kazi zao vizuri. Nyumba zao zote zimeteketezwa halafu mnakuja mnasema kuna kifuta jasho. Mheshimiwa Waziri tunaomba hili uliangalie.

Mheshimiwa Spika, kifuta jasho mtu ana shamba zaidi ya heka 10, zaidi ya heka 20 ana migomba amejenga nyumba zaidi ya Shilingi milioni 20 unampa milioni moja, unampa 100,000 moja hiyo hela inamsaidia nini? Tumewafanya Watanzania kuwa maskini kwa sababu ya hawa tembo. Kwa hiyo ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri unapokuja hapa kumalizia bajeti hii unapojumuisha hapa utueleze ni mikakati ipi umekuja nayo ili kuhakikisha mnadhibiti hawa tembo, vinginevyo hali ni mbaya na wanazaliana sijui namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri niongelee jambo jingine kuhusu suala la mipaka ya hifadhi pamoja na wananchi. Tulisikia Serikali imeunda timu ya Mawaziri Nane, Mheshimiwa Waziri kama unataka kufanya hili jambo kwa ufanisi ile taarifa ya Mawaziri Nane usiende nayo. Jiridhishe wewe mwenyewe kwa sababu haiwezekani hawa Mawaziri Nane wanaenda kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, shida iko Kyerwa nyinyi mnaishia pale Bukoba Mjini. Haiwezekani! Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri jiridhishe na taarifa hii, lakini maeneo mengine walikuwa wanafika kwa vitisho kuwaambia hawa hapa hampati kitu lazima muondoke.

Mheshimiwa Spika, hawa wananchi mnaowafukuza kama siyo Watanzania hawa, hawa ndiyo ninaoamini wanaweza wakawa wahifadhi wazuri wa kulinda vivutio vyetu na kulinda maeneo yetu. Lakini mnavyowafukuza namna hii mnajenga chuki na uadui mkubwa. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri hili uliangalie na ulifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine Mheshimiwa Waziri nilikuwa najaribu kuangalia bajeti za nchi nyingine hasa kwenye mambo ya utalii. Mungu ametujalia vivutio vingi katika Taifa letu, lakini hivi vivutio tumevitangaza namna gani? Tunaona ile Royal Tour kitu ilichokifanya lakini tuombe na sisi kama Serikali lazima tujipange kuhakikisha tunatenga bajeti kubwa ya kutosha. Ukiangalia niwasomee kidogo Waheshimiwa Wabunge muone nchi yetu ilivyo na bajeti za nchi nyingine.

Mheshimiwa Spika, ukienda Rwanda, Rwanda naona kama Mkoa wa Kagera. Rwanda bajeti yao ya utalii ni Dola Milioni 4.5. Ukienda Afrika Kusini Dola Mil. 75. Ukienda Kenya majirani zetu Dola Mil. 3.5. Ukienda Tanzania kwetu Dola 1.5, jamani hata Rwanda? Hata Rwanda kwa kweli, hii hapana! Kwa hiyo, niombe sana Serikali ijipange kuja na bajeti kubwa tutangaze hivi vivutio ambavyo Mwenyezi Mungu ametujalia ili Tanzania tupate pesa. Tunaanza kukimbizana na wafanyabiashara, tunakimbizana na watu wengine wakati tunavvyo vitega uchumi pesa iko nyingi. Tuitumie fursa hii ambayo Mungu ametujalia ili tuone tutakavyopata pesa nyingi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninakushukuru naunga mkono hoja.

SPIKA: Ahsante sana. Sijaelewa hapo umetaja Kagera halafu ukataja Rwanda ili nielewe vizuri mchango wako.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, yaani nilichokuwa nalinganisha ukiiangalia nchi ya Rwanda ni kama ina lingana lingana na Mkoa wa Kagera lakini wanatuzidi mara nne.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi na mimi nichangie. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na nguvu ya kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya katika Taifa hili, ni ukweli usiopingika Mheshimiwa Rais amepokea miradi mikubwa na ameiendeleza vizuri na tunaona anaibua miradi mingine mikubwa, kwa kweli tuna kila sababu ya kumpongeza, tuna kila sababu ya kuendelea kumuombea ili Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema, aendelee kufanya kazi vizuri, lakini haya mazuri yote tunayoyaona tunaamini ni pamoja na wasaidizi wake hasahasa akiwemo Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kazi kubwa unayoifanya ya kusimamia Wizara inayokusanya fedha. (Makofi)

Ninakupongeza sana ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, unafanya kazi kubwa nzuri, songa mbele tuko pamoja na wewe na ninaamini Mungu atakusaidia kwa kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee mikoa hii ambayo ni mikoa masikini. Ukiangalia kwenye bajeti zilizopita bado sijaona mkakati na mipango maalum ya Serikali kuweka nguvu kwenye hii mikoa maskini na miongoni mwa mikoa maskini, nisikitike mkoa wangu wa Kagera ni miongoni mwa mikoa maskini.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo ambalo linasikitisha ukija kuangalia hii mikoa ambayo ni maskini ndio mikoa ambayo zile fursa za kiuchumi haziko sawasawa. Ukija kuangalia mimi napakana na nchi ya Uganda, ukiangalia kwa majirani zetu pale, ukiangalia barabara wamekuja wameleta mpaka mpakani tena wakavuka wakaingia kwetu kidogo kutuonjesha, kwetu ukiingia hali ni mbaya.

Mheshimiwa Spika, nimeongelea barabara ya Mgakorongo kwenda mpaka Murongo, nimeongelea barabara ya Murushaka kwenda mpaka Murongo, barabara hizi zimeshatangazwa tender lakini shughuli ni kusaini barabara hizi ili ziweze kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri Mkoa wa Kagera tuna fursa nyingi sana, lakini shida iliyopo miundobinu ya barabara siyo rafiki. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, mimi ninaamini kazi unayoifanya ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, nimejaribu kufuatilia sana baada ya kuona Waziri ananiambia baada ya wiki mbili tutakwenda kusaini, baada ya wiki moja tutasaini. Sasa nikafuatilia, taarifa za ndani nilizozipata wanasema shida ni fedha. Sasa ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, wewe ndiye mwenye fedha, nikuombe sana barabara hii ambayo ni ya Murushaka kwenda mpaka Murongo, barabara ya Mgakorongo, barabara hizi zisainiwe ili tuweze kuinua uchumi wa Mkoa wa Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kyerwa sisi tunalima kahawa nyingi sana, lakini nguvu tunayotumia kuisafirisha kahawa hii kwenye barabara hizi mbovu unakuta tunatumia gharama kubwa wakati tungeweza kutumia gharama kidogo.

