Primary Questions from Hon. Masache Njelu Kasaka (16 total)
MHE. MASACHE N. KASAKA Aliuliza:-
Je, ni lini ujenzi wa mradi mkubwa wa maji Chunya Mjini na kata za jirani utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masache Kasaka, Mbunge wa Jimbo la Chunya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto inayoukabili Mji wa Chunya. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, hatua mbalimbali za muda mfupi na mrefu zimeendelea kuchukuliwa. Kwa upande wa muda mfupi, Serikali imejenga mradi wa uboreshaji huduma ya maji katika Mji Mdogo wa Chunya uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 946.8. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa tanki la ukubwa wa mita za ujazo 500, ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilometa 10.49. Mradi umekamilika kwa asilimia mia moja mwaka 2019 na umesaidia kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 36 hadi 51.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa hatua za muda mrefu, Serikali kupitia Wizara ya Maji ina mpango wa ujenzi wa mradi mkubwa wa maji kwa ajili ya wananchi wa Mji wa Chunya. Mradi huo utatekelezwa kupitia fedha za mkopo kiasi cha dola za Marekani milioni 500 kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim kwa ajili ya miji 28 Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa sasa mradi upo katika hatua ya manunuzi ya Wakandarasi wanaotarajiwa kuwepo eneo la mradi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi ifikapo Aprili, 2021 na ujenzi wa miradi unatarajiwa kuchukua miezi 24. (Makofi)
MHE. MASACHE N. KASAKA Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa matokeo ya tafiti za madini katika lugha nyepesi kwa wachimbaji wadogo ili ziwasaidie katika uchimbaji kwa kuwa Sheria ya Madini inazitaka Kampuni zinazofanya utafiti kwenye madini kuwasilisha matokeo ya tafiti hizo GST?
NAIBU WAZIRI WA MADINI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Jimbo la Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) tangu mwaka 2019 imekuwa ikitoa matokeo ya tafiti za madini kwa lugha ya Kiswahili na iliyorahisishwa ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kuelewa kwa urahisi. Aidha, GST imeandaa kitabu mahususi chenye Kichwa “Kitabu cha Madini Yapatikanayo Tanzania” ambacho nacho kimeandaliwa kwa lugha ya Kiswahili na kinabainisha maeneo yenye viashiria vya madini ya aina mbalimbali yanayopatikana nchini.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, GST imeandaa Kitabu cha Mwongozo wa Uchukuaji wa sampuli za madini na kitabu hicho ni cha mwaka huu huu wa 2021 ambacho pia kimeandaliwa kwa lugha fasaha ya Kiswahili, nyepesi na inayoeleweka, lengo likiwa ni wachimbaji wetu wadogo waweze kufaidika na lugha hiyo iliyorahisishwa. Ahsante.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itafikisha umeme kwenye vijiji ambavyo bado havijafikiwa Wilayani Chunya pamoja na Makao Makuu ya Kata za Nkung’ungu, Lualaje, Mafyeko na Kambikatoto?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu – Mzunguko wa Pili unaolenga kufikisha miundombinu ya umeme katika vijiji vyote ambavyo vilikuwa havijafikiwa na huduma ya umeme Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa niaba ya Serikali umeingia mkataba na Kampuni ya M/S Electrical Transmission and Distribution Construction and Maintenance Company Limited kutekeleza mradi huu katika Mkoa wa Mbeya ambao utekelezaji wake umekwishaanza kwa Mkandarasi kukamilisha uhakiki na kuagiza vifaa vitakavyotumika katika ujenzi.
