Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Daniel Baran Sillo (28 total)

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, utaratibu wa kuwa na Polisi Kata kila kata umesaidia kupunguza uhalifu katika maeneo mengi. Ni nini mkakati wa Serikali wa kuongeza idadi ya Polisi Kata angalau kufikia wawili?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni nini mkakati wa Serikali kuwapatia vitendea kazi Polisi Kata, kwa mfano pikipiki, ili ziwasaidie katika kutekeleza majukumu yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Malima, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali imeendelea kuajiri Askari wa Jeshi la Polisi, na jinsi bajeti itakavyoruhusu. basi tutaendelea kuajiri askari wa kutosha na hatimaye kuwafikisha walau wapatikane wawili kwenye kila kata kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mahitaji ya pikipiki kwa nchi nzima kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar ni pikipiki 4,434 na kwa awamu ya kwanza tayari Serikali imeshasambaza pikipiki 105 kwa maana ya pikipiki 95 upande wa Tanzania Bara na pikipiki 10 kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, kwa jinsi bajeti itakavyoruhusu, tutaendelea kununua pikipiki kwa awamu ili kuhakikisha zinafika kwenye kata zetu, ili kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi wetu. Ahsante.
MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina ushauri mdogo tu kwa Serikali. Kwa vile haya makosa ya uhalifu mitandaoni yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku, ninaishauri Serikali ijaribu kukiwezesha Kitengo hiki cha Cyber, ili kiwe na mfumo mzuri wa kufanya kazi zake kwa wepesi pamoja na kujaribu kurekebisha baadhi ya sheria ambazo zimekuwa kikwazo katika utendaji wao wa kazi za kila siku.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, tumepokea ushauri na tutaufanyia kazi, ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kama shida iliyopo Micheweni Wilaya ya Rungwe pia ina tatizo kama hilo la wafanyakazi wa uhamiaji kutokuwa na makazi ya kudumu ya wafanyakazi wale. Ni lini Serikali itapeleka fedha ili kuwasaidia Askari wale na siyo tu wa Uhamiaji, hata Askari Polisi kwani nyumba zao zimechakaa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba Askari wake wote wa Uhamiaji na Askari wote wanakaa makazi yaliyo bora. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jinsi fedha itakavyopatikana, tutatenga fedha kwa ajili ya kujenga nyumba ya makazi kwa ajili ya askari wa Wilaya ya Rungwe, ahsante sana.
MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uchakavu wa nyumba za Polisi zilizopo Finya, Basra maeneo ya Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa nyumba hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, nia ya dhati ya Serikali ni kuhakikisha kwamba Askari wake wote; Askari wa Uhamiaji na Askari Polisi, wote wanakaa kwenye makazi ambayo ni bora. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jinsi fedha zinavyopatikana, tutatenga fedha awamu kwa awamu kuhakikisha Wilaya ya Wete pia inapata ukarabati wa nyumba za Askari wetu.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni kazi gani zimefanyika kwenye shilingi 1,250,000,000 ambazo Serikali imepeleka kwenye Wilaya ya Micheweni kama jibu la msingi la Mheshimiwa Naibu Waziri linavyosema?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu, pengine Mheshimiwa Mbunge hajasikia vizuri, ni kwamba katika mwaka wa fedha huu wa 2023/2024 baada ya kusaini mkataba huu sasa, itaanza kazi ya ujenzi wa nyumba za makazi za askari hawa wa Uhamiaji. Kwa hiyo, kiasi hicho kilichotengwa cha shilingi 1,250,000,000 kitaanza utekelezaji wake mara baada ya kusaini mkataba.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu hili sasa naliuliza kwa mara ya tatu na Serikali inaahidi, lakini hakuna kinachofanyika. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri kwamba, wananchi wamefanya kila juhudi kuweza kujenga boma na limefikia kwenye lintel, lakini tayari kuna maboma sita pale kwa ajili ya Askari: Je, ni lini watakamilisha kazi hii ili kituo kile kianze kufanya kazi na tayari kuna nyumba sita ambazo zina Askari, lakini wanakwenda mbali na kituo hakijaanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawapongeza wananchi wa Jimbo la Ilemela kwa kazi kubwa walioifanya ya ujenzi wa maboma kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi ambayo wananchi walishaianza, Serikali inaunga mkono na nitapata fursa ya kukaa na Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi hicho niweze kuzungumza naye kuona namna bora ya kumalizia maboma haya ambayo tayari wananchi wameshayajenga.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Simiyu hatuna kabisa nyumba za Askari; Askari Polisi pamoja na Askari wa Uhamiaji. Je, ni lini Serikali itajenga nyumba hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Minza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba askari wetu wote wanakaa kwenye makazi bora. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaangalia kwenye mwaka huu wa fedha, kama Mkoa wa Simiyu hauna kituo kabisa, basi tuangalie kwenye mwaka wa fedha unaokuja ili kuhakikisha kwamba tunatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Askari Polisi pamoja na Uhamiaji. Nakushukuru sana.