Mheshimiwa Spika, lakini mikoa hii ambayo ni maskini ndiyo mikoa ambayo hata umeme wa uhakika hakuna. Umeme kwa siku unaweza ukakatika zaidi ya mara kumi, kweli hapo tunategemea hawa wananchi wanaweza wakaendelea? Tunaweza tukainua uchumi wao?

Mheshimiwa Spika, mimi kwangu nina vitongoji 617, kati ya vitongoji hivyo vitongoji 400 havina umeme; mnategemea hawa wananchi watainuka kweli? Lakini mikoa hii ambayo ni maskini fuatilia muangalie miradi ya maji, ni midogo sana. Hata hiyo iliyopo bado fedha inayoletwa kwangu mimi nina mradi wa Nkwenda mpaka Chanya, nina mradi wa Isingilo, nina mradi wa Mabila, miradi hii inavyokwenda inakwenda kwa kusasua kwa sababu fedha haiji kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, mikoa hii ambayo ni maskini uweke mpango maalum namna gani ya kuboresha miundombinu, namna gani ya kuipelekea miradi ya maji, namna gani ambayo mnaweza mkaipelekea umeme wa uhakika ili tuone kama hii mikoa inaweza ikainuka.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilisemee ni kahawa; kahawa ni zao la kimkakati, lakini zao hili, mimi nipongeze kwa sehemu Serikali imejitahidi ndani ya miaka hii miwili ya mama yetu Samia, kahawa tulikuwa tunauza bila utaratibu, lakini angalau tuemeweza kuipeleka kwenye mnada bei angalau inaweza kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini bado niiombe sana Serikali ifanye utafiti kwa nini nchi jirani ya Uganda kahawa bei iko juu kuliko Tanzania? Tunafanya kazi kubwa ya kupambana na watu wanaofanya magendo. Hebu tufuatilie; hawa Uganda wanauza wapi? Mimi ninaamini soko la kahawa dunia nzima ni moja, sasa hawa Uganda wanauza wapi?

Mheshimiwa Spika, tufanye utafiti wa uhakika ili tuweze kuwapa wakulima hawa bei nzuri tuondoe hii biashara inayoendelea ya magendo na kuanza kukimbizana na watu, kuwapiga na kufanya mambo mengine, kwa sababu hatuwezi kuzuia, kama huna bei nzuri jirani yako ana bei nzuri, watu watakimbia. Mimi Mbunge siungi mkono biashara ya magendo, lakini unazuiaje? Kwa hiyo, niombe sana Serikali iliangalie.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la kahawa kuna hii biashara ya butura inayoendelea. Biashara hii lazima tuje na mpango wa kuwawezesha hawa wakulima angalau waweze kupata fedha ambayo itawasaidia pale wanapoanza kuhudumia hii kahawa mpaka wanapofika kipindi cha kuvuna, awe na fedha ya kumsaidia kuhudumia kahawa mpaka anaipeleka kwenye soko.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri umeongelea suala la makusanyo na kwenye hotuba yako ukaeleza mwamko mdogo wa watu kulipa kodi.

