Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Daniel Baran Sillo (9 total)

MHE. GEORGE N. MALIMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Vituo vya Polisi katika Kata za Berege na Ng’hambi Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Kata ya Berege imetenga eneo lenye ukubwa wa meta za mraba 1011.5 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Kata. Ujenzi wa kituo hicho umeshaingizwa kwenye mpango wa ujenzi wa Vituo vya Polisi vya Kata 647 vitakavyojengwa nchi nzima kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025 na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kata ya Ng’hambi bado haijatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Kata.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuitaka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Kata ya Ng’hambi na kata nyingine zisizokuwa na Vituo vya Polisi vya Kata, ahsante. (Makofi)
MHE. ALI JUMA MOHAMED K.n.y. MHE. MAULID SALEH ALI aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kudhibiti mfumo wa makosa ya kimtandao (cyber crime) ili yasitokee nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, uhalifu wa makosa ya mtandaoni unasimamiwa na Sheria Na. 14 ya Mwaka 2015 na ndiyo Sheria inayodhibiti makosa haya. Sheria inaelekeza matumizi sahihi ya mtandao na imeainisha adhabu kwa makosa ya matumizi mabaya ya mtandao. Serikali katika kuimarisha udhibiti wa makosa ya mtandaoni imeanzisha mkakati wa Taifa wa udhibiti wa usalama mtandaoni wa kuanzia mwaka 2022 – 2027.

Mheshimiwa Spika, mkakati huu utawatumia wataalam mbalimbali katika kuratibu ugunduzi, kuzuia, kukataza, kufanya uchunguzi wa majibu na kuandaa mashitaka ya uhalifu. Pia, kuimarisha mazingira ya matumizi ya mtandao na kuboresha sheria iliyopo, kulinda huduma muhimu za habari, kuendeleza ujuzi kwa wafanyakazi na usalama mtandaoni, kutoa elimu kwa wadau na kuweka ushirikiano wa Serikali, wafanyabiashara na watu binafsi ili kudhibiti matukio ya uhalifu mtandaoni, ahsante.
MHE. ABDI HIJA MKASHA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Nyumba za Askari wa Jeshi la Uhamiaji Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali imekamilisha taratibu za kufunga mikataba ili kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya watumishi sanjari na ujenzi wa jengo la Ofisi ya Uhamiaji Wilaya Micheweni. Gharama ya utekelezaji wa mradi huu ni kiasi cha shilingi 2,695,937,724.80, ikijumuisha gharama za mkandarasi kiasi cha shilingi 2,549,937,724.80 na mshauri elekezi kiasi cha shilingi 146,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukamilisha taratibu za ununuzi, tayari Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi 1,250,000,000 ili kuanza utekelezaji wa mradi huu. Aidha, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji mzuri wa miradi ya maendeleo kwa wananchi wake, ahsante sana.
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR aliuliza: -

Je, lini vyombo vya usafiri vilivyosajiliwa Zanzibar vitatambuliwa Tanzania Bara?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo katika hatua ya Marekebisho ya kifungu cha nane cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, ambacho kinazungumzia usajili wa vyombo vya moto hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupokea maoni ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mapendekezo haya yatawasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Nduguti kwa kuwa ujenzi wake umesimama kwa muda mrefu sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Nduguti ni Kituo cha Wilaya ya Mkalama kilichoanza kujengwa mnamo mwaka 2015 na kukamilika mwaka 2023 na kuzinduliwa na kwa sasa kinahudumia wananchi wa Mkalama, ahsante sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE K.n.y. MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Je, upi mpango wa Serikali wa kuipatia gari la Zimamoto Wilaya ya Liwale ili kukabiliana na majanga ya moto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea na jitihada za kuliimarisha na kuliboresha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha taratibu zote za mkopo wenye masharti nafuu wa thamani ya Dola za Marekani milioni 100 kutoka Taasisi ya Abu Dhabi Export Credit Agency iliyopo Umoja wa Falme za Kiarabu kwa ajili ya kupata vitendea kazi mbalimbali, ikiwemo upatikanaji wa magari 150 ya zimamoto na uokoaji yatakayosambazwa kwa nchi nzima, ikiwemo Wilaya ya Liwale.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -

Je, lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa Sheria ya kuboresha Sheria za Jeshi la Magereza ili ziendane na wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Njau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Magereza inaendelea na mchakato wa maboresho ya Sheria ya Magereza sura 58 iliyorejewa mwaka 2002 ili ziweze kuendana na wakati, ambapo kwa sasa upo katika hatua ya kukusanya maoni ya wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Muswada wa sheria hii utawasilishwa Bungeni mara tu baada ya taratibu kukamilika, ahsante sana.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -

Je, lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa Sheria ya kuboresha Sheria za Jeshi la Magereza ili ziendane na wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Njau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Magereza inaendelea na mchakato wa maboresho ya Sheria ya Magereza sura 58 iliyorejewa mwaka 2002 ili ziweze kuendana na wakati, ambapo kwa sasa upo katika hatua ya kukusanya maoni ya wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Muswada wa sheria hii utawasilishwa Bungeni mara tu baada ya taratibu kukamilika, ahsante sana.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa Kituo cha Polisi Tarafa ya Igurubi - Igunga utakamilika?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kituo cha Polisi Igurubi ulianza mwaka 2018 kwa kushirikisha nguvu za wananchi na ulisimama mwaka 2020 baada ya kukosa fedha. Tathmini kwa ajili ya kumaliza ujenzi ili kuunga mkono jitihada za wananchi imeshafanyika ambapo kiasi cha fedha shilingi 53,000,000 zinahitajika. Fedha hizo zinatarajiwa kutengwa kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2024/2025, ahsante.