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mchakato wa mabadiliko ya sheria hii ili kuweza kufanya vyombo vya usafiri kutambulika hapa Tanzania Bara umeonekana umechukua muda mrefu sana, sasa ni kwa nini Serikali haioni haja ya kuweka mwongozo maalumu kipindi hiki wakati tunasubiria mabadiliko ya sheria hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bakar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zipo katika mazungumzo, naomba tuwe na subira na utaratibu uliopo kwa sasa uendelee kutumika. Pale mazungumzo yatakapokamilika, basi marekebisho yatafanyika ili kuhakikisha kwamba vyombo vinasajiliwa kwa pamoja.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali kwamba sasa kituo kimeanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo Kidogo cha Polisi cha Ilunda wanafanya kazi zao kwenye kibweni kidogo cha vyumba viwili, Kituo Kidogo cha Polisi Ibaga, wanafanya kazi kwenye Ofisi ya Kijiji, Kituo Kidogo cha Polisi Mwangeza wanafanya kwenye Ofisi ya Kata. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo hivi vidogo ili wenye ofisi zao waendelee na kazi zao kwa sababu wanalalamika sana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, polisi wetu ukienda kusikilizwa kesi wanaandika kwenye vikaratasi vya ajabu ajabu tena wanageuza kuangalia mahali ambapo hakuna maandishi. Ni lini Serikali itaanza kusikiliza mambo yetu kwa kutumia TEHAMA ili kuokoa kazi ambazo polisi wetu wanahangaika nazo sana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji mzuri wa vituo vya polisi kama alivyotaja. Ni maagizo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu ujenzi wa vituo vya polisi vya kata nchi nzima na Wizara yetu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeanza mkakati wa kujenga vituo vya afya vya kata nchi nzima. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge vituo vyako vitatu ulivyovitaja vilivyoko Wilaya ya Mkalama vitaingia kwenye mpango tayari kwa kujengwa katika utaratibu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la matumizi ya TEHAMA, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani imekwishaanza matumizi ya TEHAMA kwa Jeshi la Polisi na mwezi uliopita tulizindua hapa Kituo cha Polisi cha Mtumba ambacho tayari kinatumia TEHAMA. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pia jambo hili litafika Mkoa wa Singida hadi Wilaya ya Mkalama kama ambavyo ameuliza, ahsante sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ilianzisha ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Tanganyika mpaka sasa bado ujenzi hatujapata nguvu yoyote kutoka Serikalini na Serikali iliahidi kutupatia fedha za kuendeleza huo ujenzi.