Ndugu zangu, mimi nilikuwa namwomba sana Mungu, ni kwa nini Watanzania hatutaki kulipa kodi na hatutaki hata kudai risiti tu. Unatoa fedha yako mfukoni unakwenda kununua kitu lakini unaona haikuhusu. Ni kwa sababu hatuna upendo na Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, na nianze na sisi humu ndani, leo tumekuja hapa kila mmoja anaeleza anataka barabara, anataka maji, lakini wewe umewajibika vipi kuhamasisha wananchi wako, kuhamasisha wafanyabiashara ulionao, lakini wewe mwenyewe binafsi unapokwenda kununua vitu ni mara ngapi umedai risiti? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara wengi mko humu ndani, ni mara ngapi mmeiibia Serikali? Halafu tunakuja hapa tunataka barabara. Kila mmoja awajibike kwenye nafasi yake. Tulitangulize Taifa mbele, tuwe na upendo kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi hii tunayoidai siyo kwa faida ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, wala siyo kwa faida ya Mama Samia tu, ni kwa faida ya Watanzania wote. Wote tuiwa na moyo wa upendo kwa Taifa, tukalitanguliza Taifa, unapokwenda kununua kitu ukadai risiti, mimi hata kama ni shilingi 5,000 lazima unipe risiti, vinginevyo utarudisha hela yangu. Hebu tuwe na moyo wa kulitanguliza Taifa, tudai risiti tukalipe kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nina uhakika Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, hela mnayoikusanya na hili jambo ninalowaambia nimemwomba Mungu na nina uhakika Mungu alichosema na mimi ni sawa, Watanzania hatuna upendo na Taifa letu. Nina uhakika Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kama kila Mtanzania akisimama kwenye nafasi yake, akalipa kodi sawasawa, akadai risiti anapokwenda kununua, hela tunayoweza kukusanya peke yake inaweza ikakamilisha miradi yote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niwaombe sana ndugu zangu kila mmoja awajibike. Wafanyabiashara wanapodai Serikali iwahudumie na wao wawe tayari kuhakikisha wanalipa kodi kwa uaminifu. Sisi Wabunge tunapokwenda tunasema tunataka barabara, tunataka miradi ya maji, tunataka umeme, na sisi tuwajibike tuwe waaminifu kulipa kodi, tuwe waaminifu kuhakikisha tunadai risiti tunaponunua bidhaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Bilakwate, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa nguvu na afya kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa, pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri zinazoendelea kufanyika chini ya Mama yetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kwa upande wa miundombinu pamoja na ujenzi wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kwanza barabara. Barabara ni uchumi, barabara ni maendeleo, barabara ni mawasiliano, jambo ambalo mimi ninaishauri Serikali, ni kweli wamekuwa wakijijitahidi kujenga barabara lakini mimi ninao ushauri, tunapojenga barabara hebu tuangalie vipaumbele vya Serikali hasa kwa upande wa mambo ya uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano unajenga barabara, nimekuwa nikizungumzia sana barabara za Kyerwa, sizungumzii ili zijengwe tu zile barabara kwa mfano barabara ya Mgakolongo kwenda mpaka Mlongo ni barabara inayounganisha nchi ya Uganda pia ni barabara ambayo ni muhimu sana, hasa vivutio ambavyo viko Kyerwa tunayo Ibanda na Rumanyika hifadhi za Ibanda na Rumanyika ambayo ni muhimu sana. Waganda wamekuja wakija kule kwetu pamoja na watu wa Rwanda kuja kupumzika kipindi cha sikukuu. Kwa hiyo niombe sana Serikali inapojenga barabara hebu tuangalie, hizi barabara umuhimu wake ni upi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo jingine pamoja na kusemea hizi barabara zetu kwa nchi nzima ya Tanzania tunalo zao la kiuchumi zao la kimakakati zao la kahawa, hakuna Wilaya ambayo inalima kahawa nyingi kama Wilaya ya Kyerwa. Kwa hiyo, wananchi wamekuwa wakipata adha sana pamoja na wafanyabiashara kusafirisha yale mazao, kwa sababu barabara zetu unakuta mara nyingi hazijatengenezwa haziko vizuri. Kwa hiyo niombe sana hili ninalirudia na nimekuwa nikilisemea sana, siwezi kuruka sarakasi lakini mimi ni Mtumishi wa Mungu nisije nikakunyanganya hicho kiti niombe sana, barabara hii umeiweka kwenye bajeti na mmeshatangaza barabara ya Mrushaka kilometa 50, kutoka makao makuu ya Wilaya kwenda mpaka Karagwe. Niombe sana Waziri, tender imeshatangazwa na imeshafunguliwa, sasa huu mchakato wa kuanza barabara naomba ukamilike haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia barabara ya Mgakorongo kwenda mpaka Murongo, barabara hii ni muhimu sana kama nilivyoieleza niombe sana umetuahidi mnajenga kilomita 50 tukoka Murongo kuja mpaka Kigarama sasa ninaomba mchakato huu ukamilike haraka ili barabara zetu hizi ziweze kupitika na ziweze kuongeza uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ni suala la bandari. Bandari ni muhimu sana, hasa ukiangalia bandari yetu tunazungukwa na nchi nyingi sana ambazo ni muhimu Serikali imeanza kuboresha nasi kama Kamati tumekwenda tumejionea uboreshaji unaoendelea kwenye bandari zetu. Ninaomba sana Serikali iendelee kuongeza nguvu ili hizi bandari zetu ziweze kushindana na bandari nyingine, ninaamini bandari yetu itakapokuwa imeboreshwa nina uhakika majirani zetu watakimbilia kwetu kwa sababu ndiyo karibu. Kwa hiyo, niombe sana tuwezeshe Mtendaji wetu tumpe fedha za kutosha, yale mahitaji yake anayohitaji kuboresha bandari yetu aweze kuiboresha na bahati nzuri ni mbunifu mzuri. Tumuunge mkono, tumtie moyo ili asonge mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nisemehe upande wa meli. Nchi yetu imejaliwa tunayo Maziwa, tuna Mito, tuna Bahari, ninaamini tukizitumia vizuri tunaweza tukakuza uchumi wa Taifa letu. Tayari Serikali imeanza kujenga meli kubwa, tunayo MV. Mwanza Hapa Kazi Tu na nyingine, niombe sana Serikali iendelee kuweka nguvu kubwa tutumie haya Maziwa yetu, tutumie bahari tulizonazo ili kuongeza uchumi lakini pia kurahisha usafiri wa majini. MV. Mwanza pale Hapa Kazi Tu tuliitembelea ni nzuri na kazi inaenda vizuri sasa ninaomba Mheshimiwa Waziri, pale mmemuweka kijana ambaye anafanyakazi vizuri, muongezeeni nguvu, mpeni pesa aendelee kusimamia. Pia niombe Mheshimiwa Waziri niombe sana hawa watu ambao mmewaweka na mmewapa kazi kubwa sana wanafanyakazi nzuri wasiendelee kukaimu, mtu anapokuwa anakaimu anakuwa hajiamini. Kwa hiyo niombe sana Serikali iweke pesa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambao nilisemee ni kuipongeza sana Serikali na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo anaendelea kuendeleza kazi ambazo alianza mtangulizi wake na yeye akiwa Makamu wa Rais tunaona anaendelea kuweka nguvu kubwa kwa upande wa SGR, SGR ni muhimu sana. Kwa hiyo, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri endeleeni kuongeza nguvu hizi kelele panapokuwepo na ushindani lazima kelele zitokee. Kwa hiyo, ninaomba nisimamie haki, mtende haki lakini vipande vilivyobaki viweze kukamilishwa ili kurahisha usafirishaji katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine tukimaliza kujenga hizi reli zetu za SGR, ninyi wote ni mashahidi barabara zetu zimekuwa zikiharibika sana kwa sababu ya magari ya mizigo.

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri, kengele ya pili.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba sana Serikali iweke nguvu mkamilishe, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mungu anayeendelea kunijalia afya na nguvu ya kuendelea kuwatumikia wananchi wangu.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Bashe pamoja na timu yake kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye Wizara ya Kilimo, kwa muda mfupi tumeona mageuzi makubwa sana, Wizara ameitendea haki. Nazidi kumwombea neema na msaada wa Mungu ili Mungu aendelee kumpa maono makubwa kwa ajili ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kuendelea kuongeza bajeti ya kilimo na hii ni kutambua umuhimu wa Sekta ya Kilimo kuwa ndio uti wa mgongo wa Taifa, lakini pia Mheshimiwa Rais kutambua umakini na usimamizi mzuri unafanywa na Wizara ya Kilimo chini ya Mheshimiwa Bashe.

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Kilimo ndio sekta inayotoa ajira nyingi kuliko sekta nyingine yoyote, hii ni sekta muhimu kwa Taifa, tukiendelea kuweka nguvu zaidi na kuiongezea bajeti chini ya Waziri makini Mheshimiwa Bashe tunakwenda kuliongezea Taifa fedha nyingi za kigeni ambazo tunazihitaji sana.

Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu wa kuuza kahawa kwenye mnada ngazi ya AMCOS; nimpongeze sana Mheshimiwa Bashe kwa kuruhusu kahawa kuuzwa kwa njia ya mnada kupitia AMCOS, hii imekuwa na mafanikio makubwa sana, utaratibu huu wanachama wa AMCOS kukusanya kahawa yao pamoja na ushindani wa mnada kufanyika ngazi ya AMCOS inaleta uwazi, bei nzuri na inaondoa mambo mengine yaliyokuwa yamejificha katika utaratibu wa zamani.

Mheshimiwa Spika, utaratibu huu unampa nguvu mwananchi au wana AMCOS kuamua kuuza kahawa au kutouza akisubiria bei nzuri ya soko, lakini kupitia utaratibu huu tumeshuhudia bei ya kahawa kupanda mfano kwa Kyerwa mwaka 2021/2022 bei ilkuwa kati ya shilingi 1,100 mpaka shilingi 1,500. Baada ya mnada kufanyika ngazi ya AMCOS mwaka 2022/2023 bei imetoka shilingi 1,800 mpaka shilingi 2,800 na mwaka 2023, bei imefika shilingi 3,200. Haya ni mafanikio makubwa na ukombozi wa mkulima, Mheshimiwa Mama Samia na Mheshimiwa Bashe tunawashukuru sana kwa maamuzi hayo magumu yaliyokuwa yameshindikana miaka mingi.

Mheshimiwa Spika, nashauri utaratibu huu kwa kuwa umeonesha ufanisi mkubwa na umeleta uwazi, nashauri utumike kwa mazao mengine ya kimkakati kwa sababu ndio mkombozi wa mkulima.

