Primary Questions from Hon. Joseph Anania Tadayo (7 total)
MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza: -
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka sharti vikundi vya wanawake na vijana kuwa na mtu mwenye ulemavu kwa mikopo ya Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Anania Tadayo, Mbunge wa Jimbo la Mwanga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri hutolewa kwa mujibu wa Sheria za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2019 na Kanuni zake zilizoboreshwa mwaka 2021.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa kwenye kanuni hizo, hazizuii mtu mwenye ulemavu kuwa miongoni mwa vikundi vya wanawake au vijana ikiwa amekidhi mahitaji ya sheria na kanuni zake. Aidha, kundi la watu wenye ulemavu limepewa fursa mahususi ili kuwarahisishia kupata mikopo ya asilimia 10, ahsante.
MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi wa kuondoa magugu maji katika Ziwa Jipe?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Anania Tadayo, Mbunge wa Mwanga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi imeona changamoto ya uharibifu wa mazingira unaotokana na kuenea kwa magugu maji katika Ziwa Jipe. Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira tayari imefanya tathimini ya uharibifu uliopo na kuandaa andiko la mradi wa hifadhi ya ardhi, na vyanzo vya maji wenye thamani ya takribani dola za Marekani milioni sita kwa ajili ya kuondoa magugu maji katika Ziwa Jipe ambapo hadi sasa jitihada za kutafuta fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali zinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nia ya Serikali kuhakikisha inarejesha ikolojia ya Ziwa Jipe ili kuleta manufaa kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo pamoja na uhifadhi wa mazingira. Serikali inamhakikishia Mbunge kwamba mara fedha zitakapopatikana itatekeleza mradi huu mara moja. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH A. TADAYO K.n.y. MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza:-
Je, lini mradi wa maji wa Tukuyu utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na ukamilishaji wa Mradi wa Maji Tukuyu Mjini unaolenga kuhudumia wakazi wapatao 63,647 waishio kwenye Mitaa ya Mabonde, Kasyeto, Ndyonga, Batini, Bulyaga na Makandana. Utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia 85 ambapo kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni pamoja na ujenzi wa banio katika chanzo cha Mto Mbaka, uchimbaji wa mtaro na ulazaji wa bomba kuu kutoka kwenye chanzo kwenda kwenye tenki umbali wa Kilometa 9.5, uchimbaji wa mtaro na ulazaji wa mabomba ya usambazaji, umbali wa kilometa 20 pamoja na ununuzi na ufungaji wa dira mpya za maji 125.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zilizosalia ni ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye uwezo wa lita 1,500,000 pamoja na ununuzi na ufungaji wa dira nyingine mpya 5,875 ambapo kazi zote hizi zinatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2024.
MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza:-
Je, lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa Stendi ya kisasa katika Mji wa Mwanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Anania Tadayo, Mbunge wa Jimbo la Mwanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya ufinyu wa stendi ya magari katika Halmashauri ya Mwanga. Halmashuri imeandaa andiko lenye thamani ya shillingi bilioni 3.2 kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa na kuliwasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI mwezi Agosti, 2023 ambapo wataalam wanaendelea na mapitio ya andiko hilo kulingana na vigezo kwa ajili ya utekelezaji, ahsante.
MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza: -
Je, lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa Kituo cha Afya Lang’ata – Mwanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Anania Tadayo, Mbunge wa Jimbo la Mwanga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya tathmini ya Vituo vya Afya Vikongwe vinavyohitaji ukarabati. Hadi kufikia Disemba, 2023 jumla ya vituo vya afya 202 chakavu vimeainishwa kote Nchini kikiwemo Kituo cha Afya Lang’ata ambapo vitatengewa bajeti kwa ajili ya ukarabati kwa awamu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Vituo vya Afya Chakavu, pia ziko Hospitali Kongwe 50 za halmashauri zilizofanyiwa tathmini, na hospitali 38 zimeshapelekewa jumla ya shilingi bilioni 34.2 kwa ajili ya ukarabati katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 na 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, Serikali itatoa kipaumbele cha ukarabati wa Kituo cha Afya Lang’ata katika bajeti zijazo, ahsante.
Mnada wa Mifugo Kata ya Kileo Mwanga Kufunguliwa
MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza:-
Je, lini mnada wa mifugo uliojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 600 katika Kata ya Kileo, Wilayani Mwanga utafunguliwa na kuanza kazi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inawajibu wa kuhakikisha kuwa biashara ya mifugo inafanyika katika mazingira yenye miundombinu muhimu ili kurahisisha biashara hiyo. Katika kufanikisha hilo, Serikali hujenga na kukarabati miundombinu hiyo ili kuboresha mazingira ya biashara ya mifugo hapa nchini katika minada ya mifugo ya awali, upili na mipakani ukiwemo Mnada wa Kileo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilijenga miundombinu mbalimbali katika Mnada wa Kileo ikiwemo ukuta, vipakilio, ofisi na mazizi. Hata hivyo, kulingana na matakwa ya kibiashara ya mifugo minadani kuna miundombinu michache ya msingi ambayo inahitaji kukamilishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mwanga itafanya ukarabati wa dharura wa haraka wa choo cha mnada ili mnada uanze kutumika. Wizara imepanga kufanya ukarabati huo wa robo ya pili ya bajeti ya mwaka 2024/2025. Aidha, ujenzi wa miundombinu iliyobaki utafanyika katika mpango wa bajeti wa mwaka 2025/2026 wakati mnada ukiendelea kutumika.
MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Kisangara – Nyumba ya Mungu kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Kisangara – Nyumba ya Mungu yenye urefu wa kilometa 17.5, inaendelea na inategemewa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu wa 2024. Baada ya Usanifu kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, ahsante. (Makofi)