Je, ni lini Serikali italeta fedha kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi Wilaya ya Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Kakoso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze wananchi wa jimbo lake kwa kazi waliyoifanya ya kujenga kituo cha polisi mpaka hatua hiyo waliyofikia. Nimhakikishie kwamba Serikali itaunga mkono wananchi hawa na itatoa fedha ili kumalizia Kituo cha Polisi cha Tanganyika.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya ujenzi wa kituo cha polisi katika Kata ya Mchinga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema nia ya Serikali ni kuhakikisha vituo vya polisi vyote vinakamilika na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Kituo chake cha Mchinga tutazungumza naye ili tuone namna ya kukikamilisha ili kupata huduma za ulinzi na usalama kwa wananchi wake.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata ya Bassotu, Wilaya ya Hanang umekuwa ni wa muda mrefu sana. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili kukamilisha ujenzi wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Vijana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Bassotu kimetengewa fedha katika mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuweza kukamilika na kutoa huduma kwa wananchi wa Bassotu na Wilaya ya Hanang kwa ujumla.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ya kutujengea vituo vya polisi, lakini Kituo cha Polisi Chang’ombe ni cha Kimkoa wa Kipolisi Dar es Salaam. Je, Serikali mna mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi cha Tandika ndani ya Jimbo la Temeke?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea maombi ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Tandika kama alivyosema na tuweke kwenye mpango na kutengewa fedha ili tuweze kujenga kituo cha polisi kwa ajili ya ulinzi na usalama wa wananchi wa Temeke.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kuniona, wananchi wa Kata ya Kasharunga katika Kijiji cha Kasharunga katika Wilaya ya Muleba wamejenga Kituo Kidogo cha Polisi na kimekamilika. Ni lini Serikali itafungua kituo hicho kwa kupeleka askari ili wananchi waweze kupata huduma waliyoihitaji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali la Mheshimiwa Rwamlaza, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza kwa ujenzi wa kituo cha polisi katika eneo hilo na nimhakikishie kwamba tuko tayari kwenda kufungua wakati wowote hata baada ya Bunge la Bajeti na tutaleta askari tayari kwa kutoa huduma katika eneo hilo.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ujenzi wa vituo vya polisi, Mbarali, Kyela, Chunya na Mbeya DC, askari polisi hawana nyumba za kuishi, wao wanaishi uraiani yaani wamepanga. Je, ni lini Serikali itawajengea nyumba askari polisi hao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Suma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikijenga nyumba za polisi katika maeneo mbalimbali kwa awamu na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika maeneo ambayo ameyataja katika Wilaya ya Chunya, Mbarali na maeneo mengine tutatenga fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za polisi katika maeneo hayo.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Kata ya Mkiwa tumeanza ujenzi wa Kituo Kidogo cha Polisi ambacho ni kituo cha kimkakati. Mimi kama Mbunge nimechangia shilingi milioni tano kutoka katika mfuko wa jimbo na wananchi wameji-organize na wadau. Ni lini Serikali itatuunga mkono ili kumalizia kituo hicho kwa ajili ya usalama wa wananchi wetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtaturu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetenga shiliongi bilioni 3.8 kwa ajili ya kumalizia maboma yote 77 yaliyojengwa na wananchi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baadaye tuonane pengine kituo chake alichokitaja kiko kwenye maboma haya 77 ili tuweze kukimalizia katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua ni upi mpango wa Serikali wa kujenga kituo cha kisasa katika Mji wa Tunduma ili kiendane na mahitaji hasa ukizingatia ni lango kuu la SADC?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Fiyao, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yana population kubwa, lakini pia yana maeneo makubwa ya biashara kama Tunduma, yanakuwa na vituo vya polisi vya uhakika ili kulinda usalama wa wananchi na mali zao. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge eneo hilo pia tumelichukua, tulipange kwenye mpango, ili tuweze kujenga kituo cha polisi cha kisasa kama ambavyo ameomba Mheshimiwa Mbunge.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri, Kata ya Masumbwe tayari tuna eneo la kituo cha polisi, lakini pia mimi kama Mbunge kule Lulembela nimetoa shilingi milioni tatu, Gilorwanguru nimetoa mifuko 100 kwenye kituo cha polisi. Je, ni lini Serikali Kuu mtatupa support Mbogwe kuweza kukamilisha vituo hivi vya polisi vilivyopo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nicodemas Maganga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye baadhi ya majibu ni kwamba Serikali imetenga fedha kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kumalizia maboma yote ambayo wananchi wameshaanza kujenga, yapo maboma 77. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tuonane baadae pengine kituo chako pia kama kipo kwenye vile 77 kitatengewa fedha ili kumalizia kazi kubwa waliyofanya wananchi wa Mbogwe, ahsante sana.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale pamoja na kwamba haina Kituo cha Polisi cha Wilaya chenye hadhi, lakini kuna uhitaji mkubwa sana wenye Tarafa ya Kibutuka, Lilombe na Kimambi na ni ahadi ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema Serikali imepanga kujenga vituo vya polisi vya kata kwa awamu. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge pia kata zake alizotaja naamini zipo kwenye mpango, kwa hiyo, tutazitengea fedha ili ziweze kujengwa na wananchi wapate ulinzi na usalama wa mali zao, ahsante sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, Kyerwa ni Wilaya mpya lakini mpaka sasa hakuna kituo cha polisi. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Kyerwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ujenzi wa vituo vya kata, kama nilivyosema Serikali inaendelea kujenga vituo vya wilaya kwa kupitia Mfuko wa Tozo na Tuzo. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Wilaya ya Kyerwa ni moja kati ya wilaya za kimkakati kwa hiyo, tutajenga kituo cha polisi katika wilaya hiyo, ahsante sana.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi kilichokuwepo pale Mchangani kwenye Jimbo langu la Chaani ambacho kwa takribani 80% kimeshatengenezwa na wawekezaji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Usonge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana kwa ujenzi wa kituo ambacho kimefika 80% na ninamhakikishia Serikali kwa kazi hiyo nzuri iliyofanywa na wananchi, 20% iliyobaki tutamalizia katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Katika Kata ya Bukumbi wananchi na Mbunge tumejenga kituo kizuri cha afya. Lini Serikali itapeleka magari au pikipiki, kwa ajili ya usafiri wa hawa askari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani alikuwa anaulizia swali kituo cha polisi na siyo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maige, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali mpaka sasa imetoa pikipiki 105 kwa ajili ya vituo vya polisi katika maeneo mbalimbali nchini na kwa jinsi ya upatikanaji wa fedha, Serikali itatoa pikipiki kwa ajili ya kuhudumia vituo vya kata, kama alivyotaja Mheshimiwa Mbunge Maige.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Kijiji cha Pujini kilichopo Wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba ni kijiji ambacho kina matukio ya uhalifu siku hadi siku, je, ni lini Serikali itajenga kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Mwinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, Serikali ina mkakati wa kujenga vituo vya kata nchi nzima, nadhani takribani kata 4,434 zimebaki. Kama nilivyosema, vinajengwa kwa awamu, havijengwi mara moja, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kituo alichotaja kitawekwa kwenye mpango ili kiweze kutengewa fedha kwa miaka inayokuja na kujengewa kituo cha polisi katika eneo lake, ahsante sana.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuiuliza Serikali, kituo cha polisi kilichopo Kata ya Kashai kimepewa chumba kimoja katika Ofisi ya Kata na tukizingatia kwamba Kata ya Kashai ndani ya Jimbo la Bukoba Mjini ina wakazi zaidi ya 33,000. Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Kashai? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Lugangira, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Kata ya Kashai ina wananchi wengi, kama alivyotamka Mheshimiwa Mbunge, kwa hiyo namhakikishia kwamba kwa kuwa ina wananchi wengi na pia kunakuwa na hatari ya kuwa na wizi au matukio mbalimbali. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa kata yake aliyoitaja ya Kashai na yenyewe tumeichukua na tutaiingiza kwenye mpango kwa ajili ya kujengewa Kituo cha Polisi, ahsante sana.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Karanga, viongozi pamoja na wananchi wamejenga kituo kizuri sana cha polisi, lakini bado hakijakamilika na mimi nimewasaidia tofali 2,000. Je, Waziri yuko tayari kuja kukitembelea na ku-allocate bajeti ya kumalizia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa aliyofanya ya kujenga Kituo cha Polisi katika Kata aliyoitaja ya Karanga. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge niko tayari kwenda kwenye kituo hicho kukikagua na kukitengea fedha, kwa ajili ya kumalizia kazi kubwa waliyoifanya wananchi wa Karanga, ahsante sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, jeshi hili la Zimamoto ni la muhimu sana na limekuwa likifanya kazi kubwa sana, hasa kwenye Mkoa wetu wa Lindi, ikiwemo kudhibiti na kupambana na mafuriko yanayoendelea katika Mkoa wa Lindi. Hata hivyo, jeshi hili hawana Ofisi nzuri za kufanyia kazi.