Mheshimiwa Spika, naomba nimtie moyo Mheshimiwa Bashe asirudi nyuma katika hili, tunamwombea na tuko pamoja na yeye, mafanikio yoyote lazima yawe na maumivu na kuna upande mmoja lazima uumie, najua Mheshimiwa Bashe kwa kuruhusu na kusimamia utaratibu huu wako waliokuwa wakinufaika na utaratibu wa minada ya mwanzo hawawezi kufurahi hata kidogo.

Mheshimiwa Spika, niipongeze sana Serikali kwa kuanzisha Benki ya Ushirika, nataka nitoe na nishauri benki isiishie kwa wakulima wakubwa au wanunuzi wakubwa, benki hii iangalie namna itakavyomsaidia mkulima wa hali ya chini ambao ni wanachama wa AMCOS, wasaidiwe pale anapohudumia mazao yake mpaka anapopeleka mazao yake sokoni.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu pamoja na mafanikio niliyoyataja hapo juu bado wananchi wanapata wakati mgumu na biashara ya butura na kangomba ambayo biashara hii inawaacha wakulima wakiwa maskini, kama mkulima amejisajili kwenye AMCOS na shamba lake linajulikana, ni kwa nini asikopeshwe akahudumia mazao yake ili kuepukana na biashara ya kangomba na butura.