Mheshimiwa Spika, mradi wa kupeleka umeme katika Wilaya ya Chunya unahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo kilovoti 33 zenye urefu wa kilomita 245.5; kilomita 12 ya njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4; ufungwaji transfoma 12 za KVA 50; pamoja na kuunganisha wateja wa awali 814. Gharama ya mradi ni Shilingi bilioni 10.656 na utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2022.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kupunguza eneo la Hifadhi ya Msitu wa Mbiwe ili litumike kwa matumizi ya wananchi na shughuli za kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masache N. Kasaka, Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzishwa hifadhi hiyo ni kulinda bayoanuai zilizomo ndani ya hifadhi ikiwemo vyanzo vya maji vinavyotumika kwa matumizi ya binadamu na wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, Serikali haioni haja ya kupunguza eneo la hifadhi ya Msitu wa Mbiwe. Aidha, Sheria ya Misitu inaruhusu uchimbaji wa madini ndani ya hifadhi kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizopo kwa njia endelevu.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapunguza ukubwa wa Msitu wa Mbiwe na kurudisha kwa Wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Msitu wa Hifadhi wa Mbiwe una ukubwa kilomita za mraba 491 na umeanzishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 598 la mwaka 1995. Hifadhi ya Msitu wa Mbiwe ni muhimu kwa uhifadhi vyanzo vya maji, kuhifadhi mimea na wanyama, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kivutio cha utalii. Eneo hili pia ni ushoroba unaounganisha mapori ya akiba ya Rukwa - Lukwati, Lwafi na Hifadhi ya Taifa Katavi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu huo, Serikali haioni haja ya kupunguza eneo hilo.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kumalizia ujenzi wa Gereza Chunya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Gereza Chunya ulianza mwaka 2016 kama kambi kwa kujenga na kukamilisha bweni moja la kulala wafungwa, jiko la wafungwa na nyumba mbili za kuishi askari. Vilevile ujenzi uliendelea kwa jengo la utawala na nyumba mbili za kuishi askari ambapo upo kwenye hatua ya msingi. Aidha, katika mpango wa bajeti 2023/2024 Serikali imepanga kutumia kiasi cha shilingi milioni 50 ili kugharamia uendelezaji wa ujenzi wa Gereza Chunya.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa barabara inayounganisha Mikoa ya Mbeya, Tabora na Singida inayoanzia Makongolosi hadi Rungwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mbeya – Chunya – Makongolosi – Rungwa – Mkiwa yenye kilometa 503.36 kwa awamu. Sehemu ya Mbeya – Chunya – Makongolosi yenye kilometa 111 ujenzi umekamilika. Ujenzi wa sehemu ya Noranga - Itigi (Mlongoji) kilometa 25 umefikia asilimia 12 na taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi sehemu ya Noranga – Doroto kilometa 6 na Itigi – Mkiwa kilometa 25.6 zimekamilika na Mkataba umesainiwa. Kwa sehemu iliyobaki ya Makongolosi – Rungwa - Noranga kilometa 356 na Mbalizi – Makongolosi kilometa 50 Serikali inaendelea kutafuata fedha kwa ajili ya ujenzi.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi kwa kumalizia ujenzi wa Vituo vya Polisi vya Itumbi na Kambikatoto, Lupa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Vituo vya Polisi vya Itumbi na Kambikatoto ni vituo vinavyojengwa kwa nguvu za wananchi na mpaka kumalizika ujenzi wake vitagharimu kiasi cha fedha shilingi 279,780,978. Fedha inayohitajika ili kumalizia ujenzi kwa kuunga mkono nguvu za wananchi, ni shilingi 173,447,178. Fedha hizo zitatoka kwenye Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ili kumalizia ujenzi huo kama njia ya kuwaunga mkono wananchi wa Jimbo la Lupa.
MHE. SUMA I. FYANDOMO K.n.y. MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -
Je, lini barabara ya Makongolosi – Mkiwa – Chunya itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mbeya – Chunya – Makongolosi – Rungwa – Mkiwa (km 503.36) kwa awamu, ambapo sehemu ya Mbeya – Chunya – Makongolosi (kilometa 111) ujenzi umekamilika. Ujenzi wa sehemu ya Noranga – Itigi – Mkiwa (kilometa 56.9) sehemu ya Noranga – Itigi (Mlongaji) (kilometa 25) umefikia asilimia 12 na kwa sehemu ya Noranga – Doroto (kilometa 6) na Itigi – Mkiwa (kilometa 25.6) mkataba wa ujenzi tayari umesainiwa. Kwa sehemu iliyobaki ya barabara za Makongolosi – Rungwa – Noranga (kilometa 356) na Mbalizi – Makongolosi (kilometa 50) Serikali inaendelea kutafuta fedha za ujenzi, ahsante.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE K.n.y. MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza:-
Je, lini Serikali itatoa fedha kumalizia ujenzi wa Vituo vya Afya Matwiga na Mafyeko Jimboni Lupa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Jimbo la Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2019/2020 na 2021/2022 Serikali ilitenge kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Isangawana katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya katika kata za kimkakati nchini kote ikiwemo ukamilishaji wa vituo vya afya vya Matwiga na Mafyeko katika Halmashauri ya Chunya.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji katika Kata ya Ifumbo, Chunya?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Skimu ya Umwagiliaji ya Ifumbo yenye eneo la hekta 250 inayolima mazao ya mpunga, alizeti, ufuta, mbogamboga na mahindi kwa wananchi wa Chunya. Kwa kutambua umuhimu wa skimu hiyo, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi milioni 400 kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na shilingi milioni 50 kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo Wilayani katika mwaka wa fedha 2008/2009. Fedha hizo zilitumika kujenga miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo banio, vigawa maji 11, vivuko vya miguu 10 na mfereji mkuu wenye urefu wa mita 2,165.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji nchini na hasa ukizingatia mabadiliko ya tabia nchi yanayopelekea mtawanyo wa mvua zisizotabirika. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha Skimu ya Ifumbo na zingine zote za umwagiliaji nchini.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -
Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha utaratibu wa kupata baruti na zebaki unakuwa rahisi na vibali vitolewe kwa ngazi ya kijiji kwa wachimbaji wadogo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Jimbo la Lupa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuimarisha usimamizi, upatikanaji na matumizi ya baruti hapa nchini. Ili kurahisisha upatikanaji wa vibali vya baruti Wizara imesogeza huduma hiyo katika Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa yote ya kimadini nchini ikiwemo Chunya. Aidha, Serikali imesajili na kutoa vibali vipya vya biashara ya baruti kwa kampuni 25 ambazo hutoa huduma hiyo hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini katika kipindi cha mpito kwa matumizi ya zebaki imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo kushirikiana na Ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya ufuatiliaji wa taratibu za uingizaji na usambazaji wa kemikali ya zebaki nchini ili kubaini changamoto za upatikanaji wa kemikali hiyo na kuandaa takwimu za kiasi cha matumizi ya zebaki ili kujua kiasi kinachohitajika nchini ili kurahisisha utoaji wa vibali vya uingizaji na kuwatambua na kuwasajili waingizaji na wasambazaji wa kemikali ya zebaki nchini kwa mujibu wa Sheria ya Kemikali nchini ili biashara hiyo ifanyike kwa uwazi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kemikali ya zebaki kutumika katika shughuli za ukamatishaji wa dhahabu, tafiti za kisayansi zimebainisha kuwa kemikali hiyo isipotumika vizuri ni hatari kwa afya ya binadamu na mazingira, jambo lililosababisha Serikali kusaini Mkataba wa Minamata (Minamata Convention) ambao utekelezaji wake unapelekea kupunguza matumizi ya zebaki au kuondoa kabisa pale inapowezekana.
Mheshimiwa Spika, kutokana na madhara ya matumizi ya zebaki, Serikali kupitia mradi wa Environmental Health and Pollution Management Program –imeanza kutafuta njia mbadala ya uchenjuaji kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu ili kuondokana na madhara yanayotokana na matumizi ya kemikali hiyo. Mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) na kutekelezwa chini ya Baraza la Udhibiti na Usimamizi wa Mazingira (The National Environmental Management Council - NEMC), ahsante.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Makongolosi – Rungwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mbeya – Chunya – Makongolosi – Rungwa – Mkiwa (kilometa 503.36) kwa awamu; ambapo sehemu ya Mbeya – Chunya – Makongolosi (kilometa 111) ujenzi umekamilika. Ujenzi wa sehemu ya Noranga – Itigi – Mkiwa (kilometa 56.9) sehemu ya Noranga – Itigi (kilometa 25.) umefikia asilimia 72 na kwa sehemu ya Noranga – Doroto (kilometa 6) na Itigi – Mkiwa (kilometa 25.6) kazi ya ujenzi imeanza na utekelezaji wa mradi unaendelea. Kwa sehemu iliyobaki ya barabara ya Makongolosi – Rungwa – Noranga (kilometa 356) Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi, ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE K.n.y. MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza:-
Je, ni lini ahadi ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chunya itaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Chunya unaendelea katika eneo la hospitali ilipo kwa kuiongezea miundombinu muhimu iliyokuwa imepungua. Serikali katika kipindi cha mwaka 2020/2021 hadi 2023/2024 imepeleka shilingi bilioni 2.5 ambapo majengo 13 yamejengwa yakijumuisha jengo la OPD, jengo la kuhudumia wagonjwa wa dharura (EMD), jengo la maabara, jengo la kliniki ya mama na mtoto, jengo la upasuaji, wodi ya wazazi, jengo la stoo ya kutunzia dawa, wodi nne za kulaza wagonjwa, jengo la mama ngojea, jengo la kufulia na njia za kutembelea wagonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majengo yote haya yamekamilika na yanatumika. Katika mwaka 2024/2025 Serikali imetenga shilingi milioni 450 kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE K.n.y. MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -
Je, lini Serikali itapeleka watumishi wa Kada ya Afya na Elimu katika Wilaya ya Chunya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE ) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa kada za elimu na afya kila mwaka kulingana na upatikanaji wa fedha. Kati ya mwaka 2020/2021 na 2022/2023, Halmashauri ya Wilaya ya Chunya ilipokea jumla ya watumishi 397 wakiwemo wa afya 84 na elimu 313 ambapo walimu wa shule za msingi walikuwa walimu 244 na shule za sekondari walikuwa 69.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024 Serikali inatarajia kuajiri jumla ya watumishi 22,112 wakiwemo wa afya 10,112 na elimu 12,000 ambao watapangiwa vituo vya kazi katika maeneo yenye upungufu mkubwa ikiwemo Wilaya ya Chunya.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -
Je, lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha Afya Mtanila ili kiendane na vituo vinavyojengwa sasa?
MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Mtanila ni miongoni mwa vituo vya afya 202 vilivyofanyiwa tathmini kwa ajili ya ukarabati mkubwa na kuongeza miundombinu ili kuendana na mahitaji ya sasa ya utoaji wa huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga na itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa Kituo cha Afya Mtanila ili kiweze kutoa huduma bora za afya, ahsante.