MWENYEKITI: Swali la nyongeza Mheshimiwa Francis.

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati Ofisi za Zimamoto zilizopo katika Wilaya za Mkoa wa Lindi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, watumishi wa Ofisi za Zimamoto wamekuwa hawana nyumba za kuishi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwajengea nyumba za kuishi katika Mkoa wa Lindi?
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Francis Ndulane kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza linalohusiana na ukarabati wa ofisi, kadiri Serikali itakavyopata fedha itatenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa Ofisi za Zimamoto na Uokoaji katika maeneo aliyotaja Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nyumba za makazi ya Askari, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, ni kwamba kadri Serikali itakavyopata fedha itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari wetu wa zimamoto na askari wengine hapa nchini, ahsante sana.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo la wanufaika wa msamaha wa Parole, kwamba wakishafika uraiani wanatengwa na jamii na kuonekana bado ni wahalifu, jambo linalowafanya kufanya tena uhalifu na kurudi Magerezani.

MWENYEKITI: Swali Mheshimiwa Njau.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu ili marekebisho ya sheria yaweze kugusa jamii na jamii iweze kuelewa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Wapo watoto wanaozaliwa Magerezani wakiwemo na mama zao ambao watoto wale sio watuhumiwa, lakini watoto hawa hawapati haki za msingi kwa mujibu wa Katiba kama elimu na vitu vinginevyo.

MWENYEKITI: Swali Mheshimiwa.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, marekebisho haya ya sheria yatagusa vipi watoto hawa wanaozaliwa Magerezani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Felista Njau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa elimu ya kutosha kwa jamii nzima ili kuhakikisha kwamba wenzetu wanaotoka magerezani basi wasitengwe tena ili waendelee kuwa raia wema na kutimiza majukumu yao kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu watoto wanaozaliwa Magerezani, amedai wanakosa haki. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sheria hii itakapofanyiwa marekebisho itapata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kama vile jamii nzima, viongozi wa dini pamoja na Maafisa wa Magereza pamoja na Wizara nyingine za kisekta ili kuhakikisha kwamba tunatunga sheria mahususi kwa ajili ya ku-cover watoto wetu wanaozaliwa katika Magereza. Ahsante sana.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, kwanza nianze kuishukuru Serikali kwa kuamua kukamilisha kituo hiki ambacho kiko Tarafa ya Igurubi kitakachozihudumia Kata za Kinungu, Igurubi, Mwaitunduru, Mwamashiga, Kinig’inila, Mwamashimba na Mwamakona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nauliza kwamba, kwa kuwa Serikali yetu imeamua inapojenga vituo inatoa na vitendea kazi, je, Serikali ina kauli gani kuhusiana na kituo hiki kitakapokamilika, watatupatia vitendea kazi kwa ajili ya doria ?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali imeshatoa pikipiki kama 105 kama vitendea kazi nchi nzima na bado tuna mpango wa kutoa pikipiki kwa awamu ili kuhakikisha kwamba kata zote ambazo tunajenga ofisi za Polisi pia zinapata pikipiki ili kurahisisha utendaji kazi, ahsante sana.