Mheshimiwa Spika, ili tuwe na kilimo chenye tija tunawahitaji Maafisa Ugani wa kutosha, hapa Mheshimiwa Waziri Bashe lazima tumwombe sana aongeze nguvu kubwa sana, bado Maafisa Ugani waliopo hawajaweza kutimiza majukumu yao ipasavyo, Maafisa Ugani tunataka tuwaone pale mwanzo mkulima anapoanza kulima mpaka anapovuna, Maafisa Ugani wakimsaidia mkulima ipasanyo tutaongeza uzalishaji na mavuno yenye ubora na hapo ndipo tutakapoongeza mauzo ya nje na kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni. Maafisa Ugani waliopo sasa baadhi yao walio wengi tunawaona pale mkulima anapoanza kuvuna, wakianza kuwasumbua wakulima na kuwakamata hovyo, kama wangeanza tangu mwanzo mkulima anapoanza kupanda, anapalilia mpaka anavuna itaondoa sintofahamu wakati wa mavuno kuanza kukimbizana na wananchi na kutengeneza mianya ya rushwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu masoko ya kimkakati; Kyerwa tunayo masoko ya Nkwenda na Murongo, masoko haya ni ya miaka mingi yametelekezwa, nimpongeze Mheshimiwa Bashe kwa kuyachukua ili wayakamilishe, ni jambo jema kwa sababu ya umuhimu wake, masoko haya yakikamilika yanakwenda kumsaidia mkulima, lakini pia kuwavutia majirani zetu kuuza na kununua kwetu na yakaliingizia mapato ya kigeni. Nimwombe sana Mheshimiwa Bashe masoko haya yakamilike, maana tangu ameeleza kutangaza tender imepita karibu mwaka sasa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu miche ya kahawa; Kyerwa ndio Wilaya inayozalisha kahawa nyingi, lakini pamoja na kuzalisha kahawa nyingi, mibuni mingi ni ya miaka mingi na mingine imeshambuliwa na ugonjwa wa mnyauko. Ombi langu nimwombe sana Mheshimiwa Bashe kutuongeza miche ya kahawa angalau iwe shilingi 10,000 kwa sababu mahitaji ni makubwa sana na kama ajuavyo kila kilo inayouzwa inakatwa pesa kwa ajili ya kuendeleza zao la kahawa na Kyerwa ni mzalishaji mkubwa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, niendelee kumwombea Waziri mafanikio na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na nguvu ya kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na mama yetu Mheshimiwa Samia kwa kazi nzuri zinazofanyika. Ni ukweli usiopingika, kwa kweli mama anafanya kazi nzuri pamoja na wasaidizi wake. Pia Mheshimiwa Waziri wa Fedha na wasaidizi wako mnafanya kazi nzuri, tunawapongeza sana. Tunaona miradi mingi ikipelekewa fedha, kwa kweli tunajivunia uongozi wa Mheshimiwa Mama Samia Suluhu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia kwenye kilimo. Kilimo ni biashara, kilimo ni ajira, kilimo ndiyo sekta ambayo inachangia sana kwenye pato la Taifa kama tukiwekeza, na pia kilimo ndiyo sekta ambayo imeajiri watu wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza kuchangia sekta ya kilimo kwa sababu ninaamini Serikali ikiwekeza nguvu sana kwenye kilimo tunaweza tukainua pato la Taifa. Naipongeza sana Serikali, kwa muda mrefu Waheshimiwa Wabunge tulikuwa tunapiga kelele sana hapa Bungeni tukizungumzia bajeti ya kilimo, lakini kwa kweli zamu hii Mama amekuja na kipimo cha kusukwasukwa, kushindiliwa na kumwagika. Kutoka Shilingi bilioni 294 mpaka kufika Shilingi bilioni 954. Kwa kweli hii ni neema kubwa kwa wakulima na kwa Wizara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwa haya tunayoyaona kupitia bajeti hii chini ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, akisaidiana na Mheshimiwa Bashe (nakusema wewe kwa sababu ndio unayetoa fedha) tunaenda kuona kilimo chenye tija ambacho kitampatia mkulima pembejeo kwa wakati, kilimo ambacho tutapata mbegu za uhakika na zenye ubora, kilimo ambacho tutakuwa na soko la uhakika, kilimo ambacho kitamwezesha mkulima kukopa hasa kwa kutumia benki yetu ya kilimo. Katika hili naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Benki ya Kilimo iwe rafiki wa mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa kinyume, mimi sielewi kuna nini? Naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha hili mlisimamie ili hii Benki ya Kilimo iweze kumsaidia mkulima anapoanza kulima. Pia inapofika hatua ya kupeleka mazao yake kwenye soko, ninaamini tukiyasimamia haya, pato la Taifa linaenda kuongezeka kwa haraka, pia tunaona mkulima mmoja mmoja kipato chake kikiinuka, na tutakuwa na uhakika wa chakula. Nina uhakika tukilima kilimo kinachoendana na bajeti hii ambayo imeletwa na Serikali kwenye Wizara ya Kilimo, tutakuwa na uwezo wa kupeleka chakula nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyo viwanda vingi. Sera ya Serikali ya kuwa na viwanda, viwanda hivi tumekuwa tukiagiza malighafi kutoka nje. Ninaamini tukilima, tukasimamia vizuri, tutaweza kuokoa fedha nyingi inayokwenda nje na pia viwanda vyetu kupata malighafi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la kahawa. Kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati. Kahawa ni biashara, kahawa ni siasa, na pia kahawa inatuingizia fedha nyingi za kigeni. Naipongeza Serikali kwa hatua ambayo imefikia, tumekuwa tukisema sana mkulima wa kahawa amesahaulika muda mrefu, lakini leo hii tumeanza kuona kazi kubwa iliyofanywa na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Bashe na tumeanza kushuhudia mnada ambao umetangazwa, bei ya kahawa inaanza kupanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo ambao wanabeza, wanasema mfumo huo haujakaa sawa, mimi nasema, mimi ndiye Mbunge ambaye ninatoka kwenye Wilaya yenye kahawa nyingi na hakuna wilaya inayonizidi. Kahawa nyingi zaidi ya tani 35,000 zinatoka Kyerwa. Kwa hiyo, ninaposema kahawa, najua wapo waliokuwa wananufaika kupitia mfumo wa zamani, sasa naona wanasema mfumo huo ni mbaya. Siyo mbaya! Mimi naomba tuiunge mkono Serikali katika mfumo huu ili mkulima huyu ambaye amesaulika muda mrefu aweze kunufaika na zao lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Mheshimiwa Bashe kulingana jinsi ambavyo amejipanga, kazi hii itafanyika vizuri. Pia naomba minada hii inayofanyika, Serikali isiwaachie hao wataalamu kwa sababu, kama wengine wako maofisini mwenu hawa ndio wanabeza, wanaweza wakaiujumu Serikali. Kwa hiyo, naomba sana hili Serikali ilisimamie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwenye suala la kilimo, Mungu ametujalia tunayo mikoa ambayo inazalisha sana, mikoa ambayo imejaliwa mvua, na ardhi yenye rutuba. Naomba sana tutumie mikoa hii kulima mazao ambayo yanaweza yakaliingizia Taifa kipato kikubwa. Kwa mfano, Kagera, tunayo mazao ambayo tunaweza tukalima na yakaingizia Taifa fedha nyingi, kwa sababu tuna vipindi virefu vya mvua, tunaweza kulima alizeti, vanilla, na parachichi. Sasa naomba sana Serikali iainishe mikoa ambayo wanaweza wakalima mazao ambayo yanaweza yakaliingizia Taifa kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kilimo chetu kiwe kizuri, naiomba sana Serikali, imekuja na Sera ya kuunganisha wilaya na wilaya kwa upande wa barabara, lakini pia na hizi barabara zinazounganisha nchi, kwani ili kilimo chetu kiwe kizuri lazima usafirishaji wa haya mazao ukiyatoa kwenye mashamba kuyapeleka sokoni uwe mzuri na rafiki. Kwa hiyo, naomba sana hili mlifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayotoka Murushaka kwenda mpaka Kyerwa ambayo tumepewa kilometa 50, tayari tenda zimeshatangazwa. Mheshimiwa Waziri wa Fedha wewe ndio unayetoa fedha, naomba barabara hii imetangazwa na Mkandarasi anatafutwa. Sasa hivi wakati itakapofika kwako ndugu yangu Mheshimiwa Waziri wa Fedha utoe fedha kwani barabara hiyo ni muhimu, kwa sababu Kyerwa tunakuletea fedha za kigeni kutoka kwenye kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunayo barabara Mgakulongo ambayo inaunganisha nchi ya Uganda pamoja na nchi yetu. Barabara hii tumepata kilometa 50 kipande kitakachotoka mpakani mwa Uganda kuja Karagwe. Naomba sana Mheshimiwa Waziri utoe fedha barabara hizi zitengenezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka niliongelee ni suala la TCCRA. Shirika hili linafanya kazi nzuri. Sasa naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kufuta kifungu cha 6, kukitoa kwenye mamlaka ya mawasiliano, hili jambo halijakaa sawa. Ninachoomba Mheshimiwa Waziri, kazi ya TBS kubwa ambayo najua, nilikuwa nafuatilia, ni kusimamia viwango kwa vifaa vyote vinavyotoka viwandani, lakini pia kusimamia ubora. Sasa haiwezekani sasa hivi unata sheria hii uifute uipeleke huku, utakuwa una mchanganyiko, na pia itaondoa ufanisi katika Mamlaka hii ya Mawasiliano. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, Wabunge wameshauri hili uliangalie, acha kifungu hiki kibaki TCCRA ili kazi nzuri iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niongelee kuhusu utawala bora. Serikali imeanza kuboresha maslahi ya watumishi, lakini lipo jambo lingine ambalo halijakaa sawa. Watumishi hawa kumekuwa na utaratibu wa kuhamisha watumishi, unamtoa mtumishi labda Kyela unampeleka Kyerwa au unamtoa Kyerwa unampeleka Songea, zaidi ya kilometa 1,500. Mtumishi huyu ana mwenza wake, unapomtoa huku unamwacha mwenzake, tunaenda kusababishia msongo wa mawazo. Pia tunaenda kuwasababishia hawa watumishi ndoa zao kuvunjika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, kuna mahitaji mengine ambayo watu wanahitaji kabla hujamhamisha mtumishi, angalia ni wapi anapotoka, halafu na mwenzawake yuko wapi? Kama yupo ndani ya Serikali, angalau mlete karibu hata weekend waweze kutembeleana. Kwa hiyo, naomba sana hilo mliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa Kuchunguza Mgogoro wa Ardhi kati ya Mwekezaji kwenye Shamba la Malonje na Vijiji Vinavyolizunguka Shamba hilo Kikiwemo Kijiji cha Sikaungu katika Jimbo la Kwela
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye kamati hii muhimu. Kwanza nakushukuru kwa kuniamini kuwemo kwenye Kamati hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mungu aliyekuongoza kuweza kuunda Kamati hii. Nasema hivi kwa sababu, hawa wananchi inaonesha wamepata shida, wamepata mateso muda mrefu, sasa Mungu ameamua, kupitia wewe, aweze kumaliza mgogoro huu na naamini utaisha.

Mheshimiwa Spika, kama walivyochangia watangulizi wenzangu, kwa kweli ukifika kule site ukawaona wale wananchi mateso ambayo wameyapata, umaskini walionao, namna ambavyo wananchi wamepigwa na kunyanyaswa, kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha sana. Tunapenda wawekezaji, lakini wawekezaji wa namna hii kwa kweli, Serikali iwaangalie kwa karibu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo linasikitisha, niseme nimeokoka na naamini hapa Bungeni hakuna mtu ambaye ana mashaka na wokovu wangu.

MBUNGE FULANI: Wacha wee.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, lakini taasisi za namna hii ambazo tulitegemea zivutie watu kumjua Mungu, watu waache uovu, ndizo zinazofanya uovu, ni jambo ambalo linaumiza. Wakati mwingine sisi ambao tunatamka tumeokoka unaposikia mwenzako, taasisi inatangaza wokovu, halafu inafanya vitendo vya namna hii ni masikitiko makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali, taasisi za namna hii kuna haja ya kuchunguzwa. Tulisikia Uganda alijitokeza mtu mmoja anaitwa Kibwetere akawakusanya watu mwisho wa siku akawaangamiza, haya ndiyo tunayoyaona ya namna hii. Wanajificha kwenye mgongo wa kumtaja Mungu ili watu wajue hawa watu wana Mungu kumbe nia yao ni mbaya.

SPIKA: Mheshimiwa Bilakwate, hoja iliyoko Mezani inahusu Shamba la Malonje. Waheshimiwa Wabunge lazima tuelewane vizuri, ili isije ikaonekana ni dini fulani inayojadiliwa humu ndani, ili isije ikaonekana ni imani fulani ndiyo inayojadiliwa humu ndani. Kwa hiyo, muelewe tu Bunge ni lazima lifanye kazi yake Kikatiba na kazi tuliyopewa Kikatiba ninyi nyote mnaifahamu, leo sitakuwa na maneno mengi sana hapa mbele. Kwa hivyo, ni lazima Mheshimiwa Mbunge aongozwe kuelekea huko. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Bilakwate mjadala kuhusu imani pengine siku nyingine tutakapokuwa na hoja Mezani inayohusu hilo, tutaijadili vizuri, lakini kwa maana ya mjadala uliopo Mezani sasa hivi imani ya wale watu, tuwaache na imani yao, tushughulike na huu uwekezaji ambao upo kwenye Shamba la Malonje ambao umeleta changamoto. Mheshimiwa Innocent Bilakwate.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante, nafikiri ujumbe umefika.

Mheshimiwa Spika,Jambo lingine ambalo linasikitisha ukija kuangalia namna shamba hili lilivyoanza kutangazwa mpaka linafikia hatua hii kuna mazingira ambayo yanaonesha kulikuwa na rushwa. Kwa sababu gani nasema kuna mazingira? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Baraza la Mawaziri kama yangefuatwa, lakini na jambo lingine la shamba hili ni kitendo cha kuuzwa bei ndogo na baada ya mwaka mmoja hajawekeza kitu chochote cha kupandisha shamba hili akaenda kukopa zaidi ya shilingi bilioni mbili, bilioni tatu na zaidi. Jambo lingine ni uongozi wa mkoa ungechukuwa hatua juu ya vitendo hivi ambavyo vilikuwa vinaendelea.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo linanipa mashaka na kuamini kuwa, kuna mazingira ambayo sio mazuri maana Biblia inasema, “rushwa hupofusha hata haki isitendeke”. Kitendo cha Uongozi wa Mkoa kuidanganya kamati na kutengeneza mazingira ya kutushawishi tuamini kuwa, kule hakuna mgogoro ni mazingira ambayo kwa kweli, yanatia mashaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipofika tukaamua kwenda kwenye Uongozi wa Mkoa, lakini tulivyoelezwa tulifika sehemu tukasema mmh, ina maana hiki kitu kilichoundwa kuna uwongo? Yaani tuliingia kwenye wakati mgumu, lakini tukasema aah, ngoja twende na site tuone hali ilivyo. Kufika site, mnaambiwa hakuna mtu aliyepigwa risasi, mnakuta watu wamepigwa risasi, tukaambiwa na Uongozi wa Mkoa kuwa, hawa wanaolalamika wametoka Mkoa wa Mbeya, lakini tulipofika kule tukawauliza wananchi, hawa watu wanaosema wamepigwa risasi, hawa wakina mama wanaodai wamebakwa ni wa eneo lipi? Wakasema ni wa hapahapa na nyumbani kwao tunaweza kuwapeleka.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa mazingira haya sio bure. Kuna haja ya kuendelea kuchunguza.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, kuna haja ya kuendelea kuchunguza hata uongozi wa Mkoa kujiridhisha hao watu walikuwa wapo na mazingira gani hayo ambayo yalikuwa yanatushawishi. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Bilakwate kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Asia Halamga.

TAARIFA

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kumpa Taarifa ndugu yangu Mheshimiwa Bilakwate. Ukienda kule site Mwekezaji CSR yake ameamua kujenga Kituo cha Polisi ndani ya shamba, lakini hajaamua kujenga zahanati kwa wananchi kule kwenye kijiji. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Bilakwate unapokea Taarifa hiyo?

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa sababu, sisi tulitegemea Kituo cha Polisi kijengwe kwenye jamii, kisaidie jamii, lakini kimejengwa kwenye eneo ambalo muwekezaji anadai ni eneo lake. Kwa hiyo, haya mazingira kwa kweli, yanatia aibu na yanafedhehesha kwa viongozi ambao wameaminiwa na Mheshimiwa Rais waende kumsaidia, lakini hawamsaidii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja hii na naomba sana, namwomba sana Mheshimiwa Rais, mapendekezo yote ayafanyie kazi, ili wananchi wale waweze kupata haki, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia kuendelea kuwepo katika Bunge hili kuwatumikia Wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kipekee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa Watanzania. Tumeshuhudia miradi mingi mikubwa sana lakini pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Rais, hatuwezi kuacha kumpongeza Waziri wa Fedha pamoja na Wasaidizi wako mnafanya kazi nzuri na ndiyo maana tunaona miradi inakwenda vizuri kila kona na imegusa kila sekta mambo yanakwenda vizuri lakini pamoja na kukupongeza wewe pia ninampongeza Waziri wetu wa Mipango kwa mipango mizuri ambayo ameileta ninaamini Tanzania tunaendelea kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sana suala la kulipa kodi hasa kudai na kutoa risiti. Mheshimiwa Waziri uliongelea hili jambo kwa ukali sana na kwa uchungu kuonesha namna unavyoipenda nchi yako na uzalendo kwa Taifa lako. Kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha Watanzania walio wengi hatuna tabia ya kulipa kodi au kudai risiti. Hili jambo mimi nilikuwa nasema ni kukosa uzalendo, kwa sababu hii nchi ni ya kwetu sisi wenyewe na ninaamini tutaijenga sisi wenyewe kwa kulipa kodi na tunapokwenda kununua na kuuza tukatoa na kudai risiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa najiuliza tuanze sisi wenyewe Waheshimiwa Wabunge hivi sisi kweli ni wazalendo katika jambo hili? Tunalipa kodi? Tunadai risiti na kutoa risiti pale tunapouza na kununua? Mimi niwape mfano, tena wa hapa hapa ndani ya Bunge, ni mara ngapi mmenda pale canteen umenunua chakula, umedai risiti? Unapewa chakula unaondoka, hiyo ni kukosa uzalendo lazima tuambizane ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge tuwe namba moja tunapoenda kufanya mikutano tuwahimize Watanzania, kwa nini tunahitaji walipe kodi? Kwa nini tunahitaji wadai risiti? Hii ndiyo itakayosaidia miradi. Unakwenda kule unanunua kitu hujadai risiti au wewe unapofanya biashara hujatoa risiti. Unakuja hapa Bungeni unaomba mradi wa maji, unaomba mradi wa barabara hiyo ni kukosa uzalendo. Kile unachokifanya nje ndicho uje kukidai hapa. Kwa hiyo, mimi ninawaomba sana Waheshimiwa Wabunge sisi tuna nafasi kubwa, tuna maeneo mengi ya kusemea. Hebu tutoke tushirikiane na Serikali twende kuwahimiza wananchi juu ya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaamini kila Mtanzania akisimama vizuri katika jambo hili tukalipa kodi, tukatoa risiti na kudai risiti tutapata mapato mengi na ni sehemu ndogo sana ambako hatufanyi hili. Ninajua Wabunge wengi mnaweza msifurahie lakini sisi lazima tuwe mfano. Lazima tuwe mfano ili tumsaidie Mheshimiwa Waziri na tumsaidia Mheshimiwa Rais. Tunahitaji fedha nyingi kwa ajili ya miradi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana hili jambo Serikali ilichukue, tuanze kuwafundisha watoto wetu juu ya uzalendo, juu ya kulipa kodi, juu ya kutoa na kudai risiti. Hili jambo likianzia toka huko chini ninaamini mambo yatakwenda vizuri. Kwa hiyo, niombe sana hili tulisimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nilisemee, Serikali na nyinyi kuna sehemu ambapo hamfanyi vizuri. Wakati mwingine unaenda kwenye duka wanakuambia hapa tuna miezi miwili mashine ya EFD imeharibika. Jukumu lenu Serikali lipo wapi? Lazima turudi pande zote. Mimi nilikuwa najaribu kuangalia sisi tunahitaji Watanzania wakalipe kodi, hivi Serikali ikinunua hizi mashine ya EFD mkawapa wafanyabiashara wote, mimi ninaamini litaondoa huu usumbufu wa kutokuwa na mashine. Sehemu nyingine unakuta mashine imeharibika lakini haijategenezwa wanakuambia tumetoa taarifa Serikalini hakuna kinachoendelea. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri hili nalo uliangalie, wanunulieni na kuwapa mashine wafanyabiashara ili sasa liwe jukumu la sisi kufuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho nataka nikisemee, kuna hili suala la kukadiria hawa wafanyabiashara, lipa shilingi milioni 20, lipa kiasi fulani. Hili Mheshimiwa Waziri linatengeneza mazingira ya rushwa, kwa nini mfanyabiashara anapofanya biashara msiangalie biashara yake akalipa kwa mujibu wa Sheria? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaanzia labda mfano shilingi milioni 80 lakini wanashuka wanashuka mwisho wa siku, hiyo shilingi milioni 80 hupati. Unapata shilingi milioni 10 halafu nyingine inaingia kwenye mfuko wa huyo mtu ambaye wanaenda ku-negotiate. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali hili nalo mliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri umeongelea suala la kilimo kuendelea kuwekeza nguvu. Ni kweli kilimo ni uti wa mgongo mimi niombe sana Serikali mmeanza kuonesha kazi nzuri ya kuweka nguvu kubwa kwenye kilimo na mimi niwapongeze katika hili. Mmeweka nguvu kwa upande wa mazao yetu haya kimkakati tumeona mazao haya yameanza kupanda bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitoe mfano, mwaka 2022 nilikataa kuunga mkono hapa bajeti, nikitaka kahawa iuzwe kwenye mnada. Baada ya Serikali kulipokea kahawa imeuzwa kwenye mnada Waheshimiwa Wabunge imetoka shilingi 800 mpaka 1,100 sasa hivi tunaongelea shilingi 5,000 na kitu. Huu ni ushindi mkubwa na tunampongeza sana Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri Bashe kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: … na hili lisiishie hapa. Mimi naamini haya mazao yetu ya kimkakati tuki…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa. Muda wako umeisha tafadhali.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu. Awali ya yote nimshukuru kwanza Mwenyezi Mungu ambaye amenijaalia kuendelea kuwemo katika Bunge hili kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijachangia nichukue nafasi hii kuwapa pole wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa hasa kwenye Kata ya Murongo, Bugomora na Kibare kwa adha ambayo wameipata kutokana na wadhibiti wa magendo ya kahawa. Tayari nimeshawasiliana na Mkuu wa Wilaya na tumeshakubaliana wadhibiti wa magendo waende kwenye mipaka waondoe hii adha ambayo wanaipata wananchi. Ninampongeza sana Mkuu wa Wilaya ameshachukua hatua mbalimbali kwa hiyo ninaamini tabia ya kuwavamia wananchi kwenye nyumba zao haitaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kuchangia. Kwanza; nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya maeneo mbalimbali. Kwa kweli kwa upande wa ujenzi amefanya mageuzi makubwa, tunampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nimpongeze sana pacha wangu Mheshimiwa Bashungwa pamoja na timu yake, mnafanya kazi kubwa nzuri sana. Kwa kweli, tumemuona maeneo mbalimbali, kwenye madaraja, mafuriko, mpaka watu wengine wakawa wanasema siku hizi Mheshimiwa Bashungwa amekuwa mkandarasi na ni Engineer kabisa. Tunampongeza sana anafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie barabara zangu ambazo ni barabara ya Omurushaka – Nkwenda – Murongo. Barabara hii ni barabara ambayo inaunganisha Wilaya ya Karagwe ambako unatoka Mheshimiwa Bashungwa lakini pia Wilaya ya Kyerwa. Ni barabara ambayo ni ahadi ya miaka mingi tangu kipindi cha Hayati Benjamin Mkapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashukuru kwa hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa na mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Amesharuhusu barabara hii ya Murushaka – Murongo kilometa 50, ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Mkandarasi ameshaonyeshwa barabara, kilichobaki ni kupewa advance ili barabara hii ianze. Sasa nikuombe sana Mheshimiwa Bashungwa, barabara hii ni muhimu sana, mlipeni mkandarasi ili aanze barabara hii ili tuondoe yale maneno ya watu ambao hawatutakii mema wanaosema yule mkandarasi aliyepelekwa alikuwa ni Mchina aliyetoka syndicate kwa hiyo tulikuwa tunawazuga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee tena barabara ya Omugakorongo – Kigarama – Murongo, hii ni barabara ambayo inaunganisha wilaya zetu za Karagwe na Kyerwa na ni barabara ambayo ni muhimu sana. Ninaomba sana Mheshimiwa Bashungwa, baada ya tatizo lililojitokeza baada ya kupata mkandarasi wa kwanza, sasa muitangaze upya. Niombe sana barabara hii iweze kujengwa, iweze kutangazwa na mkandarasi apatikane ili akabidhiwe barabara hii, kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara hizi ninazisemea kwa muda mrefu kwa sababu ya umuhimu wake. Wilaya za Kyerwa na Karagwe ndizo wilaya ambazo zinalima kahawa nyingi sana. Pamoja na wilaya nyingine, hizi ni wilaya ambazo tuna uzalishaji mkubwa wa kahawa na tunaliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni. Kwa hiyo, ninaamini tutakapokuwa tumetengeneza barabara hizi, tunaenda kuinua uchumi wa wana-Karagwe na pia uchumi wa wana-Kyerwa na Taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana barabara hizi tuziangalie ili ziweze kutengenezwa. Jambo lingine ambalo nilisemee; Mheshimiwa Bashungwa nikupongeze sana, umeanza kuinua na umekuwa uki-promote sana wakandarasi wazawa. Hili jambo ni zuri sana lakini niombe sana pamoja na kuwainua hawa wakandarasi niombe Mheshimiwa Bashungwa, mjali na malipo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa wakandarasi wamekuwa wanakopa hela benki lakini wanapopewa kazi wanacheleweshewa malipo na mwisho wa siku wanaishia kufilisika. Kwa hiyo, niombe sana, pamoja na kuwa-promote tuhakikishe hawa wakandarasi wanalipwa kwa wakati ili tuwainue kifedha waweze kuendelea kufanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, mimi leo niliona niongelee barabara zangu pamoja na hilo la wakandarasi. Mheshimiwa Bashungwa tunaendelea kukuombea, unafanya kazi nzuri sana na Mungu akufanikishe, akulinde na yale maono yote uliyonayo yaweze kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada huu muhimu wa kuifanya Dodoma kuwa Makao
Makuu. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa nguvu na afya kuwepo Bungeni hapa na kujadili mambo muhimu kama haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kweli Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa na shujaa anafanya maamuzi ambayo ni magumu. Wenzetu walikuwa mara nyingi wanasema tunataka kiongozi atakayefanya maamuzi magumu na hakika Dkt. Magufuli amewajibu kwa maamuzi magumu, jambo ambalo limekaa tangu mwaka 1973 leo anaibuka mwaka 2018 kulifanyia maamuzi kwa kweli ni jambo la kupongezwa na niwaombe wenzangu upande wa pili wasione aibu kupongeza katika hili kwa kweli kile ambacho walikuwa wanakililia leo amewajibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada ni muhimu sana Dodoma kuwa Makao Makuu kwa kweli napongeza, nipongeze Wizara ya TAMISEMI chini ya Mheshimiwa Jafo kwa kulisimamia hili kwa kweli nawapongeza sana. Kuna watu ambao wamekuwa wanasema haya mambo ni mambo ya kukurupuka, niseme kwa kweli Serikali haijakurupuka. Jambo ambalo tunaweza kusema ni kwa kweli lilichelewa lilitakiwa lifanyiwe maamuzi miaka mingi, lakini Dodoma kuiandaa kuwa Makao Makuu halikuanza sasa hata hili jengo la Bunge ilikuwa ni sehemu ya maandalizi kuiandaa Dodoma kuwa Makao Makuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Dodoma inakuwa Makao Makuu, Dodoma ukija kuangalia iko katikati ya Tanzania, lakini maandalizi mengine ambayo niendelee kuipongeza Serikali ukija kuona barabara zinazounga Mkoa wa Dodoma, zinazounga nchi nzima kuja Mkoa wa Dodoma asilimia nafikiri zaidi ya 99 zinapitika kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo hii ilikuwa ni sehemu ya kuiandaa Dodoma kuwa Makao Makuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine sisi tunaotoka Kanda ya Ziwa kama kule Kyerwa mtu alikuwa kitoka Kyerwa kuja Dar es Salaam kupata huduma za Serikali kwa kweli walikuwa wanapata shida sana, lakini sasa ni rahisi unatoka Kagera asubuhi jioni unafika Dodoma, kesho unamaliza shughuli yako, unajiandaa kurudi kwetu. Kwa hiyo hili naipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwaombe sana, sio kila jambo linalokuja hapa Bungeni lazima tulipinge, kile kinachofanyika kizuri ndugu zangu tukiunge mkono tusiwe tunapinga kila kitu, watu watatushangaa huko nje. Kwa hiyo, mimi kama Mbunge na Mwanakamati naunga sana mkono hoja hii ya kuipitisha kuwa Dodoma kuwa Makao Makuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limenisikitisha sana lazima tuliseme, nimekuja kugundua ni kwa nini wenzetu walikuwa wanalalamika sana kuwa hawana watu wa kuwasaidia ofisini, kweli limethibitika asubuhi nimeona hata hoja ya upande wa pili waliyoileta taarifa yao jinsi ilivyokuwa, hao watu kwa kweli muwafikirie ili wapewe wasaidizi kwa sababu kama hawawezi kuandaa hata taarifa ya kuleta Bungeni kwa kweli wanahitaji msaada, muwafikirie. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niombe sana tunapoleta sheria hii Dodoma kuwa Makao Makuu lazima tuangalie mazingira ambayo ni mazuri. Kwa mfano hili nilishalisemea hata kwenye Kamati, Dodoma sasa hivi inaenda kuwa Makao Makuu, lazima tuangalie yale mambo ambayo yalikuwa yanasumbua Dar es Salaam kwa mfano Dar es Salaama unakuta kana maeneo mengine ambayo yako karibu na katikati ya mji bado hata hayajapimwa na hapa Dodoma sasa hivi hii sheria tuna uhakika inaenda kupita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie ujenzi huu unaoendelea kujenga hapa Dodoma kama upo kwenye mazingira ambayo ni sahihi maeneo haya yamepimwa. Kwa mfano, nikienda pale nyuma ya Martin Luther pale lile eneo nyuma kidogo halijapimwa, kwa hiyo tuombe Mheshimiwa Waziri tusitangaze tu kuwa Makao Makuu lazima tuhakikishe
ujenzi unaoendelea mpango Miji iwe sahihi ili ionekane kweli hapa ni Makao Makuu. Tusitangaze tu lakini tuhakikishe kila huduma zinapatikana ambazo zinaendana na Makao Makuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na barabara bado barabara nyingi hapa Dodoma hazionekani kama ni Makao Makuu, lakini tunajua kwa sababu ya uamuzi huu ambao umefanywa na Mheshimiwa Rais naamini mambo yanaenda kukamilika na kulingana na taarifa ambayo Mheshimiwa Waziri Jafo amekuwa akitupatia ya kuboresha Jiji la Dodoma tunaamini mambo yanaenda kukaa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, uamuzi huu ni uamuzi sahihi na ni uamuzi ambao unahitaji kuungwa mkono na kila Mtanzania mwenye akili timamu. Ahsante.